Ufeministi, itikadi na misingi yake (8)
Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu ya 8 ya kipindi
cha Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake. Katika kipindi cha wiki
iliyopita tulizungumzia baadhi ya misingi ya kifikra ya ufeministi ikiwa
ni pamoja na kupuuza tofauti za kimaumbile ya kibiolojia za mwanamke na
mwanaume na vilevile itikadi ya kuwapiga vita wanaume. Tulisema baadhi
ya mafeministi wanaokana suala la kuwepo tofauti za kimaumbile kati ya
mwanamke na mwanaume wanamtambua mwanaume kuwa ni adui mkuu wa mwanamke
na wanasisitiza juu ya udharura wa kupambana naye. Tulisisitiza kuwa
fikra hii inapingana na itikadi na mafundisho ya Uislamu unaomtambua
mwanamke na mwanaume kuwa wanakamilishana ndani ya familia na katika
jamii. Kipindi chetu cha leo kitaendelea kuzungumzia itikadi za
kifeministi na kukosoa misingi ya mrengo huo katika mtazamo wa dini ya
Uislamu. >>>>> <
Miongoni mwa misingi ya kifikra ya ufeministi ni kupinga na
kutupilia mbali mafundisho ya dini. Mafemenisti wanayaona mafundisho ya
dini kuwa yanachangia katika kuimarisha utamaduni wa mfumo dume, kwa
msingi huo wanaamini na kufuata thamani za kimaada na kupinga thamani za
kidini. Wanasema thamani na mafundisho ya dini ndiyo kizuizi kikuu
katika njia ya kufikiwa malengo yao kwani wanaamini kuwa dini za
Mwenyezi Mungu zinathamini na kutukuza sana familia na nafasi ya mama,
na ili kulinda nafasi hiyo zinamzuia mwanamke kushiriki katika baadhi ya
mambo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika. Vilevile wanasema
dini zinashajiisha na kuhamasisha uzazi na kuzaa, na zinakataza kuavya
mimba na kuwalazimisha watu kuzilinda na kulitambua suala hilo kuwa ni
sawa na kulinda nafsi ya mwanadamu mzima. Suala hili- wanasema
mafeministi- linawaelekeza wanawake katika kuzaa na kujizuia kuavya na
kutoa mimba. Hata hivyo kwa mtazamo wa mafeministi, kulindwa thamani na
mambo kama haya ndiyo kizuizi kikuu cha uhuru wa mwanamke katika suala
la maingiliano ya ngono na kupata burudani na anasa; hivyo basi kuna
haja ya kufanyika jitihada za kujiweka mbali na thamani na mafundisho ya
dini!
Inasikitisha kwamba, mafeministi wanaghafilika kwamba,
kadiri unavyojiweka mbali na kujitenga na dini na masuala ya kiroho
ndivyo unavyopata hasara zaidi. Hii leo mfumo wa familia umekumbwa na
mgogoro katika jamii ya Magharibi. Wanafikra na wasomi wengi wanaamini
kuwa, miongoni mwa sababu za mgogoro huo ni kujitenga na kuwa mbali na
mafundisho ya dini na masuala yaa kiroho. Mwandishi wa Marekani, Patrick
J. Buchanan, anasema waziwazi katika kitabu alichokipa jina la “Kifo
cha Magharibi” kwamba: Magharibi imo katika hali ya kugawanyika,
kutoweka na kufa. Anasema ubinafsi, kutojenga na kuanzisha familia,
kutozaa watoto, kuongezeka kiwango cha utoaji wa mimba, talaka, vitendo
vya kuingiliana kinyume na maumbile na kujamiiana watu wenye jinsia
moja, utumiaji uliokithiri wa dawa za kulevya, jinai za kutisha
zinazohusiana na masuala ya ngono na kadhalika katika nchi za Magharibi
vinatokana na kusambaratika mfumo wa familia na masuala ya kiroho. Kwa
mfano tu, mwandishi Buchanan anasema kuhusiana na suala la kuzaa kwamba:
Kuanza kuzama na kutoweka Ukristo katika nchi za Magharibi kulifuatiwa
na tukio jingine. Watu wa Magharibi waliacha kuzaa watoto kwa sababu
kuna mfungamano baina ya imani ya dini na kuwa na familia zenye jamii
kubwa, na kadiri watu wanavyoshikamana na dini ndivyo kiwango cha kuzaa
watoto kinavyoongezeka”, mwisho wa kunukuu.
Mafemenisti wamefanya jitihada za kueneza na kuhubiri
misingi yao ya kifikra katika jamii kupitia nadharia za malezi ya
kimaada. Wanaamini kuwa mtazamo jumla wa jamii nyingi unawadunisha
wanawake na kuwafanya watu wa daraja la pili. Kwa msingi huo
wanasisitiza juu ya kubadilishwa mtazamo wa jamii kuhusu wanawake na
kufutwa ubaguzi unaolenga jamii hiyo. Hapa inatupasa kusema kuwa, kila
mtu mwenye insafu anajua kwamba, mijadala inayohusiana na haki za
wanawake na mafeministi na wito wa kufanyika mabadiliko katika mtazamo
unaowaona wanawake kuwa ni wanadamu wa daraja la pili katika nchi za
Magharibi na vilevile juhudi za mafeministi za kupigania haki zao za
kisiasa, kijamii na kichumi vimepelekea kupatikana baadhi ya mafanikio
kwa maslahi ya wanawake hususan katika nchi za Magharibi. Hata hivyo
suala la kupigania haki za wanawake na kupambana na ubaguzi halipasi
kuwa kisingizio cha kutokomeza na kuua maana ya maisha, kumdunisha
mwanaume katika jamii na kulazimisha haki na majukumu sawa na
yanazofanana licha ya tofauti za kimaumbile baina ya jinsia mbili za
wanadamu. >>
Kinyume na dhana za mafeministi, thamani, matukufu na
majukumu ya kimaumbile na kaida zilizokubalika na mwanaume na mwanamke
zinasaidia sana katika kuimarisha zaidi mfungamano wa ndoa. Kwa sababu
hiyo katika familia ambazo wanaume hukosa hadhi na thamani, uwezekano wa
wanaume kukimbia majukumu yao ya kusimamia familia pia huwa mkubwa
zaidi. Vilevile kila majmui na kundi lenye uongozi na utaratibu mzuri
linaweza kufikia malengo yake vizuri na vyema zaidi. Uongozi ndani ya
familia pia ni sehemu ya dharura ya uongozi wa jamii yenye malengo
ambayo wanachama wa familia husika wanapaswa kushikamana nayo ili kuweza
kupiga hatua za maendeleo ya kimaada na kiroho. Iwapo nyumba na familia
haitakuwa na mudiri na kiongozi, na mke na mume wakawa sawa katika
kuongoza maswala ya familia, hapana shaka kwamba watalazimika kwenda
mahakamani mara kwa mara kwa ajili ya kusuluhisha hitilafu zao au kutoka
nje ya familia kutafuta utatuzi, suala ambalo si rahisi kuwezekana
wakati wote. Suala hilo huwa sababu ya kuzorota uhusiano wa kifamilia.
Msingi wa mantiki na akili ni kuwepo mudiri na mwendeshaji wa masuala ya
nyumba na familia mwenye ustahili. Na kwa kuwa aghlabu na kwa ujumla
mwanaume huwa na uwezo mkubwa wa kusimamia masuala mbalimbali ya familia
na vilevile kukabiliana na mikikimikiki na changamoto za aina
mbalimbali, huwa ndiye kiongozi na msimamizi wa masuala ya familia
kiujumla. Suala hili linaashiriwa katika aya ya 34 ya Suratul Nisaa
inayosema: Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kutokana na fadhila
alizowapa Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi…”. Ni wazi kwamba,
wanaume kwa ujumla ni bora zaidi kuliko wanawake katika masuala ya
uendeshaji wa masuala ya kiuchumi, kijamii, uwezo wa kulinda familia na
kadhalika. Hata hivyo ubora huu wa kiujumla hauna maana ya ubora wa
kidhati wa mwanaume juu ya mwanamke kwa sababu mwanamke na mwaname
wanashirikiana katika dhati ya ubinadamu na katika uwezo wa kufanya
jitihada za kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, suala ambalo halihusu
jinsia ya mtu. Katika upande mwingine tunapaswa kuelewa kwamba, Uislamu
umemlazimisha mwanaume kudhamini mahitaji yote ya mwanamke na familia na
mkabala wake amepewa pia majukumu ya kusimamia na kuendesha masuala ya
familia yake.
Katika mtazamo wa Uislamu maslahi ni kumwepusha mwanamke
kadiri ya uwezo kufanya kazi ngumu na nzito na kumbebesha mwanaume
jukumu la kudhamini na kukidhi mahitaji ya kimaisha ili mwanamke aweze
kutekeleza ipasavyo majukumu yake kama mke na mama. Hali hii huifanya
familia kuwa kituo chenye utanashati, upendo na mahaba.
Miongoni mwa itikadi za kifemenisti ni kugeuza kabisa
nafasi za wanaume na wanawake. Mafemenisti wanaamini kuwa, nafasi na
mchango wa wanaume na wanawake katika jamii na familia zinapaswa
kuarifishwa upya kwa mujibu wa usawa kamili baina ya jinsia hizo mbili
kwa sababu -kwa mtazamo wao - hakuna tofauti yoyote kati ya wawili hao.
Kwa mtazamo wao, itikadi kwamba kazi nzito na za kiufundi zinapaswa
kufanywa na wanaume na kwamba wanawake wanapaswa kufanya kazi nyepesi na
za kuvutia, inapaswa kubadilishwa. Hata hivyo katika mtazamo wa Uislamu
mwanaume na mwanamke hawafanani katika pande nyingi kwa sababu
wanatofautiana katika mambo mengi ya kimaumbile. Kwa msingi huo ni
makosa kuwapa watu wanaotofautiana kimaumbile kazi sawa na majukumu
yanayofanana. Kwa maana kwamba, kutofautiana katika sifa za kimaumbile
kunapaswa kufuatiwa na kutofautiana katika majukumu na nafasi ya jinsia
hizo mbili. >
Kipindi chetu kinaishia hapa kwa leo. Msikose kufuatilia mfululizo wa kipindi hiki wiki ijayo.