MOTO WA MIANZI

 
 MOTO WA MIANZI
MAUDHUI
SWALI:  Chambua Maudhui ya Riwaya ya Moto wa Mianzi
Historia fupi ya Mwandishi na utunzi wa kazi yake:
RIWAYA YA MOTO WA MIANZI; ni riwaya iliyoandikwa na mwandishi aitwaye Mugyabuso Mulokozi. Alizaliwa tarehe 7 Juni mwaka 1950. Mugyabuso Mulokozi ni muhadhiri katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Mwandishi huyu pia ameweza kuandika kazi mbalimbali. Baadhi ya kazi zake ni:
·         Mashairi ya kisasa aliyoandika kwa kushirikiana na K.K Kahigi.
·         Malenga wa Bara aliyoandika pamoja na K.K Kahigi
·         Mukwava wa Uhehe
·         Kunga za Ushairi na Diwani yetu aliyoandika pamoja na K.K Kahigi
·         Ngome ya Mianzi
·         Ngoma  ya Mianzi
Tukirejea zaidi riwaya ya Moto wa Mianzi; riwaya hii inahusu matukio yaliyofuatia kutekwa kwa ngome ya Kalenga mwaka 1894. Katika riwaya hii Mutwa Mukwawa alikimbila Kilolo kwa baba yake. Mugoha Muhanzala, Nyawelu wakiwa na mtoto Semuganga walipewa jukumu la kumpeleka Sapi bin Mukwava, Kilolo kwa baba yake. Mwandishi anajadili masaibu yaliyowapata njiani.
Riwaya ya Moto wa Mianzi  ni ainaya riwaya ya kimajaribio kwa kuzingatia kigezo cha fani kutokana na kwamba imetumia kanuni ambazo si zoefu katika utanzu wa riwaya kwa mfano kwenye kipengele cha fani na maudhui. Riwaya nyingine zinazofanana na riwaya husika kimaudhui ni kama vile Nagona na Mzingile.                                                                                                       Kutokana na swali ambalo limejikita zaidi katika maudhui, dhana ya maudhui ni pana. Maudhui  ni mawazo au mambo yanayosemwa ndani ya kazi ya sanaa.Maudhui yanaweza kuwa jambo lolote  linalomkera mwanadamu , kwa mfano maana ya maisha, mapenzi, mauti, ndoa, elimu, kazi, ukombozi, dini, nk.Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi.Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe na msimamo wa mwandishi.
Dhamira
Dhamira ni malengo/lengo/wazo kuu la mwandishi katika kazi ya fasihi. Zifuatazo ni dhamira chomozi katika riwaya ya Moto wa Mianzi.
Dhamira kuu
Ukombozi wa kifikra, Wanyigendo waliweza kujitambua kuwa wananyanyaswa na Wadachi na kuanza kutafuta njia ya kijikomboa kutoka mikononi mwa Wadachi. Waliweza kuwa na umoja wa dhati kwa mfano walishirikiana kijiji kimoja hadi kingine kuwapokea waliojitoa mhanga ili kumwokoa Sapi ambaye alikuwa na  Mugoha pamoja na Nyawelu. Sapi alikuwa anatafutwa na Wadachi ili wamnyonge lakini Mugoha,  Nyawelu na Wanyigendo waliweza kushirikiana ili kumwokoa Sapi. Mfano Wanyigendo waliwapokea Mugoha, Nyawelu na Sapi (uk. 14) kutoka kijiji cha Ipamba na kupokelewa Idegesi (uk.22). Hii ilionyesha walikuwa na ushirikiano baada ya kujitambua ili kumwokoa Sapi na waliweza kutumia alama mbalimbali kutoa taarifa kwa wale waliokuwa wanasafiri kwenda Kilolo, na walitumia alama za kufunga nyasi mafundo mafundo na kuyapanga njiani ili kutoa taarifa kuwa hali sio nzuri.Ukombozi wa kisiasa,
Ukombozi wa kisiasa, Ni kujikomboa kiitikadi ambapo itikadi moja inapingana na itikadi nyingine na kusababisha hali ya mvutano kati ya  matabaka. Katika riwaya hii mwandishi amefanikiwa kuonyesha ukombozi wa kisiasa uliokuwa  unafanywa na Wahehe ili kupata uhuru katika jamii zao.
