FASIHI SIMULIZI
FASIHI SIMULIZI
Madhumuni ya Kozi:Madhumuni ya kozi hii ni kuwawezesha wanafunzi kupata welewa wa dhanna, nadharia na uchambuzi wa fasihi simulizi. Kozi hii ni ya lazima kwa kila mwanafunzi anayesomea digrii ya ualimu. Mwanafunzi anashauriwa kusoma kozi hii baada ya kusoma kozi ya (Fasihi ya Kiswahili Nadharia na Uhakiki) ambayo itampa utangulizi wa fasihi kwa ujumla. Wanafunzi wengine wanaweza kusoma tu kwa malengo na upendeleo wao.
MUHADHARA WA KWANZA : FASIHI SIMULIZI KWA UJUMLA Ufafanuzi/tafsiri ya fasihi Fasihi simulizi kwa mujibu wa Mulokozi (1996), ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Hivyo fasihi simulizi inafungamana na muktadha au mazingira fulani ya kijamii na kutawaliwa na muingiliano wa mambo kama vile Fanani, Hadhira, Fani inayotendwa, Tukio, Mahali pamoja na Wakati wa utendaji.
Balisidya (1983) anasema fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.Materu, M (1983) anasema fasihi simulizi ni aina ya fasihi inayotumia mdomo kwa kuumba na kusambaza. Fasili zote zinazungumzia kitu kilelekile kwamba fasihi simulizi inategemea sana uwepo wa fanani, hadhira, jukwaa na mada inayotendwa. Hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya kisanaa ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa kwa njia ya mdomo au masimulizi. Kwa upande wa nadharia, tunaweza kusema kuwa nadharia, ni mawazo au muongozo unaomuongoza mtafiti au mchambuzi wa jambo fulani ili kuweza kulikabili jambo hilo ambalo halijapata kupatiwa ufumbuzi au ukweli wake. Kutokana na vigezo vya Mazrui tunaweza kusema kuwa; fasihi ni utumiaji wa lugha kisanaa kubainishia taratibu za maisha kwa njia ya kubuni. Fasihi kwa ujumla ni aina ya sanaa kama uchongaji, uchoraji, ususi na ufinyanzi. Kila mwanasanaa huwa na malighafi (nyenzo) ambayo huitumia kuunda sanaa yake. Kwa mfano: - Sanaa ya uchoraji – hutumia brashi, wino na karatasi. - Sanaa ya ufinyanzi hutumia udongo na maji. Fasihi hutumia mdomo au maandishi ili kutoa picha halisi ya mwanadamu katika maisha na mazingira katika kupiga hatua kimaendeleo. Nadharia ya fasihi simulizi ilianza katika elimu ya ushairi wa Wagiriki toka karne ya 18. Mnamo karne ya 20 nadharia za fasihi simulizi zimezua mikabala mikubwa katika usomaji wa matini. Kwa hiyo nadharia ya fasihi simulizi ni mawazo yanayotoa muongozo kuhusu muelekeo wa jambo fulani katika fasihi simulizi. Kwa kufanya hivyo nadharia hizo zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo kwa mfano utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, jando na unyago umeathiriwa na ujio wa wageni. Aina za fasihi Mintaarafu aina za fasihi twaweza kuzigawa kwa vigezo viwili, kigezo cha kwanza kiwe maandalizi na kigezo cha pili kiwe namna ya uwasilishaji. v Kigezo cha maandalizi Kigezo hiki kinatupatia aina mbili za fasihi ambazo ni: fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili (Rejelea: Fasihi ya Kiswahili Nadhariya na Uhakiki) v Kigezo cha uwasilishaji nacho kinatupatia aina mbili za fasihi ambazo ni: fasihi simulizi na fasihi andishi.
Sifa za fasihi- Hutumia lugha kisanaa- maneno yanayotumiwa katika fasihi huwa ni teule na yenye usanii ndani yake. - Utumiaji wa msamiati na miundo ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuibua hisiya kama vile: furaha, hasira, huzuni, huruma, n.k - Utumiaji wa lugha ndio huleta tofauti kubwa kati ya lugha ya kifasihi na lugha ya kawaida. Asili ya fasihi Kirumbi (1976) anaeleza kuwa; Fasihi humtazama binadamu na uhusiano wake na binadamu wengine, mazingira yake pamoja na viumbe wengine. Mfano: katika furaha, huzuni na misiba ni jinsi gani anachangamana na wenzake? Maoni hayo ya Kirumbi yanaungwa mkono na Nkwera (1978), yeye anasema kuwa; Fasihi ni chombo au nyenzo itumiwayo kumpa mwanadamu muongozo wa maisha yake. Vigezo vitumikavyo kubainishia fasihi 1. Kuielewa jamii na mazingira yake kijiografia, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. 2. Kuelewa matatizo ya jamii husika 3. Kuelewa migogoro ya kitabaka na kiuchumi Fasihi humtazama mwanadamu na mazingira yake na kumfanya aweze kuyatumia kwa manufaa yake. Dhumuni/lengo la fasihi ni kumfanya mwanadamu aweze kufikiria hatua ambazo anapaswa kuzichukua dhidi ya mazingira yake ili apate ahueni kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kiango na Sengo (1977) pamoja na Kirumbi (1976) wanaamini kwamba chanzo cha fasihi ni HISI (Hisiya) za mtu mmoja au wengi katika jamii. Hisi hizi huibuka katika mazingira mbalimbali kama vile sherehe za harusi, matanga, kilimo, n.k Fasihi hufafanua maisha ya binadamu katika mazingira hayo kwa kutumia nyenzo ya lugha. Fischer (1959) na Mbele (1982) wanadai kuwa chanzo cha fasihi ni kazi. Mbele anaeleza kuwa kuna ithibati kwamba binadamu walianza kuwasiliana katika kazi. Mawasiliano hayo yalijikita katika harakati za kuunda zana za kufanyia kazi. Katika mazingira hayo fasihi iliibuka kama chombo cha kumjenga binadamu kimwili na kiakili huku akijitofautisha na viumbe wengine. Mawasiliano ya awali yalikuwa ya mdomo. Jukumu/dhima ya fasihi Fasihi inatakiwa kimsingi izingatie mambo makuu mawili ambayo hujigawa katika vipengele vidogovidogo. - Kuelimisha - Kusisimua 1. Kuelimisha; katika kuelimisha fasihi hukuza na kuendeleza stadi za lugha na kuipa jamii muelekeo. Ø Huhifadhi amali za jamii Ø Huunganisha vizazi mbalimbali pamoja na kufunza. Ø Huchochea mwamko wa jamii kujiletea maendeleo kwa kufanya kazi 2. Kusisimua; fasihi huburudisha, hukuza ushirikiano, hufanya jamii ijisahaulishe mambo magumu na mazito yaliyowahi kutokea katika jamii hiyo. MUHADHARA WA PILI: MAANA YA FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni nini? Hadi sasa kuna tafsiri nyingi juu ya dhanna ya fasihi simulizi kutokana na kutoafikiana kwa wataalamu wa fasihi. Kirumbi (1975) anasema: fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo. Katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kucheza na lugha). Kwa maelezo ya Kirumbi ni kwamba chombo cha kutongolea fasihi simulizi ni midomo na kwa hiyo katika fasihi simulizi tunakuwa na masimulizi. Kuna baadhi ya wataalamu wanadai kuwa fasihi simulizi ni masimulizi ya kale ambayo hurithishwa kizazi kimoja hadi kingine. Kwa baadhi ya watu fasihi simulizi hufungamanishwa na masimulizi ya mambo ya kale. Kwa jina la kashifa fasihi hii huitwa fasihi ya kimapokeo. Baadhi ya wanafasihi hudai kuwa istilahi yenyewe ina mgogoro hivyo wanataka Istilahi mbadala itumiwe badala ya Simulizi. Kezilahabi (1989) anasema; fasihi simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhanna ya fasihi itolewayo kwa mdomo bila kuandikwa. Istilahi hii ina dosari kwani neno simulizi halina maana ya kinachosemwa –oral- bali ni kitu kinachosimuliwa –narrative-. Hivyo tafsiri ya fasihi simulizi katika kiingereza ni –narrative literature- sio –oral literature-. Pamoja na mgogoro huu kikubwa kufahamu ni kuwa fasihi simulizi ni utanzu mmoja wa fasihi. Na fasihi simulizi ni sanaa ya masimulizi na matendo inayofikisha ujumbe kwa hadhira iwe ni kwa kuimba, kutenda au kuzungumza. Fanani katika fasihi simulizi hufaulu kutoa picha halisi ya dhanna anayoikusudia iwe ni huzuni, furaha, kuchekesha au kusononesha. Katika usimuliaji fanani hujitathmini kama anafaulu au la kwa kuitazama hadhira yake. Hali hii humsaidia kubadili mbinu za usimuliaji, vilevile fanani huweza kushirikisha hadhira yake na kuleta uhai katika masimulizi yake. Vipengele muhimu vya fasihi simulizi (a) Msimuliaji (fanani); huyu ni mtendaji wa tukio la kifasihi mbele ya hadhira. Tukio laweza kuwa kutamba hadithi, kuimba wimbo au kutoa kitendawili au methali. Huyu ni muhusika anayesana kazi ya fasihi. (b) Hadhira; hawa ni walengwa wa kazi ya fasihi ambao husikiliza na kutazama kinachotendwa na fanani. Hadhira hushiriki kwa namna fulani kwenye kile kinachotendwa iwe ni kuitikia wimbo au kupiga makofi, kutingisha kichwa au mwili. Hadhira humsaidia fanani kujitathimini juu ya kile anachokitenda na mbinu ya utendaji anayoitumia. (c) Mandari; hapa ni mahali ambapo matukio ya kifasihi yanatendekea. Mandhari huweza kuwa uwanjani, kichakani, chini ya mti mkubwa au mlimani. (d) Tukio; hili ni tendo au tukio linalotendwa na fanani kifasihi. Tendo hili laweza kuwa usimuliaji hadithi, vitendawili, kuimba au kutoa methali. Kwenye fasihi simulizi kuna falsafa na mantiki ambayo haipaswi kusahauliwa wala kudharauliwa. Sengo na Kiango (1977) wanasema; fasihi huweza kulinganishwa na mwamvuli unavyokinga amali za maisha ya watu.
Umuhimu wa fasihi simulizi(i) Ni chombo cha kuwaunganisha watu kupitia sanaa zake (ii) Huchochea shughuli za uzalishaji mali kwa kuhimiza kazi (iii) Hutumika katika harakati za kuleta maendeleo kwa jamii kupitia kampeni mbalimbali mf: upangaji wa uzazi, kuhusu ukimwi, n.k (iv) Huhifadhi na kuleta pamoja tamaduni mbalimbali za jamii katika vipindi tofauti. (v) Hueleza ukweli kwa kuchambua na kuhakiki vipengele vya maisha (vi) Ni nyenzo ya kupitishia hekima na maarifa kizazi hadi kizazi. MUHADHARA WA TATU: FASIHI SIMULIZI NA UANDISHI Tangu kutawala kwa fasihi andishi Ulaya, Asia na kutumiwa na wenye nguvu za kisiasa na kiuchumi fasihi simulizi ilidharauliwa ikatwezwa, ikadunishwa na kushushwa hadhi huku fasihi andishi ikitukuzwa na kuendelezwa. Taaluma ya fasihi simulizi hivi leo inashughulikiwa kwa nguvu nyingi ili kuondokana na fikra duni zilizorithiwa toka kwa wataalamu wa kigeni kuwa sanaa kongwe ya fasihi simulizi ni ya kishenzi. Pamoja na dharau juu ya fasihi simulizi bado ukweli unabaki kuwa sanaa hii ndiyo ghala halisi la fasihi andishi. Hata sasa imebainika kuwa tenzi za Kigiriki zinazodaiwa kutungwa na manju aitwaye “Home” hazikuwa zimeandikwa kwa zaidi ya miaka miatano (500) ndipo baadaye zikaja kuhifadhiwa katika maandishi. Hivi majuzi pia wanateknolojia wameanza kukubali kuwa sehemu kubwa ya Biblia ni fasihi simulizi ya Wayahudi walioishi zama mbalimbali. Wanazidi kueleza kuwa imebainika kuwa fasihi hiyo haikutoka mbinguni bali mizizi yake ni katika jamii ya Wasumuri (Mesopotamia), Waajemi na Wagiriki. Hoja ya msingi ni kuwa fasihi andishi haijaibua dhamira mpya, zote ni zilezile ambazo zilijitokeza katika masimulizi. Mfano: Mapenzi, siasa, unyonge wa wanawake, ukombozi, uchawi na ushirikina, uzazi, ndoa na migogoro ya kitabaka. Misemo ya fasihi simulizi haijapitwa na fasihi andishi wala fani yake haijabadilika mpaka leo. Kimsingi fasihi simulizi na fasihi andishi ni kitu kimoja isipokuwa njia zinazotumiwa na fanani na hadhira katika kuwasilisha ujumbe. (i) Fanani wa fasihi simulizi hutumia mdomo, sauti, vitendo na muziki wakati fanani wa fasihi andishi hutumia karatasi na wino. (ii) Fasihi simulizi huweza kuwasilishwa kupitia maandishi na fasihi andishi huweza kutumia ala za fasihi simulizi kunogesha kazi yake na kufikisha ujumbe wake. Hivyo maandishi sio kigezo cha kuitenganisha kabisa fasihi simulizi na fasihi andishi. (iii) Matumizi ya taarabu na nyimbo za kiasili katika fasihi andishi ni uthibitisho kuwa fasihi simulizi bado inapendwa na haiwezi kufa bali kubadilika umbo tu ili kuiwezesha kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. (iv) Ukichunguza kazi mbalimbali za fasihi andishi utabaini kila mwandishi ameathiriwa na fasihi simulizi kwa namna fulani. Wapo walioathiriwa kifani na wengine kimaudhui.
Kifani Hapa tunao watunzi kama Ibrahim Hussein (Mashetani na Kinjeketile), Penina Mhando (Pambo na Lina Ubani), Shaaban Robert (Adili na Nduguze), Mohamed Said Abdullah (Mzimu wa Watu wa Kale).
Waandishi wote hao wametumia wahusika wa kifasihi simulizi kama wanyama, majitu, mazimwi na mapango.
Kimaudhui Ukichunguza kazi nyingi za fasihi andishi utagundua kuwa maudhui yake ni ya kifasihi simulizi. Vichwa vya hadithi zao ni methali fulani toka fasihi simulizi. Mfano: - Mwerevu hajinyoi - Baada ya dhiki faraja - Lila na fila havitangamani - Mwana umleavyo ndivyo akuavyo, n.k
Tanzu za fasihi simulizi za kihadithi Kuna makundi mawili makuu ya tanzu za fasihi simulizi. - Kundi moja linahusika na tanzu zenye mwelekeo wa kishairi na kundi lingine ni lile linaloshughulikia tanzu za kinathari zenye sifa za kihadithi. Tanzu za kinathari ni zile zote zinazojumuisha matumizi ya lugha ya kawaida ya maongezi na yenye mjazo. Mfano: Hadithi yoyote iliyotungwa kwa mpangilio wa visa na matukio katika namna inayochukuana na kuleta muwala (mtiririko). NGANO Ngano zinaelezwa kuwa ni hadithi za “paukwa pakawa” wakaishi raha mustarehe. Maana hii imezingatia zaidi mianzo na miisho ya ngano kutokana na tanzu nyingine za fasihi simulizi. Mara nyingi ngano huambatana na nyimbo ambazo hutumiwa kuwasilisha ujumbe, kubadili mandhari ya wahusika au kuchapuza hadithi na kinachotendeka. Vilevile nyimbo huweza kutumiwa kama kiliwazo katika kulegeza mtiririko na upeo wa matukio yanayotambwa katika ngano. AINA ZA NGANO Ngano hugawanywa katika aina mbalimbali kulingana na vigezo vitumikavyo. v Kwa kigezo cha wahusika tunapata aina mbili ambazo ni Hekaya na Kharafa/Khurafa. i. Hekaya – ni ngano ambazo wahusika wakuu na muhimu ni binadamu. Hekaya hutumiwa kuonesha jinsi watu wa tabaka fulani walivyo na hekima na busara kwa kiasi kikubwa. Mfano: Hekaya za Abunuwasi. ii. Khurafa/Kharafa- ni hadithi ambazo wahusika wake wakuu ni wanyama na wahusika wasio na uhai kama miti, mawe, majitu, n.k.
v Kwa kigezo cha matukio tunapata ngano kama vile: - Ngano zinazohusu matukio ya kijamii, mfano Waluya na Wapangwa ni makabila yenye historia zinazoelekeana sana. Ngano yoyote toka jamii hizi huchukuliwa kuwa ni ngano za aina moja kwa sababu zinahusu matukio yanayogusa historia za jamii hizo.
Tatizo la kuzingatia kigezo hiki ni tofauti ya mtiririko kama mizani ya kutambulia ngano kwa kuwa ngano hizo zinaweza kuwa na matukio na mtiririko unaoelekeana lakini zikatofautiana katika mianzo na miisho yake. v Kigezo kingine ni kutumia wahusika vikale, dhanna hii inahusu aina fulani ya mtiririko. Wahusika au picha kongwe inayojitokeza mara nyingi hutumika kama kigezo. Mfano: mtu kunyanyaswa na kufaulu baadaye. Hawa huitwa wahusika vikale. Kwa namna ingine wahusika vikale ni wale ambao hawategemei nguvu za miili yao katika kushinda bali hutumia akili, ujuzi na maarifa kwa kiasi kikubwa na hatimaye hushinda. Mifano ya wahusika hawa ni Sungura,Kobe,Nyoka, n.k UAINISHAJI WA NGANO KWA MUJIBU WA VLADMIR PROPP Propp aliainisha ngano kwa kuzingatia muundo wa ngano yenyewe akitumia Nadharia ya urasimi, nadharia hii iliasisiwa na Vladmir Propp (1928,1968) katika kitabu chake cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vyema kuanza kuchunguza aina za ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika. Ubora wa nadhairia hii, nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s) Udhaifu wa nadharia hii, nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake. Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na wahusika wasiowaerevu/wajinga mfano fisi.
MUHADHARA WA NNE: VISAKALE (TARIHI) Kisakale ni hadithi inayohusu matukio yaliyowahi kutokea zamani. M.M. Mulokozi anasema visakale ni masimulizi ya kimapokeo juu ya wahenga na mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya “chuku” na historia. Aghalabu kadhia zinazosimuliwa kwenye visakale ni kama vile njaa, kiangazi, magonjwa ya kuambukiza, uhamaji na vita. Wahusika wengi wa visakale ni binadamu wenye uwezo mkubwa au mdogo kutegemeana na mantiki wanayowekewa. Visakale hufananishwa sana na tendi kwa sababu vyote kwa pamoja huhusu masimulizi ya kishujaa. Mfano wa kisakale ni: Kisa cha Liyongo ambacho kinashabihiana sana na utendi wa Fumo Liyongo kwa kuwa vyote huzungumzia ushujaa. Tofauti kubwa ni kuwa kisakale cha Liyongo ni utanzu wa kinathari na utendi wa Fumo Liyongo ni utanzu wa kinudhumu (kishairi). MUHADHARA WA TANO: VISASILI Visasili ni hadithi zinazohusu mianzo ya maumbile, tabia au matendo fulani. Mathalan mianzo ya matendo kama vile ndoa, tohara na imani mbalimbali. Mara nyingi visasili hutumiwa katika lugha ya kimafumbo. J.G. Frazer anasema visasili ni upangaji wa matukio kinathari ambapo hapo awali matukio haya yalihusishwa na matukio kama sherehe, uganga, uchawi na uramli. Ni hadithi inayobuniwa kueleza juu ya ada fulani ilivyoanza. Hivyo kisasili huwekea mantiki tukio la kiada,chanzo chake na jinsi lilivyopokelewa na vizazi mbalimbali katika jamii inayohusika. Okpewho (1983) anadai kwamba asili ya kisasili hubadilika kulingana na mapito ya wakati kwa sababu ya usahaulifu wa watu wanaopaswa kukumbuka na vilevile kwa sababu ya mageuzi yanayoweza kutokea katika mazingira yao. Mabadiliko haya ni lazima yatatanishe toleo la kisasili cha asili. Tunaposonga nyuma katika mapito ya wakati uhakika wa kisasili hubainika zaidi. Kisa cha mwanzo kina ukweli zaidi kikilinganishwa na kisa cha hivi karibuni zaidi ikiwa tendo linalosimuliwa katika kisasili fulani lilifanyika juzijuzi halina budi kuripotiwa kwa uaminifu zaidi kwa sababu washiriki katika tendo hilo watashadidia ushuhuda wa kweli kuhusu tendo hilo. Hivyo umbuji wa mtambaji huchangia ukweli au uzushi unaopatikana katika kisasili fulani. Kwa ujumla maoni ya wengi yanaafiki kuwa kisasili ni ukweli uliokolezwa na uzushi kama hamna uzushi hicho hakiwezi kuwa kisasili. Mfano wa kisasili ni: Kisasili cha Samsoni Hiki ni kisasili kinachotoka katika Biblia, Agano la kale kitabu cha Waamuzi sura ya 13-16. Kisa kinaeleza kuzaliwa kwa shujaa Samsoni hadi kufa kwake. Kisasili kinaanza kwa kueleza jinsi Manoa ambaye alikuwa akiishi na mkewe aliyekuwa tasa yaani alikuwa hana uwezo wa kuzaa mtoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke na kumweleza kuwa atachukua mimba na atazaa mtoto mwanamume hivyo alikatazwa asitumie vileo wala divai kwani huyo mtoto atakuwa mnadhiri wa Mungu pia alikatazwa asimnyoe nywele hata siku moja. Basi mwanamke alimweleza mumewe na baadaye Manoa alimwomba Mungu amwelekeze namna ya kumlea huyo mtoto. Kisa kinaendelea kutueleza juu ya yule malaika kwani alitokea tena na kuwaelekeza cha kufanya na mwishowe mtoto mwanamume alizaliwa na kupewa jina la Samsoni. Mtoto akakua na Bwana akambarikia Samsoni. Muda wa kuoa ulipowadia Samsoni alienda kuoa mwanamke wa Timna mojawapo wa binti wa kifilisti na wakati huo Israeli walikuwa wanatawaliwa na Wafilisti. Wakati Samsoni alipokuwa anaenda Timna alikutana na simba lakini alimuua kwa mikono yake mwenyewe kwa kumpasua kama mwanambuzi. Basi kisasili hiki kinaendelea kutueleza mambo yaliyokuwa ya ajabu ajabu yenye nguvu za ziada kama vile kuwaua wanaume thelathini na kuzitwaa nyara zao ili kuwapa wale ambao walitegua kitendawili chake. Aliweza kuwakamata mbweha mia tatu na kuwafunga wawili wawili vienge kisha kuwasha moto na kuwaachia na waliweza kuteketeza mashamba ya ngano na mizeituni ya Wafilisti. Kisa hiki pia kinaeleza anguko la shujaa huyu aliyeweza kunaswa na Delila mwanamke kahaba wa kifilisti aliyeweza kumshawishi amjulishe siri ya nguvu zake na baada ya upelelezi mwingi shujaa huyu alijikuta akimweleza kuwa tangu kuzaliwa wembe haukupita kichwani mwake na ndipo Delila alipomnyoa nywele zake zote na Wafilisti waliweza kumkamata na kumtoboa macho yake mawili. Siku ya kifo chake ilikuwa ni sherehe ya Wafilisti ya kumshukuru mungu wao Dagoni kwa kuwawezesha kumkamata adui yao Samsoni hivyo walimleta mbele ya wakuu na viongozi mbalimbali pamoja na watu wengi sana. Hapo Samsoni nywele zake zilishaanza kuota hivyo alishikilia nguzo mbili zilizokuwa zimeshikilia jengo lile na kuanza kuzisukuma na jengo lile lilianguka akafa na watu wengi kuliko aliowahi kuwaua enzi za uhai wake. Mwisho mwandishi anaeleza kuwa Samsoni alikuwa mwamuzi wa taifa la Israeli kwa muda wa miaka 20. MUHADHARA WA SITA: AINA ZA HADITHI Istiara, Mbazi na Kisa (a) Istiara Ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine isiyo ya wazi. Ni masimulizi ya kiishara yenye kutumia wanyama au taashira za aina mbalimbali zinazowakilisha wanyama hao. Hadithi kama za sungura,majitu na kobe huwa zinawakusudia watu. Hadithi hizi hutumia wanyama kama vielelezo vya sifa na tabia za binadamu. Baadhi ya wataalamu wa sanaa waliotumia sana Istiara ni Shaaban Robert katika Adili na Nduguze, Kufikirika na Kusadikika. Katika kazi hizo vitu, watu na wahusika vinasimamia mawazo na adili fulani maalumu. (b) Mbazi Ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama mfano wakati wa maongezi au kumwonya mtu. Mwalimu aliyevunja rekodi katika matumizi ya aina hii ya hadithi alikuwa Yesu Kristo. Alitumia mbazi kwa kiasi kikubwa kuwaelekeza wanafunzi wake na walimwengu katika mafundisho yake.
Mfano wa mbazi ni huu: Kiongozi mmoja wa kitaifa alikuwa akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki katika kulinda usalama na amani nchini badala ya kuona suala hilo ni la watu fulani tu hasa vyombo vya ulinzi na usalama. Katika msisitizo wake huo akatoa mbazi ifuatayo............. siku moja katika nyumba fulani panya aligundua kuwa ametegewa mtego na kwa kuwa hakuweza kuutegua alienda kuomba msaada kwa ng’ombe lakini ng’ombe alikataa akidai kuwa huo ni mtengo wa panya yeye haumuhusu. Panya hakuchoka akapiga hodi kwa mbuzi na kumlilia shida yake, mbuzi naye akamjibu kama alivyojibu ng’ombe kuwa huo ni mtego wa panya wala haunihusu. Hatimaye panya akamwendea jogoo na kueleza yote lakini jogoo naye alimkatalia panya na kumkejeli kuwa huo mtego hamhusu yeye jogoo. Baada ya kugonga mwamba panya akakosa amani akihofia mtego ulioitwa.. “ ...wa panya..” kwa kweli siku nzima ile panya hakuweza kujipatia riziki akihofia mtego. Usiku ulipofika baba mwenye nyumba alishituliwa na mkewe akiambiwa kuwa mtego umefyatuka na bila shaka panya atakuwa amenaswa. Baba yule akakurupuka na kuuendea mtego huku akipuuza hadhari ya mkewe kuwa asiende giza giza, alienda huku akijifariji kuwa panya hawezi kumdhuru chochote......alipoufikia mtego ule akapeleka mkono ili auchukue na kumsulubu panya aliyewasumbua kitambo. La haula! Kumbe hakuwa panya, mzee yule akarudi nyuma haraka huku akiagiza mkewe amletee taa haraka. Baada ya taa kuletwa ikabainika mtego ulinasa nyoka na hivyo mzee yule aliumwa na nyoka yule.....ghafla hamkani ikaingia ndani ya nyumba kutafuta dawa ya kumponya mzee mwenye nyumba. Muda si muda mzee yule alikata roho kwa kuzidiwa na sumu ya nyoka na nyumba ikawa na tanzia. Siku ya kwanza wageni wachache ikabidi achinjwe jogoo kupata kitoweo. Siku ya pili wageni ni wengi kiasi ikabidi achinjwe mbuzi ili kukidhi mahitaji. Baada ya maziko siku ya tatu na kumaliza tanga akachinjwa ng’ombe.
Funzo: Hivi ule mtego ulikuwa wa panya, ng’ombe, mbuzi, kuku au baba mwenye nyumba? Mbazi hii inasadifu umuhimu wa kushirikiana kuokoa mambo ambayo yakiharibika yataathiri wengi.
