MAANA NA WAKATI: JIFUNZE NAMNA MAANA ZA MANENO YA KISWAHILI ZINAVYOBADILIKA KULINGANA NA WAKATI
MAANA NA WAKATI:
JIFUNZE NAMNA MAANA ZA MANENO YA KISWAHILI ZINAVYOBADILIKA KULINGANA NA WAKATI
Kisu-neno
hili kwaa maana ya awali au sanifu ni kifaa kirefu kilichotengenezwa kwa chuma
au bati kilicho bapa au chenye ncha kali upande mmoja, na matumizi yake makubwa
ni kukatia vitu vinavyoshikika. Kwa mfano ‘’Naomba Kisu nikatie hii
kamba’’.Lakini kwa maana ya sasa ambayo tunasema kudhoofika kwa maana ya msingi,
neno Kisu linatumika kumaanisha msichana au binti mrembo kwa mfano; Salima ni
Kisu mtaa mzima.Na mara nyingi neno hili hutumika sana na vijana hasa wanaoishi
mjini.
Kiwembe-kwa
maana ya zamani ni kifaa cha bapa chenye makali kotekote, lakini kutokana na
neno hili kudhoofika kimaana sasa vijana na watu wazima wanaoishi maeneo ya
mjini hutumia kumaanisha mtu ambaye hatulii kwenye mahusiano yake ya mapenzi
yaani mtu asiyekuwa na mpenzi mmoja. Kwa mfano; Jackson ni kiwembe cha mtaa.
Mjomba-kwa
maana ya awali Mjomba ni ndugu wa kiume wa mama au kaka wa mama lakini kutokana
na kudhoofika kwa maana ya maneno sasa neno mjomba linatumika kumaanisha Polisi
hususani wale wa barabarani,na hutumika sana na waendesha vyombo vya moto ambao
ni makonda pamoja na madereva wao kwa mfano pindi wanapogundua mbele kuna Polisi
husema “Funga mlango mbele kuna wajomba”.
Chombo-kwa
maana ya msingi ni kitu chochote cha kufanyia kazi kwa mfano; katika muktadha
wa nyumbani mama anaweza akasema “Mwanangu lete chombo cha kuwekea chakula”
Lakini kwa sasa kutokana na kudhohofu kwa maaana ya neno, chombo hutumika
kumaanisha msichana mrembo au mzuri kwa mfano; “Grace ni chombo” ikimaanisha
Grace ni msichana mrembo.Na watu wanaotumia sana msamiati huu kwa maana hiyo ni
vijana wa rika zote wanaoishi maeneo ya mjini.
Umeme-maana
yake ya msingi ni nishati ya mwanga au miale inayotoa mwanga lakini kwa sasa
neno umeme limepewa maana nyingine na wanajamii ambayo tunasema ni kudhohofika
kwa maana, sasa umeme unaamaanisha Ugonjwa wa UKIMWI kwa mfano;”Miaka mitano
sasa tangu Chande awe na umeme.” Wanachomaanisha vijana hapa ni kwamba tangu
Chande kuathirika kwa UKIMWI ni miaka mitano.
Kifaa-kwa
maana ya msingi ya neno kifaa ni kitu au chombo kinachotumika kufanyia kazi
lakini kutokana na kudhohofu kwa maana ya neno kwa sasa neno kifaa hutumika
kumaanisha msichana mrembo kwa vijana wa kiume lakini kwa upande wa vijana wa
kike hulitumia kurejelea mwanaume hodari na mwenye juhudi kazini au katika
kufanya mapenzi.kwa mfano “Hashimu ni kifaa kile” hapa wanawake ambao ni vijana
humaanisha Hashimu ni mwanaume hodari wa mapenzi.
Kigodoro-kwa
maana ya awali ni kipande kidogo cha godoro kwa mfano mtu anaweza kusema
“Naomba kigodoro nifanye mto”, Lakini kwa maana ya sasa neno hili limedhohofu
maana yake ya awali na kutumika kumaanisha sherehe za mtaani zinazoambatana na
muziki unaokesha kwa mfano “Leo kuna kigodoro mtaa wa pili” Hapa wakazi wa
mjini takribani wa rika zote wanaoishi mjini humaanisha kwamba mtaa wa pili
kuna sherehe ambayo inakesha mpaka asubuhi.
Mlima-kwa
maana ya awali neno hili linamaana ya kwamba sehemu ya ardhi iliyoinuka sana
kwa mfano;”Chuo kikuu cha Dodoma kimejengwa kwenye milima” Lakini kutokana na
neno mlima kudhohofu kimaana sasa vijana hususani wa kiume hutumia kumaanisha
makalio makubwa ya mwanamke kwa mfano vijana hawa huweza kusema “Mlima wa
Subira ni hatari” wakimaanisha Subira anamakalio makubwa sana.
Mashine-kwa
maana ya awali neno hili linamaanisha kifaa au chombo kinachotoa nguvu ya
kuendeshaa, Lakini kwa maana ya sasa ambayo ni zao la kudhohofu kwa maana ya
neno sasa wanawake na vijana wa kike wanatumia msamiati huu kurejelea Kiungo
cha uzazi cha mwanaume (uume).kwa mfano “Saidi anamashine kubwa” wakimaanisha
kuwa Saidi anauume mkubwa.
Kipanga-kwa
maana ya awali ni aina ya ndege mkubwa aina ya Tai ambaye huwa anakula wanyama
na wadudu wadogo, Lakini kutokana na kudhohofu kwa maana sasa neno kipanga
linatumika kumaanisha mtu mwenye akili nyingi darasani au sehemu ya kazi.Na
neno hili linatumiwa zaidi na wanafunzi pamoja na walimu wao katika muktadha wa
elimu.Kwa mfano “Elizabeth ni Kipanga kwa wanafunzi wa mwaka wa pili”.
Asali-maana
ya msingi ni maji matamu mazito yanayotengenezwa na nyuki lakini kwa maana ya
sasa ambayo ni kudhoohofu kwa maana ya neno watu ndani ya jamii wanalitumia
neno asali kumaanisha mpenzi au mtu anayempenda kwa mfano; “Ester anasemaBryson
ni asali wake”
Kamanda-kwa
maana ya awali neno hili linamaanisha mkuu wa jeshi au polisi kwa mfano
“Jenerali Mamnyange ni Kamanda wa jeshi la wananchi wa Tanzania” Lakini kwa
sasa neno hili limedhohofu kimaana kwa vijana wengi wanalitumi kumaanisha
rafiki wa karibu wa mtu hususani kwa vijana wa kiume kwa mfano “Naona kamanda
umepumzika”.Hapa vijana hawamaanishi aliyepumzika ni mwanajeshi au polisi ila
ni rafiki yake tu.
Ndezi-kwa
maana ya awali ni mnyama wa mwituni mwenye umbo kama panya lakini ni mdogo
kuliko paka.Ila kutokana na kudhohofu kwa maana sasa vijana wanalitumia neno
ndezi kumaanisha mtu mzembe ndani ya jamii kwa mfano;”Mavula ni ndezi sana”
Nyoka-kwa
maana ya awali ni mdudu mrefu mwembamba mwenye magamba asiye na miguu kwa mfano
“Nyoka aina ya Moma ni mkali sana” Lakini kwa maana ya sasa ambayo kitaalamu
tunasema ni kudhohofu kwa maana ya neno, Nyoka inatumika kumaanisha mtu msaliti
au mnafiki na pia katika mkutadha wa migodini nyoka n wafanyakazi wanaoingia
chini na kubeba vifurushi vya mchanga kuvitoa juu.
