CHIMBUKO LA USHAIRI.
CHIMBUKO
LA USHAIRI.
Katika makala hii tutajadili kwa kina kuhusu chimbuko la ushahiri wa Kiswahili kwa kutumia nadharia mbili kama kiunzi cha uchambuzi huu. Kabla ya kueleza chimbuko la Kiswahili ni vyema tukaeleza nini maana ya ushairi. Dhana ya ushairi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili yake. Baadhi ya wataalam hao ni kama ifuatavyo:
Shaban Robert, anasema; “ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari wa maneno.
Mnyampala anasema kuwa “ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho kitu kilichobora sana katika maongozo ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.”
Amri Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.”
Wataalamu wengine wanaeleza kuwa ushairi ni kauli zenye hisia na ubunifu, mpangilio fulani wenye urari, uwasilishaji wa tajiriba au mawazo ya mtunzi kwa maana ambayo huibua tajiriba kama hiyo katika nyayo za wasomaji au wasikilizaji na kutumia lugha ya picha yenye wizani wa sauti.
Mulokozi na Kahigi (1982) wanasema ushairi ni “sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum na fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.”
Hivyo basi kutokana na fasili za wataalamu mbalimbali tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi. Hii ina maana kwamba ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na ujumbe unaogusa hisi za wasomaji au wasikilizaji.
Baada ya kuana maana ya ushairi pia dhana ya chimbuko inafasiliwa na TUKI (2004) kuwa ni mwazo au asili ya kitu.
Baadhi ya wataalamu wameweza kuelezea chimbuko la ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia mitazamo au nadharia mbili ambazo ni kama zifuatazo:
Nadharia ya kwanza inadai kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu.
Na nadharia ya pili inasema kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la jamii ya waswahili wenyewe.
(1) CHIMBUKO LA USHAIRI NI UJIO WA WAARABU
Nadharia hii ya kwanza isemayo kuwa chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu ambayo inaungwa mkono na wataalam mbalimbali kama vile Lyndon Harries (1962) na Knappet (1979)
Kwa mujibu wa Lyndon (1962) “Swahili Poetry” anatoa hoja tatu ambazo kwa yeye zinadhibitisha kuwa ushairi wa Kiswahili umetokana na uarabu. Hoja hizo ni ushairi wa Kiswahili umetokana na Uislamu, ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa Kenya hususani Lamu. Na maudhui ya ushairi wa Kiswahili yalitokana na ushairi wa Kiarabu. Utungo wa kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka, Mwengo bin Athmani (1728)
Kutokana na nadharia hii ubora wake ni kwamba nadharia hii au mtazamo wa Harries kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni kwamba umesaidia wengine kuendelea kuchunguza zaidi kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili.
Lakini nadharia hii ina udhaifu kwani si kweli kwamba ushairi wa Kiswahili uliletwa na Uislamu bali ulikuwepo hata kabla ya ujio wa Uislamu, kwani ushairi hautenganishwi na jamii husika. Hivyo jamii za waswahili walitumia nyanja mbalimbali za ushairi katika shughuli zao mbalimbali au shughuli zao za kila siku, kama vile; shughuli za kilimo na ufugaji.
Pia ushairi wa Kiswahili ulianza karne ya 10BK na ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa. Wataalam wengi wanakubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo.
Pia udhaifu mwingine katika mtazamo wake wa kusema kuwa ushairi ulianzia pwani ya kaskazini ya Kenya si kweli kwa kuwa waswahili walikuwepo hata sehemu nyingine kama vile Kilwa na Bagamoyo ambapo ushairi wa Kiswahili ulitumika.
Hivyo tunaweza kusema kuwa hoja ya kusema ushairi wa Kiswahili ulitokana na Kiarabu haina mashiko kwa kuwa waswahili walikuwepo hata kabla ya waarabu na walikuwa na ushairi wao isipokuwa ujio wao ulileta athari kubwa kwa kuwa ulichanganya na mambo ya dini ya kiislamu pamoja na hati.
Naye Knappert (1979) “Four centuries of Swahili verse” anasema; “Ushairi wa Kiswahili ulichipuka kwenye upwa wa Kenya kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na ulianza katika karne ya 17 na pia ni ushairi wa Kiislamu wenye kuchanganya sifa za tungo za kiafrika na za kiajemi.
