Dhana ya Nadharia
Dhana ya Nadharia
Dhana
ya nadharia imejadiliwa na wanazuoni mbalimbali ambao wamekuja na mitazomo
tofauti tofauti kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Wamitila, (2003:22)
“nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani :
chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na
nje”
TUKI (2004:300) wanasema “nadharia ni
mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au
kutekeleza jambo fulani”
Fasili
hii ya TUKI inafanana kwa kiasi fulani na fasili ya Mdee (2011) anayefasili
nadharia kuwa ni mpango wa maneno uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au
kutekeleza jambo fulani. http://kapeleh.blogspot.com/2014/05/nadharia-za-maana.html
Kwa
msingi huo nadharia hubeba mawazo ,dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au lengo
la kueleza hali fulani, chanzo,muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.
Kuna
nadharia mbalimbali ambazo zimejadiliwa na wanazuoni mbalimbali, baadhi ya
nadharia hizo ni pamoja na nadharia ya maana, nadharia za kifalsafa,
kihistoria, nadharia ya fasihi, nadharia za chimbuko la lugha ya Kiswahili,
nadharia ya chimbuko na chanzo cha lugha.
Naye Wafula na Njogu (2007:7) wamefasili dhana ya
nadharia kama ni jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu
kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu. Fasili hii imeegemea hasa katika
nadharia ya uhakiki wa fasihi. Pia imetaja vitu muhimu kama vile, maelekezo
ambayo ndiyo yanamuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya
hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha.
Pia Sengo (2009:1) anafasili
nadharia kuwa ni wazo kuu fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya
pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni
dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na
kiutamaduni.
Ili kuweza kudhibitisha maelezo
yaliyotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya nadharia ni vyema
kuangalia mfano mmojawapo wa nadharia, ambayo ni nadharia ya sarufi. Katika
nadharia hii kuna wanaisimu mbalimbali wamejitokeza kuelezea nadharia ya sarufi
kwa mitazamo tofauti tofauti ambayo imeweza kuibua nadharia mbalimbali za
sarufi kama vile nadharia ya sarufi mapokeo, nadharia ya sarufi msonge na
nadharia ya miundo virai.
Katika nadharia ya sarufi
mapokeo Mgullu (1999:68) anasema ni sarufi ya kale iliyochambuliwa kwa kutumia
vigezo vya lugha za Kilatini na Kigiriki zilizokuwa na mnasaba mmoja, yaani
zilikuwa na asili moja. Kwa mantiki hiyo lugha za Kilatini na Kigiriki zilikuwa
kama kiolezi cha kuchanganulia lugha nyingine ikiwemo lugha ya Kiswahili. Kwa
mfano wanaisimu wa Kilatini waliposema kuna aina nane za maneno na baadhi yao
katika lugha ya Kiswahili wakasema kuna aina nane za maneno bila kuzingatia
kwamba lugha hutofautiana. Pia nadharia hii ilijikita na sentensi sahili,
haikujishughulisha na miundo kwa marefu
na mapana.
Baada ya kuonekana sarufi mapokeo
ina udhaifu mkubwa iliibuka nadharia ya sarufi msonge. Mgullu (1999:70) anaiona
sarufi hii ni sehemu ya mkabala wa kimapokeo isipokuwa mkabala huu unaiona
lugha kuwa ni mfumo mkuu yenye mifumo mingi ndani yake kama vile mifumo midogo
ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.
Katika karne ya kumi na nane na
kumi na tisa sarufi mapokeo ikafikia kilele ndipo ikaibuka nadharia ya sarufi miundo
virai. Nadharia hii inadokeza kuwa tungo imeundwa na viambajengo ambavyo vina
uhusiano na vipo kidarajia. Kwa mujibu wa Mgullu (1999:70) isimu muundo
imejitokeza sana katika maandishi ya akina Harris, Ferdinand De Saussure,
Trubetzkoy na Bloomfield.
Katika
mkabala huu lugha ilionekana kuwa na viambajengo kama vile: maneno, kirai,
kishazi na sentensi na kwamba viambajengo hivyo vina uhusiano mkubwa na viko
katika kidarajia toka chini hadi juu. Kwa mfano
Mkulima bora analima vizuri
Katika
sentensi hii kuna uhusiano wa karibu wa viambajengo vifuatavyo; N+V yaani
nomino “mkulima” na kivumishi “bora”, hali kadhalika, T+E, yaani kitenzi
“analima” na kielezi “vizuri”.
Katika
mkabala huu dhana ya uchamko ikaibuka kuonyesha uwezekano wa kuzalisha sentensi
bila kufika kikomo. Kwa mfano,
Waziri fisadi amekamatwa jana na rais
akiiba fedha za wananchi.
Hivyo
ili kuwa na nadharia inayokubalika katika jamii ni muhimu kuzingatia fasili ya
Sengo, (2009:1) ambaye anasema kuwa “nadharia ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo
mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani”.
Kwa
mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa,
kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
Kwa ujumla nadharia huchukuliwa
kuwa ni dira ya kumwongoza mtafiti au mchambuzi kulikabili na kulielezea vyema
jambo fulani kwa mtazamo unaotazamiwa kuwa imara zaidi kuliko ule wa nadharia
nyingine. Nadharia hutoa mwongozo katika utatuzi wa jambo fulani ambalo
halijaweza kuhakikishwa ukweli wake. Ni mawazo , maelezo au mwongozo uliopangwa
ili kusaidia kutatua au kutekeleza jambo fulani kifalsafa, kidini, kimantiki,
kijamii na kiutamaduni.
MAREJEO
http://manyamacharles.blogspot.com/2014/06/uhakiki-wa-nadharia-ya-ki-marx-katika.html
by Manyama Charles, 12 june 2014
http://nenothabiti.blogspot.com/p/fasihi.html
by Anonymmous Said, 31 October 2013 at 9:39AM
Sengo,
T.S.Y.M (2009) Fasihi za Kinchi. Dar es Salaam: The Trustees of Al Amin
Education and Research Academy
TUKI
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI
Wamitila,
K.W (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Kenya Focus
Publications Ltd
Wafula,
R.M & Njogu, K (2007) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation