Kufanana na kuhitilafiana kwa mofolojia na fonolojia



Katika kujadili swali hili tutaanza kufasili dhana kuu zilizojitokeza ambazo ni fonolojia na mofolojia. Ambapo wataalamu mbalimbali wamefasili dhana hizi huku kila mmoja akitoa fasili yake. Pia tutatalii kwa kina juu ya kuhitilafiana na kufanana kwa fonolojia na mofolojia na mwisho ni hitimisho.
             
Kwa kuanza na mofolojia, wataalamu mbalimbali wamefasili mofolojia kama ifuatavyo,
      Massamba na wenzake (2009:32) wanafasili mofolojia kuwa ni kiwango cha sarufi kinachojishughulisha na uchambuzi wa mfumo wa maneno katika lugha yaani jinsi maneno ya lugha yoyote iwayo inaundwa.
             Besha (2007:49) anasema mofolojia ni taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wamaneno katika lugha. Misingi ya wataalamu hawa wawili wanaonekana kuingiliana katika kuonyesha namna ya taaluma ya mofolojia inavyojihusisha na muundo wa maneno katika lugha. Mofimu ndio kipashio cha msingi katika mofolojia.
 
            Pia Lubanza (1996:1) anaonekana kuungana nao kwa kusema mofolojia kuwa ni taaluma inayoshuhulika na vipashio vya lugha na mpangilio wake katika uundaji wa maneno.mtaalamu anaongezea namna vipashio vinavyotumika katika kupangilia mfumo wa muundo wa maneno katika lugha. Kipashio cha msingi katika mofolojia ni mofimu.
Hivyo basi fasili ya mofolojia imeonekana kugusia uundaji wa maneno katika lugha kwa mpangilio maalumu. Hivyo mofolojia inaweza kuelezwa kwamba ni taaluma inayoshughulika na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo mbalimbali ya maneno katika lugjha.
Baada ya kuangalia taaluma ya mofolojia, kuna wataalamu mbalimbali ambao wamefasili dhana ya fonolojia, wataalamu hao nia kama wafuatao.
Habwe na Karanja (2007:42) wanafafanua fonolojia kuwa ni taaluma inayoshughulika jinsi sauti zinavyotumika, zinavyounganishwa na kupangwa katika lugha yoyote mahususi ili kuunda tungo zenye maana. Wanaeleza kuwa sauti hizo  zinazotumika katika lugha hiyo mahususi hujulikana kama fonimu.
TUKI (2004) wanaifasili fonolojia kuwa ni tawi la isimu ambalo linajishughulisha na uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha.
Vilevile Kihore ne wenzake (2004:6) wanafasili fonolojia kuwa ni tawi la isimu ambalo hujishughuliah na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambao hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu. Katika fonolojia kipashio cha msingi kinachohusika ni fonimu.
Kwa ujumla fasili zilizoelezwa hapo juu ni za msingi katika taaluma ya fonolojia kwani wataalamu wote wanaelekea kukubaliana kuifasili fonolojia kuwa ni ni uwanja waisimu unaojisgughulisha na  uchunguzi na uchambuzi wa sauti za lugha mahususi.
Kimsingi taaluma ya mofolojia na fonolojia hufanana na kuhitilafiana kwa kiasi kikubwa. Ifuatayo ni maelezo kuhusu ufanano wa fonolojia na mofolojia.
Kwanza, vipashio vya kifonolojia ndivyo vinavyouna vipashio vya kimofolojia, kwa kutumia fonimu ambacho ndio kipashio cha msingi katika fonolojia huweza kuunda mofimu ambayo ndiyo kipashio cha msingi cha kimofolojia.
Mfano:  /h/,/p/,/t/,/k/,/g/,/m/,/n/,/o/,/u/,/e/,/s/,/a/. fonomu hizo zinzweza kuunda mfuatano wa maneno kama ifuatavyo.
Pat-a =pata
Tak-a =taka
Tes-a =tesa
Musa
Maisha Uhusiano mingine ni kuwa kanuni za kifonolojia zaweza kutumika kuelezea maumbo ya  kimofolojia . Kanuni hizI si kwa kuelezea maumbo tu pia huweza kubadili umbo la neno  yaani umbo la ndani na umbo la nje. Kanuni hizo za kifonolojia ni udondoshaji, uyeyushaji, muungano wa sauti, nazali kuathiri konsonanti, konsonanti kuathiri nazali na tangamano la irabu. Mfano,
Udondoshaji, kanuni hii inahusu kuachwa kwa sauti fulani katika matamshi wakati mofimu mbili zinapokaribiana yaani katika mazingira hayo hayo ya sauti ambayo ilikuwepo hapo awali hutoweka.hapa kuangalia umbo la ndani  la neno na umbo la nje. Umbo la ndani ni jinsi neno lilivyoundwa na mofimu zake mbalimbali na umbo la nje ni jinsi neno lisikikavyo linapotamkwa.
Mfano; umbo la ndani                                            umbo la nje
Muguu                                                                         mguu
Mutu                                                                           mtu
Mujapani                                                                     mjapani
Mara nyingi irabu “u” katika mofimu “mu”  ikabilianapo na na mofimu fulani hasa konsonati halisi katika mpaka wa mofimu, irabu “u” hudondoshwa lakini inapokabiliana na irabu inayofanana nayo hubaki kama ilivyo.
Mfano;                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                         
                        Muumba-muumba                                  Muumini-muumini
                        Muuguzi-muuguzi                                  Muungwana-muungwana   
              Uyeyushaji, hii ni kanuni inayohusu ubadilikaji wa irabu fulani kuwa nusu irabu au kama wataalamu wengine waitwavyo “viyteyusho”. Viyeyusho vinavyohusika ni /w/ na /y/. kanuni hii hutokea katika mazingira ambayo irabu “u” hukabiliana na irabu isiyo fanana nayo katika mpaka wa mofimu na kuwa  /w/ lakini hubaki kama ilivyo mara ikabilianapo na irabu inayofanana nayo. Pia irabu /i/  katika mofimu inapokabiliana na irabu isiyofanana nayo hubadilika na kuwa /y/ katika mpaka wa mofimu lakini hubaki kama ilivyo inapokabiliana na irabu inayofanana nayo.
Mfano
Mu+ema-----------mwema                       Vi+ake------------vyake
Mu+ana------------mwana                        Mu+ako------------mwako
Mu+eupe---------mweupe                        Vi+ake-------------vyake
Vi+ao--------------vyao                            Vi+akula----------vyakula
Vi+umb-----------vyumba                                                                         
Tofauti na                                                                                                                             
Muuguzi ------ muguzi                                  Muumba ------- muumba
Muungano wa sauti, kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokabiliana na irabu ya mofimu nyingine katika mpaka wamofimu irabu hizo huungana na kuzaa irabu moja.
Mfano;
Umbo la ndani
Umbo la nje
Wa + enya
wenye
Wa + ingi
wengi
Ma + ino
meno
Wa + izi
wezi
Wa + enzi
wenzi
                                                                                                                                                           