Ujasiri na kujitoa mhanga
Ni hali ya mtu au watu wachache kukubali kujitoa kwa ajili ya wengi,a kwa ajili  liwaya hii wamejitokeza wahusika walio weza kujitoa muhanga kwa ajili ya watu wao mwandishi ameweza kumtumia muhusik Mugoha aliyejitolea kukamatwa na wadachi na kujiita Sapi ili aweze kumuokoa Sapi. Hii tunapata katika ukurasa wa 72 Mugoha anasema                                       “Nataka kuwahadaa. Hakuna njia nyingine”                                                                                                                “Utawahadaaje?Alizidi kuuliza.                                                                                       “Nitawaendea na kuwaambia kuwa mimi ndiye Sapi”
Pia katika ukuras wa 86-87  ujasili wa Mugoha unaendelea kujidhihilisha alipo ambiwa na Sapi baada ya kukutana nae gerezani anasema. Ni hivi, wewe ulipoamua kujitoa kwa Wadachi kwa niaba yetu, ulifanya uamuzi wa kujitoa muhanga kutoa maisha yako kwa niaba yetu. Bahati mbaya  nilikuwa usingizini  hivyo ni kama sikuwepo. Ningekuwepo nisingekubali uchukue hatua hiyo” Katika jami zetu za sasa za kitanzania na Africa kwa ujumla, wapo watu ambao hujitolea maisha yao kwa ajili ya kukomboa maisha ya ya watu walio wengi licha ya kwamba huweza kukumbana na vizingiti vingi na wengine huishia kufa au kufungwa magerezan lakini lengo ikiwa ni kuwakomboa wanajamii
Usaliti
Ni kitendo cha kwenda kinyume na makubaliano. Katika riwaya hii usaliti umeweza kujitokeza pale ambapo wanajamii wachache walikuwa wakiwasaliti wenzao na kukwamisha juhudi za kujikomboa mikononi kwa wananchi kutoka mikononi mwa wadachi. Mwandishi anamuonyesha mhusika Kafugwa akiwasaliti wazawa wenzake na kuungana na Wadachi. Usaliti huo ulipelekea kuzorota kwa mchakato wa kuumpeleka kijana Sapi na kumfikisha kwa Mukwava, kupelekea kukwama kwa shughuli za mapambano kati ya Wanyigendo na Wadachi.Katika uk 62 mwandishi anasema
         “Sapi! Mugoha! Nyawelu! Tovi! Itikeni! Juhudi zenu ni bure. Hamtaweza kutoroka.           Mmekwisha zungukwa. Wekeni silaha zenu chini; mjitoe mapema! Labda Bwana mkubwa           atawahurumia! Mnasikia!                                                                                                                   Tulimsikia vizuri kabisa! Alikuwa ni Kafugwa kawaongoza maadui kuja kutukamata”.
Katika jamii za sasa wapo watu ambao hujikuta wakiwasaliti wenzao, usaliti huo unaoweza ukajitokeza katika Nyanja za kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni,usaliti huo husababisha kukwama kwa juhudi za watu katika kuyafikia malengo yao ya kujikwamua kimaisha
Umoja na Ushirikiano
Ni ile hali ya  jamii ya watu kuwa na mawazo yanayofanana na kuyasimamia ili kuweza kufikia lengo fulani. Umoja na mshikamano ulionekana kuwa mkubwa sasna baina ya wananchi wa kalenga licha ya kukutana na changamoto nyingi za utawala wa mabavu wa mdachi. Katika riwaya hii mwandishi ameonyesha umoja na mshikamano kati ya Wanyigendo wa kijiji kimoja hadi kingine, kwa kuwaongoza Mugoha, Nyawelu pamoja na Sapi katika safari yao ya kwenda Kilolo kwa kuwapa chakula na mahitaji mengine muhimu, na pia kuwafahamisha katika sehemu zenye hatari kama katika kijiji cha Ipokela walitumia nyasi katika kuzifunga na kuziweka katika mafundo njiani. Haya tunayapata katika ukurasa wa 67-68 ambapo mwandishi anasema;                                                                                         “Tulianza kulichunguza eneo hilo tukitafuta alama iliyochorwa na  Wanyigendo.kwa kawaida    kama kuna hatari Wanyigendo waliacha alama ya mafundo matatu ya nyasi zilizoota kando ya      njia, upande wa kushoto. Mafundo hayo yalifungwa kila baada ya hatua tano kufuata usawa wa njia”.Pia Mugoha, Nyawelu na Tovi walishirikiana kufanikisha zoezi la kumtorosha Sapi ili kumtoa mikononi mwa Wadachi kwani Tovi aliwasaidia kuwaibia punda. Katika jamii yetu umoja na ushirikiano ni muhimu ili kudumisha maendeleo katika mambo mbalimbali.
