RIWAYA YA KICHWAMAJI
RIWAYA YA KICHWAMAJI
MUKHTASARI
NA UCHAMBUZI WA FASIHI: RIWAYA YA KICHWAMAJI.
UTANGULIZI:
Kichwamaji ni riwaya ya
kisasa, ambayo imejikita zaidi katika nadharia ya “utamaushi (udhanaishi)” katika
kuangalia maisha ya sasa.Ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya waafrika wa dunia
ya leo, zaidi ikizungumzia na kuweka bayana mambo au mataitizo ambayo waafrika
wa sasa wanakumbana nayo; zaidi ni waafrika wa mashariki mwa bara. Riwaya hii,
kwa kina imeweka wazi maudhui yake, ikijikita sana katika kuchora mandhari ya
Afrika ya Mashariki-Tanzania katika wilaya ya Ukerewe. Kutokana na nadharia iliyofuatwa kuandika riwaya hii,
zaidi matatizo ndio yanaonekana kikwazo hasa kwenye mafanikio ya mwanadamu hadi
msanii kufikia hatua ya kuona kwamba maisha hayana umuhimu wowote. Vilevile na
kumchukulia Mungu kuwa hayupo. Mwandishi anatanabaisha kuwa binadamu
mwisho wake, ni kifo. Dunia anamoishi
binadamu imejaa matatizo, vikwazo vya kila aina: kwamba maisha ni vurugu,
maangaiko na misukosuko n.k. Wahusika wa riwaya hii, wamechorwa kuwa ni watu
wanaoangaika kutafuta maana ya maisha, kupata fasili ya maisha ni nini? Hivyo tunaona namna ambavyo
wahusika wakuu katika simulizi ya riwaya hii; wanapitia katika shida na
maangaiko mengi. Hawafurahii uwepo wao wa maisha.
Vilevile
msuko wa visa na matukio katika riwaya hii, ni wa kuonesha jinsi gani mwanadamu
katika kuishi anapata taabu sana. Pengine hata mafanikio wanayopata hawayafurahii
kwa muda mrefu: ni furaha ya muda mfupi. Mazingira na muktadha wa riwaya hii,
yamejengwa kwa hali ya chini: hasa zaidi katika hali ya umasikini, ambapo mara
nyingi huwa ni maisha ya kuangaika na kutoa jasho nyingi ili kuweza kupata
mafanikio.
MAUDHUI
YALIYOLENGWA KATIKA RIWAYA HII:
Katika
riwaya hii mwandishi ameweka hadharani maudhui yake: kwa kuonesha wazi matatizo/vikwazo/misukosuko
inayomkatisha tamaa mwanadamu katika maisha yake. Miongoni mwa matatizo
aliyoyabainisha mwandishi, ni kama: kifo,
njaa, ugomvi, dharau, kulipiza visasi, umasikini, uwepo kwa matabaka ya walio nacho na wasionacho, kukatika
kwa furaha ya mtu ghafla, dhuluma na wivu,kunyanyasika kwa masikini kunako
sababishwa na matajiri pia viongozi kuwadharau na kuwakomoa raia wa kawaida
wasio na ofisi za kuajiriwa na serikali. Haya yote ni baadhi ya vikwazo
anavyokumbana navyo binadamu anayetafuta furaha ya maisha na mwishowe anaishia
kuvikosa kabisa; ama kuvipata lakini kwa muda. Mtazamo na mwono huu unamfanya
mwandishi wa riwaya hii, aone kwamba mwanadamu ameumbiwa matatizo tu, katika
maisha yake na kupata raha yeye kwake ni nadra sana. Hivyo kwake yeye anatazama
maisha kama mtihani na adhabu kubwa aliyopewa binadamu: kwani hawezi kuwa na
unafuu juu ya maisha.
Mtazamo
huu pia unampa picha msanii wa riwaya hii kuwa na maswali mengi juu ya uwepo wa
Mungu. Na kusema kuwa Mungu hayupo na kama yupo kwanini watu wanateseka namna
hii?, au kwa nini Mungu anakuwa na ukatili namna hii?, kama tunavyosoma na
kouna (uk.51) msanii anasema; …niliposema
hivyo tu wazee hawakuwa na shuku ya kuniuliza tena maswali. Hawakuona tofauti
kubwa kati yangu na wao. Mambo yaliharibika nilpoanza kuwaambia kwamba huenda
hakuna Mungu….vilevile katika (uk.124) mwandishi anashikilia mawazo yake ya
kuwa hakuna Mungu: mstari wa pili wa ukurasa na kuendelea, msanii anasema;
“Unafikiri nini juu ya watu wasioamini kuwa
Mungu yupo?”
“Ni wajinga,” Manase alisema mara
moja.
“Hivi wewe unafikiri mtu asiyeamini
Mungu ni mtu gani?” nilimwuliza.
“Ni mtu ambaye anataka kumfahamu
Mungu kwa kutumia kichwa chake. Mungu hawezi kueleweka kwa akili.”
“Hapo ndipo sikubaliani nawe. Mtu
asiyeamini Mungu ni mtu asiyeamua kuwako kwa Mungu kwa kutumia milango ya
fahamu peke yake. Licha ya milango ya fahamu mtu asiyeamini Mungu anatumia
akili zake.”
“Unaona, Manase; mwanadamu ameamua
kwamba kuna Mungu kwa sababu ya hali yake ya woga iletwayo na milago ya fahamu.
Kwahiyo mtu anayeamini kwamba Mungu yupo ni yule aamuaye kwa kufuata milango ya
fahamu yake. Kwake fahamu zinatawala bongo.”
Pia
mwandishi anazidi kukata tamaa zaidi na kufuata msimamo wa kuwa na mtazamo hasi
juu ya uwezo na uwepo wa Mungu: hasa pale anapomchora mhusika Kazimoto baada ya
kufiwa na mtoto wake mchanga, aliyekuwa akimtegemea sana na mke wake lakini mtoto
huyo alikufa muda mfupi baada ya kuzaliwa. Haya ni maneno ya Kazimoto: “…usiku nikiwa na mke wangu, mawazo mengi
yalinijia kichwani. Nilianza tena kufikiri juu ya Mungu.Kama kweli Mungu
alikuwepo sikuona kwanini aliweza
kufanya ukatili mkubwa kama huo. Matumaini yetu yote; kazi na taabu
tuliyopata-yote hayo chini! Sikuona maana ya maisha….” (uk.180).
Mtazamo huu wa mwanafasihi
E.Kezilahabi, umezidi kuteka mawazo yake katika riwaya hii. Ni wazi kuwa kwake
yeye haoni umuhimu wa maisha, pia amani ya mwandamu hapa duniani ni ndogo. Maswali
mengi yameteka riwaya hii: kama, maisha ni nini? Au maisha yana maana gani? Mwanadamu
ni kiumbe wa maisha gani na umuhumu wa kuishi uko wapi/ni upi kwake? Ni kwa
nini furaha haidumu katika maisha ya binadamu? Mwisho wa maisha ya mwanadamu ni
upi au ni nini? Kifo ni nini na kwa nini
watu wanakufa? Ni kwa vipi maisha yawe mafupi lakini yenye vikwazo mbalimbali? Mkondo
wa riwaya ya “Kichwamaji”,ni wa kidhanaishi,
kwa sababu mwandishi amejikita zaidi kuonesha maisha ya binadamu yalivyoumbwa
kwenye bahari yenye kila machafuko ya mawimbi mazito; hadi mwishowe, tunaona
mhusika mkuu Kazimoto akikata tamaa ya kuishi hadi hatua ya kujiua kwa kujilipua
kwa bunduki(bastola).
Ni dhahiri kuwa, maswali haya
yanamfanya mwandishi, ashindwe kupata mwafaka wa maisha yake. Pia majibu ya
maswali haya yanakosekana; pengine yakionekana ni majibu yenye mafupi yasiyoweza
kupata ufumbuzi wa maswali haya kwa kina. Katika kuendelea kuichambua kwa kina
riwaya hii, tutaona kwamba mbali ya kuwa riwaya hii imejengwa katika nadharia
ya udhanaishi, inatoa na kubainisha wazi matatizo yanayoikumba jamii ya sasa ya
mtanzania. Tutaingia kuitazama na kuielewa kwa undani zaidi riwaya hii kwa
kuzama katika kila sura ya kitabu hiki.
SURA YA 1
Katika
sura hii msanii anaanza kwa kutuonyesha bughudha, maangaiko, taabu na karaha anazo
kumbanazo mtu katika kutafuta huduma kwenye jamii anamoishi. Msanii
anadhihirisha mambo haya, kwa kutumia kalamu yake akimwaga wino( uk.1)…watu tulikuwa tukingoja kuingia ndani ya
ofisi ya Mkuu wa Wilaya tulikuwa wengi. Wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume.
Wote kama wagonjwa wangojeao kumwona daktari,…anaendelea kusema katika
mstari unaofuata …mmoja alipokuwa
akiingia ndani tuilkuwa tukisukumana kwa matako ili kuziba nafasi…Lakini
msichana aliyekuwa amekaa karibu nami mkono wa kushoto haukuonekana kuwa na
raha: alikuwa amekaa karibu na mzee na wakati wote msichana huyu alikuwa
ameweka kitambaa juu ya pua yake…
Maneno
haya yana uzito mkubwa kwa kuyatafakari katika mkondo wa riwaya hii, ama
tunaona watu wengi ambavyo wanaangaika kupanga mistari ili kuweza kuhudumiwa
katika taasisi. Ni utaratibu ambao unawafanya watu wengi waumie kwa kuchelewa
na kuharibu ratiba nyingine. Inaonekana dada katika ule mstari hana raha na
ameweka mkono wake puani. Na tunaambiwa chanzo ni kukaa karibu na mzee mmoja.
Vile vile msanii anaonesha kuwa maisha hayana maana, tunaposimuliwa kuwa:
msichana ambaye mhusika mkuu yaani kazimoto, anamwona mzuri na mwenye umbo zuri,
mwenye kuvutia: ila anatolewa kasoro na wasichana waliokuwa wamekaa karibu naye
(uk.1-2)
“Mwishowe yule aliyekuwa ametukawiza
alitoka nje hali akitabasamu. Alikuwa msichana maji ya kunde, mrefu na mwenye
uso wa mviringo. Ilikuwa alipoanza kutembea nilipotambua kwamba kiuno alichokuwa
nacho kiliweza kuvutia macho ya watu na kuleta ugomvi. Alisita kutabasamu mara
tu alipoona kwamba macho yote yalikuwa yakimtazama, na aliposikia watu wakiguna
alitembea mara moja kuelekea mlangoni ili atoke upesi. Nilisikia wasichana
waliokuwa wamekaa karibu nami wakimtoa makosa:
“Ee, dada! Poda kuzidisha!”
“Viatu vitembeze vizuri!”
“Hata mkoba wenyewe hajui kuushika!
Anaupakata kama mtoto!”
“Hata kitambaa hawezi kukifunga!”
Katika
maisha kuna kutafuta na kukaosa. Hili ni jambo ambalo huwakumba watu wengi
ambao hutafuta riziki kwa ajili ya kujipatia kipato. Hivyo ndivyo ilivyokuwa
kwa kijana Kazimoto: msomi ambaye aliamua kujishughulisha na kufanya kazi
mbalimbali ili ajipatie chochote muda wa likizo. Alienda kuomba kazi kwa mkuu
wa wilaya, ambaye walikuwa wakisoma pamoja shule ya msingi.Lakini alikosa fursa
hiyo baada ya kutoelewana na mkuu wa wilaya kwa sababu za ujana wao zilizohusu
wivu wa wasichana. Jambo ambalo lilimfanya Kazimoto kuona uchungu wa maisha;
vilevile kutaka kulipiza kisasi alichofanyiwa na rafiki yake huyo wa zamani
wakati wanasoma shule ya msingi. Mkuu huyo wa wilaya aliyeitwa Manase aliharibu
ndoto za kusoma za Rukia ambaye ni dada yake Kazimoto. Kutokana na uchungu wa
kuona dada yake anaacha shule kwa sababu ya Manase: na yeye ana kazi nzuri
alafu amemnyima kazi ya muda Kazimoto, ndipo Kazimoto anakata shauri ya kulipiza
kisasi kwa Manase.