Lakini kanuni hii haifanyi kazi wakati wote kwani kuna mazingira mengine ambayo haifuati hasa katika mofimu mnyambuliko
Mfano:-                                                                                                                                           ,                          
Wa + igizi +a +ji     -        waigizaji
  Wa+ingereza      -       waingereza    
Wa  +oko+a+ji        -         waokoaji
  Wa+ite                -       waite
                                                                                                                                                                                   
Kanuni ya nazari kuathiri konsonati, kuna baadhi ya sauti ambazo huathiriwa na nazali “n” inapokuwa inaandamia yaani kuna sauti ambazo huathiriwa zinapokaribiana au karibiana moja kwa moja na nazali “n”. mara nyingi hutokea katika maumbo ya umoja na uwingi katika maumbo ya maneno
Mfano:-
Umbo la nje
umbo la ndani
Ulimi
u+limi
Ndimi
u+limi
Urefu
u+refu
Ndefu
n+defu
Kwa hiyo kama vile ulimi mrefu
Ndimi ndefu
                                         
Hapa tunaona kwamba sauti [ l ] na [ r ] zinapokaribiana na irabu na irabu haziathiriki lakini zinapokaribiana na nazali “n” hubadilika na kuwa “d”
Kanuni ya konsonati, kuathiri nazali katika lugha y Kiswahili sanifu na hakika katika lugha nyingi za kibantu umbo la sauti ya nazali huathiriwa na konsonanti inayoliandamia. Maumbo ya nazali hutokea kutegemeana  na konsonanti zinazotamkiwa sehemu moja
Mfano:-
Mbawa
Mbaazi        
Mbegu             /m/ na /b/ hutamkiwa mdomoni
Mbuni
Nguzo   
Ngao                 /  / na /d/ zote ni sauti za ufizi.
nguo
kanuni ya tangamano la irabu, huu ni mchakato wa kifonolojia ambao huhusu athari ya irabu moja kwenye irabu nyingine kiasi cha kuzifanya irabu hizo zielekee kufanana kabisa au kufanana katika sifa zake za kimatamshi. Mabadiliko hayo ya sauti husababishwa na utangamano ambao hujitokeza katika baadhi ya vitamkwa yaani kunakuwa na namna fulani ya kufanana au kukubaliana kwa vitamkwa ambavyo ni jirani.                                        
Mfano:-
Umbo la nje
umbo la ndani
Pikia
pik+i+a
Pigia
pig+i+a
Katia
kat+i+a
Endea
end+e+a
Chekea
chek+e+a
Pokea
pok+e+a
                                                                                                               
