FASIHI LINGANISHI NA TAFSIRI TIMOTHEO CHARLES
FASIHI LINGANISHI NA TAFSIRI
TIMOTHEO CHARLES
UTANGULIZI.
Makala hii inalenga kueleza juu ya suala zima la tafsiri na mchango wake katika kukuza fasihi linganishi ya Kiswahili. Makala hii itaanza kwa kueleza maana ya fasihi linganishi na maana ya tafsiri kama ilivyofafanuliwa na wataalamu mbalimbali. Baada ya tafsiri hizo makala hii itaendelea kuchambua tafsiri katika fasihi linganishi ya Kiswahili mkazo ukitiliwa zaidi mchango wa tafsiri na kuonyesha kuwa tafsiri ni nyenzo muhimu katika kukuza fasihi. Data hizi zitaonyesha jina la kazi husika, jina la mfasiri, wakati au kipindi ambacho kazi hiyo imefasiriwa na lugha iliyotumika kufanya tafsiri. Pia makala hii itaonyesha utanzu ulioingiza kazi za fasihi za kigeni kwa njia ya tafsiri, utanzu unaokabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kutafsiri na namna ya kukabiliana na changamoto hizo. Sehemu inayofuata ya makala hii itaonyesha kwa kina utanzu mmoja kati ya zilizopo kwenye jedwali kama kielelezo cha kueleza ama tafsiri ni mbovu au ni bora katika kazi za fasihi na kisha utafuata uchambuzi wa kazi mojawapo ya fasihi msisitizo ukiwa hasa kwenye mchango wa tafsiri katika fasihi linganishi ya Kiswahili pamoja na changamoto zitokanazo na mchakato wa tafsiri katika kufasiri matini za kifasihi.
Tukianza na maana ya fasihi linganishi na maana ya tafsiri kama zilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali. Maana ya fasihi linganishi,
Wamitila (2003) anaeleza kuwa fasihi linganishi inahusu uchambuzi wa maandishi ya wakati mmoja na aina moja na katika lugha mbalimbali kwa nia ya kumiliki sifa zinazoyahusisha kama athari, vyanzo, sifa zinazofanana na tofauti za kiutamaduni. Anaendelea kueleza kuwa inawezekana kufanya hivi kwa nia ya kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au hata nadharia za kiuhakiki. Fasihi ya namna hii iliweka misingi na juhudi za wanaisimu kuanza kuilinganisha lugha mbalimbali katika karne ya kumi na tisa. Hivyo tunaweza kusema kuwa faasihi linganishi inajikita zaidi kutumia mbinu za kiulinganishi baina ya kazi mbili za kifasihi ili kujua sifa fulani fulani kama vile kufanana kwa kazi hizo, tofauti za kiutamaduni katika kazi hizo, kujua ulinganishi katika lugha yaani sarufi ya lugha katika kazi hizo za kifasihi.
Baada ya kueleza maana ya fasihi linganishi kwa kifupi ufuatao ni ufafanuzi wa tafsiri kama ulivyoelezwa na wataalamu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006) wanaeleza kuwa tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Woa wanatilia mkazo katika zoezi la uhawilishaji na kinachohawilishwa ni mawazo katika maandishi. Pia wakimnukuu Catford (1965) yeye anaeleza kuwa kufasiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha mmoja yaani lugha chanzi na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka katika lugha nyingine yaani lugha lengwa. Hapa msisitizo upo katika matini zilizoandikwa na kuzingatia zaidi ujumbe au wazo lililopo katika matini chanzi lijitokeze vile vile katika matini lengwa. Mawazo haya hayawezi kuwa sawa kabisa na ya matini chanzi bali ni mawazo yanayolingana toka matini chanzi na matini lengwa, hii ni kutokana na sababu tofauti kama vile utamaduni, historia, kiisimu na mazingira.
Naye Newmark (1982) anaeleza kuwa tafsiri ni mchakato wa uhawilishaji wa maneno kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.
Pia Nida na Taber (1969) wanaeleza kuwa tafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe vya asili vya lugha lengwa vinavyo karibiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo. Wao wanatilia mkazo uzalishaji upya wa kwa kutumia visawe asili vinavyokaribiana na matini chanzi kimaana na kimtindo. Kutokana na maana hizi tunaweza kusema kuwa tafsiri hufanywa katika ujumbe uliopo katika maandishi, ni jaribio la kiuhawilishaji, na wazo linalatafsiriwa huwa na visawe vinavyokaribiana na sio sawa kutokana na tofauti za kiisimu, kihistoria, kiutamaduni na mazingira.
Kwa kiasi kikubwa tafsiri ni nyenzo muhimu sana ya kukuza fasihi ya Kiswahili kwani husaidia katika ukuzaji wa msamiati. Kwa mfano katika makala ya G. Ruhumbika katika Makala za semina ya kimataifa ya waandishi wa Kiswahili (ii) anaeleza kwa upande wa lugha ya Kingereza inasemekana maneno mapya 12000 yaliingizwa miaka 1500 na 1650. Mfano huu unajidhihirisha hata lugha ya Kiswahili kuna maneno ambayo yameingizwa kutoka lugha za kigeni ambayo ni ya kawaida kwa sasa na yanatumika mfano neno data, drama, thieta na kathalika.
Pia tafsiri husaidia jamii lengwa kujifunza utamaduni wa jamii chazi ambapo tunaweza kujifunza mwenendo bora wa kiutamaduni, kihistoria, kiuchumi na kijamii.
Tafsiri husaidia kuchambua viepengele na mbinu za matini chanzi kama vile mtindo, muundo ujenzi wa wahusika na mandhari. Kwani tukizingatia kazi za kifasihi lazima ziwe na uwezo wa kuathiri na kuathiriwa kwa baadhi ya vipengele vya kazi zingine. Hivyo tafsiri ni nyenzo ya mawasiliano ambapo ujumbe wa lugha chanzi huwafikia jamii lengwa wakapata itikadi, tamaduni na histiria za jamii chanzi.
MAPITIO YA KAZI ZA FASIHI YA KISWAHILI ZILIZOTAFSIRIWA.
NA
|
JINA LA KAZI
|
UTANZU WAKE
|
JINA LA MFASIRI
|
KIPINDI
|
LUGHA ILIYOFASIRIWA
|
|||
1.
|
Sundiata
|
Tamthiliya
|
E. Mbogo
|
2011
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
2.
|
Safari za Guiliver
|
Hadithi fupi
|
Genesis press Kiswahili
|
2010
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
3.
|
Bwana Myombokere na Bwana bugonyoka
|
Riwaya
|
Aniceti Kitereza
|
1980
|
Kikerewe - Kiswahili
|
|||
4.
|
Wimbo wa lawino
|
Ushairi
|
Paul Sozigwa
|
1975
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
5.
|
Mabepari wa venisi
|
Tamthiliya
|
Mwl. J.K.Nyerere
|
1969
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
6.
|
Juliasi kaizari
|
Tamthiliya
|
Mwl. J. K. Nyerere
|
1964
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
7.
|
Hekaya za abuniasi
|
Hadithi fupi
|
S. Chiponde
|
1928
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
8.
|
Alfu lela ulela. Kitabu 4.
|
Hadithi fupi.
|
Edwin W. Brenn
|
1994
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
9.
|
Nitaolewa nikipenda
|
Tamthiliya
|
C.M. Kabugi
|
2010
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
10.
|
Barua ndefu kama hii
|
Riwaya
|
C. Mganga
|
1994
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
11.
|
Mfalme edpod
|
Tamthiliya
|
S.S. Mushi
|
1971
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
12.
|
Wema hawajazaliwa
|
Riwaya
|
Abdilatif Abdallah
|
1976
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
13.
|
Mtawa mweusi
|
Tamthiliya
|
EAEP LTD
|
2008
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
14.
|
Aliyeonja pepo
|
Tamthiliya
|
Maritin Mkombo
|
1980
|
Kiswahili - Kingereza.
|
|||
15.
|
Alfu lela ulela. Kitabu 2.
|
Hadithi fupi
|
Hassan Adam
|
2004
|
Kijerumani -Kiswahili.
|
|||
16.
|
Makbeth
|
Tamthiliya
|
S.S. Mushi
|
1969
|
Kingereza -Kiswahiki.
|
|||
17.
|
Mchuuzi muungwana
|
Tamthiliya
|
A. Morrises
|
1961
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
18.
|
Kisima chenye hazina
|
Hadithi fupi
|
F. Jameson
|
1928
|
Kingereza - Kiswahili
|
|||
19.
|
Robinson crusoe
|
Hadithi fupi
|
Genesis press Kiswahili
|
2010
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
20.
|
Masaibu
ya ndugu jero
|
Tamthiliya
|
A .S.
Yahya
|
1974
|
Kingereza
- Kiswahili
|
|||
21.
|
Mkaguzi mkuu wa serikali
|
Tamthiliya
|
C. Mwakasaka
|
1979
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
22.
|
Mnafiki
|
Tamhiliya
|
L.
