SIFA ZA FASIHI SIMULIZI
(a) Sifa ya utendaji
huifanya fasihi simulizi kuwa hai. Utendaji unaambatana na masimulizi
ya mdomo wa fanani na sikio la hadhira. Utendaji pia unaweza kuambatana na
muziki au ishara za mwili ambazo fanani huziwasilisha kwa hadhira yake. Utoaji
wa fasihi simulizi hutegemea sana matumizi ya
viimbo, shada, miliolio (viigizi)
na vifaa vingine vya semi. Panaweza pia kuwa na ishara zinazoonekana kama vile
midomo kuchezeshwa na kubinuliwa, kukunja uso, kubinya macho, kugusa mabega
na misogeo mingine ya mwili, na
kadhalika.
Mtendaji (fanani) ni muhimu sana katika fasihi
simulizi inayoelemea katika utendaji. Mtendaji ndiye anayefanya mambo kama
kuimba, kutamba, kusema na kadhalika. Wakati mwingine huyu hutunga tanzu za
kifasihi simulizi na huziwasilisha kwa hadhira. Mara nyingi mtendaji hueneza
kazi zilizokwisha tungwa na fanani wengine hapo zamani. Ni kwa njia hii fasihi
simulizi huenezwa na kupokezana toka vizazi hadi vizazi.
(b)
Kuweko kwa hadhira
inayokabiliana na fanani (mtendaji) kunafanya kuwe na
athari mbalimbali za kiuhusiano kati yao.
Kama utendaji wa fanani hauiridhishi hadhira, fanani anaweza
kuirekebisha kazi yake na kuifanya iwe bora zaidi. Kipimo cha uzuri wa
uwasilishaji wake kitatokana na athari inayojitokeza kwa hadhira yake. Wakati
hadhira hiyo inapojishirikisha katika utendaji, kimsingi itaweza kupanua mbinu
na nafasi ya welewa wa dhamira zinazoelezwa na fanani.
(c)
Suala la mazingira
pia ni la muhimu sana. Mazingira huathiri mara zote
usanii wa tungo pamoja na maudhui yake. Kwa mfano ziko tungo ambazo kimsingi
huambatana na matukio maalum. Aidha, hata kama tungo hizo zikipitwa na wakati,
zinaweza zikabadilishwa na fanani ili kusadifu mazingira maalumu ya wakati huo.
Wakati mwingine, fasihi simulizi huwa na tabia ya kuwa na ujitegemeaji. Mara nyingi fasihi simulizi hujitegemea katika sanaa za ghabi (mf. muziki) na kuchota uhai wake kutokana na vitendo na vitabia vya fanani, toni ya muziki na kadhalika. Kutokana na tabia hii ya ujitegemeaji, fasihi simulizi ikiwekwa katika maandishi huonekana kuwa chapwa kwa sababu mambo kama vidoko, miondoko, na ngoma vinakuwa havimo. Vitu hivyo haviwezi kuhifadhiwa kimaandishi na kwa hivyo hii ndio sababu ya kujitofautisha na fasihi andishi; fasihi simulizi ina maisha, yaani ni hai.