Hapa tunaona kwamba kitendea -i- kinawakilishwa na maumbo mawili yaani –i- na –e- hapa tunaona kwamba –i- hujitokeza pale tu ambapo irabu ya mzizi wa neno ni ama o au e kiambishi hiki –i- hubadilika na kuwa –e-. hapa ni wazi kwamba kiambishi cha kutendea huathiriwa na irabu ya mzizi na hii ndiyo tungamano ya irabu.
Zaidi sana mofolojia na fonolojia zote ni nyanja za isimu zinazounda maarifa fulani ya lugha kwa kuchunguza sauti na maumbo ya maneno yatokananyo na sauti za lugha hiyo na mpangilio wake. Nyanja zingine za isimu ni kama fonetiki, sintaksia na semantiki.
Mfano:-     Neno
                        Limia
-          Lina sauti tano (5) (kifonolojia) zinazounda
-          Mofimu tatu (3) (kimofolojia)
 Tembea
-          Sauti nne (4)
-          Mofimu mbili (2)
Baada ya kuangalia ufanano huo kwa kina, sasa uelezwe utofauti wa taaluma hizo. Tofauti zinazojitokeza ni pamoja na hizi zifuatazo:-
          Maana, katika kigezo cha maana inaonekana kwamba fonolojia hujihusisha zaidi na uchambuzi wa sauti za lugha mahususi kwa mfano sauti za lugha ya Kiswahili wakati mofolojia inajikita zaidi katika uchambuzi wa maumbo ya maneno. Hapa fonolojia huangalia kuna sauti ngapi zalizounda au zilizotumika katika neno fulani wakati mofolojia huangalia neno fulani limeundwa kwa vipende vingapi
Mfano:-
Lima          - sauti nne (4) /l/, /i/, /m/, /a/ (fonolojia)
-          Vipande au mofimu mbili (2) lim – a (mofolojia)
Jamila       - sauti sita (6) /j/,/a/,/m/,/i/,/l/,/a/
-          Kipande kimoja, jamila
Masikio    - sauti saba (7) /m/,/a/,/s/,/i/,/k/,/i/,/o/
-          Vipande viwili (2) ma + sikio
        Tofauti ya vipashio, kipashio cha msingi cha kifonolojia ni fonimu wakati kipashio cha msingi cha mofolojia ni mofimu.
Mfano:-
Analima    -  fonimu saba (7) /a/,/n/,/a/,/l/,/i/,/m/,/a/
-          Mofimu nne (4) a-na-lim-a
Sema         - fonimu nne (4) /s/,/e/,/m/,/a/
-          Mofimu mbili (2) sem-a
Baya         - fonimu nne (4) /b/,/a/,/y/,/a/
-          Mofimu moja
Ukongwe, taaluma ya fonolojia ni kongwe kuliko taaluma ya mofolojia ambayo ilianza baada ya kuibuka taaluma hii ya fonolojia.
            Dhima ya vipashio, kipashio cha kimofolojia yaani mofimu kina uamilifu mkubwa sana katika lugha hasa kwa kuangalia mofimu huru ambazo huweza kusimama peke yake na kutoa maana kamili mfano baba, mama, safi, nzuri. Maana ya mofimu huru yaweza kuwa ya kileksika ama kisarufi. Lakini pia mofimu funge huleta utegemezi wenye maana sana katika neno ambapo ni tofauti na kipashio cha kifonolojia yaani fonimu ambayo ikiwa peke yake inakuwa haina maana
Mfano:-
Alilala -  kifonolojia /a/, /l/, /i/, /l/, /a/, /l/, /a/
Mofimu hizo hazitakuwa na maana katika muktadha huo, ila tu zitakapoungana kuunda neno.
Alilala – a- mofimu awali ya nafsi ya tatu umoja katika nafasi ya kiima
              -li- mofimu awali ya wakati uliopita katika nafasi ya kiima.
             -lal- mzizi (mofimu kiini)
              -a- kiambishi au mofimu tamati cha maana.     
                                                        
            Mwisho vipashio vy akifonolojia hutengwa katika kila umbo la neno baina ya fonimu moja na nyingine wakati si kila kipande au mofimu katika umbo neno hutengwa. Kwa mfano mzizi na mofimu huru daima hazitengwi.
Mfano:-
Sema        - /s/,/e/,/m/,/a/
-          Sem-a
Juma         - /j/, /u/, /m/, /a/
-          Juma
Safi           - /s/, /a/, /f/, /i/
-          Safi
           Hivyo basi pamoja na kuwepo tofauti hizo taaluma hizi mbili hukamilishana sana kwani uwepo wa taaluma moja hupelekea kuimarika kwa taaluma nyingine na kutokuwepo  kwa taaluma moja hudhoofisha taaluma nyingine. Na hii ndiyo maana hatuwezi kuchunguza sauti za lugha ikiwa lugha hiyo haitakuwa na mfumo na mpangilio maalumu ya maumbo ya maneno na hatutachunguza maneno kama hatutakuwa na sauti zinazopelekea kuundwa kwa maneno hayo.
Powered by Blogger.