JIFUNZE LUGHA YA KISWAHIL

 
MAANA YA FASIHI NA UCHAMBUZI WA VIPERA VYAKE


Williady, (2015) Fasihi ni tawi moja wapo la sanaa linalotumia lugha katika kuwasilisha ujumbe wa mdomo au wa maandishi.
Wamitila (2004) Fasihi ni sanaa inayotumia luha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja na maisha yake na huathri, hugusa au huacha athari fulanina hupatikana katika umbo ambalo linatambuliwa na jamii Fulani.
Kwakuwa fasihi ni aina ya sanaa, ni vyema mwanafunzi akajua pia maana ya sanaa.
                                                            MAANA YA SANAA
(Williady: 2015) Sanaa ni ujuzi au ufundi wenye kuleta manufaa kwa uma.
                                                            UMBO LA SANAA
Tunaposema umbo la sanaa tunamaanisha matawi yanayojenga sanaa. Matawi hayo nipamoja na;
Fasihi, maonyesho, ususi, uhunzi, ufumaji, utarizi, uchongaji, ufinyanzi, uchoraji na muziki. 
         
      
                                           AINA/ KUMBO/ TANZU ZA FASIHI
Katika kumbo ya fasihi na taaluma zake kuna aina kuu mbili za fasihi, ambazo ni;
  Fasihi Simulizi 
Fasihi Andishi
                              TOFAUTI KATI YA FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI
                  Namna ya uwasilishaji wake. Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia yam domo wakati fasihi andishi uwasilishwa kwa njia ya maandishi.
                  Mabadiliko. Fasihi simulizi huweza kupokea mabadiliko ya papo kwa papo wakati fasihi andishi hurekebishwa baada ya toleo jipya.
                  Utendaji wake kwa hadhira na fanani. Hadhira na fanani katika fasihi simulizi huwa ni yakiutendaji, wasikilizaji wanaweza kuchangia mawazo kwa    kutoa maoni, kuuliza maswali au kushadadia masimulizi ya fanani. Fasihi andishi  hadhira hawawezi kuchangia lolote.
                   Ukongwe. Fasihi simulizi niyazamani zaidi, ilianza wakati mwanadamu alipoanza kutumia mdomo katika mawasiliano. Fasihi andishi ilianza pindi maandishi yalipobuniwa.
                  Vidato na elimu. Fasihi simulizi haiitaji mtu ajue kusoma ama kuandika, inamuhitaji mtu mwenye uwezo wa kuzungumza. Fasihi andishi inamhitaji   mtu anayejua kuandika na kusoma.
                    Umiliki. Fasihi simulizi inamilikiwa na jamii nzima wakati fasihi andishi humilikiwa na mwandishi aliyeandika na kupiga chapa kazi hiyo.
                     Idadi ya tanzu. Fasihi simulizi inatanzu nyingi zaidi kuliko fasihi andishi.
                    Kuhifadhi. Hapo kale fasihi simulizi ilihifadhiwa kichwani, kwa sasa fasihi simulizi yaweza kuhifadhiwa katika vinasa sauti, kaseti na santuri. Fasihi  andishi yenyewe huifadhi wake ni kwa njia ya maandishi.
                   Mwingiliano wa tanzu kwa kiasi. Fasihi simulizi huweza kuingiliwa kwa kiasi kikubwa na tanzu nzingine kama vile methali, vitendawili, nyimbo na  nahau wakati fasihi andishi huweza kuingiliwa na tanzu nyingine kwa kiasi kidogo.
                                                 UFAFANUZI WA AINA ZA FASIHI
                                                                    1.Fasihi simulizi
Fasihi simulizi ni aina ya fasihi inayotumia mdomo na utendaji wa viungo vya mwili katika kuwasilisha maudhui ya fanani kwa hadhira iliyokusudiwa.
                                                       TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
                                                       Hadithi, uigizaji, ushairi na semi
                   
                                                            VIPERA VYA HADIDHI
      Ngano, vigano, hekaya, soga, tarihi, visa, visasili, shajara, istiala, michapo na mbazi
                                                             VIPERA VYA UIGIZAJI
      Miviga, michezo ya jukwaani, majigambo, utani, vichekesho, ngonjera, mgomezi na  
      mazungumzo
    
                                                              VIPERA VYA USHAIRI
       Nyimbo, maghani, ngonjera, mashairi, tenzi na tendi
     
                                                                 AINA ZA NYIMBO
      Bembezi, nyimbo za mapenzi, nyiso, nyimbo za jadi, nyimbo za harusi, nyimbo za watoto
      nyimbo za sifa, nyimbo za kampeni, nyimbo za maombolezo na nyimbo za chombezi.
   
                                                                VIPERA VYA SEMI
       Methali, misimu, lakabu, nahau, vitendawili. utani, misimu, mafumbo, masaguo, mizungu na 
       misemo

                             MAJUKUMU / DHIMA ZA FASIHI SIMULIZI KATIKA JAMII
       Kuelimisha, kuburudisha, kusisimua, ukombozi, kutoa mwongozo kwa jamii, kutunza amali 
       za jamii (historia na utamaduni), kujuza na kuunganisha vizazi nz vizazi, kufundisha,    
       kudumisha uhusiano, kudumisha ushirikiano na kukuza stadi za lugha
              
                     MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA USIMULIZI WA HADITHI
Ili msimuliaji aweze kutongoa au kusimulia hadithi kwa usahihi inampasa awe na weledi wa kutosha juu ya mbinu za kusimulia hadithi. Mbinu hozo ni hizi;
                                               A)      Dhima na maudhui
Msimuliaji wa hadithi anapaswa kujua lengo kuu (dhima) la hadithi yake. Vilevile msimuliaji anapaswa kujua maudhui ambayo ni jumla ya mambo yote yanayopelekea hadithi kutiririka vizuri kwenye mkondo wake.
                                                 B)      Msuko
Msuko wa matukio kwa jina jingine unafahamika kama muundo. Kipengele hiki cha muundo kinahusu mpangilio wa hadithi kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
                                                C)      Kusisimua
Kusisimua ni mbinu inayovuta umakini kwa watu. Msimuliaji anaweza kutumia mbinu kadhaa zitakazo msisimusha msomaji, mbinu kama vile taharuki, miguno na kelele za kutisha.
                                               D)      Urudufishaji
Huu ni urudiaji rudiaji katika fasihi simulizi. Mara nyingi msimuliaji anashauriwa kurudia rudia maneno, falsafa, nahau au vitendawili vilivyobeba lengo kuu la hadithi yake.
                                              E)      Chombezo
Chombezo ni kipengele kidogo kinacho elezwa na mtambaji wa hadithi chenye lengo la kupunguza ukakasi ama ukalia ama vitisho vilivyotokana na maudhui ya hadithi Fulani.
                                              F)      Nyimbo
Nyimbo zina kazi nyingi katika masimulizi ya hadithi. Moja wapo ya matumizi hayo ni kama vile kuondoa uchovu kwa wasikilizaji, kuvuta usikivu, kuwakaririsha hadhira falsafa au lengo kuu la hadithi hiyo.
                                                        MAMBO MENGINE
                                                       a)  Utulivu kwa hadhira
                                                       b)  Ujenzi wa wahusika
                                                       c)  Matumizi ya tamathali za semi
                                                       d)  Ujenzi wa taswira
  
                                                         2. FASIHI ANDISHI
Williady (2015) fasihi andishi ni aina ya fasihi inayowasilishwa kwa ustadi wa maandishi yenye kuleta maana.
Wamitila (2004) fasihi andishi ni sanaa inayowasilishwa kwetu kwa maandishi. 
                                                 TANZU ZA FASIHI ANDISHI 
                                                      RIWAYA (NATHARI)
                                                      USHAIRI (NUDHUMU)
                                                      TAMTHILIYA (SANAA ZA MAONYESHO)
                                                FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI 
Fani na maudhui katika fasihi ndio maumbo mawili makuu yanayobeba sanaa hii. 
                                                                         FANI
Fani ni ufundi unaotumiwa na msanii katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa, fani sio ujumbe bali ni mfano wa kipaza sauti kinachotumika kufikisha ujumbe.
                                                            VIPENGELE VYA FANI
Fani inavipengele vingi, kila kipengele kina husika kipekee kwa kutofautiana na kipengele kingine. 
                                                       Vipengele vya fani ni pamoja na;
                                                                     a)   Muundo
 Kipengele hiki hutumiwa kueleza mpangilio wa kazi ya kifasihi. Kwa ufupi kwenye kipengele cha muundo tunaangalia umbo la kazi ya fasihi, mfano kazi yaweza kugawanywa katika sura mbalimbali, sura hizi ndizo ujenga muundo.
                                                                     b)  Mtindo
Williady (2015) mtindo ni mbinu za kipekee zinazomtofautisha msanii mmoja na mwingine. Mfano katika fasihi simulizi kipengele cha nyimbo hadhira inaweza kusikia wimbo kwa mara ya kwanza na kutambua wimbo huo umeimbwa na nani bila ya kuambiwa na mtangazaji, hii huweza kutokea pindi mwimbaji mashuhuri anayetumia mtindo wa peke yake katika sauti na mpangilio wa mashairi anapotoa wimbo mpya. Huu ndio huitwa mtindo. Katika fasihi andishi mtindo unaweza kujitokeza kwa njia za kipekee za mtunzi katika matumizi ya lugha, methali na misemo, msuko na mpangilio wa vina na mizani katika ushairi.
                                                                   c)   Mandhari
Williady (2015) Mandhari ni eneo au mazingira ya kweli au yakubuni ambayo hutumiwa na mwandishi katika kuwajenga wahusika na uhusika wao. 
                                                                    d)  Matumizi ya Lugha
Williady (2015) Matumizi ya lugha ni ustadi wa msanii katika kutumia lugha itakayoleta mvuto kwa wasomaji au wasikilizaji wa kazi ya fasihi.
Katika kutumia lugha msanii lazima azingatie kipengele cha uteuzi wa maneno yanayoendana na hadhira yake, maneno hayo ndiyo yatakayoleta mfungamanisho katika ya msanii, hadhira na ujumbe uliokusudiwa.
                                                                   e)   Matumizi ya tamathali za semi(usemi)
Williady (2015) Tamathali maanayake ni neon moja au kifungu cha maneno kilicho sukwasukwa na kufichwa maana.
Baadhi ya tamathali za semi katika Kiswahili ni pamoja na;
Tashibiha, sitiari, tafsida, tashihisi, chuku, kinaya,dhihaka, mbalagha,tabaini
                                                                    f)    Mbinu nyingine za kisanaa
Hapa huwa na mchanganyiko wa mbinu kadhaa katika usimulizi na silazima mbinu hizo zitumike zote kwa wakati mmoja. Mfano wa mbinu hizo ni pamoja na;

 Takriri, kuchanganya ndimi, tanakali sauti, taswira, lakabu, nahau na misemo
       
                                                                  e)   Wahusika
Williady (2015) wahusika ni viumbe hai au viumbe ambao si hai wanaobebeshwa majukumu na msanii ili kuwafikishia hadhira ujumbe uliokusudiwa.
                                                     MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI
(williady: 2015) Maudhui ni jumla ya mawazo anayoyazungumzia msanii au mtunzi katika kazi ya fasihi.
Maudhui hujumuisha vipengele mbalimbali, kama vile;Dhamira, ujumbe, falsafa, mafunzo, migogoro na mtazamo.
TANBIHI: Kuna baadhi ya wataalamu wa lugha wanakiweka kipengele cha migogoro upande wa fani na kunabaadhi wanakiweka kipengele hiki upande wa maudhui. Mimi nakiweka upande wa maudhui kwa kuwa migogoro inabeba kwa kiasi kikubwa ujumbe kuliko ufundi.
                                                                      DHAMIRA
Dhamira ni shabaha kuu ya mtunzi wa kazi ya fasihi. Shabaha hii ukusudiwa ni nani wakumlenga nayo. Msanii anaweza kuwalenga kimaudhui watoto, wanawake, wasomi au watu wote katika jamii. Shabaha hii yaweza kuandikwa au kutongolewa kwa mdomo ikiwa na lengo la kupongeza, kuhimiza, kushauri, kutoa taarifa na kukosoa.
                                                                       UJUMBE
Ujumbe ni mawazo yanayotokana na dhamira, mawazo haya yaweza kujitokeza waziwazi au kwa kificho.
                                                                       FALSAFA
Falsafa ni hekima hekima ya mtunzi. Mtunzi huamini kuwa  kupitia imani hii jamii inaweza kupata suluhisho la matatizo yanayowakabili. Kwa mfano shekhe Shaaban Robert aliamini kuwa kila mwanajamii akiwa na utu basi haki na upendo vitapatikana kirahisi.
                                                                       MAFUNZO
Mafunzo ni nasaha anazotoa mtunzi ambazo huifundisha hadhira maadili Fulani. Maana ya mafunzo hutegemea namna hadhira inavyofasili nasaha hizo.
                                                                       MIGOGORO
Migogoro ni misuguano au mikinzano ama kutoelewana kati ya pande mbili au zaidi ndani ya kazi za fasihi.
                                                              AINA ZA MIGOGORO
                                                               Mgogoro kati ya mtu na mtu
                                                              Mgogoro kati ya mtu na jamii
                                                              Mgogoro kati ya jamii na jamii 
                                                              Mgogoro wa nafsi
 
                                                                      VI. MTAZAMO
Mtazamo na jinsi mwandisi anavyotazama na kuyachukulia matukio katika ulimwengu na athari zake kwa wanajamii. Mfano waandishi wengi wa mashairi wanamtazamoa huu “Kuibuka kwa maovu mengi duniani kwasasa  ni matokeo ya binadamu kuasi dini.
Tafadhali wasiliana na mwl. Majumbeni kwa,
               
     
                   hwilliady@ymail.com
                  majumbeni@gmail.com 


UCHAMBUZI WA VIPERA VYA FASIHI SIMULIZI KWA MUJIBU WA M. M.MULOKOZI

Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za FasihiSimulizi.

Kwa upande wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987).


Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.

Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.

Fasihisi Simulizi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni M.M.Mulokozi (1996) anasema Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. 

Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.
 
Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila(2003).

Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)

M.M.Mulokozi katika makala yake ya tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba 21(1989) amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.

Umbile na tabia ya kazi inayohusika: katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari, kimafumbo, kiwimbo na kighani), muundo wa fani hiyo na wahusika.

Kwa upande wa muktadha na namna ya uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi ni tukio hivyo huambatana na muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).

Kwa hiyo kwa kutumia vigezo hivi, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kama ifuatavyo;

1. Masimulizi

Hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari.

2. Muundo

Mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio.

3.Wahusika

Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji.

Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.

Masimulizi yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano. 
Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha.  Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.

Istiara. Hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Mbazi; hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima.

Kisa; hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.

Utanzu mwingine wa masimulizi ni utanzu wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.

Visakale; haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.

Mapisi; haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli.

Tarihi; haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.

Kumbukumbu; haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.

Visasili; hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa Semi
Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambacho ni kufunza.

Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.

Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha muundo ambapo methali huundwa na muundo wa pande mbili ambazo hutegemeana.

Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. 
Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo.

Misimu; ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Hivyo vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha yaani hutokea wakati maalum na mazingira maalum.

Mafumbo; ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Lakabu; haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha kificho yaani maana yake hufichwa.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi
Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.

Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;

Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. 
Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.

Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.

Bembea;
hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.

Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.

Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.

Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.

Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.

Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.

Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza.

Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.

Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini nakadhalika.

Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.

Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.

Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.

Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.

Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.
              
Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.

Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.

Sifo;
hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.

Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.

Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
 
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.
Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.

Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.

Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.

Sifo, hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.

Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo
Mazungumzo ni maongozi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia.

Utanzu huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.

Hotuba;
haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.

Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.

Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.

Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo
.
Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.

Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo
Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi
Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.

Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-

Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.

Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo.

Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo.
 
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.
      
MAREJEO:

Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi: Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.

TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).
 
                                                           METHALI ZA KISWAHILI
                                           ZIMEKUSANYWA NA MWL. MAJUMBENI
Methali ni nyenzo ya msingi katika makuzi ya fasihi ya Kiswahili. Tangu kale Methali zimetumika katika kujenda jamii kwa kutoa maonyo na kuambukika tabia njema hasa kwa vijana wanaochipukia.
Wataalamu wengi wameeleza maana ya Methali, lakini maana halisi bado inaendelea kushabihiana japokuwa kuna mikinzano katika baadhi ya maeneo. Maana halisi ya methali itabaki kuwa,
 “Methali ni kipera cha semi katika fasihi simulizi kinachojengwa kwa pande mbili, pande moja ni yenye kuuliza swali na nyingine yenye kujibu swali zikiwa na lengo la kufunza amali za jamii kwa vijana.
Mwl. Majumbeni amekusanya methali nyingi katika lugha ya Kiswahili, baadhi ya methali ameziweka humu kwenye blogi yake kwa lengo la kutoa mchango wake katika ukuzaji na uendeshaji wa shughuli zote zinazohusu lugha ya Kiswahili.
Zifuatavyo ni baadhi ya METHALI , zikiwa vimepangwa ki - alfabeti:
                         “A”
1.       Adhabu ya kaburi aijua maiti
2.       Adui mpende
3.       Aibu ya maiti aijua mwosha
4.       Aisifuye mvua imemnyea
5.       Ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke
6.       Achambaye na gunzi hatakatiki
7.       Akimbiaye mvua, akimbia shibe
8.       Akiba haiozi
9.      Akili ni mali
10.    Akili ni nywele kila mtu ana zake
11.    Akili nyingi huondoa maharifa
12.    Akipenda chongo, huita kengeza
13.    Akumulikaye mchana, usiku akuchoma
14.    Akutendaye mtende mche asiyekutenda
15.    Anaekula kibudu, ashibisha tumbo wala si nafsi
16.    Alalaye usimwamshe, ukimwamsha utalala wewe
17.    Alisifiye jua, limemwangaza
18.    Aliye kando haangukiwa na mti.
19.    Aliyekupa wewe kiti, ndiye aliyenipa mimi kumbi
20.    Aliyetota, hajui kutota
21.    Amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga
22.    Amnyimaye punda adesi, kampunguzia mashuzi
23.    Ana hasira za mkizi
24.    Anayekataa wengi ni mchawi
25.    Amtukanaye jumbe hafikwi na kesi
26.   Anayekuja pasi na hodi, huondoka pasi na kuaga
27.   Anayeonja asali, huchonga mzinga
28.   Anayetaka hachoki hata akichoka keshapata
29.   Angakaanga, tu chini agae
30.   Angenda juu kipanga, hafiki mbinguni
31.   Angurumapo simba, mcheza nani?
32.   Aninyimaye mbaazi, kanifunguzia mashuzi
33.   Atupaye kopo la choo, hafikwi na haja
34.   Apewaye ndie aongezwaye
35.   Asiye bahati habahatiki / habahatishi
36.   Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu
37.   Asiyejua jua maana, haambiwi maana
38.   Asiyekujua hakudhamini
39.   Asiyekubalikushindwa si mshindani
40.   Asiyekuwapo machoni, na moyoni hayupo
41.   Asiyekuwapo na lake halipo
42.   Asiye na mengi, ana machache
43.   Asiye na meno, hapewi nyama ya kiuno
44.   Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu
45.   Asiyeuliza, hanalo ajifunzalo
46.   Atangaye sana na jua, hujua
47.   Atangazaye mirimo si mwana wa ruwari
48.   Auguwaye, huangaliwa
49.   Avuaye nguo, huchutama
50.   Avumaye bahariki papa (kumbe wengine wapo)
              “B”
51.   Baada ya dhiki, faraja
52.   Baada ya kisa, mkasa
53.   Baada ya chanzo, kitendo
54.   Baba wa kambo si baba
55.   Bandu! Bandu! Huisha gogo
56.   Baniani mbaya, kiatu chake dawa
57.   Bendera hufuata upepo
58.   Bembea umpa raha apendae
59.   Bilisi wa mtu ni mtu
60.   Bura yangu sibadili na rehani
         “C”
61.   Cha mlevi huliwa na mgema
62.   Chanda chema huvikwa pete
63.   Chema chajiuza, kibaya chajitembeza
64.   Chombo cha kuzama hakina usukani
65.   Chombo kilichopikiwa samaki, hakiachi kunuka vumba
66.   Chovya – chovya! Yamaliza buyu la asali
67.   Chururu si ndo!ndo !ndo
68.   Dalili ya mvua ni mawingu
69.   Damu nzito kuliko maji
70.   Dau la mnyonge halendi joshi
71.   Dawa ya moto ni moto
72.   Debe tupu haliachi kuvunda
73.   Dua la kuku halimpati mwewe
74.   Dua mbaya haombolezewi mtoto
          “E”
75.   Elimu ni bahari
76.   Ellimu ni ufunguo, haina mwisho
77.   Elimu ya mjinga ni majungu 
       “F”
78.   Fadhili za punda, mashuzi, na msihadhari ni ng’ombe
79.   Fimbo iliyo mkononi, ndiyo iuayo nyoka
80.   Fimbo ya mbali, haiui nyoka
81.   Fuata nyuki, ule asali
82.Fumbo mfumbie mjinga, mwerevu hulingamua
83.   Fungato haliumizi kuni
84.   Funika kombe mwanaharamu apite
             “G”
85.   Ganda la mua la jana, chungu kaona kivuno
86.   Gonga gogo usikilize mlio wake
87.   Gonga! Gonga! utoka cheche
            “H”
88.   Haba na haba hujaza kibaba
89.   Halla! Halla! Mti na macho
90.   Hamadi, kibindoni, silaha, iliyo mkononi
91.   Hamna! Hamna! Ndimo mlimo
92.   Hapana marefu yasiyo na ncha
93.   Hapana masika yasiyo na mbu
94.   Hapana msiba usiokuwa na mwenziwe
95.   Hapana siri ya watu wawili
96.   Hapana ziada mbovu
97.   Haraka haraka haina Baraka
98.   Hasara humfika mwenye mabezo
99.   Hasira, hasara
100.                        Hauchi – hauchi unakucha
101.                        Hayawi! Hayawi! Huwa
102.                        Heri  kufa macho kuliko kufa moyo
103.                        Heri kufa mwili kuliko kufa roho
104.                       Heri kujikwaa dole, kuliko kujikwaa ulimi
105.                        Heri nusu ya shari kuliko shari kamili
106.                        Hewalla! Haigombi
107.                        Hiari yashinda utumwa
108.                        Hucheka kovu, asiyefikiwa na jeraha
109.                        Hakunyimae tonge, hakunyimi neon
  
                              “I”                      
110.                        Ihsani haiozi
111.                        Ikiwa hujui kufa, tazama kaburi
112.                        Iliyopita si ndwele, ganga ijayo
113.                        Ivushayo ni mbovu
114.                       Ivumayo haidumu ikidumu inamkono wa mtu
115.                        Iwapo nia, njia hupatikana
                          “J”
116.                        Jicho moja halizuii kutazama uchi
117.                        Jifya moja haliinjiki chungu
118.                        Jina jema hung’aa gizani
119.                        Jino la pembe si dawa yap ego
120.                        Jitihada haiondoi kudura
121.                        Jongoo hulia “uta wangu u kule”
122.                        Jogoo la shamba haliwiki mjini
123.                        Joka la mdimu linalinda watundao
124.                        Jungu bovu limekuwa magae
125.                        Jungu kuu halikosi ukoko
                       “K”
126.                        Kafiri akufaaye si Islamu asiyekufaa
127.                        Kamba hukatikia pembamba
128.                        Kanga moja, haistiri maungo
129.                        Kanga iliyotota, Uganda maungo
130.                        Kanga hazai ugenini
131.                        Kata pua, unga wajihi
132.                        Kawaida ni kama sheria
133.                        Kawia ufike
134.                        Kazi mbaya si mchezo mwema
135.                        Kelele za mlango haziniwasi usingizi
136.                        Kenda karibu na kumi
137.                        Kiburi si maungwana
138.                        Kichango, huchangizana
139.                        Kidole kimoja hakivunji chawa
140.                        Kiingiacho mjini si haramu
141.                        Kikulacho ki nguoni mwako
142.                        Kila chombo kwa wimbile
143.                        Kila mlango kwa ufunguo wake
144.                        Kila mtoto na koja lake
145.                        Kila mwamba ngoma, ngozi huivuta kwake
146.                        Kila ndege huruka kwa bawa lake
147.                        Kilio huanza mfiwa, ndipo na wa mbali wakaingia
148.                        Kimya kingi kina mshindo
149.                        Kinga na kinga ndipo moto uwaka
150.                        Kinyozi hajinyoi na akijinyoa hujikata
151.                        Kinywa ni jumba la maneno
152.                        Kipendacho roho hula nyama mbichi
153.                        Kipendacho moyo ni dawa
154.                        Kipya kinyemi, ingawa kidonda
155.                        Kisebusebu na kiroho papo
156.                        Kisokula mlimwengu, sera nale
157.                        Kitanda usichokilala, hujui kunguni wake
158.                        Kivuli cha fimbo hakimfichi mtu jua
159.                       Kivuli cha mvumo huwafunika walio mbali
160.                       Kiwi cha Yule, ni chema cha Yule, hata ulimwengu wishe
161.                        Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza
162.                        Koko haidari mai
163.                        Konzi ya maji haifumbatiki
164.                        Kosa moja haliachi mke
165.                        Kozi mwana mandanda, kulala na njaa kupenda
166.                        Kuagiza, kufyekeza
167.                        Kuambiana kupo, kusikilizana hapana
168.                        Kucha Mungu si kilemba cheupe
169.                        Kuchamba kwingi kuondoka na mavi
170.                        Kufa kikondoo, ndiko kufa kiungwana
171.                        Kufa, kufaana
172.                        Kufa kwa jamaa, harusi
173.                        Kufa kwa mdomo, mate hutawanyika
174.                        Kuishi kwingi ni kuona mengi
175.                        Kujikwaa si kuanguka, bali ni kwenda mbele
176.                        Kukopa harusi, kulipa matanga
177.                        Kuku havunji yayile
178.                        Kuku mwenye watoto halengwi jiwe
179.                        Kula kutamu, kulima mavune
180.                        Kulea mimba si kazi kazi kulea mwana
181.                        Kulenga si kufuma
182.                        Kumla ngulu si kazi, kazi kumwosha
183.                        Kunako matanga, kumekufa mtu
184.                        Kunguru mwoga hukimbiza bawa lake
185.                        Kupanda mchongoma kushuka ngoma
186.                        Kupotea njia ndiko kujua njia
187.                        Kutoa ni moyo usambe ni utajiri
188.                        Kutu kuu ni la mgeni
189.                        Kutwanga nisile unga, nazuia mchi wangu
190.                        Kuzima koleo si mwisho wa uhunzi
191.                        Kwa mwoga huenda kicheko kwa shujaa huenda kilio
192.                        Kwenda mbio si kufika
193.                        Kwenye miti hakuna wajenzi
                                     “L”
194.                        La kuvuma halina ubani
195.                        La kuvunda halina ubani
196.                        Lake mtu halumtapishi bali humchefua
197.                        Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo
198.                        Liandikwalo ndilo liwalo
199.                        Lila na fila hazitangamani
200.                        Lipitalo, hupishwa
201.                        Lisemwalo lipo, ikiwa halipo, lipo nyuma linakuja
202.                        Lisilokuwepo moyoni halipo machoni
                                      “M”
203.                        Maafuu hapatilizwi
204.                        Macho hayana pazia
205.                        Mafahali wawili hawakai zizi moja
206.                        Maiti haulizwi sanda
207.                        Maiti hachagui sanda
208.                        Maji hufuata mkondo
209.                        Maji huteremkia bondeni, hayapandi kilimani
210.                        Maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga
211.                        Maji usiyofika hujui wingi wake
212.                        Maji ya kifuu ni bahari ya chungu
213.                        Maji yakimwagika hayazoleki
214.                        Majumba makubwa husitiri mambo
215.                        Majuto ni mjukuu, mwishowe huja kinyume
216.                        Mambo kikowa
217.                        Manahodha wengi chombo huenda mpera
218.                        Maneno mema humtoa nyoka pangoni
219.                        Maneno makali hayavunji mfupa
220.                        Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika
221.                        Maskini akipata, matako hulia mbwata
222.                        Maskini na mwanawe, tajiri na mali yake
223.                        Mavi usiyala, wayawingiani kuku­?
224.                        Mavi ya kale hayanuki
225.                        Mbaazi ukikosa maua, husingizia jua
226.                        Mbinu hufuata mwendo
227.                        Mbio za sakafuni, huishia ukingoni
228.                        Mbiu ya mgambo ikilia ina jambo
229.                        Mchagua jembe si mkulima
230.                        Mchagua nazi, hupata koroma
231.                        Mchakacho hujao, haulengwa na jiwe
232.                        Mchama ago hanye hanyeli, huenda akauya papo
233.                        Mchelea mwana kulia, hulia yeye
234.                        Mchele mmoja, mapishi mengi
235.                        Mcheka kilema hafi bila kumfika
236.                        Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao
237.                        Mcheza kwao hutunzwa
238.                        Mcheza na tope humrukia
239.                        Mchimba kisima, hakatazwi maji
240.                        Mchimba kisima huingia mwenyewe
241.                        Mchimba kisima humtia mtuwe
242.                        Mchonga mwiko hukimbiza mikono yake
243.                        Mchovya asali hachovyi mara moja
244.                        Mchuma janga hula na wakwao
245.                        Mchumia juani hula kivulini
246.                        Mdharau mwiba mguu huota tende
247.                        Mdharau biu, hubiuka yeye
248.                        Meno ya mbwa hayaumani
249.                        Mfa maji hukamata maji
250.                        Mficha uchi hazai
251.                        Mfinyanzi hulia gaeni
252.                        Mfuata nyuki hakosi asali
253.                        Mfukuzwa kwao hana pa kwenda
254.                        Mgaagaa na upwa hali wali mkavu
255.                        Mganga hajigangi
256.                        Mgema akisifiwa Tembo hulitia maji
257.                        Mgeni hachomi chaza mtaani akanuka
258.                        Mgeni ni kuku mweupe
259.                        Mgeni njoo mwenyeji apone
260.                        Mgonjwa haulizwi uji
261.                        Miye nyumba ya udogo, sihimili vishindo
262.                        Mja hana hiari
263.                        Mkamatwa na ngozi ndiye mwizi
264.                        Mkamia majihayanywi, akiyanywa humpalia
265.                        Mkata hana kinyongo
266.                        Mkata hapendi mwana
267.                        Mkate mkavu wa nyumbani ni bora kuliko nyama ya shuwa yap engine
268.                        Mke ni nguo, mgomba kupalilia
269.                        Mkono mmoja hauchinji ng’ombe
270.                        Mkono mmoja haulei mwana
271.                        Mkono mtupu haulambwi
272.                        Mkono usioweza kuukata, ubusu
273.                        Mkosa kitoweo, humangilia
274.                        Kabuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu
275.                        Mkulima ni mmoja, walaji ni wengi
276.                        Mla cha mwenziwe na chake huliwa
277.                        Mla cha uchungu na tamu hakosi
278.                        Mla kuku wa mwenziwe miguu humwelekea
279.                        Mla mbuzi hulipa ng’ombe
280.                        Mla kwa miwili hana mwisho mwema
281.                        Mla, mla leo, mla jana kala nini?
282.                        Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe
283.                        Mlenga jiwe kundini hajui limpataye
284.                        Mlilala handingwadingwa, mwenye macho haambiwi tule
285.                        Mlimbua nchi ni mwananchi
286.                        Mnyamaa kadumbu
287.                        Mnywa maji kwa mkono mmoja, kiu yake I pale pale
288.                        Moja shika si kumi nenda uje
289.                        Moto hauzai moto
290.                        Mpanda farasi wawili, hupasuka msamba
291.                        Mpanda ovyo, hula ovyo
292.                        Mpemba akipata gogo, hanyi chini
293.                        Mpemba hakimbii mvua ndogo
294.                        Mpemba hashoni tomo dogo
295.                        Mpiga ngumi ukutani huumiza mkonoe
296.                        Mpofuka uzeeni hapotei njia
297.                        Msafuri kafiri
298.                        Msafiri maskani, ajapokuwa sultani
299.                        Msasi haogopi miiba
300.                        Msema pweke, hakosi
301.                        Mshare kwenda msituni haukupotea
302.                        Mshoni hachagui nguo
303.                        Msitukane wagema na ulevi ungalimo
304.                        Msitukane wakunga na uzazi ungalimo
305.                        Mstahimivu, hula mbivu
306.                        Mtaka cha uvunguni huinama
307.                        Mtaka nyingi nasaba hupata nwingi msiba
308.                        Mtaka nyingi faida husogeza nyingi hasara
309.                        Mtaka yote hukosa yote
310.                        Mtaka hunda haneni
311.                        Mtegemea nundu haachi kunona
312.                        Mtegemea ndugu hufa masikini
313.                        Mtembezi hula miguu yake
314.                        Mteuzi haishi tama
315.                        Mti hawendi ila kwa nyenzo
316.                        Mtondoo haufi maji
317.                        Mtoto akibebwa hutazama kisogo cha mamaye
318.                        Mtoto akililia wembe mpe
Hizo ni baadhi ya methali zilizokusanywa na mwl. Majummbeni .
Kama wewe ni mtafiti au mdau wa Kiswahili unataka kujua kuhusu methali au unahitaji methali vingi zaidi kwa matumizi ya kufundishia au kuandika tasnifu, tafadhali wasiliana nami kwa,
              
     
                   hwilliady@ymail.com
                  majumbeni@gmail.com 



   FILAMU NI SEHEMU YA FASIHI YA KISWAHILI



Historia ya Filamu Afrika

Barani Afrika sanaa ya filamu ilianza kuonekana kutoka kwa wakoloni, ambao waliitumia kama zana ya kuwaelimishia Waafrika, lakini wakiamini kwamba Waafrika hawakuwa na uwezo wa kutenganisha ukweli na uongo (Diawara 1992). Mtazamo huu kwa sasa umeshapitwa na wakati, kwani Waafrika wamekwishaelimika kiasi cha kutosha kung’amua mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye jamii zao. Kwa ufupi, Waafrika wa sasa wamehamasika tofauti na wale wa miaka ya ukoloni. Pia, si Waafrika wote ambao hawakuweza kutenganisha ukweli na uongo, bali ni mtazamo au kasumba tu iliyojengwa na wakoloni wakati huo ili kuwadharau Waafrika.  
Ukadike (1994:1) anaeleza kuwa mwanzoni Waafrika hawakuweza kumiliki filamu mpaka ilipofikia miaka ya 1960  ambapo nchi nyingi za Afrika zilikuwa zikipata uhuru. Anaendelea kusema kuwa kutokana na wimbi hili la kujipatia uhuru, mataifa ya Afrika kama vile Senegal, Mali, Burkina Faso, Nigeria na Tanzania yalianza kuwa na mamlaka juu ya sanaa hii kwa kutengeneza filamu zao wenyewe. Waandaaji wa filamu wa Afrika walibadili mwenendo wa filamu kutoka  ule wa wakoloni ambao ulikuwa na lengo la kuimarisha utawala wa kikoloni na kueneza utamaduni wao. Hivyo wasanii wa Kiafrika  wakaanza kuitumia sanaa hii kama chombo muhimu katika mapambano ya kuudumisha utamaduni wa Mwafrika. Walifanya hivi kwa kuchunguza kwa kina utamaduni wa Afrika na kuanza kujenga upya pale ambapo ukoloni ulikuwa umedunisha na kupotosha. Ukadike (1994:166) anaendelea kusema kuwa waandaaji hawa walionyesha hamu ya kuwasiliana na jamii zao, kuamsha uelewa na kisha kuhamasisha jamii zao kupambana na changamoto zinazowakabili.
Cham (1996) anaeleza kwamba, filamu za Kiafrika zimekuwa zikiendana na hali halisi ya jamii za waandaaji wa filamu. Anasema pia kwamba waandaaji hawa wamekuwa wakitumia filamu kama njia ya kusaidia jamii kuondokana na mawazo ya kitumwa, na kukabiliana na changamoto zinazowakabili. Juhudi hizi zinathibitishwa na mwandaaji wa filamu aitwaye Kabore (2000) anaposema kuwa yeye kama msanii ana jukumu la msingi la kuyatilia maanani anayoshiriki, kwa kuwa ana mizizi na historia ambayo imeungana na historia ya jamii yake. Anaongeza kuwa daima anaiakisi hali hii kwenye filamu anazoandaa. Msimamo huo wa Kabore unakuja kipindi ambacho waandaaji wa filamu wanaingiza vionjo vya Kiafrika ili kuyalenga mambo muhimu yanayoendana na maisha ya watu wa jamii husika. Historia hii fupi ya filamu Afrika katika utafiti huu itasaidia katika kutoa picha na kuonyesha maendeleo na malengo halisi ya filamu za Kiafrika. Waandishi waliozungumzia historia hii wanasisitiza kuwa filamu za Kiafrika zinapaswa kuendana na maisha na hali halisi ya jamii husika ili kuweza kuisaidia jamii hiyo.

Historia na Maendeleo ya Filamu Nchini Tanzania

Kwa mujibu wa  Smyth (1983:129-143), filamu nchini Tanzania ni utanzu wa fasihi ambao ulianzishwa kipindi cha wakoloni. Filamu chache zilizoanzishwa wakati huo zilikuwa na lengo la kuendeleza utawala wa kikoloni na kueneza utamaduni wao. Katika Afrika  hakukuwa na sehemu yoyote  ambapo palianzishwa kiwanda cha utengenezaji filamu za hadithi ndefu za kifasihi,  bali filamu nyingi zilikuwa ni za makala za kuzungumzia matukio halisi. Katika makoloni ya Waingereza, utengenezaji wa filamu za hadithi ndefu umekuwa na mafanikio na kuenea Afrika Magharibi kuliko Afrika ya Kati na Afrika Mashariki. Miongoni mwa sababu zilizokwamisha mafanikio ya utengenezaji wa filamu za kifasihi ni kukosekana kwa mfumo wa kubadilisha fedha za kigeni, udhibiti wa mgawanyo wa fedha hizo na ufinyu wa soko la taifa. Pia kushindwa kwa serikali za Kiafrika kurudisha na kuzitumia fedha zilizopatikana kutokana na kodi ya sinema katika uzalishaji wa ndani wa filamu.
Kwa mujibu wa Nottcut na Lathan (1937), sanaa ya filamu  ilianza kuingia nchini Tanzania miaka ya 1920. Kwa upande wa Tanzania maendeleo ya filamu yalichochewa na nchi za Ulaya na za Kiafrika. Mwanzoni kabisa mwa  miaka  ya 1920 kulianza kuonekana filamu za Kizungu zilizoletwa na wakoloni kwa lengo la kuimarisha utawala wao katika koloni la Tanganyika. Katika miaka ya 1930 Tanganyika ilichaguliwa kama kituo cha kimataifa cha filamu kilichokuwa chini ya Wamisheni ambacho kiliitwa BEKE (Bantu Educational  Kinema Experiment). Utengenezaji wa filamu katika kipindi cha ukoloni nchini Tanzania, unaweza kuangaliwa kuanzia miaka ya 1933 hadi 1960.
Mponguliana (1982) anaeleza kuwa historia ya filamu Tanzania imegawanyika katika vipindi viwili, yaani wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni. Vipindi hivi vilitofautiana kulingana na matukio yaliyokuwa yakitokea wakati huo. Kwa mfano, filamu zilizoonyesha harakati za kupigania uhuru zilitengenezwa wakati wa ukoloni. Baada ya ukoloni, filamu zilibeba maudhui yaliyoendana na harakati za Azimio la Arusha. Mgawanyo huu ni muhimu hasa katika utafiti huu kwani unatusaidia kutathmini endapo filamu za sasa pia huakisi kinachotokea katika jamii ya Kitanzania wakati huu. Pia itatusaidia kuonyesha maendeleo ya filamu katika vipindi mbalimbali kama baada ya Azimio la Arusha na wakati wa uchumi au soko huria.

Filamu  Kipindi cha Ukoloni

Notcutt na Lathan (1937) wanaeleza kuwa katika kipindi cha ukoloni filamu zilitumika katika mchakato wa kutawala, kuwatia kasumba na kuwapumbaza Watanganyika. Wakoloni  walianza kwa kuingiza filamu kutoka nchini Uingereza ambazo ziliakisi mienendo na utamaduni wa kikoloni. Utengenezaji wa filamu Tanganyika ulianza kati ya miaka ya 1935 na 1936 chini ya kampuni iliyojulikana kama Bantu Educational Cinema Experiment. Makao yake makuu yalikuwa Vugiri katika milima ya Usambara, Tanga, ambapo mtunzi alikuwa Notcutt na Waingereza wenzie. Filamu nyingi zilizotengenezwa kipindi hiki zililenga kueneza elimu ya kikoloni na kuimarisha ukoloni. Birihanze (1971) katika Jarida la UMMA anaeleza kuwa katikati ya miaka ya 1960 TANU iliamua kuanzisha Kampuni ya Filamu ya Taifa (TFC). Anasema kwamba hata baada ya kuanzishwa kwa kampuni ya filamu ya taifa hakuna sera zilizowekwa kuhusiana na filamu.
Mponguliana (1982) anaelezea kuwa filamu za mwanzo nchini Tanzania zilitumia lugha ya Kiingereza na maneno machache ya Kiswahili, Kisukuma na lugha nyingine za kikabila. Anaendelea kueleza kuwa utengenezaji wa filamu za kifasihi ulianza Tanganyika miaka ya 1950. Filamu hizi zilizingatia vigezo vya kifasihi kama vile fani, maudhui, maana, muktadha wa kifasihi, na matumizi ya lugha yenye mvuto iliyosheheni tamathali za semi. Baadaye, kampuni ya Afrika Kusini ilipewa jukumu la kutengeneza filamu kwa kutumia mandhari na waigizaji wa Tanganyika na kwa lugha ya Kiswahili katika mikoa ya Dar es salaam na Dodoma. 

Filamu Baada ya Ukoloni

Kipindi hiki kinaanzia mwaka 1961, yaani baada ya Tanganyika kupata uhuru, na kuendelea mpaka miaka ya 1990. Toka kipindi hicho kumekuwa na mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha kama siasa, utamaduni, hali ya uchumi, na mtindo wa maisha ya watu kwa ujumla. Hali hii imeathiri kazi mbalimbali za fasihi kwa kuzifanya ziwe na sura mbalimbali. Mponguliana (1982) na Mwakalinga (2003) wanaelezea kuwa katika miaka ya 1960 kulikuwa na jitihada za awali za kufufua tasnia ya filamu nchini Tanzania. Katika kufanikisha hilo mwaka 1963 ilianzishwa Kampuni ya Filamu ya Taifa (NFC) iliyokuwa na jukumu la kusimamia maadili katika utengenezaji wa filamu, na shughuli nzima ya uendeshaji wa filamu nchini Tanzania.
Mwaka 1964 wataalamu wa filamu kutoka Yugoslavia walifika Tanzania kupanga upya masuala ya filamu. NFC ilisaidia katika kutengeneza filamu za makala simulizi zilizoelezea mambo halisi kutegemeana na matukio maalumu kama vile ziara za kitaifa, gwaride na shughuli nyingine muhimu. Kati ya filamu hizo ni Tanganyika Triumphant (1962), Road Ahead (1963) na The Land of Promise (1963). Kwa sasa, filamu hizi zinatumika katika kuonyesha kumbukumbu za matukio ya kitaifa kama vile Siku ya Uhuru. Wakati wa Azimio la Arusha filamu ilikuwa chombo muhimu katika kutangaza sera za Ujamaa na Kujitegemea, na Vijiji vya Ujamaa. Wakati huo TANU ilikuwa mstari wa mbele katika kuendeleza filamu nchini Tanzania. Filamu wakati wa sera ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea zililengwa kuonyesha masuala kama vijiji vya ujamaa, elimu ya kujitegemea na ukombozi. Kwa ufupi, filamu zilizotolewa wakati wa Azimio la Arusha zilihamasisha harakati za ukombozi. Lakini, kwa upande mwingine, mabepari waliokuwepo wakati ule walitumia filamu na televisheni kama chombo cha kutekeleza matakwa ya ubepari, urasimu na propaganda.
Kulikuwa na juhudi za kuwachanganya Watanganyika kwa kuwaonyesha filamu za Kizungu ambazo hazikuwa na uhusiano na mambo yaliyokuwa yanatokea kwenye jamii ya Kitanganyika. Walitumia filamu kupinga itikadi ya kijamaa ili kuwanyima au kuwanyang’anya Watanganyika ari ya kuzitazama filamu zilizolenga kuusimika ujamaa na kuhamasisha ukombozi. Filamu nyingi zilizoingizwa Tanganyika wakati ule zilikuwa za Kizungu na zilitengenezwa kwa ajili ya soko la Marekani. Mfano wa filamu hizo za kibepari ni kama vile Hammer na Slaughter. Wahusika na mandhari iliyotumika katika filamu hizi ilikuwa ni ya Kizungu. Mathalani, katika filamu ya Slaughter, kulikuwa na wahusika Jim Brown na ex-Green Beret ambao walikuwa askari wa kibepari wa Marekani. Filamu hizi zilioonyesha matukio ya vurugu, ngono, matukio ya kikatili na makosa ya jinai kama mauaji. Hii iliwafanya Watanganyika, na Waafrika kwa ujumla kuwa na woga katika harakati za ukombozi za kupigania haki zao Birihanze (1971:43) katika Jarida la UMMA.
Mponguliana (1982) anaeleza kuwa filamu zilizochezwa na wasanii wa Kitanganyika zilianza kuonekana kati ya miaka ya 1960 na 1970. Filamu ya kwanza inayojulikana kama Muhogo Mchungu ilitoka miaka hiyo na ilichezwa na Rashid Mfaume Kawawa ambaye kwa wakati huo alikuwa  miongoni mwa viongozi wa nchi. Rashid Mfaume Kawawa, alichukua uhusika na kucheza kama wahusika wengine. Hii ilifuatiwa na Fimbo ya Mnyonge iliyotoka mwaka 1974. Harusi ya Mariam pamoja na Yomba Yomba zilitoka mwaka 1983. Kutazama mapitio haya ya historia ya filamu Tanzania kutasaidia kuonyesha jinsi tasnia ya filamu ilivyopiga hatua, na kuonesha inakoelekea.
Kuanzia miaka ya 1980, kumekuwa na kushamiri kwa tasnia ya filamu kutokana  na mfumo wa soko huria. Katika kipindi cha soko huria yaani kuanzia miaka ya 1990 kulikuwa na  uhuru wa kuanzisha makampuni binafsi ya habari na kazi mbalimbali za sanaa. Mfumo wa soko huria ulichochea makampuni binafsi kuwa na mwamko wa kufadhili filamu zilizokuwa na dhumuni la kuelimisha watu/ jamii katika nyanja mbalimbali kama masuala ya kijamii na ya kiuchumi. Kushamiri kwa tasnia filamu kumeendelea mpaka miaka ya karibuni yaani miaka ya 2000 na ambapo soko la filamu limechukua sura mapya na limepiga hatua kwa kuwa na wasanii wengi (Kabore 2003: 171).


UCHAMBUZI WA VIPENGELE VYA NAUDHUI KATIKA FILAMU ZA TASWIRA NA VITA YA USHINDI 



Dhamira  katika Filamu ya Taswira

Katika filamu hii dhamira mbalimbali zimejitokeza, tunazijadili kama ifuatavyo:
 
Elimu ni suala la msingi katika maisha ya mwanadamu, na ni kitu muhimu katika jamii yoyote ile kwani humfanya mtu awe na uwezo wa kupambanua vitu na kupambana na mazingira yake (Muhura 2009: 161). Kwa jumla, elimu huwasaidia wanajamii kupata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Elimu ni urithi wa taifa. Wapo waandishi  ambao wamezungumzia suala la elimu katika fasihi. Msokile (1993: 22-23) katika uhakiki wa riwaya ya Shida ameeleza kwa kirefu suala la elimu  kwa kuwatumia wahusika  Chonya na Matika. Msokile anaona kuwa elimu ni chombo cha ukombozi na msingi mkubwa wa kumfanya mtu apate maarifa ili aweze kupata kazi na kuwa na uwezo wa kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.
Katika filamu ya Taswira suala la elimu limeonyeshwa kwa kiasi kikubwa, na msako huu wa elimu umeweza kusukuma mbele ploti ya filamu na kuibua matukio na dhamira mbalimbali. Filamu hii inaonyesha jinsi umaskini unavyosababisha wanafunzi wa kike kama Trace kupata matatizo wanapotaka kujiunga na vyuo vikuu. Kutokana na haja ya kupata elimu, umasikini, uwezo mdogo wa kifedha walionao wasichana wengi  huwashawishi kujiingiza katika njia za mkato za  kutafuta pesa ambazo aghalabu si halali,  kama kuuza miili yao ili waweze kupata pesa. Kwa mfano, wapo wasichana wa vyuo vikuu hapa nchini ambao hujihusisha na masuala ya kuuza miili yao ili wapate fedha za kutumia vyuoni. Hali hii inaonyesha jinsi wanafunzi wasichana yanavyoweza kukumbana na matatizo mbalimbali katika harakati za kutafuta elimu.

Athari za Ubinafsi 

Ubinafsi ni hali au tabia ya mtu au watu wachache kufanya vitendo au vitu fulani ili kuweza kujinufaisha wao wenyewe bila kujali maisha ya wengine (Muhura 2009: 81). Katika filamu ya Taswira, ubinafsi unajitokeza kwa kumuangalia mhusika James ambaye anataka kutumia mali ya urithi kwa manufaa yake binafsi bila kumshirikisha ndugu yake, Tamala. James anatumia mali hii na mke wake Jesca, ambapo baadaye anapata fundisho kwa mkewe Jesca kumkimbia baada ya kumfilisi. Pia ubinafsi unajitokeza kwa kumuangalia mhusika Dkt Gumbo ambaye alijali maisha yake na ya familia yake tu, bila kuwajalia wengine, yaani, Tamala na Trace ambao aliwapa ujauzito na kuwatelekeza. Katika filamu hii ubinafsi unasababisha wahusika wengi kutelekezwa, kuhangaika kwa mateso na hatimaye wengine kufa. Matokeo ya ubinafsi wa James na Dkt. Gumbo yanasababisha maisha ya Tamala yawe ya kuhangaika na kutangatanga, kwani mwishowe Tamala anarudi kijijini na kuishi maisha ya taabu huku kaka yake (James) akitumia mali ya urithi pamoja na Jesca, mkewe. Pia ubinafsi wa Dkt Gumbo ulisababisha Trace kufariki dunia. 

Umalaya na Ngono Zembe

Umalaya na ngono zembe ni hali ya mtu kuwa na wapenzi wengi na aghalabu kufanya kitendo cha ngono bila kutumia kinga. Zipo kazi mbalimbali za fasihi ambazo zimezungumzia suala la umalaya na ngono zembe. Kwa mfano, Mponda (1988) amejadili suala la umalaya kwa kuangalia riwaya ya Nyota ya Huzuni. Katika riwaya hii Makokoto amesawiriwa kuwa na tabia ya umalaya. Huyu ni mwanaume wa makamo ambaye ni mzinzi na mlevi. Kutokana na uzinzi wake amesababisha madhara makubwa  kwa watu wa jamii yake.
Katika filamu ya Taswira masuala ya umalaya na ngono zembe ni dhamira ambazo  zimejitokeza kwa kiasi kikubwa. Umalaya unajidhihirisha  kwa kumuangalia Dkt. Gumbo alivyokuwa akijihusisha na mapenzi holela na wanawake tofautitofauti kwa nyakati tofauti, kama vile Tamala, Trace na Mama Sospeter, mkewe, bila kutumia kinga. Kutokana na tabia yake hiyo, Dkt. Gumbo alimsababishia Tamala ujauzito  na kumtelekeza. Pia anajikuta akijihusisha katika mapenzi na binti yake Trace, bila kujua kwamba ni binti yake aliyezaliwa na Tamala baada ya yeye kumtia ujauzito Tamala na kumtelekeza. Hii inajidhihirisha pale Dkt. Gumbo anaposema, “Hivi wewe hujui kuwa mimi nina mke wangu? Je, mke wangu akijua unadhani itakuwaje?” Maneno haya aliyasema kwa Tamala na Trace kwa nyakati tofauti. Hii hii inaonyesha kuwa Dkt. Gumbo alitaka kufanya nao mapenzi kutimiza haja zake za kimwili na hakuwa na mapenzi ya dhati kwao.
Katika jamii ya Kitanzania, suala la umalaya na ngono zembe linatokea kwa vijana na hata watu wazima. Kwa upande wa wasichana, masuala ya umalaya na ngono zembe yamesababisha matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mimba zisizotarajiwa. Pia, umalaya umehatarisha afya za watu, wanawake kwa wanaume kwa kuwaweka katika uwezekano wa kupata maambukizi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa. Wapo wasichana ambao wamebakwa na wengine wamelazimika kukubali  ngono zembe kutokana na shida mbalimbali za kimaisha. Pia, ukosefu wa huduma muhimu kutoka kwenye familia zao na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya athari ya  ngono zembe kumewafanya wasichana kujiingiza katika kufanya ngono zembe. Hivyo basi, ni jukumu la Watanzania kupiga vita umalaya na ngono zembe kwa kuwa waaminifu katika mapenzi.
 

Ndoa na Uhusiano wa Kimapenzi

Wapo wasanii mbalimbali ambao wamezungumzia suala la ndoa na uhusiano wa kimapenzi. Zipo nyimbo, mashairi tamthiliya na kazi nyingine za kifasihi ambazo zimeangalia suala hili. Kwa mfano, baadhi ya mashairi ya Shaaban Robert yanaonyesha suala la ndoa na uhusiano wa kimapenzi. Katika kitabu cha Mapenzi Bora (1970), Shaban Robert anazungumzia kwa kirefu suala la mapenzi kuwa ni mwangaza na taa katika giza, na kuwa  mapenzi yana baraka  na huondoa ubaguzi baina ya watu. Kwa mujibu wa Muyaka kama alivyonukuliwa na Senkoro ( 2007: 151- 152), amezungumzia masuala mbalimbali kama vile mapenzi. Kwa mfano, katika shairi la “Mahaba” anaeleza jinsi mapenzi yalivyo na nguvu, kwani yanapomuingia mtu huwa kama mpumbavu, wala hasikii na haoni ubaya wowote kwa muhibu wake. Mtu akiwa na hali hii hajali yasemwayo. Mapenzi ya kweli huleta raha ndani ya roho. Kwa hiyo hapa mapenzi yamezungumzwa kwa upande chanya. Katika filamu ya Taswira, suala la uhusiano wa kimapenzi limezungumziwa kwa kirefu. Matukio na matendo ya wahusika yanatawaliwa na uhusiano wa kimapenzi. Hii inajidhihirisha kwa kumuangalia Dkt. Gumbo  ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe, Mama Sospeter, Tamala na Trace. Mapenzi haya yanaonekana kuwa hayakuwa ya kweli kwani Dkt. Gumbo hakuwa mwaminifu kwa mkewe, na aliwakana na kuwatelekeza Tamala na Trace hasa pale walipompa taarifa kuwa  ni wajawazito. Dkt. Gumbo alionekana kushangazwa na kuamua kukana ujauzito na kuwalazimisha watoe mimba hizo. Hii inaonyesha jinsi Dkt. Gumbo alivyokuwa hana mapenzi ya kweli ila tu alitaka kutimiza shida na haja zake za kimwili. Angelikuwa na mapenzi ya kweli angelikubali ujauzito na kuahidi kuwatunza watoto.
Uhusiano mwingine wa kimapenzi unajionyesha kati ya Sospeter na Trace. Sospeter ana mapenzi ya kweli kwa Trace ila anabadili nia yake baada ya kuona kuwa Trace anataka kumsingizia ujauzito ambao si wake. Kwa mantiki hiyo, inaonekana kwamba mapenzi ya kweli yanahitaji uaminifu. Katika jamii ya Kitanzania kumekuwa na migogoro na usaliti katika uhusiano wa kimapezi kutokana na kukosa uaminifu na utu baina ya watu. Watu wanafarakana kwa sababu ya kukosa uaminifu. Ili kuwepo na mapenzi ya kweli inabidi kufuata maneno kama ya Shaaban Robert katika kitabu chake cha Mapenzi Bora (1975:26)  ubeti wa 360 ambapo anaelezea kuwa mapenzi huchukuliwa kama upendo wa kweli na urafiki na yanayofanya moyo usisikitike, yanayojali usawa na haki na huzuia majonzi. Hii inamanisha kuwa mbali na uaminifu lazima kuwepo na upendo na urafiki, usawa na haki ndipo mapenzi yatakuwa ya furaha na yenye kudumu.

Usaliti

Usaliti, ambao waweza kuhusisha utapeli na udanganyifu, ni dhamira ambayo hutawala katika kazi mbalimbali za fasihi kama vile tamthilia, riwaya, hadithi fupi na filamu. Katika filamu ya Taswira, dhamira hii inajidhihirisha kwa kuwaangalia Jesca, Dkt. Gumbo, James na Trace. Jesca hakuwa na mapenzi ya kweli kwa James. Nia yake ilikuwa kumfilisi, kwa kuuza  mali zote na kukimbilia Botswana na wanae, akimwacha James hana kitu. Kwa upande mwingine, Dkt. Gumbo  anamsaliti mkewe kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa. Lakini hata nje pia anaishia kuwatelekeza anaowapa ujauzito. Kwa mfano, anamtelekeza Tamala baada ya kumpa ujauzito. Vile vile Dkt. Gumbo anamlaghai Trace kwamba atamsomesha na hatimaye anambaka na kumtelekeza baada ya kumpa ujauzito. 
Udanganyifu unaendelea kujitokeza pale ambapo Trace anamua kujihusisha katika mapenzi na Sospeter ili aweze kumsingizia ujauzito aliopewa na Dkt. Gumbo. Tatizo au hali kama hii ya kusingizia ujauzito inajitokeza katika jamii ya Kitanzania. Wapo wanawake na wasichana ambao wanapewa ujauzito na kujaribu kuwasingizia watu wengine ili waweze kupata matunzo. Hii hutokana na kutelekezwa na anayehusika na ujauzito huo. Pia hali ngumu ya maisha huwafanya wanawake na wasichana hao  kufanya udanganyifu kama huo.  Madhara ya usaliti na udanganyifu katika ndoa au uhusiano kwa ujumla yanaweza kufarakanisha familia kwa kuleta migogoro isiyokwisha na kurudisha maendeleo nyuma kutokana na kukosa umoja kati ya watu. Kwa jumla, usaliti, utapeli na udanganyifu katika uhusiano wa kimapenzi hutokea kwa kiwango kikubwa katika jamii ya Kitanzania. Wapo wasichana wadogo na wanawake  ambao wamekumbwa na kuathirika na hali kama hii, na, imewasababishia kukata tamaa na hatimaye kujiua wanapoona kuwa hawana pa kukimbilia. Hali hii inawapata hasa wanawake wa umri mdogo ambao hawawezi kusimama peke yao, na kwa kiasi fulani inatokea kwa watu wazima pia.

Ubakaji

Kubaka ni kitendo cha kufanya tendo la ngono na mtu bila ridhaa yake. Idadi ya matukio ya ubakaji inayozidi kuongezeka kuripotiwa kwenye vyombo vya habari inadhihirisha jinsi ubakaji ulivyo tatizo kubwa katika jamii ya Kitanzania. Matukio hayo yanahusisha watu wazima wanaobaka watoto wadogo, vijana wanaobaka vijana wenzao, watu wazima kubaka watu wazima wenzao, na wanaume (na vijana) wanaobaka  vikongwe. Katika filamu ya Taswira ubakaji unajitokeza pale Dkt. Gumbo anapombaka Trace, na hatimaye, kumpa ujauzito na kumtelekeza. Matukio ya ubakaji hutokea  sehemu nyingi kama sehemu za kazi na waathirika wengi ni wanawake, ambao huishia kupata mimba na maradhi. Aidha, wanaume wabakaji hujiongezea nafasi za kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Matatizo haya ya kubakwa, hutokea wakati wa  kutafuta nafasi za ajira, nafasi za masomo au misaada mbalimbali. Pia, upo ubakaji wa vikongwe na watoto wadogo, ambao, huweza kufanyika kwa ajili ya imani za kishirikina. 
Suala la athari za tamaduni za kigeni hasa kwa vijana limezungumziwa na wataalamu mbalimbali wa fasihi. Dhamira hii pia inajitokeza katika umbo la mgongano wa tamaduni kati ya utamaduni wa jadi wa Kiafrika na utamaduni wa Kimagharibi. Suala hili limejadiliwa katika tamthiliya za Ibrahimu Husein (Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo wa Thim), Penina Muhando (Hatia), Ngugi wa Thiongo (Nimerogwa Nisiwe na Mpenzi), na Euphrase Kezilahabi katika riwaya zake tatu za Kichwa Maji, Dunia Uwanja wa Fujo, na Rosa Mistika. Wote hawa kwa viwango tofauti wameonyesha jinsi vijana au kizazi kipya kilivyoathiriwa na tamaduni za kigeni mpaka kufikia mahali ambapo vijana hawajui waegemee upande gani.
Katika jamii ya Kitanzania upo uzoefu na taratibu za maisha ambazo zimezoeleka na zinategemewa zifuatwe na wanajamii. Taratibu hizi za maisha zaweza  kuwa mila na desturi, mavazi, kusalimiana na uhusiano katika jamii. Kutokana na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali kutoka nchi za kigeni taratibu hizi za maisha zimebadilika, na watu wanadai kwamba wanakwenda na wakati. Ngugi wa Thiong’o (1968) katika tamthiliya ya The Black Hermit, na p’Okot Bitek katika Wimbo wa Lawino (1975) wanakubaliana kwamba ukoloni na Ukristo ndizo sababu kuu zilizozusha mgogoro baina ya imani ya Mwafrika na ile ya Mzungu. Waandishi hawa wanasisitiza kuwa maisha ya Mwafrika yalivurugwa na Mzungu. Uvurugaji huu uliwafanya baadhi ya watu weusi kukosa mizizi kabisa, wakawa wanayumbayumba baina ya tamaduni wasizozifahamu vizuri.
Mathalani, katika tamthiliya ya Wakati Ukuta, mwandishi ameonyesha jamii ambayo imevamiwa na utamaduni wa kigeni, au usasa. Mara nyingi vijana huwa wa kwanza kufuata mienendo na matendo mapya ya maisha kwa kuwa huwa hawajazama katika mfumo maalumu wa maisha na wana tamaa zaidi ya kujaribu mienendo mipya. Kwa hiyo, ni rahisi kwa vijana kubadilika kwa vile imani zao za kimsingi huwa zinaendelea kujengeka (Wafula 1999: 18). Katika uigaji huu wa tamaduni za kigeni kumepelekea kuwa na mmomonyoko wa maadili ambao umewafanya  watu au wanajamii fulani kuenenda kinyume na mazoea, mila na desturi zao na utamaduni wa jamii kwa ujumla. Mila na desturi hizo huweza kuwa mavazi yaani jinsi watu wanavyovaa, mtindo wa maisha na uhusiano na mienendo  ya watu kwa ujumla (Chiraka 2009:14).
Katika filamu ya Taswira kuna viashirii vinavyoonyesha athari za tamaduni za kigeni ambazo zimesababisha mmomonyoko wa maadili. Hii inajidhihirisha kwa  kuangalia tabia za wahusika mbalimbali ambao wanaenda kinyume na maadili, mila na desturi za jamii ya Kitanzania. Kwa mfano, mtindo wa maisha na mahusiano ya watu katika familia ya akina Sospeter ni mtindo wa ambao umeegemea zaidi Magharibi. Kwa mfano, tabia ya kukumbatiana na kubusiana hadharani, hasa baina ya watoto na wazazi wao, ni kiashirii cha athari za utamaduni wa kigeni. Uhusiano wao katika familia hauoneshi uzoefu wa maisha ya Kitanzania na ya Kiafrika kwa jumla.
Pia mtindo wa uvaaji wa Trace unaashiria kuathiriwa na tamaduni za kigeni. Hii inawakilisha uvaaji wa wasichana wengi hasa waishio mijini ambao wameiga uvaaji wa Kimagharibi. Mitindo hiyo ya uvaaji inahusisha mitindo ya nywele ya kigeni, kuvaa nguo fupi (sketi fupi), uvaaji wa blauzi ambazo zinaonyesha sehemu kubwa ya matiti na ambazo huweza kusababisha vishawishi vya kingono kwa wanaume. Kwa mtazamo wa mtafiti, uvaaji wake huo ndio ulimfanya hata Dkt. Gumbo amtamani Trace kimapenzi, kwani alikuwa akivaa sketi fupi zinazoonyesha maumbile na pia blauzi ambazo zilionyesha sehemu fulani ya matiti yake. Hii inaashiria kuathiriwa na tamaduni za kigeni.
Vile vile, zipo kazi nyingine ambazo zinaonyesha athari za uigaji wa tamaduni za kigeni. Kwa mfano, katika Wimbo wa Lawino uliotungwa na p’ Okot Bitek (1975), Lawino ambaye alikuwa akidumisha mila na desturi za Kiafrika anaonekana  kumkosoa Clementine ambaye ameathiriwa na tamaduni za kigeni kwa kuiga mtindo wa mavazi na nywele na hata kupaka rangi ya mdomo pamoja na uvaaji kwa ujumla, (u.k. 39). Mwandishi anaonyesha jinsi Clementine, mwanamke wa kisasa, anavyoiga utamaduni wa Kimagharibi ambapo anawakilisha wanawake wengi ambao wanaiga mitindo ya uvaaji bila kujali mila na desturi zao.
Pia matumizi ya maneno ya Kiingereza wakati wa kuongea Kiswahili, yaani uchanganyaji misimbo ni kiashirii kimojawapo cha kuonyesha athari za utamaduni wa kigeni. Kwa mfano, wahusika Sospeter na Trace wanaonekana wakitumia maneno machache ya Kiingereza katika maongezi yao, hasa pale Sospeter anapomwambia Trace, “Let’s  just be friends” (ikimaanisha kuwa naomba tuwe marafiki tu). Sospeter alimwambia Trace maneno hayo alipoanza kumtamani kimapenzi. Matumizi ya majina ya Kizungu pia yanaweza kuwa kiashirii cha athari za utamaduni wa kigeni. Majina hayo ni kama: Trace, Sospeter, James na Jesca. Majina ambayo yangefaa kutumika kama kiashirii cha Utanzania ni yale yenye asili ya Kibantu kama Baraka, Bwana Maige, Majuto ambayo hutolewa kimila bila kubatizwa. Waandishi wengi wa Kiafrika hasa Ngugi wa Thiong’o, Chinua Achebe na p’Okot Bitek wanaonyesha katika kazi zao jinsi walivyokuwa wakipinga tamaduni za kigeni ambazo zililetwa na wakoloni ukiwemo Ukristo, majina ya Kikristo na utamaduni wa Kimagharibi kwa ujumla.
Katika jamii ya Kitanzania athari za tamaduni za kigeni zinajidhihirisha pia kwa  vijana wengi kuathiriwa na mtindo wa uvaaji wa Kimagharibi. Kwa mfano, akina dada kuvaa nguo fupi yaani (vimini) kwa lugha ya mtaani, ni kudhihirisha kuwa wanakwenda na wakati. Matokeo yake tunaona kuwa kesi za kubakwa zimekuwa nyingi. Athari nyingine ni kwamba, wakipita mitaani wanadhalilishwa kijinsia kwa kutukanwa na kutaniwa na vijana au watu wa jinsia ya kiume. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani uvaaji huo usivyokubalika katika jamii yetu ya Kitanzania.
Jamii ya Kitanzania inawatarajia wanawake au akina dada kuvaa nguo ndefu ili kujisitiri, lakini kutokana na utandawazi watu wanaiga utamaduni wa kigeni bila kuangalia mazingira na madhara yake. Kwa ujumla athari za tamaduni za kigeni zimeanza toka wakoloni walipoingia nchini Tanzania, tokea utawala wa Wareno, Wajerumani na Waingereza. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, hali hii imezidi kuongezeka kutokana na utandawazi na kukua kwa teknolojia ya vyombo vya habari na mfumo wa kijigitali. Kwa jumla, hali hii imeathiri sana utamaduni wa Mtanzania kiasi kwamba tunashindwa kutofautisha utamaduni wa Mtanzania ni upi na wa kigeni ni upi. Utamaduni wa Mtanzania umepoteza dira kutokana na mwingiliano wa tamaduni. Athari hizi za tamaduni za kigeni zimechangiwa na mataifa yanayoendelea kuiga mambo yanayoendelea katika mataifa yaliyoendelea. Hii inajitokeza kwa kuangalia suala la utandawazi ambapo mataifa yanayoendelea hulazimika kuiga mambo ambayo yako nje ya utamaduni.
Katika kudhibiti uigaji wa tamaduni ambazo zinakiuka maadili na utamaduni wa Kitanzania, ipo bodi ya filamu ambayo inasimamia mambo hayo. Kwa kuwa filamu zinatakiwa kudumisha utamaduni na maadili ya jamii, ziko  filamu ambazo zilifungiwa na Bodi ya Filamu Tanzania kutokana na kukiuka taratibu za kimaadili. Filamu hizo zilihusika na kuonyesha masuala ya uhusiano wa jinsia moja. Baadhi ya filamu ambazo zimeonekana kumomonyoa maadili ni pamoja na Mtoto wa Mama. Inye Plus, Inye Ndembendembe na Inye Gwedegwede ambazo zinalaumiwa kwa kuharibu utamaduni na maadili ya Kitanzania kwa kuonesha mavazi na matendo yasiyokubalika katika jamii. Filamu hizo zimeondolewa katika soko kwa sababu pamoja na mapungufu mengine, zinachochea uhusiano wa jinsia moja
( Daily News ya tarehe 28 Aprili 2011).
 
Suala la malezi na utu bora limezungumziwa na baadhi ya waandishi katika kazi zao. Taib (2009: 137-138) anamwelezea  mwandishi Shaaban Robert katika kazi zake kuwa anaongozwa na falsafa ya utu katika maisha ya mwanadamu. Maelezo haya yanapatikana katika kitabu cha Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini (uk.100). Mwandishi anaendelea kusema kuwa utu unaonekana pia katika kazi zake mbalimbali kama Utu Bora na pia katika shairi la “Adabu” ( u.k 4). Malezi bora na adabu  ni mambo ambayo yanajenga utu wa mwanadamu, kwani humaanisha kuwa mtu mwenye adabu ndiye mwenye utu. Kwa mtazamo wa Shaaban Robert, suala la malezi bora, adabu, heshima, hekima na utu ni vitu ambavyo vinaendana na vina uhusiano wa karibu.
Katika filamu ya Taswira, dhamira iliyotajwa hapo juu imejitokeza kwa kuangalia matendo ya mhusika Sospeter ambaye alilelewa katika malezi bora na akawa mtu mwenye adabu, heshima, hekima na utu katika kuwasaidia wengine. Hii inajidhihirisha pale ambapo Sospeter anaonyesha heshima kwa wazazi wake na pia kwa Tamala. Sospeter anakubali kuishi na Trace nyumbani kwao na kuonyesha upendo na kumjali. Hekima inajionyesha pale ambapo Sospeter anaamua kuwapatanisha na kuwaunganisha baba yake na Tamala, hususani pale anaposhauri  wamchukue mama Trace (Tamala) kutoka kijijini ili aende kuishi nao mjini. Hii inatokkea baada ya Mama Sospeter na Trace kufariki. Baada ya kuafikiana na baba yake, Sospeter  anamfuata Tamala kijijini.
Katika jamii ya Kitanzania suala la malezi bora, utu, wema, heshima, hekima yanatokea katika jamii yetu. Wapo wazazi ambao wanawalea watoto wao katika malezi mazuri ambayo yanawafanya watoto hao kuwa na heshima na upendo  wa kujali wengine wenye shida. Kwa upande mwingine, wapo wazazi ambao hawawalei watoto wao katika maadili na kuwasababishia kukosa upendo, moyo wa kujali wengine na hatimaye kukosa heshima na hekima, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
 
Mimba nje ndoa  na utoaji mimba ni masuala ambayo yanawakumba wasichana wengi katika jamii ya Kitanzania. MOEVT (2006) inaeleza kuwa mimba nje ya ndoa  huwapata wasichana katika umri mdogo kutokana sababu mbalimbali. Sababu hizo ni kama vile mila na desturi za jamii ambazo huweza kuwachochea kufanya mapenzi katika umri mdogo. Sababu za kiuchumi kama hali ngumu za maisha huweza kuwafanya wasichana kujihusisha na masuala ya kimapenzi wakiwa katika umri mdogo sana. Pia sababu nyingine ni tabia tu za wasichana kupenda kujihusisha na masuala ya ngono katika umri mdogo na hii husababishwa na mabadiliko ya kibaiolojia yanayotokea kwenye miili yao ambayo huwafanya wasichana kuwa na tamaa au mihemko ya kufanya mapenzi bila kuchukua tahadhari.
Katika filamu ya Taswira, hali hii inajidhihirisha pale ambapo Dkt. Gumbo anafanya mapenzi na Tamala na kumsababishia ujauzito, hatimaye kumtelekeza bila kufuatilia taarifa zozote za mama na  mtoto. Hii inasababisha afanye mapenzi na Trace na kumpa ujauzito bila kujua kwamba ni binti yake. Baadaye Dkt. Gumbo anamwambia Trace atoe mimba hiyo kwa kuwa eti ingeleta mgogoro katika ndoa yake. Trace hakubaliani na uamuzi wa Dkt. Gumbo kwa sababu anajua athari za utoaji mimba. Hii inaonyesha kuwa alikuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na athari za utoaji mimba na anamwambia Dkt. Gumbo kuwa amtafutie nyumba yake ya kuishi. Baada ya mke wa Dkt. Gumbo kupata taarifa za ujauzito wa Trace anamlaghai Trace kwa kumpa dawa ambazo anadai kuwa zingemsaidia katika ukuaji wa mimba. Badala yake dawa hizo ni za kutoa mimba, na, zinamfanya Trace kupata maumivu makali na baadaye kupelekwa hospitali na kufanyiwa upasuaji. Katika tukio hilo, madaktari wanafanikiwa  kumuokoa mtoto lakini, kwa bahati mbaya, Trace anapoteza maisha. Kifo cha Trace kinaonyesha jinsi mabinti wanavyoweza kuhatarisha maisha yao kwa kujaribu kunywa madawa ya kutoa mimba. Pia, inaonyesha jinsi wasichana wanavyopata matatizo katika kulea mimba hizo kama vile kukosa matunzo, kutelekezwa na hatimaye vifo.
Katika jamii ya Kitanzania suala la mimba nje ya ndoa na utoaji mimba linatokea sana hasa kwa wasichana wa umri mdogo. Kama ilivyolezwa hapo awali kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo hilo. Wasichana na wanawake walioathirika na tatizo hilo wamefikia hata kuwatupa watoto majalalani kutokana na ugumu wa maisha  na kutokuwa tayari kubeba mimba hizo na kutunza watoto. Hii inatokana na kukosa elimu ya kutosha juu ya kujikinga na mimba nje ya ndoa. Kuhusiana na suala la utoaji mimba, kwa mfano, wapo madaktari ambao badala ya kuwaelimisha wanawake juu ya athari za utoaji mimba wao wanakuwa mstari wa mbele kuwashinikiza watoe mimba, ili madaktari hao, waweze kujipatia kipato kwani utoaji mimba umekuwa kama mradi kwa baadhi ya madaktari. Hii inaonyesha ukosefu wa maadili kwa baadhi ya madaktari. Kwa upande wa Tanzania, suala la utoaji mimba siyo halali kwa mujibu wa sheria. Kutoa mimba ni kosa la jinai ambalo linachukuliwa kama uuaji. Ipo mijadala mbalimbali iliyofanyika kuhusiana na suala hili, ikiwemo mijadala ya bungeni. Hii ni katika harakati za kupiga vita utoaji mimba, kwamba ni kitendo kisichokubalika katika jamii ya Kitanzania. Pia ni kinyume cha haki za binadamu.

