Mimi ni waziri, nina haki zangu, ajitetea Wasira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira amesema yeye ni waziri na ana haki zake, baada
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kumtaka aachie nyumba
anayoishi ya Bodi ya Sukari kwa kuwa haimuhusu kwa sasa.
Juzi,
PAC iliiagiza Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kumwandikia barua ya
kumtaka mwanasiasa huyo mkongwe aondoke kwenye nyumba ya bodi hiyo
iliyopo Masaki jijini hapa, aliyoishi tangu akiwa Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika na iwapo haitawezekana, aanze kulipia tozo ya pango.
Hata
hivyo jana, Wasira aliiambia gazeti hili kuwa hawezi kujibizana na PAC
kwa kutumia magazeti na kwamba kama kuna maagizo yoyote yametolewa, kipo
chombo kitakachoshughulikia.
“Mimi ni waziri nina haki
zangu, PAC haihusiki na mtu binafsi wala siyo ofisa mahesabu. Kwa nini
unaniuliza mimi, si uwaulize PAC?” alihoji Wasira.
Akijibu
maelezo hayo ya Wasira, mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema jana
kuwa kamati yake haina nia ya kumshambulia waziri huyo kwa kuwa ana haki
ya kupewa nyumba na Serikali.
Alisema iwapo Serikali
bado inataka waziri huyo aendelee kukaa kwenye nyumba hiyo, ilipe kodi
na kama ikishindwa wampe nyumba nyingine.
“Hapa suala
siyo mzee Wasira binafsi, ni Serikali kukaa kwenye nyumba ya umma
isiyolipia kodi,” alisema Zitto. Aliongeza kuwa Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndiyo iliyobaini kuwa nyumba
hiyo hailipiwi kodi na kuitaka irejeshwe kwa Bodi ya Sukari.