Nafasi ya Mwanamke katika jamii
Mwandishi Mulokozi amemchora mwanamke kama mtu jasiri kwa kumwonyesha mhusika wake Nyawelu ambaye alitenda matendo ya kijasiri kama kuwalinda wenzake usiku wakiwa wamelala. Pia kitendo cha kutembea usiku na mtoto mgongoni ni kitendo cha ujasiri sana, na  alikuwa mbele kabisa ya msafara, mfano uk.wa 23 “Baridi kali, Nyawelu aliuvunja ukimya ule huku akijaribu kumfunika mtoto vizuri zaidi kwa mbeleko yake ya ngozi; pi uk.wa 27 Nyawelu alikuwa ni msichana wa ajabu, alikuwa mvumilivu, mkomavu na jasiri aliweza kustahimili wakati sisi tuliojiita wanaume tulipoporomoka kama vifusi kwa uchovu”
Pia Nyawelu aliweza kumkamata askari Mwafrika  aliyekuwa akiwatumikia Wadachi  na kumfunga kamba. Hii ni kwa sababu baadhi ya Waafrika  waliungana  na watawala kuwapinga  waafrika wenzao.Hili linajidhihirisha katika ukurasa wa 19,Chusu anamwabia Nyawelu,  “Nawe ukamkamata ukamfunga kamba na kumchapa viboko?” “Sikumchapa, nilimfunga tu. Nyawelu alieleza.
Nyawelu amechorwa kama mwanamke mchapakazi,Walipokuwa Uzungwa na wenzake aliweza kuamka usiku na kumkatia punda majani.Katika ukurasa wa 56 Nyawelu anasema, “Mlipolala nilimsikia punda akilia . Nikakumbuka kuwa tulikuwa hatujampa chakula. Nikaamka kwenda kumkatia majani.”
Suala la ukatili na udhalilishaji,
Hivi ni vitendo ambavyo ni kinyune na haki za binadamu.Kulikuwa na udharirishaji uliofanywa  na wadachi baina ya watu watu wa kalenga kama vile walikuwa wakivuliwa nguo hadharani, kuchapwa  viboko vingi ka wanyama na kunyongwa.Haya yanajionyesha katika uk 44 ambapo mnyigndo mmoja alidhalilishwa kwa kuchapwa viboko vingi baada ya Sakalani kudhani kuwa alikuwa anamjua Sapi na kukataa kumtaja.Sakalani alisema“Piga yeye hamsa wa- ishirini,” Sakalani aliamuru.Papo hapo askari wawili  walimbwaga chini yule mtu, wakamlaza vizuri kifudifudi na kumteremsha kaniki aliyojifunga kiunoni. Halafu askari mwingine  alipokea mjeledi kwa mzungu  akaanza kumcharaza.” Baada ya kuchapwa  yule askari akamwambia “Vya  Bwana mkubwa tayari,sasa pokea changu,Alimwongezea  kiboko cha ishirini na sita”.Vile vile katika jamii yetu kuna baadhi ya watu katili wanaodhalilisha wengine mfano kuwatukana mbele ya wenzao. 
Matabaka
Hii ni hali ya  kutokuwepo kwa usawa baina ya pande mbili,yaweza kuwa katika Nyanja ya kisiasa, kiuchumi,kiutamaduni na kijamii . Katika riwaya hii matabaka yaliyojitokeza kwa uwazi ni matabaka ya kisiasa baina ya wenyeji(Wanyigendo) na wageni(Wadachi) ambapo Wadachi walikuwa wakiwatawala wenyeji kimabavu. Tabaka tawala likiongozwa na Bwana mkubwa ambaye ni Sakalani wanachi walikuwa hawana maamuzi yoyote kila kitu waliamuliwa na utawala wa kidachi, mfano ukurasa wa 36, Lwang’a  anasema, “Alfajiri na mapema tuliamshwa na mpiga mbiu aliyekuwa akipita nyumba hadi nyumba akipuliza pembe na kutangaza kwa kuu  “Myuu! Myuu! “Sikilizeni! Sikilizeni! Enyi wana Kipengelo! Taarifa ya serikali mzungu! Sikilizeni! Sikilizeni! Sikilizeni! Leo Bwana mkubwa anakuja kila mtu anatakiwa kwenye uwanja wa kijiji”. Mtu ambaye alikuwa haudhurii kwenye mkutano alikuwa anaadhibiwa kwa kuchapwa viboko au kunyongwa.
