Ukawa kujadili mustakabali wa siasa nchini leo
Dar es Salaam. Wenyeviti wanaounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), leo watakutana kwenye mkutano wa faragha
kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali zinazohusu mustakabali wake na
hali ya kisiasa nchini.
Wenyeviti hao, Freeman Mbowe
(Chadema), James Mbatia (NCCR Mageuzi), Emanuel Makaid (NLD) na Profesa
Ibrahim Lipumba (CUF) wanakutana kwenye mkutano huo ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa kalenda ya Ukawa.
Juhudi za kuwapata
viongozi hao ili kuthibitisha ziligonga mwamba lakini Katibu Mkuu wa
NCCR Mageuzi Bara, Mosena Nyambabe alisema jana kuwa mkutano huo
utafanyika kama ilivyopangwa.
“Ninachofahamu mkutano
huo lazima utafanyika lakini siwezi kujua utafanyikia wapi kwa hapa Dar
es Salaam kwani ratibu zote wanazifahamu viongozi wenyewe,” alisema
Nyambabe.
Awali, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James
Mbatia alimwambia mwandishi kuwa mkutano huo utakuwa na ajenda
mbalimbali likiwamo suala la kuangalia mgombea wa nafasi ya urais
kupitia umoja huo.
Ajenda nyingine alizotaja ni kura ya
maoni ya Katiba Inayopendekezwa, changamoto ya uandikishaji wa Daftari
la Mpigakura, hali ya uchumi na tathmini ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.
Mbatia
alisema: “Ajenda hizo tunazijadili na lengo ni kuhakikisha tunatafuta
majibu ya changamoto mbalimbali zilizopo kwa sasa,” alisema na kuongeza:
“Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Mbali
na ajenda hizo, mwongozo wa umoja huo imekuwa ni jambo linalodaiwa kuwa
changamoto katika utekelezaji wake. Kuhusu maandalizi ya mwongozo wa
umoja, Mbatia alisema suala hilo pia litakuwa sehemu ya ajenda hizo.