JINSI MWANDISHI WA KAZI ZA FASIHI ZA WATOTO NA VIJANA ANAVYOPASWA KUZINGATIA SAIKOLOJIA YA WATOTO NA VIJANA: UCHAMBUZI KUTOKA KATIKA KITABU CHA MWENDO.
JINSI MWANDISHI WA KAZI ZA FASIHI ZA WATOTO NA VIJANA ANAVYOPASWA
KUZINGATIA SAIKOLOJIA YA WATOTO NA VIJANA: UCHAMBUZI KUTOKA KATIKA
KITABU CHA MWENDO.
Fasihi
ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine, mvuto ni kitu cha msingi sana katika
sanaa. Fasihi ya watotona vijana pia kama sanaa ni muhimu pia kuzingatia
kipengele hiki. Kwa mantiki hii, mwandishi ili aweze kufanikisha kuiteka
saikolojia ya watoto na vijana katika kazi yake ni lazima ahakikishe kazi hiyo
inamvuto kwa watoto. Dhana ya mvuto katika fasihi ya watoto na vijana inahusisha
vipengele kadhaa, kabla ya kuangalia vipengele hivi kwa kina ni vema tukafasili
dhana muhimu zinazojitokeza katika swali. Dhana hizo ni pamoja na Fasihi ya
watoto na vijana na dhana ya saikolojia ya watoto na vijana katika kazi za
fashi. Baada ya kuangalia dhana hizi kwa kina ndiposa tutahusianisha na riwaya
ya “Mwendo”.
Kwa
mujibu wa Wamitila (2003) Fasihi ya watoto ni fasihi maalum inayoandikwa kwa
ajili ya watoto.
NOUN
(2010) Wanasema Fasihi ya watoto ni dhana inayorejelea fasihi inayowalenga
watoto pekee. Wanaendelea kusema, Fasihi ya watoto huweza kuwa hadithi,
ushairi, visakale, drama ambazo zimetungwa kwa ajili ya watoto wadogo na vijana.
Vilevile wanaongezea kusema kuwa Fasihi ya watoto inajikita katika mambo makuu
matatu, jambo la kwanza ni endapo mhusika mkuu ni mtoto au kijana, dhamira
inayowahusu watoto na lugha rahisi na Fasihi ya watoto inakuwa fasihi ya watoto
endapo tu wazo na dhamira inahusiana na urahisi wa lugha.
Fasili
zote hizi,zinatupa mwanga hasa juu ya dhana ya fasihi ya watoto na vijana, vitu
vya msingi ni kwamba fasihi hii ni lazima iwe na dhamira pamoja na lugha
rahisi. Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa, fasihi ya watoto na vijana ni sanaa
itumiayo lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyo chini ya umri wa
miaka kumi na minane (18).
Dhana
ya saikolojia ya watoto na vijana tunaweza kusema ni yale mambo ambayo yanatakiwa
kuzingatiwa katika kazi za Fasihi ili kumvutia mtoto na kijana. Sigh na wenzake
(2002) wanasema Fasihi ya watoto na vijana lazima iwe inaonesha matendo na
maisha ya mhusika kinaganaga, mhusika awe anatia hamasa na lazma iwe
inaburudisha.
Kwa
ujumla saikolojia ya watoto na vijana katika kazi za fasihi hulenga yale mambo
ambayo ni lazima yawepo katika kazi hiyo ili kuwavutia watoto na vijana. Kwa
hiyo ili mwandishi afanikiwe kuiteka saikolojia ya watoto na vijana ni sharti
azingatie mambo hayo, mambo hayo ni pamoja na haya yafuatayo:
Kazi
iwe na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto na vijana, miundo migumu
na sentensi ngumu hazipendekezwi kutumika katika fashi ya watoto na vijana
isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Pia
mwandishi anapaswa kuandikia mada inayowavutia watoto na vjiana, kwa mfano
watoto wengi wanapenda kazi zinazosimulia juu jasura, safari na kadhalika kwa
hiyo mwandishi akiandika juu ya mada hizi atakuwa amefanikiwa.
Vilevile
mwandishi anapoandikia hadhira ya watoto na vijana ni lazima hadithi yake iwe
fupi na ya kiutendaji kwani kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo huweza
kupoteza mvuto kabisa kwa watoto.
Mwandishi
anapowachora wahusika wake ni lazima kuwe na mhusika mwema na mhusika mwovu,
kwani hali hii huwavutia sana watoto.
Katika
kazi za fasihi ya watoto, wahusika kama wanyama wapewe uhai, hii huwavutia sana
watoto.
Pia
kazi za fasihi za watoto na vijana sharti ziwe na michezo kwani watoto hupenda
sana michezo.
Kazi
iwe na picha tena za rangi, hii huwafanya watoto kutosahau kwa urahisi kile
walichosoma lakini pia huwasaidia kuhusisha matukio katika hadithi na ulimwengu
halisi.
Taharuki
na fantasia pia ni vitu muhumu katika kazi za watoto, fantasia huleta mvuto wa
pekee katika kazi za watoto na hivyo kufanya watoto wengi kufurahia sana kazi
ambazo zina fantasia.
Kwa
hiyo haya ndio mambo muhimu ambayo kila mwandishi wa kazi za watoto na vijana
anapaswa kuyazingatia pale anapotunga kazi inayowalenga watoto na vijana
kinyume na hapo watoto na vija huweza kutoipenda kazi yake.
Baada
ya kuangalia vipengele muhimu vinavyopaswakujitokeza katika kazi ya watoto na
vijana sasa ni wakati wa kuangalia jinsi vilivyozingatiwa katika riwaya ya
“Mwendo.”
“Mwendo”
ni riwaya iliyoandikwa na Elieshi Lema na kuchapwa na E&D mwaka 1998, ni
riwaya inayohusu mila na tamaduni za kimakonde kwa kuangalia jinsi mila hizi
zinavyomwandaa mtoto kukabiliana na mabadiliko yanayojitokeza katika makuzi
yake. Kwa ujumla riwaya hii inahusu mabadiliko katika makuzi ya mtoto hususani
wa kike.
Mwandishi
wa riwaya hii amejitahidi kuzingatia mambo muhimu katika utunzi wafasihi ya
watoto na vijana ambayo huathiri saikolojia ya watoto na vijana katika kazi ya
fasihi. Vipengele alivyojaribu kuvizingatia mwandishi wa riwaya hii ni pamoja
na hivi vifuatavyo:
Kwa
kiasi kikubwa mwandishi amezingatia kipengele cha picha. Picha katika riwaya
hii zimejitokeza kwa kiasi kikubwa sana na picha zilizotumika zinaendana na
kile kinachosimuliwa. Kwa mfano picha nyingi zinaonesha utamaduni wa kimakonde
wa kuchonga vinyago; na hivyo mtoto au kijana anaposoma riwaya hii anakuwa
anavutiwa na hizi picha kwa hiyo anapata ujumbe kwa urahisi, hii inamfanya
mtoto apende kuendelea kusoma riwaya hii.
Mhusika
mkuu ni mtoto, mwandishi amemtumia Felisia kama mhusika mkuu. Felisia ni mtoto
ambaye anasoma darasa la saba mwandishi amemtumia kuwakilisha watoto wengine
ambao wanaumri kama wake na ambao
wanahitaji kujua hatua za makuzi yao. Kwa hiyo kazi alizopewa Felisia kama
mhusika mkuu zinasadifu uhusika wake kama mtoto. Wahusika wengine watoto ni
Hamiata, Bene na wanafunzi. Kwa hiyo mtoto atakapoona kuwa wahusika wakuu katika riwaya hii ni
watoto wanaweza kushawishika kusoma kazi hii.
Wazo
kuu la riwaya linawalenga watoto, hiki pia ni kipengele muhimu sana katika
utunzi wa fasihi ya watoto na vijana kama wazo kuu haliwalengi watoto na vijana
ni hakika kazi hiyo haitapokelewa vema. Katika riwaya hii mwandishi ameonesha
ni jinsi gani watoto wanavyopata changamoto katika makuzi yao hususani watoto
wa kike, kwa hiyo amefanikiwa katika kipengele hiki.
Vilevile
katika riwaya hii mwandishi ametumia lugha ambayo ni rahisi kueleweka, miundo
ya sentensi sio migumu pia vielevile msamiati mgumu au misemo migumu
haikutumika katika riwaya hii. Kwa msingi huo mtoto hatapata ugumu wowote
anaposoma riwaya hii na hivyo atapenda kuendelea kuisoma.
Pia
mhusika mkuu (Felisia) amechorwa vizuri; watoto wanapenda mhusika mkuu achorwe
vizuri, mwandishi wa riwaya hii amefanikiwa kufanya hivyo kwani amemchora
Felisia kama mhusika shujaa na mwema,
baada ya kupitia vikwazo mbalimbali kwa mfano, kuzuiwa kuendelea na masomo
lakini tunaona mwishoni anafanikiwa kurudishwa darasani na anashangiliwa na
wanafunzi wenzake (ukurasa 65). Watoto wanapenda hali kama hii ionekane katika
kazi zao.
Taharuki
imetumika katika riwaya hii. Taharuki ni chombo muhimu sana katika fasihi ya
watoto na vijana, taharuki inamfanya msomaji wa hadithi aendelee kusoma ili
ajue kile kinachofuatia. Katika riwaya hii taharuki zinazoonekana ni pale
ambapo Felisia alionekana kukata mawasiliano ghafla na rafiki yake Hamiata
(ukurasa 3 na 4), mwandishi hakuonesha sababu yoyote hivyo kumfanya msomaji
kuendelea kusoma ili kujua kilichompata Felisia.Taharuki nyingine ni pale
ambapo Felisia alifungiwa ndani kwa muda wa mwezi mmoja, akiwa ndani alijiuliza
maswali juu ya nini kitakachofanyika siku ya kuchezwa unyago, alijiuliza
huwenda atakeketwa na kutoka damu au ni kitu gani kitakachofanyika. Hivyo
katika hali kama hii taharuki hutokea na kumfanya msomaji aendelee kusoma ili
kujua nini kitakachotokea.
Matumizi
ya fantasia pia yameonekana katika riwaya hii. Katika (ukurasa wa 14) kuna
hadithi inayosimulia juu ya mwanamme akitembea juu ya nyayo lakini cha kushangaza
anasikia nyayo zinaonge, “aaah, mbona unanikanyaga sogea kando”. Kwa hiyo hii
ni fantasia ambayo humfanya mtoto aifurahie riwaya hii anapokuwa anasoma.
Fantasia nyingine inapatikana (ukurasa 20) hapa tunaona matukio ya ajabu,
kitendo cha mwanamke kuongea na mzimu na kisha kuilekeza njia sio jambo la
kawaida katika ulimwengu halisi, hivyo hii pia humfanya mtoto apende kusoma
riwaya hii kwa sababu ya maajabuajabu haya.
Kitu
kingine kinachowavutia watoto na vijana ni mwisho mzuri wa hadithi. Katika
riwaya hii mwandishi amezingatia kipengele hiki. Tunaona mhusika mkuu
amefanikiwa kurejea darasani lakini pia tunaona amefanikiwa kuondoa wasiwasi
wake baada ya kupata elimu ya makuzi anaonekana kujiamini na anaonekana kuwa
tayari kukabiliana na ukubwa. Kwa ujumla riwaya hii imeisha vizuri, Felisia na
Hamiata wanaonekana kufurahi. Kwa hiyo mtoto atakaposoma riwaya hii naye
atafurahi kwani imeisha kwa furaha na sio kwa huzuni.
Hata
hivyo licha ya mwandishi kutumia vipengele muhumu vinavyoteka saikolojia ya
watoto katika fashi yao pia ameonesha udhaifu, udaifu huo unajitokeza katika
vipengele vifuatavyo:
Riwaya
ni ndefu.Watoto hawapendi hadithi ndefu, wanaposoma hadithi na kuona ni ndefu
sana huwa wanakata tamaa, na hatimaye huacha kuendelea kusoma.Riwaya hii ina
kurasa sabini kwa hiyo ni ndefu sana kwa watoto. Kwa hiyo mwandishi anaonekana
kushindwa katika kipengele hiki.
Haina
michezo. Watoto wanapenda michezo ionekane katika hadithi zao, hii itawafanya
wasichoke kusoma hadithi na hivyo kwa njia hii ujumbe utawafikia kwa urahisi.
Katika riwaya hii mwandishi hakuzingatia kipengele hiki.
Vilevile
riwaya hii sio ya kiutendaji, imejikita katika masimulizi kwa kiasi kikubwa
hali ambayo huwachosha watoto wanapokuwa wanasoma hadithi za namna hii. Kwa
hiyo watoto hawatavutiwa na riwaya ya namana hii kwa sababu haina utendaji,
wahusika sio wa kiutendaji, hivyo mwandishi ameshindwa katika hili.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa mwandishi wa riwaya hii amezingatia kwa kiasi
kikubwa saikolojia ya watoto katika utunzi wake. Matumizi ya fantasia,
taharuki,picha, lugha nyepesi na kadhalika ni nyenzo muhimu katika kuvutia
watoto kupenda kazi yake. Kwa hiyo riwaya hii sio rahisi kukimbiwa na watoto
kwani vipengele vingi vinavyohitajika
katika fasihi ya watoto vimezingatiwa. Hata hivyo wandishi angefanikiwa kabisa
kuiteka saikolojia ya watoto endapo riwaya ingekuwa ya kiutendaji, yenye
michezo na fupi, kwa kuwa vipengele hivi havipo mtoto atakapokuwa anasoma
riwaya hii atahisi vitu fulani vinakosekana. Kwa hiyo ni vema waandishi
wazingatie saikolojia ya watoto na vijana kwa upekee wake wanapokuwa wanatunga
kazi za fasihi inayowalenga watoto na vijana.
MAREJEO
Lema,
E. (1998).Mwendo. Dar es salaam:
E&D.
NOUN
(2010).Children’s Literature. Lagos:
National Open University of Nigeria.
Sigh,
M.na wenzake (2002). “Heroes and Heroine in Children’s Literature around the
world” katika http://www.ericdigests.org/2004-1/heroes.htm
17.05.2012, 12:24.
Wamitila,
K.W. (2003).Kamusi ya Fasihi, Istilahi na
Nadharia. Nairobi: Focus Publication.