Uhusiano wa Sintaksia na Matawi mengine ya Isimu
Uhusiano wa Sintaksia na Matawi mengine ya Isimu
Dhana
ya sintaksia imejadiliwa na wanazuoni mbalimbali ;
Massamba na wenzake (1999:34)
anasema “sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na uchunguzi wa mpangilio
wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipasho vyake”. Wanaendelea kusema, utanzu
huu huchunguza sheria au kanuni
zinazofuatwa katika kuyapanga maneno ili yalete maana inayokubalika na
kueleweka katika lugha husika.
Habwe na Karanja (2004) wanasema
“sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi
nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi”
TUKI (2004)anasema “sintaksia ni tawi
la isimu linaloshughulikia uchanganuzi wa taratibu na kanuni za mahusiano baina
ya maneno katika tungo” kwa ufupi sintaksia ni tawi la isimu ambalo
linachunguza muundo wa tungo pamoja na uhusiano wa vipashio hivyo vinavyounda
tungo ambayo ni nukta pacha, neno, kirai na kishazi.
Kwa ujumla sintaksia ni tawi la
isimu ambalo linahusu namna maneno yanavyoungana na kuhusiana kirai, kishazi na
sentensi. Sintaksia inachunguza namna maneno yanavyojipanga katika sentensi kwa
kuzingatia kanuni za sarufi ya lugha husika.
Kwa hiyo kutokana na kwamba sintaksia
pia ni kitengo mojawapo kinachounda maarifa ya lugha, kwamba, sintaksia haiwezi
kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kutokana na uhusiano mkubwa uliopo
baina ya vitengo hivi. Vitengo hivi hutegemena na kuathiriana. Hivyo basi
tunaweza kuonesha jinsi sintaksia isivyoweza kutenganishwa na vitengo vingine
vya lugha yaani fonolojia, mofolojia na semantiki kama ifuatavyo:
Uhusisno
uliopo kati ya sintaksia na fonolojia.
Massamba na wenzake (1999:34)
wanasema “fonolojia ni uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha mahususi” Ni
jinsi ambavyo vitamkwa au sauti za lugha zinavyoungana ili kujenga maneno
yanayokubalika katika lugha. Ni dhahiri kwamba kuna uhusiano usio na mashaka
kati ya sintaksia na fonolojia kwa sababu hatuwezi kuwa na miuundo mikubwa bila
kuwa na mpangilio sahihi wa sauti katika lugha.
Mfano
1. ‘anacheza’ hili ni neno lakini pia ni sentensi, hivyo linaweza
kuchanganuliwa kifonolojia
kama, /a/n/a/ch/e/z/a/. kwa hiyo mpangilio sahihi wa sauti hizo ndizo
zinazounda neno ‘anacheza’.
Mfano
2 (a). neno “debe” neno hili limeundwa na konsonanti irabu konsonanti irabu
(KIKI).
2. (b). “edbe” hili limeundwa na
irabu konsonanti konsonanti irabu (IKKI).
Katika
mfano 2a, neno “debe” lina maana na limefuata kanuni na mpangilio unaokubalika
katika lugha ya Kiswahili, lakini katika mfano 2b neno “edbe” halina maana
katika lugha ya Kiswahili kwa sababu halina mpangilio sahihi wa vitamkwa au
fonimu.
Kwa
hiyo mpangilio sahihi wa sauti katika maneno ndio husaidia kupata vipashio
vikubwa zaidi katika lugha kama vile kirai, kishazi na sentnsi. Kwa hiyo
sintaksia na fonolojia haviwezi kuenganishwa.
Uhusiano
uliopo kati ya sintaksia na semantiki.
Habwe na Karanja wakimnukuu Richard na
Wenzake (1985) wanasema “Semantiki ni stadi ya maana. Semantiki ni utanzu
unaochunguza maana katika lugha ya mwandamu”. Wanaendelea kusema semantiki
hutafiti maana za fonimu, mofimu, maneno na tungo. Hivyo kutokana na fasili hii
maana hushughulikiwa katika vitengo au viwango vyote vya lugha ambavyo ni
fonolojia, mofolojia na sintaksia. Kwa mfano,
1 Mtoto
mtiifu amefaulu mtihani.
2 Mtihani
mtoto amefaulu mtiifu.
3 Mtiifu
mtoto mtihani amefaulu.
Katika
mifano hii sentensi (1) ina maana kutokana na kwamba imefuata mpangilio sahihi
wa maneno katika tungo na sentesi zilizobaki hazina maana kutokana na sababu
kwamba hazijafuata mpangilio ulio sahihi wa kimuundo katika lugha ya Kiswahili.
Kwa mantiki hii, kwa kuwa semantiki hushughulikia viwango vyote vya lugha, basi
hushughulikia pia kiwango cha sintaksia ambapo huangalia maana za tungo, kwani
tungo lazima ikubalike kwa wazungumzaji wa lugha husika, pia tungo lazima ilete
maana. Kwa mantiki hiyo kuna uhusiano usio na mashaka kati ya sintaksia na
semantiki kwa sababu mpangilio sahihi wa maneno katika sentensi ndiyo huleta
maana na bila mpangilio sahihi wa maneno maana hupotea.
Uhusiano
uliopo kati sintaksia na mofolojia.
Besha (2007:49) anasema “mofolojia ni
taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wa maneno katika lugha’.Pia Rubanza
(1996:1) anasema “mofolojia ni taaluma inayoshughulikia vipashio vya lugha
katika kuunda maneno”. Maumbo ya kimofolojia huathiri vipengele vingine vya
kisintaksia kama vile kipengele cha umoja na wingi, katika maumbo ya
kimofolojia ndicho kinachoathiri umbo linalofuata jina na kuathiri muundo wa
sentensi nzima. Kwa mfano,
1 Mtoto
alikuwa anajifunza kusoma.
2 Watoto
walikuwa wanajifunza kusoma.
Katika
mifano hii kiambishi m- na wa- katika upande wa kiima vimeathiri
utokeaji wa viambishi a- na wa- katika upande wa kiarifu. Hivyo
taaluma ya sintaksia na mofolojia haziwezi kutenganishwa.
Kwa ujumla sintaksia kama tawi mojawapo la
isimu linauhusiano wa moja kwa moja na matawi mengine kwani haiwezi
kutenganishwa na vitengo vingine vya lugha kutokana na uhusiano mkubwa uliopo
baina ya vitengo hivi. Hutegemeana na kuathiriana kwa kiasi kikubwa, mfano
huwezi kupata mofolojia bila kupitia ngazi ya fonolojia na pai huwezi kuwa na
ngazi ya sintaksia bila kupitia ngazi ya fonolojia na mofolojia lakini vitengo
vyote hivi hutawaliwa na kitengo cha semantiki ili kuleta mawasiliano miongoni
mwa wazungumzaji.
MAREJEO
Besha,
R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Mackmillan Aidan
Habwe,
J na P. Karanja (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.
Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Massamba,
D.P.B na wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu: Sekondari
na Vyuo. Dar essalaam:
TUKI.
Rubanza,
Y.I (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania.
TUKI
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI.