Mali za Kapteni Komba kupigwa mnada
Mali za Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba
Dar es Salaam. Mali za Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Kapteni John Komba zimetangazwa kupigwa mnada kutokana na
kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali
hizo zinahusisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,214 lililopo
Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, kiwanja namba 1030 kilichosajiliwa kwa
jina la John Damiano Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu
wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, Kampuni ya Uwakili ya
Mpoki & Associates Advocates inayoiwakilisha CRDB imetangaza kuuza
eneo hilo la kibiashara lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya
mafuta, maduka makubwa, benki, sehemu ya kufanyia mazoezi, hospitali na
huduma nyingine za kijamii.
“Tayari eneo hilo lina
nyumba kubwa ya kuishi upande unaotazamana na barabara mpya ya Bagamoyo.
Kwa upande wa kusini mwa jengo kuu linalotazama barabara hiyo kuna
nyumba nyingine ya kuishi, fremu za maduka na ofisi,” ilisomeka sehemu
ya tangazo hilo.
Alipoulizwa juu ya gharama halisi
anazodaiwa Kapteni Komba na muda wa deni hilo, mmiliki wa Kampuni ya
Mpoki & Associates Advocates inayoratibu mnada huo, Mpale Mpoki
alisema maelezo yote yanayohusu kiasi cha mkopo na muda wa deni
yatajibiwa na CRDB wenyewe.
Hata hivyo, uongozi wa CRDB
haukupatikana jana kuzungumzia suala hilo na Kapteni Komba alipoulizwa
alisema hakuna jambo kama hilo... “Hakuna kitu kama hicho, waulize hao
waliotoa hilo tangazo.”