Polisi: Hatukumpiga risasi Ponda
Khadija Ahmad, mke wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa akiondoka katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro jana baada ya kesi inayomkabili mumewe kuahirishwa hadi Februari mwaka huu. Picha na Juma Mtanda
Morogoro. Shahidi wa pili katika kesi
inayomkabili Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini, Sheikh
Ponda Issa Ponda ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro kuwa,
hawakuhusika kumpiga risasi mtuhumiwa huyo na kwamba alikamatwa katika
Hospitali ya Muhimbili akitibiwa jeraha alilodai lilitokana na risasi.
Akitoa
ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo shahidi Jafert
Kibona, ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Morogoro, alisema Agosti 9, 2013, polisi walipata taarifa kuwa, Sheikh
Ponda angekwenda Morogoro kwenye kongamano, hivyo waliwataka waandaaji
kumsalimisha polisi kiongozi huyo.
Kibona ambaye kwa
sasa ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mtwara, alisema polisi
walimtaka Sheikh Ponda kujisalimisha kutokana na kutafutwa kwa tuhuma za
kutoa maneno ya kashfa na uchochezi, Dar es Salaam na Zanzibar.
Hata
hivyo, Sheikh Ponda alikaidi amri hiyo, badala yake aliendelea kutoa
maneno ya kashfa na uchochezi katika kongamano la Morogoro, alidai
shahidi huyo mahakamani hapo.
Alidai walishindwa
kumkamata Ponda baada ya wafuasi wake kumwingiza kwenye gari dogo na
kumtorosha, kabla ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa
kiongozi huyo alijeruhiwa kwa risasi bega la mkono wa kulia.
Kibona
alisema walikwenda Hospitali Mkoa wa Morogoro, lakini hawakumkuta Ponda
na siku iliyofuata walipata taarifa kuwa amelazwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili. Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alimuuliza shahidi huyo
kuhusu mtu aliyempiga risasi Ponda, ikiwa polisi ndiyo pekee waliokuwa
na silaha siku hiyo.
Aliuliza pia kwa nini polisi walishindwa kumkamata Ponda wakati hakuwa na silaha. Kesi itatajwa tena Februari 2 na 19 mwaka huu.