FASIHI YA KISWAHILI YA MAJARIBIO
FASIHI YA KISWAHILI YA MAJARIBIO
Makutano ya Fasihi Simulizi na
Fasihi Andishi
F.E.M.K. Senkoro
Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Ikisiri
Makala hii inatalii maana ya fasihi ya Kiswahili ya majaribio, kwa kupitia
kanuni za kifasihi simulizi ambazo zinaelekea kuwa msingi na mwimo wa
majaribio hayo. Makala inaonyesha kuwa kanuni hizi ndizo ambazo
zimejidhihirisha hata katika fasihi ya Kiswahili ya hivi karibuni ya waandishi
waliofanya majaribio ya aina mbalimbali, wakiwemo wa tamthilia, riwaya na
hadithi fupi. Makala inatumia zaidi mifano kutoka katika tamthilia za Lina
Ubani (P. Muhando) na Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi (E. Hussein) na pia
riwaya ya Rosa Mistika (E.Kezilahabi) kueleleza majaribio hayo. Swali ambalo
hatimaye linajadiliwa ni, je, majaribio haya yanafuata kanuni zipi? Upya una
nafasi gani katika majaribio? Na, je, majaribio mahsusi ya fasihi fulani
yanaanza na kuisha wakati gani?
1.0 Utangulizi
Kanuni za utanzu wowote wa fasihi huambatana na kuamuliwa na maana ya
utanzu huo. Tuongeapo kuhusu kanuni za uwanja fulani wa fasihi hapohapo
tunajaribu kuangalia yale mambo yajitokezayo mara kwa mara katika uwanja huo.
Pia tunazingatia ukweli kuwa kanuni hizo hazibakii hivyohivyo kwani huweza
kubadilika kufuatia mabadiliko katika utanzu unaohusika.
Kwa vile majaribio mengi yaliyofanyika katika fasihi andishi ya Kiswahili
yanaelekea kuwa yamechota kutoka katika fasihi simulizi ya Kiswahili / Kiafrika,
makala inaanza kwa kuzipitia kanuni hizo za fasihi simulizi - kanuni mahsusi
zinazoifanya fasihi simulizi ijitegemee. Kanuni hizi huzoeleka tangu wanajamii
wengi wakiwa watoto wadogo wanapotambiwa na wakubwa wao hadithi, visa, na
ngano; wanapotegewa vitendawili pamoja na mafumbo, na kadhalika. Katika
makala hii tumechagua kanuni 12 tu kati ya kanuni nyingi, nazo ni:
• Uelezwaji au utambwaji
• Sifa anazopaswa kuwa nazo mtambaji
• Hadhira na nafasi yake katika uelezaji/utambaji
• Taswira na Ishara
• Mianzo na Miisho ya Kifomula
• Marudiorudio
• Taharuki
• Ucheshi
• Tanakali sauti
• Kuingiliana kwa tanzu
• Muundo
• Majina ya wahusika
22
2.0 Nafasi ya Utambaji na Mtambaji
2.1 Utambaji
Fasihi haiwi fasihi simulizi hadi itambwe na itolewe kwa njia ya mdomo. Uelezaji
au utambaji mara nyingi hutegemea aina ya hadhira. Kwa mfano, utambaji katika
utanzu uleule mmoja, tuseme wa misemo, utaweza kutofautiana kulingana na
hadhira: misemo itakayotolewa kwa watoto wadogo ni dhahiri kuwa itatofautiana
na ya watu wazima. Uelezaji na utambaji wa tanzu mbalimbali za fasihi simulizi
kwa watoto wakati huohuo hutumika kuwapa mazoezi ya usemaji na utambaji ili
wawapo watu wazima nao wawe wasanii; na pia wawe watumiaji wazuri wa
lugha katika maongezi, hotuba na kadhalika. Wakati huohuo, utambaji
huwafundisha watoto kuwa na kumbukumbu za mambo wanayoelezwa na pia
wanayoyaeleza.
Uelezaji huu hauwezi kukamilika bila kuwa na mtambaji mzuri kwani, ijapokuwa
katika fasihi simulizi kila mtu ana uhuru wa kueleza kisa, hadithi au ngano
aliyokwishaisikia kwa mwingine, si kila mtu anaweza kuwa mtambaji bora.
Katika fasihi simulizi za jadi hapakuwa na sheria za "haki za kunakili" kama
zilizopo leo katika baadhi ya tanzu za fasihi hii, kwa mfano katika nyimbo za
bendi zilizorekodiwa.
Mtambaji anatakiwa awe na sifa kadhaa. Kwanza, awe na uwezo wa kuipa upya
habari yoyote anayoieleza ili kuifanya hadhira iifurahie kwani aghalabu hutokea
kuwa baadhi ya wanahadhira wameshawahi kuisikia habari hiyo ikitambwa na
mtu mwingine. Ufundi wa utambaji hujitokeza hasa katika kuielewesha hadhira
ufafanuzi wa yale mtambaji ayaonayo hayajaeleweka vizuri lakini wakati huohuo
aweze kuitoa habari hiyo kiupya na kisanii bila kuhubiri. Mtambaji basi huwa ni
msanii, mburudishaji, mwelimishaji na mtoa maoni kuhusu masuala ya kijamii
yanayoigusa hadhira yake.
Pili, ili aweze kuyamudu yote hayo, msanii hana budi awe anaufahamu fika
utamaduni na historia ya jamii ambamo yale ayaelezayo yametoka. Hana budi
kutopea katika mila na jadi anazoziibusha katika maudhui ya habari
anayoishughulikia. Inamlazimu awe mtaalamu wa lugha aitumiayo na awe mjuzi
wa misemo, nahau, taswira na ishara mbalimbali zinazojenga jambo analolieleza.
Iwapo mtambaji anawapa vijana mazoezi ya kukumbuka mambo wanayoelezwa,
inabidi yeye mwenyewe awe na sifa hii ya kumbukumbu. Hana budi kuwa mtu
mwenye uwezo wa kutunga na pia kuing'amua hadhira yake pale inapombidi, kwa
mfano, abadili mtindo wake labda kwa kuinghiza wimbo hata pale ambapo utanzu
anaoushughulikia si ule wa nyimbo..
Mtambaji huyu huyu hatakiwi awe na aibu bali awe mtu mchangamfu mwenye
kuifurahia habari anayoieleza ili pale anapohitajika kutia madoido afanye hivyo,
23
na pale inapombidi kutumia maneno ambayo katika muktadha mwingine
yangekuwa matusi, asione aibu kuyatumia kifasihi simulizi. Wakati huohuo
mtambaji ni mwigizaji kwani aghalabu anahitajiwa achukue nafasi za wahusika
mbalimbali, wanawake kwa wanaume, watoto kwa wakubwa, wanyama kwa
binadamu.
Mtambaji hatakiwi awe anafahamu historia, mila, utamaduni na jadi za kale tu.
Anatakiwa pia afahamu fika nguvu mbalimbali za kijamii za leo; na awe daraja
kati ya nguvu hizo na zile za mambo ya kale, kwani fasihi simulizi si juu ya
mambo ya zamani tu bali pia huhusu yale yatokeayo leo.
2.2 Nafasi ya Hadhira katika Utambaji
Hadhira, sawa na mtambaji, ni muhimu sana katika uelezwaji na upokelewaji wa
fasihi simulizi. Hadhira ni kichocheo kinachoimarisha uelezwaji na utambwaji
wa fasihi hii. Huongezea ari ya ubunifu wa mtambaji, na wakati mwingine
huweza hata kumsahihisha au kumsaili mtambaji.
Mara kwa mara hadhira pia huwa sehemu ya utambaji kwa kushiriki katika
sehemu mbalimbali, kwa mfano, penye kiitikio, mkarara na matumizi ya nyimbo,
kutegua vitendawili, kumalizia methali, na hata kupiga makofi.
Hata hivyo kiasi cha kushiriki kwa hadhira hutegemea jambo linaloelezwa.
Iwapo jambo lielezwalo ni zito lenye kuhitaji tafakuri na kuwaza kwa undani,
hadhira mara nyingi hubaki kimya bila kushiriki ila tu pale panapohitaji maswali
yaulizwe au majadiliano yafanywe; ijapokuwa mara nyingi hili hutokea mwishoni
baada ya habari kuelezwa.
Kwa hiyo basi, tunaweza kusema kwa jumla kuwa uhakiki wa fasihi simulizi ni
wa papo kwa papo kwani katika kushirikiana na fanani au msanii hadhira
huihakiki pia kazi itolewayo. Kwa kuihakiki hivi, msanii au mtambaji
hurekebisha maelekezo yake au huyaelekeza kule hadhira inapotaka.
2.3 Mtambaji na hadhira katika fasihi ya Kiswahili ya majaribio
Katika fasihi ya Kiswahili ya majaribio, hasa katika tamthilia, waandishi
wamezichota sifa za mtambaji na kuzihamishia katika mtiririko wa tamthilia zao.
Mathalani, Bibi na Mwenehogo katika tamthilia ya Penina Muhando ya Lina
Ubani na mhusika mwenye jina hasa la Mtambaji katika tamthilia za E. Hussein
ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi wametumiwa sana na waandishi hawa kuwa
kiungo baina ya hadhira na wahusika wengine pamoja na matukio muhimu ya
tamthilia hizi. Tangu mwanzo wa tamthilia, wahusika hawa wanaowawakilisha
watambaji wa hadithi wanazianza tamthilia kwa fomula ya kihadithi, na kila mara
wametumiwa na wanatamthilia hawa kufafanua yanayotokea katika mfululizo wa
visa mbalimbali.
24
Watambaji katika tamthilia hizi wanakuwa kama waelezaji wa hadithi ndani ya
hadithi, wanaunda hadithi mbadala ambazo hata hivyo zinazijenga “hadithi” za
msingi za tamthilia hizi. Wahusika hawa wanakuwa kama vile wanaishirikisha
hadhira katika kuiunda tamthilia. Ndio maana, kwa mfano, Mwenehogo katika
Lina Ubani, ijapokuwa ni mchekeshaji, tena mlevi, anatumiwa mara kwa mara
kuunda “vihadithi” vya kuichekesha hadhira, lakini vyenye kubeba ujumbe mzito
unaohusiana na dhamira anazozishughulikia Penina Muhando. Vivyo hivyo,
Mtambaji katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi anapomwongelea kijana
anayepigana na joka anamwita “kijana wetu” ili kifanya hadhira ijisikie kuwa
hadithi au kisa kinachoelezwa si cha mtambaji tu bali ni cha wote wanaoitazama
au kuisoma tamthilia. Katika kuzitamba hadithi zao, wahusika hawa wana jukumu
la kuitahadharisha hadhiya ya watazamaji au wasomaji kuwa yanayoelezwa si
ukweli au uhalisi bali ni mwigo tu wa ukweli na uhalisi huo.
Katika kujaribu kuishirikisha hadhira kwenye tamthilia hizi, watambaji wanauliza
maswali hapa na pale, hasa kwa njia ya kiitikio, ili kujaribu kukaribia hali halisi
ilivyo ya ushirikishwaji wa hadhira katika fasihi simulizi. Mathalani, mhusika
Mtambaji katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi daima hujaribu kuwaamsha
watazamaji/wasomaji kwa kuwauliza kama aendelee au asiendelee na kisa
anachokieleza, na hadhira inatakiwa kujibu, “Endelea!” sawa na vile ambavyo
watoto walizoea kumjibu bibi au babu wakati akitamba hadithi.
Ni katika tamthilia hizi hizi ndimo ambamo watambaji wanamalizia utambaji wao
kwa kuomba wapewe mji. Tamthilia zinamalizika kwa fomula ya vitendawili, na
kwa hakika, wahusika hawa wanapotuomba mji sisi hadhira, na tunapowapa miji
hiyo, wanaahidi kututegulia vitendawili vilivyofumbwa katika tamthilia hizi. Ila,
kinyume na ilivyo katika fasihi simulizi, humu hatupewi jibu. Ni kama kwamba
tunatakiwa turudi nyuma, tuzisome au kuziangalia upya tamthilia hizi ili kupata
majibu yatakayotutegulia utendawili uliomo ndani yake. Tendo la kuzisoma upya
na kuyatafakari kwa undani zaidi yale yaliyosimuliwa katika tamthilia hizi ndilo
uteguaji wa kitendawili.
Hata hivyo, nionavyo mimi, mwishoni mwa Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi
hadhira inabaki na maswali zaidi ya mwishoni mwa Lina Ubani. Utendawili wa
Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi unadhihirika zaidi kwani visa vimefumbwa mno
kiasi cha kujiuliza mwandishi alimaanisha nini; kuliko ule wa Lina Ubani ambao
umepatiwa majibu yasiyohitaji maswali. E. Hussein, basi, ana haki na stahili ya
kuitaka hadhira impe mji kuliko P. Muhando.
3.0 Fani katika Fasihi Simulizi
Ni vigumu kutoa kauli ya jumla kuhusu fani katika fasihi simulizi, kwani hii
itategemea utanzu unaohusika pamoja na maudhui yanayotolewa katika utanzu
huo. Hapa tutaeleza kwa kifupi tu baadhi ya vipengele vinavyoweza kujidhihirisha
katika fani ya fasihi simulizi kwa jumla.
25
3.1 Taswira na Ishara
Mara kwa mara utolewaji wa fasihi simulizi hutegemea sana matumizi ya taswira
na ishara, hasa katika tanzu za ngano-tata, methali, vitendawili na habari za
kimafumbomafumbo. Hapa yamejaa matumizi ya tamathali za semi zenye
kufananisha watu na vitu, au vitu vya aina moja na vya aina nyingine, na
kadhalika. Uhuru wa kisanii humruhusu mtambaji, kwa mfano, katika kuelezea
ujasiri wa shujaa mmoja, aseme kwa dhati kuwa moyo wa shujaa huu haukuwa
wa kawaida, ulitengenezwa kwa mawe. Moyo wa jiwe hapa ni ishara ya ugumu
wa moyo huo wenye kutoa taswira ya ushujaa na ujasiri.