Chale-kwa
maana ya awali ni alama au mkato anaokuwa nao mtu mwilini baada ya kuchanjwa na
mganga kwa mfano;”Salome anachale nyingi mgongoni” Lakini kwa maana ya sasa
kutokana na kudhoofu kwa maana inatumika kumaanisha mtu mwenye hisia za haraka
kutambua au kuhisi vitu au hali hususani ya hatari,kwa mfano Jambazi ndeka
anamachale sana hakamatwi na Polisi.
Mshikaki-kwa
maana ya awali ni nyama iliyokatwa vipande vipande na kuchomekwa kwenye
uchelewa au msumali kisha kuchomwa,kwa mfano “Jana nilinunua mshikaki na
chipsi” Lakini kutokana na kudhohofu kwa maana sasa katika jamii neno hili
linatumika kumaanisha ni mkao wa watu zaidi ya wawili kwenye pikipiki, kwa
mfano: “Watu waliopanda mshikaki wamepata ajali mbaya”.
Msala-kwa
maana ya awali ni mkeka mdogo unaotumiwa kusaliwa na watu wa dini ya kiislam
hususani wanawake wakiwa nyumbani,kwa mfano; “Mama Abdul aliusafisha msala wake
kabla ya kuanza kusali” Lakini kwa maana ya sasa kutokana na kudhohofu kwa
maana neno msala linatumiwa na vijana kumaanisha jambo ambalo sio salama,jambo
lenye matatizo au shida au kitu cha shari au hatari kwa mfano; “John kapelekwa
kituo cha polisi kuna msala kafanya”.
Mzuka-kwa
maana ya awali ni ni zimwi au pepo kwa mfano; “Swaumu amenisimulia hadithi ya
mzuka” Lakini kwa maana ya sasa neno mzuka limepoteza hadhi yake kimaana kwani
kwa sasa vijana wanalitumia kama ifuatavyo;kwenye muktadha wa salamu humaanisha
ni shwari,salama,Amani kwa mfano; “mtu anapoulizwa unaonaje na hali hujibu
mzuka yaani shwari au safi” lakini kwenye muktadha wa kawaida hutumika
kumaanisha morari au mdadi wa kufanya kitu kwa mfano; “Leo sina mzuka wa
kusoma” kwa maana kwamba leo hana morari au hamu ya kusoma.
Askari-kwa
maana ya awali ni mtu anayelinda na kuhani Nchi kwa mfano “Julias ni askari wa
Jeshi la polisi” lakini kwa maana ya sasa ambayo inaonyesha jinsi neno hili
linavyodhohofika kimaana sasa vijana wanalitumia neno hili kama kijana yeyote
mkakamavu na shupavu au jasiri kwa mfano “Bapipo ni askari wangu” kwa maana ya
Bapipo ni jasiri au shupavu.Lakini pia neno hili hili vijana hulitumia
kumaanisha rafiki kwa mfano unaweza
ukakuta kijana kawakuta wenzake wamekaa akitaka kuwasalimu utasikia anasema
“Askari wangu vipi naona stori zimekolea” na wakati hakuna ambaye analinda au
ni askari wa jeshi fulani, wote ni raia wa kawaida.
Chana-kwa
maana ya kawaida neno hili linatumika kumaanisha kitendo cha kupasua kitu kama
vile karatasi, nguo n.k kwa mfano; “Joyce anachana nguo” Lakini kutokana na
maana ya neno hili kudhohofika sasa watu ndani ya jamii wanalitumia kumaanisha
kitendo cha kuimba nyimbo au mashairi kwa kufokafoka kwa mfano; “Mr Blue
anachana siku hizi” kwa maana ya kwamba siku hizi Msanii Mr Blue anaimba
mashairi ya kufokafoka.
Mistari-kwa
maana ya awali neno hili linatumika kuonesha muondelezo wa mchoro ulinyooka kwa
mfano; “Mwalimu alisema kila mwanafunzi achore mstari mnyoofu” Lakini kwa maana
ya sasa kutokana na kudhohofu kwa maana ya neno jamii inalitumia neno hili
kurejelea mashari ya nyimbo kwa mfano; “Kama kweli wewe ni msanii tupe mistari”.
