MAUDHUI

 
 
 
 

MAUDHUI


Maudhui ya kazi ya fasihi hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mbalimbali yanayowasukuma watunzi mbalimbali kutunga kazi ya kisanaa (Senkoro, 2011).
Kwa ujumla maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.
Dhana hii ya maudhui ni pana sana, kwani hujumisha dhamira, ujumbe, migogoro, mtazamo, msimamo na falsafa ya mwandishi. Ila kulingana na mwongozo tutahakiki maudhui ya riwaya ya “Mzimu wa Watu wa Kale” kwa kufuata vigezo vifuatavyo;
Ø  Muhtasari wa mtunzi na utunzi wake
Ø  Uainishaji wake
Ø  Dhamira chomozi na
Ø  Riwaya nyingine zinazofanana na riwaya hii ya “Mzimu wa Watu wa Kale” kimaudhui.
MUHTASARI WA MTUNZI NA UTUNZI WAKE:
Mohamed Said Abdulla alizaliwa tarehe 25 Aprili 1918 mtaa wa Malindi Zanzibar. Alipelekwa chuoni ambako alijifunza kusoma Kurani. Mwaka 1928 mpaka 1937 alisoma masomo ya msingi katika shule ya serikali, mwaka 1938 alifanikiwa kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari. Baada ya kuhitimu aliajiriwa kuwa ofisa wa afya ambako alifanya kazi hiyo mpaka mwaka 1958 wakati ajira yake ilipokatishwa. Baada ya kuachishwa kazi katika idara ya afya alifanikiwa kupata ajira nyingine ya uhariri wa gazeti la Mkulima. Alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka kumi, hadi mwaka 1968 pale alipoachishwa tena kazi ya uhariri katika gazeti hilo. Baada ya kuachishwa kazi hiyo alipata kazi ya utayarishaji kipindi cha redio kilichoitwa Sadiki Ukipenda katika Sauti ya Unguja.
Mohamed Said Abdulla alifanikiwa kuoa mke na kupata watoto wawili katika maisha yake. Vile vile ni miongoni mwa watetezi wakubwa walifanya utetezi katika kuikomboa nchi ya Zanzibar kutoka mikononi mwa Wakoloni. Na hii ndio ilikuwa sababu ya yeye kuwa katika hatari ya maisha yake. Miongoni mwa beti zake za kuwatupia watu ujumbe utakaoweza kuwapotezea nguvu ya kutaka kuinyakuwa Zanzibar. Njama ilianza kupangwa na wakoloni ili kumuondoa Bwana Msa katika hii dunia. Mohamed Said Abdulla aliuawa yeye, mke wake  na watoto wake wawili wa kike 1992 katika kipindi cha mapinduzi ya Zanzibar. Hili lilikuwa pigo kubwa sana kwa Wazanzibari wote kwa kuuawa Bwana Msa katika mazingira ya kutatanisha (wiki pedia).
Katika taaluma ya uandishi mchango wake unaonekana sana katika taaluma ya fasihi kwani aliandika na kuchapisha vitabu mbalimbali vya fasihi kama vile riwaya, hadithi fupi na tamthiliya. Mohamed Said Abdulla ameandika riwaya saba ambazo ni;
·         Mzimu wa Watu wa Kale (1966)
·         Kisima cha Giningi (1968)
·         Duniani Kuna Watu (1973)
·         Siri ya Sifuri (1974)
·         Mke Mmoja Waume Watatu (1975)
·         Mwana wa Yungi Hulewa (1976)
·         Kosa la Bwana Msa
Mwaka 1958 Mohamed Said Abdulla aliandika riwaya yake ya kwanza ya “Mzimu wa Watu wa kale” iliyochapwa mwaka 1966. Kutokana na uandishi wa kitabu hicho alitunukiwa nishani ya juu ya uandishi. Aliandika pia vitabu vingine kama vile Kivuli Kinaishi ambayo ni tamthiliya na mke wangu ambacho ni kitabu cha hadithi fupi. Pia alikuwa mhariri na mwandishi wa vitabu tofauti ambavyo viliinyanyua lugha ya kiswahili katika daraja la juu na kuiongezea umaarufu mkubwa eneo la Afrika Mashariki.
 Mzimu wa Watu wa Kale hii ni riwaya ya kwanza kabisa ya Mohamed Said Abdulla ambapo alifupisha jina na kuwa Bwana Msa, pia ndiye aliyekuwa muhusika mkuu katika riwaya hii ya Mzimu wa Watu wa Kale, riwaya hii inaonesha namna ambavyo Bwana Msa kwa kipawa alichopewa anagundua kwamba Bwana Ali aliuawa. Katika uchunguzi wake pia anagudua kuwa Baniani Seti anaipora maiti ya Bwana Ali Sh. 50,000 na kusafirisha mwili wake hadi kwenye msitu wa Mzimu wa watu wa kale. Spekta Seif na Najum wanashangaa kutokana na uwezo wa kipekee wa Bwana Msa wa kufukua ukweli wa mambo.
UAINISHAJI WAKE:
Hii ni riwaya pendwa ambayo inazugumzia juu ya upelelezi, na hii ndiyo sababu inaifanya riwaya hii kuwa katika kundi la riwaya pendwa kwani riwaya pendwa mara nyingi zinajengwa na dhamira kuu ya upelelezi, mapenzi,  usaliti, na dhamira nyingine zinazozungumzia mambo yanayopendwa katika maisha ya kawaida na mara zote hutilia mkazo kipengele cha fani kuliko maudhui. Wahusika wake mara nyingi wahalifu, wadhulumiwa (waliotendewa kosa), wapelelezi wakiwemo polisi na ni dhahiri kuwa kama tulivyoona katika riwaya hii wahusika wake wote wana sifa hizo.
                                                                          
DHAMIRA CHOMOZI:
Dhamira ni mawazo makuu ambayo mwandishi ameafiki kuifikishia jamii yake. Dhamira kuu katika riwaya hii ni “upelelezi na athari za dhuluma” pia kuna dhamira mbalimbali chomozi kama vile; hali ngumu ya maisha na umasikini, uchoyo na ubahili, dhana potofu na imani za ushirikina, athari za madawa ya kulevya, matabaka, umuhimu wa kuwa na subira,  umuhimu wa elimu, umuhimu wa kuthamini lugha ya Kiswahili, kujitoa mhanga, uvumilivu na kutokata tamaa,  ujasiri, suala la dini, nafasi ya vyombo vya dola, rushwa, athari za kulipiza kisasi na fitina, mapenzi na ndoa na matabaka
Upelelezi
Hali ya kufanya uchunguzi juu ya jambo fulani ili kubaini chanzo chake, sababu ya kutokea kitu hicho au hata kubaini mambo mbalimbali. Katika kujadili dhamira ya upelelezi mwandishi anaonesha kuwa suala la upelelezi sio tu kwa watu wenye majukumu hayo ya upelelezi bali suala hilo ni kwa watu wote wenye nia ya kujitolea, katika kulionesha hili, mwandishi anaonesha juhudi za Bwana Msa katika kufanya upelelezi juu ya chanzo cha kifo cha Bwana Ali, Bwana Msa anajitolea kushirikiana na Najum katika kutafuta chanzo cha kifo cha Bwana Ali, bila kukata tamaa na hadi mwisho kupata taarifa zote kuhusiana na kifo chake. Kwa mfano katika sura ya14 kuanzia ukurasa wa 70 hadi 84 Bwana Msa alipokuwa akitoa maelezo juu ya kifo cha Bwana Ali mbele ya Banyani, spekta Seif na Najumu.
Dhuluma
Hii ni hali ya mtu kuchukua kitu ambacho kilikuwa ni halali kwa mtu mwingine na kukifanya kuwa chake bila idhini ya mhusuka. Katika kujadili suala la dhuluma mwandishi Mohamed Said Abdulla anaelezea kuwa dhuluma ni mbaya sana katika maisha, huweza kumfikisha mtu katika hali mbaya. Mwandishi anasema;
    “Bwana Ali alitaka kumkimbia mtoto wake Ahmed kwa kudai kuwa si mtoto wake na
               kutaka kumuacha kiholela holela”.Ukurasa wa 78
Mwandishi anaendelea kusemakuwa
                 “Haki ya mtu haipotei bure, dhuluma haikumfikisha mbali Bwana Ali, labda
                    imempakatisha boga tu makaburini kwa watu wa kale.” Ukurasa wa 78.
Vile vile anaonyesha jinsi ambavyo Banyani na boi wake (Hamisi) walitaka kudhulumu pesa ambayo Bwana Ali alikuwa ameipokea kutoka kwao na hivyo anaonesha namna ambavyo walizichukua zile fedha na kurudisha mfuko kwa maiti na kutafuta namna ya kuificha maiti.  Hivyo dhuluma ni mbaya katika maisha na anaishauri jamii kuachana na tabia ya dhuluma.
Dhamira ndogondogo zilizojitokeza ni kama vile.
Hali ngumu ya maisha na umasikini.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo kuna hali mbaya kwa watu ambao wanaishi eneo la Bwana Msa, anaonesha jinsi ambavyo Bwana Msa alivyo na maisha magumu kwani hata koti ambalo anavaa limeshonwa kwa sindano ya mkono, vile vile kanzu ya Bwana Ali nayo pia imeshonwa viraka, pia mwandishi hakuishia hapo katika kuonesha hali ngumu ya maisha anaonesha pia namna mbavyo nyumbani kwa Bwana Ali kulivyo anaonesha vibanda viwili ambacho kimoja kilikuwa kinatumika kwa jiko na cha pili kinatumika kwa kujisaidia haja kubwa lakini vibanda vyote viwili vilikuwa havina mlango. Mwandishi anasema;
            “Vibanda viwili cha mkono wa kushoto kimefungwa kipande cha gunia mlangoni
kinachoningi’nia katikati hakimzuii mtu kuona kwa juu wala kwa chini na kumsitiri
aendaye haja huko msalani, kibanda cha pili kilikuwa jiko , nacho kilikuwa wazi na
             mtu aliweza kuona mabonge ya udongo matatu manne yaliyotumika kuwa majifya
            navijinga viwili vitatu vilivyo kwisha tumika ukurasa wa 12”
 Huu ni mfano mzuri katika kuonesha hali ngumu ya maisha. Katika jamii yetu pia kuna hali ngumu ya maisha tunaona watu wengi sana katika jamii wanakosa sehemu ya kulala, wanalala njaa kwa kukosa chakula. Hivyo ni jukumu letu kama wanajamii kufanya kila liwezekanalo kuondokana na hali ngumu ya maisha, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kuacha uvivu.
Uchoyo na ubahili
Katika kujadili dhamira hii, mwandishi anaonesha namna ambavyo uchoyo na ubahili umetawala kwenye mioyo ya watu. Katika jamii yetu amemtumia Bwana Ali kama mfano wa watu bahili ambao tunaishi nao kila siku, mwandishi anasema;
              “Bwana Ali alikuwa akishtaki njaa kila baada ya saa mbili, na hainyamazi
mpaka ashibe, lakini alivyokuwa yeye ni mtu bahili sana hakuweza kujilisha kwa
namna tumbo lake lilivyohitaji; kwa hiyo ubahili wake ulimwonyesha dawa rahisi
              sana- kutafuna tambuu na kumeza mateukurasa wa 7.
Mwandishi anaendelea kuonesha jinsi ambavyo Bwana Ali alikuwa pia mchoyo katika uk.7 mwandishi anasema; “alikuwa mtu mwenye choyo na tamaa, hasa katika masaala ya mali”. Hivyo ni wazi kuwa hata katika jamii yetu kuna watu wachoyo na wenye tamaa hivyo ni vyema tukaachana na tabia kama hizo, katika kuonyesha hili mwandishi amemtumia Ahmed Ali ambaye alikuwa ni kijana wa Bwana Ali lakini hakupendezwa na ubahili wa baba yake, katika ukurasa wa 8, mwandishi anasema;
                  “Kwa hakika alikuwa akifikiri, kwa maana ubahili wa baba yake ulimkaa kama donge kubwa la uchungu rohoni mwake…., ubahili wa baba yake hausemeki”.
Hivyo basi mwandishi anatuonesha jinsi ambavyo ubahili ulivyo hata unaleta vikwazo kwa watu tunaoishi nao na hivyo tunapaswa kuachana na ubahili, uchoyo pamoja na tamaa.
Umoja na mshikamano
Umoja na mshikamano ni kitendo cha kushirikiana baina ya mtu na mtu, kundi na kundi au baina ya pande mbili ili kufikia/kufanikisha lengo au jambo llilokusudiwa. Katika kitabu hiki mwandishi anatuonesha umoja na mshikamano baina ya Bwana Msa na Najum, hii inaonekana dhahiri pale wanapoungana kwenye suala la kutafuta chanzo cha kifo cha Bwana Ali. Wanafanya kazi hiyo kwenye mazingira magumu kwa pamoja ili tu kujua Bwana Ali alipo na kwa nini hakurudi nyumbani kama kawaida yake. Bwana Msa pamoja na Najum wameshirikiana sana kwa pamoja na kwa umoja kuanzia mwanzo wa upelelezi hadi mwisho wa upelelezi kama inavyoonekana ukurasa wa 6  hadi ukurasa wa 86 katika hii riwaya. Pia kuna ushirikiano baina ya Bwana Msa, Najum, na spekta Seif. Hii inaonesha wazi katika hatua za upelelezi waliokuwa wakifanya, spekta Seif aliwapa ushirikiano wa hali ya juu Bwana Msa pamoja na Najum katika kujua sababu ya mauaji ya Bwana Ali, hii inajidhihirisha wazi katika sura ya 10 ukurasa wa 51.
Katika jamii yetu suala la umoja na ushirikiano linaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa kwani jamii nyingi zimeshindwa kuendelea kwa sababu hakuna umoja na ushirikiano miongoni mwa wanajamii pia hakuna umoja na mshikamano kwenye baadhi ya ndoa, wafanyakazi, viongozi na hata kwa wanafunzi. Mfano mzuri ni wanafunzi wa vyuo vikuu wengi wao wamekuwa wazembe na wategeaji katika suala zima la kufanya kazi ambazo zinatolewa katika makundi na kusababisha kazi nyingi kuchelewa kukusanywa kwa muda husika.
Hivyo basi ni vema tukajenga tabia ya kushirikiana kwa pamoja ili kuleta maendeleo katika jamii kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na pia umoja ni nguzo kuu ya maendeleo ya jamii kwa kila nyanja.
Uzembe kazini/ kutokuwajibika.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo watu huwa ni wazembe katika kazi zao, hii inaonekana pale ambapo askari Kalungu anaposinzia katika eneo la kazi stesheni badala ya kuwajibika kazini kwake ukurasa wa 51. Mwandishi anatuonesha mfano mzuri hata kwa jamii tunayoishi watu wengi ni wazembe kazini kwao badala ya kufanya kazi hukalia mambo yasiyowahusu kupiga umbea au hata wengine kusinzia kazini kwao na kurudisha nyuma ufanisi wa kazi yao na kusababisha makosa mbalimbali kazini kwao. Hivyo ni vyema tukaachana na uzembe na tuwajibike wakati tungali kazini kwetu.
Ujasiri
Ujasiri ni hali ya kuthubutu kutenda jambo ambalo ni gumu yamukini linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu husika. Katika riwaya hii ya“Mzimu wa Watu wa Kale” suala la ujasiri linajitokeza pale ambapo Bwana Msa na Najum wanathubutu kuingia mzimuni, wanaazimia kuingia mzimuni japokuwa wanashuhudia maajabu mbalimbali. Mfano mzuri mwandishi mwenyewe anasema;
   
“Ndani mlikuwa na kiza kama uwanda wa ahera. Kiza kilikuwa kimetapakaa kinavuja.
           Sauti za komba na mabundi-wasiojua kwa sababu ya kiza kilichozagaa”. {U kurasa wa 26.}
Vilevile mwandishi anaendelea kusema katika ukurasa wa.33
                “Ndani kama tulivyosema, kiza tororo! Hapana mmoja aliyemuona mwenziwe  
                 Kunatisha!”.
 Hivyo tunaona hali halisi ya mzimuni ilivyokuwa inatisha hali ambayo ingepelekea Bwana Msa na Najum kukata tamaa mapema kwa sababu kunatisha lakini kutokana na ujasiri waliokuwa nao hawakukata tamaa bali waliendelea kuingia mzimuni na hatimaye waliweza kubaini kifo cha Bwana Ali.
Katika jamii suala la ujasiri linaonekana maeneo mbalimbali kwa watu baadhi ambapo ujasiri wao umepelekea kuwepo na ufanisi katika mambo mbalimbali. Mfano, kuwepo kwa viongozi jasiri katika vyama vya siasa kumepelekea kufahamika kwa mambo mbalimbali yaliyokuwa ni ya siri, tena ambayo jamii haikuyafahamu. Mfano mzuri ni kuwepo kwa Richmond na fedha ya rada kumetokana na viongozi jasiri waliothubutu kujitoa muhanga kuibua siri ya vigogo wa serikali.
Uvumilivu na kutokata tamaaa
Hii ni hali ya ustahimilivu wa hali ya juu ambapo mhusika anapambana na mambo makubwa ya ajabu yanayo katisha tamaa lakini yeye anaonesha msimamo wa kukabiliana nayo na kutokubali kushidwa.
Katika riwaya hii mwandishi Mohamed Said Abdulla amewatumia wahusika ambao ni Bwana Msa na Najum ili kutuonesha kuhusiana na suala la uvumilivu na kutokata tamaa. Bwana Msa pamoja na Najum wanaonekana kutokata tamaa katika kupeleleza chanzo cha kifo cha Bwana Ali na hata mwisho walipobaini chanzo cha mauaji ya Bwana Ali. Tunaona dhahiri katika ukurasa wa 26, 27, na 28 kuwa safari ya kuelekea kwenye kichaka cha Mzimu wa watu wa kale ilikuwa ni ngumu sana lakini Bwana Msa na Najum walijitahidi bila kukata tama, kunaonekana kulikuwa na umande ambao uliloanisha suruali zao pia tope la kule kileleni lilikuwa linateleza lakini walijitahidi sana lakini kikubwa zaidi waligongwa na vizuu hadi kuzimia na kujeruhiwa lakini hawakukata tamaa bali waliendelea na kazi yao mpaka mwisho.
Katika jamii yetu watu wengi wamekuwa hawafikii malengo na matarajio yao kutokana na kukata tamaa, suala la uvumilivu kwa walio wengi halipo na ndio maana mtu anapokumbana na kikwazo tu hukata tamaa na kutoendelea na kile ambacho alikuwa akikifanya. Mwandishi anatuasa tuwe na moyo wa kuweza kuvumilia mambo kama ilivyo kwa Bwana Msa pamoja na Najum ili kuweza kufanikisha yale ambayo tumeyakusudia kuyatenda kwani katika kufanya jambo lolote lile ni dhahiri kuwa kuna vikwazo na ugumu wake,  hivyo moyo wa kuvumilia mambo unahitajika.
Kujitoa mhanga
Katika riwaya hii ya mzimu wa watu wa kale tunaona kwamba Bwana Msa akishirikiana na Najum walijitoa muhanga kuingia katika kichaka kiitwacho mzimu wa watu wa kale ambacho ni kichaka hatari nia ikiwa ni kumtafuta Bwana Ali ambaye hakurudi nyumbani kwake na hivyo Bwana Msa anasema;
           “Mimi na wewe Najum, hatudhuriki kwa mzimu maana sote wawili tunajua kwamba vivuli  
           vya maiti havimjii mtu ila katika ndoto,……………….Bismillah, twende zetu” katika
(ukurasa wa 24).
 Mbali na hatari ya kufa katika kichaka kile, lakini waliazimia kukabiliana na lolote lile ambalo lingeweza kutokea  ili wafanikishe suala zima la kumtafuta Bwana Ali, Ukurasa wa 25-27 tunaona kwamba Bwana Msa na Najum, wanaendelea na safari yao na makwazo mfano Najum anapigwa kumbo la nguvu na vizuu wa watu wa kale lililomfanya azimie.Na anapozinduka wanaendelea na safari yao.
             “ile hali ya kuingia katika mzimu wa watu wa kale ilikuwa kujitoa sadaka kwa chochote
              kile ambacho kingetokea, walikuwa tayari”
Pia katika ukurasa wa 32”Ndani ya mzimu” tunaona kwamba kuna giza totoro! Hapana mmoja kumwona mwenziwe ni kunatisha, lakini walipiga moyo konde na katika ukurasa wa 38, mwandishi anaeleza kuwa Bwana Msa na Najum walimwona Bwana Ali akiwa makaburini na amekatwa kichwa huku akiwa amenyoosha miguu yake na kupakata kichwa chake, Bwana Msa anasema;
                          “Njoo, Najum! Njoo umtazame Bwana Ali kakatwa kichwa”
Bwana Msa na Najum pia walijitoa mhanga katika kuhakikisha kwamba muuaji ambae alihusika na kifo cha Bwana Ali anapatikana, hivyo walijitoa mhanga kufuatilia chanzo na muhusika ili naweze kufikishwa katika sheria na hivyo waliamua kuripoti tukio polisi ili waweze kusaidiwa katika utafiti wao. Mfano katika uk.48 tunaona kwamba Bwana Msa anamwambia Najum kuwa waende kutoa taarifa polisi ili wasaidiwe, anasema;
                           “Unajua we, sasa twende polisi tukapige ripoti”
Na katika ukurasa wa 49 – 50, mwandishi anaeleza jinsi  Bwana Msa na Najum walipofika stesheni ya polisi na kutoa maelezo yao kwa Inspekta Seif juu ya kifo cha Bwana Ali ambae alitoka alasiri jana na hakurudi kulala na kugundulika kuwa kauawa.
