Muswada wa Takwimu wadunda tena bungeni, warudishwa
Dodoma. Muswada wa Sheria ya Takwimu uliokuwa uwasilishwe bungeni katika mkutano wa 18, hautawasilishwa tena hadi hapo taratibu za kikatiba zitakapokamilika.
Taarifa ya kutowasishwa kwa
muswaada huo bila kutaja sababu zilitolewa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda, muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha leo.
“Muswada wa Takwimu unaondoka kwasababu bado serikali inataka kuufanyia kazi,”alisema Spika Makinda.
Akizungumza
nje ya bunge, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema kuwa
muswada umeondolewa ili kuwezesha kufuata taratibu za kikatiba.
“Inabidi
muswada huu uende Zanzibar kujadiliwa na upate theluthi mbili wakati wa
kupigiwa kura bungeni kutoka kwa wabunge wa pande zote,”alisema
Nchemba.
Hii ni mara ya pili kwa muswada huo kushindwa kupitishwa baada ya kukosekana kwa theluthi mbili ya wabunge bungeni.
Aidha,
Spika Makinda alisema muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi uliokuwa
upigiwe kura leo, utapigiwa kura kesho baada ya kukosekana kwa theluthi
mbili ya wabunge kutoka pande zote.
“Muswada wa Utawala
wa Kodi bado kuna kazi ndogo tu ya kupigiwa kura lakini tumetambua bado
wabunge wote hawajafika,”alisema Makinda.
Alizitaka kamati za vyama kukutana ili kuweza kupata utaratibu mzuri wa kuifanya kazi hiyo kesho.
Katika
hatua nyingine, Spika Makinda alitangaza kuchaguliwa kwa Mbunge wa
Bukoba Vijijini, (CCM) Jasson Rweikiza, kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Nafasi hiyo
iliachwa wazi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja baada ya Bunge
kutaka kuvuliwa kwa nafasi hiyo baada ya kupata mgawo katika sakata la
Akaunti ya Tegeta Escrow.