SWALI: Jadili uhusiano wa fasihi simulizi na fasihi andishi.
UTANGULIZI
Tangu
kutawala kwa fasihi andishi Ulaya, Asia na kutumiwa na wenye nguvu za
kisiasa na kiuchumi fasihi simulizi ilidharauliwa ikatwezwa, ikadunishwa
na kushushwa hadhi huku fasihi andishi ikitukuzwa na kuendelezwa.
Taaluma ya fasihi simulizi hivi leo inashughulikiwa kwa nguvu nyingi ili
kuondokana na fikra duni zilizorithiwa toka kwa wataalamu wa kigeni
kuwa sanaa kongwe ya fasihi simulizi ni ya kishenzi. Pamoja na dharau
juu ya fasihi simulizi bado ukweli unabaki kuwa sanaa hii ndiyo ghala
halisi la fasihi andishi. Hata sasa imebainika kuwa tenzi za Kigiriki
zinazodaiwa kutungwa na manju aitwaye “Home” hazikuwa zimeandikwa kwa
zaidi ya miaka miatano (500) ndipo baadaye zikaja kuhifadhiwa katika
maandishi. Hivi majuzi pia wanateknolojia wameanza kukubali kuwa sehemu
kubwa ya Biblia ni fasihi simulizi ya Wayahudi walioishi zama
mbalimbali. Kimsingi fasihi simulizi na fasihi andishi ni kitu kimoja
isipokuwa njia zinazotumiwa na fanani na hadhira katika kuwasilisha
ujumbe.
KIINI
Fasihi simulizi na fasihi andishi zinahusiana katika vipengele mbalimbali kama ifuatavyo:
(i) Fasihi
simulizi huweza kuwasilishwa kupitia maandishi na fasihi andishi huweza
kutumia ala za fasihi simulizi kunogesha kazi yake na kufikisha ujumbe
wake. Hivyo maandishi sio kigezo cha kuitenganisha kabisa fasihi
simulizi na fasihi andishi.
(ii) Ukichunguza
kazi mbalimbali za fasihi andishi utabaini kila mwandishi ameathiriwa
na fasihi simulizi kwa namna fulani. Wapo walioathiriwa kifani na
wengine kimaudhui.
(iii) Zote mbili ni kazi za sanaa zinazotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa hadhira yake.
(iv) Pili fasihi simulizi na fasihi andishi zote mbili zinaundwa kwa fani na maudhui
(v) Zote ni kazi za kisanaa zitumiazo maneno teule kufikisha ujumbe
(vi) Zote maudhui yake humhusu mwanadamu na maisha yake katika kumletea maendeleo katika Nyanja zote.
HITIMISHO
Fasihi simulizi na fasihi andishi ni sanaa za lugha zinazotofautiana njia za uwasilishaji tu lakini maudhui yake yanafanana.