Waandishi wa tamthilia za Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi na Lina Ubani
wametumia ishara kadhaa pia katika visa vya kazi zao. Mathalani, Zimwi ambalo
linajitokeza katika Lina Ubani na Joka katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi
huweza kuwa ishara ya mfumo wa kiutawala wa mabavu, wakati ambapo Huila
na Kijana katika tamthilia hizi ni viwakilisho vya wapigania uhuru na watetea
haki katika jamii zao. Vilevile, ndani ya hadithi ya Iddi Amin Dada ambayo
inajitokeza katika Lina Ubani mna kiwakilisho cha zimwi hilo – kiwakilisho cha
utawala wa aina hiyo. Taswira na ishara nyingine ambazo tunaweza kujiuliza
zinawakilisha nini ni, kwa mfano, mkunazi rahmani na jogoo katika Jogoo Kijijini
na Ngao ya Jadi.
3.2 Mianzo na Miisho ya Kifomula
Katika jamii mbalimbali kuna mianzo ainaaina ya utoaji wa tanzu tofautitofauti
za fasihi simulizi. Hapa tutatoa mifano michache to ijitokezajo katika fasihi
simulizi ya Kiswahili.
Upande wa vitendawili mtoa kitendawili huanza na:
Mtambaji: Kitendawili!
Hadhira: Tega
Baada ya mwanzo huu wa kifomula ndipo kitendawili kinapoteguliwa. Iwapo
hadhira itashindwa kukitegua basi mtegaji huomba "mji". Akubalipo mji
aliopewa hapo huitegulia hadhira kitendawili hicho. Hii tabia au mtindo wa
kuomba "mji” ni dhahiri kabisa kuwa ulitokea katika jamii za baadaye sana baada
ya kuzuka kwa miji. Katika makabila mbalimbali mtegaji aliomba apewe ng'ombe
au mali yoyote iliyotokana na mazingira yaliyohusika.
Upande wa utanzu wa ngano au visa, na hadithi, mianzo iko ya aina nyingi zaidi,
labda kwa sababu utanzu huu umesambaa zaidi ya nyingine za fasihi simulizi.
Mwanzo au kianzio kilichoenea ni cha fomula ya:
Mtambaji: "Hadithi hadithi"
Hadhira: "Hadithi njoo"
26
Mtambaji: "Hapo zamani za kale..."
Mwingine ni:
Mtambaji: "Paukwa"
Hadhira: "Pakawa"
Mtambaji: "Paukwa"
Hadhira: "Pakawa"
Mtambaji: "Hapo kale alikuwako..."
Wakati mwingine baada ya hizo "paukwa-pakawa" mtambaji huweza kurefusha
kianzio kwa:
Mtambaji: "Kaondokea chenjagaa
Kajenga nyumba kakaa
Mwanangu Mwana siti
Kijino kama kijiti
Cha kujengea kikuta
Na vilango vya kupita.
Hapo kale alikuwako..."
Pia hutokea kuwa kabla ya kianzio hiki, badala ya "paukwa- pakawa" mtambaji
huanza kama ifuatavyo:
Mtambaji: "Atokeani"
Hadhira: "Naam Twaibu"
Mtambaji: "Atokeani"
Hadhira: "Naam Twaibu"
Mtambaji: "Kaondokea chenjagaa..."
Kianzio ambacho kimezoweleka sana siku hizi, hasa baina ya watoto ni:
Mtambaji: "Hadithi hadithi"
Hadhira: "Hadithi njoo, uongo njoo, utamu kolea!"
Mtambaji: "Hapo zamani za kale"
Hadhira: "Ehe!"
Mtambaji: "Alikuwako / Walikuwako..."
Kauli hii ya "uongo njoo" haipunguzi uzito wa lile linaloelezwa bali husisitiza tu
kuwa jambo hilo linaelezwa kiubunifu na kuwa siyo uhalisi wenyewe.
Kuhusu kumalizia, mara nyingi mtambaji humalizia kwa, "Na hadithi yangu
imeishia hapo." Pia mtambaji, hasa baina ya watoto, huweza kumalizia kwa
"Hadithi yangu ndiyo hiyo, kama nzuri ipokeeni, kama ni mbaya, nirudishieni."
27
Katika Lina Ubani na Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi fomula hizo za mianzo na
miisho zimetumiwa na waandishi pale ambapo tamthilia zimeanza kama hadithi
na zimeisha kama vitendawili.
3.3 Marudiorudio
Katika fasihi simulizi, kuna nia tofautitofauti katika matumizi ya mbinu ya
kurudiarudia kauli au neno fulani yanayofanywa na watambaji.. Wakati mwingine
si kauli au maneno tu yanayorudiwa bali pia matukio fulani, wazo fulani, au
mkarara/kiitikio, hasa katika nyimbo.
Marudio marudio hayo yanatumiwa na wasanii kwa makusudi tofautitofauti.
Wakati mwingine hutumiwa ili kusisitiza jambo fulani la kimaudhui analotaka
kulionyesha fanani au msanii. Mara nyingine marudio marudio haya yanasaidia
kutoa dhana ya kupita kwa wakati. Kwa mfano, iwapo mtambaji anataka kueleza
juu ya muda mrefu sana uliopita baina ya tukio moja anaweza kusema:
Siku zikapita
Siku zikapita
Siku zikapita
Zikageuka kuwa miezi
Miezi nayo ikapita
Ikapita
Ikawa miaka ambayo pia
Ilipita
Ikapita
Ikapita
Vuli zikaja zikapita
Masika yakawasili yakapita
Vipupwe na viangazi vikaja na kupita
Lakini bado
Bwana yule na mkewe
Hawakupata mtoto
Na ugumba na utasa ukaendelea..."
Hapa ni dhahiri kwamba marudio yanatufanya sisi hadhira tuipate dhana ya
wakati vizuri zaidi kuliko kama mtambaji angesema tu "siku nyingi zikapita ila
yule bwana na mkewe hawakupata mtoto."
Maridiorudio yametumiwa na waandishi wa tamthilia za Kiswahili za majaribio
kwa lengo hilo hilo la kuponyesha kupita kwa wakati. Mathalani, katika tamthilia
ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi dhana hii ya wakati imeelezwa katika sehemu
mbalimbali kwa kurudiwa kwa kauli ya:
Miaka ikapita,
miaka ikapita,
28
miaka ikapita;
watu wakaoana,
watu wakazaana
na kaumu ikazidi.
Inakuwa ni jukumu la hadhira kukadiria wingi wa miaka hiyo iliyopita, na hasa
kutokana na kitendo cha watu kuzaana na kaumu kuongezeka.
3.4 Taharuki
Sawa na katika fasihi andishi, tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hutumia mbinu
ya taharuki ili kuvuta usikivu wa hadhira. Hii hufanya hadhira kujiuliza mara
kwa mara kuhusu matukio yatakayofuatia kuwa yatakuwa ya namna gani.
Ujengaji wa taharuki hutofautiana kutoka mtambaji mmoja hadi mwingine, hata
kama kisa kinachoelezwa ni kilekile kimoja. Mtambaji mwenye ujuzi, uzoefu na
kipawa zaidi atafaulu kuishikilia hadhira yake katika uzi wa taharuki zaidi ya yule
ambaye ndio kwanza anauingia ulimwengu wa utambaji.Ufundi wa kuishikilia
hadhira katika taharuki unaweza kuletwa si kwa yale yanayoelezwa tu bali pia
jinsi yanavyotolewa na mtambaji. Mabadiliko ya sura ya mtambaji, kwa mfano,
huweza kuifanya hadhira ijue kuwa jambo litakaloelezwa baada ya muda mfupi ni
la kutisha, kwa hiyo wawe na taharuki na ari ya kulisubiri. Hata mabadiliko ya
kiimbo cha sauti ya mtambaji huweza pia kuleta hali hiyo ya taharuki.
Mbinu nyingine itumiwayo pia katika fasihi andishi ili kuumba hali ya taharuki ni
ile ya kuchelewesha matukio fulani au majibu ya maswali fulani ambayo
msimuliaji huyafanya yawazukie wasikilizaji au watazamaji wake. Haya
hucheleweshwa hadi baadaye sana wakati ambapo hadhira huwa
imekwishaning'inizwa katika kamba ya taharuki kwa muda mrefu.
Kwa mtambaji mahiri majibu yote hutolewa, au yale ambayo hayatolewi
yanaachwa kwa makusudi kabisa ili hadhira irudi nyuma na kutafakuri
yaliyotambwa.
Waandishi wa tamthilia ya Kiswahili ya majaribio nao hali kadhalika wameitumia
mbinu hii ya taharuki. Kwa mfano, kisa anachokieleza Mtambaji katika Ngao ya
Jadi, kinatufanya sisi tuambatane na Kijana katika mapambano na Joka lenye
vichwa sabini huku tukiwa na shauku ya kujua hatima ya mapambano haya.
Katika nyoyo zetu, tunataka Kijana ashinde kwenye mapambano haya, lakini
tunashikwa na shauku kwani tunajua kuwa anapambana na adui ambaye si wa
kawaida; anapambana na joka la vichwa sabini. Je, ataweza kuvidengua vichwa
hivi, kimoja hadi kingine?
3.5 Ucheshi
Mbinu ya ucheshi, sawa na nyinginezo za fani, hutumiwa na mtambaji kwa nia
tofautitofauti. Kama ilivyo katika baadhi ya kazi za fasihi andishi, vivyo hivyo
katika fasihi simulizi ucheshi hutumiwa kuwa kipumuo, hasa baada ya matukio ya
29
kutisha au maelezo marefumarefu yenye kuwachosha wasikilizaji. Mbinu hii
huweza kutumiwa, kwa mfano, pale ambapo mtambaji labda kaiweka hadhira
yake katika hali ya taharuki kwa muda mrefu, au kaieleza juu ya mambo ya
kitanzia na ya kusikitisha, na sasa wanahitaji kupumua na kutabasamu kidogo.
Katika Lina Ubani maneno ya mhusika Mwenehogo yana ucheshi mwingi sana
ndani yake, ucheshi ambao unatufanya sisi watazamaji au wasomaji tuburudike na
kupumua wakati tukitafakari mivutano iliyopo baina ya akina Huila na wanasiasa.
Hata Ngonjera ya Mota inatufanya tutabasamu tunapoona namna mtoto
anavyoitafsiri hadithi ya kiutu uzima inayoelezwa na Bibi.
3.6 Tanakali sauti
Maneno ya ki-tanakali sauti ni yale ambayo yanaigiza sauti ya kitu fulani au tendo
fulani. Haya yameenea sana katika tanzu mbalimbali za fasihi simulizi, nayo
yanasaidia sana kuyafanya yale anayoyaeleza mtambaji yaeleweke kwa hadhira
yake. Yanasaidia sana kukamilisha hisia za hadhira, kwani mara nyingi
hushughulikia milango yote mitano ya fahamu za mtu: ya kunusa, kusikia, kuona,
kuhisi, na kuonja.
Katika Jogoo Kijijini, kwa mfano, E. Hussein katumia mbinu hii mara kadhaa
kuumba hali anayotaka iumbike akilini mwa hadhira. Mtambaji kasema,
mathalani:
..... Mara
Kupi
Jua lilikupiza
Pa
Mwanga kajikatiza
Zi
Na giza kaingia (uk. 17)
Maneno "kupi", "pa" na "zi" ni ya kitanakali-sauti, ijapokuwa "sauti" zenyewe ni
za kuwazika tu kwani hakuna mtu aliyewahi kusikia "sauti" ya jua likikupiza, ya
mwanga ukijikatiza, au ya giza likiingia.
3.7 Kuingiliana kwa Tanzu
Kutumiwa kwa utanzu mmoja wa fasihi simulizi katika utolewaji wa utanzu
mwingine ni mbinu ya kifani itumiwayo na wasanii wa fasihi hii kwa nia
mbalimbali. Kwa mfano, si jambo geni kukuta wimbo, au kipande cha wimbo,
ndani ya ngano au hadithi. Wimbo, au kipande hiki, huweza kutumiwa ili kuleta
msisitizo wa jambo fulani aonalo mtambaji kuwa lina umuhimu, na kwa hiyo
katika wimbo huo maudhui ya jambo hilo yanarudiwa. Pia huweza kutumiwa
kama njia ya kuondoa uchovu pale ambapo msanii anang'amua kuwa ametoa
maelezo marefu mno ya kinathari. Hapa msanii huweza kubadili pia na kuingiza
mbinu za ushairi.
30
Baadhi ya wasanii au watambaji hutumia mbinu za kuingiza tanzu nyingine katika
kazi zao kuwa njia ya kuleta mtiririko wautakao utakaounganisha sehemu na
sehemu katika visa vyao. Mara nyingi tanzu ndogondogo kama vile methali,
vitendawili na misemo hujitokeza sana hasa katika ngano, visa, na hadithi. Hizi
hutumiwa na wasanii katika kuimarisha maudhui ya tanzu zao, na aghalabu
methali hutumiwa mwishoni mwa utambaji ili hadhira ilipate fundisho humo.
Waandishi wa tamthilia za Kiswahili za majaribio nao hali kadhalika waliitumia
mbinu hii ya kuingiliana kwa tanzu katika tamthilia zao. Kama
ilivyokwishakuelezwa, pamoja na kwamba vitendawili na ngano ni tanzu mahsusi
zinazojitegemea katika fasihi simulizi, waandishi hawa wamezichanganya tanzu
hizi na ule wa tamthilia ambao kwa hakika ni utanzu mgeni wakaunda tamthilia
mpya. Katika Lina Ubani pia, utanzu wa wimbo umejitokeza sana, na tunauona
katika wimbo wa Bibi ambao kwa hakika ni sehemu ya hadithi inayotambwa.
Hali hii ya kuingiliana kwa tanzu za fasihi simulizi inatia shaka namna ambavyo
wanazuoni wamekuwa wakiziainisha tanzu hizo. Inawezekana kabisa kuwa tanzu
za fasihi simulizi ya Kiafrika hazitakiwi kuainishwa mojamoja; lakini hili
linahitaji utafiti zaidi.
3.8 Muundo
Si rahisi kutoa kauli ya dhati kuhusu miundo ya tanzu mbalimbali za fasihi
simulizi kwani tanzu hizi ni nyingi na zinatofautiana kutoka sehemu hadi sehemu.
Muundo rahisi kuueleza ni ule wa vitendawili ambavyo daima huwa na mianzo na
miisho ya kifomula. Kwamba miundo hufuatana na mianzo na miisho ya tanzu
mbalimbali ni rahisi kuelezeka. Lakini hii ni mianzo na miisho tu. Yaliyomo
katikati yake, ambayo aghalabu ndiyo muhimu, yana utata kueleza miundo yake.
Tuwezalo kufanya hapa ni kutoa kauli ya jumla tu kuhusu kigezo hiki.
Kuna visa, ngano, na hadithi ambazo miundo yake ni ya moja kwa moja.
Muundo hapa unamaanisha mfuatano au mtiririko wa matukio, vitendo, na hata
mawazo yalivyopangwa. Kwa hiyo, katika tanzu hizo zenye miundo ya moja kwa
moja matukio yake ni ya moja kwa moja yenye mwanzo, kati, na mwisho; sawa
na vile ambavyo siku huanza na alfajiri - asubuhi - adhuhuri - mchana - jioni -
usiku. Mianzo ya tanzu hizi mara kwa mara hutoa tatizo au mgogoro, na
mgogoro huu hutatuliwa au kuchambuliwa katika sehemu ya kati na hatimaye
sehemu ya mwisho huonyesha mgogoro ukiwa umetatuliwa. Mara nyingi
tunapofuatilia mgogoro ujitokezao katika kisa chenye muundo wa moja kwa moja
hapo hapo huwa tunamfuatilia mhusika mkuu na kubadilika pamoja na kukua
kwake, kwani aghalabu mgogoro mkuu humzungukia yeye.
Waandishi wa tamthilia ya Kiswahili ya majaribio nao hali kadhalika wametumia
miundo changamani kwani matukio mbalimbali yamejengwa kufuatana na
utambaji ambao huenda mbele na kurudi nyuma kama watakavyo watambaji
wake. Kwa hiyo, kwa mfano, Lina Ubani inaanza na kilio cha Bibi ambaye
31
kampoteza mwanawe, halafu hatua kwa hatua, tunarudishwa nyuma na
mwandishi ambaye anatutaka tuyafuatilie matukio tangu mwanzo hadi kufikia
hapa kwenye maombolezo ya Bibi ambayo kwa hakika ni mwanzo wa tamthilia
na ni mwisho wa hadithi.Wimbo unaojitokeza katika tamthilia ya mwandishi
huyuhuyu ya Nguzo Mama ni mfano mzuri pia wa kuingiliana kwa tanzu. Wimbo
huu unaorudiwarudiwa na akina mama kwenye tamthilia hii unatakiwa usisistize
ugumu wa kuisimamisha nguzo ambayo inatakiwa iwakilishe ukombozi wa akina
mama hao.
3.9 Wahusika
Katika fasihi simulizi kuna wahusika wa aina mbalimbali: watu, wanyama, ndege,
wadudu, mimea, na hata vitu visivyo na uhai kama vile mawe. Pia wahusika wa
kiajabu-ajabu, wa kuwazika tu kama vile mashetani, hutumiwa katika fasihi hii.
Wahusika hawa wote huweza kuingiliana pale ambapo mhusika mtu huweza
anakutana na hata kuongea na mhusika asiye mtu kama vile jini, shetani, mti, au
hata jiwe. Hali kadhalika, katika ulimwengu wa fasihi simulizi si ajabu kukutana
na wanyama, miti, au ndege wanaofanya matendo sawa na ya watu. Si ajabu
ndege wakichumbiana, wakioana na kufanya sherehe za harusi kama watu tu.
Wahusika wa aina zote hizi hawawezi kuingiliana na kuongea baina yao katika
ulimwengu wa fasihi simulizi tu, kwani hata katika majaribio ya kifasihi andishi,
mathalani, katika tamthilia hizo mbili, wahusika watu wanapambana na wahusika
wa kiajabuajabu ambao katika hali ya kawaida hawajawahi kuonekana, kushikika
wala kusikiwa – zimwi na joka la vichwa sabini.
Hadhira inatakiwa iamini kabisa kuwa wahusika wa aina hii wapo kwani
wahusika wote hawa kwa njia hii ama ile, wanahitajiwa wawakilishe tabia,
mienendo na matendo ya watu halisi. Kwa mfano ujanja wa mhusika maarufu
katika baadhi kubwa ya visa na hadithi za fasihi simulizi za Afrika ya Mashariki,
Sungura, unahitajiwa uwakilishe ule wa watu watundu; wakati ambapo
"uchinichini" wa Mzee Kobe ni kiwakilisho dhahiri cha wale watu ambao kwa
kawaida ni wapole ijapokuwa katika upole wao mmejificha ujanja na hekima.
Sawa na fasihi simulizi ya Afrika Mashariki ambamo Sungura ndiye mhusika
mjanja sana, fasihi simulizi za sehemu zingine pia huwa na mhusika apendwaye
na maarufu kwa ujanja wake. Kwa mfano huko nchini Ghana mhusika huyu ni
Buibui, wakati huko Nigeria mhusika-pendwa ni Kobe. Aghalabu wahusika
wajanja huwa ni wanyama au wadudu wadogo. Ujanja wao unapowapumbaza
wahusika wakubwa-wakubwa kama vile Tembo, Simba, au Kiboko na kutufanya
sisi hadhira tuwaone kuwa ni wajinga, husaidia sana katika kuleta ucheshi ndani
ya lile linaloelezwa. Si hivyo tu, bali pia wahusika hawa husaidia sana kujenga
maudhui ya kazi za fasihi simulizi. Kwa mfano, kila wawapo washindi dhidi ya
wahusika wengine wakubwa tunapata funzo kuwa ushindi katika jambo lolote lile
hautokani na umbo, wingi au idadi, bali hutokana na mbinu, ujanja na utundu.
Funzo hili huweza kupanuliwa zaidi na kuwapa moyo watu au mataifa manyonge
yanayopigania haki zao.
32
Mara nyingi wahusika wakubwa-wakubwa hutumiwa na wasanii ili kusuta
majivuno na maringo, pamoja na tabia za mabavu za baadhi ya watu katika jamii.
Wahusika Zimwi na Joka katika majaribio waliyoyafanya E. Hussein na Penina
Muhando wana uakilishi wa namna hiyo. Kwa hiyo basi hata ukubwa au udogo
wa wahusika wa fasihi simulizi huweza kutumiwa katika kukosoa na kusahihisha
mienendo ya baadhi ya wanajamii.
Hata hivyo haimaanishi kuwa wahusika wa aina hiyo hapo juu ndio tu walioko
katika fasihi simulizi; kwani wako wahusika watu pia ambao hutumiwa
kuwakilisha pande kuu mbili zinazovutana daima katika ulimwengu wa fasihi
simulizi: upande wa wema au haki, na ule wa ubaya na dhuluma; ambapo wale
wa upande wa wema na haki mara kwa mara huwashinda wahusika wabaya
wenye dhuluma.
Kwa upande mwingine kunayo matumizi ya wahusika wasio miili, madubwana
wa ajabu-ajabu, mashetani, na pia majini. Hawa hutumiwa kwa makusudi
mbalimbali. Mara nyingi wanasaidia sana kujenga taharuki katika habari
inayoelezwa. Tunapokutana na joka lenye vichwa sabini, halafu atokee kijana
mdogo ajitape kuwa yeye ataliua, tunafuatilia kwa makini na mioyo ikitudunda,
matendo ya mhusika huyu kuliko tungeelezwa tu kuwa kulikuwa na joka kubwa.
Wahusika wa aina hii pia hutumiwa kuwajenga wahusika watu. Tunapomwona
mhusika mtu akishuka hadi katika ulimwengu wa majini na kuongea na kupata
ushauri wa Mfalme wa Majini, sisi hadhira humwona mhusika huyu, hasa kama ni
kiongozi, kuwa bora na imara kuliko wengine. Ijapokuwa wahusika wa namna hii
wanatumiwa katika fasihi simulizi, kuwapo kwao hakupunguzi kuaminika kwa
yale yanayoelezwa. Kinyume chake, yale yaelezwayo yanaaminika na kuisisimua
hadhira zaidi ya vile ambavyo yangekuwa iwapo yangeelezwa kwa kutumia
wahusika watu tu.
Tuchunguzapo matumizi ya wahusika katika fasihi simulizi tutaona wazi kuwa
hawa hutegemea maeneo ya kijiografia. Kwa mfano, mhusika Kanga mara nyingi
atapatikana katika fasihi simulizi itokanayo na jamii zenye kulima mtama, wakati
ambapo Nyani na Tumbili mara nyingi watatoka katika jamii za kilimo cha
mahindi. Wahusika katika fasihi simulizi hutumiwa wakati mwingine kiishara.
Simba, kwa mfano, huwakilisha ufalme na utawala; Jogoo ni mkuu wa familia,
naye huashiria siku njema anapowika; Fisi huwakilisha matumizi ya nguvu,
uchoyo na ulafi; Kondoo ni kiwakilisho cha upole na hata wakati mwingine
upumbavu; Sungura mara nyingi huashiria ujanja, wakati ambapo Mzee Kobe ni
kisima cha busara na hekima; Tausi anasimamia uzuri na maringo; Bundi mara
nyingi ni ishara mbaya ya balaa na hata kifo; na Nzige huonyesha njaa, na hata
uroho na ulafi.
Katika sehemu ifuatayo tutakitumia kipengele hiki cha wahusika wa kifasihi
simulizi kuona ni kwa namna gani kimeathiri majaribio ya fasihi andishi ya
Kiswahili.
33
3.9.1 Wahusika wa kifasihi simulizi katika fasihi andishi ya Kiswahili
Pamoja na wahusika hao wa kifasihi simulizi waliotumika katika Jogoo Kijijini
na Ngao ya Jadi na Lina Ubani, wako pia wahusika wa kifasihi simulizi katika
kazi nyinginezo za fasihi andishi ya Kiswahili. Mathalani, katika riwaya fupi ya
Shaaban Robert ya Adili na Nduguze, Adili anachanganyikana na hata
kuwasiliana na majini, na nduguze Adili wanageuzwa kuwa manyani. Unyama wa
nduguze Adili wa kumtupa ndugu yao baharini ili tu wamrithi mpenzi wake na
wairithi mali yake ni kielelezo tu cha unyama wa ubepari ambao ulikuwa
umeshashamiri hata enzi za Shaaban Robert. Ni pale tu wanapobadilika na
kujivua uhayawani ndipo wanapogeuzwa kuwa watu.
Mara kwa mara wahusika katika fasihi simulizi wanawakilisha pande kuu mbili:
upande wa wema/haki na upande wa ubaya/uonevu.. Labda ni katika misingi hii
ndimo ambamo hata baadhi ya waandishi wa fasihi ya Kiswahili wameathiriwa
katika uundaji wao wa wahusika. Sifa na majina ya wahusika wao hubaki kuwa
ileile tangu mwanzo hadi mwisho. Mfano mzuri wa waandishi wa namna hii ni
ule wa E. Kezilahabi katika riwaya yake ya Rosa Mistika ambamo majina ya
wahusika wake yanawakilisha tabia zao zisizobadilika tangu mwanzo hadi
mwisho wa riwaya. Tukitumia mifano ya Rosa Mistika, Flora, Regina na
Emmanuel tunaweza kulithibitisha hili.
Rosa Mistika, pamoja na kuwa ni jina jingine la Bikira Maria, lakini linamaanisha
ua waridi lenye fumbo. Kwa hiyo jina la mhusika huyu ni lile la ua moja tu.
Flora maana yake ya asili ni mimea, kwa hiyo jina la mhusika huyu si la ua wala
mmea mmoja tu bali linajumuisha mimea yote. Huenda mwandishi alitutaka
tumwone Rosa kuwa yu dhaifu sana kama ua moja tu alinganishwapo na Flora
ambaye anawakilisha mimea yote. Haya yanadhihirika hata katika maelezo
tunayopewa, kuhusu wahusika hawa mwanzoni mwa riwaya hii (uk. 4):
Rosa alikuwa msichana mzuri, mrefu kiasi, mnyenyekevu na mnyamavu. Kama
akienda kuogakisimani utamwona kabla ya kuvua nguo anaanza kuangalia huku
na huko, huvua, huoga upesiupesi, huvaa, huchukua maji na kurudi nyumbani.
Alikuwa hapendi kuangaliwa kwa muda mrefu. Ukimwangalia machoni
huinamisha kichwa.
Flora akienda kuoga hujiangaliaangalia kwa muda mrefu kabla ya kuoga.