Na katika uk.80, tunaona kwamba kutokana na kujitoa muhanga na nia yao kubwa ya kumpata muuaji, na kufuatilia chanzo cha kifo cha Bwana Ali, mwandishi anasema muuaji alipatikana na keshakamatwa ambae ni Mwarabu mgeni  na sababu yake alisema ya kuwa alimharibia nyumba yake alipokuwa Kongo maana alikuwa na pesa nyingi za kuchezea na kufisidia wake wa watu. 
Katika jamii yetu kuna watu wengi hujitoa mhanga kwa ajili ya kutaka kufanikisha mambo ambayo huwa wameyakusudia. Hivyo mwandishi anatuonesha kuwa kujitoa mhanga ni njia mojawapo ya kuweza kuyafikia malengo ambayo tumeyakusudia na ili kufanikisha malengo, lazima tusikate tamaa, tuvumilie na tujitolea mhanga ili tuweze kuyafikia malengo.
Umuhimu wa kuthamini lugha ya kiswahili.
Hii ni dhamira nyingine ambayo imejitokeza katika riwaya hii. Mwandishi kwa kumtumia mhusika mkuu Bwana Msa ili kutuonesha ubora wa kuthamini lugha yetu na umuhimu wa kutumia kiswahili sanifu katika mazungumzobadala ya kuiga lugha nyingine. Bwana Msa anasema;
              “Lakini katika maelezo yangu nitatumia Kiswahili change mwenyewe, sitaiga Kiswahili
                    cha kibaniani…” katika uk.70.
Lugha ya baniani ni lugha ambayo haina lafudhi na matamshi ya kiswahili mfano mwandishi anasema;
           “Banyani aliruka, kashtuke, kisha akajikaza akasema, ile biashara bana: mi wapi
                     Weza pigana fanga, bana watu naweka rahani bana” ukurasa.66.
 Hii inaonesha jinsi ambavyo mwandishi amekusudia kuasa jamii kutokuiga lugha mbalimbali au kuchanganya lugha na hatimaye kuharibu lugha husika. Katika jamii yetu suala la kuchanganya lugha linatumiwa na wajunzi wa lugha na hata pia wazawa wa luha husika hii hupelekea kudunisha lugha husika na kuibuka kwa lugha ambazo sio rasmi au sanifu mfano mzuri tunaona watu wengi wakichanganya Kiswahili na kiingereza jambo ambalo linasababisha upotoshaji wa lugha sahihi, mfano utamsikia mtu akisema nilikuwaroom, nigei kitabu, lipa buku tusepe, nimepoteza mane, michogo haijakaa freshi, na maneno mengine mengi ambayo yanapotosha lugha husika. Hivyo mwandishi anatukumbusha kuithamini lugha yetu na kuachana na dhana potofu, ambapo wengi huamini kuwa kuchanganya lugha ni ujuzi wa lugha na pia wengine huona kuwa ni usomi, lakini tukitumia lugha ipasavyo tutaidumisha na kuikuza.
Rushwa
Hii ni hali ya kupokea au kutoa kitu ambacho hukustahili kutoa au kupewa ili kusudi uweze kupata, kupewa au kufanyiwa jambo ambalo ni kinyume na utaratibu maalumu. Rushwa kupotosha haki za binadamu na hata kusababisha ukosefu wa ukweli.
Katika riwaya hii suala la rushwa limejitokeza pale ambapo Bwana Msa anaposilia kuhusu Seti kumshirikisha boi wake kumpa kitu kidogo ili kuficha siri ya Seti ya kuchukua sh. 50,000 kwa Bwana Ali alizompa kwa kumuuzia shambaa baada ya Ali kuwa ameuwawa kwa kukatwa panga na mwarabu. Bwana Msa anasema kuwa;
                     “Ulimpa boi wako shauri hili, na ukamrubuni kwa chochote naye akakubali” hapa
                       inaonekana wazi kuwa alipewa hongo ili kuficha siri hivyo” katika uk.74.
Katika jamii suala la rushwa limeenea sana na limepelekea ukosefu wa haki kwa wanajamii na pia kuwanyima walengwa uhuru binafsi wa kusema ukweli. Mfano mzuri mtu hushindwa kusema ukweli au kutoa ushahidi wa ukweli kutokana na rushwa ambayo amepewa hasa katika mahakama mbalimbali, au hata kwenye ofisi mbalimbali.
Dhana potofu na imani za ushirikina.