Mkabala huu una ubora kwani Knappert amekubali kuwa, ushairi wa Kiswahili ulitokana na waswahili wenyewe.
Hata hivyo hoja yake ina udhaifu kidogo kwani ushairi wa Kiswahili ulianza kabla ya karne ya 10 BK na pia amejikita katika maudhui ya mambo mengine kama vile siasa, uchumi na kijamii. Vilevile amechanganya chimbuko la ushairi wa Kiswahili na Uarabu.
(2) USHAIRI NI ZAO LA WASWAHILI WENYEWE
Nadharia hii ya pili inasema kuwa ushairi ni zao la waswahili wenyewe. Nadharia hii imejadiliwa na wataalamu mbalimbali akiwemo Shaban Robert, Jumanne Mayoka (1993) na F.E.M.K. Senkoro, Mulokozi na Sengo.
Kwa mujibu wa Mayoka (1993) anasema ushairi umetokana na jamii ya wanadamu wenyewe na umesheheneza ukwasi mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika katika hatua zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika historia ambayo mwanadamu amepitia, Kwa mfano kuwa msamiati uliotumika tangu enzi za kuishi mapangoni, enzi za uwindaji, ujima, utumwa, vita vya makabila, uvamizi wa wageni, ukoloni na harakati za kupambana na ukoloni hadi kupata uhuru na maendeleo yake.
Kwa mujibu wa nadharia hii tunaweza kupata ubora wa nadharia. Ubora wa hoja hii ni kwamba, kila jamii ina sanaa yake na ushairi ni moja kati ya sanaa hizo ingawa inaweza ikaathiriwa na sanaa ya jamii nyingine. Pia ushairi umekuwa ukikua na kuendelea kadri jamii inavyokuwa na kuendelea.
Ingawa upo ubora lakini kuna mapungufu kadhaa. Udhaifu wa hoja hii ni kwamba si kweli kuwa katika kipindi hicho ushairi ulikuwa tayari umesheheni ukwasi mkubwa wa lugha, na kama ulikuwa kweli umesheheni huu ukwasi wa lugha alipaswa kutuonesha huo utajiri wa lugha anaouzungumzia katika ushairi.
Senkoro (1988) anasema kuwa ushairi uliibuka pale lugha ilipoanza katika kipindi cha uhayawani (kipindi ambacho mwanadamu alipoanza kupambana na mazingira yake) kwenda katika kipindi cha urazini (maana) ili kumwezesha binadamu na mazingira yake kwa mfano, zana za kazi zilizotumika ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana hizo.
Hoja hii inathibitisha kuwa chimbuko la ushairi ni waswahili wenyewe, kwani umefanikiwa kueleza kuwa katika jamii yoyote ile maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii huambatana au huenda sambamba na maendeleo ya sanaa mbalimbali ikiwemo ushairi uliotumika katika harakati mbalimbali za maisha ya mwanadamu.
Pamoja na kuwa nadharia hii imeonesha kukubalika na wataalamu mbalimbali kama vile Senkoro, Mayoka na Shekhe Amri Abeid, lakini bado ina mapungufu. Hii ni kwa sababu imeshindwa kuonesha muda maalumu ambapo ushairi wa Kiswahili ulianza na ni wapi ulianza kutumika. Hili ni suala ambalo linahitaji uchunguzi wa kina ili kulibaini.
Hivyo basi, kutokana na nadharia hizo mbili tunaungana na nadharia inayosema kuwa, chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la waswahili wenyewe, kwa sababu waswahili wana utamaduni wao ambao ulikuwepo kabla ya ujio wa Waarabu. Na waliutumia ushairi huo katika shughuli mbalimbali za kijamii, kwa mfano katika harusi, jando na unyago.
MAREJEO:
Knappert, J. (1979). Four
centuries of Swahili Verse. Heinemann. London.
Mayoka, J.K. (1993). Mgogoro
wa Ushairi na Diwani ya Mayoka. Ndanda Mission
Press.Tanzania.
Mulokozi, M.M. (1996). Fasihi
ya Kiswahili.Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.
Dar-es-Salaam.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Ushairi,
Nadharia na Tahakiki. DUP. Dar-es-Salaam.
TUKI. (2004). Kamusi ya
Kiswahili Sanifu.TUKI.Dar-es-Salaam.