SURA YA 2
Katika
sura hii tunaona mkondo wa udhanaishi unaendelea. Katika masimulizi; Kazimoto
bado ana hasira ya kuendelea kulipiza kisasi kwa Manase kutokana na kumharibia
masomo dada yake. Ni sura ambayo msimulizi anazidi kutusasambulia kisa kizima
ambacho kinamfanya Kazimoto afikirie sana juu ya maisha ya dada yake
yalivyoharibiwa na rafiki yake wa karibu Manase. Rukia alishindwa kuendelea na
darasa la tisa: lakini Kazimoto alikuwa na shauku ya kuendelea kumsomesha ili
apate elimu bora.(uk.18)…Rukia alishindwa
kuingia darasa la tisa, lakini mimi nilikuwa na nia ya kumwelimisha…
Kazimoto
alifanya juu chini na kumtafutia mdogo wake shule, alifanikiwa kuipata Dar es
Salaam. Kama asemavyo msimulizi katika (uk.18) …nilimtafutia shule na baada ya kuipata kichini chini kama ilivyo
kuwa kawaida, nilipata shule moja huko Dar es Salaam… Aliamua ampeleke Dar
es Salaam mdogo wake ili akaendelee na masomo ila shule haikuwa na mabweni: Manase
alikata shauri ya kuomba Manase akae na Rukia kwani Kazimoto alikuwa bado
anasoma chuo kikuu Dar es Salaam na hakuwa na ndugu ye yote huko wa kukaa na
dada yake Rukia. Aliona rafiki yake Manase ndiye ambaye angeweza kukaa na Rukia
kipindi anaposoma.
“Tabu sasa ikawa ni mahali pa kupanga: shule
yenyewe haikuwa na malazi kwa wanafunzi. Manase wakati huo alikuwa akiishi
Oystebay, na kwa kuwa alikuwa na nyumba kubwa nilifikiri ataweza kuishi na
ndugu yangu. Licha ya nyumba kuwa kubwa wakati huo uliuwa ni wakati ambao
uhusiano kati yangu naye uilikwa mzuri.Nilipomwambia Manase taabu yangu
alikubali kukaa na ndugu yangu. Wakati huo mimi nilikuwa nimekwisha ingia chuo
kikuu.”
Baada
ya Manase kuamua kukaa na Rukia, mambo yalienda kinyume na matarajio. Ndipo
msanii anatanabaisha jinsi ambavyo Manase alimgeuka na kumuharibia masomo Rukia
kwa kufanya naye mapenzi ya lazima alipokataa wakati akijua kuwa ni ndugu yake
wa jirani na pia ni mwanafunzi. Rukia alipata mimba na kufukuzwa shule na
baadaye kufukuzwa na Manase nyumbani kwake. Rukia alirudi kijijini akiwa
mjamzito aliyeenda kusoma na kurudi nyumbani akiwa amechuma tunda la mimba. Kazimoto
anasema kuwa baada ya Manase kuanza ukatili huo Rukia alimwandikia barua za
kumjulisha juu ya hali ile: ili ikiwezekana ahame kwa Manase lakini kutokana na
uwezo mdogo wa kiuchumi, Kazimoto alimsihii aendelee kuvumilia: lakini hali
ilikuwa ndivyo sivyo kwa dada yake hadi kumwandikia barua kuwa: “Kaka usiponitafutia mahali pengine pa kukaa
mimi nitarudi nyumbani. Heri kuacha shule!” Hali hii iliendelea kumkumba
Rukia hadi alipotimuliwa na Manase kwa matusi juu yake akimwita Malaya. Msimulizi
anatuonesha kwa maneno ya Kazimoto kuwa baada ya muda mfupi kumsihi dada yake
aendelee kuvumilia: alipokea barua kutoka kwa Rukia ikisema kama ifuatavyo:
Barua
yenyewe: (uk.19)
Kaka mpendwa,
Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo nimechukua kalamu ili
nikueleze mambo yote. Nimeona kwamba siwezi kuwa nakuficha wewe mambo, hali
mambo yenyewe hayawezi kufichika. Wewe ukiwa kaka yangu na ndiye uliyenitafutia
nafasi hii ya shule ninakupa heshima. Fahamu kwamba mambo haya sijapata
kumweleza mtu mwingine isipokuwa wewe peke yako.
Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa
raha kwa muda wa juma moja tu. Baada ya juma hilo, niliona Manase anaanza
kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya majuma mawili mambo yalizidi kuwa mabaya,
kwani nilipokuwa naoga niliona jicho lake kwenye tudu la ufunguo.
Mwishowe aliniambia wazi alichokuwa
anataka. Nilimwambia: Manase! Kaka yangu akifahamu litakuwa jambo la aibu sana!
Lakini yeye alijibu kwamba wewe ni mwanaume kama yeye. Alifikia hata hatua ya
kutumia nguvu! Na kweli alitumia nguvu bila utashi wangu.
Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa
kujifunza kwa kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu yameharibika. Shule
nimekwisha acha. Jambo ambalo limenisikitisha sana ni hili lifuatalo: Jana
usiku Manase alirejea nyumbani mlevi. Alikuwa na tikiti ya basi. Baada ya
kunitukana kwa maneno ambayo siwezi kukuandikia, alianza kupanga vitu vyangu
sandukuni. Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka, machozi
yanilengalenga, sijui nitasema nini kwa baba na mama. Usifike kuja kuniaga
kwenye kituo cha basi nisije nikazimia.
Sina mengi.
Nduguyo,
Rukia Mafuru.
Barua hii inadhihirisha udhanaishi kwa msanii
wa riwaya hii. Kwani katika barua anatuonesha namna mtu ambavyo anahangaika
kujikomboa katika hali ngumu ya maisha: lakini mambo yanaenda kinyume na
kugonga mwamba na shida kuzirudia. Katika sura hii mwandishi anaenda mbali
zaidi, akisimulia namna ambavyo Kazimoto anapoenda likizo anafika njiani na
kukutana na watu wakimuuliza, na wengine kumshangaa kurudi kwao kutokana na
shida pamoja na mambo ya ajabu yaliyo kuwa yakitokea kwao Kazimoto. Kijiji
kizima kilikuwa kikifahamu mambo hayo na ndio maana kila mtu aliyekutana na
Kazimoto njiani alimshutuka na kumshangaa. Mfano, Kazimoto anasema: …mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa
kijana mmoja tuliyekuwa tukisoma pamoja zamani. Yeye sasa alikuwa ameoa na
alikuwa na watoto watatu.
“Wewe kwa nini umekuja nyumbani?”
aliniuliza kwa mshangao bila hata kunisalimu kwanza.
“Kwa nini? Mbona huwa nakuja nyumbani
karibu kila likizo?”
“Heri ungebaki huko. Huku umejileta
hatarini.”
“ Hatari gani?”
“ Hatari gani? Hujui?”
“Hata sina habari!”
“Ndugu yangu,utasimuliwa nyumbani.”
Mtu wa pili kukutana naye alikuwa
mzee. Mzee huyu alikuwa akipeleka ng’ombe wake mtoni kunywa maji. Alikuwa
ameenea vumbi nyweleni.
“Kazimoto! Umekuja kujionea
mwenyewe!” alisema.
“Kuona nini?”
“Ha! Huna haraka?”
“Hata sina!”
“Mambo Fulani yametokea pale
nyumbani kwenu ambayo yameshangaza kijiji cha Mahande.”
Kazimoto
aliendelea kuelekea nyumbani kwa wasiwasi, huku kila mtu aliyekuwa anakutana
naye njiani alizidi kumtia wasiwasi na kumuuliza juu ya matatizo ya nyumbani
kwao. Katika (uk.23), tunaona Kazimoto anakutana na Mzee Kabenga: na kumuuliza
habari za nyumbani kwao, ambapo mzee Kabenga anashindwa kumsimulia yaliyokuwa
yakitokea kwa jirani yao; anamsihi Kazimoto aende nyubani na ataweza kujua
habari zote huko nyumbani kwao. Msimulizi anazidi kusimulia matatizo yaliyokuwa
yakiikumba familia ya kwao Kazimoto: mataizo hayo yaliweza kubainika kuwa ni
imani za kishirikina. Ni watu ambao walikuwa wakiisumbua familia ya mzee Mfuru
kwa sababu ya kutaka kuchukua shamba lao. Mambo haya yanaongelewa katika sura
hii kuanzia (uk.23-39).Ni matatizo na dhoruba ambazo walikuwa wakikumbana nazo
familya ya mzee Mfuru, hasa wakati wa usiku na kuwanyima usingizi: hakika
walikosa amani na kukata tama ya kuishi hadi kufikia hatua ya kumwambia
Kazimoto kuwa wanaangaishwa na wachawi, kwa kuwa yeye amesoma hadi chuo kikuu;
hivyo atafanikiwa. Mama yake Kazimoto
anamwambia mtomto wake hivi: … “Hufahamu
kwamba sisi wote hapa maisha yetu yote yamo hatarini? Kwa kuwa wewe umesoma
nafikiri we ndiwe utakuwa wa kwanza kuuawa.”(uk.24).
SURA YA 3.
Mkondo
au nadharia ile ile ya udhanaishi bado ndio mwongozo wa kitabu hiki. Katika
sura hii mwandishi anatueleza jinsi ambavyo: mhusika Kazimoto, anavyoamka
asubuhi na mapema bila kuwaaga watu aliokuwa akiishi nao na kwenda kumuona na
kumpa pole rafiki yake Kamata anayeishi kijiji cha Saku, kwa matatizo
yaliyomkumba. Kazimoto alifika kwa rafiki yake Kamata mnamo saa nne asubuhi na
kumkuta mke wake Kamata, jina lake ni Matilda. Katika riwaya hii, tunambiwa
kuwa Kamata hakuwepo na alikuwa kazini kwake; alikuwa ziwani kwani shughuli
yake kubwa ilikuwa ni uvuvi. Kazimoto alienda kumpa pole rafiki yake kwa
matatizo yaliyomkuta. Kamata anamsimulia matatizo hayo:
“Kazimoto, furahi kuniona sasa.
Nilikuwa maiti, na ninafikiri kwamba sasa ungekuwa unalia karibu na kaburi
langu. Nilikuwa mfu. Hadithi yenyewe ni hivi: siku moja vijana wawili walinipitia
hapa kwenda kunywa pombe. Vijana hao ni majirani. Tulipofika huko kwenye pombe tulikunywa
sana. Kumbe wenzangu walikuwa na nia mbaya. Giza lilipoingia walikuwa wanajitia
pombe kidogo, mimi nikitiliwa pombe nyingi. Mwishowe nilijiona naanza kulewa.
Niliwaomba ruhusa kuondoka, lakini wao walikataa. Waliahidi kunisindikiza mpaka
nyumbani. Niliendelea kunywa karibu kama saa sita za usiku waliniambia kwamba
walikuwa tayari kunisindikiza. Nilijaribu kusimama, nilijiona bado na nguvu za
kuweza kutembea bila kushikwa. Tulipofika mbali kutoka mahari pa kunywea pombe,
mmoja wao alisema: “Kamata.”
“Nilisimama. Mara niliona kila
mmoja wao ameshika rungu. Hofu ilinishika na pombe yote iliruka. Niliona mwisho wa maisha yangu hapa
duniani.
“Jamani! Kweli mniue! Mniue kabisa,” nilijitetea.
“Ua kabla hajasema maneno mengi!” mmoja
alisema. Hapo hapo nilipigwa rungu la mgongo. Nilianguka chini.
“Jamani kweli sasa mmeniua!”
“Mara moja nilisikia rungu linalia
juu ya kichwa change. Nilizimia.
Kesho yake asubuhi nilipozinduka
nilijiona nimelala ndani ya maji. Majani yalikuwa marefu hata sikuweza
kuona mahali popote. Akili ziliponirudia
sawa sawa nilikaa kwa muda nilifikiri.. nilikumbuka hadithi kidogo. Niliona
nguo zangu zimeenea damu. Nilipojishika kichwani nilishangaa kutupa kidole
ndani ya shimo. Nilianza tena kuogopa. Njljiona maii tena. Nilijaribu kusimama.
Maumivu yalikuwa mengi mno. Niliposimama nilijiona kwamba nilikuwa nimelala
karibu na ziwa. Nilisikia sauti za watu. Nilijivuta polepole. Wale watu
waliponiona walistuka, kama kwamba waliona mzuka fulani. Ndio wale vijana ambao
ulikuwa nao ziwani. Nilipowakaribia
walinitambua: “Kamata! Umekuwaje?”waliniuiza. nipelekani nyumbani
nikamwone mke wangu,” niliwaambia. “Waliponifikisha nyumbani, mke wangu alianza
kulia baada ya kunitafutia maji na kunisafisha. Wale vijana waliosha vidonda
vyangu. Maumivu yalikuwa makali. Niliomba nipelekwe hospitali ya Bukonyo…”(uk.44-45).
Matatizo
yaliyomkumba Kamata, ni matatizo ambayo tumekuwa tukisikia yakiwakumba watu, na
hata pia kushuhudia yakiwakumba ndugu zetu. Kazimoto alitaka kujua chanzo cha
hayo yote: Kamata alimweleza kama ifuatavyo:
“Sikutaka
kukueleza pale nyumbani kisa kilichofanya nipigwe.”
“Ebu
nuileze.” “…sababu yenyewe ni kwamba wale vijana walijaribu kumtongoza mke wangu.
Alipowakataa waliona kwamba alikuwa akiwakataa kwa sababu mimi nilikuwa hai.
Kwa hiyo walikata shauri ya kuniua…(uk.47). Vile vile masimulizi katika
sura hii yanazidi kuhusu maisha yenye raha kidogo pamoja na shida. Ndipo
tunapomuona Kazimoto anakutana na mwanamke Nyabuo wa kufanya naye mapenzi ya
muda pale walipokutana kwenye pombe alipokuwa kwa Kamata. (Uk.52-60). Pia
tunaona kwenye sura hii ndipo Kazimoto, anapowaambia wazee waliokuwa
wakimuuliza maswali ya kuhusu kisomo: kuwa hakuna Mungu.( Uk.51). Kazimoto
anasimulia jinsi ambavyo alipata misukosuko njiani wakati alipokuwa anarudi
nyumbani kwako, alipata ajali njiani. (Uk.62-63)
“Nikiwa
juu ya baiskeli nilijiona katika hali ya upweke. Mawazo mengi yalinijia
kichwani. Mara niliona baiskeli yangu inaongezeka mwendo: nilikuwa nimefikia
mwendo mkali. Nilijaribu kufunga breki baada ya kuona kundi la ng’ombe mbele
yangu barabarani kabisa. Nilifunga breki kwa nguvu. Nilisikia kitu fulani kama
mlio wa chuma. Baada ya kupunguza mwendo baiskeli ilianza kwenda kasi sana.
Nilitambua mara moja kwamba sikuwa na breki za nyuma. Niliogopa kutumia za
mbele. Kutahamaki niliona ng’ombe mmoja hatua kumi hivi mbele yangu. Nilimgonga
ubavuni. Nilisikia ng’ombe analia. Baiskeli ilianguka mbali na mimi nilipita
juu ya mgongo wa ng’ombe na kuanguka upande mwingine. Kidogo yule ng’ombe
anikanyage tumboni aliporuka kuwakimbilia wenzake. Nilisikia watoto waliokuwa
wakichunga wale ng’ombe wakinicheka na kunizomea.
“Hilo! Linabahati! Kama lingeanguka juu ya
pembe, leo lingeona cha mtema kuni!”
“Tazama mandizi yake!” walisema.
Hii
ni safari ya kumuona rafiki yake ambayo misukosuko ya maisha ilimkumba mhusika
mkuu Kazimoto wakati akienda na kurudi kutoka kumsabahi rafiki yake Kamata.
SURA YA 4
Hiii
ni sura fupi ambayo inaeleza jinsi Kazimoto alivyofika nyumbani kwao usiku
akitoka kwa Kamata. Aliwasili nyumbani kwao usiku na kukuta ndugu zake
wamekwisha lala; lakini mibweko ya mbwa waliokuwa wamewafuga ndio iliyomfanya
mama yake ashtuke na kwenda kuangalia chumbani kwa Kazimoto na kumkuta
amewasili toka safarini: baada ya kondoka bila kuaga nyumbani. Mama yake
alichukua jukumu la kumhoji kama mzazi ili kujua alipokuwa, kwa muda wote huo
(uk.64). Kazimoto hakupendezwa na maswali aliyokuwa akiulizwa na mama yake,
kwani yalimuudhi na kutopenda kabisa kusikia akiulizwa hivyo.
Baada
ya hapo kesho yake, mama yake alichukua jukumu la kumtibu mtoto wake: kwa
kumkanda sehemu alizoumia alipopata ajali, na baadaye baba yake Kazimoto na
Kabenga walimwita Kazimoto na kumpeleka kwenye chumba cha maongezi ili kumuonya
mtoto wao kwa kuondoka bila kuaga mtu hali akijua kuwa aliwaacha watu humo
ndani.(uk.66-67).
SURA YA 5
Sura
hii tunapata kujua kwa ufupi kuhusu wahusika Vumilia na Tegemea(uk.68): ambao
maisha yao yalikuwa ni ya taabu. Vumilia na mama yake Tegemea waliishi sana
maisha ya kuwa na wanaume wengi bila kuolewa kwa muda mrefu kidogo. Ni sura
ambayo tabia za Kazimoto za kuingia kimahusianao na msicha Vumilia zinapoelezwa.
“Mimi nilimfahamu Vumilia ambaye nilikuwa na uhusino naye. Ya zamani
hayanuki.”(uk.69). Kazimoto anaamua kumfuata usiku Vumilia akiwa na mdogo wake
Kalia: ni baada ya wazazi wake kuwa wamesinzia kutojua kinachoendelea. Wanafika
kwa Tegemea na kumchukua Vumilia usiku. Baada ya kufika kwa Tegemea muda huo
ambao hapakuwepo na kulandalanda kwa watu kwa kuwa ulikuwa muda wa watu kupumzika:
Kazimoto na Kalia walishtuka na kushangaa kusikia sauti ya Kabenga ndani ya
chumba cha Tegemea. Alikuwa akicheka na kunong’ona na Tegemea ndani ya chumba
cha kulala. Mara walikuwa wakizozana na kupatana juu ya mambo yao ya kimapenzi
humo chumbani, na vijana hawa wawili waliokuwa wakiwanyemelea katika dirisha la
chumba cha Vumilia waliwasikia.
“
…Kalia alikuwa akicheka kwa ndani hali ameziba mdomo…”
“Anayezungumza humo ndani
umemtambua?”aliniuliza.
“Nafikiri nimemtambua.” Ni Kabenga.”
“Kumbe mzee huyu ni hatari!
Uhusiano ulianza lini?”
“Tangu zamani,”Kalia alisema, “isipokuwa
mlikuwa bado hamjagongana. Kama nasikia huu ndo umeleta mpango wa kumuoza
Vumilia kwa Manase. Tuza anapinga sana uchumba huu na Manase mwenyewe hapendi.
Juzi juzi walimtuma Vumilia kwenda kuzungumza kidogo na Manase. Lakini nasikia
Vumilia alimkuta Manase anaishi na kimada. “Gonga dirisha umchukue mke wako,
twende naona baridi. (”uk.70-71)
Vilevile
, kuna msemo usemao kuwa, tabia urithishwa. Hili ndilo lililomkuta Kalia na
Kaka yake baada ya Kalia kuona sasa naye kusindikiza kaka yake katika safari za
kuchukua vimada, wakati yeye anaambulia patupu ilikuwa imefika kikomo. Naye
sasa alidai kuwa anataka kuwa anapata wasichana pindi kaka yake naye anapopata.
Kazimoto anasema kuwa; ndani ya nyumba Kalia alianza kutoa manung’uniko yake
ambayo nilifikiri kuwa ya kitoto.
“Bwana , nimeona sasa siwezi kuwa
nakupeleka kuchukua wanawake. Wewe unapata mimi siambulii lolote. Usiku kama wa
leo siwezi kupata usingizi vizuri.” Vumilia alicheka.
“ Sasa unataka tugawane?”
nilimwuliza. “Nataka na wewe uwe unanisaidia kupata wasichana. Yaani siku
unayoleta name niwe naleta.(”UK.72)’
Si
hayo tu, bali pia, katika sura hii ya tano ndipo pia mihimili ya udhanaishi
inapojidhihirisha wazi kwetu: tunaposoma riwaya hii kwa umakini. Mawazo na
ndoto za kuwepo maisha baada ya kifo ndipo tunapokutana nayo tena katika
mazungumzo kati ya Kazimoto na Kalia. (Uk.73-74) … Asubuhi na mapema Kalia alikuja chumbani mwangu.
“Amekwenda?”
“Nilimsindikiza peke yangu. Wewe
ulikataa!”
“ Mimi sikukataa isipokuwa name
sasa anahitaji mwanamke.”
Alinyamaza kwa muda. “Leo nimeota
ndoto ya ajabu,” alisema tena.
“ Ulikuwa na mwanamke?”
“Hata nimeota nikiwa mbinguni.”
“Sema kweli!”
“Kabisa!” Ulikuwa peke yako huko
mbinguni?”
“Tulikuwa wengi sana” Tuseme
mlikuwa katika hali gani?”
“Tulikuwa wote tunafurahi na mimi niliweza kuwatambua
wenzangu niliokuwa nikifahamiana nao duniani.”
“Mlikuwa na miguu na kila
kitu?” “Ndiyo lakini tulikuwa
hatutembei; tulikuwa tunakwenda tu.”
“Ulimwona Mungu?”
“Hata! Isipokuwa tulikuwa tukifahamu
kwamba kulikuwa na nguvu fulani juu yetu, ambaye nafikiri ndiye Mungu mpenzi.”
“Mlikuwa katika rangi gani?” “Sikuona rangi.”
“Yaani hukutofautisha kati ya
Mzungu na mtu mweusi.” “Mimi sikuona rangi.”
“Lakini Kalia kabla ya kwenda
mbinguni lazima ufe.” “Ndiyo.”
“ Unakumbuka jinsi ulivyokufa na jinsi ulivyofanya safari yako ya kwenda
mbinguni?”
“Ndiyo.” Niliwaona baba na mama
wamezunguka kitanda changu, halafu baada ya muda nilijiona hali yangu imegeuka.
Nilikuwa nikitangatanga mara nilipowaona wenzangu wanakuja kunipokea. Nilikuwa
mbinguni tayari.
“ Ulivyoona wewe mbingu hiyo mbali na dunia?”
“ Hata! Mara fulani fulani Mungu mpenzi alikuwa anaturuhusu kuja
ulimwenguni. Tuliwaona watu, lakini wao waliuwa hawawezi kutuona. Harafu
tulirudi. Tulipokuwa tunafika mahali fulani mara hali yetu iligeuka tukajiona
mbinguni tena. Hali hii ya kugeuka tulikuwa tumezoea kuiita ‘kupokelewa na
Mungu mpenzi’.”
“Bado sijaelewa, yaani mliuwa
mkitembea kwa miguu?”
“ Hapana, tulikuwa tunakwenda tu,
halafu hali yetu kuigeuka na
tukajiona mbinguni tena.”
“Mlikuwa mnakwenda tu namna
gani?” “Kwa nini wewe huelewi?”
“Kwa nini kila mara unasema Mungu
mpenzi?”
“Kwa sababu tulipokuwa mbinguni
tuliona kwamba Mungu anatupenda vile kwamba tuliona vigumu kumkosea kwa sababu
ya aibu kubwa.”
Baada
ya mazungumzo hayo; mtihani ulibaki kwa Kazimoto, kutafakari alioambiwa na
Kalia kuhusu kufa na kwenda mbinguni. Alitafakari juu ya kufa, na alibaini
kwamba kufa ni kugeuka hali “…yes, a change of state,”… nilisema kwa
kiingereza, (Uk.75). Pia alibaini kuwa mbingu haikuwa mbali nasi. Vilevile waliokufa
tuko karibu nao. Hatuwezi kuwaona kwa sababu hali yetu haijageuka. Jambo lingine
ambalo alilitambua ni kuwa wale ambao hawatendi dhambi ndio wanaotambua kwamba
Mungu anatupenda vile kwamba ni aibu kumkosea. Kuhusu watu ambao hutenda dhambi
huishia motoni kama adhabu yao, ni suala ambalo alilikumbuka Kazimoto na
kumuuliza Kalia: “…Asee, hukusikia kwamba kulikuwa na watu wengine motoni?”
“Hata!
Sikusikia.”
Mwongozo
tunaoupata kwenye sura hii, ni kuwa, maisha ya starehe duniani yanakuwepo, ila
baadae yanaisha pale mtu anapokufa. Baada ya kufa maisha mengine yanasadikika
kuwepo mbinguni, ambayo ni tofauti kabisa na maisha yale ya ulimwenguni. Ndipo
tunaweza kujiuliza kwamba, maisha ni nini au kitu gani?
SURA YA 6
Sura
ya sita ni sura ambayo inazungumzia namna ambavyo mtu huweza kuiga tabia mbaya
kutoka kwa nduguye au rafiki yake hadi kuona maisha mabaya. Ni sura ambayo
msimulizi anaeleza jinsi ambavyo Kalia alianza kuiga mambo ambayo alikuwa
anaona kaka yake akifanya. Tunaelezwa jinsi alivyofikia hatua ya kumvamia na
kumbaka msichana aliyekuwa anachunga ng’ombe, (uk.80-81).Lakini hayo yote Kalia
aliyaiga kwa Kazimoto. Vilevile anasimulia ambavyo Kazimoto alimdharau Kabenga
kwa tabia yake ya kuingilia mke wakati ana mke wake wa halali. Pia katika sura
hii tunaambiwa kuwa Rukia hali yake ilianza kuwa mbaya sana kutokana na ugonjwa
uliomsibu. Ndipo walipoitwa Tuza na Tegemea ili kumsaidia Rukia kwani
alikaribia kujifungua: mama yake Rukia anagoma kula mpaka bintiye
atakapojifungua,(uk.76). Chuki dhidi ya Manase inamkumba Kazimoto baada ya dada
yake kukaribia kuijfungua kwa sababu ilikuwa mimba ya Manase na alimtelekeza
Rukia.
Udhanaishi
juu ya maisha yanarejea tena kwenye mawazo ya Kazimoto. Ni pale ambapo aliona
nyuki anaanguka katika maji na kujaribu kujitetea ili kuona maisha yake.
Alichukua jukumu la kuokoa maisha ya nyuki huyo kama tunavyoona; “ …Juu ya jiwe niliona kibwawa kidogo cha
maji. Ndani ya maji haya niliona nyuki ameanguka akiogelea. Nilijongea karibu.
Mwanzoni nilifurahi kumwona huyu mdudu akipigania maisha. Lakini baada ya muda
mfupi nyuki alikata tamaa. Nguvu zilimwishia alisambaza mbawa zake, miguu yake
ilianza kupiga pole pole kama mtu aliyekata roho. Huruma iliniingia moyoni.
Niliona kwamba nilikuwa na uwezo wa kuokoa maisha yake kwa tendo moja dogo tu ambalo lilikuwa haliitaji hata tone
moja la jasho. Nilijiona Mungu mdogo. Nilitazama tena pande zote, watoto, nyumba
na miti, vyote vilikuwa chini yangu.
Nilichukua kijiti kidogo sana ambacho
kwacho nilimtoa yule nyuki majini. Mbawa zake zilipokauka aliruka bila kusema
asante. Aliruka bila hata kujua nani amemwokoa. Kwa huyu mdudu nilikuwa na
nguvu ambazo haziwezi kufahamika. “Labda mfano huu unaweza kumsaidia mwanadamu
katika kuelewa fumbo la Mungu,” nilisema moyoni. “Lakini labda haiwezekani.
Tuseme kama yule nyuki akinifikiria mimi kuwa mwenye uwezo usioeleweka sio
kusema kwamba mimi ni Mungu, kuna mwenye uwezo zaidi kuliko mimi. Labda hata
mwanadamu anaweza kusema kwamba kuna mwenye uwezo kuliko yule tunayemfikiria
kuwa ni Mungu. Lakini kama ni vile tutakwenda nyuma mpaka wapi? Labda tunaweza
kusema kwamba ni wakati. Wakati wenyewe ni Mungu maana haukuumbwa.”
Katika
kutafakari jinsi alivyookoa maisha ya nyuki na kuyalinganisha na mwanadamu
anavyohangaika: mara akilinganisha na uwezo wa uwepo wa Mungu, Kazimoto
alichoka. Aliamua kuchukua kitabu na kujisomea: kilizungumzia maarifa na tamaa
zinavyompeleka mtu katika mabaya na mazuri katika maisha yake. (Uk.79-80).
Kuanzia
ukurasa wa (82), masimulizi yanahusu habari za kifo cha Rukia. Kabenga na Kalia
ndio waliomfuata na kumpasha habari za kifo cha dada yake Kazimoto;
“…Sikuona kwa nini walinikimbilia mimi
kama kwamba mtoto alikuwa wangu. Waliponifikia Kabenga ndiye aliyekuwa wa
kwanza kuzungumza. “ Kazimoto, ndugu yako ha… ako kati… katika hali mbaya sana.
Nilikaza mwendo ili niwahi; nifike kabla hajaaga dunia. Kabenga alipoona kwamba
sasa sauti zinaweza kusikika alinigeukia. Alinitazama usoni. Nami nilielewa.
“ Kazimoto,” alisema, “ndugu yako
amekufa!” Niliinama. Uchungu ulionipata ulikuwa mwingi.
“Kazimoto,” Kabenga aliendelea huku
akiweka mkono juu ya bega langu, “twende nyumbani; watu nyumbani wanakungoja
wakupe pole ya msiba.”
Kazimoto
alienda nyumbani na kukuta msiba. Alienda moja kwa moja katika chumba alimokuwa
amelazwa marehemu dada yake. Alimshuhudia kwa kumgusa kwa mkono akiwa amelazwa
kwenye kitanda. “…wakati huo huo machozi
yalijaa machoni. Niliyaacha yatelemke.”
Baada
ya kifo cha Rukia, mama yake Kazimoto, naye alizimia. Baba yake ndiye
aliyemjulisha Kazimoto, … nilipotoka nje
baba aliwaacha watu waliokuwa wamemzunguka wakimpa pole akaja kuzungumza nami.
“Kazimoto, mama yako amezimia. Amelazwa upande mwingine alikuwa akimwagiliwa
maji kichwani. Niliingia ndani ya nyumba tena. Chumbani alimokuwa amelazwa
niliwakuta Tuza na Tegemea. Walikuwa wamekaa karibu naye. Mmoja alikuwa
akimpepea kwa sahani; mwingine alikuwa akimwagilia maji kichwani. Nilipomshika
mkono niliona kwamba moyo ulikuwa bado ukipiga ingawa bado kwa hafifu.”
Baada
ya Kazimoto kushuhudia mama yake akiwa amezimia, alipewa wosia aliomwachia
marehemu dada yake.
“Kazimoto,” Tuza alisema, “ndugu yako amekufa kwa sababu amekosa nguvu;
alikuwa hajala vizuri kwa muda mrefu uliopita.”
“Hayo usemayo ni kweli,” nilimwambia.
“ Amekufa akitaja jina lako.”
“ Alisema nini kuhusu jina langu?”
“Alikulilia; akikuomba umsamehe kwa
yale yote yaliyotokea kwake. Amekuomba usisikitike sana. Hata yeye alikuwa
haoni tena maana ya kuishi.”
“Ndiyo hayo aliyosema?”
“Nimesahau jambo moja. Amesema
kwamba, maadam yeye akitoweka kama yalivyokwisha kutimia, anakutakia uhusiano
mzuri na Manase. Yeye amemsamehe ni zamu yako sasa kumsamehe.(”uk.83)
Kutokana
na hali ya huzuni iliyokuwa imeikumba familia ya mzee Mafuru, usiku Kazimoto
alianza kufikiri juu ya kifo. “Nilifikiri
jinsi kifo changu kitakavyonijia – kwa ugonjwa, kwa ajali au kwa kukatwakatwa
na wezi? Labda kwa uzee au kwa sumu! Huenda nikajiua mwenyewe! Nilikumbuka
ndoto ya Kalia. Niliwakumbuka wale ng’ombe, sisimizi, nyuki na mengine mengi
niliyoyaona huko machungani. Niliona kwamba adhabu kubwa ya mwanadamu ni maisha
yenyewe. Nilimkumbuka mlevi mmoja niliyemkuta akipiga mti mweleka mpaka akaumia
mwenyewe. Maisha ndiyo yaliyokuwa yakimsumbua wala si pombe. Wakati huo usiku
niliyaona maisha kuwa chanzo cha yote. Sikuona kwa nini mwanadamu alicheza
ngoma na kupiga vishindo chini. Sikuona kwa nini alicheza twisti mpaka utumbo
ukakaribia kukatika. Kwa nini mwanadamu alijidai kupiga mpira kwa kichwa
kitunzacho bongo, sikuona. Mwanadamu mwenye akili hufurahi apitishapo moshi
puani! Kweli, kama sigara za aina fulani zikitengenezwa , sigara ziwezazo
kupitisha moshi masikioni, mwanadamu atanunua na kupenda hizo zaidi kuliko za
siku hizi? Yote mwanadamu mwenye akili anafanya kwa jina ambalo limepumbaza
akili. Jina ‘Furaha’ ambalo ni neno jingine la adhabu.
Hii ni adhabu ambayo kila mwanadamu
amepewa – kutunza maisha yake. Maisha ambayo hayashibwi wala kuridhishwa. Zaidi
ya hayo mwenye nguvu anatunyang’anya maisha haya wakati wowote bila hata
kutuarifu. Kweli, mfano wa adhabu hii kali ni yule mtu aliyeamrishwa kujaza
maji ndani ya pakacha. Na sisi wanadamu tumekubali kufanya hivi kwa jina la
‘Furaha’. Maisha matamu! Yaani adhabu ni tamu. Ndiyo kusema tuna akili kweli
wanadamu? Maswali haya yalinizunguka sana kichwani. Mara fulani niliamua kwamba
mwanadamu hana akili. Kama angekuwa na akili angekataa adhabu hii; na kama yule
ambaye ametupa adhabu hii angetushurutisha tungejua sote. Mara zingine niliona
amfuata. Mwanadamu amekusudia kuacha adhabu hii. Mwisho wa mwanadamu utaletwa na mwanadamu
mwenyewe. Vita vya kwanza vilishindwa kuleta mwisho huu. Vita vya pili pia
vilishindwa. Tegemeo sasa ni vita vya tatu au vya nne. Wakati usingizi uliponichukua,
sikumbuki.”( Uk.84-85).
Kauli
ya ‘maisha hayana maana’ ilizidi kujidhihirisha kwa Kazimoto: ni wakati mama
yake alipokufa siku iliyofuata baada ya kifo cha Rukia. Ilikuwa ni siku ya
kuzika mwili wa Rukia ambapo mama yake Kazimoto alilia kwa ukali na huzuni kwa
mwanae. Uk.85: Wakati wa kuchimba kaburi,
mama alikuwa ndani ya nyumba akiongea mambo ambayo yalikuwa hayaeleweki. Lakini
kaburi lilipokwisha, Tuza na Tegemea walimshika na kumsaidia kutoka nje ili
aone binti yake akizikwa. Alipofika tu mlangoni na kouna shimo lililokuwa limechimbwa tayari kumzika binti yake alilia
kwa sauti ya juu sana . “Rukia! Rukia!” hali akionyesha kwa mkono wake kaburi.
Halafu alia- nza kulia kwa namna ya pekee. “Kichwa! Kichwa!’ alitotoma na
kuanguka chini. Wakati alipobebwa kupelekwa kitandani alikuwa amekwisha kufa.
Kifo chake kilipotangazwa kila mmoja alishangaa. Huo ndio ulikuwa mwisho wa
mama yangu. Nilikuwa siwezi kumuona tena maishani. Nilikuwa siwezi kusikia tena
sauti yake. Mola alimnyima ile furaha
kubwa wapatayo akina mama wakati mtoto anapooa. Huo ndio uliokuwa mwisho wa mama aliyempenda binti
yake wa pekee kama pumzi na mwanadamu. Alikuwa amenyang’anywa pumzi yake.
Niliyakumbuka tena maneno yake: “Kazimoto,tuache tupumzike tuache tulie. Huu ni
ugonjwa umeletwa na vijana, na utatumaliza sisi kina mama wenye mabinti.
Ninajiona kwamba nitakwenda na binti yangu.”
Katika
mwendelezo wa sura hii, mwandishi anamlizia kwa kutuonesha kuwa ndugu wafiwa
walipekekwa na watu wailokuwa wamekuja kuwaanali kwa msiba, ili kuwaliwaza.
Walipelekwa katika sehemu za kunywea pombe. Walinunuliwa pombe na watu hao.
Ndipo tunapoona mawazo ya kulipiza kisasi yanaibuka tena kwenye mawazo ya
Kazimoto. Safari hii ilikuwa ni malipizo kwa Kabenga. Kwa sababu vifo vya ndugu
zake Kazimoto, vilitokana na Manase mtoto wa Kabenga ndio maana Kazimoto
alitaka kulipiza kisasi. Alifanya hivyo, baada ya jaribio lake la kumuua
Kabenga kushindikana sababu ya woga wake: ndipo alipoamua kuchoma nyumba ya
mzee Kabenga. (Uk. 87-89).
SURA YA 7.
Ni
mwendelezo na msimamo au mtazamo ule ule uliotumika kuandika riwaya hii katika
visa vyake. Ni juu ya jambo moja la maisha ambalo lilikuwa likumsumbua kijana
Kazimoto pia katika sura hii ya Saba. Kudhihirisha hilo soma maneno yafuatayo
kwenye uk.90:
“Nilipofika
mtoni sikukuta mtu. Nilikaa kwa muda nikiyatazama maji yakitelemka kuelekea
ziwani. Niliaza kufikiria kama kweli maisha ya binadamu hayawezi kulinganishwa
na maji yatelemkayo kutoka mlimani kuelekea ziwani au baharini. Maji yalikuwa yakitelemka
kwa kasi sana; kurudi juu yalikuwa hayawezi. Yalikuwa hayasukumwi na nguvu
kutoka nje isipokuwa yalikuwa yakinda tu kwa sababu kulikuwa na mteremko.
Yatake yasitake yalipaswa kuteremka. Nilishangaa kuona kwamba watu wengine
wamelinganisha maisha ya binadamu na mtu apandaye mlima akisukuma jiwe na
kurudi nyuma kuokota jiwe. Niliona kwamba mwanadamu anateremka kama maji kwa
kasi sana; na kama maji ya mto yakusanyavyo takataka za kila aina ndivyo
mwanadamu akusanyavyo taka wakati wa maisha yake. Maji yakifika ziwani
yamekwisha kusanya taka nyingi; pia mwandamu afikapo mwishoni mwa maisha yake
huwa amekusanya taka kadri ya muda alioishi. Niliona heri ningekufa ningali
mtoto.”
Kazimoto
anaendelea na tafakari yake juu ya maisha, kwa kutoa mifano ambayo sio rahisi
mtu kuielewa haraka bila kuitafakari kwa kina. “Nilipokuwa nikivua nguo zangu niliona mjusi akiwa amejibanza kati ya
ufa wa jiwe. Yeye alifikiri nilikuwa simuoni.
Nilikwenda pole pole na mara nilikata mkia wake. Mjusi alijisukuma
ndani. Mkia wake ulianguka chini. Ulipapatika. Nilishangaa, kwani maisha yote
alikuwa nayo mjusi aliyekuwa ndani. Sikuona kwa nini mkia uliruka kwa muda
mrefu vile kama kwamba ulikuwa bado umeungana na mjuisi. Nilijitumbukiza
majini. Baada ya kuoga niliona mkia ukiburuzwa na mamia ya sisimizi kuelekea
kwenye kishimo kidogo.”uk.91.
Masimulizi
sasa yanaingia katika mtazamo mwingine ila unaolenga ujumbe ule ule na msimamo
ule wa msimulizi. Kazimoto anasimulia maswahibu yaliyomkuta mdogo wake Kalia:
alipouwa sasa amejiingiza katika tabia mbaya sana bado ni mdogo. Kalia alichukua
hela ambayo ilisahaulika ndani ya nyumba pale baba yake alipokuwa akihesabu
pesa zake. Alikuwa akimchukulia Tegemea pesa baada ya kuwa naye kimapenzi hali
Tegemea alikuwa mama mkubwa wa kumzaa. Kitendo hicho cha kuchukua hela
kilimponza Kalia baada ya kuonwa na baba yake na kupigwa vikali na baba yake (uk.91-92).
Katika ukurasa wa (93) kituko kingine kinasimuliwa: kilimhusu Kazimoto. Ni
baada ya mama yake Vumilia, Tegemea; kuwavamia mzee Mafuru na familia yake kwa
malumbano ambayo yalikuwa ni kuhusu Kazimoto kuwa na mahusiano ya kimapenzi na
Vumilia mtoto wake Tegemea hali akijua kuwa alikuwa akiozeshwa kwa Manase.
Kazimoto alionywa vikali na babayake, baada ya kukiri mwenyewe kuwa alikuwa
akitembea na Vumilia. Uk.94-95.
Masimulizi
yalihamia kwa Kalia. Muda huu Kalia alibainika akijirusha na Tegemea. “Kweli Kalia alikuwa akifuata nyayo zangu;
niliona aibu kwa jambo nililolitenda. Kalia alikuwa haendi kwingine isipokuwa
nyumbni kwa Tegemea. Badala ya kupitia mlango wa nyuma yeye alipiti mlango wa
mbele. Kweli, Kalia alikuwa sasa akinipitia katika mambo yangu. Mimi nilizoea
kupitia mlango wa nyuma. Alipoingia nilitembea pole pole kuelekea nyumba ya
Tegemea. Nilijibanza ukutani. Mimi nilifikiri kwamba alikuwa akimtongoza
Vumilia. Nilishangaa kumsikia akiongea chumbani mwa Tegemea.
“ Umemaliza kuvua?” Tegemea aliuliza.
“ Tayari,” Kalia alijibu.
“Njoo tulale.”
“Huna haja ya kunikaribisha.” Nilisikia Kalia
akirukia kitandani. Kijana mbichi!
“Angalia usivunje kitanda changu.”
“ Shuka zaidi upande huu; mgongo wangu uko nje.”
“Unafahamu kwa nini Kalia nakupenda?” “Niambie!”.
“ Unanikumbusha siku zangu za
zamani nilipokuwa nikitembea na vijana wadogo kama wewe. Mimi huwa nafurahi
kuona kijana mzuri akiruka ruka juu ya kifua changu. Huwa kama ninanyonyesha mtoto
mdogo. . . haraka gani Kalia; mimi nipo kwa ajili yako.”uk.96-97.
Umdhaniaye
ndiye, kumbe siye; kikulacho kinguni mwako. Misemo hii ilijidhihirisha kwenye
sura hii, pale ambapo mchawi aliyekuwa akiisumbua familia ya mzee Mafuru alipojulikana.
Alikuwa ni jirani yao, mzee Kabenga. Kalia alimjulisha Kazimoto.
“Nilipofungua nilimwona Kalia. Kwa
muda mrefu tulikuwa hatujazungumza
vizuri, hasa siku ile niliyomwambia kuwa alifanya vibaya kuiba shilingi
zangu.
“ Nina mambo ya kukwabia.”alisema.
“ Ingia ndani.” Aliingia. Niliwasha
taa. Alikaa juu ya kiti, name nilikaa kitandani, shuka yangu imenizunguka.
“ Kazimoto, nimevumbua siri kubwa.’
Siri gani?’
“ Nimemfahamu yule aliyekuwa akitupia
mchanga wakati wa usiku.” ‘Nani?’ “..Kabenga.”
“Wewe umefahamuje?” Alicheka
kidogo.
“Kazimoto, siku hizi katika mambo
ya wanawake nakuzidi wewe. Kwa muda nilikuwa nikimwendesha Tegemea . . .
Tegemea siku moja aliniambia siri yake na Kabenga. Siri yenyewe ni hii: Kabenga
ni marafiki wa muda mrefu. Tegemea siku moja alimwomba Kabenga shamba la kulima
pamba. Kabenga alimwambia kwamba alikuwa na mashamba mengi sana. Lakini kwa
bahati mbaya serikali ilimleta baba kuishi humo kwa kuwa alkuwa hayatumii yote.
Kwa hiyo njia ilitafutwa ya kutufanya sisi tuhame ili apate kumpa Tegemea
mashamba haya. Nami naona habari hii ni ya kweli.” Uk.98-99.
SURA YA 8.
Ndani
ya sura ya nane, tunapata kusimuliwa maisha mengine yahusuyo kijana Kazimoto.
Lakini hapa maisha hayakuwa ya Kazimoto peke yake, vilevile yalimhusu pia
msichana Sabina. Sabina alikuwa msichana mbichi jirani na akina Kazimoto, ndugu
yake Manase na mtoto wa mzee Kabenga na Tuza. Kazimoto anaeleza jinsi ambavyo
Sabina alivyokuja kutoka Tabora alipokuwa anafanya kazi ya kufundisha: na
alikuja kumpa pole Kazimoto kutokana na msiba ulitokea kwao. Ni miongoni mwa
wanafamila ya mzee Kabenga ambao walikumbwa na kisasi cha Manase. Sura hii pia
inadadavua zaidi mawazo ya Kazimoto baada ya kukutana na Sabina. Kama
ilivyokwisha simuliwa, Kazimoto sasa alitaka alipize pia kwa Sabina kama
alivyofanya Manase kwa Rukia dada yake Kazimoto.
Kazimoto
alindelea na mawazo yake ya kutaka kulipiza kisasi kwa Sabina. Uk. 102: anasema, “ Ng’ombe mzee akikanyaga
matopeni harudi mpaka achinjwe pale pale. Hapa sasa kulikuwa na ng’ombe mzee.