Ubao-kwa
maana ya awali ni kwamba neno hili linatumika kumaanisha sehemu ya gogo au mti
iliyopasuliwa vizuri lakini kwa sasa ndani ya jamii neno hli la ubao linatumika
kumaanisha njaa yaani hali ya kuhisi njaa kwa mfano; “Jamani mimi ninaubao
tutakula saa ngapi?”
Chonga-kwa
maana ya awali neno hili linamaana ya kwamba ni kitendo cha kufanya ncha kwa
kutumia chombo chenye makali kwa mfano; “Hamisi anachonga mshale kwa kutumia
kisu” ila kwa sasa kutokana na kudhohofu kwa maana ya neno siku hizi neno hili
wanajamii wanaalitumia kumaanisha kitendo cha mtu kuongea sana kwa mfano;
“Janeth anachonga kama chiriku” kwa maana kwamba Janeth anaongea sana.
Uwawa-kwa
maana ya awali neno hili linatumika kumaanisha kitendo cha kutolewa uhai kwa
mfano “Mzee Rashidi ameuwawa jana usiku na majambazi” lakini kwa sasa neno hili
limedhohofu maana yake ya awali kwani vijana analitumia kumaanisha hali ya mtu
kutokuwa na pesa kwa mfano; “Hapa nilipo nimeuwawa namtafuta wa kunikopesha.”
Msenge-kwa
maana ya awali linamaana ya mwanaume mwenye kufanyiwa vitendo vya kishoga au
mwanaume hanithi lakini kwa jamii ya sasa hususani vijana wa kiume wanalitumia
kumaanisha kijana yeyote wa kiume hata kama hana tabia hizo kwa mfano
utawasikia vijana wengi katika maongezi yao wakisema “Yule msenge Bwire ni
anajua huwa habahatishi” kwa maana Bwire ni kijana anayejua mambo kwa uhakika
na wala sio shoga au hanithi.
Zege-kwa
maana ya awali ni mchanganyiko wa kokoto,mchanga,saruji na maji ambayo hutumika
katika kujengea kwa mfano; “Nyumba yetu imejengwa kwa msingi wa zege” lakini
kutokana na kudhohofu kwa maana neno zege sasa linamaana ya chakula ambacho ni
mchanganyiko wa viazi mbatata na
mayai(chipsi yai) kwa mfano; “Naomba zege mbili haraka” kwa maana kwamba
anaomba chipsi yai.
Mende-kwa
maana ya awali neno hili lina maana ya mdudu mwenye rangi ya kahawia mwenye
mabawa na miguu mine ambao hupenda kukaa sana chooni kwa mfano; “Chooni kwao
kuna mende wengi” lakini kwa sasa neno hili linatumika kumaanisha mtu ambaye ni
mlevi wa pombe,kwa mfano; “Bokasa ni mende wa kijijini” kwa maana Bokasa ni mtu
mlevi kijijini.
Ngano-kwa
maana ya awali mmea aina ya nafaka unaotumika kutengenezea chakula lakini kwa
sasa kwasababu ya kudhohofu kwa maana ya neno watu ndani ya jamii wanalitumia
kumaanisha kilevi aina ya pombe hususani bia kwa mfano; “Usiku wa jana tulikula
sana ngano” kwa maana usiku huo walikunywa sana pombe.
Fataki-kwa
maana ya awali ni karatasi zilizotengenezwa na kutiwa baruti ndani ambazo
hutumiwa mara nyingi kwenye sherehe kwa mfano; “Usiku wa mwaka mpya tulirusha
fataki tatu” lakini kutokana na kudhohofu kwa maana ya neno sasa neno hili
wanatumia kurejelea mwanaume mtu mzima anayetembea na wasichana wenye umri
mdogo hususani wanafunzi wa shule kwa mfano; “Mzee Jangara ni Fataki”kwa maana
kwamba Mzee Jangara anatembea na wasichana wadogo kama wajukuu zake au watoto
wake.