Taguaba
|
1973
|
Kingereza
- Kiswahili.
|
|||
23.
|
Orodha
|
Tamthiliya
|
Said, D. Kiango
|
2006
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
24.
|
|
Riwaya
|
|
1973
|
Kingereza - Kiswahili.
|
|||
25.
|
Uhuru wa watumwa
|
Riwaya
|
Thomas Nelson
|
Kingereza - Kiswahili.
|
||||
Utanzu ulioingiza zaidi fasihi ya kigeni ni tamthiliya. Hii ni kwa sababu tamthiliya na muundo wake ni zao toka Ulaya. Hapa Afrika tulikuwa na sanaa za maonyesho tu baada ya ujio wa wakoloni ndio tamthiliya zikaingizwa Afrika kwa lengo la kuchekesha. Baadhi ya wataalamu kama vile Mulokozi (1996) anaeleza kuwa Afrika kulikuwa na sanaa za maonyesho. Anasema tamthiliya asili yake ni huko Ulaya ambapo zilitokana na miviga na viviga na ziliathiri sana sanaa za maonyesho baada ya kuingia Afrika. Kutokana na maeleza haya tunaweza kusema kuwa ujio wa tamthiliya umeathiri sanaa za maonyesho za jadi. Hivyo utanzu ulioingiza fasihi ya kigeni ni tamthiliya kwani hata muundo wake ni wamagharibi. Hapa Afrika tamthiliya zilitafsiriwa kwa lengo la kuigizwa. (Mwansoko na wenzake 2006).
Lugha ambazo zimejitokeza zaidi kufanikisha suala la tafsiri ni Kingereza, Kiswahili, Kijerumani na Kikerewe. Lugha iliyojitokeza sana ni Kingereza zaidi ya Kijerumani na Kikerewe kama nilivyozionyesha katika jedwali.
Utanzu unaokabiliwa na changamoto na nyingi wakati wa kufasiri ni ushairi. Baadhi ya wataalamu kama vile Mwansoko na wenzake (2006; 43) wakimnukuu Newmark (1988) wanaeleza wazi kuwa ushairi ndio utanzu mgumu zaidi kufasiri katika fasihi. Sababu ya ugumu huu ni ushairi umebinafsishwa sana na una mshindilio mkubwa wa mawazo. Wanaeleza kuwa katika ushairi kizio cha kwanza cha maana ni neno kinachofuatia ni mstari. Mstari ni dhana yenye maana zaidi katika ushairi kuliko katika tanzu nyingine. Kwa maelezo haya tunaweza kueleza changamoto za ushairi ni kama vile ushairi umesheheni sitiari, tamathali za semi, umbo lenye mpangilio maalumu, sheria za mashairi ya kimapokeo kama vile vina, mizani na mishororo. Vipengele hivi ni vigumu hasa katika kuvitafutia visawe vyake. Ili kutatua tatizo hili lazima mfasiri azingatie vipengele vyote na awe na uweledi wa taaluma husika ya fasihi.
Katika uchambuzi kwa kutumia kitabu cha “Black hermit” kilichoandikwa na Ngugi wa Thiong’o (1968) na kutafsiriwa kama “Mtawa mweusi” na EAEP ltd (2008). Katika kutathmini ama tafsiri ni bora au ni mbovu Newmark (1988) anapendekeza mbinu au njia zinazotumika katika kutathmini. Mbinu hizo ni mbinu ya ulinganishi kati ya matini chanzi na matini lengwa, mbinu ya uasili, mbinu ya kupima uelewa, mbinu ya kupima usomaji, mbinu ya kupima ulinganifu na mbinu ya tathmini rejeshi. Katika makala hii nitatumia mbinu ya ulinganishi kata ya matini chanzi na matini lengwa. Katika kutumia mbinu hii nitazingatia vipengele vya; sarufi, muundo, upotoshaji wa maana kwa kuzingatia udondoshaji, uongezaji, ufafanuzi wa ziada pamoja na uteuzi mbaya wa visawe (msamiati). Tofauti hizi husababishwa na sababu za kiisimu, kiutamaduni, kihistoria na kimazingira. Tukianza na;
Sarufi; katika kipengele hiki tunazingatia suala la upatanisho wa kisarufi. Ni jukumu la mfasiri kuhakikisha kwamba anazingatia na kuhifadhi upatanisho wa kisarufi kati ya matini chanzi na lengwa. Lakini wakati mwingine kipengele hiki hakitekelezeki. Mfano wafasiri wa tamthiliya ya “Black Hermit” iliyotafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” hawajazingatia upatanisho wa kisarufi na kufanya matini ya tafsiri ipoteze ubora wake na hivyo kuwa mbovu.