(c) Kisa/kidahizo Ni masimulizi mafupi yanayohadithia tukio moja bila ya kulifafanua kwa mfano; kidahizo cha nyani na mtoto wake.
Nyani na mtoto wake walikwenda kula mahindi katika shamba, wakala, wakala, wakala, halafu mtoto aliuliza, ...... “mama tunakula tu,je mpaka uko wapi?” mamaye akamjibu .... “we kula tu mpaka wataweka wenyewe.”Kidahizo chaweza kutokana na tukio la kweli lenye kuchekesha. MUHADHARA WA SABA: NGANO ZA KWANINI Ngano za kwanini? Hizi ni ngano zinazoeleza na kufafanua mianzo ya kaida za kiutamaduni. Katika maisha anamoishi mwanadamu. Tofauti ya ngano za kwanini na visasili ni kwamba hazishirikishwi na imani za kishirikina kama visasili vilivyo. Ngano za kwanini nyingi ni zile zinazoelezea sababu za viumbe fulani kuwa na sifa fulani.
Mfano:- Sababu za koo kuchakura - Mbuni kuwa na shingo ndefu - Ndevu kuota kidevuni na moyo kudunda - Kupatwa kwa jua, n.k
MUHADHARA WA NANE: SEMI NA VITENDAWILI1. Semi Semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Semi zinajumuisha tanzu kama vile methali, vitendawili, mafumbo, misimu, lakabu na kauli tauria (Mulokozi 1996). Semi hugawanywa katika vipera kama vile: - Misemo - Vitendawili - Methali - Mafumbo - Mizungu - Lakabu - Nahau, n.k
2. Vitendawili Kitendawili ni usemi wenye kuchochea fikra na udadisi wa jambo. Huwa ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbue.
Muundo wa kitendawiliVitendawili vingi huwa na muundo mmoja tu. Muundo wa kimapokeo huwa na sehemu nne ambazo ni: (a) Kiingizi/kitangulizi - fanani huanza kwa kusema.... kitendawili ..... na hadhira hujibu ...... tegaaaa. (b) Fumbo lwenyewe - mf. Kuku wangu katagia mibani? (c) Swali la msaada – mf. Tudokeze basi (iwapo jibu linafahamika huwa hakuna haja ya swali la msaada) (d) Jibu la fumbo – iwapo wote watashindwa kutoa jibu mtegaji hupewa mji na kisha kutoa jibu.
Mtindo wa kitendawiliVitendawili huwa na mtindo wa majibizano. Mtambaji hutoa kitangulizi cha kitendawili na fumbo lenyewe mf. Kitendawili......kuku wangu katagia mibani. Mtambiwa hujibu tega na kutoa jibu la kitendawili chenyewe – nanasi. Dhima ya vitendawili (i) Vitendawili hutegwa kwa lengo la kukomaza fikra na falsafa. (ii) Hutegwa ili kuburudisha na kuliwaza (iii) Hutumiwa kama chombo cha kufanya bongo ziwe na ustadi,busara na mahiri wa urazini katika kupambana na maisha. (iv) Huwaandaa vijana kuelewa mazingira yao yalivyo. (v) Hutumika kufunza adabu za vizazi vilivyopita. (vi) Hufanya vijana wawe wepesi wa kufikiri,kuamua na kutoa majawabu maridhawa. (vii) Huchochea itikadi za jamii kwa vijana (viii) Hutajirisha na kupamba mazungumzo (ix) Hutumiwa kwenye kuanzisha, kutofautisha, kukatisha au kukamilisha hadithi.
USANIFU WA VITENDAWILI Vitendawili hujipambanua kwa lugha ya kawaida vikijihusisha zaidi na silika,itikadi,utamaduni,uchumi,siasa na uhusiano wa matabaka ya kijamii. Vitendawili vya Kiswahili vina utanashati mkubwa wa lugha. Vina matumizi makubwa ya tamathali za usemi,lugha ya kishairi na mafumbo. Mbinu zitumiwazo katika vitendawili (i) Mliolio Vitendawili huwa na mbinu ya tanakali za sauti katika uwasilishaji wake. Mfano: - Parakacha ti – ugonjwa wa matende - Pa funika,pa funua – unyayo wakati wa kutembea (ii) Ushairi Ni mbinu ya kutumia mapigo ya kimuziki kwa utaratibu maalumu wakati wa kuwasilisha kitendawili. Mfano: - Mchana uu,usiku uu- macho - Futi kafutika futi, futi kafutika futi – kumbi, fuu, nazi, maji. (kumbi limefunika kifuu,kifuu kimefunika nazi na nazi imefunika maji) - Huku ng’o na kule ng’o – giza (iii) Tashihisi Ni mbinu ya kuvipa uhai na uwezo wa kutenda kama binadamu vitu visivyo na uwezo huo. Mfano: - Popo mbili zavuka mto – macho - Popote niendapo ananifuata – kivuli - Kila nipitapo nasikia wifiwifi – mbaazi (iv) Dhihaka Hii ni mbinu ya kumhujumu na kumdunisha mtu kwa kutumia vitendawili. Mfano: - Kitu kidogo kimemtoa mfalme kitini – haja - Kamba ndogo imefunga dume zima – usingizi.
MUHADHARA WA TISA: METHALI Methali ni tungo fupifupi zenye hekima na busara zitumiwazo kuonya,kuadibu na kuadilisha jamii.Methali ni sehemu ya lugha inayoweza kufananishwa na kiungo cha lugha na kitoweo cha lugha. Hutumiwa kutafakari na kuyapima maisha,kujifunzia jumuiya na kutawalia jamii na mazingira ya binadamu. Sifa za methali kwa mujibu wa M.M.Mulokozi: - Methali huwa ni usemi mfupi na wenye urari wa maneno japo maneno hayo si mepesi na ya kawaida. - Usemi huo ukubalike kwa watumiaji wa lugha husika. - Usemi huo uwe unamleta msikilizaji katika kufikiri, kuchambua na kupatanisha ukweli ili ang’amue maana ya ndani ya usemi huo. - Methali huwa na maana ya ndani na maana ya nje ambayo huelezwa kama mafumbo yanayohitaji ufafanuzi au ufumbuzi ili ziendane na mazingira halisi ya jamii. MUUNDO WA METHALI Methali nyingi huwa na muundo wa sehemu mbili. Sehemu ya kwanza huwa ni wazo/fumbo/swali na sehemu ya pili huwa ni jibu au ukamilifu wa wazo/fumbo. USANII WA METHALI Methali huwa na urari wa maneno yenye busara,mvuto wa lugha na tamathali mbalimbali za usemi. Urari wa maneno Mfano: - Harakaharaka,haina Baraka - Polepole ya kobe,humfikisha mbali Tashibiha Mfano: - Utajiri ni kama umande - Ujana ni kama moshi - Ufalme ni kama maua Sitiari Mfano: - Mapenzi ni majani,huota popote - Kukopa harusi,kulipa matanga - Ulimi ni upanga Balagha/chuku Mfano: - Chovya chovya,humaliza buyu la asali - Bandu bandu,humaliza gogo Kejeli Mfano: - Mfinyanzi hulia gaeni - Hindi ndiko kwenye nguo na wendapo uchi wako - Wagombanao hupatana - Ukienda kwa wenye chongo fumba lako jicho - Asiyesikia la mkuu huvunjika guu DHIMA YA METHALI (i) Ni kuwa ghala na kielelezo cha utamaduni wa mwafrika (ii) Hutumika kuonya (iii) Hutoa mausia (iv) Hushauri (v) Hufunza (vi) Husuta (vii) Hutia hamasa (viii) Hushauri mtu kufanya maamuzi magumu
MUHADHARA WA KUMI: USHAIRI SIMULIZI Dhana ya ushairi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili yake. Kabla ya karne ya 10BK ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa. Naye Mnyampala (1970) kama alivyonukuliwa na Massamba D.P.B. katika Makala ya Semina ya Kimataifa ya waandishi wa Kiswahili (2003) anasema ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale. Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongezi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalumu kwa shairi. Hapo tunaona dhahiri kuwa Mnyampala anauona ushairi ukiwa umejengwa na vitu viwili mahususi, ambavyo ni maneno ya hekima na sanaa yenyewe. Tena Mnyampala katika dibaji hiyo hiyo anasisitiza juu ya sanaa ya ushairi kwa kusema: Amri Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.” Ushairi, ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na vina ushairi una ufasaha wa kuwa na maneno machache au muhtasari wa mawazo na maono ya ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu. Mulokozi (1989) anasema ushairi hupambanuliwa na lugha ya kawaida kwa kutumia lugha na mbinu za kimuktadha. Kauli za kishairi hupangwa kwa kufuata wizani maalumu na mawimbi ya sauti na mara nyingi lugha ya mkato na mafumbo hutumika. Ushairi una fani zinazoambatana na muziki wa ala na wakati mwingine hupata wizani wake kutokana na mapigo ya muziki huo wa ala. Mulokozi (1989) amegawa ushairi katika mafungu mawili ambayo ni nyimbo na uwasilishaji. Nyimbo ni kila kinachoimbwa hivyo hii ni dhanna pana inayojumuisha tanzu nyingi za kinathari kama vile hadithi ambazo huweza kuingia katika kundi la nyimbo pindi zinapoimbwa. Vipera vya nyimbo ni tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
1. Nyimbo ni utanzu wa ushairi simulizi ambao unajigawa katika vipera mbalimbali vifuatavyo: (i) Tumbuizo Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha. (ii) Bembea/pembejezi Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto. (iii) Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka. (iv) Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini. (v) Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. (vi) Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha. (vii) Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari. (viii) Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza. (ix) Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini. (x) Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini na kadhalika (xi) Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari. (xii) Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji. (xiii) Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto. (xiv) Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kusifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila. (xv) Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.
2. Maghani Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyofanya utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi. Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi.
Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuliingiza katika fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu, wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.
Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu, pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha. Kivugo huwa hakiandikwi bali hutungwa papo kwa papo.
Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vilevile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji ambayo huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba. Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.
Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na ina visa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
Ngano; hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.
Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.
Mazungumzo Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi, ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia. Utanzu huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.
Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.
Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.
Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilevile kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.
Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.
Maigizo Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wake kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.
Ngomezi Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.
Hitimisho Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu una udhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:- Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali. Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo. Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo. Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.
MUHADHARA WA KUMI NA MOJA: TAARABU Taarabu ni ngoma ya kusisimua inayotumia ala za asili kama vile zeze,marimba,gambusi na filimbi kufuatana na mwimbaji. Neno taarab ni la kiarabu lenye maana ya furaha,kusherehekea,kuimba na kupiga muziki. Nidhamu ya taarab ni tofauti na ngoma nyingine. Katika taarab hakuna taratibu za kucheza. Wapiga ngoma na vinanda hukusanyika mahali pamoja wakizingirwa na wasikilizaji. Ngoma inapoanza wasikilizaji hupaswa kutega masikio tu kusikiliza mlio wa vinanda na sauti za maneno ya mtribu/manju wa ngoma yenyewe. CHANZO NA MAENDELEO YA TAARAB KATIKA JAMII YA KIGENI Taarab ni muziki wa kigeni ulioingia kwa waswahili kati ya miaka ya 1870 na 1888 wakati wa utawala wa Barghash Bin Said. Sultan huyu alikuwa mpenda muziki na hususan ngoma ya taarab. Alikuwa na Masuria (wake wasiohalali) tisini na tisa na mke mmoja kukamilisha mia. Kimaudhui nyimbo za taarab zilikuwa za kusifu na kumtukuza Sultani au kusifu na kukomaza mapenzi ya jumuiya ya kifalme kwa kuburudisha na kuchekesha wakubwa. Waimbaji wa taarab waliajiriwa katika nyumba za wafalme kuwastarehesha na vimada wao. Baada ya Sultan Barghash bin Said kutoka waliofuata walikuwa watawa na hapakuwa na utawala wa utulivu hivyo taarab ilipungua. Ngoma ya taarab ilipata umaarufu kati ya miaka ya 1920 hadi 1950 wakati wa Siti binti Saad. Baadaye uliingia mfumo wa amali ya jamii ya Unguja. Mabadiliko ya kwanza yalianza wakati Watribu walipoanza kutumia mashairi ya Kiswahili yaliyoimbwa kwa mahadhi ya kiarabu na kutunzwa katika sahani za santuri. Mashairi haya yaliimbwa kwa mahadhi ya Kiswahili lakini nidhamu yake ilibaki vilevile. Wakati wa ukoloni taarab zilitumiwa kwa lengo la kustarehesha na kwa upande mwingine zilisaidia kupalilia tabaka tawala kwa sababu haikujishughulisha na mapambano ya wananchi na migogoro yao na uovu wa kitabaka na kibepari. Nyimbo zilikuwa za mapenzi na kusifia ubwana na ubibiye. Je,taarab ni fasihi simulizi? Siti binti Saad anasadikiwa kuwa ndiye Mtribu wa kwanza kutoa santuri za nyimbo za taarab. Kama ilivyo kawaida fani za fasihi simulizi hurithiwa kwa kurithishana kwa mdomo. Nyimbo nyingi hasa za miaka 30 nyuma hazijulikani watunzi wake. Hivyo huwenda zikawa na mabadiliko ya maneno ndani ya mashairi yake ambayo yalizuka kwa ajili ya watu kupokezana kwa mdomo. MAUDHUI NA SANAA YA TAARAB Maudhui ya taarab kwa kiasi kikubwa hivi sasa yameibuka kutokana na hisiya za watribu. Maudhui hayo yanaweza kugawanywa katika matapo yafuatayo: kuna nyimbo za mapenzi, uasherati na ugoni. Nyimbo za mapenzi: katika tapo hili nyimbo nyingi zinazotungwa ni zile zinazoashiria mapenzi ya mke na mume. Mapenzi haya huweza kuwa kati ya mke na mume,mapenzi ya wazee,mapenzi ya jamii,mapenzi ya kindugu na mapenzi ya nchi. Mfano: WIMBO: Chura ALBUM: sina hakika KUNDI: JKT Taarab
Chura nakuuliza, unipe jibu makini, kwa kila inyapo mvua, wakimbilia bwawani Huna nguo za kufua, na wala huna sabuni, Nijibu yapate tua, maji utayafanyani
Chorus Chura punguza vituko, na wako uhayawani, umezua sokomoko, watu hawaelewani Ukivunjika mgongo, dawa atakupa nani?
Mwenzenu nilihisi, ni mlinzi kisimani, Mtu utamzuia maji, akiyatamani Akaja dada Rukia, na ndooye mkononi, chura ukajing’atua, ukajitosa pembeni
Chura punguza vituko ………………………
Chura bora kuamua, wende kulima shambani, Mazao kujipatia, wende kuuza sokoni Nguo kujinunulia, isitiri maungoni, Au ukitaka ndoa, nenda kaoe nyumbani.
Chura punguza vituko ……………………… MUUNDO WA TAARAB (i) Nyimbo za taarab zenye beti zenye mistari mitatu na haziitikiwi na zikiitikiwa huwa ni kurejelewa/kurudiwa kwa mstari wa mwisho katika kila ubeti. (ii) Beti zenye mistari minne – waimbaji huimba mistari mitatu na waitikiaji hudakia mstari wa nne. (iii) Beti zenye mistari mitano – muimbaji huimba mistari mitatu na kiitikio huwa mistari miwili ya mwisho. Taarab nyingi huwa na beti tatu au nne na wimbo huchukua dakika nane hadi kumi (8-10). LUGHA YA TAARAB Nyimbo za taarab hutumia Kiswahili cha hali ya juu kama ilivyo katika kaida (kanuni) za ushairi wa Kiswahili. Vipengele vingine vya kishairi kama urari wa vina,mizani na arudhi za ushairi wa Kiswahili huzingatiwa katika taarab.

Chura punguza vituko ……………………… MUUNDO WA TAARAB (i) Nyimbo za taarab zenye beti zenye mistari mitatu na haziitikiwi na zikiitikiwa huwa ni kurejelewa/kurudiwa kwa mstari wa mwisho katika kila ubeti. (ii) Beti zenye mistari minne – waimbaji huimba mistari mitatu na waitikiaji hudakia mstari wa nne. (iii) Beti zenye mistari mitano – muimbaji huimba mistari mitatu na kiitikio huwa mistari miwili ya mwisho. Taarab nyingi huwa na beti tatu au nne na wimbo huchukua dakika nane hadi kumi (8-10). LUGHA YA TAARAB
Nyimbo za taarab hutumia Kiswahili cha hali ya juu kama ilivyo katika kaida (kanuni) za ushairi wa Kiswahili. Vipengele vingine vya kishairi kama urari wa vina,mizani na arudhi za ushairi wa Kiswahili huzingatiwa katika taarab.
[www.mwalimuwakiswahili.com]