Maji-kwa
maana ya awali ni kwamba neno hili linamaanisha kiowevu kinachopatikana katika
bahari, mvua au maziwa lakini kwa kudhohofu kwa maana ya neno watu ndani ya
jamii wanalitumia neno hili kumaanisha Kilevi aina cha pombe kwa mfano; “Minja
na Chibago wanapiga maji sio mchezo” hii inamana kwamba Minja na Chibago
wanakunya sana pombe.
Bandua-kwa
maana ya awali inamaana ni kitendo cha kutenganisha au kuachanisha vitu
vilivyogandiana au ni kitendo cha kuondoa kitu kilichobandikwa kwa mfano; “Mama
kasema nibandue magazeti yote ukutani” lakini kutokana na kudhohofu kwa maana
ya neno sasa vijana wanalitumia neno bandua kumaanisha kitendo cha watu kufanya
tendo la ndoa kwa mfano; “Hassan kambandua Sara usiku wa jana” kwa maana ya
kwamba Hassan jana alifanya mapenzi na Sarah.
Ngoma-kwa
maana ya awali ni ala ya muziki inayotengenezwa kwa kuwamba ngozi kwenye mzinga
kwa mfano; “Ngoma zilipigwa kwenye harusi ya dada” lakini kwa maana ya sasa
neno hili linatumika kumaanisha ugonjwa wa UKIMWI kwa mfano; “Bakari amekufa
kwa ngoma”
Hii
inamaana kuwa Bakari alifariki kwa ugonjwa wa UKIMWI.
Chemka-kwa
maana ya awali ni hali ya kupata joto lakini kwa sasa neno hilo linatumika
kumaanisha kitendo cha mtu kushinwa kufanya kitu kwa mfano; “Chausiku amechemka
kufaulu mtihani” yaani Chausiku kashindwa kufaulu mtihani.
Msimbazi-kwa
maana ya awali ni eneo linalopatikana jijini Dar es salaam maeneo ya kariakoo
hususani eneo la kilabu ya simba na pia maeneo ya kigogo ambapo kuna kituo cha
ufundi cha kanisa katoliki, lakini kwa sasa neno msimbazi hutumika kumaanaisha
noti ya shilingi elfu kumi kwa mfano; “Fomu ya usajili inauzwa kwa msimbazi tu”
kwa maana kwamba fomu hiyo inauzwa shilingi elfu kumi tu.
Bati-kwa
maana ya awali inamaana ya bamba la chuma lenye mikunjokunjo kama
matuta madogo hutumika kuezekea nyumba kwa mfano; “Baba kanunua bati hamsini
kwa ajili ya kumalizia ujenza wa nyumba” lakini kwa sasa neno bati linatumika
kumaanisha shilingi mia ya kitanzania ka mfano; “Kama unabati naomba ninunue
nyembe” kwa maana kuwa anaomba shilingi mia anunue nyembe.
Kilo-kwa
maana ya awali ni kwamba neno hili linatumika kumaanisha uzani wa kitu kwenye
latini kwa mfano; “Dada ameagizwa mchele kilo mbili” lakini kwa maana ya sasa
neno kilo linamaana ya shilingi laki moja za kitanzania kwa mfano; “Juzi
nimeokota kilo nne” akiwa na maana kwamba Juzi ameokota shilingi laki nne za
kitanzania.
Dongo-kwa
maana ya awali ni sehemu ya udongo iliyomeguka lakini kwa sasa vijana wengi wa
kiume na wa kike wanatumia neno dongo kumaanisha majungu au kejeli kwa mfano;
“Deusi anapenda madongo sana” kwa maana kwamba Deusi anapenda kejeli au kuapiga
majungu watu.