UFAHAMU NA UFUPISHO

 UFAHAMU NA UFUPISHO

Maana ya ufahamu
Ufahamu ni neno linalotokana na neno kufahamu. Kufahamu ni kuwa na taarifa sahihi na za kutosha juu ya jambo au tukio fulani kiasi cha kuweza kumuelewesha mtu mwingine. Ni ile hali ya kujua na kuelewa jambo na kuweza kulifafanua au kutoa taarifa zinazohusiana na habari hiyo.
Umuhimu wa ufahamu
*    Ufahamu hutuwezesha kukuza uelewa wa mambo mbalimbali
*    Ufahamu hutusaidia kukuza uwezo wa kujenga hoja
*    Ufahamu husaidia kujieleza kwa ufupi na kwa ufasaha
*    Ufahamu hukuza uwezo wa kuchambua mambo
*    Ufahamu huchochea ari ya kujisomea kwa wanafunzi
Aina za ufahamu
Kuna ufahamu wa kusikiliza na wa kusoma. Aina ya ufahamu hutegemea njia aitumiayo mtu kupata taarifa.
1. Ufahamu wa kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni ule ambao mtu anapata taarifa kwa kusikiliza habari hiyo toka kwa mtu au kifaa kilichorekodiwa. Inawezekana kupata habari hiyo kwa kusimuliwa au kusomewa.
Ili kupata habari inayosikilizwa au kusomwa lazima msikilizaji azingatie mambo yafuatayo.
   *    kuwa makini kwa kile kinachosimuliwa au kusomwa
   *    kuhusisha mambo muhimu na habari inayosimuliwa
   *    kujua matamshi ya mzungumzaji
   *    kubainisha mawazo makuu
   *    kuelekeza mawazo kwenye kila kinachosikilizwa
   *    kumtazama usoni yule anayesimulia kama ni mtu
Kuna watu hawamudu kutamka matamshi sahihi ya Kiswahili hivyo huna budi kuzingatia matamshi kwa mfano: husema laha badala ya raha au feza badala ya fedha au ngombe badala ya ng’ombe. Ukigundua tatizo la matamshi alilonalo mzungumzaji wako itakuwa rahisi kuelewa anachosema.
2. Ufahamu wa kusoma
 Ufahamu wa kusoma ni uelewa unaopatikana kwa njia ya kusoma: Kwa mfano:
(i) kusoma kwa sauti
(ii) kusoma kwa haraka na kimya
(iii) kusoma kwa makini
Kusoma kwa sauti
Kusoma kwa sauti ni aina ya usomaji ambao humwezesha msomaji kupata ujumbe na kuweza kutamka kwa lafudhi ya Kiswahili sahihi.
Kusoma kwa sauti humfanya msomaji ajisikilize na kujipima juu ya uwezo wake wa kutamka maneno inavyotakiwa. Tena hupima kasi aliyonayo na uwezo wa kuelewa yale ayasomayo. Ni muhimu msomaji azingatie matamshi sahihi ya lugha, ilia pate maana sahihi ya maandishi yenyewe. Kwa mfano,mwandishi wa tungo hii “Alilima barabara ikapendeza sana” alikuwa na maana ya barabarayaani njia. Msomaji akisoma “Alilima barabara ikapendeza sana ” maana itakayopatikana sio njiakwa sababu mkazo umetiwa pasipostahili.
Msomaji hana budi kukwepa athari za lugha nyingine katika usomaji wa Kiswahili.
Kusoma kimya
Kusoma kimya ni njia ambayo msomaji anapitisha macho kwenye maandishi kwa haraka bila mazingatio ya kina. Lengo la usomaji huu ni kupata maana ya jumla bila mazingatio ya kina. Si ya undani. Kwa kusoma kimya msomaji anasoma haraka. Kwa mfano, usomaji wa aina hii hutumika kusoma magazeti au wakati mwingine usomaji wa aina hii hutumiwa sana na watu wenye mambo mengi ya kusoma na muda walionao ni mfupi.
