HISTORIA YA FASIHI SIMULIZI YA KIAFRIKA KWA MTAZAMO WA NADHARI ZA UTANDAWAZI, UTAIFA NA HULUTISHI.
Utangulizi
Fasihi simulizi kwa mujibu wa Mlokozi (1996), ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Hivyo fasihi simulizi inafungamana  na muktadha au mazingira fulani ya kijamii na kutawaliwa na muingiliano wa mambo kama vile Fanani, Hadhira, Fani inayotendwa, Tukio, Mahali pamoja na Wakati wa utendaji.
            Balisidya (1983) anasema fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
Mteru,M (1983) anasema fasihi simulizi ni aina ya fasihi inayotumia mdomo kwa kuumba na kusambaza.
            Fasili zote zinazungumzia kitu kilelekile kwamba fasihi simulizi inategemea sana uwepo fanani, hadhira, jukwaa na mada inayotendwa. Hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya kisanaa ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa kwa njia ya mdomo au masimulizi.
Kwa upande wa nadharia, tunaweza kusema kuwa nadharia, ni mawazo au muongozo unaomuongoza mtafiti au mchambuzi wa jambo Fulani ili kuweza kulikabili jambo hilo ambalo halijapata kupatiwa ufumbuzi au ukweli wake.
             Nadharia  ya fasihi simulizi ilianza katika elimu ya ushairi wa Wagiriki toka karne ya 18. Mnamo karne ya 20 nadharia za fasihi simulizi zimezua mikabala mikubwa katika usomaji wa matini. Kwa hiyo nadharia ya fasihi simulizi ni mawazo yanayotoa muongozo kuhusu muelekeo wa jambo Fulani katika fasihi simulizi. Kwa kufanya hivyo nadharia hizo zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo kwa mfano utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, jando na unyago umeathiriwa na ujio wageni.
                                                  
                                                            MJADALA            
Watafiti wa kimagharibi na wa kiafrika wameangalia mambo mengi yaliyoikabili fasihi simulizi ya kiafrika na mawazo yao ni kama yafuatavo:
            Kwa kuanza na mawazo ya wana nadharia ya utandawazi na ambayo imegawanyika katika makundi matatu ambayo ni:
            Nadharia ya Ubadilikaji taratibu.  Muasisi wa nadharia hii ni Charles Dawin (1809-1882), na wafuasi wake waliamini kuwa kuna misingi anuai kuhusu kanuni zinazoongoza asili na maendeleo ya utamaduni wa mwanadamu. Kundi hili liliona kuwa dhana ya ubadilikaji taratibu misingi yake mikuu ni Viumbe hai.
            Wanasema Viumbe hai vyote vinakuwa katika mchakato wa mabadiliko mbalimbali hadi kufikia kwenye maumbo yao ya sasa. Hivyo na Fasihi simulizi imepitia michakato mingi ya mabadiliko mpaka kufikia katika umbo lake la sasa mfano Fasihi  simulizi ya kipindi cha Ujima ni tofauti na fasihi iliyofuata katika vipindi vingine kama vile wakati wa Utumwa, Ubepari  hata mfumo tulionao sasa.
             Hivyo fasihi similizi ya kiafrika hubadilika kutoka kipindi kimoja hata kingine kutokana na mabadiliko ya kijamii. Kwa ujumla wasisi hawa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni jamii yenyewe na kutokea kwa kufanana kwa kazi za fasihi simulizi kutoka jamii moja hadi nyingine kunasababishwa na hatua sawa za mabadiliko kiakili na kijamii kwani jamii moja iliyozagaa ulimwenguni kote akili zao ni sawa.
            Nadharia ya Msambao, Waasisi wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na wanaubadilikaji taratibu ambao (wanaubadilikaji taratibu) waliamini kuwa kufanana kwa fani mbili za kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa za kimaendeleo, wanamsambao  wanaamini kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea sababu ya msingi ya mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani jamii hizo ziliwahi kukutana kwa namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana baadhi ya mila na desturi.
            Kwa ujumla mawazo ya wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa kutoka katika jamii imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo dhaifu. Hivyo basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi ya kiafrika ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda sehemu nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano ushairi wa simulizi wa kiswahli ulitoka Uarabuni na uajemi kuja Afrika na huko ndiko ambako kulionekana kuwa kumesataarabika kuliko Afrika na ndio maana ushairi huo uliletwa huku Afrika.
Wananadharia hii wanaamini kuwa asili ya fasihi simulizi ya kiafrika ni ulaya, jambo ambalo hatuwezi kukubaliana nalo kwani kila jamii ina fasihi yake na kutokea mfanano wa baadhi ya kazi za fasihi  huenda kuna kuathiriana kwa namna Fulani miongoni mwa jamii hizo.
Nadharia ya Kisosholojia. Nadharia hii ya kisosholojia ina mihimili mitatu ambayo ni  ule wa Umahususi na sio umajumui, mkazo katika utendaji na mhimili unaosisitiza dhima ya fasihi simulizi katika jamii.
Kwa kuanza na mhimili wa Umahususi, nadharia hii ilijikita zaidi katika jamii peke yake badala ya kujikita katika taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla kama walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi. Hii ilikuwa baada ya kugundua dosari zilizofanywa hapo kabla, Dosari ya kutoa tamko la juu juu na la jumla zaidi ambapo matamko hayo mara nyingi yalitupilia mbali vipengele fulani vya lugha na mienendo mingine ya jamii.
Pia katika mhimili wa utendaji, Wanasosholijia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji (performance) wa kazi mbalimbali ya fasihi simulizi. Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya fasihi wanaujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa husika na jambo hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha utendaji. Vilevile  wamedokeza sifa za ndani za fasihi simulizi ya kiafrika, na hivyo wao wanaona kuwa ili kujua fasihi simulizi ya kiafrika ni vyema kuangalia jamii na utendaji wa kazi husika.
 Katika msisitizo juu ya dhima ya Fasihi simulizi katika jamii, Wanasosholijia wanaamini kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.
Hivyo ili kuelewa historia ya fasihi simulizi kutokana na mawazo ya wanasosholojia ni wazi kwamba  unapaswa kuangalia jamii husika, utendaji na dhima ya fasihi katika jamii husika, kwani mihimili hii ndiyo chanzo au historia ya fasihi simulizi ya jamii husika. kutokana na mawazo ya wananadharia hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya kiafrika ni ndani ya jamii za Kiafrika zenyewe na singinevyo.
Nadharia ya Utaifa. Nadharia hii ilizuka kwenye vugu vugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa  wanadai kuwa wananadharia wa nadharia ya utandawazi hawakuwa  na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za kiafrika, Kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na wazungu kupita mlango wa ukoloni.
Nadharia ya Utaifa. Imeasisiwa na S. Adeboye, Babalola, Daniel P. Kunene na J. P Clark. Katika ndharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa kuondoa. Kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti bali kuyahariri matokeo yao. Na wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.
Hivyo Ili kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu  na wanazuoni wa taifa au jamii hiyo. Kwasababu wataalamu na wanazuoni hao ndio wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.
 Kiujumla wananadharia ya kitaifa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ya kiafrika inapatikana ndani na jamii ya kiafrika na ili kuchunguza fasihi ya jamii husika sharti wataalamu na wanazuoni wa jamii hiyo wahusishwe.
Nadharia Hulutishi. Nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni wa kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza taaluma ya fasihi ya kiafrika. Wanandharia hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni na ya kijadi zimeathiriana  na kuingiliana. Miongoni mwa waasisi na wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na M.M. Mlokozi, Johnson na Ngugi wa Thiong`o.  Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na wakijadi.
Kwa ujumla nadharia zote tatu zimejaribu kuangalia chimbuko la fasihi simulizi na kutoa muelekeo kuhusu asili ya fasihi simulizi ya kiafrika, Hata hivyo fasihi simulizi ya kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni lakini ilianza kupata athari mara baada ya ujio wa wageni, athari na muingiliano wa fasihi simulizi hauoneshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwakuwa fasihi yoyote lazima iathiriwe na iathiri fasihi nyingine. Hivyo basi kila jamii au taifa huwa na fasihi yake na utamaduni wake ambapo maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza kuathiriana na hivyo kuathiri pia fasihi ya jamii husika.
  
MAREJEO.
Materu, M. (1983). “Fasihi simulizi na uandishi wa Kiswahili katika Fasihi,” Makala ya semina za Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI. 
Mlokozi, M. M. (1996). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. TUKI.
Okpewho, I. (1992). The study of Oral Litereture. Bloomington and Indianapolis. Indians: University Press.
 







FASIHI LINGANISHI YA KISWAHILI NA TAFSIRI
1.0 Utangulizi
Makala haya yanalenga kufanya uchunguzi katika kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili zilizotafsiriwa. Katika uchunguzi huu, vitu tutakavyoangalia ni pamoja na mapitio ya fasihi za Kiswahili zilizotafsiriwa, tathimini ya mapitio hayo kwa kuangalia utanzu uliotafsriwa zaidi, lugha zilizojitokeza zaidi katika tafsiri hizo na kisha tutaangalia utanzu unaokabiliwa na changamoto nyingi zaidi wakati wa kutafsiri. Pia tutaangalia uchambuzi wa kazi teule kwa kuangalia kama ni tafsiri  bora au mbovu na kuangalia mchango wa kazi hiyo katika fasihi linganishi ya kiswahili pamoja na chagamoto zitokeazo wakati wa kufasiri matini za kifashi.Na mwisho kabisa ni hitimisho juu ya mjadala huu.
2.0 Usuli
Dhana ya Fasihi linganishi kwa kumrejelea Henry Remak (1971) anafasili fasihi linganishi kama uwanja wa kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusianao ya kifasihi nje ya mipaka ya nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo. Kwa maelezo haya ya Remak tunachoweza kusema ni kwamba fasihi linganishi haiishii kuangalia mahusino ya kifasihi peke yake bali huangalia mahusiano kati ya fasihi na fani nyinginezo zisizo za kifasihi.

Kwa upande wa tafsiri, Catford akinukuliwa na Mwansoko (2006) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa).

Kwa ujumla tafsiri ni mchakato wa uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au maana katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine (kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa).
3.0 Mapitio ya kazi zilizotafsiriwa
Tafsri imeonekana kuwa nyenzo muhimu sana katika kukuza na kusambaza fasihi. Katika uaandaaji wa makala haya data zilizokusanywa za kazi za kifashi zilizotafsiriwa ni kumi na tatu (13), kazi hizi zimeoneshwa vizuri katika jedwali hapo chini. Kwa kuangalia data hizi tunaweza kuona mchango wa tafsri katika fasihi ya Kiswahili. Tafsiri imesaidia kuingiza utanzu mpya wa fasihi andishi katika fasihi ya Kiswahili, hapo mwanzo kabla ya tafsri, fasihi ya kiswahili haikuwa na utanzu wa tamthilia lakini kwa kutumia tafsiri hivi sasa tamthilia ni moja kati ya tanzu muhimu katika fasihi ya Kiswahili. 

Vilevile tafsiri imesaidia kueneza fasihi ya Kiswahili na utamaduni wake, kuna kazi za fasihi ya kiswahili zilizotafsiriwa kwa lugha nyingine za kigeni kwa mfano riwaya ya “Utengano” imetafsiriwa kama “Separazione” katika lugha ya kiitaliano, hii inaashiria kuwa fasihi ya kiswahili imeenea hadi mataifa mengine. Pia tafsiri inakuza lugha ya fasihi husika, kupitia tafsiri msamiati mpya unaingia katika lugha husika, tukijua kwamba lugha ndio mhimili wa fasihi, kwa hiyo msamiati ukiimarika fasihi pia huimarika.

Jedwali hili hapa chini linaoonesha data zilizokusanywa zinazoonesha fasihi ya Kiswahili iliyotafsiriwa ama kutoka lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya kigeni au kutoka lugha yakigeni kwenda lugha ya Kiswahili.

Jedwali la data za vitabu vilivyotafsiriwa
Jina la kitabu
Utanzu
Mfasiri
Wakati
Lugha husika
Barua ndefu kama hii
Riwaya
Charles Maganga
1994
Kiingereza-Kiswahili
Kusanyiko la mashairi
Ushairi
Ally A. Jahadhymy
1975
Kiingereza-Kiswahili
Tufani
Tamthilia
Samweli S. Mushi
1969
Kiingereza-Kiswahili
Shetani msalabani
Tamthilia
Ngugi Wa Thiong’o
1982
Kiingereza-Kiswahili
Wimbo wa Lawino
Ushairi
Paul Sozigwa
1975
Kiingereza-Kiswahili
Mtawa Mweusi
Tamthilia
Ngugi Wa Thiong’o
1970
Kiingereza-Kiswahili
The freeing of slaves in East Africa
Riwaya
EALB
1967
Kiswahili-Kiingereza
Separazione
Riwaya
Flavia Aiello
2005
Kiswahili-Kiitaliano
Mkaguzi wa Serikali
Tamthilia
Joshua Madumulla
1999
Kiingereza-Kiswahili
Hadithi ya Mvuvi na Samaki wa Dhahabu
Tamthilia
Joshua Madumulla
2001
Kiingereza-Kiswahili
Nitaolewa Nikipenda
Tamthilia
Clement M. Kabugi
1982
Kiingereza-Kiswahili
Orodha
Tamthila
Saifu D. Kiango
2006
Kiingereza-Kiswahili
Mabepari wa Venisi
Tamthilia
J.K Nyerere
1969
Kiingereza-Kiswahili
4.0 Tathimini ya mapitio ya kazi zilizotafsriwa
Kulingana na data zilizokusanywa tunaweza kuona utanzu uliotafsiriwa sana kutoka lugha za kigeni hususani Kiingerza ni tamthilia, hii ni kutokana na sababu zifuatazo:

Kwa lengo la kujifunza utamaduni wa kigeni lakini pia wasanii walipata fursa ya kujifunza mbinu za utunzi wa utanzu huu kwani ulionekana kuwa ni mgeni katika mazingira ya kiafrika.Kwa ajili ya kusomwa na kuigizwa, (Mwansoko 2006). Pia kwa lengo la kufikisha maudhui fulani katika jamii ya lugha lengwa.

Sababu nyingine ya kufasiri kazi za kifasihi hususani tamthilia ni kukuza lugha zenye maandishi machanga (G. Ruhumbika 2003). Lugha nyingi za kiafrika Kiswahili kikiwa ni miongoni mwao hazikuwa zimeendelea sana kimaandishi, hasa maandishi ya kifasihi, kwa hiyo tafsiri za tamthilia zililenga kukuza maandishi ya lugha ya kiswahili. Na vilevile tamthilia ilitasiriwa sana kwa lengo la kuongeza machapisho ya fashi ya Kiswahili.

Lugha zilizojitokeza sana katika kufanikisha suala la tafsiri, kwa mujibu wa data zilizokusanywa ni Kiswahili na Kiingereza. Hii ni kwa sababu wafasiri wengi walikuwa wanamudu vizuri lugha hizi mbili kuliko lugha nyingine za kigeni.

Katika ukusanyaji wa data hizi imegundulika kwamba utanzu unaokabiliwa na changamoto zaidi katika kufasiri ni utanzu wa ushairi. Changamoto hizi hutokana na vitu kama vile: Lugha yake kuwa ngumu na ya kisanaa, kutumia maneno ya mkato na machache, matumizi ya lugha ya kitaswira, muundo na mtindo wake kuwa tofauti na tanzu nyingine, kwa mfano urari wa vina na mizani ni moja ya vipengele muhimu katika ushairi na ni vipengele ambavyo huleta changamoto sana katika kufasiri mashairi.

Namna ya kuziepuka changamoto hizi Mwansoko (2006) akimnukuu Newmark 1988 amependekeza njia zifuatazo: Kuchagua aina ya ushairi katika lugha lengwa inayoshabihiana na lugha chanzi au iliyo mwafaka zaidi kwa matini lengwa yake.Mfasiri hushughulikia tamathali za semi, picha na istiari zote katika shairi na kuzifasiri ipasavyo katika lugha lengwa. Kusawazisha shairi. Pia mfasiri anapaswa kufasiri vipengele vya shairi kulingana na jinsi linavyomwingia   na kumwathiri yeye.
Kwa kuzingatia vipengele hivi angalau mfasiri anaweza kukabiliana vyema na changamoto za kufasiri ushairi.
5.0 Uchambuzi wa kazi teule “Nitaolewa nikipenda”
“Nitaolewa nikipenda” ni tamthilia iliyoandikwa na Ngugi Wa Thiong’o na Ngugi Wa Mirii, awali kwa lugha ya Gikuyu kama “Ngaahika Ndeenda” na baadaye akaitafsiri kwa lugha ya Kiingereza kama “I will marry when I want”. Tafsiri ya Kiswahili ilitoka katika lugha ya Kiingereza na tafsiri hii ilifanywa na Clement M Kabugi (1982). Kwa kweli tunaweza kusema tafsiri ya “Nitaolewa 

Nikipenda” ni tafsiri bora ya fasihi. Kwa mujibu wa Hassan (2011) anaonesha sifa za tafsiri ya kifasihi kuwa ni pamoja na: Fasihi iliyotafsiriwa lazima ionyeshe hisia, izingatie fani na maudhui, iwe ina ruhusu ufafanuzi wa maana tofautitofauti, inatumia mbinu maalumu ili kuibua athari za kimawasiliano, inatabia za kupindisha kaida za lugha, inaelezea hisia binafsi.

Kwa ujumla vipengele hivi vimezingatiwa kwa kiasi kikubwa katika tafsiri ya “Nitaolewa Nikipenda”. Mfasiri amejitahidi katika kuifanya matini lengwa ifanane na matini chanzi. Amefanikiwa kufasiri kwa kuzingatia mtindo wa kiuandishi wa tamthilia ya matini chanzi. Matini chanzi imeandikwa kwa mtindo wa kishairi lakini pia tunaona tafsri yake imeandikwa kwa mtindo huohuo, hili ni suala muhimu sana katika kufasiri matini za kifasihi, hivyo tunaweza kusema kipengele hikikimefanikiwa.

Vilevile tafsiri imezingatia muundo wa matini chanzi, matini chanzi inamuundo wa matendo matatu na hivyo ndivyo inavyoonekana katika matini lengwa. Pia katika uhawilishaji wa vipengele vya kisanaa kama vile nyimbo, tamathali za semi na nahau, kwa kiwango kikubwa zimetafsiriwa kwa ubora unaohitajika. Mfano wa wimbo uliotafsiriwa vizuri:
Kiingreza                                                                             Kiswahili
Wangeci the beautiful one                                               Wangeci kisichana kizuri
Wangeci the beautiful one                                               Wangeci kisichana kizuri
With the body slim and straight like eucalyptus               Kizuri kama malaika
With the body slim and straight like eucalyptus uk.23     Kizuri kama malaika uk.29
Ukiangalia kwa haraka unaweza kusema kuwa tafsiri hii imekosewa hususani katika mistari miwili ya mwisho lakini kimsingi mfasiri amefasiri vizuri kwa lengo la kuleta athari ya kimawasiliano katika utamaduni wa lugha ya Kiswahili. Kwa mfano msemo “A man brags about his own penis, however tine”, umetafsiriwa kama“Kila ndege huruka kwa ubawa wake”.A fool’s walking stick supports the clever”.Uk.22 ametafsiri kama“mjinga ndiye aliwaye”.Tafsiri ya namna hii pia mi naona ni nzuri kwani imetafsiriwa kimawasiliano na kimsingi haijapoteza maana ya msemo wa matini chanzi.

Vilevile tafsiri hii ni bora kwani unapoisoma haionekani kama imetafsiriwa, msomaji wa lugha lengwa anaposoma anapata athari ileile kama ilivyokusudiwa katika matini chanzi, hii ni kwa sababu vipengele vya fani na maudhui vimetafsriwa vizuri, kwa kiwango kikubwa mfasiri kafanikiwa kuhawilisha maudhui kama ilivyokusudiwa katika matini chanzi. Hivyo kwa misingi hii tunaweza kusema tafsiri hii ni bora. Lakinihii haimaanishi kuwa hakuna mapungufu katika tafsri hii. Mapungufu yapo ingawa ni machache sana.

Kuna upotoshaji wa maana katika baadhi ya vipengele vilivyotafsiriwa kwa mfano, sentensi “Even if poverty was to sell at five cents i would never buy it” imetafsiriwa kama “Dhiki hata ikiuzwa kwa senti moja naweza kununua, uk. 4”. Kimsingi tafsiri kama hii inapotosha maana ambayo ilikusudiwa katika matini chanzi, sentensi ya matini chanzi inalaani dhiki lakini hii ya matini lengwa inaona ni mbaraka. Pamoja na makosa haya kwa kiwango kikubwa mfasiri kafanikiwa, hata hivyo wataalamu wa tafsiri wanaamini kuwa hakuna tafsri iliyokamilifu na hiki ndicho tunachokiona katika tafsri hii.
5.1 Mchango wa tafsiri katika Fasihi Linganishi ya Kiswahili
Tafsri hutusaidia kujua na kuliganisha tamaduni za jamii nyingine na ile iliyoandikiwa tafsiri. Tamthilia ya “Nitaolewa Nikipenda” imetungwa katika mazingira ya jamii ya kikuyu, hivyo tafsiri ya tamthilia hii imesaidia kujua utamaduni wa Wakikuyu. Kwa mfano katika ukurasa wa 65, tunaweza kuona jinsi ndoa ya kikuyu inavyofungwa, utaratibu wa utoaji mahari pamoja na nyimbo ziimbwazo wakatika wa sherehe.

Pia kupitia tafsiri tunaweza kujua historia ya jamii husika. Katika tafsiri ya tamthilia hii tunaona historia ya taifa la Kenya tangu wakati wa ukoloni hadi wakati wa uhuru. Kwa hiyo hapa tunaelewa yale yote wananchi wa Kenya waliyoyapitia wakati wa ukoloni, kwa mfano katika uk. 32 mwandishi anaonesha adha walizopitia wananchi wa Kenya katika harakati za kupigania uhuru na baadae wakafanikiwa, uk 33. Pia tunaona katika uk. 34 wananchi wanaingia katika kipindi kingine cha uhuru lakini bado wanaendelea kupata adha zilezile kama walizozipata wakatiwa ukoloni.