Hutazama matiti yake ambayo sasa yalikuwa yanaanza kuwa makubwa;
hujipapasapapasa kwa mikono kutoka mgongoni mpaka pale matako
yanapotelemkia; halafu tena hujiangaliaangalia. Hata kama amemaliza kuoga,
hungoja mpaka jua limkaushe ndipo avae. Akienda saa nane kisimani atarudi saa
kumi na moja na jiwe lake mkononi, ingawa kisima kilikuwa maili moja tu
kutoka nyumbani. Kila mara alitukanwa na mama yake kwamba alikuwa mvivu.
Regina akisema kwenda kulima, yeye hubeba mtoto ubavuni. Akiambiwa
kuweka moto jikoni, yeye huchukua majiani kutoka paa la jiko.
Maelezo haya ni ya makusudi kabisa yanayotutaka tuwaone wasichana hawa
wawili kuwa ni tofauti. Mmoja ni dhaifu, na mwingine ni imara zaidi. Huenda
ndiyo maana hadi mwishoni mwa riwaya hii, Flora anastahimili misukosuko ya
34
maisha na anabaki kuwalea wadogo zake baada ya vifo vya wazazi na dada yao,
wakati ambapo Rosa anashindwa kustahimili vishindo hivyo vya maisha na
anajiua. Na hili linatufanya mwishoni mwa riwaya hii tukubaliane kwa kiasi
kikubwa na Zakaria ambaye anakana kabisa na kusema kuwa si yeye
aliyesababisha kujiua kwa Rosa anaposema, “Ee Mungu wangu. Haya yote
yametokea kwa sababu ya ubaya na udhaifu wake (Rosa) mwenyewe.” (uk. 98,
msisitizo ni wangu). Hadhira inatakiwa iyapime yote haya sambamba na hulka ya
Rosa, na inatakiwa imlinganishe Rosa na dadake mdogo, Flora, wote wamekulia
na kupitia maisha karibu sawa – tangu ya malezi makali ya baba yao hadi ya
shuleni, mbali na nyumbani na mbali na malezi makali ya mzee wao, ambako
kuna kukutana na wavulana. Hasta hivyo, maisha hayo yanamshinda Rosa wakati
ambapo Flora anayashinda. Mimea huweza kustahimili vishindo vya vurugu za
hali ya hewa kuliko ua moja ambalo linanyauka na kudondoka kiurahisi.
Katika dini ya Kikristo, Emmanuel ni jina lingine la Yesu Kristo, nalo lina maana
ya “Mungu yu pamoja nasi”. Kuzaliwa kwa Emmanuel kunaleta uhusiano mzuri
kidogo pamoja na amani katika familia ya Zakaria na Regina kwani huyu ni mtoto
wa kiume ambaye Zakaria amekuwa akimlilia siku zote akimlaumu Regina kwa
kumzalia wanawake tu kama iwelezwavyo ukurasa wa 23:
Wale vijana walikimbia bila kuangalia nyuma. Walifikiri bado anawafuata.
Zakaria aliwasikia kwa mbali wakimtukana.
Mshenzi, utaoza na binti zako!”
Zakaria hakuwajibu lolote. Regina na Rosa walikuwa wamenyamaza tu.
“Mshenzi, unanizalia wasichana tu! Unaniletea taabu nyumbani bure tu!”
Zakaria alifoka.
Regina hakujibu; aliogopa kumdhihaki...
Kinyume na hali hiyo ya kukosekana kwa amani na furaha katika mji wa Zakaria,
tukio la kuzaliwa kwa Emmanuel linaelezwa ifuatavyo:
Zakaria alirudi usiku nyumbani siku hiyo. Alikuwa amekwishapata habari
hizo njema njiani. Alimbeba mtoto. Alimpa pongezi mke wake.
“Regina! Sasa mji huu umekuwa wako.”...
Usiku huo Zakaria aliimba aleluya karibu usiku kucha. Kesho yake
alikwenda posta. Mke wake alishangaa kumwona jioni anarudi na vitu
vyote alivyokuwa ametaja. Alianza kupata sauti. Alianza kuzungumza
kwa furaha. Hata watu wa kijijini waliona ajabu... (kur. 24 – 25)
35
Emmanuel, basi, kama jina lake linavyomaanisha, analeta furaha kwa muda
katika nyumba ya Zakaria na Regina.
Katika riwaya hii, Regina ni mhusika ambaye amependelewa kuliko wahusika
wengine wote. Maana ya jina Regina ni malkia, na kwa hakika, ukiondoa
umasikini wa vitu alio nao regina, mhusika huyu amepewa sifa za
umalikiaumalkia. Tangu mwanzo hadi mwisho tunamwona mhusika huyu kuwa
ni mama mwadilifu ambaye anawalea watoto wake kwa mapenzi makubwa sana.
Ana huruma nyingi na pia hata anapoonewa na Zakaria ambaye kwa kiasi
kikubwa ni mhusika hasi, mlevi, mwizi, na mgomvi; hatumwoni akilalamika sana.
Zakaria anapoiba pesa za ada ya Rosa, Regina anajishughulisha kutafuta pesa
zingine. Pamoja na matatizo mengi aliyopewa na Zakaria maishani mwake, bado
tunamwona Regina akianguka na kufa mara tu anapomwona mumewe amekufa.
Ndiyo maana hata katika makaburi matatu ya Rosa, Regina na Zakaria, ni juu ya
kaburi la katikati la Regina ndiko ambako kumeota mchungwa wenye matunda
mazuri sana kuliko michungwa ya makaburi ya Rosa na Zakaria. Mwandishi hapa
ametumia ukatikati kama ishara itokanayo na dini ya Kikristo ambamo Yesu
Kristo alisulubiwa katika msalaba ulio katikati ya ile ya wenye dhambi wawili.
Ndiyo maana twaambiwa:
Hata baada ya miaka kumi, matunda yalipokuwa yakiiva, watoto hawa
walizoea kutoka Mwanza kuja kuchuma matunda kutoka ule mti wa
katikati. Walikula damu na mwili wa mama yao. Walimkumbuka mama
yao. (uk. 97; msisitizo ni wangu)
Sawa na Wakristo wanavyoamini kuwa Chakula cha Bwana au Sakramentiu
Takatifu inayotolewa kwa mvinyo na mkate ni kiwakilisho cha mwili na damu ya
Yesu, watoto hawa wanapokula machungwa mazuri yatokayo juu ya kaburi la
mama yao huwa wanakula damu na mwili wa Regina. Kwa maana nyingine ni
kwamba Regina anaendelea kuishi hata baada ya kufa.
Wahusika Rosa, Flora, Emmanuel na Regina tumewaita kuwa ni wahusika wa
kifasihi simulizi kutokana na ukweli kuwa majina yao yanawakilisha matendo na
nafasi zao katika hadithi hii; na kwa hakika, wahusika hawa wanabaki na sifa zao
zilezile tangu mwanzo hadi mwisho wa riwaya. Inaonyesha kuwa Kezilahabi
alipoandika riwaya ya Rosa Mistika alinuia kwa makusudi kabisa kufanya
majaribio ya kutumia uhusika wa kifasihi simulizi si katika maana ya majina ya
wahusika wake tu, bali pia hata katika matendo na hulka zao ambazo zinabaki
kuwa zilezile tangu mwanzo hadi mwisho kwani wabaya wanabaki kuwa wabaya
na wema wanabaki kuwa wema.