Vilevile usomaji wa aina hii huwa wa muhimu kama msomaji atakuwa amepewa kazi zinazomlazimu asome maandishi mengi. Kwa mfano, msomaji anatakiwa  atoe taarifa maalumu ambayo haipatikani kikamilifu kwenye kitabu kimoja. Njia hii itamwezesha kusoma maandishi mengi kwa muda mfupi na kupata alichohitaji. Kwa sababu usomaji huu ni wa haraka,ufahamu wake ni wa juujuu.
Kusoma kwa makini
Huu ni usomaji wa kimya ambamo msomaji huvuta fikra zake zote kwa kile anachokisoma. Katika njia hii msomaji huzingatia maana ya kila neno,sentensi na aya kwa makini. Lengo la usomaji wa njia hii ni kupata uelewa kamili na wa ndani.
Usomaji huu huhitaji muda,utulivu katika mawazo na mazingira yanayomzunguka. Kwa mfano, mwanafunzi akipewa kazi ya kuchambua kitabu cha hadithi, atalazimika kusoma kimya na kwa makini ukurasa hadi ukurasa. Atachunguza yaliyomo katika sentensi hadi sentensi akichagua yale ya msingi anayohitaji. Wakati mwingine atachunguza pia maneno na jinsi yalivyotumika katika habari hiyo. Au labda msomaji ni mwandishi wa habari, atalazimika kusoma kwa makini habari kutoka kwenye magazeti mengine kisha atoe taarifa sahihi. Hali kadhalika likiwepo tangazo la kazi, usomaji wa aina hii ndio utakaohitajika. Kama habari ni fupi mtu huisoma zaidi ya mara moja. Ni vizuri msomaji akianza kusoma aendelee mwanzo mpaka mwisho.
Upimaji wa ufahamu
Ili kujua kwamba kilichosomwa kimeeleweka msomaji hupewa maswali. Akijibu kwa usahihi inaonesha ameelewa na akijibu vibaya ina maana hakuelewa.
Kubainisha mawazo makuu
Mwandishi au msimulizi akizungumza huwa ana ujumbe anaotaka uwafikie watu. Wakati mwingine hupanga ujumbe huo kwa namna nyepesi ili msomaji na msikilizaji wauone haraka. Mara nyingine huchanganya wazo zaidi ya moja kutoka aya moja lakini mawazo hayo yanakuwa yanahusiana. Ni wajibu wa msomaji au msikilizaji kutambua mawazo ya mwandishi au msimulizi.
      Zingatia mifano ifuatayo
(a) Wanafunzi wa shule yetu ni wakarimu na wachapa kazi hodari.
v Tungo hii ina mawazo mawili yaani ukarimu na uchapaji kazi
(b) Kila mtu ana lake, na tabu kuzidiana,
     Yakupasa ukumbuke, raha pia hupita,
     Na hilo lifahamike, kwa urefu na mapana,
     Na tabu huzidiana, kila mtu ana lake.
         (Uhuru, Januari, 31, 1992)
Wazo kuu katika ubeti huu wa shairi linaweza kufupishwa kwa sentensi moja tu. Tabu na raha hapa duniani huzidiana baina ya mtu na mtu.
Maana ya maneno na misemo
Katika habari ambayo mtu anapata katika kusikiliza au kusoma aghalabu kuna maneno magumu. Hivyo maana ya maneno itapatikana kulingana na matumizi (maana iliyokusudiwa). Kama msomaji ameshindwa kupata maana anashauriwa kutafuta maana katika kamusi ya Kiswahili.
Tazama mfano ufuatao:
Kwa muda mrefu mashirika mengi ya umma yamekuwa yakikabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha,wakati mwingine baadhi ya mashirika hayo yakiwa katika hatari ya kufilisika. Katika kujaribu kuyaokoa serikali mara nyingi imejaribu kuyapatia ruzuku au kuyaunganisha yale yenye shughuli zinazofanana.