Vilevile tafsiri husaidia kukuza fasihi ya lugha lengwa. Kupitia tafsiri fasihi ya lugha lengwa inanufaika na kuingizwa vipengele kadhaa vya lugha hususani misemo au methali ambazo hazikuwepo katika lugha lengwa, hivyo kwa kutafsiri misemo hii lugha lengwa nayo pia itakuwa imenufaika na misemo hiyo, kwa mfano, msemo; “when axes are kept in a one basket they must necessarily knock agaist each other” umefasiriwa kama;“vyuma vikiwa katika gunia moja havikosi kugongana” uk. 24. Kwa hiyo tunaweza kuwa tumeongeza msemo mwingine katika Kiswahili kupitia tafsiri hii. Vilevile tafsri ya tamthilia hii imeongeza idadi ya machapisho ya fasihi ya Kiswahili na hivyo itakuwa imeimarisha fasihi ya Kiswahili.

Pia tafsiri hutusaidia kujua itikadi ya mwandishi na pengine itikadi ya jamii husika. Kwa muktadha wa tamthilia hii tunaona mwadishi, anapinga sana tamaduni na  mtindo wa maisha ya kimagharibi ikiwa ni pamoja na dini za kigeni, lugha zao na mambo yote yaliyoletwa na wakoloni, uk. 5.

5.2 Changamoto katika kufasiri matini za kifasihi
Matiniza kifasihi ni tofauti kabisa na matini nyingine, lugha ya kifasihi ni tofauti kabisa na lugha ya 
kawaida na hii ndio haswa husababisha kuwapo na changamoto. Lugha ya kifasihi imetawaliwa na misemo, nahau, methali na tamathali za semi, vipengele hivi kimsingi ndio huunda lugha ya kifsihi. Na kwa hiyo mfasri anapokuwa katika mchakato wa kufasiri matini za kifashi ni lazima akumbane na changamoto katika kufasiri vipengele hivi. Kwa mfano anaweza kukutana na methali au msemo ambao haupo katika lugha lengwa kwa hiyo katika mchakato wa kufasiri anaweza kukosa kisawe cha methali au msemo huo katika lugha lengwa na akaishia kufasiri kisisisi au kutumia kisawe ambacho hupotosha maana. Kwa mfano, methali “A rich man’s fart does not stink” imetafsriwa kama“Mashuzi ya tajiri hayachukizi”. Ugumu aliopata mfasiri katika kufasiri methali ndio maana akaamua kufasiri kisisisi, lakini kimsingi ingetakiwa kutafutwa kisawe chake.

Tofauti za kiutamaduni, kuna maneno mengine ambayo sio rahisi kupata kisawe chake katika lugha nyingine, kwa hiyo mfasiri anapokutana na maneno kama hayo hupata changamoto kubwa kwa mfano, maneno kama kiruru na kang’aari uk. 103ni maneno ya kitamaduni yanayomaanisha aina ya pombe na hivyo mwandishi ameyaacha kama yalivyo.          

Endapo mfasiri hatokuwa na taaluma ya kutosha juu ya fasihi, hataweza kufasiri kwa uzuri  misemo, mafumbo, nahau, tamathali za semi na hata miundo na mitindo inayotumika katika kazi husika, kwa hiyo kufasiri matiniza kifasihi pia uhitaji utaalamu katika uwanja huo.
6.0 Hitimisho
Katika makala haya tumeangalia vitabu vya fasihi ya Kiswahili vilivyotafsiriwa, tumeangalia umuhimu wa tafsiri katika fasihi linganishi na pia tumeangalia changamoto zinajitokeza katika kufasiri matini za kifashi. Kwa hiyo kulingana na makala haya tunaweza kuona nafasi ya tafsiri katika taaluma ya fasihi linganishi, hivyo kuna ulazima mkubwa mtu anayeshughulika na tafsiri awe ni mjuzi wa fasihi, hii ni kwa lengo la kuzalisha zao bora la tafsiri ya kifasihi. Lakini pia kuna ulazima mkubwa kwa mtaalamu wa fasihi linganishi kujua taaluma ya tafsiri kwa sababu anapofanya ulinganishi kati ya tafsri na kazi za kifasihi ni lazima awe na uelewa wa kutosha juu ya taaluma ya tafsri. Kwa hiyo fasihi linganishi na tafsiri, kimsingi ni taaluma zinazoshikamana kuliko kuachana.
Marejeo
Aiello, F. (2005). “Translating a Swahili Novel into “Kizungu”: Separazione, the Italian                                  edition of Said Ahmed Mohamed’s Utengano”. Swahili Forum 12, 99-107.                                            Johannes Gutenberg University: Mainz, Germany.
Gromova, N.V (2004). “Tafsiri Mpya za Fasihi ya Kirusi. Kiswahili”. Swahili                                                   Forum 11, 121-125. Johannes Gutenberg University: Mainz, Germany.
Hassan, B.A (2011). Literary Translation:  Aspects of Pragmatic                                                       Meaning.                   Cambridge   Scholars Publishing: Cambridge.
Mwansoko, H.J.M na wenzake(2006) .Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na Mbinu. TUKI.                       Dar-es-salaam
Remak, H.H. (1971). Comperative literature: Its Definition and Function. Carbondale:                            Southern Illinois.
Ruhumbika, G. (2003). “Tafsiri za Fasihi za Kigeni Katika Ukuzaji wa Fasihi ya                        Kiswahili”.Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahil (2003). TUKI. Dar es Salaam.
Wa Thiong’o, N. & Wa Mirii (1982). I Will Marry When I Want. East African Educatinal                                            Publishers: Nairobi.
Wa Thiong’o, N. & Wa Mirii (1982). Nitaolewa Nikipenda. East African Educatinal                                Publishers: Nairobi.












CHIMBUKO LA RIWAYA NINI?

 Katika kujadili, mjadala huu, utajikita zaidi kwa kutoa maana ya riwaya kutoka kwa wataalamu mbalimbali, maana ya riwaya ya Kiswahili, maana ya chimbuko, Kisha mjadala huu utaelekea zaidi katika kuelezea chimbuko la riwaya ya Kiswahili kutokana na wataalamu mbalimbali waliopata kueleza asili ya riwaya hiyo ya Kiswahili, na hicho ndio kitakachokuwa ni kiini cha swali. mwisho kabisa hitimisho la kazi litapata kuonyeshwa pamoja na maoni ya wanakikundi .Kwa kuanza na maana ya riwaya imejadiliwa kama ifuatavyo:
Wamitila (2003:178), anasema riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina, yenye kuchukua muda mwingi katika maandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Muhando na Balisidya (1976:62), wanasema riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake.Wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35000 hivi na kuendelea.
Nkwera (1978:109), anasema riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza kutosha kufanya kitabu kimoja au zaidi. Ni hadithi ya kubuniwa iliyojengwa juu ya tukio la kihistoria na kuandikwa kwa mtindo wa ushairi iendayo mfululizo kwa kinaganaga katika kuelezea maisha ya mtu au watu na hata taifa.Anaendelea kusema kuwa riwaya ina mhusika mkuu mmoja au hata wawili.
Senkoro, anasema riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake. Anaendelea kusema kuwa ni hadithi ndefu ya kubuni, yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatiwa kwa undani na upana wa maisha ya jamii.
Hivyo inaonyesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi, na mambo hayo ni; lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari, isawiri maisha ya jamii, iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu, wahusika zaidi ya mmoja, iwe na mpangilio na msuko wa matukio, lazima na maneno kuanzia elfu thelathini na tano na kuendelea, na mwisho riwaya ni lazima ifungamane na wakati yaani visa na matukio ni lazima viendane na matukio.
Baada ya kuangalia maana ya riwaya kutokana na wataalamu mbalimbali sasa ni vyema kutoa maana ya riwaya ya Kiswahili kaba ya kujadili chimbuko la riwaya.
Riwaya ya Kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili katika lugha ya kisahili.Pia ni ile riwaya ambayo inawahusu waswahili wenyewe.
TUKI (2004:48) inasema chimbuko la maana yake ni mwanzo au asili.
Tanzu za asili zinaonyesha kuwa ndio zilichangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuibua riwaya za Kiswahili.Na yafuatayo ni mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya chimbuko la riwaya ya Kiswahili.
Madumulla (2009) ameeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, na ngano inayosimuliwa kwa mdomo.Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na maandiko ya fanai ya ushairi hususa ni tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndiyo maanadishi yaliyotamba katika pwani ya afrika mashariki. Wazungu na waarabu hawakubadilishana maarifa kwa urahisi na hivyo pakapelekea kuwa na majilio ya taratibu za maandiko ya ya kinathari. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa Kiswahili toka katika lugha za ulaya na kufanya riwaya za Kiswahili kutokea.Mfano wa riwaa hizo ni kama vile; Habari za mlima iliyoandikwa na Sheikh Ali Bin Hemed (1980).
Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi.Anaendelea kusema kuwa riwaya za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za kiwsahili.Anasema riwaya mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa. Ndiyo riwaya ya kwanza kutafsiriwa kwa Kiswahili.Pia Senkoro (2011) anaeleza kuwa  riwaya ni utanzu uliozuka  kutokana na hali mahususi za kijamii.Riwaya kama ile ya kiingereza ya Robinson  Crusoe iliyoandikwa na Daniel Defoe  ni miongoni mwa riwaya za mwanzo. Anasema riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni na viwanda.Suala la ukoloni  na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa mawanda mapana zaidi  ya yale ya ngano na hadithi fupi. Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya mapinduzi ya viwanda huko ulaya kilifanya waandishi waandike maandiko marefu kwani wakati huo ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi.
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo; ni fani za kijadi za fasihi pamoja na mazingira ya kijamii.
Fani za kijadi za fasihi,Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haikuzuka hivihivi tu bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi, na ndipo zikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo.Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile; riwaya za kingano,tendi,hekaya, visakale,historia, sira, masimulizi ya wasafiri, insha na tafsiri.
Ngano, Mulokozi anasema, kuwa ngano ni hadithi fupi simulizi pia huwa ni hadithi za kubuni na nyinga hasa zinawahusu wanyama wakali,pia zinahusu malaika,binadamu, mazimwi na majini. Anasema kuwa mara nyingi ngano huwa na msuko sahihi na wahisika wake ni bapa na wahisika hao ni mchanganyiko wa wanyama, mazimwi na binadamu.Anatolea mfano wa ngano zilizo chukua visa vya kingano kuwa ni kama vile riwaya ya Adili na Nduguze ya Shaban Robart (1952), Lila na Fila ya Kiimbila(1966), Kusadikika ya Sharban Robart (1951) na baadaye yakafuata machapisho mengine kama vile;Mfalme wa Nyoka ya  R.K. Watts.Dhamira za riwaya za kingano ni kama vile choyo,mgongano wa kimawazo na tama.
Hekaya, ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabu yaani yasiyokuwa ya kawaida. Mara nyingi masaibu hayo hufungamanishwa na mapenzi. Pia hekaya ni ndefu kiasi yaanai sio ndefu kiasi cha kama riwaya.Katika jamii ya waswahili hekaya zilijkuwa zimeenea sana kipindi cha kabla ya ukoloni.Mifanio ya hekaya ni kama vile;Hekaya za Abunuasi ya C.M.C.A. 1915, Sultan Darai (1884), KIbaraka ya (1896) na hekaya ya Jonson, F. na Brenn, E.W.katika hekaya ya Alfa-Lela-Ulela ya kuanzia 1929.Hizo ndizo baadhi ya hekaya za mwanzo lakini baadaye ziliathili riwaya za Kiswahili kama vile; Hekaya ya Adili na Nduguze ya Sharban Robart  (1952), hekaya ya Ueberu Utashindwa ya Kiimbila (1971),na Hekaya ya A.J.Amiri,ya Nahodha Fikirini, (1972).
Tendi (utndi), ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, ambao waweza kuwa ni wa kijamii au kitaifa.Kwa kawaida baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya ila tu badala ya kuwa na umbo la kinathari zenyewe zina umbo la kishairi. kuna tendi za aina mbili ambazo ni tendi andishi na tendi simulizi.Riwaya pevu kama tendi huwawiri mawanda mapana ya kijamii na kihistoria.Huwa na wahusika wababe yaani mashujaa wenye kuwakilisha pande zinazopingana.Mtano wa tendi ni kama vile; Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mlima ya Hemedi Abdallah, (1895), Utendi war as (Ghuli), utenzi wa Fumo liyongo wa Mohamed Kijumwa K. (1913).Tendi katika riwaya za Kiswahili imetumia wahusika wawili tu ambao ni wahusika wa kubuni na wale wa kijadi wa kiafrika.
Visasili, hizi ni hadithi zinazohusu asili na hatima ya watu, vitu, viumbe, ulimwengu na mataifa, na pia huangalia uhusiano wa wanadamu na mizimwi pamoja na miungu. Hadithi za kivisasili zinapoonyeswa huaminika kuwa na kweli tupu hasa kwa kusimulia matukio mengi ya kiulumwengu.
Mfano wa visasili; Lila na Fila ya Kiimbila (1966) ambayo imekopa motifu ya asili ya ziwa ikimba huko Bukoba.Hadithi ya Mungu wa Kikuyu huko Kenya.Roza Mistika ya Kezilahabi (1971), Nagona (1987) na Mzingile (1991), Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robart.
Visakale, ni hadithi ya kale kuhusu mashujaa wa taifa,kabila au dini.Mara nyingi visa kale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni, na hadithi hizi hupatikana karibu katika kila kabila na kila lugha.Baadhi ya visakale vya Kiswahili masimulizi huhusu chimbuko la mij ya pwani, mijikenda,mwinyi mkuu huko Zanzibar.Visa kama hivi ndivyo vinavyopelekea kuandikwa kwa riwaya za kliswahili. Mfano wake ni riwaya ya Abdalla Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972) katika kitabu cha Habari za Wakilindi, Kisima cha Giningi ya M.S.Abdulla (1968) na ile Hadithi ya Myombekela na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buhliwali (1980) ya A. Kitereza.
Visasuli, hizi ni hadithi zozote ambazo huelezea chimbuko au asili ya kitu chochote na maranyingi visasuli havina uziyo wowote kulinganisha na visasili.mafano wake ni;kwa nini paka anapenda kukaa jikoni(mekoni), Kwa nini mbuni hana mabawa yaani hapai angani, kwa nini kima anamuogopa mamba,kwanini mbwa huishi na binadamu,kwa nini fisi hupenda kula mifupa.Katika hadithi hizi watu huwa hawaamini sana bali wanachukulia kuwa ni utani tu.
Masimulizi ya kihistoria, haya ni masimulizi mya matendo ya mwanadamu katika muktadha wa wakati,na ni fani muhimu sana katika jamii yeyote ile.Masimulizi halisi ya kihistoria yaweza kuwa ni ya m domo au hata maandishi na yote huwa ni chemichemi nzuri ya riwaya. Mfano wa riwya hizo ni; Habari za pate za Fumo Omari Nabhany (1913) ambayo yalikuwa ni maandishi ya masimulizi na uchambuzi.Riwaya zingine zilizoathiriwa na matukio ya kihistoria ni; Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934), Kifo cha Ugenini ya O. Msewa (1977), Kwa Heri Iselamagazi ya B. Mapalala (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika (1992).
Sira,ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu au watu.Sira huweza kuwa wasifu yaani zinazohusu habari za maisha ya mtu zikisimuliwa na mtu mwingine au zaweza kuwa tawasifu yaani habari za maisha ya mtu zikisimuliwa nay eye mwenyewe. Sira iliathiri kuchipuka kwa riwaya hasa kwa kuonyesha masilmulizi ya maisha ya mtu toka utotoni mpaka uzeeni. Masimuliza ya riwaya hizi yalikuwa katika masimulizi na hata katika maandishi pia kwa maana kabla ya ukoloni yalikuwepo mandishi yaliyohusu maisha ya mitume na masahaba.Mifano ya hadithi hizi ni;Kurwa na Doto ya M. S.Farsy (1960), Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971),Kichwa Maji ya Kezilahabi (1974) pamoja na Dunia Uwanja wa Fujo (1975),Mzimu wa Baba wa Kale ya Nkwera (1967),na riwaya ya Maisha Yangu baada ya Miaka Hamsini ya Sharban Robart (1951).
Msimulizi ya wasafiri,  hizi ni habari zinazosimulia masibu nya wasafiri katika nchi mbalimbali. Hekaya za riwaya chuku za kale zilisaidia kukuza riwaya.Mfano Alfa –Lela –Ulela na hadithi ya Robinson Kruso huko 1719 ilihusu safari ya baharini ya mhusika mkuu ambaye baadaye  merikebu aliyokuwemo ilizama, ndipo akalazimika kuishi peke yake katika kisiwa kidogo.Na katika riwaya za Kiswahili kuna baadhi ya riwaya za masimulizi kama vile;Mwaka katika Minyororo ya Samweli Sehoza (1921),Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932) ya Martin Kayamba.Na  uhure wa Watumwa na Kwa Heri Eselamagazi.
Insha, ni maandiko ya kinathari yenye kuelezea,kuchambua au kuarifu kuhusu mada Fulani.Zipo insha za zina nyingi kama vile,makala,hotuba,tasnifu,michapo,barua, sira  maelezo n.k insha nyingi ni fupi mfano kuanzia maneno kama 500 na 10000 japo zingine zaweza kuwa ni ndefu kiasi cha kuwa tasnifu za kufikia kiwango cha kuwa kitabu.Mfano wa insha ni Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robert na Kichwa Mji ya Kezilahabi.
Shajara, ni kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku .Uandishi wa shajara ulianzia huko Asia na baadaye ndio ulipopata kuibuka ulimwenguni kote.Jadi hii ya kiasia iliathiri utunzi wa riwaya hasa zile za kisira.Mfano wa shajara ni ile iliyotungwa na Lu Shun  iitwayo Shajara ya Mwendawazimu (1918).
Romansia (chuku) hii ni hadithi ya mapenzi na masaibu ya ajabu.Zikua maarufu sana huko  Uingereza hasa karne ya 6 na 12 na Ufaransa pia zilikuwepo na pamoja na China ambapo hadithi zilizofanana na riwaya zilitungwa.mfano hadithi za Hsiao-shuo .Watunzi wa riwaya za kisasa zimekuwa na mafanikio makubwa sana kutokana na riwaya hizo za chuku hii ni kwa sababu watunzi wengi wlikuwa wamesoma kazi nyingi za riwaya za wakati ule.
Drama, maigizo mengi hasa ya tamthiliya yaliathiri sana riwaya hasa kwa upande wa usukaji wa matukio na uchanganyaji wa ubunifu na uhalisia.Mfano ni riwaya nyingi za Charles Dickens zina msuko uliosanifiwa kwa uangalifu kama msuko wa tamthiliya.
Baada ya kujadili fani za kijamii hatuna budi sasa ya kujadili mazingira ya kijamii kama yalivyopatwa kuelezwa na Mulokozi.Anaeleza kuwa, kufikia karne ya 16 fani za kijamii zilikuwa zimekwisha enea na kufahamika katika maeneo mengi,hivyo kulihitajika kuwe na msukumo wa kijamii, kiteknolojia na kiuchuni.Msukumo huo wa kundeleza fani za kijadi ulikuwa ni wa aina tatu ambao ni;
Ukuaji mkubwa wa shughuri za kiuchumi huko ulaya,ukuaji huo ulifungamana na biashara ya baharini ya mashariki ya mbali na kuvumbuliwa kwa mabara mawili ya amerika na ukuaji wa viwanda hasa vya nguo huko ulaya.Mabadiliko haya yalizua tabaka jipya la mabwanyenye waliomiliki viwanda na nyenzo nyingine za kichumi.Tabaka hilo lilihitaji fani mpya za fasihi, lilikuwa na wakati wa ziada wa kujisomea, uwezo wa kifedha wa kujinunulia vitabu na magazeti.Hivyo tangu mwanzo ilitawaliwa na ubinafsi uliojidhihirisha kiitikadi.Kwa mfano Robinson Kruso ni riwaya ilyosawili ulimbikizaji wa mwanzo wa kibepari.Ilimhusidhs muhusika asiye staarabika aitwaye Fraiday au Juma. Ubinafsi hu ulijitokeza pia katika utungaji wake ,na haikusomwa hadharani bali kila mtu alijisomea mwenyewe chumbani mwake.
Mageuzi ya kijamii na kisiasa, mabadiliko haya yalifungamana na mabadiliko ya kiuchumi. Mataifa ya ulaya yalianza kujipambanua kiutamaduni na kisiasa yaliyojitenga na dola takatifu ya kirumi.Mabadiliko hayo yalianza kujenga utamaduni wa kitaifa na mifumo ya elimu iliyo hiyaji maandishi katika lugha zao wenyewe.Mfano wa mageuzi ya kijamii na kisiasa iliyofanyika ni kama vile; Misahafu ya Dini Kama Biblia ilanza kutafsiriwa kwa lugha za ulaya, Martin Lther alichapisha Biblia kwa lugha za kidachi miaka ya 1534.Hivyo basi inaonyesha kuwa kadiri elimu ilivyopanuka na nduvyo wasomaji wa vitabu walivyoongezeka na kufanya kuwe hadhira kubwa nzuri ya wasomaji na watunzi wa riwaya.
Ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa vitabu, yaani kwa kutumia herufi iliyoshikamanishika.Ugunduzi huu uliofanywa na Johnnes Gutenberg huko ujerumani mwaka 1450 uliorahisisha kazi ya uchapaji vitabu katika nakala nyingi nakuondoa kabisa haja ya kunakili misswada kwa mikono. Bila ugunduzi huo kufanyika haingewezekana kuchapisha riwaya nyingi na kuzieneza kwa bei nafuu.Nmifano ya riwaya hizo ni kama vile; Pamela ya Samwel Richardson (1740).
Kutokana na wataalamu mbalimbali kueleza chimbuko la riwaya ya Kiswahili, inaonekana kuwa,riwaya ni utanzu wa fasihi ambao kuzuka kwake kulifungamana na fani za kijadi pamoja na mazingira ya kijamii.Fani za kijamii kama vile, ngano, visasili, visasuli, visakale,insha,na nyinginezo zizosimuliwa bila ya kuandikwa kabla ya karne ya 16,zilichochewa na kupewa mwendelezo baada ya kukua kwa sayansi na teknolojia huko ulaya,hasa baada ya ugunduzi wa mitambo ya kupiga chapa kazi za fasihi.                                                          
MAREJEO
Madumulla, J.S. (2009), Riwaya ya Kiswahili, Historian a Misingi ya Uchambuzi. Nairobi: Sitima
Printer and stations L.td.
Mulokozi, M.M.(1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili.Dar es Salaam.TUKI.
Mhando, P. na Balisidya,(1976), Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania
Publishing House.
Nkwera, F.V. (1978),Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo.Dar es Salaam: Tanzani Publishing
House.
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Nairobi.Kenya: Oxford University Press.
Senkoro, F.E.M.K.(2011), Fasihi Andishi.Dar es Salaam.Kauttu L.t.d.
Wamitila, K.W.(2003),Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication.  
Powered by Blogger.