Kazi yangu ilikuwa ni kumsukuma matopeni, na kumwacha akitapatapa roho ili
kumaliza siku zake za mwisho. Manase alimtia mimba ndugu yangu, akafa. Ngugu
yake sasa alikuwa karibu nami. “Kwa nini nami nisifanye kama yeye?”
nilijiuliza. Yeye mwenyewe Manase mtoto wa Kabenga, alisema mimi mwanaume kama
yeye. Nami, mtoto wa Mafuru, nilikata shauri kutumia njia yoyote ili kumpata
huyu msichana, sio kumpata tu kwa siku moja, isipokuwa mpaka nihakikishe kwamba
tumbo lake lilikuwa zito.”
Sabina
ni msichana ambaye alikuwa ameanza tayari kukata tamaa ya kuolewa. Alikuwa ni
msicha ambaye umri wake ulikuwa unaelekea kukosa mchumba. Alikuwa na miaka 26.
Sababu ya kufikisha miaka yote hiyo bila mchumba ni kwamba, alikuwa ni msichana
aliyefuata sana dini na wavulana waliomfuata aliwajibu kwa majibu yenye
kurejelea bibilia. Pia walimwona kuwa ni mwenye kiburi na aliyewadharau
wanaume. Wanaume wengi walimkimbia baada ya kuona hawapati cho chote isipokuwa
maneno. Sabina alikuwa ameanza kukata tamaa ya kuolewa na aliamini kuwa Mungu
alikuwa akimjaribu yeye na alikuwa hataki kupoteza imani yake, (uk.100 na
uk.103-104), Kazimoto anamuuliza Sabina kinachomfanya asiwe na mume. Na Sabina
anamjibu. Katika majibizano hayo tunaona Sabina mbali na kumwamini Mungu,
tunaona anasema kuwa ana machungu ya kutoolewa na ana huzuni moyoni.
Zaidi
masimulizi yanazidi kutuonesha Kazimoto anavyojitahidi kumpata Sabina msichana
aliyekuwa mzuri mnene na mfupi kiasi. (Uk.106,107,108,109). Sabina tayari ameshakuwa
wa Kazimoto na ni wapenzi wasio weza kuitilafiana. Mapenzi yao sasa yalinoga
hadi Sabina akawa anamfulia na kunyooshea nguo Kazimoto. Jambo ambalo
lilimfanya Kazimoto kumsahau kabisa Vumilia: wazo la kulipiza kisasi liliitika
kichwani mwake, uk.109, Kazimoto anaonyesha mapenzi ya dhati kwa Sabina,
anakimbia kwenda kumuona baada ya Kabenga kuwataarifu kuwa hali ya Sabina
imekuwa mbaya, na aliumwa ghafla. Mapenzi sasa yalinoga sana na Kazimoto
anaamua kumchumbia Sabina ili awe mkewe, uk.113.
Wahenga
walisema, “Asiyefunzwa na mama yake, basi ulimwengu humfunza.” Ni methali yenye
maana yake ambayo ukweli huu ulijidhihirisha kwa Kalia. Kalia aligeuka na kuwa
Nunda mla watu pale kijijini. Kalia alianza tabia ya kuwavamia wanawake usiku
na kuwalazimisha kufanya nao mapenzi: waliokataa aliwatishia kwa visu na silaha
ili wakubaliane naye. Baada ya kugundulika, Kalia alifukuzwa kijijini. Kuanzia
hapo kila mtu akawa anamwinda yeye, kwani amekuwa tayari ni adui wa kila mtu,
(uk.110 – 111). Nadharia ya maisha hayana maana yoyote ilionekana kuwa na
mantiki kubwa sana: ni baada ya kusikia habari za kifo cha Kalia. Japo alkuwa
adui wa watu kwa muda ule Kalia mwili wake ulikutwa unaelea majini huko mtoni.
“Mna
habari?” Kabenga alianza kusema. “Mwili wa Kalia umekutwa ukielea majini huko
mtoni kwa siku mbili.” Watu wameuona, lakini hakuna mtu apendaye kujiweka
hatarini. Mwishowe nimejitolea kuja kuwaambia. Heri twende tukautoe kabla
haujaharibu maji yote ya mtoni, watu wakakosa mahali pa kuoga.” Uk.114. ndivyo
kifo cha Kalia kilivyojulikana pasi na mtu kujua amekufaje. Na katika mazishi
ya mwili wa Kalia watu wachache walihudhuria mazishi hayo; hasa familia ya mzee
Mafuru na mji wa Kabenga ndio walioshiriki kikamilifu kwenye maziko hayo kwa
sababu alikuwa ndugu yao.
SURA YA 9
Kazimoto
bado anaendelea kutazama kwa jicho pana na anajiuliza juu ya maisha ya
mwanadamu na hapati jawabu lake kwa urahisi. Anazidi kutuonyesha misukosuko
inayomfanya mwanadamu kuyajutia maisha. Uk.115, anaeleza jinsi ambavyo Tegemea
alivyokutwa anaiba viazi kwenye shamba la Mafuru. Mafuru anamsamehe Tegemea kwa
kuona kwamba aliiba kwa sababu ya njaa ya chakula. “Swali hili, baba alilikatisha upesi kwa kuwaambia wasijali sana.
Halikuwa jambo baya kumsaidia mtu mwenye njaa walau siku moja.”
Vilevile
anajaribu kujiuliza juu ya mwanadamu na akili zake. Anasema kuwa mwanadamu
akili zake ni fupi, uk.116. Mfano unatolewa kuudhibitisha kuwa binadamu akili
yake ni fupi, akimwelezea kijana ambayea alipita katika njia ambayo ilikuwa
imezibwa kwa miiba ili watu wasipite. Kijana huyo alilazimisha kupita na
kukutana na joka kubwa ambalo lilimdonoa na akafa pale pale. Ndivyo
anavyomfananisha mtu anayejiuliza maswali juu ya Mungu na kujaribu kumchunguza
Mungu. Maisha hubadilika. Ndivyo anavyobadilika Kazimoto; baada ya kuona kwamba
barua aliyomwandikia Manase kwa hasira ya kulipiza kisasi haikuwa na maana
tena, bali ni kumuomba samahani Manase na Manase anamsamehe,( uk.117).
Kazimoto
akiwa tayari ameshafika kwa Manase na sasa ni mgeni wao: anashuhudia mzee
aliyekuwa ni mfanyakazi wa ndani akikaripiwa na Salima mke wa Manase. Ni mzee
ambaye ki-umri ukilinganisha na Salima hakupaswa kukaripiwa na kijana mdogo
kama Salima ijapo ni mfanyakazi wake. Uk.120. Bado suala la maisha linazidi
kuumiza kichwa cha Kazimoto; tunaona linajitokeza tena katika mazungumzo yake
na wenyeji wake. Wanaongelea juu ya wanawake wanaojiremba na kujiangalia kwenye
kioo kila mara, pia na watu ambao ni wasomi lakini hawachani nywele. Katika
kutafakari maisha, Manase analeta mada ambazo mifano yake inagusa maisha ya
binadamu, pia zaidi katika imani ya Mungu. Wanajadiliana namna Yesu alivyokufa,
Kazimoto anasema Yesu alijiua kwani alijua kwamba atakufa. Hivyo alijiua
akiona, Salima anamjibu kuwa anahitaji imani, uk.122. Wazo la kifo na mwisho wa
mwanadamu, linazidi pia kujitokeza tena katika mazungumzo. Kazimoto ansema kuwa
kufa ni kugeuka hali. Na kama kufa ni kugeuka hali basi mtu baada ya kufa
anageuka tena kwa mara ya pili. Swali linaloleta dhana ya maisha baada ya kifo
kuwepo. Uk. 123. Katika uk.124, ndipo uwepo na kutokuwepo kwa Mungu
unazungumziwa hapa kama ambavyo tumekwisha ona katika utangulizi wa uchambuzi
wa riwaya hii.
Vilevile
suala la mbingu linajitokeza katika mazungumzo. Ndipo tunapomwona Manase
akimuuliza Kazimoto kuhusu mbingu. “Tuseme
wewe unafikiri nini juu ya mbingu?” Manase aliniuliza. Swali lenyewe
sikulielewa vizuri. Hata hivyo nilijaribu kumjibu. Mwanadamu ni kiumbe ambaye
amejaribu kutafuta mbinu nyingi ambazo zilimwezesha kupata furaha. Kwa kuwa
ameshindwa kupata furaha hapa duniani amejenga kichwani kitu kama mbingu, yaani
mahali ambapo anategemea kupata furaha baada ya kufa.”
“Kwa hiyo wewe umeona kwamba wazo la
mbingu limeletwa na kushindwa kwa mwanadamu kupata furaha hapa duniani.”
“Ndiyo.” Tulinyamaza kwa muda.
“ Na kwamba ni hali ya kujitakia
jambo jema tu.”
“Kabisa.”
“Je wewe unaona kwamba mbingu ipo
au haipo?”
“Ninaona vigumu uamini kwamba
ipo……” Udhanaishi. Uk.122 – 124, mambo na mtazamo wa kuwepo
kwa mbingu na Mungu unasumbua vichwa vya watu watatu: Kazimoto, Manase na
Salima. Pia uk.125.
Mambo
ya kijamii yahusuyo maisha ya binadamu yanajadiliwa. Ni mambo ya kifamilia na
mahusiano zaidi. Suala la uaminifu katika ndoa linajadiliwa kwa mitazamo
mbalimbali ya wahusika hawa watatu. Inafikia muda fulani wa kutoelewana kidogo
kati ya Manase na Mkewe Salima, uk.126 – 127. Mwanadamu sasa anagusiwa juu ya
uzuri na ubaya wake. Na ni mada anayoileta Kazimoto, izungumzwe mezani.
Kazimoto anauliza: “Wewe unafikiri nini
juu ya ubaya na uzuri wa binadamu?”
“Mimi ninaona watu wabaya ni wale
niwachukiao,” Manase alidakia mara moja. Ninachukia wale watu wanaojidai kwamba wao ni wajuzi wa
kila kitu. Hawa ndio waletao chuki duniani. Kama ulivyosema mwanadamu si rahisi
kueleweka…”uk. 127 – 128. Pia hapo hapo mada inayohusu vijana wadogo
kuijiingiza kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo inaingizwa na Kazimoto, na
inajadiliwa kwa kila mtu kutoa mtazamo wake. Kazimoto anauliza, “ Unafikiri
nini kisa cha ugonjwa huu, Manase?” nilimwuliza .
“Ugonjwa gani?”aliniuliza.
“Huu ugonjwa wa vijana kuanza mchezo mbaya wangali umri wa miaka kumi na
miwili na mara zingine kujazana mimba ovyo na kuharibiana maisha. Unafikiri kitu
ganai kimeleta mambo haya kwa haraka
namna hii au labda unafikiri ulimwengu umegeuka, basi?”
“Mimi ninaona kwamba sababu kubwa
ni kwamba ndoa imepoteza maana yake. Zamani jambo la maana ambalo kila
mwanadamu alikuwa akitegemea maishani
lilikuwa ndoa. Lakini siku hizi kama elimu na pesa yamezuka na ndoa
imekuwa kama kitu kisicho na thamani. Vijana wako tayari kuahairisha ndoa,
lakini wasome, ingawa wana umri wa miaka thelathini au zaidi. Unafikiri wakati
wote huu watakuwa wanafanya nini? Hawawezi kukaa kama mabikira.”
“ Wewe huoni kwamba ndoa imepoteza maana kwa
sababu ya vijana kuchezeana wangali bado watoto wadogo, kabla hata ya kufahamu
mambo mengi ya maana usemayo?” Manase hakujibu swali langu vizuri, lakini
wakati huu Salima aliingilia kutoa mawazo yake.
“Mimi ninaona kwamba sababu kubwa ni malezi ya nyumbani. Malezi ya
nyumbani yamelegea kupita kiasi. Licha ya malezi mabaya kuna hii hali ya
wasichana wadogo kutembea na dada zao. Msichana atafanya mambo yale yale
aliyoyaona dada yake akifanya wakati wakitembea pamoja. Mvulana pia atafanya
hivyo hivyo. Itakuwa vigumu kuondoa uovu huu sasa kwa sababu kizazi kimoja
kinafunza kizazi kinachofuata.”
“ Ndiyo Manase alisema kwamba uovu umo ndani
yetu sisi,” alidakia….”( Uk.128 -130).
Katika
sura hii hitimisho linaongelea maisha ya mwanadamu yalivyo hatarini muda wote,
na kusema kwamba binadamu anatembea na kaburi lake kichwani kama anavyofanya
konokono: ingawa mwanadamu anajiweka kichwa kichwa na kujiona anaweza na yuko
sawa bila tabu yo yote. Binadamu anashindwa kulifahamu hili wakati konokono
anakuwa mwelewa juu ya hili jambo. Mwisho kabisa wa sura hii tunaona barua ya
Kazimoto aliyoandikiwa na Sabina wakitegemea kuoana na tayari ni wachumba. Uk.
131.
SURA YA 10
Sura
ya pili imeisha kwa kuona barua ya Sabina kwa Kazimoto: iliyokuwa ikimtaka
Kazimoto kupendekeza mwaka ambao wapendanao hao, wataoana. Hadithi hii
inaendelea kuzungumzwa na Kazimoto katika sura ya kumi. Kazimto anasimulia
jinsi ambavyo yeye alikuwa akichukia uchumba wa muda mrefu ila alibadili mawazo
hayo, baada ya kupokea na kuuelewa ushauri wa mchumba wake, yaani Sabina.
Kazimoto aliona ni vyema kusubiri kama alivyoshauriwa na Sabina, uk.132.
Mara
kwa mara katika kipindi hicho, Kazimoto alikuwa anakwenda mara kwa mara
kijijini kwao. Mabadiliko fulani yalikuwa yamekwisha anza kutokea. Miongoni mwa
mabadiliko hayo yalikuwa ni kuolewa kwa Tegemea na Kabenga. Tegemea aliolewa na
Kabenga, na tayari alikuwa mke wa kabenga: kijijini wote walimfahamu kama mke
wa Kabenga. Waliishi maisha ya ndoa kwa kufanya shughuli za kiuchumi; kama
kulima, ambapo tunaona Tegemea hakuzoea maisha hayo ya shida kidogo. Alikuwa
hajui kulima na aliona taabu kufanya hivyo ila alilazimishwa kulima na Kabenga
kwa sababu ya uzembe wake. Tunaona malumbano yanatokea kati yao wakiwa
shambani, hadi kupigana:
“Umeolewa
ama hukuolewa? Wewe sasa ni mke wangu nafanya nitakavyo! Unakaa chini!”
alikemea Kabenga.
“ Mimi siwezi kulima! Kama ni chakula mtaninyima!” Tegemea alijibu.
“ Utalima!”
“ Mimi nimesema siwezi!”
“Nimesema utalima na utalima!”
“ Kama mambo ni hivi mimi nakwenda nyumbani!”(
uk.134)
Hayo
ndiyo maisha aliyoanza nayo Tegemea kwenye ndoa yake. Baada ya kuanza na furaha
anakutana na msemo usemao ‘mwanzo huwa ni mgumu’. Hizo ndizo karaha za maisha –
maisha ni mateso na maangaiko pamoja na vurugu, baada ya kuwa raha na furaha (utamaushi).
Pia
badiliko jingine lilikuwa ni kwenye familia ya Mafuru ambapo tunaambiwa kuwa
Mzee Mafuru alioa mke mwingine baada ya kufiwa na mke wake. Mama huyu wa kambo
kwa Kazimoto, aliitwa Nzura, uk.136. Vilevile badiliko jingine lilikuwa ni Manase
kuamishwa kituo cha kazi. Lakini Kazimoto anazungumzia mke wake Manase
alivyojifungua mtoto na mtoto huyo alikuwa wa ajabu kidogo. Pia badiliko
jingine lilikuwa ni kwa Kamata aliyekuwa amehaguliwa kuwa mwanangwa wa kijiji
cha Saku. Baada ya miezi mitatu Kamata alijenga nyumba nzuri yenye bati, uk.137.
Katika
uk.138, msanii anatuonyesha tukio ambalo lilitokea. Tukio hilo lilikuwa linaongelea
namna ambavyo Kazimoto alikuwa akijiandaa kuanza kutangazwa kwa ndoa yake
kanisani. Malumbano yalitokea kati ya Kazimoto na Padri, pale ambapo padri
alikuwa akizozana na Kazimoto juu ya kutangaza ndoa yake kanisani ilionekana
kuwa padri aligoma kidogo kufanya hivyo kwani kuna hatua ambazo zilikuwa
zimekiukwa kabla ya kuanza kutangaza ndoa ya hao wapendanao. Pia tunaona ambavyo
Kabenga alidai mahari makubwa kuzidi uwezo wa familia ya mzee Mafuru. Jambo
ambalo lilileta kutoelewana baina ya Kabenga na Mafuru. Masimulizi yanaendelea
kuongelea juu ya mazungumzo ya Kazimoto na Sabina kuhusu watakavyofanya ndoa
yao, uk. 139-143.
Palipo
na mafanikio, hakika vikwazo haviepukiki. Ndivyo ilivyokuwa kwa uchumba wa
Kabenga na Sabina. Mtu mabaye hakujitambulisha alikuja na taarifa mbaya juu ya
Sabina lakini lengo lake likiwa ni kutaka kuvunja uchumba wao . . . nilipokaa na baada ya kumsalimu yule
mgeni, baba alisema, “Kazimoto, kuna jambo moja tu ambalo ninataka kufahamu. Na
ninataka uniambie ukweli kabisa. Uongo haufiki mbali nami. Ninataka uniambie
ukweli kabisa. Je, umekwisha kata shauri kabisa kumwoa Sabina?”
“Nisingekuwa nimekata shauri
nisingekuwa nimekusumbua namna hii. Kazi yote umekwisha fanya; ninawezaje
kubadili nia sasa?”
“Sitaki maelezo, wala sitaki
uniulize mimi. Niambie kama umekwisha kata shauri kabisa ama bado.” “Nimekwisha kata shauri.” Nilimjibu.
“Sijui utasemaje sasa. Kuna mgeni
hapa amekuja na siri kubwa.” Nilimtazama mgeni.
“Wewe ndiye Kazimoto?” aliuliza.
“Ndiye,” nilimjibu
“Wewe ndiye unataka kumuoa Sabina?”
“Ndiyo.”
“Uchumba wenu ulianza lini?” “Miaka
mitatu imepita sasa.”
“Unafahamu habari zozote kuhusu maisha yake huko Tabora?”
“Kidogo tu. Lakini habari kamili sina.”
‘Hufahamu?’ “Sifahamu sana.”
“Mimi Sabina ni jamaa yangu hasa na baba’ke
amekwisha fika nyumbani kwangu kuleta posa.” ‘Jina lako nani?’ nilimwuliza. Alinyamaza kwa muda mfupi halafu
aliniambia, “Fungameza”.
“Sabina ni nani kwako?” nilimwuliza
tena.
Ujamaa wenyewe ni wa mbali kidogo,
na sidhani kwamba unaweza kuelewa kwa urahisi hata kama nikikueleza. Ni jambo
la maana sana. Hili jambo ndilo limenifanya nije hapa wakati kama huu . . .
Fungameza anaendelea kueleza mambo mabaya na tabia mbaya ambazo anasema kuwa
Sabina alikuwa akizifanya kipindi yuko Tabora. Miongoni mwa tabia hizo ni
kwamba alishawahi kuolewa na jambazi ambaye alikuwa akimfungia ndani. Pia
anaeleza habari za ukoo wake, akisema kuwa babu yake Sabina alikufa kwa ukoma
na nyanya yake alikuwa mchawi. Vilevile anasema kuwa Sabina alitoa mimba mara
mbili akiwa huko Tabora . . . UK. 145-147.
Pamoja
na vizingiti alivyojaribu kuviweka bwana Fungameza, ila ndoa ilifanikiwa kufungwa
kati ya Kazimoto na Sabina: wapenzi waliopendana. Masimulizi yanaelezea vizuri
jinsi watu hao walivyofunga ndoa yao kuanzia ukurasa wa 149 hadi 151. Pia
tunaambiwa kuwa baada ya shughuli za sherehe kumalizika katika miji ya Mafuru
na Kabenga, siku tatu bibi harusi na bwana harusi, sasa walihamia kwenye makazi
yao wenyewe walipokuwa wanafanya kazi zao. Kuondoka kwao huko kuliambatana na
nasaha za mzee Kabenga kama mzazi wa wanandoa hao; hasa zaidi akiwaasa juu ya
maisha yao ya ndoa, uk. 151 – 152. Kazimoto anaeleza jinsi walivyofika kazini
kwao kama maharusi wapya na kupokelewa vizuri kwa shangwe na walimu wenzao. Kama ilivyo kawaida kwa Kazimoto, udhanaishi
ulimjia tena kichwani mwake na kuanza kujiuliza juu ndoa yao. Kazimoto anasema:
“Kweli sasa nimeoa! Sasa nimepata faida
gani?” Mbona mimi ni Kazimoto kama zamani. Sioni tofauti kati yangu na watu
wengine, isipokuwa kuambiwa ‘mkeo hajambo?’ kila asubuhi na popote niendako.
Mke wangu aniita ‘bwana’ngu’, kama kwamba yeye amenichukua. Nani sasa amechukua
mwingine? Tumechukuana. Ndiyo, tumechukuana lakini mimi bwana yeye bibi. Kuna
tofauti gani kati ya bwana na bibi?”. . . Uk,153.
Kila
lenye mwanzo huwa halikosi mwisho. Ndivyo inavyodhihirika katika uk, 154, pale
ambapo uadui uliokuwepo baina ya Kazimoto na Manase, pia kati ya familia ya
Mafuru na Kabenga mgogoro huu ulikuwa juu ya mashamba. Barua kutoka kwa Manase
inamfikia Kabenga ambayo lengo lake lilikuwa ni kushirikiana pamoja ili kuweza
kuboresha kipato cha familia zao na kuondoa uadui huo. Ifuatayo ni barua ya
Manase kwa Kazimoto;
“ Bwana Kazimoto,
Sikuweza kufika harusini kwa sababu ya matatizo fulani ya mke wangu
Salima ambaye, anaendelea kukonda kila siku. Sababu inayomfanya akonde hivyo
siijui. Tumejaribu dawa za hospitali lakini hazifai. Hakika ukimwona sasa
utamsahau. Mimi sijui nifanye nini ili nipate kumrudisha katika hali yake ya
zamani.
Nafikiri litakuwa jambo zuri kama
mtaweza kututembelea likizo ya Desemba. Labda nyinyi mtaweza kumtuliza. Jambo
la pili ni hili: nasikia baba’ko na baba’ngu siku hizi wana uhusiano mzuri
sana. Mji mmoja ukikosa mboga kwa siku moja
unakwenda kuchukua kwa jirani. Jirani akichinja ngo’mbe anapeleka mguu
mzima kwa mwenziwe. Zaidi ya hayo wanasaidiana sana wakiwa taabuni. Na ninasikia kwamba watoto wa kwenu wamezoea
kwetu vile kwamba mgeni akifika ni vigumu kutambua ni watoto
wa mji gani. Kwa hiyo ili kufanya mgogoro wa mashamba usahaulike kabisa
tunaweza kujaribu kuwafanya walime pamoja .
Mimi ninapeleka shilingi mia tatu, wewe pia ukiongeza kiasi hicho,
tunaweza kuwasaidia kulimisha shamba moja kubwa kwa trekta. Sina mengi.”
Haya
ni mawazo mazuri ya Manase yaliyokubaliwa na Kazimoto pamoja na mkewe Sabina
ili kuweza kumaliza kabisa mgogoro wa familia zao wa zamani. Matatizo mengine
yaliikumba nyumba ya Kazimoto, baada ya kazimoto kutoka shuleni akakuta mkewe
analia. Sababu ilikuwa ni kwamba alipokea barua ya mpenzi wa zamani wa Kazimoto
ambaye anaitwa Pili, uk,156. Pia Kazimoto alipokea barua fupi iliyotoka kwa Vumilia:
“Nasikia
kwamba umemwoa Sabina. Hayo yote kwangu ni sawa. Lakini siwezi kuficha kwamba
nikiwa naishi hapa duniani nitakuchukia daima. Sina mengi, isipokuwa
kuwatakieni heri na fanaka katika maisha yenu.”
Kazimoto
anasema hivi juu ya barua hii: “Barua
hiyo niliisoma mara mbili. Niliona kwamba labda chuki haitakwisha kamwe
ulimwenguni. Chuki itakanyagwa na mapenzi, lakini itajitokeza tena katika umbo
jingine”, uk, 158.
SURA Ya 11
Kama
ilivyo kawaida ya jamii nyingi duniani na hasa barani Afrika, mtoto ni tunu ya
kipekee kwenye familia. Basi pia hata kwa familia ya Kazimoto na ukoo mzima
ulikuwa na hamu kubwa ya kuona Sabina anapata mtoto. Hii tunaishuhudia ambapo
msimulizi wa riwaya hii anapogusia jambo hili mwanzoni mwa sura ya kumi na
moja, uk.159 – 160. Pia kama ilivyo nuizi ya riwaya hii suala kupoteza maisha
kwa watu halipuuziwi kuelezwa pale linapobidi na kujitokeza. “ Tulinyamaza kwa muda. Halafu Tunza akaanza
kunieleza juu ya watu ambao walikuwa wamekwisha kufa kijijini kwetu kwa muda wa
miezi mine iliyopita.
“Wazee wote karibu wamekwenda.
Ajabu ndiyo hiyo. Wazee wanafuatana, mmoja baada ya mwingine,” alisema.
Wanapasuka tu kama kuni.”
Baada
ya habari hizo za kifo kusimuliwa kwa Kazimoto, sasa mada iliyofuatia ni
Tegemea kueleza nia iliyomleta kwa Kazimoto haikuwa kumwangalia Sabina na
ujauzito, bali pia ni kumfuatilia mtoto wake Vumilia ambaye walipoteana na
alikoelekea hawakuagana. Tegemea anamwuliza Kazimoto habari za Tegemea kama alishawahi
kuzisikia kuwa yuko sehemu yo yote anayoifahamu. Kazimoto na Tegemea
wanajadiliana na kuamua kwenda kumtafuta Vumilia ambaye maisha yake yalikuwa ya
shida na taabu sana, miangaiko na mateso ya kila namana kama kwamba hakuwa na
mzazi. Kuanzia uk, 161 hadi 175, tunasimuliwa namna Kazimoto na Tegemea
walivyofuatilia na kufahamu anapoishi Vumilia ili mama yake aweze kumtoa kwenye
hadha za dunia alizokuwa anakumbana nazo. Mwisho tunaona watu hawa, wanafanikiwa
kumwona Vumilia lakini yeye anapinga kabisa kurudi kwa mama yake na kuamua
kuendelea kuishi na mme wake, Moyokonde. Vumilia hakika aliridhia kuishi maisha
ya taabu sana na mme wake baada ya kukataa kurudi nyumbani kwa mama yake. Hii
ni ishara ya kumpenda Moyokonde hata kwa hali aliyokuwa nayo pia na kukubaliana
na hali ya maisha yao. Ijapokuwa ilikuwa ni hali ngumu ambayo maisha ya wapendanao
wawili hawa: wanaishi. Moyokonde ni mchoma mkaa ambaye kipato chake ni kidogo
sana kulinganisha na mfumo wa gharama za maisha. Lakini pia haikuwa hali ngumu
ya maisha tu, bali Vumilia alishakumbwa na matatizo ya kuvamiwa na vijana
walitaka kumfanyia matendo ya ubakaji pamoja na kutaka kumuua, kama Moyokonde
anavyomsimulia Kazimoto, uk. 172. Pia kabla ya hapo, Vumilia alikuwa akitajwa
kuishi maisha ya shida sana; mfano, kufanya umalaya na kuangaika huko na huko,
akitafuta kazi na pengine kufanya kazi za udangulo na kuuza baa.
SURA YA 12
Katika
sura hii, ndipo tunapoona matatizo yanaikumba familia ya Kazimoto. Ni kipindi
kigumu ambacho matumaini na matarajio ya kupata mtoto waliyemtegemea yalipofika
mwisho, pale alipofariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa sababu ya kuwa
na kichwa kikubwa ambacho, kilisababisha mtoto huyo kufa. Kazimoto alipatwa na
butwaa hasa baada ya kufikishwa wodini
alipokuwa amelazwa mkewe, na kutaarifiwa ya kuwa mtoto wao amekatisha maisha
baada ya kuzaliwa muda mfupi kama tunavyoona uk, 179. Kazimoto alikuwa na
matumaini makubwa sana hasa kuhusu mtoto ila matumaini yake hayakuwa kama ilivyotarajiwa.
Kwani alikuwa amekwisha anza kutayarisha mambo ambayo baadae yangekuwa matumizi
katika malezi ya mtoto wao. Kazimoto aliona maisha hayana maana tena kwake, pia
aliamua kusema ya kuwa Mungu hayupo: basi kama yupo ni mkatili. uk,180.
SURA YA 13
Kwa
ufupi katika sura ya kumi na tatu, tunaona ya kuwa kutokana na matatizo
yaliyowakumba wakina Kazimoto na mkewe, sasa wanaamua kutuliza mawazo. Waliamua
kwenda kuwatembelea Manase na Salima hasa kipindi cha likizo ya mwezi Desemba.
Walifanya hivyo. Walipanda basi na kwenda kwa Manase. Walipofika huko walikuta
maisha kidogo yamebadilika tofauti na ilivyokuwa awali. Manase hakuwa na gari lake, lilikuwa tayari
limeharibika na kuchakaa. Mke wake Salima alikuwa amekonda kiasi kwamba ilikuwa
vigumu kidogo kwa mtu aliyemwona miezi kadhaa iliyopita asingeweza kumtambua
haraka. Walikaa kwa siku kadhaa na kuwajulia hali wenyeji wao kama ilivyokuwa
dhima ya likizo hiyo hasa kwao.
Katika
kuendelea kukaa nyumbani kwa Manase kama wageni waliowatembelea, ndugu zao:
siku moja wapo kwenye meza ya chakula wanaendelea na kuweka kitu tumboni pia na
mazungumzo; ghafla aliingia mtoto aliyekuwa na kichawa kikubwa sana. Alikuwa ni
mtoto wa familia ya Manase. Kazimoto alimshangaa na kushutuka huku akiuliza kwa
mshangao kuwa ni mtoto wa nani na kwa nini alikuwa hivyo. Jambo ambalo lilimkosesha
amani Salima na kugutuka akikimbilia chumbani kwao kwa kilio kikubwa na kumshutumu
Manase kwa kusababisha hatari hiyo. Manase alimjbu Kazimoto sababu ya mkewe
kuwa vile. Kwamba aliposema maneno yale juu ya yule mtoto alimtonesha kidonda
cha uchungu aliokuwa nao kuhusu mtoto huyo, kwani aliugua ugonjwa wa kichwa
ambao chanzo chake ni Manase kuuchota kwa Pili aliyekuwa mpenzi wake wa zamani.
Kazimoto pia alishutuka kwani tayari naye
alikuwa ameisha wahi kutembea na pili. Pia mtoto wao alizaliwa kwa shida kwa
sababu ya kuwa na kichawa kikubwa ambacho ndio ugonjwa huo. Baada ya Sabina kuyasikia
maneano ya Manase na kuvuta kumbukumbu ya kifo cha mtoto wake: na pia kukumbuka
barua ya Kazimoto aliyokuwa ameandikiwa na Pili, naye Sabina alianguka chini na
kuzimia ghafla, uk,191 - 193. Maisha yalikuwa magumu kwao. Amani ilitoweka
ndani ya nyumba kwa muda. Wanaume ndio waliokuwa chanzo cha upotevu wa amani
hiyo.
SURA YA 14.
Hii
ndio sura inayokamilisha kisa kinachozungumzwa katika riwaya hii. Ni sura ya
mwisho ambayo kama ilivyo nadharia na mwono uliotumika kuandika kitabu hiki:
mhusika mkuu Kazimoto anakata tamaa ya maisha hadi anafika hatua ya kujiua. Ndipo
Kazimoto anapolinganisha maisha ya mtoto anayejifunza kutembea na maisha ya
binadamu. Kazimoto anaona mtoto anajaribu kutembea halafu anashindwa na
kuanguka chini. Hali hii anafananisha na maisha ya mtu aliyefanya mambo mengi
duniani alafu baadae anashindwa kitu kidogo na matumaini yake yanaishia hapo
ama maisha ya mwanadamu na kifo chake, uk,194.
Baada
ya mawazo hayo, Kazimoto alihojiana na mkewe kama ifuatavyo:
“Mke wangu,” nilimwita.
“Bwana’ngu,”aliitikia.
“Sijui kwa nini ninaishi.”
“Nimechoka na maswali yako ya
kijinga.” Alisema.
“Huwezi kuishi kama watu wengine?
Wewe nani?”
“Mimi sijijui,” nilimwabia.
“Hakika sikufahamu kwamba wewe ni
kichwamaji namna hiii! Sikufahamu!”
Alilia, machozi yakamtoka. Kwa muda mfupi machozi yake yalikuwa mekundu.
Alikwenda kulala . . .”
Baada
ya hapo Kazimoto utamaushi ulikuwa tayari umemzidi nguvu, hadi anaamua kujiondoa
duniani, kama anavyonena; . . .nilikwenda
ndani ya chumba cha kulala. Sabina alikuwa amejifunika shuka akilia kwa kwikwi.
Nilichukua kitu fulani. Nilikuwa sifahamu jambo nililokuwa ninafanya, isipokuwa
nguvu Fulani zilizokuwa zikiniongoza – sauti! Sauti! . . . Sabina alipoamka,
ndugu zangu, kwa kusikia mlio wa bunduki, alimkuta mumewe amelala chini karibu
na meza, kichwa chake kikivuja damu, bastola pembeni. Alipotazama juu ya meza
aliona kijikaratasi kidogo kilichokuwa kimeandikwa manenao haya:
Nimejiua, siwezi kuendelea kuzaa kizazi kibaya. Pia sikuona tofauti kati
yangu na mdudu au mnyama. Akili! Akili! Akili ni nini? Pia nikiwa duniani sikuwahi
kupata kukutana hata siku moja na mtu anayeamini kwamba kuna Mungu. Watu anaogopa
kufa na kwenda motoni hao nimewaona, tena wengi sana. Mtu ye yote asilaumiwe
kwa kifo changu. Mimi kabla ya kufa ninaungama mbele ya ulimwengu kwamba nilimwua
ndugu yangu ingawa sikumgusa, uk,194 - 196. Huo ndio
ulikuwa mwisho wa maisha ya Kazimoto na mwisho wa riwaya hii.
Lakini
mwisho wa kitabu hiki kinamsifia mhusika kama jasiri na mkombozi wa maisha ya
Afrika. Na pengine kuona kuwa kifo sio suluhisho la matatizo katika maisha: na
hivyo mbinu sahihi ni kupambambana matatizo hayo kwa kutafuta mbinu sahihi za
kuyatatua, uk, 196.