Mfano: Matini chanzi: sorting out beans spread in a basin. (uk. 1)
Matini lengwa: akichagua
harage katika bakuli. (uk. 1)
Matini chanzi: if this be a curse put upon me (uk. 4)
Matin lengwa: kama hili ndilo laana nililopewa (uk. 4)
Matini chanzi: away from influence af tribal elders (uk. 43)
Matini lengwa: atengwe na maongozi ya wazee wa kabila (uk. 65)
Katika matini Kiingereza sentensi ipo sawa lakini mfasiri anapotosha upatanisho wa Kisarufi kwa kutumia “harage” badala ya “maharage”. Katika sentensi ya pili ya Kiingereza “if this be a curse put upon me” limetafsiriwa kama “kama hili ndilo laana nililopewa”badala ya “kama hii ndio laana” tungo hizi zimefanya kukosekana kwa upatanisho wa kisarufi katika matini lengwa na katika sentensi ya tatu neno “maongozi” linapaswa kuwa “uongozi”.
Muundo; huu ni mpangilio wa kazi husika ya fasihi. Katika tamthiliya ya “black hermit” mtunzi ametumia muundo sahihi wa tamthiliya kwa kufuata mkondo wa kiaristito naa majina ya wahisika yapo mwanzoni na kufuatwa na maelezo ya wahusika au vitendo. Lakini wafasiri wa “mtawa mweusi” wamekiuka kabisa muundo uliopo kwenye matini chanzi hivyo kusababisha tafsiri kuwa tenge. Wafasiri wametumia muundo wa filamu ambapo majina ya wahusika yanakaa katikati na kufuatwa na maelezo au vitendo.
Upotoshaji wa maana; jukumu lingine la mfasiri anatakiwa azingatie maana ile ile ya mwandishi. Lakini wakati mwingine wafasiri hawazingatii hili. Baadhi ya sababu zinazo sababisha upotoshaji wa maana katika tamthilia ya “black hermit” ni pamoja na;
Udondoshaji; hapa mfasiri huacha baadhi ya vipengele vilivyopo katika matini chanzi kwenye matini lengwa. Kwa mfano;
Matini chanzi; forced community work.
Matini lengwa; kazi za kulazimishwa.
Matini chanzi: This temptation harping on weak flesh (uk4)
Matini lengwa; Jaribu hili linalirudia rudia mwili wangu (uk.5)
Matini chanzi; ask me to ……… to …………., Oh, Oh. (uk. 33)
Matini lengwa; kaniambia ni …… ni……………. (uk. 49)
Katika mifano hii kuna baadhi ya maneno ya yaliyoachwa yaani hayajafasiriwa kama vile “community”, “weak”na “oh, oh”.
Uongeza; hapa katika kipengele hiki mfasiri anaweza kuongeza vionjo na madoido ambayo hayakwepo katika matini chanzi hadi kufikia kiwango cha kupotosha maana. Kwa mfano katika tafsiri (zao) “mtawa mweusi” mtafsiri ameongeza baadhi ya maneno; mfano;
Matini chanzi ; opens in a street corner (uk. 18)
Matini lengwa ; lilianzia mahali fulani mjini
(uk. 24)
Matni chanzi; can’t you se
Matini lengwa; wewe mwenyewe huoni
Matini chanzi; ooo my mother wept
Matini lengwa; ooo mama yangu aliangusha kilio
Matini chanzi; you insist? (Uk. 38)
Matini lengwa; anaendelea kushikilia uzi (uk. 56)
Uteuzi mbaya wa msamiati; Katika suala la hili yawezekana mfasiri akachagua maana isiyo sahihi kati ya maana nyingi zilizo katika lugha lengwa za neno katika lugha chanzi. Kwa mfano;
Matini chanzi: Matini
lengwa
… in a basin (uk.1) …katika bakuli
(uk.1)
…carrying (uk. 1) …akichukua (uk.1)
Do without husband siwezi kuishi
bila mwanaume
I have tasted the pains of beating nimeona maumivu ya mapigo.