Katika mtiririko huohuo wa kujaribu kuyapa uhai mashirika haya,serikali imeamua kuyapa uhuru zaidi,ambapo sasa yanaweza kupanga bei za huduma na bidhaa zao kwa lengo la kuyawezesha kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku.
Tunatazamia kwamba mashirika yote yatatumia vizuri fursa hii ili kujiimarisha kiuchumi. Ni kwa kuzingatia ufanisi na kuepuka ubadhirifu na wizi wa mali na fedha ndipo vyombo hivi vitaweza kujikwamua kweli kweli……
(Maoni yetu, Uhuru, 1992)
Baadhi ya maneno magumu katika habari hiyo ni: kufilisika, ruzuku, uhai, huduma, bidhaa, ufanisi, ubadhirifu na kujikwamua.
Maana za maneno hayo:
kufilisika: ni ile hali ya mashirika ya umma kushindwa kuzalisha mali kiasi
                   kwamba matumizi ya uzalishaji kuzidi mapato.
ruzuku:     fedha zitolewazo na serikali kusaidia mashirika ya umma
uhai:           misaada hasa ya kifedha itolewayo na serikali kuu kwa mashirika
                    kuondokana na tatizo la kufilisika
huduma:     gharama zitolewazo kama vile za maji, umeme,elimu n.k
bidhaa:        mali zizalishwazo viwandani kama vile viatu, nguo, biskuti n.k
ufanisi:         hali ya utendaji wa kazi kwa ubora/umaridadi zaidi
ubadhirifu:  utumiaji mbaya wa mali ya shirika, srikali,kampuni n.k
kujikwamua: kuondokana na matatizo,kutotegemea misaada toka serikalini.
KUFUPISHA HABARI
Kufupisha habari ni kuandika muhtasari wa habari iliyosomwa kwa kutumia maneno ya anayefupisha habari hiyo kulingana na mawazo aliyoyabaini. Zoezi la kubaini mawazo makuu katika kifungu cha habari, humwongoza msomaji katika uandaaji wa ufupisho wa habari aliyosoma. Ufupisho hukamilika msomaji aunganishapo mawazo yake mwenyewe. Habari yenyewe huwa na maana sawa na ile ya awali ila msomaji hutumia maneno yake mwenyewe isipokuwa dhana ibaki ileile.
Hatua za kufuata katika ufupisho
(i) Soma habari yote mpaka uielewe
(ii) Chagua taarifa na maneno maalumu
(iii) Linganisha taarifa muhimu na habari ya asili
(iv) Andika muhtasari kama inavyotakiwa
(v) Linganisha usawa wa ufupisho na habari ya asili.
Mara nyingi habari iliyofupishwa huwa ni theluthi moja (1/3) ya habari ya awali.
Ili kupata idadi ya maneno katika ufupisho; hesabu idadi ya maneno kwenye mstari wowote uliokamilika kisha zidisha kwa idadi ya mistari. (Idadi yaweza kuzidi au kupungua kwa maneno yasiyozidi 10).
Matumizi ya ufupisho
(i) Hutumika wakati wa kutayarisha ripoti na kumbukumbu za mikutano.
(ii) Husaidia wakati wa kudondoa hoja kutokana na mihadhara au hotuba
(iii) Hutumika katika kuandaa shajara au kumkumbu za kila siku
(iv) Husaidia katika uhariri wa habari
(v) Husaidia kuokoa gharama hasa katika uandishi wa simu ya maandishi
 Angalia mifano ifuatayo:
(a) Shirika la Afya la Muhimbili (MMC) linadaiwa kuwa lilinunua dawa yenye
     thamani ya shilingi 1,128,980 kwa  bei ya shilingi 13,385,000 kutoka kwa
     kampuni moja mjini Dar es Salaam.