36
3.10 Neno kuhusu fasihi ya majaribio
Itaonekana dhahiri kuwa katika makala hii istilahi ya fasihi ya majaribio
imetumika bila kupewa maelezo kamili. Hili linatokana na ukweli kuwa si rahisi
kueleza fasihi ya majaribio ni nini hasa. Inawezekana kabisa kuuliza, je kwa vile
hakuna kazi moja ya fasihi inayofanana kabisa na kazi nyingine, si kila kazi mpya
ya fasihi ina majaribio fulani?
Tunadhani kuwa ili kazi fulani iitwe kuwa ni fasihi ya majaribio haina budi
kuambatana na upya ambao unaweza kuelezeka kinadharia, na hata ikiwezekana
nadharia hiyo iwe imeelezwa na mwandishi mwenyewe au na wahakiki wa wakati
huo. Wakati ambapo E.Hussein na P. Muhando walianzisha mjadala kuhusu
maana hasa ya tamthilia ya Kiswahili, wakaandikia suala hili tasnifu na makala
mbalimbali ambazo zilihusu sanaa za maonyesho na fasihi simulizi ya Kiafrika,
Kezilahabi alifanya majaribio na falsafa ya Udhanaishi, akionyesha kuwa maisha
hayana maana kwani mtu anazaliwa ili afe. Kwa Kezilahabi, maisha ni fumbo
sawa na Rosa alivyo ua waridi lenye fumbo. Nadharia hizi ndizo ambazo
ziliwaongoza waandishi hawa hadi wakafanya majaribio ya kuzitumia kusana
kazi zao.
Hii ina maana kwamba pamoja na majaribio madogomadogo ambayo yanajitikeza
katika kila kazi mpya ya fasihi, ni yale tu ambayo yameambatanishwa na nadharia
fulani na mijadala fulani ya kifasihi ndiyo tunayoweza kuyapa sifa za kuwa
matapo fulani ya kimajaribio. Katika fasihi ya Kiswahili tunaweza kuyataja
majaribio ya washairi huria, Kezilahabi, E. Hussein, M.M. Mulokozi, K.K.
Kahigi, na wengineo wa aina hiyo, kuwa yaliunda tapo la majaribio katika ushairi
wa Kiswahili. Hawa walikinzana na washairi wa kimapokeo waliosisitiza kuwa
vina na mizani ni uti wa ushairi wa Kiswahili, wakatunga mashairi yasiyofuata
arudhi na kanuni za urari wa vina na mizani. Haya yalikuwa ni majaribio
yaliyoambatana na mjadala na malumbano makali.
Nionavyo mimi, majaribio hukoma kuitwa hivyo yanapotoa mazao ya kazi za
kifasihi ambazo zinakubalika na hazionekani kuwa na upya tena. Leo hii tamthilia
zinazotumia vipengele vya kifasihi simulizi na vya sanaa za maonyesho za
Kiafrika si kazi za kifasihi zinazoonyesha upya wowote kwani zimezoeleka na
kukubalika. Vivyo hivyo, mashairi yasiyofuata urari wa vina wala mizani
hayaonekani mapya wala mageni kwani yameshazoeleka na yanasomwa shuleni
na vyuoni. Kazi za namna hii basi, zimekoma kuwa za kimajaribio.
Upya wa nadharia pamoja na wa kazi za kifasihi zinazotokana na nadharia hizo
ndio huunda majaribio. Huenda upya wa istilahi ya Uhalisiamazingaombwe
ambayo leo hii inatumika kuzieleza zile kazi za kifasihi zinazounganisha uhalisi
na uajabuajabu, unaunda kazi mpya za majaribio katika fasihi ya Kiswahili.
Mathalani, upya huu unaonekana katika riwaya fupi za Kezilahabi za Nagona na
Mzingile, na pia katika kazi mbalimbali za Said Ahmed Mohamed (Khamis) kama
vile riwaya yake ya Babu Alipofufuka na hadithi fupi ya “Sadiki Ukipenda”,
ijapokuwa “upya” huu unaelekea kuwa wa kiistilahi zaidi ya kimtindo kwani,
37
kama makala hii inavyoonyesha, vipengele vya maajabuajabu ndani ya fasihi
ndivyo ambavyoi vimekuwa vikijenga msingi wa fasihi simulizi, hasa ndani ya
ngano, visasili, visajanja, visapanda, vitendawili na tanzu zinginezo za fasihi hii
ambazo zimekuwapo kwa karne nyingi. Kwa hakika, vipengele hivi pia
vilishajaribiwa na kutumiwa na waandishi kama vile Shaaban Robert katika kazi
zake za Kusadikika, Kufikirika na Adili na Nduguze kiasi kwamba inakuwa
vigumu kuona upya wa majaribio ya Kezilahabi, Mohamed na waandishi wengine
wa kisasa wanaotumia mtindo wa Uhalisiamazingaombwe; mtindo ambao ni
kama pombe ya zamani katika kibuyu kipya. Kama vile Mazrui na Mazrui (1995)
wanavyodokeza kuwa mabadiliko ya lugha ni ushahidi wa mabadiliko mapana
zaidi katika mfumo wa utamaduni unaohusika, inawezekana basi, kuwa hata
mabadiliko ya fasihi nayo ni kielelelezo cha mabadiliko mapana zaidi ya
kitamaduni katika jamii husika. Swali la ni mabadiliko gani yanayozaa fasihi ya
Kiswahili ya majaribio mahsusi katika wakati mahsusi na si wakati mwingineo, ni
swali linalohitaji utafiti zaidi ili kujibiwa kwa usahihi zaidi.
Marejeo/Kazi zilizopitiwa
Hussein, E. 1976, Jogoo Kijijini na Ngao za Jadi, nairobi: Oxford University
Press.
Kezilahabi, E. 1975, Rosa Mistika. Dar es Salaam : Dar es Salaam University
Press.
Kezilahabi, E. 1990, Nagona, Dar es Salaam: Dar-es-Salaam University Press.
Kezilahabi, E. Mzingile, 1992, Dar es Salaam : Dar es Salaam University Press.
Mazrui, A. na Mazrui, A. (1995), Swahili, State and Society. Nairobi. East
African Educational Publishers.
Mohamed, S. A. 2001, Babu Alipofufuka, Nairobi : The Jomo Kenyatta
Foundation.
Mohamed, Said Ahmed, Sadiki Ukipenda na Hadithi Nyingine, Nairobi : The
Jomo Kenyatta Foundation, 2002.
Muhando, P. Lina Ubani, 1982, Dar es Salaam : Dar es Salaam University Press.
Robert, Shaaban (1972) Adili na Nduguze, Nairobi : Nelson.