Historia na maendeleo ya tafsiri ulimwenguni na nchini Tanzania.
Historia na maendeleo ya tafsiri ulimwenguni na nchini Tanzania.
Katika
mjadala huu, tutaanza na utangulizi ambapo tutajadili dhana ya tafsiri kwa
mujibu wa wataalamu mbalimbali, pia tutaangalia nini maana ya historia kisha
tutaingia katika kiini cha swali kwa kujadili maendeleo ya tafsiri ulimwenguni
katika vipindi mbalimbali pia historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania
na tutaangalia kazi inayoaminika kuwa ndiyo tafsiri na kwanza nchini Tanzania
na kisha tutatoa hitimisho la mjadala wetu.
Taaaluma
ya tafsiri imeweza kuelezwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
Mwansoko
na wenzake (2006), wanafasili tafsiri kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo
katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
AS-Safi
akimnukuu Dubois (1974), anaeleza kuwa tafsiri ni uelezaji katika lugha
nyingine au lugha lengwa wa kile
kilichoelezwa katika lugha nyingine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo
wa matini chanzi.
Catford (1965:20) anaeleza tafsiri ni, Kuchukua mawazo yaliyo
katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo
yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa).
Kutokana
na fasili hizo tunaweza kusema kuwa tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe,
au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa
bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi.
Baada
ya kujadili dhana ya tafsiri, sasa tunaweza kujadili kwa ufupi kuhusu dhana ya
historia.
Wanjala
(2011), anaeleza kuwa historia ni taarifa, maelezo na uchambuzi wa matukio,
watu na nyakati teule zinazoathiri maisha ya wanajamii husika, sasa na hata
siku za usoni.
Historia
na maendeleo ya tafsiri ulimwenguni imeelezwa na wataalamu mbalimbali ambao ni
kama vile Mwansoko na wenzake (2006), Wanjala (2011), Mshindo (2010), Sofer
(2006) ambapo wataalamu hawa wamegawa historia na maendeleo ya tafsiri katika
vipindi vifuatavyo:
Enzi
za kale. Kipindi hiki kinajumuisha wakati wote wa kihistoria kati ya mwaka 300KK
hadi 300BK. Hiki ni kipindi ambacho kilikuwa na maendeleo ya sayansi na taaluma
nyingi za kisasa ambapo zinasadikika zilianzia huko Misri. Ugunduzi na
ustaarabu ulioletwa na wamisri uliigwa na wayunani na kuwa chimbuko la
ustaarabu wa ulaya. Mbinu iliyotumika na wayunani kuchota maarifa ya wamisri ni
tafsiri. Wayunani walikaa misri kwa muda na kujifunza lugha ya wamisri na elimu
yao. Mambo waliojifunza waliyafasiri kwa kiyunani na kwenda kuyasambaza huko
ulaya.
Enzi
za giza. Hiki ni kipindi kati ya karne ya 5 hadi 11. Kipindi hiki kiliitwa
kipindi cha giza kwasababu kilitawaliwa na misingi ya utamaduni kuoza na uozo
wa kijamii kukita mizizi ambapo mambo kama ubashi, ukahaba na unajisi
vilikithiri, pia shughuli za elimu zilikwama huko ulaya. Katika kipindi hiki
kulikuwa na mapigano kati ya waislamu na wakristo ambapo baada ya mapigano hayo
maarifa ya wagiriki yaliyosheheni ujuzi wa sayansi yalifasiriwa kwa kiarabu.
Pia baadhi ya mataifa mfano Hispania yalichukua vitabu ambapo vilikuwa
vimesheni maarifa ya sayansi na kuyapeleka kwao na kutafsiri katika lugha zao.
Tafsiri hizo zilipelekea ulaya kutoka katika kipindi cha giza na kuingia katika
kipindi cha ufufuko wa elimu na maarifa. (Renaissance)
Enzi
za ufufuko. (Renaissance) inamaana ya ufufuko wa hamu kuu ya elimu na maarifa.
Kipindi hiki kilivuma sana ulaya kusini hasa Italia kikiwa na lengo la kufufua
shughuli za elimu na utamaduni. Wazungu walipofika Uarabuni walistaajabia elimu
ya kisayansi wakayachukua maarifa hayo na kuyafasiri katika lugha mbalimbali mfano
kifaransa, kijerumani na kiingereza. Fasili hizo zilizua msisimko wa shughuli
za kielimu, maarifa na utamaduni.
Enzi
za kati. Hiki ni kipindi kilichoonesha muamko wa kidini katika karne ya 16
ambapo ilianza ujerumani na kusambaa katika maeneo mengine ulimwenguni. Mwamko
huu ulipinga muundo, mwelekeo, falsafa na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya
wakati huo na matumizi ya lugha moja ya kilatini katika misa na mafunzo. Hali
hii ilisababisha mgawanyiko katika dini ya kikristo, watu mbalimbali walitafsiri
maandiko matakatifu katika lugha mbalimbali kwa mfano Martin Luther King
alitafsiri biblia takatifu kutoka kilatini kwenda kiingereza (1611) ikaitwa The
King James Bible, pia alitafsiri biblia kutoka kilatini kwenda lugha ya
kijerumani. Baada ya kuona tafsiri ya kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika
maandiko hayo matakatifu . Jarome alitafsiri biblia ya kigiriki na kiebrania
kutoka kwenye lugha ya kilatini
Enzi
za kisasa. Kipindi hiki kilikuwepo karne ya 20 ambapo kilijulikana kama kipindi
cha tafsiri kutokana na wingi au mfumuko wa tafsiri. Kipindi hiki kimetawaliwa
na masafa marefu ya mawasiliano, maendeleo makubwa ya kielimu na ethnolojia,
utandawazi na usomi wa lugha, isimu na fasihi. Mikataba ya kimataifa baina ya
mashirika ya umma na ya binafsi inafasiriwa kwa yeyote anayehitaji taarifa
hizo. Tafsiri ilikolea katika karne hii kutokana na kuzuka kwa mataifa mengi
huru yanayoteua lugha rasmi, lugha za taifa na lugha za elimu.
Kwa
hiyo baada ya hitaji kubwa la watu kutaka kuwasiliana na jamii au watu wa
mataifa, kabila tofauti. Kutokana na hitaji lake kubwa hilo imepelekea taaluma
hii kukuwa kwa kasi sana ukilinganisha kipindi cha nyuma hasa baada ya mapinduzi ya viwanda karne ya
18.
Baada ya kujadili historia na
mandeleo ya tafsiri ulimwenguni, sasa tunaweza kujadili historia na maendeleo
ya tafsiri nchini Tanzania.
Kwa ujumla historia na maendeleo ya
tafsiri nchini Tanzania haina historia ndefu sana kwani inaanzia mnamo karne ya
19 ambapo tunaweza kugawa historia na maendeleo haya katika vipindi vitatu
ambavyo, ni kabla ya utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na
baada ya uhuru.
Kabla ya utawala wa kikoloni, wamisionari
walitafsiri vitabu mbalimbali vya kikristo ikiwemo biblia takatifu kutoka lugha
ya kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila kwa lengo la
kueneza dini na ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.
Wakati wa utawala wa kikoloni, hiki
ni kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki wakoloni hasa waingereza
walitafsiri maandiko mbalimbali ya kitaaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya
Kiswahili. Mfano Pia kabla ya uhuru baadhi ya kazi za fasihi zilitafsiriwa kwa
mfano tamthiliya ya Mzimu wa Watu wa Kale iliyotafsiriwa na Mohamed
S. Abdalla (1960)
kutoka lugha ya kiingereza (Shrine of The Ancestors).
Baada ya uhuru ambayo ni kuanzia
mwaka 1961, katika kipindi hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri
vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili mfano mzuri ni Mwalimu Julius K.
Nyerere ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya
wa huko Uingereza William Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya Juliasi Kaizari
(Julius Caesar) (1963) na tamthiliya ya Mabepari wa Venis (The Merchant of
Venis) (1969).
Kazi
nyingine zilizotafsiriwa baada ya ukoloni ni pamoja na ushairi wa Wimbo wa
Lawino iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), kutoka lugha ya kiingereza
(Song of Lawino), riwaya ya Uhuru wa Watumwa
iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau (1967) kutoka lugha ya
kiingereza (The Freeing of The Slaves in
East Africa). Pia kazi nyingine za fasihi ambazo zimetafasiriwa kwa lugha
ya Kiswahili hapa Tanzania ni pamoja na Nitaolewa Nikipenda ambacho
kimetafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982) kutoka lugha ya kiingereza (I will marry when I Want).
Kwa sasa maendeleo ya taaluma ya
tafsiri nchini Tanzania yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na
teknolojia. Taaluma ya tafsiri kwa sasa inafundishwa katika elimu ya sekondari
na vyuo mbalimbali. Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri
zimeongezeka kwa mfano Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya
Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA),
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na International Language Orientation
Services (ILOS). Pia wapo wafasiri binafsi wanaofasiri lugha mbalimbali kama
vile Kiingereza, Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa nakadhalika.
Baada ya kujadili kuhusu historia na
maendeleo ya tafsiri ulimwenguni na nchini Tanzania, tunaweza kueleza kuwa, kwa
hakika ni kazi ngumu kupata kazi ya kwanza kufasiriwa nchini Tanzania, ila kwa
kutumia kigezo cha kihistoria tunaweza kusema kwamba kazi ya kwanza kutafsiriwa
nchini Tanzania ilikuwa ni biblia takatifu ambayo ilitafsiriwa na wamisionari
kutoka katika lugha ya kiingereza kwenda lugha nyingine za makabila kwa lengo
la kueneza dini na utamaduni wa kikristo ambayo pia ilikuwa ni njia ya kueneza
ukoloni.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa
taaluma hii ya tafsiri inazidi kukua karne hadi karne kutokana na maendeleo ya
sayansi na teknolojia yanayofungamana na maendeleo ya taaluma ya lugha na
ongezeo la mataifa huru yanayozungumza lugha tofauti. Kwa hiyo tafsiri ni kama
nyenzo kuu ya kuunganisha watu wa mataifa haya na hutumika kama njia kuu ya
mawasiliano.
MAREJEO.
As-Safi (1997) “Translation theories, strategies
Cartford. (1965). A linguistic Theory Translation.
Mshindo. B.H. (2010). Kufasiri na Tafsiri. Oxford University
Press. Dar es salaam.
Mwansoko. H.J.M na wenzake. (2006).
Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na Mbinu. TUKI. Dar es salaam.
Sofer.
M. (2006). The Translator’s Handbook.
Schreiber Publishing Rockville. U.S.A.
Wanjala,
S.F. (2011). Misingi ya Ukalimani na
Tafsiri. Kwa shule, vyuo na ndaki. Serengeti Bookshop.
Mwanza.
Uainishaji wa matini za tafsiri na mbinu za kutafsiri.
Uainishaji wa matini za tafsiri.
Lengo
la mfasiri bora katika kufanya tafsiri ni kutoa zao bora kabisa la tafsiri, ili kutimiza azma hii hulazimika kuainisha
kwanza aina ya matini ya tafsiri kabla hajaanza kufanya tafsiri. Ni muhimu kwa
mfasiri yeyote yule kuainisha kwanza aina ya matini kabla hajaanza kutafsiri
kwani kila aina fulani ya tafsri huwa na mbinu yake muafaka ya kutafsiri matini
husika.
Wataalam
wa tafsiri wamejaribu kuainisha matini za tafsiri kwa kutumia mikabala mitatu,
mikabala hiyo ni:
(a) Kwa
kutumia kigezo cha mada.
(b) Kwa
kutumia kigezo cha matumizi ya istilahi.
(c) Kwa
kutumia kigezo cha dhima kuu za lugha.
(a) Kwa kutumia kigezo cha mada.
Kwa
kutumia kigezo hiki tunapata aina kuu tatu za matini, mada inayozungumziwa
katika matini ndio hutusaidia kujua kuwa hiyo ni aina fulani ya matini,
kinachoangaliwa ni maudhui ya matini inayoshughulikiwa. Kwa hiyo kwa kigezo
hiki tunapata:
i) Matini
za kifasihi; mfano, riwaya, hadithi fupi, tamthilia n.k
ii) Matini
za kiasasi; mfano, maandiko ya kisiasa na kiserikali kama vile hotuba, risala,
propaganda n.k.
iii) Matini
za kisayansi. Matini za namna hii huhusika na fani zote za sayansi kama vile
fizikia, kemia, baiolojia n.k.
(b) Kwa kutumia kigezo cha matumizi ya
histilahi.
Kigezo
hiki huangalia kiwango cha matumizi ya istilahi za uwanja fulani maalum katika
matini husika. Hivyo kutokana na kigezo
hiki tunapata makundi matatu; matini zenye kiwango cha juu cha istilahi, matini
zenye kiwango cha kati cha istilahi na matini zenye kiwango cha chini cha
istilahi. Hivyo kwa kuangalia kiwango cha ujitokezaji wa istilahi katika matini
tunapata matini zifutatazo:
i) Matini za kiufundi, hizi zinakuwa na matumizi
makubwa ya istilahi.
ii) Matini za nusu ufundi, hizi zinakuwa na kiwango
cha kati cha matumizi ya istilahi (zinakuwa na istilahi chache).
iii) Matini zisizo za kiufundi, hizi zinakuwa hazina
matumizi ya istilahi na hivyo hutumia msamiati wa kawaida.
(c) Kwa kutumia kigezo cha dhima kuu za
lugha.
Kwa
mujibu wa Bülher (1965) lugha yoyote ile duniani ina dhima kuu tatu ambazo ni:
i) Dhima
elezi (expresive function). Kazi ya lugha ni kuelezea hisia za mzungumzaji au
mwandishi bila kumjali msikilizaji au msomaji. Kiini ni mwandishi au
mzungumzaji.
ii) Dhima
arifu (informative function). Hapa lugha hutumika kutolea taarifa. Kiini cha
dhima hii ni ukweli wa mambo.
iii) Dhima
amili (provocative function). Lugha hutumika kuchochea hisia za msikilizaji au
msomaji. Kiini cha dhima hii ni hadhira.
Kulingana
na dhima hizi tatu za lugha tunapata aina tatu za matini ambazo ni:
i) Matini
elezi.
Matini hizi huegemea zaidi upande wa mwandishi, mfano
fasihi, maandiko ya kimamlaka kama vile hotuba, mikataba, maandiko ya kisheria,
maandiko ya kitaaluma, wasifu, tawasifu, shajara n.k.
ii) Matini
arifu.
Hii ni matini inayokusudia kutoa maarifa kuhusu mada
yoyote au jambo fulani. Sifa za matini arifu ni pamoja na kwamba huwa katika
muundo maalumu au maumbo sanifu, mfano; kitabu, makala, jarida, ripoti, tasnifu
n.k.
iii) Matini
amili.
Matini amili huegemea zaidi upande wa hadhira,
mwandishi huchochea hisia za wasomaji ili watende kama yeye anavyotaka. Mfano;
mialiko, matangazo, maelekezo (jinsi ya kutumia kitu).
Vigezo
hivi vyote vilivyotumika kuainisha matini za tafsiri vyote vinajaribu kuonesha
kuwa kuna aina tofautitofauti za matini ambazo mfasri anaweza kukutana nazo. Kwa
ujumla matini hizo zinaweza kuwa za kisayansi, za kifasihi au za kisheria.
Kwa
misingi hii sisi tunaona kwamba kigezo kizuri zaidi cha kuainisha matini za
tafsiri ni kigezo kinachozingatia dhima za lugha, hii ni kwa sababu kigezo hiki
kinakwenda mbele zaidi na kuangalia kusudi la matini husika na kwa hiyo hii
itamsadia mfasiri kujua nia au kusudi la matini na kumrahisishia kuchagua mbinu
inayofaa kufasiri matini husika. Pia vile vile katika kigezo hiki aina zingine
za matini zilizoainishwa kwa kuzingatia kigezo cha mada na kigezo cha matumizi
ya istilahi huapatikana katika kigezo hiki. Kwa mfano, katika kigezo cha mada
tunapata matini kama za kifasihi, kisayansi na kiasasi lakini matini hizi
huweza kuainishwa kama matini elezi tunapotumia kigezo cha dhima kuu za lugha.
Kwa
hiyo kigezo cha dhima kuu za lugha ni kigezo muafaka zaidi katika uanishaji wa
matini za tafsiri kwani hukusanya taarifa nyingi muhimu ambazo huhitajika na
mfasiri ili kuteua njia muafaka zaidi katika kufasiri.
Mbinu za kutafsiri.
Baada
ya kuangalia aina mbalimbali za matini sasa tuangalie mbinu zinazoweza kutumika
katika kufasiri aina fulani ya matini.
Kazi
ya kufasiri inahitaji umakini wa hali ya juu; ili kupata tafsiri iliyobora,
wataalam wamebuni mbinu mbalimbali za kufasiri kutegemeana na matini husika.
Kuna mbinu nne zinazohusika katika tafsiri, mbinu hizo ni kama zifuatazo:
i) Tafsiri ya neno kwa neno
ii) Tafsiri sisisi
iii) Tafsiri ya kisemantiki
iv) Tafsiri ya kimawasiliano
Hebu
sasa tuziangalie kwa kina mbinu hizi na namna zinavyoweza kutumika katika
matini ya tafsiri.
i) Mbinu ya tafsiri ya neno kwa neno.
Hii
ni mbinu ambayo kwayo maneno hufasiriwa kwa kuchambuliwa mofimu zinazounda
maneno hayo na kwa kuzingatia maana ya msingi/maana ya kikamusi ya maneno
katika matini hiyo.
Mfano.
1. Alisafiri kwa basi. Sentesi hii
inaweza kufasiriwa kwa mbinu ya neno kwa neno kama ifuatavyo:
A
– li – safiri kwa basi.
S
/he |past| travel by bus.
Mfano.
2. Alikunywa maji mengi.
A
– li – ku – nyw – a maji mengi.
S
/he |past| |inf.| drink water many.
Mfano.
3. Walimpa msukumo mkubwa kwenye biashara yake.
Wa
– li – m – p – a msukumo mkubwa kwenye biashara yake.
They
|past| |object| |give| pressure big in business his/her.
Mfasiri
anayetumia mbinu hii ni lazima achambue mofimu za lugha chanzi na ndipo aandike
chini ya matini ya lugha chanzi. Katika mbinu hii muundo wa lugha chanzi utazingatiwa
hata kama muundo wa lugha hizo mbili haufanani. Mbinu hii hutumika zaidi katika
masuala ya utafiti wa lugha lakini pia huweza kutumika katika hatua za awali
mfasiri anapoanza kufasiri matini.
Udhaifu
wake.
a) Mbinu hii haitoi maana kwa uangavu, unaposoma
maana haijitokezi.
b) Maana za misemo na nahau hupotea kwa sababu
hutafsiriwa kisisisi.
c) Husomeka vibaya yaani haina mtiririko
unapotaka kufuatilia ujumbe.
d) Hukiuka muundo wa lugha lengwa na hivyo husababisha
kupotea kwa ujumbe uliopkuwa umekusudiwa.
ii) Mbinu ya tafsiri sisisi.
Hii
ni mbinu ambayo hutumika kufasiri maneno yakiwa pwekepweke kwa kuzingatia maana
zake za msingi yaani maana za kikamusi. Katika mbinu hii mfasiri anapofasiri
huzingatia muundo wa lugha lengwa.
Hebu
tuangalie mifano ifuatayo:
Mtoto wa nyoka ni nyoka.
o The
chilid of a snake is a snake.
Ø
Subira huleta heri.
o Patience
brings blessing.
Ø
Penye nia pana njia.
o Where
there is a will there is a way.
Ø
Mwenda pole hajikwai.
o He
who moves forward slowly does not trip.
Ø
Walimpa msukumo mkubwa kwenye biashara
yake.
o They
gave him/her a big push in his/her business.
Mifano
hiyo hapo juu huonesha tafsiri sisisi inayvofanyika, licha ya kuzingatia muundo
wa lugha lengwa lakini pia mbinu hii ina ubora na udhaifu wake.
Ubora
wake ni kwamba maana halisi ya lugha chanzi huzingatiwa kwa kuwa maneno
hufasiriwa kwa kuzingatia maana ya msingi.
Udhaifu
wa mbinu hii ni kwamba:
a) Haizingatii muktadha, kwa mfano methali,
nahau na misemo pia hufasiriwa kisisi.
b) Wakati mwingine hutoa tafsiri mbovu, hupotosha
ujumbe uliokuwa umekusudiwa.
iii) Mbinu ya tafsiri ya kisemantiki (tafsiri ya wazi)
Katika mbinu hii wafasiri husisitizwa kuzingatia vipengele vyote vya matini chanzi. Kila neno katika matini chanzi hufasiriwa bila kuacha neno lolote. Vipengele vya kisemantiki huzingatiwa kwa ukaribu.
Pia
vilevile ni muhimu kuelewa mwandishi alikusudia nini na hivyo kumfanya mfasiri
anapofasiri asibadili chochote katika matini chanzi.
Mfano
wa tafsiri ya kisemantiki:
Ø
Ilikubaliwa kwamba….
o It
was agreed that….
Ø
Mheshimiwa spika, nachukua nafasi hii…
o Honorable
speaker, I take this opportunity…
Ø
At the end of the day.
o Mwisho
wa siku.
Ø
Ladies and gentlemen.
o Mabibi
na Mabwana.
Faida
ya mbinu hii ni kwamba inasaidia kueleza ukweli wa mambo kama ulivyo katika
matini chanzi. Pia husaidia kuleta msamiati mwingi katika lugha lengwa, hii ni
kwa sababu neno ambalo litakosa kisawe chake katika lugha lengwa litachukuliwa
kama lilivyo kutoka katika lugha chanzi na hivyo kuingiza msamiati mpya katika
lugha lengwa.
Udhaifu
wa mbinu hii ni:
a) Mbinu hii huweza kusababisha kuwa na matini
pana na fafanuzi, matini huweza kuwa ndefu kuliko ile matini ya lugha chanzi.
b) Huweza kupatikana matini inayosomeka vibaya.
c) Huwa na mjirudio wa taarifa.
d) Haihamasishi mfasiri kuzingatia taarifa za kitamaduni.
e) Maranyingi hutumika kufasiri matini elezi
kama vile fasihi, wasifu, tawasifu, nyaraka za kisheria, nyaraka za kisiasa,
hotuba n.k.
iv) Mbinu ya tafsiri ya kimawasiliano.
Hii
ni mbinu inayotumika katika kufasiri matini ikizingatia zaidi ulewekaji wake
katika hadhira lengwa. Mbinu hii husisitiza kuzingatia utamaduni wa lugha
lengwa. Zao la tafsiri linatakiwa lieleweke vyema katika lugha lengwa bila
ukakasi kwa maana kinachosisitizwa hapa ni uwepo wa mawasiliano yaani ujumbe
uliokusudiwa katika lugha chanzi ufike katika lugha lengwa bila kupotoshwa.
Katika
mbinu hii mfasiri anakuwa huru kutumia methali, nahau na misemo. Matini
zinazofaa katika kutumia mbinu hii ni kama vile matini zenye lengo la
kuelimisha au kushawishi au kuarifu.
Mifano
ya tafsiri ya kimawasiliano:
Ø
Tanzania National Electric Supply Company
Limited.
o Shirika
la umemeTanzania.
Ø
A bird in the hand is worth two in the
bush.
o Fimbo
ya mbali haiui nyoka.
Ø
A burnt child dreads fire.
o Mtoto
akililia wembe, mpe.
Ø
Actions speak louder than words.
o Ada
ya mja hunena, mwungwana ni kitendo.
Ø
A drowning man will catch at a straw.
o Mfa
maji haachi kutapatapa.
Ø
All good things come to those who wait.
o Subira
huvuta heri.
Ø
A stitch in time saves nine.
o Usipoziba
ufa utajenga ukuta.
Ø
As you sow, so you shall reap.
o Mpanda
ovyo, hula ovyo.
Ø
Charity begins at home.
o Kutoa
ni moyo si utajiri.
Ø
Clothes don’t make the man.
o Usichague
mchumba siku ya Idi.
Ø
Mtoto wa nyoka ni nyoka.
o Like
father like son.
Ø
Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.
o Wonders
never end!
Kwa
hiyo mfasiri yeyote yule ni muhimu kuteua mbinu atakayotumia wakati wa
kutafsiri kulingana aina ya matini anayotaka kutafsiri. Hata hivyo ni vigumu
kutumia mbinu moja pekee katika kutafsiri, kwani mbinu zote huweza kujitokeze
katika tafsiri kwa mfano, maneno mengine huweza kufasiriwa kisisi au
kisemantiki lakini pia ni lazima iwepo mbini ambayo inatawala mbinu zote.
Wataalam wengi wa tafsiri wanapendekeza mbinu ya tafsiri ya kimawasiliano
itumike zaidi hususani katika matini zenye lengo la kuelimisha au kuleta athari
sawa na ile ile iliyopo katika matini chanzi. Matini kama vile za kisheria
mbinu muafaka zaidi ni ile ya kisemantiki.
Zoezi.
1. Taja na fafanua aina za matini ya tafsiri.
2. Kwa kutumia kigezo cha dhima kuu za lugha,
taja na fafanua aina za matini za tafsri.
3. Ainisha kigezo kinachofaa kuainisha matini za
tafsiri kasha toa sababu kwanini kigezo hicho kinafaa.
4. Taja na fafanua mbinu zinazotumika katika
tafsiri.
5. Onesha ubora na udhaifu wa mbinu ya
kisemantiki.
6. Tafsiri sentensi ifuatayo kwa kiswahili:
A habit
is a second nature.
i)
Kisisisi……………………………………………………………………
ii)
Kisemantiki……………………………………………………………..
iii)
Kimawasiliano………………………………………………………….
7. Tafsiri sentensi ifuatayo kwa kiingereza:
Maji yakimwagika hayazoleki.
i) Kisisisi…………………………………………………………………………
ii)
Kimawasiliano…………………………………………