Mwandishi anaonesha namna ambavyo watu huamini uchawi na namna gani ambavyo mtu akiugua kwa muda mrefu watu husema karogwa mfano mzuri ni Kipwerere mabaye baada ya kuugua sana watu waliamini kuwa;
                   “Karogwa na wachumba waliomhitaji wakamkosa, wengine wakaamini kuwa chanzo               
                    cha ugonjwa wake umedhurika katika kile kichaka kiitwacho “muzimu wa watu wa  
                   kale”  alipokuwa akipita, siku hizo bado kigoli na huku anakula ndizi ya kipukusa; kwa   
                 hiyo shetani wa muzimuni alimshika na kumpanda kichwani, wala hatamtuliza na kumpa
                    nafasi ili apate chano ya ng’ombe Uk11”.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo wazee waliamini kuwa mtoto wao kasibika na shetani, hivyo mwandishi anatutaka tuondokane na imani potofu kwani huchangia kukwamisha maendeleo na kurudisha nyuma uchumi wa taifa. Mwandishi pia anaonesha jinsi ambavyo watu wanachangishana pesa kwa ajili ya kununua ng’ombe wa kutambikia mzimu ili ipate kulala na watu wa kiamboni wapate kutulia, pia anaonesha namna ambavyo watu wana dhana potofu juu ya nyani na kima wanaoishi katika mzimu wa watu wa kale hawapigwi kwa sababu jamii inaamini kuwa ni vizuu vya watu wa ke, hii ni imani potofu. Pia tunamuona Najum na Bwana Msa jinsi wanavyo usujudia mzimu kabla ya kuingia ndani. Hii huhusiana na imani za kishirikina, na hata katika jamii yetu kuna mambo mengi hutendeka kwa ajili ya wanajamii kushikilia mila au imani fulani na kudumaza maendeleo, hivyo ni vyema tukaachana na imani zisizofaa.
Matumizi ya dawa za kulevya
Mwandishi anaonesha namna ambavyo matumizi ya madawa ya kulevya yalivyo na madhara hasa kwa yule anayetumia madawa hayo, mfano mzuri anoonesha uvutaji bangi unavyochangia watu kuchomana visu na hata kupelekea vifo vya watu mbalimbali, mwandishi anaseama;
                        “Boi wa Banyani (Hamisi) anavyovuta bangi anavuta bangi ambazo humpelekea  
                          kupigana visuuk.62.
Pia mwandishi anamuonesha Sufra ambaye ni mvutaji bangi na ambaye amewahi kuwauuwa Sharifu na mwanaye. Mwandishi anasema;
                           “Sufra ni mvuta bangi maarufu, ana duka kubwa la tambuu na sigara. Sufra ndiye   
                             aliyewaua Sharifu na mwanae kwa kuwachoma kisu” uk 63.
Hivyo mwandishi anaonesha madhara yanayotokana na kuvuta bangi na tumbaku, anaonyesha kuwa uchafuzi wa fizi ni mojawapo ya athari zitokanazo na uvutaji tumbaku. Uk.67 mwandishi anasema;
                         “Banyani fizi zake zimechafuliwa na tumbaku anyotumia”.
Katika jamii yetu, suala la madawa ya kulevya limekuwa likipingwa vita kila kunapokucha kwani limeonekana kukithiri sana. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuliangalia na kulikemea, kwani tunaona kuwa matumizi ya madawa ya kulevya yana madhara kwa jamii na hata kwa watumiaji wenyewe.
Matabaka
Hii ni dhamira mojawapo ambayo mwandishi ameizungumzia katika kitabu hiki cha “Mzimu wa Watu wa Kale” mwandishi anaonesha kuwa;
                “‘njia kuu ya magari’ iliigawa Baraste katika pande mbili kubwa kubwa; upande mmoja
                  kuna machunga mazuri yaliyochanganyikana na kichaka kiitwacho ‘mzimu wa Watu wa
                  Kale’ na kuishia karibu na nyumba ya Bwana Ali, na upande wa pili ndiko kwenye
                 maskani ya watu, makonde yao, maduka, soko na stesheni ya askari.” uk.6.
Hivyo kuna matabaka kati ya watu wenye uwezo wa hali ya juu kimaisha  na watu wasio na uwezo  kwani tunaona wazi kuwa watu wasio na uwezo wanaishi Kikwajuni na sehemu za mnazi mmoja lakini watu wenye uwezo wa juu, wenye maduka, waliishi sehemu za Baraste.
Katika jamii yetu pia suala la matabaka lipo, matabaka honekana kuanzia sehemu tunayoishi, makazi na hata kwenye utawala tulionao. Matabaka ni mabaya na ni vema tukawa na umoja na mshikamano tukaondoa matabaka yaliyopo ili tuweze kupata maendeleo. 
Mapenzi na ndoa
Katika kujandili suala la ndoa mwandishi anaonesha kuwa kuna ndoa ya kulazimishwa au ndoa ya kuchanguliwa mume. Mfano mzuri ni kipwerere ambaye anaolewa na mtu mbaye sio changuo lake (Bwana Ali) kwani Bwana Ali alimuoa kipwerere kutokana na mali alizokuwa nazo baada ya kuelewana na wazazi wake tu lakini kipwerere mwenyewe hakumpenda Bwana Ali kama mwandishi anavyosema;
                    “Lakini sijui kwa sababu ya mali maana ukiwa na mali huko sio bahati, wote wale
                      waliokuwa wakimkamia kumwoa walirushwa wasimpate, akaja Bwana Ali…”uk.9.
Kutokana na mapenzi haya yasiyo ya dhati kipwerere aliishi kwa Bwana Ali pasipo kupata furaha ya ndoa kwa muda wa miaka kumi na hivyo kuonekana muda wote akisononeka kama mwandishi anavyosema;
                      “miaka kumi tena sasa tangu kipwerere yuko kwa mumewe lakini muda wote huo
                      alikuwa akisononeka tu, mgonjwa si mgonjwa, mzima si mzima…” uk.9-10.
Haya maelezo yanasawiri vyema jinsi kipwerere alivyokosa raha akiwa kwenye ndoa. Aidha yote haya yalisababishwa na ubahiri wa mumewe (Bwana Ali) kiasi cha kutokumjali mke wake hata katika masuala muhimu kama vile matibabu kama asemavyo mwandishi;
                  “na kwa hiyo kila dhofu lihali likizidi kumkondesha kipwerere, wazee wake humshika
                    mumewe Bwana Ali, atoe ngombe mmoja ili apewe chano mtoto wao, apate kupumzika,
                   lakini Bwana Ali huzidi kuwapa ahadi za mbele tu, mwaka baada ya mwaka mpaka leo
                   uk.10”.
Kutokana na ubahiri huo kunasababisha kukithiri kwa ugonjwa wa kipwerere hivyo kuthibitisha kuwa Bwana Ali hakuwa na mapenzi ya dhati kwa mkewe. Kwa hiyo mwandishi anaonesha dhahiri kuwa hakukuwa mapenzi ya dhati kati ya Kipwerere na mumewe Bwana Ali.
Hivyo basi katika jamii yetu ya leo ni dhahiri kuwa hakuna mapenzi ya kweli baina ya wanandoa kwa sababu kuna udanganyifu mwingi katika ndoa na pia ndoa nyingi hazidumu kutokana na kuosekana kwa mapenzi ya dhati baina ya wanandoa. Hivyo basi ni vyema tukiwa na mapenzi ya dhati kwa wake zetu na waume wetu ili kusudi tudumishe ndoa na uaminifu katika familia na jamii kwa ujumla.
Athari za kulipiza kisasi (kuwa na fitina).
Kisasi ni hali ya kumfanyia mtu kitu kibaya kwa ajili ya kulipa mabaya ambayo aliwahi kukufanyia. Mfano katika riwaya ya “Mzimu wa Watu wa Kale” Bwana Ali ameonekana kuwa alikuwa anaishi Kongo pamoja na Waarabu. Bwana Ali alikuwa na mali nyingi ambazo alidhulumu kutoka kwa Waarabu na kukimblia Unguja. Baada ya muda Bwana Ali alisikia kuwa moja kati ya Waarabu hao ameingia Unguja, Bwana Ali aliuza mali zake zote kwa bei ya chini ya shilingi 60,000 ili aweze kukimbia. Mfano mwandishi anasema;
                “Mimi Ali bin Boman,nakiri kuwa nimestakabadhi kwa Seti B. Sumatra, shs.50,000/-  leo  
                 na zimebaki 10000 nita stakabadhi kesho mjini” katika uk 30.
Baada ya kuuza mali Bwana Ali ameonekana kuuawa kwa kukatwa kichwa uk73. Vivyo hivyo katika jamii zetu za sasa kuna watu wenye tabia za kulipiza visasi kwa mabaya wanayotendewa. Kutokana na tendo hilo mwandishi anatufundisha kuwa si vizuri kulipa visasi.
Nafsi ya vyombo vya dola
Vyombo vya dola ni pamoja mahakama, serikali, na polisi. Vyombo vya dola hushirikiana na wananchi kusaidiwa wanapopatwa na matatizo. Katika riwaya hii nafasi ya vyombo vya dola inaonekana kwani tunaona Inspekta Seif na askari Chombeko wanaambatana na Bwana Msa na Najum kufanya utafiti ili wajue ni nani hasa amehusika katika mauaji ya Bwana Ali. Wanashirikiana hadi kugundua kuwa aliuawa na mwarabu mgeni wa Mmanga kutoka kongo mbaye alimkata panga shingoni na kutenganisha kiwiliwili na kichwa, pia katika kuangalia nafasi ya vyombo vya dola tunaona Inspekta Seif akimwambia Bwana Msa aichie polisi uchunguzi katika kupima ni hatua ngapi kutoka kichwa kilipoa hadi maiti ilipo kama anavyosema uk.
             “mfano kutoka katika kitabu”
Katika jamii tunaona wazi kuwa serikari nayo ina jukumu la kusaidiana na wanancihi wake katika kutatua matatizo mbalimbali pia kuhakikisha usalama wa kila raia ili kujenga taifa lenye umoja na mshikamano. Hivyo ni jukumu letu kutambua nafasi ya vyombo vya dola na kushirikiana nao ili kuondoa na kutatua matatizo yalipo katika jamii.  
Suala la dini
Katika riwaya hii tunaona kuwa kuna dini iitwayo kibanyani ambapo haimrusu mtu kuua maana baada ya Bwana Msa kuelezea ukweli juu ya kifo cha Bwana Ali, Banyani anafurahi kutolewa kutoka dhambi ya mauaji ya Bwana Ali, mwandishi anasema;
               “diyo bana iyo bana kwa hakika kuwa katika dini ya kibanyani, zaidi kuliko katika dini
                  nyinginezo ni dhambi zisikuwa na mfano” uk74
Kwa hiyo tunaona hii dini inakwenda kinyume na inatenda mambo mengine kinyume kwani tumeona kuwa katika dini hii ni dhambi zisizokuwa na mfano, kwa hiyo mwandishi anashauri kuwa na dini nyingine lakini sio hii dini ya kibanyani dini ambayo hutoa kafara juu ya mzimu. Katika jamii yetu leo tunaona kuwa dini nyingi sana zimeenea sana, na kila mmoja huamini kuhusiana na dini anayohudhuria.  