Uzalendo
Hii ni hali ya mtu au watu kuipenda nchi yao  kuwa tayari kuitumikia , kuilinda, kuipigania na kuitetea kwa hali yoyote kwa mfano kupoteza uhai kwa ajili ya wengine  Mwandishi katika riwaya hii ameonyesha suala la uzalendo kwa kuwaonyesha Wanyigendo jinsi walivyokuwa wakipambana  na Wadachi, walishirikiana kwa pamoja katika hali na mali. Mfano mwandishi amemtumia mhusika wake Lwang’a, akisema, “Awepo asiwepo la muhimu ni kwamba sisi ni Wanyigendo tunawajibika kumsaidia iwapo atafika pande hizi”.Pia ukurasa wa 47 ambapo akina Mugoha Nyawelu na Lwang’a, walikuwa wakimzungumzia Sapi aliyekuwepo mbele yao lakini kwa jina tofauti la Msavilana  ili asigundulike na watu. Pia kitendo cha Nyawelu, Mugoha na Sapi kuwa tayari kutembea usiku mwendo mrefu kumtorosha Sapi ili kuokoa uhai wake inaonyesha hali ya uzalendo kwani hawakuogopa kufa, wanyama wakali wala hatari yoyote ambayo ingeweza kuwapata wakati wa usiku. Hii inapatikana katika kurasa zote za kitabu hiki.Hata katika nchi zetu kuna watu wenye hali ya uzalendo wanaojitoa kwa ajili ya nchi yao na wenzao pia katika kutetea uhai na haki.
Utawala wa mabavu
Ni utawala unajikita katika kutuma nguvu kama vile jeshi na wanachi kuto kuwa huru kuchangia mawazo yao. Katika riwaya hii utawala wa kutumia nguvu ndiyo ulitawala kwani watu walio enda kinyume na utawala huo walinyongwa na wengine kufungwa,pia vitisho vikali viliendelea kutolewa kwa yeyete atakaye pinga utawala wa kidachi. Haya tunayaona katka  uk 46 Sakalani anasema “hivyo kama msipotii mtakamatwa na kupelekwa Bomani kuchapwa na kufungwa. Wale watakaosaidia au kuficha maadui watakamatwa na bila shaka watanyongwa. Pia amri ziliendelea kuwa na kuwafanya watu kuishi kwa uwoga na kukosa uhuru Sakalani anasema
“ Amri ya moja , kuanzia sasa marufuku kwa mutu yeyote  ya kipengelo kwenda nje ya kijiji hii ila kwa luksa maalumu ya selikali”
“Amri ya mbili,kutoka sasa marufuku kabisa kwa mtu yeyeto wa kipengelo kutembea usiku. Kama mtu naonekana usiku askali napiga yeye risasi, shauri kwisha”
Hitimisho
Maudhui yaliyopo katika riwaya hii yanasadifu kwa kiasi kikubwa mambo yaliyopo katika jamii ya sasa kwa mfano suala la usaliti. Katika riwaya hii tumeona suala la usaliti baina ya Waafrika wao kwa wao wakisalitiana kipindi cha kupigania uhuru wao na kumpinga Mdachi, vile vile katika jamii yetu ya sasa tunaona jinsi ambavyo viongozi wetu wakishapata madaraka wanaanza kuwasaliti Watanzania wenzao. Pia suala la matabaka; tumeona tabaka la wazungu ambao ni Wadachi na ambalo ndilo tabaka la juu linalomiliki kila kitu na tabaka la Waafrika ambao ni watu duni wananyanyaswa na kuonewa. Vile vile matabaka haya yapo katika jamii yetu. Kuna tabaka la wenye navyo yaani matajiri na viongozi na tabaka la wasionavyo yaani raia wenye hali duni, masikini ambapo tabaka la wenya navyo linawanyanyasa watu wa hali ya chini na wale walioshika hatamu za uongozi wanawaanyanyasa raia wengine wanaoishi katika shida. Na pindi watu hawa wa tabaka la chini wanapoungana na kudai haki zao wanazuiliwa na vyombo vya dola na wakati mwingine wanapigwa na wengine kuuwawa.
MAREJELEO
Mulokozi, M.M (1996) Moto wa Mianzi; Morogoro; ECOL Publication
Powered by Blogger.