UHALISIA WA KIJAMAA

 UHALISIA WA KIJAMAA

Kwa mujibu wa Senkoro, F.M.K (1987), Uhalisia wa kijamaa ni hatua ya  juu ya uhalisia wa kihakiki. Ni uhalisia ambao msingi wake mmojawapo mkuu ni wa harakati za kitabaka. Harakati hizi katika uhalisia huu huonyeshwa katika uhalisia wake wote bila kuficha jambo lolote lile.
Kwa mujibu wa Njogu, K na Wafula R.M (2007), Uhalisia wa kijamaa ni mbinu ya utunzi na uhakiki inayomzingatia binadamu kama uti wa mgongo wa kuwepo kwa ulimwengu na maana ya ulimwengu ule. Waundaji wa nadharia hii wameathiriwa na mtazamo wa Kimaksi kuhusu ulimwengu na historia. Maxim Gorki mmojawapo wa waasisi wa uhalisia wa kijamaa, anasema kwamba mambo yote mazuri yanayotamanika ulimwenguni yameumbwa au kuelezwa na binadamu.
Kwa mujibu wa Wamitila, K.W (2003), Uhalisia wa kijamaa ni mtazamo ambao hujaribu kusisitiza uwasilishi wa uhalisia unaotilia mkazo mkubwa maendeleo ya kihistoria yanayokiuka ubepari na kufikia usoshalisti. Kazi za kifasihi ambazo zimeandikwa katika misingi ya uhalisia hupaswa kulenga kuwafikia wasomaji wa kawaida.
         Vigezo vya uhalisia wa kijamaa
        Huonyesha uhalisia wake kwa uelekeo wa kijamaa. Uhalisia wa kijamaa huonyesha mambo katika misingi ya kijamaa kwa namna ya kupinga matabaka hivyo njia ya uzalishaji mali humilikiwa kwa usawa.
       Huwa na muundo fulani wa kihistoria ambao huonekana kama mvutano kati ya matabaka. Ili jamii iwe na mabadiliko au maendeleo lazima iwe na historia fulani kwa kutoka katika hatua moja kwenda nyingine. Mfano Karl Marxy na Fredrick walisema “jamii zote ulimwenguni ilibidi zipitie katika hatua ya       ukatili       umwinyi       ubwanyenye       ukabaila         ubepari        ujamaa, ili jamii iweze kufikia usawa na hivyo kuleta maendeleo katika jamii.
         Kusisitiza kuwa maisha ni matendo na kwa ubunifu ambao nia yake ni kuonyeresha ukuaji wa binadamu na kuweza kuibuka mshindi katika mapambano ya nguvu za kiasili. Lengo kubwa la nadharia hii  ni kuonyesha namna waandishi wanavyowatumia wahusika mbalimbali katika jamii wanavyotakiwa kuwa watu wenye ujuzi na mbinu mbalimbali za kuweza kupambana na matatizo yanayowakumba katika jamii, mfano masuala ya unyonyaji, rushwa, matabaka na umaskini, ili mwisho wake waweze kuyashinda matatizo hayo.
       Chanzo kikuu cha mivutano ni uzalishaji mali. Hii hutokea pale ambapo tabaka la chini linapojaribu kupambana na tabaka la juu ili kuweza kumiliki nyenzo mbalimbali za uzalishaji mali kama vile mashamba na viwanda, hali ambayo hupelekea tabaka la chini kupata usawa katika jamii.
        Fasihi huchukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu. Tunaona kuwa waandishi wengi wa fasihi huandika kazi zao kwa lengo la kulikomboa tabaka la chini kutoka kwenye mikono ya dhuluma, unyonyaji na uonevu ili kuweza kuleta usawa katika tabaka hilo tawaliwa kwenye nyanja zote za maisha yaani; kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.
        Hulenga maisha ya baadaye  na ujenzi wa jamii mpya yenye raha na ufanisi. Uhalisia wa kijamaa hupigania jamii yake kuachana na mambo yanayokwamisha maendeleo katika jamii husika kwa kuwachora wahusika wanaopigana kuleta mabadiliko katika nyanja zote yaani kifikra, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ili wawe  na jamii moja yenye raha na ufanisi.
