Wafuasi 30 wa CUF wapata dhamana Kisutu
Wafuasi wa Chama cha Wananchi CUF, wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi CUF
wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama na kukaidi amri
halali ya polisi na kufanya maandamano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana
waliyopewa.
Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru jana
aliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kukamilisha masharti ya
dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika na
kila mdhamini asaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh 100,000.
Baada
ya washtakwia hao kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu
aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 12,2015 kwa ajili ya kuangalia kama
upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Juzi, Mawakili
wa Serikali, Joseph Maugo na Hellen Mushi, katika shtaka la kwanza
alidai kuwa Januari 27,2015 katika eneo la Temeke washtakiwa hao kwa
pamoja walikula njama ya kufanya uhalifu.
Akisoma hati
hiyo ya mashtaka, Maugo katika shtaka la pili alidai kuwa siku hiyo ya
tukio, washtakiwa 28 kati ya 30 wanaokabiliwa na kesi hiyo, wakiwa
katika ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke bila ya
kuwa na uhalali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano
kuelekea Mbagala Zakhem.
Katika shtaka la tatu,
ambalo nalo pia linawakabili washtakiwa 28 kati ya 30 , Wakili huyo wa
Serikali, Maugo alidai kuwa siku hiyo hiyo ya tukio katika eneo la Mtoni
Mtongani waligoma na kutojali tangazo halali lililotolewa na polisi
lisilowaruhusu kuandamana na hata kufanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa
wanaokabiliwa katika kesi hii ni Shabani Ngurangwa (56), Shabani
Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma Mattar (54), Muhamed Kirungi
(40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed(39), Abdul Juma(40), Hassan
Said (37), Hemed Joho (46) na Mohamed Ibrahim (31).
Pamoja
na Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina
(47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma (33), Salehe Ally (43), Abd
Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally(32) , Said Mohamed (40),
Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Abdallah Said(45),Rehema Kawambwa
(47), Salma Ndewa (42), Athuman Said (39).
Kwa upande
wa washtakiwa Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37) wao hawahusiki
katika shtaka la pili na tatu ambayo yanawakabili wenzake.