Dhana ya Lugha kienzo na umuhimu wake katika utengenezaji wa kamusi

 Dhana ya Lugha kienzo na umuhimu wake katika utengenezaji wa kamusi

Katika kujadili mada hii tutaangalia dhana ya lugha kienzo kama ilivyojadiliwa na wataalamu mbalimbali, mifano ya lugha kienzo kutoka katika kamusi, umuhimu wa lugha kienzo na mwisho tutatoa hitimisho juu mada hii.
Dhana ya lugha kienzo imejadiliwa na wataalamu mbalimbali, miongoni mwa wataalamu hao ni pamoja na:
Bwenge (1995) kama alivyonukuliwa na Mdee (1997) wanasema kuwa lugha kienzo ni lugha au ni mtindo utumikao kufasili au kueleza leksimu za lugha. Kwa kifupi lugha kienzo ni lugha itumikayo kuifafanua au kuifasili lugha. Anaendelea kusema dhima ya lugha za lugha kienzo ni: kueleza lugha kwa ufasaha, utoshelevu , kwa muhtasari na uwazi ili kumwezesha  mtumiaji kupata na kuelewa mara moja kile anachokitafuta bila kumchosha akili.
Fasili hii inaelezea dhana ya lugha kienzo kwa ujumla katika lugha,  lakini hata hivyo kamusi nayo ina lugha inayotumiwa kuelezea taarifa mbalimbali zinazohusu kidahizo ambazo huingizwa katika kamusi. Lugha hii ndio huitwa lugha kienzo ya kamusi.

Lugha kienzo ya kamusi kwa mujibu wa Mdee (1992) akinukuliwa na Mdee (1997) ni lugha ya mjazo au msimbo inayotumiwa kueleza vidahizo katika kamusi. Lugha hii ndio anayoitumia mtunga kamusi kutoa maelezo ya kisarufi, ya kimaana ya kidahizo, maelezo amabayo mtumiaji wa kamusi huyatafuta anaporejelea kamusi. Anaendelea kufafanua kuwa lugha kienzo ya kamusi hujengwa kwa maneno, vifupisho vya maneno, alama za vituo, na alama mabalimbali kadri ya mahitaji ya kamusi, tarakimu , herufi n.k amabazo zimesimbwa dhana za kilekskografia.
Kulingana nafasili hii lugha kienzo ya kamusi huchukuliwa kama msimbo, kwa maana kwamba lugha kienzo ya kikamusi haiwezi kueleweka kwa mtu wa kawaida hadi asimbuliwe maana za lugha kienzo zilizotumika katika kamusi husika. Na hii ndio sababu kamusi nyingi hufafanua kwanza lugha kienzo ilyotumika katika ukurasa wa jinsi ya kutumia kamusi.
Baada ya kuangalia fasili ya lugha kienzo sasa tuangalie mifano ya lugha kienzo inayotumika katika kamusi. Tutaangalia mifano ya lugha kienzo katika kamusi ya TUKI (2004) na Mdee na wenzake (2011). Baadhi ya mifano ya lugha kienzo kutoka katika kamusi hizi ni pamoja na hii  ifuatayo:
Vifupisho
agh. – aghalabu
kd – kidini
 ms/(mse) /– msemo,
nh – nahau,
sie/<sie> – sielekezi.
Tarakimu 
1,2,3. Zimetumika kutenga maana za maneno. Tarakimu zilizo kwenye mabano ya mduara  (1), (2), (3), zimetumika kutenga misemo na nahau. Tarakimu za kipeo kama vile paa1, paa2, paa3, paa4  zimetumika kuonesha maana mbalimbali za hiponimia.
Alama 
, alama ya mkato inatenga orodha ya sinonimu na mfuatano wa vinyambuo.
; alama nuktamkato inatenganisha fasili moja na nyingine ya kidahizo zinazoachana kidogo, fasili na sinonimu ya kidahizo, misemo, methali au nahau na fasili, mfano mmoja wa matumizi na mwingine, kategoria moja na nyingine.
~ inaashiria nafasi ambayo inatakiwa kukaliwa na kidahizo katika fungu la maneno au sentensi bila ya kurudia kukiandika. Mfano pig.a  ~ana, ~iana.
     Alama ya mshale huashiria vibadala
[  ]  kuonesha upatanisho wa kisarufi: [a-/wa-] au uelekezi wa kitenzi [ele].
<  >  kuonesha uamilifu wa vitenzi, katika Mdee na wenzake,  mfano; <ele>, <sie>
(  )  kuonesha muktadha wa matumizi, mfano; dini (din), ubaharia (bah), ushairi                            (ush), tarakimu za orodha ya misemo.
/  / kuonesha asili ya neno, mfno; /Kar/, /Kng/, /Kih/
       kuonesha mnyambuliko wa neno unapoanza baada ya maelezo ya neno                                                kutolewa.
Pia namna ya kufasili kidahizo katika kamusi zote hizi mbili imetokea katika mitindo tofauti. Kwa mfano katika kamusi ya Mdee na wenzake (wameshatajwa), mtindo wao katika kufasili kidahizo unaweza kuonekana katika mifano ifuatayo:
jaala nm [i-] mambo yafanyikayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu; majaliwa.
alama nm [i-/zi-] 1mchoro unaoonesha alama 2 maksi moja au zaidi anazotuzwa mtahiniwa                          baada ya  jaribio au shindano.
fundisha kt <ele> 1 –pa mtu maarifa fulani; elimisha 2 –pa mtu au mnyama maelekezo au             mazoezi ya kufanya kitu fulani.
tibua kt <ele> fanya kitu kilichotulia au kutwama kivurugike kichanganyike na uchafu k.m maji kwenye ndoo, bwawa au kisima.       
Vidahizo hivihivi katika TUKI (wameshatajwa) vimefasiliwa kwa mtindo tofauti kama ifuatavyo:
jaala nm mambo mtu afanyayo kwa uweza wake Mungu; majaliwa
alama nm 1 mchoro au kitu cha kutambulisha kitu; ishara, athari 2 maksi.
fundish.a kt [ele] 1 toa mafunzo; elimisha 2 wezesha mtu au mnyama kutenda kitu fulani kwa                  kumpa mafunzo au mazoezi.
tibu.a kt [ele] vuruga kitu kilichotulia k.v maji katika kisima na kufanya yawe na topetope.
Mtindo wa kufasili vidahizo kama inavyoonekana umetofautiana, fasilinyingine zimefafanuliwa sana na nyingine zimeelezwa kwaufupitu. Kwa hiyo utofauti huu wa kufasili kidahizo pia ni moja ya lugha kienzo iliyotumika kwa mtindo tofauti katika kausi hizi mbili.
Baada ya kuangalia mifano ya lugha kienzo inayotumika katika kamusi sasa tunaweza kuangalia umuhimu wa lugha kienzo katika utungaji wa kamusi. Lugha kienzo inachukua nafasi muhimu sana katika kamusi, umuhimu wa lugha kienzo ni kama ifuatavyo:
Lugha kienzo husaidia kuleta uwekevu katika utengenezaji wa kamusi, yaani kufupisha maelezo yasiwe marefu. Kwa mfano matumizi ya alama na vifupisho mbalimbali kama vile bugia kt <ele>, buluu, /King/. Hapa badala ya kusema hiki ni kitenzi elekezi ametumia alama na vifupisho ili kuweka uwekevu, na badala ya kusema neno buluu linaasili ya lugha ya kiingereza ametumia ufupisho ili kuweka uwekevu, au katika neno kanisa [li-/ya-] badala ya kusema neno hili lipo katika geli ya li-/ya emetumia kifupisho li kuweka uwekevu.
Husaidia kutolea taarifa mbalimbali za kikamusi kikamilifu. Kwa mfano fasili na matumizi yake kama vile kambarau nm [i-/zi-] 1 winchi ya kuinulia vitu vizito, kali –enye ubapa ulionolewa na unaoweza kukata kitu, -iliyochongoka: shoka limenolewa na sasa ni kali. Kwa hiyo taarifa hizi humsaidia mtunga kamusi kuelezea kidahizo kwa ukamilifu na kieleweke vizuri kwa mtumiaji wa kamusi, kwa kutumia vifupsho, na maelzo mafupi ya fasili na mifano ya matumizi ya kidahizo hicho.