Masuala ya Kijinsia

Dhamira hii imezungumzia nafasi ya mwanamke na mwanaume katika jamii. Masuala ya kijinsia yanazungumziwa sana katika jamii yetu ya Kitanzania. Kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika jamii, wapo waandishi mbalimbali ambao wamezungumzia suala la nafasi ya mwanamke katika jamii. Mwanamke amesawiriwa katika nafasi mbalimbali kutegemeana na mtazamo wa mwandishi.  
Katika filamu ya Taswira mwanamke amesawiriwa katika pande mbili yaani upande chanya na hasi. Kwa upande chanya mwanamke amesawiriwa kama mtu shupavu, asiyekata tamaa kwa haraka na jasiri wa kuweza kupambana na vikwazo mbalimbali katika maisha. Ujasiri, ushupavu na kutokata tamaa kunajidhihirisha kwa kuwaangalia wahusika Tamala na Trace mwenyewe. Tamala kwa mfano, amekuwa ni mwanamke shupavu na jasiri katika kupambana na changamoto mbalimbali zilizomkabili katika maisha. Mbali na kutelekezwa na Dkt. Gumbo wakati wa ujauzito, anajitahidi kutunza na kulea mimba yake mpaka anapojifungua. Mbali na hayo, Tamala anajitahidi kufanya shughuli za kiuchumi, yaani, kilimo, ili aweze kujikwamua na hali ya maisha aliyokuwa nayo. Mapato haya yanamsaidia katika kutatua matatizo yake kama kulipa ada ya Trace mpaka anapomaliza shule. Anamsisitiza mwanaye pia kuwa shupavu kwa kusema kuwa mwanamke shupavu kila mara hutafuta njia mbadala ya kuweza kujikwamua katika maisha.” Maneno haya yanaonyesha jinsi Tamala anavyomshauri mwanawe na kumfundisha kuwa shupavu. Trace naye amesawiriwa kama mwanamke jasiri, shupavu na asiyekata tamaa haraka. Haya yanajidhihirisha pale Trace anapotaka kutimiza ndoto zake za kupata elimu ya juu. Ili kufika lengo hili, anatafuta ufadhili kwa mshauri wa wanafunzi na anataka kujitolea figo yake ili apate fedha ya karo. Ndoto zake hazikutimia kwani alibakwa na kupata mimba ya Dkt. Gumbo na hatimaye kufa.
Vilevile Mke wa Dkt. Gumbo amesawiriwa katika nafasi chanya kwa kuonesha uwajibikaji wake. Amesawiriwa kama mwanamke anayefanya kazi kwa bidii kwa kujishughulisha na biashara ya kuendesha kampuni  iliyoitwa Kilua Investment. Mama Sospeter anadiriki kwenda hata, nchi za mbali kutafuta mawasiliano na malighafi kwa ajili ya kuendeleza kampuni, akiongozana na mwanae Sospeter. Hii inaonyesha kuwa wanawake wanaweza kufanya shughuli ambazo wanaume wanafanya.
Kwa upande wa pili, mwanamke katika filamu ya Taswira amesawiriwa katika nafasi hasi kwa kumwangalia Tamala na Trace. Tamala anatumiwa kama chombo cha starehe na Dkt. Gumbo kwa kukubaliana kufanya urafiki na, hatimaye, kuwa na uhusiano ya kimapenzi nje ya ndoa. Katika filamu hii mwanamke anaonekana kama chombo cha starehe pale Tamala anapopata ujauzito wa Dkt. Gumbo na kutelekezwa. Vilevile Dkt. Gumbo anajikuta akiwa na uhusiano kimapenzi na Trace bila kujua kuwa ni binti yake na ambaye pia Dkt. Gumbo alimkana baada ya kupata ujauzito. Pia nafasi hasi inajidhihirisha kwa kumuangalia Mke wa Dkt Gumbo, ambaye anaonyesha na roho mbaya na ya kinyama ya kumdhuru Trace, pale anapompa dawa za hatari za kutoa mimba.
Katika jamii ya Kitanzania wanawake wanachukuliwa katika nafasi mbalimbali. Wapo wanawake wanaotaka kujikomboa kutokana na matatizo mbalimbali kwa kujikwamua wao wenyewe. Hawa wanawakilisha ukombozi wa mwanamke ingawa wanakabiliwa na changamoto ili kufikia malengo yao. Wanawake katika kundi la pili wanataka kupata huduma muhimu kwa kuuza miili yao lakini mwisho wake wanaishia kupata ujauzito na maradhi. Pia kundi lingine la wanawake ni lile la wenye roho za kinyama, ambalo linadhamiria kudhuru na kuumiza wanawake wengine. Kwa hakika, wanawake wanapaswa kuenenda katika njia inayofaa, inayopaswa na kuweza kuigwa na watu wengine katika jamii. Hivyo basi, wasijidhalilishe kwa kujiona kuwa wao ni viumbe duni bali wajitahidi kujikomboa kwa kujikwamua kwa kufanya shughuli za kiuchumi na kuepuka utegemezi. Kwa mfano, wapo wanawake wengi wanaishi maisha kama ya Tamala kwa kuuza vyakula, wengine wanafanya shughuli za kilimo na biashara nyingine ndogondogo ili waweze kujikwamua katika matatizo ya kiuchumi. Fedha wanazozipata wanazitumia katika kulipia ada za watoto wao na kuongeza pato la familia. Tabia za akina baba wengi kutelekeza familia zao kwa sababu mbalimbali, huwasababishia akina mama, kuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia. Pia wapo wasichana ambao wanaishi maisha kama ya Trace na wanatamani maisha ya juu ambayo hawana uwezo nayo. Hii huwafanya wasichana wengi kujiingiza katika matatizo mbalimbali. Jamii ya Kitanzania hususani wanawake, wanapaswa kuwa makini katika kutafuta mbinu faafu za kujikwamua kiuchumi na katika matatizo mengine pia.
Hatuwezi kuongelea masuala ya jinsia bila kugusia nafasi ya mwanaume katika jamii. Katika filamu ya Taswira, mwanaume amesawiriwa katika nafasi mbili, yaani nafasi chanya na nafasi hasi. Kwa upande wa nafasi chanya, Dkt. Gumbo amesawiriwa kuwa ni baba mwajibikaji na ambaye anajali familia yake. Anaonekana akimjali mke wake, pamoja na mwanae (Sospeter). Pili, Dkt. Gumbo anaonekana kuwa mshauri mzuri,  hasa pale anapomshauri Trace kuhusu na hatari za kutoa figo. Kwa upande wa nafasi chanya pia, tunaweza kumwangalia Sospeter ambaye alikuwa mwenye mapenzi ya kweli kwa Trace. Yeye hakuwa mdanganyifu, bali Trace mwenyewe ndiye aliyekosa uaminifu. Pia, alikuwa ni kijana mwenye busara na mshauri mzuri na mwenye utu kwa sababu alijali shida za watu wengine, mfano familia ya akina Trace.
Mwanaume katika filamu hii ya Taswira pia amesawiriwa katika nafasi hasi, hasa kwa kumuangalia  mhusika Dkt. Gumbo kwa anaonyesha tabia ya umalaya ya kujihusisha na mapenzi na wanawake zaidi ya mmoja huku akijua kuwa ana mke wake ndoa. Hii inajidhihirisha kwa kumuangalia Tamala na Trace ambao walijihusisha  kimapenzi na Dkt. Gumbo mwisho wake walitelekezwa. Pia Dkt. Gumbo amesawiriwa kuwa mnyanyasaji kwa kumnyanyasa Trace kijinsia, pale anapombaka. Katika jamii ya Kitanzania wapo wanaume ambao wanafanya mambo yenye manufaa kwao binafsi na kwa jamii nzima na pia wapo wale wanaofanya mambo ambayo hayakubaliki kijamii. Wapo wanaume ambao kutokana na hulka na mienendo yao wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu kama umalaya na kuwasababishia watu wengine matatizo. Wapo wanaume watu wazima ambao wanajihusisha kufanya mapenzi na wasichana wadogo bila kuona aibu wakidai kwamba wanakwenda na wakati.
 Suala la unyanyasaji wa kijinsia na ukatili linajitokeza pia katika filamu ya Taswira. Tunavyojua kuwa kuna aina mbalimbali za unyanyasaji wa kijinsia kama unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia na kingono. Katika filamu hii ya Taswira, unyanyasaji wa kijinsia unaojitokeza kwa kiasi kikubwa ni ule wa kingono na ule wa kisaikolojia. Hii inajidhihirisha kwa kumuangalia mhusika Trace ambaye ananyanyaswa kingono na kisaikolojia. Kitendo hiki cha unyanyasaji kinafanywa na Dkt. Gumbo ambaye alimlazimisha Trace kujihusisha kimapenzi bila ridhaa yake na kumtishia kumnyima mahitaji ambayo alikuwa akiyategemea kutoka kwake yaani  ufadhili wa kujiunga na chuo kikuu. Kwa hiyo, Trace analazimika kujihusisha kimapenzi na Dkt. Gumbo ili aweze kupata ufadhili.

Ukatili

Ukatili ni hali ya kumtendea mtu mwingine kitendo kisichostahili kufanywa kwa binadamu yeyote yule. Suala la ukatili katika filamu hii linajitokeza pale ambapo mke wa Dkt. Gumbo alipojaribu kumpa Trace vidonge vya kutoa mimba. Mke wa Dkt. Gumbo alifanya hivyo, baada ya kugundua kwamba mume wake ndiye aliyehusika na ujauzito huo, ambao ulisababisha Trace kufariki na  mtoto aliyezaliwa, kupoteza mzazi wake. Mke wa Dkt. Gumbo hakujali utu na uhai wa mtu, ili mradi lengo lake la kuhakikisha kuwa mimba ile inatoka, linatimia.
Suala la ukatili katika filamu hii pia, linasababishwa na ushawishi. Hii inajidhihirisha pale ambapo James anakubali kushawishiwa na mkewe Jesca ili wamtese Tamala wakati alipokuwa akiishi pamoja nao katika nyumba ya urithi. Jesca ni wifi mkatili ambaye anamshawishi James afanye ukatili kwa Tamala. Wote wawili wanamnyanyasa Tamala kwa kumnyima haki za msingi kama elimu, na anaishia tu kufanya kazi za nyumbani. Pia wakati alipokuwa anaumwa hawakumjali wala kumpeleka hospitali mpaka alipozimia ndipo walimpeleka hospitali. Tamala alipopata nafuu alirudi nyumbani akidhani kuwa maisha yangebadilika lakini haikuwa hivyo. Alipoona kuwa taabu zinazidi na hakuna dalili za mabadiliko aliamua kuondoka na kwenda kuishi na shangazi yake. Ushawishi na ukatili wa mawifi katika jamii yetu ya Kitanzania upo na umekuwa ni tatizo katika kusambaratisha jamii. Filamu hii ya Taswira imeakisi hali halisi ya mahusiano katika ndoa ambao unasababisha migogoro mbalimbali katika familia.

Uongozi

Suala la uongozi katika filamu ya Taswira pia, limegusiwa. Katika filamu hii, uongozi wa kijiji umeonekana ukiwajibika katika kuwasaidia wananchi kutatua masuala mbalimbali ya kijamii kama vile migogoro na masuala mengine ya kifamilia na ya kijamii kwa ujumla. Pia uongozi unaozungumziwa katika filamu hii unasisitiza kufuata na kuheshimu  sheria za nchi, hususan sheria za umilikaji wa ardhi. Hii inajidhihirisha kwa kuwaangalia wahusika Tamala na Baraka ambao walikwenda kutoa taarifa katika uongozi wa kijiji kuhusu uharibifu wa mashamba yao uliofanywa na mifugo. Uongozi huo wa kijiji ulifikia uamuzi kuwa wafugaji wote walipie fidia ya uharibifu wa mazao uliofanyika. Hii inaonyesha kuwa uongozi wa kijiji pamoja na maamuzi  wanayofanya yanaheshimiwa na wanakijiji.

Umaskini

Umasikini ni hali ya kukosa mali, ufukara na ukata (TUKI 2004). Umaskini ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayozikumba nchi zinazoendelea. Kutokana na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, umasikini unajitokeza kwa kiasi kikubwa na kuathiri maisha ya watu. Watanzania walio wengi ni masikini sana mpaka kiasi cha kushindwa kumudu maisha yao na kuacha urithi wowote wa mali kwa watoto wao (Chiraka 2009:54). Umaskini umesababisha watu wengi kushindwa kupata huduma muhimu kama elimu, huduma za kiafya na hata maji. Zipo kazi mbalimbali za sanaa ambazo zimezungumzia suala la umaskini. Mathalani katika Riwaya ya Shida, Chonya na Matika wanakutana na hali ngumu ya maisha mpaka wanaamua kwenda mjini kutafuta maisha. Huko mjini wanakumbana na hali ngumu zaidi mpaka wanaamua kurudi tena kijijini ambapo wanagundua kuwa elimu ndiyo mkombozi wa maisha yao. Vilevile katika tamthiliya ya Ngoswe Kitovu cha Uzembe dhamira ya umaskini ni mojawapo ya dhamira zilizojadiliwa. Hali hii inajidhihirisha kwa kuangalia malazi pamoja na mavazi ya wahusika.
Katika filamu ya Taswira suala la umaskini limejitokeza kwa kuangalia maisha ya Tamala na Trace. Umaskini wa familia ya akina Trace unajidhihirisha kwa malazi, yaani nyumba yao waliyokuwa wakiishi ilikuwa ni ya udongo. Pia maisha yao yalikuwa duni kiasi ambacho Tamala alishindwa kumlipia Trace ada ya chuo kikuu. Hali hii ilimlazimu Trace kutafuta ufadhili kwa watu wengine ambapo ilimsababishia kupata mimba na hatimaye kufa. Umaskini unaweza kusababisha watu kujiingiza katika mambo ambayo yanahatarisha maisha yao. Kwa mfano wapo wasichana waliojiingiza katika masuala ya mapenzi ili waweze kupata fedha za kujikimu. Hali hiyo huwaweka katika mazingira hatayarishi ya kuweza kupata ugonjwa wa UKIMWI na madhara mengine.

  Migogoro katika Filamu ya Taswira

Migogoro ni kipengele kimojawapo kinachotumika kuelezea maudhui. Kutokana na mivutano inayotokea katika kazi ya fasihi, yanazuka matukio ambayo yanasaidia katika kupata maudhui. Wamitila (2003) anaeleza kuwa mgogoro hutumiwa kurejelea mvutano unaokuwako kati ya mhusika mmoja na mwingine katika kazi ya fasihi au katika akili ya mhusika mmoja. Migogoro ni sehemu muhimu katika msuko wa kazi ya fasihi na huchukua  sehemu kubwa ya kazi hiyo. Mgogoro hujitokeza kwa njia mbalimbali. Senkoro ( 1982:4 ) anaeleza kuwa katika kazi ya fasihi kuna migogoro kati ya wahusika,  ama vikundi vya wahusika, familia zao, matabaka yao na kadhalika. Migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kiutamaduni au kisiasa. Halikadhalika kuna migogoro ya kinafsia ambayo inatokea katika nafsi ya mhusika.  
Katika filamu hii ya Taswira ipo migogoro mbalimbali iliyojitokeza. Kwa mfano kuna mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Chanzo cha mgogoro huu ni wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu. Baada ya wakulima kuona hali hiyo, wanatoa taarifa katika serikali ya kijiji na inaamuliwa kwamba wafugaji walipe fidia ya uharibifu wote uliofanyika. Katika jamii ya Kitanzania ipo migogoro ya ardhi kati wa wakulima na wafugaji. Kwa mfano, kuna mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji wa Kimasai Arusha na Morogoro kiasi cha serikali kuingilia kati kwa kuwahamishia baadhi ya wafugaji katika mikoa mingine.
Mgogoro mwingine ambao unajitokeza katika filamu ya Taswira ni ule wa mirathi uliosababishwa na dhuluma ya mali ya urithi kati ya ndugu wawili, James na Tamala. Suala hili linajidhihirisha pale ambapo James anamdhulumu Tamala urithi walioachiwa na baba yao. James alitumia mali ya urithi vibaya kwa kujinufaisha yeye pamoja na mke wake bila kumjali mdogo wake (Tamala). Hali hii inaonyesha jinsi mali ya urithi inavyoweza kuleta  mgogoro katika familia. Hata hivyo, mwisho wa James haukuwa mzuri kwani alifilisiwa mali zote na mkewe (Jesca) na kumuacha hana kitu. Kutokana na hali hiyo James alishikwa na ugonjwa na kuamua kurudi kijijini alikokuwa akiishi Tamala na kumuomba  msamaha. Tamala kutokana na huruma zake alimsamehe kaka yake. Hali hii inaungwa mkono na usemi kuwa, “Damu nzito kuliko maji.”
Mgogoro mwingine mkubwa unaojitokeza katika filamu ya Taswira ni kati ya Trace na familia ya Dkt.  Gumbo. Suala la ufadhili wa Trace hatimaye lilizua mtafaruku mkubwa kati wa  watu wa familia ya Dkt. Gumbo. Uhusiano wa kimapenzi kati ya Dkt. Gumbo na Trace ambao  ulisababisha Trace kupata ujauzito na kuleta mgogoro kati Dkt. Gumbo na mkewe. Matokeo yake Trace alikufa. Hii inaonyesha jinsi migogoro ya kimapenzi inavyoweza kuwa na athari kubwa katika maisha ya watu. Trace anapewa vidonge vya kutoa mimba na Mke wa Dkt. Gumbo na hatimaye anafariki. Katika jamii ya Kitanzania ipo migogoro mingi kati ya makundi mbalimbali ya watu. Migogoro hii yaweza kuwa na vyanzo mbalimbali kama ukosefu wa haki, uonevu, mapenzi, wivu, tofauti za kiuhusiano na usaliti.

Falsafa ya Mtunzi katika  Filamu  ya Taswira

Senkoro (1980) anaeleza kuwa falsafa hubainisha msimamo ama mtazamo wa msanii kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ndio unaoweza kuwatofautisha wasanii mbalimbali. Katika filamu ya Taswira falsafa ya mtunzi ni kuhusu maisha na changamoto zake. Mtunzi anaona kuwa katika kukabili matatizo hayo binadamu anakumbana na vikwazo mbalimbali ambavyo vinazuia mafanikio. Kwa mfano vikwazo katika kutafuta elimu vinatokea kwa hiyo ni vyema kufanya uchaguzi sahihi na kutumia njia sahihi ya kutatua matatizo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Pia binadamu ana taswira mbalimbali katika akili yake. Katika kutimiza hayo binadamu hujiwekea mafanikio kwa asilimia mia moja bila kujali kuhusu changamoto au vikwazo ambavyo vinaweza kutokea. Kwa mfano, Trace alijenga taswira akilini mwake kuwa atafanikwa kupata elimu lakini haikuwa hivyo. Kwa ufupi falsafa ya mtunzi hapa inaonyesha kuwa maisha ni safari ndefu na yana changamoto zake.

Ujumbe katika Filamu ya Taswira

Katika filamu ya Taswira ujumbe unaopatikana ni kuwa ingawa kuna mitihani mingi katika kufikia malengo ya kimaisha tusikate tamaa.. Pia katika kufikia malengo ya baadaye inabidi kuwasikiliza waliotutangulia, yaani wazazi hasa wanapotoa ushauri; kwani “asiyesikia la mkuu huvunjika guu”. Mfano mzuri ni Trace ambaye hakusikia maneno na ushauri wa mama yake kuhusu kuridhika na hali ya maisha waliokuwa nayo. Kushindwa kufanya hivyo kulimfanya Trace hatimaye kufariki.
Katika sehemu hii, tumeona dhamira mbalimbali zikijadiliwa pamoja na falsafa na ujumbe. Sehemu inayofuata, dhamira mbalimbali, falsafa na ujumbe vitajadiliwa. 
Vita vya Ushindi ni miongoni mwa filamu za Kiswahili ambazo zinaonyesha jinsi watu na jamii ya Kitanzania wanavyoishi katika mazingira tofautitofauti. Filamu hii  inaonyesha migogoro mbalimbali inayotokea ambayo chanzo chake kikuu ni uzazi na imani. Zipo imani za kijadi na zile za kidini. Katika kutatua migogoro hiyo watu wanategemea imani hizo. Watu wanaona  kwamba imani zao huweza kutatua matatizo mbalimbali ambayo yanawakumba watu. Miongoni mwa dhamira katika filamu hii zitajadiliwa katika kipengele cha 5.5.1 hadi 5.5.8.
Uzazi ni kielelezo cha kuwepo na kukua kwa jamii ya mwanadamu popote pale ulimwenguni. Ijapokuwa uzazi ni kitambulisho kikubwa cha kuwepo (uhai) na kukua kwa jamii, mtazamo juu ya jambo hili kwa jamii moja au nyingine unaweza kufanana au kutofautiana kulingana na mazingira ya jamii. Katika ontolojia ya Kibantu, uzazi huchukuliwa kama kitu muhimu sana katika asili ya Wabantu na kinachoweza kuleta mshikamano katika ndoa na ndani familia. Kwa Wabantu, uzazi ni suala zito na linaheshimiwa  na kuthaminiwa katika jamii zao. Katika jamii za Wabantu kuna sherehe mbalimbali zinazofanywa ambazo lengo na madhumuni yake ni kuuenzi uzazi.  Kwa mfano, sherehe za kuzaliwa na kumpa mtoto jina zinaashiria kusherehekea kuongezeka kwa ukoo. Hivyo wanajamii wanasherehekea kwa lengo la  kumkaribisha mwanafamilia mpya katika jamii (Mbiti 1969).
Hali kadhalika, katika sherehe za jando na unyago lengo mojawapo kubwa la kuwafunda vijana huwa ni kuwaeleza umuhimu wa uzazi katika jamii zao. Hii ina maana kwamba msisitizo kwa vijana hao huwa ni suala zima la ndoa ambalo ndilo linalounganisha mwanamke na mwanaume hatimaye kupata watoto ambao wataendeleza ukoo  na jamii yao kwa ujumla. Hata katika ibada za matambiko yanayofanywa na jamii nyingi za Kibantu zinahusu uzazi kwa maana kwamba huombwa mizimu kuuendeleza ukoo wao kwa kuwapa kizazi na waondokane na laana ili ukoo uendelee (Mbiti 1969). Hivyo, ibada kama hizo zilizotajwa, zinazofanywa na jamii  za Kibantu kwa namna moja au nyingine, zinahusishwa moja kwa moja na suala zima la uzazi.
Mbiti anaendelea kueleza kuwa baadhi ya jamii za Kiafrika wanaamini kuwa raha ya ndoa ni kupatikana kwa watoto. Na ndoa yenyewe hutambulika pale tu mwanamke atakaposhika mimba na kuzaa. Mwanamke anaposhindwa kuzaa watoto hata kama atakuwa na sifa nyingine nzuri, nyumba hiyo hujawa na huzuni na hujiona kama wana mkosi na laana kutoka kwa wahenga wao. Na mwanamke anapokosa uzazi huaminika kuwa ametenda kosa kubwa sana. Kutokana na mtazamo wa Kiafrika  ni kwamba suala la uzazi lina uhusiano wa moja kwa moja na ndoa na mapenzi. Watu wanapooana wanatarajia kupata watoto ambao ndiyo wanakuwa kiungo cha familia yao. Pia kutokana wa mtazamo wa jamii ya Kitanzania ambayo ni miongoni mwa jamii za Kibantu ni kuwa, watu wanapooana lazima wazae. Lakini mwanamke ndiye huonekana kiini au mlengwa wa kuleta matunda. Kunapotokea matatizo ya uzazi katika familia mtu wa kwanza kulaumiwa ni mwanamke na siyo mwanaume. Mwanamke huanza kupata manyanyaso kutoka kwa ndugu upande wa mume, akiwemo mama mkwe na mawifi. Hali hii imesababisha kusambaratika kwa ndoa nyingi hasa kutokana na shinikizo kutoka kwa wazazi na ndugu wengine.
Katika filamu ya Vita vya Ushindi suala la uzazi, mapenzi na ndoa  limesawiriwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwaangalia wahusika Fred na Stella katika maisha yao ya ndoa. Wahusika hawa wawili wamekuwa na mapenzi ya kweli kwa muda mrefu. Japokuwa Stella alishindwa kupata mtoto kwa muda mrefu lakini mume wake alivumilia na alionyesha kuridhika na hali hiyo. Kutokana na shinikizo kutoka kwa wazazi wa Fred, maisha ya Fred na Stella yalibadilika kutokana na tatizo la uzazi alilokuwa nalo Stella. Wazazi wa Fred walimshinikiza Fred amwache Stella na amuoe Jane. Wazazi walitawaliwa na mtazamo wa Kiafrika kuwa mwanamke akishaolewa  lazima azae na si vinginevyo. Tatizo hili la kutokuzaa kwa  Stella limezusha mgogoro mkubwa kati ya familia ya Fred na familia ya Stella. Hii inaonyesha jinsi jamii inavyolichukulia suala la uzazi kuwa ni muhimu hasa katika  ndoa.
Pia inaonyesha nafasi ya mwanamke mwenye matatizo ya uzazi na jinsi alivyochukuliwa katika jamii kwamba anaonekana kuwa chanzo cha matatizo hayo. Hata hivyo, shinikizo hilo la Fred kumwacha Stella na kuoa mke mwingine halikufanikiwa kwa sababu Stella alikuwa mshika dini. Maombi yake yalimsaidia na hata hatimaye alipata ujauzito na kufanikwa kupata mtoto wa kiume.
Kwa mtazamo wa Kiafrika, watu wengi huona kuwa ili kuishi pamoja katika ndoa, kuzaa ni lazima. Wanasahau upande mwingine kuwa kuzaa ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Hapa inaonyesha kuwa katika jamii za Kibantu uzazi ni suala muhimu, na ndio maana katika filamu hii Stella alipatwa na misukosuko kutokana na tatizo la kutozaa. Hii inaakisi hali halisi ya maisha ya watu katika jamii ya Kitanzania kwani wapo wanawake wengi wenye matatizo ya uzazi ambao wananyanyasika katika ndoa zao. Hii imewasababishia matatizo ya kisaikolojia hatimaye kuvunjika kwa ndoa zao.

 Ushirikina na Uganga  

Suala hili limejitokeza katika tamthilia kadhaa, mathalani, tamthilia ya Emmanuel Mbogo, Ngoma ya Ng’wanamalundi na Ibrahim Hussein, Kinjekitile. Kwa ujumla, ushirikina na uganga kama itikadi za jadi katika tamthiliya hizi zinasawiriwa kama amali muhimu za jamii zifaazo kutumiwa kutatua baadhi ya matatizo ya kimaisha. Uchawi na itikadi za ushirikina, vilevile ni tatizo sugu lenye kukwamisha maendeleo (Mulokozi 1996:210). Zipo imani za aina mbalimbali lakini imani zinazozungumziwa hapa ni imani za kijadi ambazo zinahusisha ushirikina au nguvu za mizimu na miungu wengine. Nguvu hizi kama ilivyoelezwa hapo awali hutumika katika kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii na watu wanaziamini kuwa zinafanya kazi.
Katika filamu ya Vita vya Ushindi, imani za kijadi yaani ushirikina limejitokeza kwa kiasi kikubwa. Hii inajidhihirisha kwa kumwangalia Mama Fred, Mama Jane, Jane  na mganga Masolosolo. Wahusika wanaamini kuwa nguvu hizi zinafanya kazi hasa pale walipotaka kuiharibu ndoa ya Fred na Stella kutokana na tatizo lake la  kutozaa. Mama Fred anaona kuwa njia pekee ya kumuondoa Stella  kwenye ndoa ni kutumia ushirikina na uganga. Katika kutimiza hilo Mama Fred anaamua kwenda kwa mganga ambaye anawapatia dawa ambazo wanaamini zingefanya kazi. Katika kudhihirisha ushirikina na uchawi wao, Mama Fred anamtuma Jane kuchukua nguo za ndani za Stella ambazo zilianikwa kwenye kamba ili waweze kuzifanyia uchawi. Jane anafanya hivyo na anafanikiwa kuzipata. Hii inaashiria kwamba uchawi unaweza kufanywa kwa kupitia nguo za mtu. Nia yao kubwa ilikuwa kutaka kumwachisha ndoa yake. Pia, katika ushirikina wao  Mama Fred na Jane wanadiriki kuamka usiku na kwenda kuwanga chumbani kwa akina Stella. Kutokana na kushika dini, Stella alikuwa na nguvu za kuweza kupambana na uchawi. Alipata uwezo wa kuwaona wakati wakiwa wanawanga usiku na kumwamsha mumewe ili aweze kushuhudia.
Katika jamii wapo watu ambao wanategemea nguvu za uchawi na uganga katika kutatua matatizo yao mbalimbali. Jamii nyingi hasa zile ziishizo vijijini na maskini zinaamini sana ushirikina. Pia mijini ushirikina upo kwani baadhi ya watu wenye nyadhifa zao ambazo wanaamini kuwa nguvu za sihiri zinaweza kuwasaidia kupata madaraka au wasiondolewe katika madaraka. Hudiriki kusafiri safari ndefu kwenda kutafuta nguvu za sihiri ili waweze kudumu katika madaraka. Mbali na viongozi, wapo watu wa kawaida ambao hutumia uganga katika kutatua matatizo kama magonjwa, mahusiano ya kimapenzi na kadhalika. Imefikia hatua mpaka waganga wanajinadi na kujitangaza kwenye magazeti na mabango ili kuvutia biashara. Kwa hiyo, hii inaonyesha kuwa masuala ya uganga yamefanywa kama shughuli ya kujipatia pesa. Lakini mwishoni inaonyesha kuwa nguvu hizo hazidumu kwani watu wanaotegemea sana nguvu hizi mwisho wake huanguka (hushindwa).
Usaliti ni miongoni mwa dhamira zinazojitokeza katika kazi mbalimbali za fasihi.
Usaliti ni hali ya kwenda kinyume na makubaliano yaliyofanyika hapo awali kati
ya makundi mawili au pande mbili. Usaliti unatokea katika nyanja mbalimbali kama siasa, mapenzi, michezo na uhusiano kwa ujumla. Zipo kazi mbalimbali ambazo zimegusia suala la usaliti. Kwa mfano, katika Mashairi ya Chekacheka (1995), Mvungi anaelezea suala la usaliti wa viongozi katika shairi la Taifa Wamelizika. Anaeleza kuwa baadhi ya viongozi ni wasaliti wa wananchi kwani hawajali maslahi ya wananchi bali yao binafsi.
 
Katika filamu ya Vita vya Ushindi usaliti unaojitokeza ni usaliti wa kimapenzi yaani usaliti katika ndoa. Hii inajidhihirisha kwa kumwangalia mhusika Fred jinsi alivyoweza kumsaliti mkewe kwa  kubadili uelekeo au msimamo wake wa awali kuhusiana na suala la  kudumisha mapenzi na ndoa kwa mke wake Stella. Usaliti huu ulichochewa na mama yake Fred ambaye alikuwa akimpiga vita Stella kwa sababu alikuwa hazai. Mwanzoni kabisa inaonyesha kuwa Stella na Fred walikuwa na mapenzi ya kweli na walikubaliana kuishi bila kujali tatizo la uzazi. Lakini baadaye anaonekana akibadili nia yake ya na kuanza kumnyanyasa Stella. Suala la usaliti na kubadili nia katika ndoa linatokea katika jamii yetu ya Kitanzania. Wapo wanaume wengi ambao wamesaliti ndoa zao  kutokana na sababu mbalimbali. Sababu hizo zaweza kuwa tabia au hulka binafsi za wanaume kuwakwa na tamaa, wanawake kutowajali waume zao, matatizo ya uzazi hasa kwa upande wa mwanamke, ukosefu wa maadili na ulevi.  Tatizo la uzazi katika baadhi ya familia limewafanya wanaume kuwaacha wake zao na kwenda kutafuta wanawake wengine nje ya ndoa ambao wanadhani kuwa wanaweza kuwazalia watoto. Usaliti umepelekea wanaume wengine kuwa na ndoa za  mitala na uhusiano wa siri na hata kupata magonjwa ya zinaa kama UKIMWI na kuhatarisha ndoa zao kwa ujumla. Hivyo, usaliti katika ndoa unaweza kuwa na madhara makubwa. Mashindano kati ya mke mkubwa na mke mdogo (wake wenza), yanaweza kutokea pale ambapo mmojawapo anaweza kufanya mambo ya kishirikina ili waweze kuwa na sauti zaidi kwa mume wao. Hali hii huweza kuleta madhara kwa familia nzima. Vilevile wapo wanawake ambao wanasaliti ndoa zao kwa kukosa auminifu na kuwa na uhusiano na wanaume wengine.

 Unyanyasaji wa Kijinsia

Hili ni suala linalojitokeza kwa kiasi kikubwa katika kazi mbalimbali za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na ushairi. Watunzi wanajaribu kuonyesha hali duni ya mwanamke katika jamii ya sasa ili kutafuta sababu ya hali hiyo na kupendekeza ufumbuzi. Baadhi ya waandishi wa tamthiliya wanaogusia suala hilo ni  Muhando, katika Nguzo Mama, Machozi ya Mwanamke, Mulokozi, katika Mukwawa wa Uhehe, Mazrui, katika Kilio cha Haki na Ebrahim Hussein Kwenye Ukingo wa Thim. Unyanyasaji wa kijinsia ni suala ambalo linatokea sana katika jamii zetu za sasa na limekuwa ni chanzo cha matatizo kama mafarakano katika familia na  hata ulemavu. Kwa mfano Jarida la FEMA (2010:11) linaeleza kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni tendo lolote lenye mtazamo wa jinsia linaloweza kumsababishia mtu adha au kero, madhara na mateso ya kimwili, kisaikolojia na kingono.
Katika filamu ya Vita vya Ushindi, unyanyasaji wa kijinsia unajitokeza kwa kumwangalia mhusika Stella jinsi alivyokuwa akinyanyaswa na Fred  baada ya kushinikizwa na wazazi wake amwache. Stella alinyanyaswa kutokana na tatizo la kukosa uzazi. Fred anadiriki kumwambia mkewe kuwa kama anaona mambo yamebadilika ni vyema afungashe vitu vyake aondoke aende kwao. Majibu haya kutoka kwa Fred yanamuumiza sana Stella na kumfanya kukosa raha.
Hii inaonyesha unyanyasaji wa kijinsia kwa kutishia kumwacha mwanamke ni kumnyanyasa kisaikolojia. Usemi huu unaweza kulinganishwa na ule wa kwenye Wimbo wa Lawino (1975) pale Ocol anapomwambia Lawino, “Mwanamke kaa kimya, fungasha vitu vyako uondoke(uk. 121). Wimbo huu wa Lawino ulioandikwa na Okot p’ Bitek unaonesha jinsi Ocol alivyokuwa akimdharau mkewe kuwa hajasoma na ni mshamba kwa hiyo hafai kuwa mke wake. Hii inaonyesha dharau, na unyanyasaji wa kijinsia. Hii ilisababishwa na Ocol kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke wa nje ambaye ni Clementine.
Katika Filamu ya Vita vya Ushindi Stella ananyanyasika, lakini anaonyesha ujasiri  kwa kuwa anamwamini  Mungu na anaendelea kufanya maombi juu ya suala hilo. Katika jamii ya Kitanzania suala hili la unyanyasaji linatokea kwa kiasi kikubwa na wanawake wengi wamekuwa wakiathirika kutokana na unyanyasaji wanaoupata katika ndoa. Wanaume ndiyo wamekuwa chanzo cha unyanyasaji na dharau hasa pale wanapokuwa na uhusiano nje ya ndoa, tabia inayopelekea wawe wadanganyifu na kuwadharau wake zao. Unyanyasaji huu umeleta matatizo katika ndoa kama kufarakana na kutengana. Pia umeweza kusababisha maumivu na uelemavu hasa pale unyanyasaji wa kipigo unapotokea kwa wanawake.

  Ujasiri na Uvumilivu

Kutokata tamaa, ujasiri na uvumilivu kunajitokeza kwenye kazi mbalimbali za fasihi. Kwa mfano katika riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie, mhusika Mama Ntilie anachorwa kuwa mvumilivu, jasiri na asiyekata tamaa ya maisha. Hii inajidhihirisha kwa jinsi anavyoweza kuvumilia matatizo ya ulevi wa mume wake bila kukata tamaa. Anaamua kufanya biashara ndogondogo kwa lengo la kutokomeza umaskini unaoikabili familia yao. Katika riwaya hii pia Kurwa ni mmoja wa wahusika wavumilivu na jasiri katika kuyakabili matatizo.
Katika filamu ya Vita vya Ushindi, dhamira hii inajidhihirisha kwa kumwangalia mhusika Stella ambaye anaonyesha ujasiri katika kupambana na changamoto ambazo zinamkabili. Mbali na kunyanyaswa kutokana na kutozaa, Stella hakukata tamaa, aliendelea kumuomba Mungu akitegemea kuwa atamsaidia. Stella aliendelea kuwa mnyenyekevu na mvumilivu mbali na matatizo na manyanyaso yote aliyoyapata katika ndoa yake kutoka kwa wazazi wa Fred na Fred mwenyewe. Alivumilia mpaka Mungu (kwa imani yake) alipomjalia kupata mtoto. Wanawake wengi wamekuwa wakipata matatizo haya katika ndoa zao lakini wamekuwa wavumilivu ili waweze kutunza watoto na familia kwa ujumla.

  Starehe        

Starehe ni hali ambayo mtu au watu hujiliwaza kwa kufanya matendo ambayo wao hufikiri wanaweza kupata raha au faraja ya namna fulani. Zipo starehe za aina mbalimbali kama kutumia vinywaji, kujihusisha na masuala ya mapenzi, kushiriki katika michezo mbalimbali na kadhalika. Starehe hutegemea mtazamo wa mtu mwenyewe kuwa ni kitu gani anapenda. Kitu fulani kinaweza kuwa starehe kwa mtu mmoja na kuwa karaha kwa mtu mwingine.  Katika filamu hii ya Vita vya Ushindi suala la starehe linajidhihirisha kwa kumwangalia Fred na marafiki zake ambao  wamekaa baa wakinywa pombe na wanawake wanaoendesha ukahaba.
Starehe zao hizi zinasababisha mpaka kutafutiana wapenzi. Kwa mfano, Rich anamtafutia Fred mwanamke wa kustarehe naye wakati anajua fika kuwa Fred ana mke wake. Fred anaingia katika mkumbo wa kujihusisha kimapenzi na mwamke wa nje, yaani Wema, kutokana kuchanganywa na wazazi wake kuwa Stella hafai. Matokeo yake ni kwamba waliishia kufanya starehe na kusahau familia zao. Kwa kuwa Fred alikuwa ni mcha Mungu  hakutarajiwa kunywa pombe na kujihusisha na masuala ya mapenzi nje ya ndoa. Kwa mtazamo huu Fred anachukuliwa kuwa ametenda dhambi kwa kukiuka amri za Mwenyezi Mungu ambazo zinakataza watu kutumia kilevi cha aina yoyote, kutamani na kuzini na mke wa mtu na kadhalika.  
Kwa ujumla starehe kupita kiasi hasa unywaji wa pombe, umekuwa na madhara makubwa katika familia mbalimbali. Ulevi umefanya watu kuwa maskini kupunguza kipato cha familia na kushindwa kuhudumia familia ipasavyo. Ulevi pia unaweza kusababisha kupoteza maisha kutokana na kunywa pombe kali kupita kiasi. Madhara mengine ni kama kuvunjika kwa familia, umalaya, ukatili na unyanyasaji, ukosefu wa maadili katika familia, na kutokuwajibika. Katika jamii ya Kitanzania matukio kama unywaji wa pombe, wanaume kufanya uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa yanatokea na kuathiri maendeleo ya jamii kwa ujumla. Zipo familia zilizosambaratika kutokana na athari za starehe za kupita kiasi. Starehe pia zimepelekea  watu  kuathirika na magonjwa yasiyopona kama UKIMWI.

 Utoaji wa Mimba na Mimba Nje ya Ndoa

Kama ilivyoelezwa hapo awali katika filamu ya Taswira, dhamira hii pia inajitokeza katika filamu ya Vita vya Ushindi. Hii inajidhihirisha pale ambapo mchumba wa John anamlazimisha John waitoe mimba. John anaonekana kutokukubaliana na suala hilo. Wanaamua kumuona daktari ambaye anawaeleza kuwa kutoa mimba ni hatari. Uamuzi wa kwenda kumuona daktari unaonyesha jinsi John alivyokuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na athari  za utoaji mimba. Pia inaonyesha jinsi baadhi ya madaktari wanavyoweza kutoa ushauri mzuri kwa kuzingatia maadili ya kazi zao. Ushauri wenye busara  huepusha madhara kwa watu hasa wasichana wanaotaka kutoa mimba.
Kama ilivyoelezwa hapo awali katika uchambuzi wa filamu ya Taswira kuwa suala la utoaji mimba kwa wasichana ni tatizo katika jamii yetu ya Kitanzania. Wasichana wengi wanadiriki kutoa mimba bila kujali athari zake. Hii yaweza kuwa ni kwa sababu  za kiuchumi au kutelekezwa na wapenzi wao. Pia yawezekana kuwa vitendo vya utoaji mimba vinatokana na mtazamo kwamba mimba nje ya ndoa ni aibu. Hivyo wasichana hutoa mimba ili kukwepa aibu hiyo bila kujali kuwa wanahatarisha maisha yao. Filamu ya Vita vya Ushindi inatoa mwongozo mzuri kuhusiana na suala la utoaji mimba kwa kuzingatia ushauri wa daktari ambaye anakataza na kukemea kitendo hicho kwa kuonyesha madhara yake. Kwa upande wa madaktari, utoaji mimba waweza kuwa chanzo cha kuwaingizia kipato cha ziada. Hii inashadadiwa na matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa maadili ya udaktari kwa ujumla.
    Dini, Imani na Maadili
 
Suala la dini, imani na maadili limezungumziwa na waandishi mbalimbali wa kazi za fasihi kama vile riwaya na mashairi. Kwa mfano, kazi za Siku ya Watenzi Wote, Inkshafi, Utenzi wa Mwanakupona na Malenga wa Mvita zimeelezea nafasi ya dini katika maisha ya binadamu. Kufuata dini kunaonekana kama njia inayoweza kumkomboa mwanadamu dhidi ya tamaa, ufisadi, ubinafsi na matatizo mengi ya maisha yanayoikumba jamii. Dini inaonekana kuwa suluhisho la maisha na inatoa mwangaza juu ya tabia zinazofaa kufuatwa kama kuaminiana, kuheshimiana, kupendana na kuwa na nia safi. Dini ina lengo kuu la kumfanya binadamu awe mwema zaidi na kuwa na maadili mazuri (Njogu na Chimerah  2008: 24). 
Kwa upande wa tamthiliya, dini kama asasi ya kijamii imejitokeza katika tamthiliya kama Aliyeonja Pepo na Mkwawa wa Uhehe. Watunzi wa tamthiliya hizi wanaonyesha kuwa hakuna tamthiliya hata moja iliyokanusha kuwepo kwa Mungu na mitume wake (Mulokozi 1996: 209). Katika filamu ya Vita vya Ushindi, dini iliyozungumziwa ni dini ya Kikristo. Dini hii inaonekana kuwa suluhisho la matatizo ya maisha na inatoa mwangaza juu ya tabia njema zinazofaa kufuatwa. Pia dini inaonekana kuleta kuaminiana, kusameheana na kuungana na vizazi viliyopita.
Dini ya Kikristo, inajidhihirisha kwa kuwaangalia wahusika Stella na Fred ambao wanaonekana wakisoma  Biblia na kufanya maombi  kwa kutegemea sana nguvu za Mungu. Kwa mfano, Stella anapopata matatizo ya kukosa amani katika familia, anafanya maombi na Mungu anasikia sala zake. Pia Stella katika tatizo lake la uzazi anamtegemea Mungu kwa maombi na hatimaye anapata mtoto anayemwita Jacob. Stella anaamini kwamba ukiwa na imani kwa Mungu  yote yanawezekana. Katika jamii ya Kitanzania zipo dini mbalimbali kama vile dini ya Kikristo, Kiislamu  na imani za kijadi na watu wanaamini kuwa Mungu yupo na anasaidia watu katika shida mbalimbali. Wapo watu wengi wanaotegemea maombi wakati wanapopatwa na matatizo mbalimbali . Kwa mfano, katika makanisa na misikiti kuna vipindi vya kuombea mapepo, kuomba mvua, amani, kuombea wagonjwa  na matatizo mengine.

Migogoro katika Vita vya Ushindi

Migogoro katika jamii au makundi ya watu haiepukiki. Migogoro hiyo huweza kuleta madhara au maendeleo. Ila kwa kiasi kikubwa migogoro huleta mafarakano katika makundi mbalimbali ya jamii. Katika filamu hii, chanzo kikubwa cha migogoro hii ni suala la uzazi. Stella ni mhusika ambaye alikuwa na tatizo la kutokuzaa. Familia ya upande wa Fred ilimnyanyasa Stella kutokana na tatizo hilo. Mgogoro huu ulitokana na shinikizo kutoka kwa wazazi. Mwishoni inaonekana kuwa mgogoro huu ulipata muafaka kwa Stella kufanikiwa kupata mtoto. Mgogoro mwingine ni mvutano kati imani za kijadi na  nguvu za kiroho (Ukristo). Nguvu za imani ya Kikristo ndio inabeba hata jina la filamu yenyewe, Vita vya Ushindi, ikiwa na maana mapambano ya pande mbili kati ya Ukristo na imani za uchawi na ushirikina. Stella na Fred wanawakilisha upande unaofuata nguvu za kiroho wakati Jane, mama Jane na mama Fred walifuata (imani za ushirikina na uganga). Katika mgogoro huu upande uliokuwa unafuata nguvu za kiroho yaani dini ya Kikristo ulishinda. Hii inaonyesha jinsi nguvu za Mungu zinavyoweza kushinda ushirikina na uganga hivyo kuwafanya waganga kuonekana waongo.

Falsafa ya mtunzi katika filamu ya Vita vya Ushindi

Njogu na Chimerah (1999:48)  wanaeleza kuwa mwandishi au mtunzi wa kazi ya fasihi husimulia tajiriba mbalimbali ambazo zimemkumba au zimeigusa jamii yake. Kwa hiyo, kazi ya fasihi haitungwi kwa kujistarehesha tu, bali huakisi hali ya maisha ya jamii fulani. Baadhi ya waandishi huongozwa na msimamo wa kinadharia ambao huonyesha falsafa yao ya maisha na pia kazi zao zinaathiriwa na mazingira yaliyomlea na kumkuza. Kwa mfano, mwandishi aliyekulia katika mazingira ya dini atabainisha falsafa yake katika mazingira ya kidini. Katika filamu ya Vita vya Ushindi mtunzi ameegemea kwenye falsafa ya maisha hususani, nafasi ya dini na imani za kijadi. Mtunzi anaona kuwa dini katika jamii ina nafasi kubwa na muhimu katika kutatua matatizo mbalimbali ya maisha. Kwa upande, mwingine mtunzi ameongozwa na Ontolojia ya Kibantu kwa kuhusisha na kuonyesha masuala ya uzazi na nafasi ya  imani za miviga na sihiri katika jamii. Msanii anataka kutuonyesha kuwa jamii za Kiafrika huyachukulia maisha kwa uasilia.
 
Ujumbe katika filamu hii ya Vita vya Ushindi ni kuwa watu wategemee nguvu za
Mungu kupitia dini, katika kutatua matatizo yao ya maisha na siyo kuegemea nguvu za sihiri (ushirikina na uganga). Mungu ndiye muweza wa kila jambo, na nguvu zake zinatenda kazi kuliko nguvu za sihiri. Pia filamu hii inatufunza kuwa subira yavuta heri. Kuvumiliana katika masuala ya ndoa na uzazi ni muhimu na siyo kumnyanyasa mwanamke. Pia wazazi wanaaswa kuwa wasiwe na tabia ya kuingilia ndoa za watoto wao wanapoona kuna tatizo la uzazi kwani Mungu ndiye anayewajalia au kutokuwajalia watu kupata watoto.
Filamu ya Taswira na Vita vya Ushindi. Imebainika kwamba kuna dhamira radidi au motifu ambazo zimejitokeza katika filamu zote mbili. Hii ni pamoja na motifu ya safari na msako wa kutafuta maisha bora; suala la mimba nje ya ndoa na suala la utoaji mimba, starehe,  unyanyasaji wa kijinsia na nafasi ya mwanamke. Kufanana kwa dhamira hizi kunaashiria kwamba filamu hizi zimeakisi masuala mbalimbali ambayo yanatokea katika jamii na pia inaonyesha kuwa matatizo hayo ni sugu katika jamii ya Kitanzania na bado hayajatafutiwa ufumbuzi thabiti.
Kitendo cha wasanii wa kazi mbalimbali za fasihi kuonyesha masuala ambayo yanafanana ni uthibitisho kuwa kile kilichosawiriwa kimelenga yale yanayotokea katika jamii. Kwani ni dhahiri kuwa, wasanii huwa hawajitengi na jamii katika utunzi wa kazi zao. Hii ni sawa na mtazamo wa Mulokozi (1996) kuwa fasihi kama kazi ya ubunifu, husawiri vipengele vya maisha, uhusiano na hisia za watu katika muktadha fulani. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha katika filamu hizi mbili. Masuala ya uhusiano, vipengele vya maisha ya watu kama elimu, migogoro, changamoto mbalimbali, shughuli za kiuchumi na kadhalika vimegusiwa. Sura hii imechambua maudhui ikizingatia vipengele vya dhamira, wahusika, mandhari, migogoro, motifu na ujumbe. Kwa kutumia vipengele hivyo vilivyotajwa, maudhui yameweza kujadiliwa na kueleweka.

Powered by Blogger.