       Huamini baada ya wafanyakazi wa viwandani kuchukua silaha na kupigania haki yao dhidi ya mwajiri ambaye daima ni mnyonyaji wa nguvu zao, hali hii husababisha mapinduzi ambayo huzaa jamii isiyo na matabaka. Kazi nyingi za uhalisia wa kijamaa huamini kuwa suluhisho la unyonyaji wa tabaka la chini ni tabaka hili (wanyonge ambao ndio wafanyakazi wa tabaka lenye nguvu) kupambana na tabaka tawala kwa kutumia silaha ili kuzipigania haki zao kwa kupambana na wanyonyaji, wanauhalisia wa ujamaa wanaamini kuwa kutapelekea mapinduzi katika jamii  husika hivyo kuzaliwa kwa jamii mpya isiyo na matabaka wala unyonyaji na hatimaye jamii kuishi katika misingi ya usawa.
          Riwaya ya Nyota ya Rehema iliyoandikwa na Mohamed Suleiman ni riwaya ya uhalisia wa kijamaa kulingana na maudhui yake kama ifuatavyo:
        Uhalisia wa kijamaa huwa na muundo fulani wa kihistoria ambao huonekana kama mvutano kati ya matabaka ambao chanzo kikuu cha mivutano hiyo ni uzalishaji mali. Kwa kutumia riwaya ya Nyota ya Rehema, mwandishi Mohamed Suleiman ameonyesha muundo wa Umwinyi ambao wachache wanahodhi mashamba na mazao na kuwaweka maskini kuyalima na kulipia kodi kwa kuwafanyia kazi na kuwapatia sehemu ya mazao wanayozalisha, ambapo vitendo hivyo husababisha mivutano baina ya tabaka tawala na tawaliwa. Mfano, kulitokea mivutano kati ya Karimu na Rehema pale ambapo Karimu alidiriki kumpeleka Rehema kwa mwanasheria Bwana Mudir kwa nia ya kumdhulumu urithi wa shamba na nyumba katika eneo la Ramwe ambalo Bwana Fuad alimpa Rehema lakini bila kumpatia hati miliki.  Na baada ya kifo cha Fuad ndipo Rehema aliponyang’anywa urithi huo baada ya Karim kutengeneza hati za kugushi na kumlazimisha Rehema kuweka sahihi kwa kidole chake. Mfano Rehema alisema, 
“Konde zilizomo na shamba lenyewe ni mali yangu Bwana Mudir na mimi ndiye mtoto wa marehemu Bwana Fuad … Baba Fuad Salum” Yule kijana alitaharuki sikumbuki Bwana Mudir alipayuka kijana mkakamavu kwa sauti yenye kulipa kila neno uzito wake kuwa al-marhum kaacha zaidi ya watoto wawili, mmoja ni Samiri ambaye yupo Ulaya anamaliza masomo yake, wa pili ni Ahli wa Bwana Mudir wa jimbo la mjini (mke wa Karim). (uk.143)
Hivyo kutokana na unyonyaji uliofanywa na tabaka tawala ilipelekea kutokea kwa mapinduzi ambayo yalileta mabadiliko makubwa katika jamii hiyo na hivyo kukawa na usawa katika umilikaji na uzalishaji mali.
          Uhalisia wa kijamaa hulenga maisha ya baadaye na ujenzi wa jamii mpya yenye raha na ufanisi. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi amemtumia mhusika Rehema aliyekuwa anajaribu kupigania haki yake ili apate urithi na aje kuishi maisha ya raha na ufanisi, pia Sulubu ambaye alidiriki hata kumuua Karim alipelekwa gerezani, tendo hili liliwafanya wananchi wakaandamana na kupinga unyanyasaji na kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa kimwinyi, ili waweze kujenga jamii mpya isiyo na matabaka. Mfano mwandishi anasema,
“Poeni wananchi! poeni wananchi! Dhuluma imeshapinduliwa! Haki tupu! Uhuru na haki …!”  "Hekaheka za mapinduzi zilipomalizika Rehema, Sulubu na mtoto wao wanarejea katika shamba lao la pakani na kuendelea kuamrisha … ”  (uk. 168)
Hivyo inadhihirika katika riwaya hii kuwa uhalisia wa kijamaa huwa na lengo la kujenga jamii mpya yenye maendeleo, kwani juhudi zote huwa ni kwa ajili  ya kupinga dhuluma na kuleta jamii yenye raha na ufanisi.
            Uhalisia wa kijamaa huonyesha uhalisi wake kwa uelekeo wa kijamaa. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema imeonyesha sana maudhui yake kuwa ya uhalisia wa kijamaa mfano kwa kurejelea wahusika kama Kidawa, Chiku, Rehema na Ruzuna wameonyesha kuishi maisha ya kijamaa (uk.43-44). Vilevile Bi Kiza na mzee Juma nao upendo wao kwa Rehema unaonyesha ujamaa na pia kitendo cha wananchi wa tabaka la chini kuungana kumtetea Sulubu pale alipokamatwa  baada ya kumuua Karim, umoja huo ulionyesha ujamaa wao kupambana na serikali hatimaye wakafanya mapinduzi ya utawala uliokuwa madarakani (uk.168)
“sauti za wanyonge moja ikiamsha nyingine, zilivuma na kushinikiza Mtoeni Sulubu! Mtoeni Sulubu! Mtoeni Sulubu! … ”
Hivyo katika riwaya hii ya Nyota ya Rehema imeonyesha wazi suala la uelekeo wa uhalisia wa kijamaa.
          Uhalisia wa kijamaa huchukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu. Maudhui katika riwaya hii ya Nyota ya Rehema yameonyesha uhalisia wa kijamaa kwa kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu kama inavyoonekana katika (uk.168) ambapo wananchi wa tabaka la chini wanaungana katika kupinga dhuluma na unyanyasaji uliokuwa unafanywa na serikali juu yao baada ya kufungwa kwa Sulubu, pia katika (uk.80-82) tunamuona Bi Kiza akipigania haki ya Rehema binti yake Fuad katika kutafuta urithi wa kiwanja alichoacha mama yake Aziza baada ya kifo chake. Bi Kiza anasema,        “nimekuja kukuchukua”
                      “Ukadai haki zako”
                        Marehemu mama yako … kaacha vitu            
                         chungu nzima Ramwe …”
kadhalika (uk. 167-168) Sulubu alifikia kumcharanga mapanga Karim aliyetaka kuwadhulumu eneo la shamba lao. Mwandishi anasema,
“Sura aliyoiona ilikuwa ya kiwiliwili cha Karim kimeanguka kifudifudi, vipande viwili …” Hivyo mwandishi wa riwaya hii ameonyesha jinsi uhalisia wa kijamaa unavyochukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu katika jamii.
           Uhalisia wa kijamaa huamini baada ya wafanyakazi wa viwandani kuchukua silaha na kupigania haki yao dhidi ya mwajiri wao ambaye daima ni mnyonyaji wa nguvu zao, hali hii husababisha mapinduzi ambayo huzaa jamii isiyo na matabaka. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi amamtumia mhusika  Sulubu ambaye alikuwa mme wa Rehema katika kutetea haki za wanyonge. Suala hili la utetezi wa haki za wanyonge ilipelekea Sulubu kuhukumiwa kunyongwa kwa kosa la kumuua Karim ambaye alitaka kumnyang’anya shamba lakini wananchi wengine wakashirikiana na wanajeshi kupinga suala hilo na hatimaye kukafanyika mapinduzi, mfano mwandishi anaposema,
“Ndipo ambapo vizazi vya wanyonge vilivyokuwa jeshini vilipounda nguvu kwa siri na kufanya mapinduzi yaliyofanikiwa muda mfupi na kabla Sulubu kunyongwa (uk.168).
Hapa ndipo tunaona wanajeshi wanaipindua serikali yao na wananchi wanakuwa huru na kuondokana na suala la matabaka na kuishi kijamaa.
