VIPENGELE VYA KIFANI KATIKA RIWAYA

 
 VIPENGELE  VYA KIFANI KATIKA RIWAYA
SWALI: Jadili kipengele cha fani katika riwaya ya Bina-Adamu kwa kuzingatia mielekeo chomozi ya kifani katika riwaya ya Kiswahili ambayo ni:

Mwendo wa riwaya.
Naratolojia.
Msuko wa vitushi.
Uhusika na wahusika.
Mtagusano.
Kipengele cha lugha.
Mbinu za kibunilizi.
Mtindo.

YALIYOMO
UTANGULIZI…………………………………………………………………………….…..1
v  Historia fupi ya mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu. ……………...……1
v  Baadhi ya kazi zake alizowahi kuandika……………………………………....1
v  Muhtasari wa riwaya hii……………………………………………………..…1
v  Uainishaji wa riwaya hii kwa kujigeza katika kigezo cha fani………………….2
KIINI CHA KAZI……………………………………………………………………...……....2
v  Mielekeo chomozi ya fani katika riwaya hii……………………………………2
Ø  Naratolojia………………………………………………...…………….2
Ø  Msuko wa vitushi…………………………………………...…………..3
Ø  Mwendo wa riwaya………………………………………...…………...6
Ø  Mtindo……………………………………………………...…………...7
Ø  Uhusika na wahusika……………………………………...…………….9
Ø  Mianzo na miisho ya riwaya  .………………………………………….10
Ø  Mtagusano……………………………………………….…………….11
Ø  Kipengele cha lugha…………………………………….……………..12
Ø  Mbinu za ubunilizi……………………………………….…………….15
§  Taharuki...…………………………………….……………...15
§  Utomeleaji…………………………………….……………...16
§  Ujadi………………………………………………….………17
§  Ufumbaji……………………………………………..……….17
§  Dayolojia………………………………………….….……...18
§  Usawili wa wahusika…………………………………..……..19
§  Ulinganuzi na usambamba………………………...………….20
§  Mbinu ya majazi…………………………………..………….20
HITIMISHO………………………………………………………………….………………21
MAREJELEO……………………………………………………………………..………….22
Bina-Adamuni riwaya iliyoandikwa na Wamitila KyalloWadi na kuchapishwa na Phoenix Publishers mwaka 2002, Nairobi, Kenya.
Wamitila KyalloWadializaliwa mwaka 1966 katika nchiya Kenya. Ni mwandishi mwenyeshahada ya Ph. D katika somo la fasihi. Mwandishi huyuamebobea katika fani za fasihi ambazo nitamthiliya, hadithi fupi, riwaya na mashairi.Pia ni mhakiki wa fasihi ambayeamechapishamakala mbalimbali katika majarida ya kisomi Afrika, Ulaya na Marekani:
Baadhi ya kazi zake ni kama zifuatazo:
-Bina-Adamu-2002
-Jumba la Huzuni-2006
-Kamusi ya Ushairi-2006
-Kuku na Mwewe-2006
-Harufu ya Mapera-2012
-Nguvu ya Sala (Riwaya)
-Shingo ya MbungenaHadithi Nyingine-2007
-Uncle’s Jokes-2007
-Wingu la Kupita             
Bina-Adamuni riwaya inayotumiasitiari ya kijijikuangalia hali ya mataifa ya ulimwengu katika kipindi hiki ambapo hali za kijamii, kisiasa na kiuchumi zinadhibitiwa na ubepari wa mataifayaliyoendelea. Hii ni riwaya changamano yenye ufundi wa lugha na kimtindo, inayomfanya msomaji awaziesiotu yanayozungumzwa bali pia muundo wa riwaya ya Kiswahili.Hii ni riwaya dhati ambayo ipo katika kigezo cha fani upande wa riwaya changamano ambazo hutumia lugha fiche, mandhari fiche, majina na mtiririko wa matukio huwa changamano.
Kwa mujibu wa Wamitila katika kamusi yake ya fasihi, isimu na nadharia, (2003) anaonyesha aina tofautitofauti za riwaya kama vile riwaya changamano, riwaya sahili, riwaya kiambo na nyinginezo. Katika uainishaji huu, riwaya huweza kuainishwa kwa kutumia vigezo vya kifani, kimaudhui, upeo wa kijiografia na kigezo cha usimulizi. Pamoja na vigezo vyote hivyo, riwaya huweza kugawanywa katika makundi makuu mawili yaani riwaya dhati na riwaya pendwa.
Katika kuainisha riwaya hii ya Bina-Adamu, tunaiainisha kwa kujigeza katika kigezo cha fani ambapo tunaona kuwa hii ni riwaya changamani kwa sababu mwandishi ametumia lugha ya mafumbo, hivyo msomaji anahitajika kuwa na ufahamu wa kutosha ili aweze kuielewa riwaya hii. Kwa mfano katika ukurasa wa 100, mwandishi anasema:
“Nilikumbuka vituko kadhaa nilivyopitia huko nyuma kuanzia Zakongwe wazee walinieleza matatizo mengi waliyokabiliana nayo zamani walipokuwa wakipambana na mazimwi yaliyovamia nyumba miaka mingi iliyopita.”
Hapa mwandishi ametumia mazimwi kuelezea jinsi gani nchi za kiafrika zilitawaliwa na wakoloni na ndipo wakaamua kupambana nao kuwaondoa. Hapa tunaona kuwa ili msomaji aweze kuelewa maudhui yaliyomo katika riwaya hii anapaswa kutumia tafakuri ya hali ya juu sana. Mara nyingi waandishi hutumika mbinu hii ya ufumbaji ili kukwepa mkono wa dola na kuepuka udhibiti wa kazi zao za fasihi.
Mwandishi wa riwaya hii amefanikiwa kwa kiwango cha juu katika utunzi wake katika kipengele cha fani na maudhui pia. Kwa kujikita katika kipengele cha fani, mwandishi amefanikiwa kutumia mielekeo chomozi ya kifani kwa kiasi kikubwa. Mielekeo chomozi ya kifani ambayo imejidhihirisha katika riwaya hii ni kama ifuatavyo:
Naratolojia; hikini kipengele ambacho huelezea namna ambavyo usimulizi umefanyika katika kazi ya fasihi. Dhana ya usimulizi kwa mujibu wa Madumulla (2009:110), ni dhana katika fasihi inayobainisha sehemu alipo anayesimulia hadithi au tukio, kwa jinsi hiyo, msomaji anapata picha ya jinsi matukio yanavyohusiana, yanavyosababishana na yanavyo endelea mwanzo hadi mwisho.Msimuliaji anaweza kutumia usimulizi shahidi au usimulizi maizi. Naratolojia husaidia kuelewa maudhui kutokana na jinsi mtunzi alivyoipangilia kazi yake. Ili usimulizi uweze kueleweka kwa hadhira, mtunzi hana budi kuwa na taaluma hiyo ya usimulizi na uzingativu wa lugha anayoitumia kulingana na jamii aliyoikusudia kuifikishia ujumbe.
 Katika kitabu hiki cha riwaya ya Bina-Adamu, usimulizi shahidi umetumika kwa kiasi kikubwa. Usimulizi shahidi kwa mujibu wa Wamitila (2006:41),ni usimulizi ambao hutofautiana na usimulizi wa nafsi ya tatu kutokana na sifa yake ya kutoweza kuyaona yote isipokuwa, kama tulivyoona, usimulizi wa tendi. Anaendelea kusema kuwa msimulizi anayepatikana katika kazi iliyosimuliwa hivi huwa ana mkabala mmoja tu maalum. Mawazo anayoyatoa kuhusu tukio mtu au hali huwa yake tu. Mwandishi wa riwaya hii amejikita kwa kiasi kikubwa katika aina hii ya usimulizi kwani tunaona matumizi ya nafsi ya kwanza yametumika kwa kiasi kikubwa sana kuanzia mwanzo wa riwaya hii hadi mwisho japo ametumia aina nyingine ya usimulizi. Kwa mfano katika ukurasa wa 7 mwandishi anasema:
“Nilipozaliwa niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa.”
Pia ametumia usimulizi shahidi katika ukurasa wa 32 ambapo anasema:
 “Nilishindwa kuelewa. Lakini ili kuuficha mshangao wangu niliamua kumuuliza maswali.” Katika ukurasa wa 79 mwandisi anasema:
“Nilianza kujilaumu kwa kutomwelewa nyanya yangu.”
Pia usimulizi maizi umetumika kwa kiasi fulani katika riwaya hii. Wamitila (2006:40) anasema kuwa usimulizi maizi ni usimulizi ambao hufuata mkondo unaodhihirisha ufahamu wa siri na mambo yote. Katika usimulizi maizi, msimulizi huwa na sifa za ki-ungu na humaizi na kuelewa kila kitu kinachowahusu wahusika, mandhari, hadithi, mwelekeo, saikolojia ya viumbe wa hadithini, na kadhalika. Kwa mfano ukurasa wa 7 mwandishi anasimulia kwa kuwaelezea watu watatu ambao waliishi kijijini kwao hapo zamani. Mwandishi anasema:
 “Mmoja alikuwa mhubiri aliyeishi upande wa pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyumba yake siku hizi imebakia kuwa banda kuu baada ya mkewe kuondoka kwa kulalamika chakula kimepotea na wamebakia kula vyakula vinavyotolewa kama sadaka na waumini.”
Katika   ukurasa wa 8 mwandishi anasema:
“Mkazi wa tatu hakujulikana kwa jina na watuwengi kijijini. Lakini alikuwa na watoto watatu; huntha waliondoka zamani na haijulikani walikozamia.”
Msuko wa vitushi, kwa mujibu wa Mbunda Msokile (1992:206) ni mtiririko au mfuatano wa matukio yanayo simuliwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mbinu hii ya Msuko wa vitushi husaidia katika kufikisha maudhui kwa hadhira na humrahisishia msomaji katika usomaji.
Pia Wamitila (2006:6) anatoa maana ya msuko kuwa ni mfuatano wa matukio yanayopatikana katika kazi ya kifasihi kwa kutegemea uhusiano wake kiusababishi. Yaani tukio fulani linasababishwa na nini? Hivyo basi kipengele hiki huangalia motifu mbalimbali alizotumia mwandishi pamoja na mjongeo wa vitushi.
Motifu kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu (2010:963) ni sababu, matilaba au malengo, msukumo wa kufanya jambo fulani. Zipo aina nyingi za motifu ambazo zinaweza kutumika katika kazi ya fasihi. Baadhi ya motifu zilizo tumika katika riwaya hii ni motifu ya safari ambayo huonyesha mhusika au wahusika wakiwa katika safari.Motifu hii ya safari inajidhihirisha kuanzia sura ya kwanza hadi sura ya mwisho ya riwaya hii ya Bina-Adamu. Kwa mfano katika ukurasa wa 12 anasema:
 “Nilikuwa bado nimesimama niliposhituka nimepigwa teke la nyuma na kuambiwa haya anza safari yako ya ufumbuzi.” 
Pia motifu hii ya safari imejidhihirisha katika ukurasa wa 27 ambapo mwandishi anasema:
“Baada ya safari ndefu tulitokeza sehemu iliyokuwa na miti mingi ajabu”
Vilevile katika ukurasa wa 76, mwandishi anasema:
“Badala ya kuifuata ile njia niliyokuwa nimependekezewa na yule kijana, nilishika njia tofauti iliyoishia baharini.”
Vilevile katika ukurasa wa 33 mwandishi anasema:
“Baada ya kutembea mita kama mia moja hivi, nilitokea mahali palipokuwa na majengo yaliyoonekana kama ya miaka mingi.”
Pia ukurasa wa 89, mwandishi anasema:
“Nilianaza safari yangu tena. Nilikuwa sijaenda mbali niliposikia mmoja wao akiniita kutoka nyuma.”
Motifu ya safari imejidhihirisha tena katika ukurasa wa 88 ambapo mwandishi anasema:
“Wewe ni Msafiri,” aliniambia, inamaana bado hujaimaliza safari yako. Jikaze. Ufikapo mwisho wake utajua maana ya wimbo huu.”
Aina nyingine ya motifu ambayo imejitokeza katika riwaya hii ni motifu za majini au baharini. Aina hii ya motifu huhusisha safari ndani ya maji. Katika ukurasa wa 15 mwandishi anasema:
“Niliamua kuufuata ushauri wake. Hatukuenda sana kabla ya kutumbukia kwenye mto uliokuwa na maji mengi ajabu lakini hatukuzama, badala yake tulielea juu juu……….”
Pia katika ukurasa wa 21, mwandishi anasema:
 “Nilipozinduka nilikuwa kwenye mto wa ajabu. Maji yake yalikuwa yakienda kwa kasi ya ajabulakini mara hii hayakuwa yakienda nyumanyuma bali yalienda mbele”.
Vilevile mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu ametumia motifu ya mambo ya ajabu ajabu, majini na mazimwi kwa kiasi kikubwa sana. Motifu hii hujumuisha vitu ambavyo havionekani katika mazingira halisi lakini huwasilisha dhana fulani kwa hadhira, ambayo ikiletwa katika uhalisia inaeleweka. Motifu hii imejitokeza sehemu nyingi katika riwaya hii. Kwa mfano katika ukurasa wa 10, mwandishi anasema:
 “Nilijaribu kushikashika hapa na pale kama mtu asiyekuwa na uwezo wa kuona. Nilishitukia nimepigwa kofi kali “huyu ni nani anayewakanyaga wanangu? Mjinga gani? Mnatufuatia nini mpaka huku nyie? Wajinga wakubwa, kwanini hamtosheki na dunia yenu?” ilisema sauti ya kike kwa uchungu.”
Pia katika ukurasa wa 78, mwandishi anasema:
 “Nilipozinduka lile gogo lilikuwa karibu sana na nilipokuwa nimelala. Nilipigwa na butwaa kubwa. Nililiangalia tena. Lilichukua sura ya nyanya kisha baada ya muda nikaona likichukua sura ya mke wangu halafu Hanna.”
Vilevile mwandishi ametumia motifu hii katika ukurasa wa 14 ambapo anasema:
“Nilipotua nilishitukia nimesimama na jitu refu, nilijitahidi kusimama ili niweze kuliona jitu hilo vizuri. Ilikuwa shida kuliona sawasawa. Miguu yake ilikuwa mikubwa ajabu. Nilirudi nyuma kuweza kuliona vizuri lakini likarefuka nikashindwa kuliona vizuri.”
Pia mwandishi anaendelea kuonyesha motifu hii katika ukurasa wa 137, ambapo anasema:
“Niliguswa bega la kulia na kugeuka kwa wepesi wa ajabu lakini sikumwona yeyote. Niliangalia mbele kisha nikaguswa bega la kushoto,usishangae, sauti hapa zinaingiliana, ndio uhalisia mpya huu.”
Pia katika Ukurasa wa 156, mwandishi anasema:
“Majini ya pale yamemshika! Jinsia yake itabadilika!”
Vilevile katika ukurasa wa 144, mwandishi anaonyesha motifu hii kwa kusema:
 “Nilikuwa na nia ya kusogea karibu na kuangalia vizuri nilipopigwa ngoto kali na kuambiwa kwa sauti ya juu, huna muda wa kumangamanga hapa kama mmanga. Huntha umewaona au hata kuwatambua? Je, na Peter P….?”
Aina nyingine ya motifu ni motifu ya ndoto. Motifu ya ndoto hutumiwa na msanii wa kazi ya fasihi kwa lengo la kuwasilisha dhamira nzito katika jamii au hutumika motifu hii kwakukwepa mkono wa dola katika kuwasilishakatikakile alichokusudia kwa jamii. Wakati mwingine, mwandishi anapotumia ndoto huwa ni mbinu ya kuipa kazi yake upekee au kuepuka kuwasilisha dhamira kwa njia ya kawaida pasipo kuonyesha athari ya mhusika moja kwa moja. Katika kuthibitisha hili, mwandishi anaonyesha ukurasa wa 77 ambapo anasema:
“Ghafla nilisikia sauti iliyofanana na iliyonijia katika ndoto.”
Kwa upande wa mjongeo wa vitushi katika riwaya hii ni sahili kwa sababu visa na matukio yamepangiliwa moja kwa moja kuanzia mwanzo hadi mwisho. Tunaona kuwa mwandishi anamuonyesha Bina-Adamu jinsi anavyoanza safari yake, vikwazo anavyokutana navyo katika safari yake hadi anapofika mwisho wa safari yake. Mbinu hii humsaidia katika kuumba matukio na kuyaendeleza katika kazi za fasihi,
Mwendo wa riwaya ni ule mtiririko na mshindilio wa vitushi katika riwaya kwa kuzingatia vigezo vya Msuko, mandhari, masafa ya kiwakati na kijiografia. Katika riwaya hii ya Bina-Adamu, mwandishi ametumia Mwendo wa polepole. Tumebaini kuwa ni Mwendo wa polepole  kwa sababu zifuatazo:
Kwanza mwandishi anasimulia kila tukio hatua kwa hatua ambapo harushi matukio ya riwaya hii. Usimulizi shahidi uliotumika katika riwaya hii unadhihirisha hili kwani kila kile anachokisimulia, amekishuhudia. Kwa mfano katika ukurasa wa 54, mwandishi anasema:
“Nilitokeza mbele ya wazee waliokaa na vijana kwenye kikundi. Wote walikuwa wakifanya kazi huku wakiongea. Waliponiona walinijia na kunialika kujiunga nao. Wawili waliondoka na kurudi na sahani lililokuwa na chakula. Niliwaangalia.”
Pili, maudhui yaliyotumika katika riwaya hii, kwa kiasi kikubwa ni ya kitanzia kitu ambacho kinatudhihirishia kuwa Mwendo wa riwaya hii ni wa polepole. Kwa mfano, katika ukurasa wa 144-145 mwandishi anasema:
“Nakumbuka kijijini kulikuwa na barabara iliyokuwa na daraja dhaifu. Mwaka mmoja palitumbukia gari dogo wakafa watu wawili. Viongozi walisema watafikiria la kufanya. Kimya. Miaka miwili baadaye hali hiyo ikajirudia, mara hii wakasema tumejifunza. Kimya. Mara ya tatu lilitumbukia basi la abiria wakafa watu mia, ikawa mara hii lazima tutajenga daraja upya kuzuia tanzia ya kitaifa kama hii. Mpaka leo bado, wanangojea kukumbushwa.”
Pia katika ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Mwenzetu amepigwa risasi nyingi ajabu, kwa kudhaniwa mwizi, kudhaniwa tu unasikia?”Utanzia mwingine unaojitokeza katika ukurasa wa 137 na ukurasa wa 148.
Tatu, Mwendo wa riwaya hii ni wa polepole kwa sababu za kijiografia ambapo mwandishi anaonyesha mandharia ya kiafrika na mandhari ya kimagharibi kwa kuonyesha kipindi kirefu ambacho Bina-Adamu alikuwa katika safari yake. Kama mwandishi angeonyesha maramoja kuwa amefika huko alipokuwa akienda ambako ni nje ya bara la Afrika pasipo kuonyesha matukio aliyoyafanya njiani, ungekuwa ni mwendo wa haraka.Kwa mfano katika ukurasa wa 130-131 anaonyesha majengo ya Mefu na jengo la Pembetano ambako Bina-Adamu alikuwa amefika huko.Pia mwandishi anaonyesha mandhari ya nchi za kimagharibi katika ukurasa wa 119 anaposema:
“Darling, huyu anatoka jana. Hawa ndio wanaojua furaha. Nilitamani kuwaeleza kuwa maisha yetu yalikosa furaha kwa sababu ya umasikini na uongozi mbaya.”
Katika maneno hayo hapo juu, ni ya watu wawili ambapo awalimmoja alikuwa Afrika lakini kwa wakati huualikuwa nje ya Afrika na kukutana na mwenzake huko ughaibuni.
Mwendo wa riwaya husaidia katika kubaini masafa ya wakati na masafa kijiografia katika kazi za fasihi.
Mtindo kwa mujibu wa Wamitila (2006: 28),ni upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye hutokeza au huonyesha nafsi na au labda upekee wamtunzi huyu. Kwa ujumla, mtindo hurejelea mbinu aitumiayo msanii wa kazi ya fasihi katika kufikisha ujumbe wake.Mwandishi wa riwaya ya Bina-Adamu ametumia monolojia kwa kiasi kikubwa katika kazi yake kwanzia sura ya kwanza hadi sura ya mwisho. Katika ukurasa wa 7, mwandishi anasema kuwa:
“Nilipozaliwa niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijij chetu na mpaka leo hii unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa. Kijiji chenyewe kimezungukwa na mito isiyokaukwa na maji pande zote na kimejitenga na vijiji vingine vinavyohusiana nacho kama Utaridi na Kausi. Katikati pana mti mkubwa ulioota na unaoonekana na mtu akiwa mbali na kilipo kijiji chenyewe”.
Pia ametumia dayolojia ili kuipa uhai kazi yake. Katika ukurasa wa 15,mazungumzo kati ya Hanna na Bina-Adamu mwandishi anasema:
“Mimi naitwa Hanna, unaweza ukasema Anna ukitaka’’,aliniambia. Anaongea kama yeye kabisa, nilijiambia.”