Huwasaidia watengenezaji wa kamusi kutofautisha taarifa moja na nyingine kwa kutumia mabano na alama za uelekezi.  Mfano; alama < > huonesha uamilifu wa vitenzi ambao ni  <ele> na <sie>, [  ] huonesha upatanisho wa kisarufi [a-/wa-], (  ) huonesha muktadha wa matumizi, mfano; kidini (dn), kibaharia (bah), kishairi (ush), /  / huonesha asili ya neno, mfano; /Kar/, /Kng/, /Kih/.
Husaidia kukamilisha maelezo ya fasili hasa pale inapobainika kuwa maelezo ya fasili bado hayatoshelezi katika kuelezea maana ya neno husika. Mfano, Balbu kitufe cha kioo kinachotoa mwanga wa umeme; . Picha hii inafanya fasili ya kidahizo kuwa dhahiri zaidi na hivyo ni rahisi kwa mtumiaji kujenga dhana ya kitajwa hicho.
Lugha kienzo humsaidia mtungaji kamusi kuitofautisha kamusi yake na kamusi nyingine. Hii ina maana kwamba katika kufasili vidahizo mtungaji kamusi yuko huru kutumia mtindo wake ambao utamwezesha kufasili kidahizo kwa ufasaha, uwazi na ufupi bila kuacha uvulivuli wa maana ya kidahizo hicho. Na mtindo huu  wa kufasili kidahizo ndio utamfanya kamusi yake ionekane bora au isiyokuwa na ubora.
Pia lugha kienzo husaidia kupamba kamusi na kuifanya iwe na mvuto kwa wasomaji. Kwa mfano picha na michoro mbalimbali katika kamusi ya Mdee na wenzake (wameshatajwa) imefanya  kamusi hii iwe na mvuto.
Pamoja na umuhimu wa lugha kienzo katika utungaji wa kamusi lakini pia lugha kienzo ina umuhimu kwa mtumiaji wa kamusi. Umuhimu wa lugha kienzo kwa mtumiaji wa kamusi ni pamoja na:
Kumsaidia mtumiaji wa kamusi kujua asili ya kidahizo husika hasa vile vyenye asili ya kigeni, kwa mfano Ilani /Kar/. Kwa hiyo mtumiaji wa kamusi ataelewa kuwa neno ilani lina asili ya kiarabu.
Kumsaidia mtumiaji kamusi kuelewa taarifa za kidahizo kwa urahisi kama vile kategoria. Taarifa mbalimbali za kidahizo humsaidia mtumiaji kuelewa maana ya kidahizo  kwa hurahisi.
Vilevile lugha kienzo humsaidia mtumiaji wa kamusi kujua mipaka ya matumizi ya neno husika. Mfano neno linatumika katika mazingira ya kidini, sheria au neno ni la kilahaja.
Pia humsaidia mtumiaji wa kamusi kujua kategoria mbalimbali za maneno kwa mfano. kambarau nm, bugia kt. Kwa hiyo mtumiaji anapoona maneno haya atajua ni ya kategoria gani ya maneno.
Kwa ujumla hakuna kamusi isiyokuwa na lugha kienzo na kila kamusi ina lugha kienzo yake ingawaje hutofautiana kwa kiasi kidogo sana hasa katika matumizi ya alama, vifupisho na mtindo wa kufasili kidahizo, kwa mfano alama [] katika kamusi ya Mdee na wenzake (wameshatajwa) imetumika kuonesha upatanisho wa kisarufi ilihali katika kamusi ya TUKI (wameshatajwa) imetumika kuonesha uelekezi wa kitenzi. Kwa hiyo kutokana na tulivyokwisha jadili lugha kienzo ni muhimu sana katika kamusi kwani husaidia ufafanuzi wa kidahizo ambacho ndio msingi wa kamusi na pasipo lugha kienzo itakuwa vigumu sana kuelewa taarifa mbalimbali za vidahizo.

MAREJEO
Mdee, J.S. (1997). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Mdee, J. S. na wenzake. (2011). Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn Publishers (K) Ltd.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Powered by Blogger.