Sentensi iliyofupishwa: Shirika la Muhimbili limeibiwa shilingi 12,256,020.
(b) “……ukisikia katoka basi yuko naye, saa nyingine hushinda naye kutwa. Hata
      akisafiri hamwachi na haya si ya leo hata kabla yako wewe…..”
Sentensi iliyofupishwa: Walipendana kama pete na kidole na hiyo hawakuanza leo.
(c)  Shabiki mwenye subira, kutokeza nimeona,
     Nieleze wenye papara, wasiwazuie wana,
     Kukipanua kwa sura, Kiswahili kikaona,
     Lugha hai ninanena, hukua kila mara.
       (Uhuru, Agosti 7, 1991)
Ubeti huu wa ushairi unaweza kufupishwa kwa wazo moja kuu kama ifuatavyo:
Wazee  wasiwazuie vijana kukuza lugha.
Soma shairi lifuatalo kisha jibu maswali yanayofuata:
1.  Tofauti kubwa sana, kama tukisema haki,
     Kidogo nitayanena, yote hayakamiliki,
     Kwanza neno la maana, kuwa kwa kipindi hiki,
     Nini tofauti yake, zamani na siku hizi?
2. Tofauti nakwambia, tazama pale kisaki,
    Bati nakukatalia, nyumba nane hazifiki,
    Na sasa zimeenea, bati tupu za malaki,
    Hiyo tofauti yake, zamani na siku hizi.
 3. Wewe kwa mawazo yako, nchi haibadiliki,
     Kwanza nenda Kariakoo, pamejengwa handaki,
     Na shilingi tano zako, hupati lau mshikaki,
     Kuna tofauti gani, zamani na siku hizi?
4.  Bwana wewe nakwambia, kunisikia hutaki,
     Zamani najipatia, shilingi moja kaniki,
     Sasa nakukatalia, elfu hupati kaki,
     Kuna tofauti gani, zamani na siku hizi?
5.  Sasa nenda Kinondoni, pitia na Khariri,
     Kulikuwa maporini, na wala hakupitiki,
     Zama hizo Magomeni, wala hapatamaniki,
     Hiyo ndiyo tofauti, zamani na siku hizi.
6.  Nisemeje tofauti, hata wewe usadiki,
     Nyumba zote za makuti, hilo halikataliki,
     Zamani haya mashati, tulishona ya makaki,
     Kuna tofauti gani, zamani na siku hizi?
 
7.  Zamani Elizabeti, utawala wa mikiki,
     Kulikuwa masharti, utake au hutaki,
     Sasa ikaja bahati, ndugu yetu Mzanaki,
     Bwana tofauti nyingi, zamani na siku hizi.
8.  Ingali bahati yetu, na wala haifutiki,
     Mwingi ni Raisi wetu, yeye fitina hataki,
    Serikali hapa kwetu, yatupendeza kwa haki,
    Je, kwa watangazaji, kuna tofauti gani?
9.  Vipindi walivipanga, vya zamani sio haki,
     Watunzi waliwatenga, hawakufanyiwa haki,
     Sasa twaita malenga, jina zuri si la chuki,
     Kumbe kuna tofauti, ya sasa ni nzuri sana.
10. Basi hapa mwisho wangu, mengine naweka baki,
      Siri una Mbwiga wangu, maliza yaliyobaki,
      Naogopa walimwengu, wasije wakahamaki,
      Basi hiyo ndugu zangu, ndiyo tofauti yake.
         (Uhuru, Januari, 30, 1992)
Maswali
(a) Andika kichwa cha shairi hili kwa maneno yasiyozidi matano (5)
(b) Eleza wazo kuu linalotolewa na kila ubeti
(c) Kwa maneno yasiyozidi hamsini (50) toa maoni yako kwa
      kulinganisha maisha ya zamani na ya sasa.

(d) Andika ufupisho wa shairi hilo kwa maneno kati ya 100-150
Powered by Blogger.