             Uhalisia wa kijamaa husisitiza kuwa maisha ni matendo na ubunifu ambao nia yake ni kuonyesha ukuaji wa binadamu na kuweza kuibuka mshindi katika mapambano ya nguvu za kiasili. Katika riwaya hii ya Nyota ya Rehema mwandishi amewatumia wahusika Rehema na Sulubu ambao maisha yao yameelezwa kiuyakinifu. Kwanza maisha ya Rehema yanaonyeshwa tangu alipozaliwa kisha kukataliwa na baba yake hatimaye akatoroka kwenda mjini na kukumbana na misukosuko mingi na anaamua kurudi kijijini kwa baba yake kuomba msamaha. Lakini baada ya kukumbwa na yote haya Rehema anaamua kuolewa na Sulubu ambaye alikuwa mtu mwema na mchapa kazi. Wakiwa pamoja Rehema na Sulubu waliendelea kupatwa na misukosuko hatimaye wanaibuka kuwa washindi. Pia tunaona Rehema na Sulubu walionekana kuwa wabunifu pale ambapo walihamia kwenye shamba lisilokuwa na rutuba baada ya kunyang’anywa shamba lao la urithi. Rehema na Sulubu wanaamua kuwachoma na kuwasagasaga wadudu ili kurutubisha shamba lao. Mfano mwandishi anasema,
 Njia rahisi ya mwisho  aliyoiona Rehema ilikuwakuwa sagasaga sangara, konokono na jongoo ili kuwageuza mbolea … ” (uk. 154)
Hivyo basi Mohamed S. Mohamed ameonyesha jinsi tabaka la chini linavyokuwa na ubunifu ili kuweza kuibuka na ushindi dhidi ya tabaka tawala katika kuleta usawa katika jamii.
          Uhalisia wa kijamaa huonyesha kuwa chanzo kikuu cha mivutano ni uzalishaji mali. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi anaonyesha jinsi au namna suala la ardhi kama chanzo cha uzalishaji mali linavyoleta migogoro katika jamii. Kwa kudhihirisha hilo mwandishi amewatumia wahusika kama Rehema na Sulubu ambao walikuwa na mgogoro au mvutano na Karim kuhusu shamba la urithi alilopewa Rehema. Mwandishi anaowanyesha Karim na mke wake wakipingana juu ya wazo la kwenda kumdhulumu Rehema shamba lake ambalo alipewa na baba yake kama urithi. Mfano Salma anasema,
“Karim! Haiwezekani! Shamba lile walipewa na marehemu baba mwenyewe”  (uk.164)
Mgogoro mwingine ni wa Karim kutaka kudhulumu shamba la Rehema na mumewe, suala hilo lilipelekea kifo cha Karim ambaye aliuawa na Sulubu mme wa Rehema. Mfano Rehema anasema,
 “Sura niliyoiona ilikuwa ya kiwiliwili cha Karim kimeanguka kifudifudi vipande viwili…” (uk.168).
Pia tunaona mvutano mwingine ni kati ya tabaka tawala na tabaka tawaliwa (chini) mvutano huu unatokana na kufungwa kwa Sulubu ambapo wananchi wanaungana na kupinga serikali yao hatimaye mapinduzi yakatokea. Mfano mwandishi anasema,
 “Sauti za wanyonge moja ikiamsha nyingine zilivuma na kushinikiza, Mtoeni Sulubu! Mtoeni Sulubu!” (uk.168)
 mwandishi ametumia migogoro hii ili kuonyesha mapinduzi yenye kuleta usawa katika jamii.
              Kwa ujumla mwandishi wa riwaya ya Nyota ya Rehema ya mwandishi Mohamed S. Mohamed amejaribu kuonyesha namna/jinsi usawa unavyoweza kupatikana katika jamii. Suala hili la usawa katika jamii isiyokuwa na matabaka Mohamed amejaribu kuonyesha namna suluhisho linavyoweza kupatikana kuwa kuwa ni tabaka la chini kuweza kufanya mapinduzi kama harakati za kimapinduzi zilizokuwa zikifanywa na wahusika kama Sulubu Rehema pia hata Wanajeshi. Hata hivyo katika jamii ya sasa uhalisia wa kijamaa unaonekana kushindwa kutekelezwa katika jamii kutokana  na nguvu za mfumo wa kibepari unaonekana kuitawala dunia na watu wake kwa ujumla.
MAREJELEO:                                                                                                                 
Masebo J.A and Nyangwine N, (2002) Nadharia ya Fasihi. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.
 Mazrui A and Syambo B (1992) Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers
Mohamed S.M (1976), Nyota ya Rehema. Nairobi: Oxford University Press East Africa Ltd.
Njogu K & Wafula R.M (2007) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Kenya: The Jomo Kenyatta Foundation.
Senkoro F.E.M.K (1987) Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publishing Centre.
Wamitila K.W (2003) Fasihi, Istilahi na Nadharia. Kenya: Focus Books.
Powered by Blogger.