Katika tafsiri ya Kiswahili neno la kiingeraza “basin” limefasiriwa kama “bakuli” badala ya “beseni”, neno “carrying” limetafsiriwa kama “akichukua” badala ya “akibeba”, neno “do” limetafsiwa kama “kuishi” badala ya “kufanya”, neno “tasted” limetafsiriwa kama “nimeona” badala ya “nimeonja” na kauli ya mwishi inatakiwa kuwa “kuliko hii”. Uteuzi wa msamiati katika matini legwa umepotosha maana iliyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Mchango wa tafsiri katika fasihi linganishi ni pamoja na huu ufuatao;
Tafsiri inatusaidia kulinganishi utamaduni wa jamii moja na nyingine. Mfano mzuri ambazo inatuelezea utamaduni wa kabila la Marua lililopo Kenya katika suala la desturi zao ambalo mume akifariki mke anarithiwa na kaka mtu au mdogo mtu. (uk.38). Mila na desturi hizi hapo awali katika jamii za waafrika hususani hapa nchini katika familia mke akifa alirithiwa. Lakini suala hili kwa sasa jamii imeliacha kwa kiasi Fulani kutokana na maendeleo ya elimu.
Tafsiri inatusaidia kulinganisha itikadi za jamii za Kiafrika. Kupitia kabila la Marua waafika walikuwa na mtazamo hasi wa kutochanganyikana na wala kutokuoana wala kuolewa na wazungu kutokana na wazungu kuwatawala kipindi cha ukoloni. Hali hii inadhibitishwa na maongezi ya Remi (uk. 52). Lakini kwa upande wa wazungu wao wanaitikadi chanya kwa waafrika. Wanaamini kuwa mapenzi hayajalishi rangi wala kabila bali watu kupendana. Haya yanathibitishwa na maongezi ya Jane. (uk.53). Baada ya uhuru waafrika wengi wakuwa na mitazamo hasi kwa wazungu kutokana na matendo ukoloni.
Tafsiri inatusadia kulinganisha historia ya jamii katika vipindi tofauti. Kwa mfano jamii ya Marua kipindi ukoloni matatizo yalivyokuwa tofauti na yale ya uhuru. Hivyo historia hii inatudhihirishia hata katika jamii zetu matatizo yaliyoletwa na ukoloni yalikuwa tofauti na yale ya uhuru.
Changamoto katika kufasiri zinajitokeza katika mambo yafuatayo;
Kwanza kutokuwa na ujuzi wa lugha na sarufi inayohusika. Ni jukumu la mfasiri kujua vizuri lugha anazozishughulikia kiundani zaidi ikiwa ni pamoja na sarufi sahihi, miundo, mitindo nakadhalika. Kama mfasiri hajui basi husababiasha upotofu wa tafsiri na umbovu.
Kutokuwa na taaluma ya uwanjwa maalumu. Wafasiri wengi wanafasiri pasipo kuangalia taaluma zao mahususi. Kwa mfano mtaalamu wa isimu anafasiri matini za kifasihi lazima kwa hali yoyote atasababisha utenge wa tafsiri.
Kutokuwa na vifaa vya kukuwezesha kutoa tafsiri nzuri na bora. Vifaa kama vile kamusi za matini mahususi katika taaluma mahususi husababisha ugumu wa kupata visawe husika.
Tafauti za kiutamaduni, itikadi, mazingira na historia husababisha changamoto kubwa katika tafsiri.
Pia tofauti za kiisimu na maendeleo ya sayansi na tekinolojia yanasababisha changamoto kubwa katika tafsiri mathilani sayansi na tekinolojia huleta istilahi ambazo ni vigumu kuzipatia istilahi zake.
Naweza kuhitimisha kwa kusema kuwa ingawa tafsiri ni nyenzo muhimu sana katika kukuza fasihi ya Kiswahili kuna baadhi ya upotoshaji wa ujumbe uliokusudiwa kutafsiriwa kutokana na mambo kadhaa kama vile itikadi ya mfasiri, historia, utamaduni na mazingira aliyopo mafasiri.
Marejeo
East African Educational Publishers Ltd (2008) Mtawa Mweusi. Kenya: Sitima Printers
Stationers Ltd.
Mulokozi, M. M (1996) Utangulizi
wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu
Huria.
Mwansoko, H.J.M. na wenzake
(2006) Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia
na Mbinu.
Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982) Approaches to Translation. Oxford:
Pergamon.
Newmark, P. (1988) A Textbook of
Translaton. London: Prentice Hall.
Ngugi wa Thing’o (1968) Black Hermit. Kampala-Uganda: East
African Educational
Publishers Stationers Ltd
Nida, A. E. na Charles, R.
T. (1969) The Theory and Practice of
Translation. Netherlands:
EJ. Brill.
Ruhumbika, G. (1978) “Tafsiri za Kigeni katika Ukuzaji wa Fasihi
ya Kiswahili” Makala
kwenye Semina za Kimataifa
ya Waandishi wa Kiswahili Dar es Salaam.