Mila na desturi
Mila na desuri katika riwaya hii  huhusu jamii ya watu wa kiamboni na huendeshwa kwa kufuata utaratibu unaohusisha utoaji wa kafara na matambiko ya mizimu katika mzimu wa watu wa kale. katika kutoa kafara, watu huchanga pesa ili kununua n’gombe wa kuchinja ili mizimu iweze kutulia. Mwandishi anasema;
                      “Mpaka uje wakati na wao waone ni mno tena, mizimu haitulii mpaka itambikiwe”
Hata kwenye jamii yetu kuna watu hufanya kafara mbalimbali ili kufanikisha mambo mbalimbali. Hivyo basi mwandishi anaonesha namna ambavyo tunakosa maendeleo kwa kutumia pesa kwenye mambo ya kiimani. Hivyo ni vyema tukaondokana na mila zilizopitwa na wakati.
Umuhimu wa elimu
Elimu ni maarifa, ujuzi au mwelekeo anaoupata mtu kutokana na chanzo kimoja hadi kingine, kwa njia ya kusoma, kusimuliwa, kufundishwa au hata kuona. Elimu ndio chombo kikuu cha ukombozi wa mwanadamu dhidi ya unyonyaji, umasikini, rushwa na hata ukandamizaji.
Katika hii riwaya kumejitokeza elimu za aina mbalimbali mfano mwandishi anasema;
                 “Bwana Msa alikuwa na elimu za siri za aina mbili, yaani elimu ya ndoto na elimu ya na
                   kivuli”
Ambapo Bwana Msa alitumia elimu ya ndoto katika kuona mambo yaliyo mbali na upeo wa macho ya kawaida ya mwanadamu mfano kuhusu kifo cha Bwana Ali. Pia alikuwa na uwezo wa kufasili vivuli, kusoma kiarabu japokuwa hakuwa mwarabu (uk.28). Pia Najum naye alikuwa na elimu na ndio maana aliweza kucheruka juu ya karatasi iliyoonesha kuwa haina sahihi na tarehe kuwa sio halali, uk.30. Pia umuhumu wa elimu inaoneshwa uk.40, uk.52 na uk.54 katika toleo la mwaka 1971. Hivyo mwandishi anaonesha kuwa elimu huleta maendeleo na bila elimu hakuna maendeleo. Katika jamii tunaona wazi kuwa jamii nyingi zimeelimika na kupata elimu, japokuwa elimu ambayo tunayo hatuitumii ipasavyo ili kuleta maendeleo mfano katika kuunda katiba mpya elimu ya hali ya juu inahitajika ili kujenga misingi ambayo taifa litaitumia katika kuleta maendeleo na kuondoa umasikini, unyonyaji na hata rushwa ambayo ni adui wa maendeleo. Hivyo basi ni vyema tukatumie elimu ambazo tumezipata katika maisha yetu kwa ujumla kwa kufanya hivyo tutakuwa na maendeleo ya hali ya juu.
Wizi
Ni kitendo cha kuchukua mali ya mtu mwingine kwa siri na kujimilikishia. Katika riwaya hii suala la wizi linaonekana pale ambapo
RIWAYA ZINAZOFANANA NA RIWAYA HII KIMAUDHUI:
Hii riwaya inafanana na riwaya nyingine kama vile;
Ø  Simu Ya Kifo (EALB 1965), iliyoandikwa na Katalambula
Ø  Kisima Cha Giningi (Evans 1968), iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø  Duniani Kuna Watu (EAPH 1973), iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø  Siri Ya Sifuri (EAPH 1974), iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø  Mwana Wa Yugi Hulewa (EAPH 1976), iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø  Kijacho Chembamba (Tamasha 1980), ilyoandikwa na Ganzel, E
Ø  Dimbwila Damu (AP 1984), iliyoandikwa  na Ben Mtobwa
Ø  Kosa la Bwana Msa (AP 1984), iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø  Mauaji Ni Nani (Jomssi 1987), iliyoandikwa na Simbamwene
Ambazo huzungumzia kuhusiana na upelelezi (Mlokozi, 1996).
HITMISHO.
Kwa ujumla riwaya hii huzungumzia masuala ambayo yanajitokeza katika jamii. Mambo haya yanadumu kwa vipindi tofauti tofauti, kutoka kipindi cha uhuru mpaka leo hii masuala ya umasikini, uchoyo, uzembe kazini, wizi, rushwa, dhuluma, suala la ukosefu wa upendo wa dhati katika ndoa na mambo mengine kama vile fitina yamekuwa yakiikumba jamii na kusababisha kurudisha maendeleo nyuma, hivyo basi ni bora jamii ikaelimishwa na kuachana na haya masuala kwani yanapoendelea amani inakosekana na kusababisha kukosekana kwa umoja miongoni mwa wana jamii na kufaya taifa au wanajamii kutopiga hatua katika sauala zsima la maendeleo.
MAREJELEO
Senkoro F.E.M.K (1987). Fasihi na Jamii: Press and Publicity Center, Dar es salaam.
Senkoro F.E.M.K (2011). Fasihi: Kampuni ya Utamaduni, Tafsiri &Uchapishaji, KATTU,
                Dar es salaam.        
Muhammed Said Abdulla (2008). Mzimu wa Watu wa Kale: Kenya Literature Bureau, Nairobi.
Mlokozi, M.M (1996). Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania: TUKI, Dar es salaam.
Powered by Blogger.