“Hapa ni wapi?”
 “Umeuliza swali hilo mapema mno! Ulipotoka hukufunzwaharakaharaka hainaBaraka?”
Hayo ni mazungumzo kati ya Bina-Adamu na Hanna,alipokuwa nataka kujua ni wapi aliko na anaelekea wapi. Majibizano pia yametokea uk 34-35, piauk. 47 mazungumzo baina ya Bina-Adamu na mzee mmoja aliyekuwa anamwambia Bana-Adamu asimshangae:
 “Usishangae Bina-Adamu Msafiri!” alisema Yule mzee kwa sauti dhaifu lakini imara.
 “Kulifanyika nini huku?” niliuliza.
“Matokeo ya mchezo!”                          
“Wa nani?...…..”
Majibizano pia yametokea uk 68-69,uk 70-71, uk 95-97,uk 108,uk 119,uk 124,uk 127-128,uk 130,uk 141-142,uk147,uk 150-151,uk 152-153,uk 154-156.
Matumizi ya nafsi katika riwaya  hii yaBina-Adamunafsi  zote  tatu zimetumika lakini nafsi  ya kwanza na ya  tatu ndizo zilizotumika kwa kiasi  kikubwa  zaidi kuliko nafsi ya pili.
Kwa kuanza na nafsi ya kwanza  umoja  hii ndiyo imetawala kwa kiasi kikubwa  takribani riwaya yote  kwa  mfano  nafsi  ya kwanza  umoja   imetumika  ukurasa wa  7 mwandishi anasema:
“Nilipozaliwa niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo hii unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa”
Pia matumizi ya nafsi ya kwanza yanajitokeza katika ukurasa wa 11, 12, 15, 27, 52, 59, 67.87, 119, 121, 129 na kadhalika.
Vilevile nafsi yakwanza wingi imeonekana katika ukurasa   wa 74 mtunzi anasema:
 “Tulizunguka kuangalia nyumbanyingine lakinitukashindwa kuzimaliza kwa siku moja”
Matumizi yanafsi ya pili umoja na uwingi pia yamejitokeza kwa kiasi kidogo. Mfano nafsi ya pili umoja  katika ukurasa wa  16, 88, 124,125 na 154  na  nafsi   ya pili uwingi inajidhihirisha katika ukurasa  wa 112 mwandishi  anasema:
“Tatizo lenu kuu, hamtaki kuukabili uhalisia wenu na kujitahidi   kuubadilisha……………”
Pia kwa kiasi fulani nafsi ya tatu imetumika katika umoja na uwingi .kwa  kuanza na nafsi  ya tatu umoja  nafsi  hii  imetumika  katika   kurasa zifuatazo  18, 19, 50,  55,  58,  86,  87, 97, 103, 108,  117,  124,  126, 128, 132, na sehemu nyinginezo. Mfano katika ukurasa wa 132 mtunzi anasema:
 “ Alinizungusha  nyumbani  akinieleza ,  “ Hii ni friji ambayo  ina uwezo  wa kumfanyia  mtu mambo mengi.”
Kwa upande wa nafsi   ya tatu uwingi imejitokeza katika ukurasa wa 17, 19, 38, 50, 57, 99, 100, 101, 102, 113 na kadhalika. Mfano katika ukurasa wa 100 mwandishi anasema:        
 “Walielezea matatizo waliyoyapata siku hizi: karo ya watoto, upungufu wa chakula, magonjwa, matatizo ya kazi, hospitali kukosa dawa, wizi wa nguvu; tuseme shida za kila aina.”
Pia katika kipengele cha mtindo, mwandishi hutumika lugha kwa namna ya kipekee sana na kibunifu sana. Kipengele cha matumizi lugha kitajadiliwa kwa undani katika mbinu za kibunilizi na katika mtagusano ambapo kuna matumizi ya lugha mbalimbali.
Umuhimu wa matumizi ya nafsi ya kwanza ni kuonesha ushahidi wa matukio anayoyasimulia kwa hadhira yake kwa ukina.  Na matumizi ya nafsi ya pili humufanya msomaji kujiona kuwa yeye ndiye mlengwa mkuu wa kazi husika. Matumizi ya nafsi ya tatu humweka karibu msomaji wa kazi husika.Mbinu hii ya mtindo, hutumika kwa lengo la kuipa uhai kazi ya fasihi, kuwachora wahusika wake, kuonyesha upekee wa kazi ya mtunzi na kufikisha ujumbe kwa hadhira.
Uhusika na wahusika. Wahusika kwa mujibu wa Senkoro, (2011:7) ni watu ama viumbe waliokusudiwa wawakilishe dhana, mawazo au tabia za watu katika kazi ya fasihi. Uhusika wa wahusika katika riwaya ya Bina-Adamu unajitokeza pale wanapopewa sifa na tabia fulani na kuweza kuwa wawakilishi wa watu wema au wabaya.  Katika riwaya hii mwandishi ameonyesha wahusika wanaojipambanuawaziwazi na wahusika ambao hawajipambanui waziwazi.
Wahusika ambao wanajipambanua waziwazi ni kama vile, Mhubiri, Mwanasayansi, Kichaa na Bina-Adamu Msafiri. Kila mhusika, uhusika wake unaonekana katika riwaya hii kulingana na mwandishi wa riwaya hii alivyompa uhusika huo. Kwa mfano uhusika wa Bina-Adamu unajidhihirisha kuanzia mwanzo wa riwaya hii hadi mwisho. Uhusika wake unaonyesha matendo na tabia ambazo zinastahili kuigwa katika jamii kwani anaonyesha juhudi ya kufanya uvumbuzi ambao unaibua dhamira ya upelelezi na kufanya mapinduzi.
Pia mwandishi ameonyesha wahusika ambao hawastahili kuigwa katika jamii kutokana na jinsi walivyochorwa na mwandishi. Kwa mfano P.P ambaye ni Peter Pan hastahili kuigwa katika jamii kwa mfano, Ukurasa wa 71 mwandishi anasema:
“Sasa huyu P.P ni nani anayeelekea kuhusika na kila kitu? Nilijiuliza. Niliyakumbuka maafa niliyoyaona huko nyuma nilikoelezwa yalitokana na bomu lake.”
Pia mwandishi ametumia wahusika ambao uhusika wao ni wa ajabuajabu kwa sababu wana sifa kama mizimu. Kwa mfano. Mwanishi anamchora mhusika Hanna kama mhusika ambaye anabadilikabadilika na wakati mwingine anatokea na kupotea. Mwandishi anathibitisha hili katika ukurasa wa 32 kwa kusema:
“Hanna alikuwa ametoweka sasa lakini wale viumbe wa ajabu walikuwa wakiongoza njia,”
Licha ya mwandishi kutumia wahusika wanaobadilikabadilika wamefanikiwa kuonyesha uhusika wao kwa kutoa msaada mkubwa wa kumwongoza Bina-Adamu.
 Kwa upande wa wahusika wasiojipambanua waziwazi, mwandishi anamwonyesha mhusika X katika ukurasa wa117 ambapo mwandishi anasema:
“Jina langu ni X. Basi karibu leo na kesho. Karibu utafika kwenye Bustani ya Eden ya pili!”
Mianzo na miishoni mbinu ambayo hutumiwa na wasanii wa kazi za fasihi katika kazi zao kwa kusudi la kuiandaa hadhira katika kazi husika, kuonyesha mwazo wa hadithi na uhitimishwaji wa hadithi. Mbinu hii mara nyingi hutumika katika kazi za fasihi simulizi na katika fasihi andishi kwa kiasi kidogo. Kazi za kifasihi za zamani zinautofauti mkubwa sana kwa na kazi za siku hizi. Kazi nyingi za kifasihi za zamani zilikuwa zikifuata mianzo na miisho ya kifomula kwa sehemu kubwa tofauti na kazi za siku hizi ambazo mara zinakuwa na mianzo ya kawaida. Mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu ametumia mianzo ya kawaida ambayo siyo ya kifomula. Kwa mfano katika ukurasa wa 7, anaanza kwa kusimulia visa vyake moja kwa moja pasipo kufuata mianzo ya kifomula ambavyo huanza kwa namna ya kipekee kama vile, “hadithi hadithi…..”, “puakwa…..pakawa”, na mianzo mingineyo. Mwandishi anaanza kwakusema:
“Nilipozaliwa niliwakuta watu wakiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa. Kijiji chenyewe kimezungukwa na mito isiyokaukwa na maji pande zote.”
Pia katika kuhitimisha riwaya hii, mwandishi hajaonyesha miisho ya kifomula ambayo mara nyingi huishia na maneno kama vile, “hadithi yangu ikaishia hapo”, na “wakaishi kwa raha mstarehe”. Mwandishi amemalizia kazi yake kwa kawaida sana ambapo anaiacha hadhira yake bila kuridhika kwani haonyeshi dhahiri nini kiliendelea baada ya Bina-Adamu kufika alipokuwa amekwenda kuwatafuta huntha watatu jambo ambalo ni tofauti na kazi nyingi za kifasihi ambazo huwa na miisho ya kifomula.
Mtagusano ni kipengele kinachohusiana na muingiliano wa vipengele mbalimbali katika kazi ya fasihi kutokana na athari za utamaduni na sayansi na teknolojia. Mtagusano umejitokeza kama dhamira, madhari na lugha.
Mtagusano unajidhihirisha katika riwaya hiikwa kusadifu dhamira za kimagharibi kama vile uonevu ambapo waafrika wanateswa na kuonewa pindi waendapo nchi za magharibi. Kwa mfano katika ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Mwenzetu amepigwa risasi nyingi ajabu kwa kudhaniwa mwizi; kudhaniwa tu, unasikia? Tunajua tu ni kwa sababu ya rangi tu, unasikia rangi tu!”
Pia mtagusano kama dhamira, unajidhihirisha katika ukurasa wa 128 ambapo tunaona watu wakiufanyia uchunguzi ubongo wa Alberty Einstean ili kuweza kutambua akili alizokuwa nazo kabla ya kifo chake. Mwandishi anaonyesha dhamira hii ambayo inafungamana na dhamira za kimagharibi wa kuonyesha namna watu wenye upeo mkubwa wa akili wanavyofanyiwa katika nchi zilizo endelea. Mwandishi anasema:
“Kwanini Albert Einstein alikuwa na akili za ajabu. Tunauchunguza ubongo wake sasa!”
“Ubongo wake?”
“Ehh, tuliufukua baada ya kifo chake!”
“Huku hakuna miiko?”
“Baada ya kifo aliipoteza haki ya mwili wake. Tunachunguza kiini ili kuiendeleza jamii ya kesho.”
Kwa upande wa mandhari kama mtagusano, mwandishi anatumia madhari ya kimagharibi kwa sehemu kubwa na hivyo kutumika kama mtagusao. Mwandishi anathibitisha hili kwa kusema:
“Kwanza kuna jengo la Mefu” (ukurasa wa 130)
“Jengo la pili ni Pembetano” (ukurasa wa 131)
 Pia mwandishi ametumia lugha za kigeni katika kazi hii. Kwa mfano katika ukurasa wa 20 ametumia neno la kilatini Vitas lenye maana ya maisha. Pia ukurasa wa 38 ametumia neno la kijerumani Fyuraa ambalo kwa Kiswahili linamaanisha kiongozi. Vilevile mwandishi ametumia maneno ya kiingereza kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano; International water (ukurasa wa 50), Reconditioned car (ukurasa wa 50), Global village (ukurasa wa 87), Global pillage (ukurasa wa 87), Darling (ukurasa wa 119), the soul  of Black folk, (ukurasa wa 126), Balance of power (ukurasa wa 142), Dollar (ukurasa wa 142), Rhythm (ukurasa wa 143), na Global villain (ukurasa wa 155).
Matumizi ya lugha, mwandishi ametumia lugha nyepesi na ya kawaida iliyojaa Methali, nahau, vitendawili, tamathali za semi na mbinu nyingine ya kisanaa ili kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa mujibu wa Senkoro (2011) fasihi ni sanaa itowayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa. Kipengele hiki ni muhimu sana kwani ndicho kinachotofautisha fasihi na sanaa nyingine. Kwa kiasi kikubwa mwandishi wa riwaya hii ametumia lugha ya kawaida iliyojaa misemo, methali, tamathali za sina mbinu nyingine za kisanaa kama ifuatayo.
Misemo na nahau, katika riwaya hii misemo na nahau vimeonekana katika kurasa mbalimbali kwa lengo la kuijulisha hadhira wakati unaohusika katika kazi ya fasihi husika, misemo hiyo imesawiriwa na mwandishi kama ifuatavyo:
Usiwe yule fisi wa masimulizi (uk.54)
Kichwa cha nyoka hakistahimili kilemba (uk13)
Msahau jana kesho humkumbusha (uk125)
Kila ukombozi unahitaji shujaa (uk128)
Usipende mwanga kabla hujalijua giza (uk106)
Kuaga dunia (uk47)
Methali, hizi ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa jamii (Mlokozi 1989). Katika riwaya hii mtunzi ametumia methali mbalimbali kamavile;
“Msahau jana kesho humkumbusha” (uk.125)
“Mgeni njoo mwenyeji apone” (uk.139)
“Haraka haraka haina Baraka” (uk.23)
“Kidole kimoja hakivunji chawa” (uk.88)
“Hasira hasara” (uk.15)
“Mwenye pupa hadiliki kula tamu” (uk.140).
“Kigumba kwa nguruwe kwa binadamu kichungu” (uk143)
“Kichwa cha nyoka hakistahimili kilemba” (uk13)
“Msahau jana kesho humkumbusha” (uk125)
“Kila ukombozi unahitaji shujaa” (uk128)          
“Usipende mwanga kabla hujalijua giza” (uk106).
Mwandishi katumia methali, misemo, vitendawili na nahau kwa lengo la kumfanya msomaji asichoke,kuonyesha ufundi wake katika lugha anayoitumia, kuweka msisitizo juu ya jambo fulani, pia matumizi ya misemo kama methali husaidia kuonya jamii juu ya jambo fulani.
Tamathali za semi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kuvitia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Katika riwaya hii mwandishi ametumia tamathali za semi mbalimbali kama zilivyoainishwa hapo chini.
Tashibiha, hii ni hali ya kulinganisha vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno kama vile; “kama”, “mithili” na “mfano wa”. (Senkoro 2011).
Tamathali hii imetumika katika riwaya ya Bina Adam! Mfano:
“Umati wenyewe umekodoa macho pima huko juu kama kuku anayemwangalia mwewe” (uk.69)
“Nilivuta tabasamu na kutoa pumzi kama kiboko kasha nikaogelea hadi ukingoni na kutoka” (uk.77)
“Lakini niliweza kuziona pia zake za miguu zilizokuwa kubwa kama masahani” (uk.63)
“Anaendelea kung’ang’ania mlingotini tu kama kima”(uk.91)
Tashihisi, hii ni tamathali ambayo vitu visivyokuwa na sifa za binadamu hupewa sifa za kutenda kama binadamu. Mfano katika riwaya hii tamathali hii imejitokeza kama ifuatavyo,
“Uwongo umechukua kiti na kuketi kijijini”(uk.75)
“Huko mbele kulikuwa na msululu mkubwa wa milima”(uk.32)
“Niliamua kuifuata ile njia pana iliyoishia kunitokomeza”(uk.144)
Mbinu nyingine ya lugha iliyojitokeza katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni:
Tanakali sauti, haya ni maneno yaundwayo kutokana na sauti zinazofanana nayo. Mfano katika (uk.125) mwandishi ameandika:
“Kutokwa na machozi yaliyoanguka nde! Nde! Nde!”
Mdokezo, hii ni hali ya kutamka maneno bila kuyamalizia ili kuleta maana halisi. Mfano katika (uk.122)
Mwandishi ameandika:
“Hi..i.ndiyo...njia…a a ya..peke..e..e. kuhakiki..isha kuwa hukw..amizwi…pia katika” (uk.21)
Pia mwandishi ameandika:
“Nyoka…Nyoka…..”
Takiriri, hii ni tamathali ya semi ambapo sehemu ya neno hurudiwa rudiwa au neno zima. Mwandishi hutumia mbinu hii kwa ajili ya kusisitiza juu ya jambo fulani. Katika riwaya hii mwandishi ametumia takriri kuonyesha msisitizo wa mambo anayoyazungumzia katika kazi yake, takriri zilizo tiumika ni kama vile:
“Beberu …….!Beberu……!Beberu……….!Nilijiambia akilini nikiliangalia, beberu, beberu, beberu, linanuka beberu” (uk14)
“Kwanini? Kwanini? Kwanini?” (uk 22)
“Hatimaye nilianza kutapika. Nikatapika, nikatapika, nikatapika”. (uk83)
“Nyoka …….! Nyoka………!” (uk21)   
Pia riwaya hii imeshehenezwa na taswira kwa kiasi kikubwa. Madumulla J. S (2009: 153) akimnukuu Senkoro F. M. E. K,anasema,taswira ni mkusanyiko wa picha mbali mbali ziundwazo kwa maelezo ya wasanii katika kazi ya fasihi. Anaendelea kusema kuwa ni lugha inayochora picha ya vitu au mahali kwa kutumia ishara.
Hivyo, taswira ni lugha ya picha ambayo hutumiwa na mtunzi kufikisha ujumbe mzito kwa hadhira. kuna aina mbili ya taswira yaani ya wazi ambayo huwa na mkusanyiko wa picha mbali mbali zinazotoa ujumbe wa moja kwa moja bila kuficha na zisizowazi ni zile ambazo hazitoi ujumbe wa moja kwa moja ambayo humhitaji msomaji afikiri sana.
Katika riwaya ya Bina-Adamu mwandishi ametumia taswira mbali mbali katika kufikisha ujumbe, taswira hizo ni kama zifuatazo:
“Kijiji”- mataifa ya ulimwengu katika kipindi hiki hali za kijamii, kisiaa na kiuchumi zinadhibitiwa na ubepari wa mataifa yaliyoendelea (juu ya jarada)
“Paani”- madarakani (uk. 67)
“Maganda, makokwa na makaka”- kile kidogo wanacho kipata watu
“Ngazi”-dhamana ya kuingia madarakani
“Matunda”-utajiri.
“Kitambara”-bendera (uk. 68)
Taswira zingine ni mawe, beberu, mkoba na nyingine nyingi.
Umuhimu wa kutumia mbinu hiii, ni kukwepa mkono wa dora, kufikisha ujumbe kwa hadhira na kumfakarisha msomaji wa kazi ya fasihi.
Kipengele kingine cha mwelekeo chomozi wa kifani uliotumika katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni mbinu za kibunilizi.Mbinu za kibunilizi ni mbinu mbalimbali za kiubunifu ambazo huzipa kazi za fasihi upekee. Mbinu hizi za kibunilizi ambazo zimejitokeza katika riwaya hii ni kama zifuatazo:
Taharuki kwa mujibu wa Wamitila (2006:8) ni ile hali ya matarajio ambapo tuna hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye. Anaendelea kusema kuwa ni hali ya kusisimua inayompata na kumshika msomaji kiasi cha kuwa na hamu kubwa ya kujua hali au mambo ya baadaye. Pia Senkoro (2011:70) anasema kuwa ujengaji wataharuki hutofautiana kutoka mtambaji mmoja na mwingine, hata kama kisa kinachoelezwa ni kilekile kimoja. Katika riwaya hii mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuijenga kazi yake kitaharuki toka mwanzo wa riwaya hadi mwisho. Msomaji anakuwa na hamu ya kutaka kujua nini kitakachotokea katika safari ya Bina-Adamu Msafiri katika harakati za kuwatafuta Huntha watatu. Katika riwaya hii msomaji anataka kujua uvumbuzi utakaofanywa na Bina-Adamu.
Kwa mfano katika ukurasa wa1mwandishi anasema:
 “Nilipozaliwa niliwakuta watu wakiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo hii unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa.”
Hivyo msomaji hupata dukuduku la kutaka kufahamu juu ya nani Msimuliaji,na ni pahala gani panaposimuliwa na hivyo kuendelea kusoma kazi hiyo ili afahamu juu ya simulizi husika. Pia kazi hii inamjengea taharuki msomaji kwa kutaka kung’amua kuwa P.P ni nani ambaye amechorwa kwa kufumbwa toka mwanzo na jina lake kamili linakuja kujulikana mwishoni kuwa ni Peter Pan. Kwa mfano uk 151,
“Umesema Peter ..e..e..r?Ndiye P.P. kumbe?”
“Ndiye huyu!
“Hiyo P ya pili inamaanisha nini?”
“Jina lake kamili ni Peter P…”
“Kumbe ndio maana anatupa mawe ovyo ovyo tu!”
Hivyo, matumizi ya taharuki humsaidia sana msomaji kupata hamu ya kuendelea kusoma.Vile vile taharuki humtoa uchovu msomaji na kuinua ari mpya ya kusoma.
Kipengele kingine cha mbinu za kibunilizi ambacho kimejidhihirisha katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni utomeleaji. Huu ni uchopekaji wa vijitanzu vingine vya fasihi ambavyo ni tofauti na utanzu unaoshughulikiwa. Riwaya ya Bina-Adamu imejengwa kwa utomeleaji ndani yake. Hili linajidhihirisha katika ukurasa wa 87 ambapo mwandishi anaonyesha wimbo ufuatao
“Shusha, shushaa…….thamani ya hela shushaaa!
Bana, banaa….ugavi wa hela banaa!
Kata, kata…..matumizi ya hela kataa!
Hurisha, hurishaa……soko la hela hurishaa!
Punguza, punguzaa……mishahara duni punguzaa!”
Vilevile wimbo umejitokeza katika ukurasa wa 149, ambao unasema:
“Oh nchi hii! Nchi yangu niliyoivumbua……
Enzi yangu, salama uongozwapo na mfalme mmoja
Chimbuko la johari za gharama
Oh, jinsi ulivyotukuka uvumbuzi wako
Kuingia katika duara hii ni kuwa huru
Suala si KUWA, SWALI NI WAPI PA KUWA!”
Pia mwandishi ametumia mbinu ya ujadi. Ujadi ni matumizi ya kauli ambazo hufungamana na jamii husika iliyokusudiwa na mwandishi. Hii inaonekana pale mwandishi anapotumia methali, vitendawili na nahau. Baadhi ya methali hizo ni:
“Haraka haraka haina Baraka” (ukurasa wa 23)
“Hasira hasara” (ukurasa wa 15)
“Msahau jana, kesho humkumbusha” (ukurasa wa 125)
“Matumaini ni chajio kizuri lakini kiamsha kinywa kibaya” (ukurasa wa 88)
Vitendawili, katika ukurasa wa 82 ambapo mwandishi anasema:
“Muda si muda nilishindwa hata kupiga hatua moja kutokana na giza lahuku ng’o na kule ng’o msituni.”
Ufumbaji ni matumizi ya kauli zenye maana fiche katika kazi za fasihi. Mwandishi ametumia mbinu ya ufumbaji kwa kiasi kikubwa. Ufumbaji umejitokeza katika uumbaji wa mandhari, katika lugha, katika maudhui na katika uumbaji wa wahusika.Katika uumbaji wa mandhari, mwandishi amejitahidi kuyaficha sana. Siyo rahisi kuyatambua kwa urahisi pasipo kufanya uchunguzi wa kutosha. Aidha ametumia mandhari ya nchi za kiafrika na yale ya kimagharibi. Kilicho bainisha hapa na kufanya madhari ya kimagharibi kujulikana ni kutumia maneno kama vile jengo la pembe tano ambalo linatufanya tubaini kuwa nchi inayozungumziwa ni Marekani ambako kuna jengo la Mefu na jengo la Pembetano, maarufu kama Pentagonijapokuwa hajaitaja nchi husika kwa uwazi kama ni nchi ipi. Mwandishi anayazungumzia majengo haya katika ukurasa wa 130 na 131. Anathibitisha hili kwa kusema:
“Kwanza kuna jengo la Mefu” (ukurasa wa 130)
“Jengo la pili ni Pembetano” (ukurasa wa 131)
Pia ufumbaji katika mandhari unaojitokeza katika ukurasa wa 133 na 134. Katika ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Kumbe hata huku wanawapiga risasi watu kwa kuwadhani ni wezi? Je, kama huku msingi wao mkuu ulikuwa rangi, kwetu ulikuwa nini ambako watu wanapigwa risasi na polisi kila mara?”
Katika ukurasa huu mwandishi anaendelea kusema:
“Kila siku P.P anasisitiza hii ndiyo nchi bora katika sayari zote”!
Katika kipengele cha lugha, ufumbaji umejitokeza katika riwaya hii. Mwandishi ametumia lugha iliyojaa taswira, misemo, tamathali za semi, misemo na mbinu mbalimbali katika kipengele hiki jambo ambalo linamfanya msomaji wa riwaya hii kuwa na tafakuri ya hali wa juu ili aweze kubaini kilichokuwa kimekusudiwa na mwandishi. Kwa mfano, katika ukurasa wa 100, mwandishi anatumia lugha ya mafumbo kwa kusema:
“Nilikumbuka vituko kadhaa nilivyopitia huko nyuma kuanzia Zakongwe wazee walinieleza matatizo mengi waliyokabiliana nayo zamani walipokuwa wakipambana na mazimwi yaliyovamia nyumba miaka mingi iliyopita.”
Vilevile ufumbaji umejitokeza katika uumbaji wa wahusika. Mwandishi ametumia wahusika fiche na baadhi yao kuwapa sifa ambazo kiuhalisia hawawezi kuwa kama walivyopewa uhusika wao katika riwaya hii. Kwa mfano ameweza kumchora mhusika Hanna ambaye ana matendo ya ajabu ajabu ambapo anakuwepo mahali fulani kwa wakati fulani na kutoweka ghafla wakati mwingine. Katika ukurasa wa 32, mwandishi anasema:
Hanna alikuwa ametoweka sasa lakini wale viumbe wa ajabu walikuwa wakiongoza njia,”
Pia amemtumia mhusika P.P ambaye hajipambanui wazi wazi na kujulikana kwa wepesi. Hata Bina-Adamu Msafiri alikuwa na shauku ya kumjua huyu mhusika hadi mwisho wa riwaya hii. Licha ya jina lake kujulikana mwishoni kama Peter Pan; bado siyo rahisi kumwelewa mhusika huyu kama alikuwa anawakilisha mtu gani katika mazingira halisi ya Magharibi.
Mbinu nyingine ya kibunilizi ni matumizi ya dayolojia. Dayolojia ni mazungumzo ya majibizano baina ya wahusika wawil au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana.Katika riwaya ya Bina-Adamu mwandishi ametumia mbinu hii ili kuwezesha kuondoa uchovu kwa wasomaji wake.Pia kupitia mbinu hii ya kibunilizi mwandishi ameweza kujiongezea ufundi wa kiutunzi kwa mfano katika ukurasa wa 23 kuna majibizano kati ya Hanna na Bina-Adamu,
“Hapa ni wapi?”
“Umeuliza swali hilo mapema mno! Ulikotoka hukufunzwa haraka haraka haina Baraka”
“Na nani?”
“Na babu!”
“Ala, amemjuaje huyu? Au labda ni mke wangu katika sura nyingine?”
Vilevile dayolojia imejitokeza katika uk 34 mwandishi anasema:
“Wewe ndiye Bina-Adamu msafiri?”
“Ehhh…”
“Tulijua utapita hapa!”
“Mliambiwa na nani?”
“Na babu yako.”
“Babu alikufa miaka mingi iliyopita!”
“Kumbe? Ndiyo maana hata kuongea kwake kulikuwa kwa shida!”
Pia dayolojia imejitokeza katika ukurasa wa 35,47,68,70,71,na72.Tunaona  matumizi haya ya dayolojia yanaonesha kila hatua ambayo mhusika Bina-Adamu msafiri amepitia na vikwazo alivyokutana navyo.Umuhimu wa matumizi ya dayolojia katika masimulizi ni kumuwezesha msomaji kufuatilia kila kinachotokea katika riwaya.Vilevile humfanya msomaji asichoke kusoma kazi husika anayoisoma.
Usawili wa wahusika ni mbinu nyingine ya kibunilizi ambayo hutumiwa na mtunzi kwa lengo la kuwachora, kuwaelezea,kuwafafanua na kuwatambulisha kwa kuwapamajina, dhima, sifa, tabia na matendo. Katika riwaya ya Bina- Adamu mwandishi ametumia mbinu ya maelezo,ulinganuzinausambamba, kuzungumza na hadhira, namajazi kwa nia ya kuwachora na kuwafafanua wahusika wake.
Mbinu ya maelezoniileinayotumia ufundi wa mtunzi katika kuelezea wahusika wake, mbinu hii imetumiwa katika kitabu hiki cha Bina- Adamu katika ukurasa wa 7mpaka 8, unasema:
“Zamani za kale paliishiwakaziwachachesana na labdawatatu. Mmoja alikuwanimhubirialiyeishi upande wa pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyuma yake siku hizi imebakia kuwa bandakuubaada ya mkwewekuondokakwakulalamikachakulakimepotea na wamebakiakulavyakulavinavyotolewa kama sadaka na waumini. Ukiinamia upande wa pili kulikuwa na kichaaaliyeishi upande huo katika kibandakilichofanana na kidungu cha kuwingiandegeshambani; kipompakaleo. Wanakijijiwanasemakichaahuyoalikuwamgangakabla ya wanakijijikumbatizakichaa.Hadithi yake inasimuliwa kwenye vijiji vya mbaliwanakoamini kuwa alikufamiakamingiiliyopita. Mkaziwa tatu hakujulikana kwa jina na watu wengi kijijini. Lakini alikuwanawatotowatatuhuntha; Waliondokazamani na haijulikaniwalikozamia.”
Kutokana namaelezo ya mwandishi tunatambua sifa, tabia na matendo ya wahusika hawawatatu, mbinu hii humfanya mtunzi awe karibu na jamii yake.
Mbinu nyingine ni kuzungumziwa na wahusika wengine ambapo wahusika waliotumika na mwandishi wanatoa sifa na tabia za mhusikamwingine. Mbinu hii imejitokeza katika ukurasa wa 71 unasema:
“Mwalimualiwaeleza ni kwaninihuyo P. P anawatupia watu mawe kwa kumbwewe?
“Alisemaanapendakuchezachezatu”                   
“Kuwatia watu vivimbe vichwani?”
“Tuliambiwa ni mtundu na jeuri”
“Wa kuwagotoa watu vichwa?”
“Labdakwake huo ni mchezo!”
Pia, imejitokeza katika ukurasa wa 24, 55 na 71
Ulinganuzi naUsambamba ni mbinu bunilizi ambayo hutumika na mtunzi kwa njia ya kuwafafanisha na kuwatofautisha kati ya mhusika mmoja au zaidi na wahusika wengine. Mbinu hii imetumika katika ukurasa wa 67:
“Kila kiongozi anakaahuko juu paani, hukondikoanakochumiamatundakwaurahisi na kuwatupia watu walioko chini ambao ndiowaliomshikiangazi ya kupanda juu. Lakini kamawengine ambao wanachofanya ni kulawakashiba kwanza kasha kuyatupa makaka, makokwa na maganda huko chini yanakong’aniwa na umati mkubwa ulioko huko. Wengine wanaibana kuhamishia kwingine, labda ughaibuni”. Katika mbinu hii tunapata sifa, tabia na matendo ya wahusika kwa kuwatofautisha na wahusika wengine.
Wamitila (2006) anasema kuwa, mbinu ya majazi ni mbinu au njia sahali au nyepesi sana ya uhusika, waandishi wa kazi za kifasihi huweza kuyatumiamajina ya wahusika ambayo huakisi mandhari, wasifu, tabia,itikadi pamoja na vionjo vyao.
Hivyo, majazi ambayo mtunzi anawapa wahusika majina kulingana na tabia, sifa, dhima na matendoyao. Hii imetumika katika ukurasa wa 7 na 8.
Mhubirinakichaa ukurasa wa 7 mpaka ukurasa wa 8.
Zamani za kale paliishi wakaziwa chache sana na labda watatu. Mmoja alikuwanimhubirialiyeishi upande wa pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyuma yake siku hizi imebakia kuwa bandakuu baada ya mkwewekuondokakwakulalamikachakulakimepotea na wamebakiakulavyakulavinavyotolewa kama sadaka na waumini. Ukiinamia upande wa pili kulikuwa na kichaaaliyeishi upande huo katika kibandakilichofanana na kidungu cha kuwingiandegeshambani; kipompakaleo. Wanakijijiwanasemakichaahuyoalikuwamgangakabla ya wanakijijikumbatizakichaa.
Mwanasayansi ukurasa wa 53,
“Baada ya muda nilimwona yule mwanayansi na wenzake. Walikuwa wakielekea nilikokuwa nikidhamiria”.
Bina-Adamu Msafiri ni mhusika mkuu katika riwaya hii ambaye alikuwa akisafiri kutafuta ufumbuzi wa jambo kusuhusiana na kijiji chao. Hii imejidhihirisha katika ukurasa wa 34:
“Wewe ni ndiye Bina-Adamu Msafiri?”
“Ehhh…”
“Tulijua utapita hapa!”
“Mliambiwa na nani?”
“Na babu yako”
Hii pia imejitokeza katika ukurasa wa 86. Mbinu hii humsadia msomaji kupata dhamira na ujumbe kwa urahisi zaidi.
Kwa ujumla riwaya hii ya Bina-Adamu, imefanikiwa kufikisha ujumbe kwa kupitia vipengele vya fani na maudhui. Kwa mfano katika dhamira ametoa dhamira ambazo zipo katika jamii yetu ya kiafrika. Dhamira hizi ni kama vile ubaguzi wa rangi, uongozi mbaya, unyonyaji, historia na uhistoria, ukandamizwaji wa nchi za Afrika unaofanywa na nchi za Magharibi. Vipengele vya mielekeo chomozi ya kifani vilivyotumika katika riwaya ya Bina-Adamu ni muhimu sana katika kukikamilisha kipengele maudhui.
MAREJELEO
Madumulla, J.S (2009) Riwaya ya Kiswahili: Nadharia, Historian a Misingi ya Uchambuzi,Sitima Printers and Stationers Ltd, Nairobi, Kenya.
Msokile, M. (1992) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi; TUKI, Dar es Salaam.
Senkoro, F.E.M.K. (2011) Fasihi: Mfululizo wa Lugha na Fasihi, Kitabu cha Kwanza, KAUTTU, Dar es Salaam.
TUKI (2010) Kamusi ya Kiswahili Sanifu; TUKI, Dar es Salaam.
Wamitila, K. W. (2002) Bina-Adamu; Phoenix Publishers Ltd, Nairobi.
Wamitila, K.W. (2006) Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake, Phoenix Publishers Ltd, Nairobi.
Wamitira, K. W. (2003) Kamusi ya Fasihi;Istilahi na Nadharia, Nairobi Focus Publishers, Nairobi.
Powered by Blogger.