FANTASIA NA DHIMA YAKE KATIKA TENDI. Na Charles Timotheo.
FANTASIA NA DHIMA YAKE KATIKA TENDI.
Na Charles Timotheo.
Ikisiri
Fasihi simulizi na andishi kwa pamoja huchangia sifa moja ya kuwa sanaa ya lugha katika kufikisha ujumbe wake kwa jamii husika. Hii ndiyo ithibati ya sanaa yoyote kuwa fasihi. Kama uwasilishaji wa mawazo katika jamii utafanyika bila kutumia lugha kisanaa basi hapo hakuna fasihi. Katika kutumia lugha na mbinu nyingine za kisanaa katika kufikisha ujumbe kwa jamii, wakati mwingine kuna kuvuka mipaka ya uhalisia kwa kuhusisha wahusika na mambo ya kinjozinjozi au fantasia kwa makusudi. Mtindo huu wa kutumia fantasia katika kazi za kifasihi ni kinyume kabisa na wanataaluma wanao amini katika ukweli na uhalisia. Wafuasi wa nadharia ya uhalisia wanadai kuwa mwandishi au msanii wa kazi za fasihi anapaswa kuitoa picha ya jamii bila kuidunisha wala kuipigia chuku. (Wafula na njogu, 2007 wanaeleza hayo). Kwa kuwa fantasia inakimbia ukweli wa uhalisia katika kazi za fasihi je mbinu hiyo ina dhima gani kifasihi? Makala hii yatahusu dhima ya fantasia katika tendi.
Utangulizi
Wamitila (2003) anaeleza kuwa fantasia ni sawa na njozi, njozi ni dhana inayotumiwa kuelezea kazi ya fasihi ambayo ina sifa ambazo zinakiuka uhalisi.Anaendelea kufafanua kuwa ni kazi yenye sifa za kindotondoto au kutaka kuamilisha hali isiyo ya kawaida. Njozi hupatikana sana katika maandishi yanayolenga hadhira ya watoto.Sifa za kinjozi huweza kupatikana katika fasihi inayohusishwa na matapo mbalimbali ya kifasihi.Hutumiwa kueleza kazi za kinathari ambazo huwa na mandhari ya ajabu, matukio magumu kukubalika katika hali ya kawaida na hata wahusika wasioweza kupatikana katika uhalisi. Kutokana na fasili hiyo ya Wamitila tunaweza kusema kuwa wahusika katika kazi zenye fantasia ni wahusika kama vile mazimwi,mashetani ,majini na vitu vingine ambavyo havidhaniwi kuwepo katika jamii, yaani haviwezi kupatikana katika uhalisia .Fantasia nyingi huwa na motifu za zafari, au msako wa utafutaji au ufumbuzi wa kitu falani. Fantasia pi inatumika katika kazi nyingine za kifasihi kama vile riwaya, tamthiliya na hadithi fupi. Kwa mfano riwaya ya marimba ya majaliwa ya E. MBOGO.
Matumizi ya fantasia katika tendi ni suala la kawaida katika tendi. Matumizi ya fantasia yanapojitokeza katika fasihi, huleta upya ambao unakuwa haujazoeleka na hivyo kuwashutua wahakiki wa fasihi. Mshtuko huu ndio uliozaa istlahi ya uhalisiamazingaombwe kama inavyotumiwa zaidi na Senkoro (2006). Dhana hii inatumika kuzieleza zile kazi za kifasihi zinazounganisha uhalisi na uajabuajabu.
Makala haya yatahusu dhima ya matumizi ya fantasia katika tendi. Hili linatokana na ujitokezaji wa mara kwa mara wa sifa hii katika kazi nyingi za tendi hali ambayo inakiuka uhalisia unaoamini kuwa fasihi ni kioo cha jamii. Fasihi kama kioo cha jamii inapaswa kuakisi kile kinachotokea bila kukipotosha kwa kuingiza mambo yasiyo halisi. Kwa kuwa mbinu hii ya kifani inajitokeza katika kazi nyingi za tendi hasa zile za visasili, makala haya yatatumia kisasili kimoja cha kidini kutoka katika maandiko matakatifu yaani Biblia katika Agano la kale katika kitabu cha Waamuzi. Kisasili hicho ni Kisasili cha Samson. Kwa kuwa makala haya ni ya kitendi basi tuangalie kwa ufupi maana ya tendi kama inavyofasiliwa na wataalamu mbalimbali.
Maana ya tendi
Wataalamu mbalimbali wameelezea dhana ya utendi, miongoni mwao ni Wamitila (2003), anaeleza utendi ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja. Kimsingi utendi huwa na sifa nyingi na huweza kuleta pamoja hadithi ya kishujaa, mugani, visasili, historia pamoja na ndoto za taifa Fulani. Wamitila anaendelea kusema kwamba kuna aina mbili za tendi ambazo ni tendi zinazohusisha fasihi simulizi na tendi zafasihi andishi. Pia anasema tendi ni tungo ndefu ambazo huimbwa na mafundi fulani na huwahusu mashujaa, walioishi katika jamii fulani. Nyimbo hizi zinagusia maisha ya mashujaa hao, kuzaliwa kwao, kuishi kwao, shida zao, vita, matendo yao ya kishujaa na vifo vyao.
Mulokozi (1996), anaeleza kuwa utendi (epic) ni utanzu mashuhuri sana katika kundi la ghani-masimulizi. Utendi ni ushairi wa matendo ni tungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio huweza kuwa ya kihistoria na visakale/ visasili.
Kutokana na maelezo hayo, Wamitila na Mulokozi wanaelekea kufanana katika kufafanua dhana ya tendi, wote wanazungumzia juu ya ushairi mrefu unaoelezea matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii na wanaeleza kuwa tendi huweza kuwa historia au visasili. Hivyo kutokana na maelezo hayo tunaona kuwa tunaweza kupata tendi katika umbo la visasili ambapo huwa na matukio yamhusuyo shujaa yaani maisha yake kwa ujumla na matendo ya kishujaa anayoyafanya, kisasili cha Samsoni kinakidhi sifa hii hivyo inadhihirisha kuwa ni tendi ingawa matini, maudhui yake na vipengele vyake vimeegemea katika umbo la kisasili
Sifa za tendi (epic)
Tunaweza kuainisha sifa za tendi kwa kifupi kama ifuatavyo;
Tendi zina dhima mbalimbali. Dhima hizi zaweza kuwa za kutunza historia, kutunza lugha, kuelimisha, dhima za kijamii na hata kuburudisha. Wakati mwingine tendi huwa na dhima ya kuhamasisha na kutambulisha jamii. Mulokozi anakubaliana na tendi kuwa na kazi nyingi na msingi wa tendi kuwa na kazi hizo unatofautiana kati ya jamii na jamii.
Sifa ya urefu, ama kuhusu suala la urefu ni suala linalobadilikabadilika. Hivyo kile kinachoitwa kirefu katika tendi sio ile hadithi au simulizi la utendi bali ule urefu wa utendaji, hii ni kwa mujibu wa Mulokozi 1996.
Sifa zinazohusu maudhui, katika sifa hii kuna maudhui yanayohusu shujaa, matatizo, maisha yake, au masuala jamii anamoishi shujaa husika.
Muhtasari wa kisasili teule na fantsia inavyojitokeza
Kisasili cha Samsoni
Hiki ni kisasili kinachotoka katika Biblia, Agano la kale kitabu cha Waamuzi sura ya 13-16. Kisa kilieleza kuzaliwa kwa shujaa Samsoni hadi kufa kwake. Kisasili kilianza kwa kueleza jinsi Manoa ambaye alikuwa akiishi na mkewe aliyekuwa tasa yaani alikuwa hana uwezo wa kuzaa mtoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke na kumweleza kuwa atachukua mimba naya atazaa mtoto mwanamume hivyo alikatazwa asitumie vileo wala divai kwani huyo mtoto atakuwa mnadhiri wa Mungu pia alikatazwa asimnyoe nywele hata siku moja. Basi mwanamke alimweleza mumewe na baadaye Manoa alimwomba Mungu amwelekeze namna ya kumlea huyo mtoto. Kisa kinaendelea kutueleza juu ya yule malaika kwani alitokea tena na kuwaelekeza cha kufanya na mwishowe mtoto mwanamume alizaliwa na kupewa jina la Samsoni.
Mtoto akakua na Bwana akam’barikia Samsoni. Muda wa kuoa ulipowadia Samsoni alienda kuoa mwanamake wa Timna mojawapo wa binti wakifilisti na wakati huo Israeli walikuwa wanatawaliwa na Wafilisti. Wakati Samsoni alipokuwa anaenda Timna alikutana na simba lakini alimuua kwa mikono yake mwenyewe kwa kumpasua kama mwanambuzi. Basi kisasili hiki kinaendelea kutueleza mambo yaliyokuwa ya ajabu ajabu yenye nguvu za ziada kama vile kuwaua wanaume thelathini na kuzitwaa nyara zao ili kuwapa wale ambao walitegua kitendawili chake. Aliweza kuwakamata mbweha mia tatu na kuwafunga wawili wawili vienge kisha kuwasha moto na kuwaachia na waliweza kuteketeza mashamba ya ngano na mizeituni ya Wafilisti.
Kisa hiki pia kinaeleza anguko la shujaa huyu aliyeweza kunaswa na Delila mwanamke kahaba wakifilisti aliyeweza kumshawishi amjulishe siri ya nguvu zake na baada ya upelelezi mwingi shujaa huyu alijikuta akimweleza kuwa tangu kuzaliwa wembe hukupita kichwani mwake na ndipo Delila alipomnyoa nywele zake zote na Wafilisti waliweza kumkamata nakumng’oa macho yake mawili.
Siku ya kifo chake ilikuwa ni sherehe ya Wafilisti ya kumshukuru mungu wao Dagoni kwa kuwawezesha kumkamata adui yao Samsoni hivyo walimleta mbele ya wakuu na viongozi mbalimbali pamoja na watu wengi sana. Hapo Samsoni nywele zake zilishaanza kuota hivyo alishikilia nguzo mbili zilizokuwa zimeshikilia jengo lile nakuanza kuzisukuma na jengo lile lilianguka akafa na watu wengi kuliko aliowahi kuwaua enzi za uhai wake. Mwisho mwandishi anaeleza kuwa Samsoni alikuwa mwamuzi wa taifa la Israeli kwa muda wa miaka 20.
Fantansia zilivyojitokeza katika tendi.
Katika kisasili hiki kuna mambo kadhaaa yanaelezwa ambayo katika ulimwengu hayawezi kutokea bila uwezo wa nguvu za ziada. Zifuatazo ni fantasia zilizojitokeza katika Kisasili cha Samsoni.
Kwanza fantasia ya kwanza ipo katika hali ya kuzaliwa kwa Samsoni au kutabiriwa kuzaliwa kwake. Katika simulizi hii mama yake Samsoni alikuwa Tasa yaani hawezi yaani asiyeweza kuzaa lakini wakati huo huo malaika anamtokea mama yule na kumueleza kuwa atachukua mimba na kumzaa mtoto wa kiume (Amu 13:3-5) “Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akauwambia, Tazama wewe u tasa huzai; lakini utachukua mimba...”
Pili, kitendo cha Samsoni kutonyolewa tangu kuzaliwa kwake ambalo ni agizo alilopewa mama yake na malaika wa bwana, jambo ambalo si la kawaida katika ulimwengu wa kawaida kwani si rahisi kumkuta mtu ambaye hakuwahi kunyolewa tangu kuzaliwa kwake hadi kuwa mtu mzima kabisa kama Samsoni (Amu 13:5) “Kwani tazama utachukua mimba nawe utamzaa mtoto mwanamume na wembe usipite juu ya kichwa chake....”
Pia kitendo cha malaika kumtokea mke wa Manoa. Mwanamke huyu alitokewa na malaika mara kadhaa kuelezwa kuhusu kuzaliwa na mambo yanayompasa kuyafanya kipindi cha ujauzito wa Samsoni. Hili pia ni jambo ambalo si la kawaida labda linaweza kutokea kwa kufikirika tu, kwa imani na si kwa kulithibititisha hasa kisayansi. Katika (Amu 13:2) “Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke....:”
Fantasia nyingine ni Samsoni kumuua simba kama mbuzi. Hili ni jambo ambalo si la kawaida sana kwani mwandishi ameeleza hili pale Samsoni na wazazi wake walipokuwa wakielekea Timna kwenda kuoa. Samsoni alingurumiwa na simba katika mashamba ya mizabibu na yeye alimpasua kana kwamba anampasua mbuzi na wala hakuwa na kitu chochote mkono mwake. Hili limeoneshwa katika (Amu 14:6) “Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana mbuzi wala hakuwa na kitu chochote mkononi...”
Kitendo cha Samsoni kuwapiga wanaume thelathini. Baada ya kitendawili cha Samsoni kuteguliwa ilimpasa awalipe wale vijana waliotegua kitendawili chake, hivyo ilim’bidi awapige wanaume thelathini huko Ashkeloni ili achukue nyara na kwenda kulipa. Hili limeoneshwa katika (Amu 14:19) “Roho wa Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkelani akapiga watu waume thelathini katika watu hao na kuzitwa nyara zao na kuwapa hao.....”
Tukio ligine lisilo la kawaida ni Samsoni kuwakamata mbweha mia tatu na kuwafunga vienge katika mikia yao. Hili Samsoni alilifanya baada ya kwenda kwa mke wake na kukuta ameozwa kwa mtu mwingine hivyo aliona hakuna kinachomfanya kumzuia kuwadhuru wafilisti kwani tayari alikuwa ameshanyang’anywa mke. Samsoni aliwakamata mbweha mia tatu na kuwafunga vienge vya moto katika mikia yao na kisha kuvitia moto na kuwaachia wakimbilie katika mashamba ya ngano na kutekeleza matita na ngano na mashamba ya mizeituni hili limeoneshwa (Amu 15:4-5).
Pia Samsoni kuwaua watu elfu wa mfupa wa taya la punda. Watu wa Yuda walimfunga Samsoni kamba ili kumtia mikononi mwa wafilisti, Samsoni alikubali na walipofika kwa wafilisti Samsoni alizikata zile kamba mbili mpya alizofungwa nazo kama kitani iliyoteketezwa kwa moto na hapo ndipo alipochukua mfupa mbichi wa taya ya panda, akawapiga watu elfu kwa mfupa huo (Amu 15:14-15).
Samsoni kuzikata kamba saba mbichi alizofungwa nazo. Delila alikuwa akimpeleleza Samson kuhusu asili ya Nguvu zake hivyo Samsoni akamwambia wakinifunga kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado hapo ndipo nitakuwa dhaifu. Basi Delila akaletewa kamba mbichi saba na kumfunga nazo Samsoni mwandishi anasema Samsoni alizikata kama vile uzi wa pamba ukatavyo ukiguswa na moto. Katika (AMU 16:9) “Na yule mwanamke... Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatavyo ukiguswa na moto, basi hiyo asili ya Nguvu zake haukujulikana.”
Fantasia nyingine ni Kuangusha Nyumba kubwa kwa kushikilia nguzo mbili kubwa zilizokuwa katika nyumba ile. Hili lilikuwa ni jambo la mwisho Samsoni kulifanya katika uhai wake kabla ya kifo chake ambacho ndio lilikuwa anguko lake. Baada ya Wafilisti kumtesa sana nywele zake zilianza kuota na alipoitwa kwenda kucheza alizishika nguzo za ile nyumba iliyokuwa na watu wengi waume kwa wake, wakuu wote wa Wajilisti na kuiangusha kitu kilichosababisha kifo chake na cha wote waliokuwamo ndani.
Hivyo basi tunaweza kusema kwamba mambo hayo hapo juu yanaweza kutokea katika ulimwengu wa kufikirika tu, katika ulimwengu wa kiuhalisia hayapo na wala hayawezi kuthibitishwa kisayansi.
Dhima ya Fantansia katika Tendi
Baada ya kuangalia muhtasari wa kisasili cha Samsoni pamoja na fantansia inavyojitokeza basi tuangalie sababu za kuwepo kwa fantasia hizo. Kwa kuwa mambo hayo ya kindotondoto si halisi je yaepukwe? Tunapojibu swali hilo ndio tunapata sababu za waandishi kutumia fantasia na mchango wa mbinu hiyo kifasihi. Dhima kuu za fantasia katika tendi ni pamoja na;Kumwibua na kumwonyesho kwa uwazi mhusika Shujaa.Hii ni mojawapo ya dhima kuu ya matumizi ya fantansia katika tendi. Mara nyingi mhusika shujaa wa kitendi ni lazima awe na ruwaza fulani ya maisha ambayo kwa asilimia kubwa au karibia maisha yake yote yanajawa na mambo ya kinjozinjozi au kindotondoto. Wataalamu wengine husema anatumia nguvu za sihiri. Mara nyingi mhusika shujaa wa kitendi kuzaliwa kwake huwa ni kwa ajabuajabu na pengine hukataliwa na jamii yake. Lakini kukua kwake na mambo anayoyapitia huwa ni ya ajabuajabu na hiyo ndiyo fantansia yenyewe. Mfano katika kisasili cha Samsoni. Samsoni anazaliwa na mama tasa aliyetokewa na malaika lakini katika kukua kwake Samsoni hakuwahi kunyolewa nywele na zaidi alifanya mambo ya ajabuajabu. Mfano katika katika aya 14:6.Kujenga msuko wa matukio katika Tendi.Mohamed (1995) anauita msuko huu ni Ploti. Anaifafanua ploti kuwa ni msukumo wa hadithi katika mpangilio fulani. Anazidi kufafanua kuwa msukumo huu hujengwa na wahusika wanaotenda na kutendana na kuathiriana kusababisha matukio, mwendo na kasi ya kwenda kiwakati na pahala. Ufafanuzi huu unafanana na ule wa Wamitila (2011) unaodai kuwa msuko ni mpangilio wa matukio katika kazi ya kifashi.Hivyo basi dhima mojawapo ya kutumia fantansia katika tendi ni hiyo ya kuibua matukio ili kufanikisha msuko. Katika kisa cha Samsoni kuzaliwa kwake kule kwa ajabuajabu na kutokunyolewa kwake nywele kumesaidia kusukuma mbele na kufanikisha usimulizi wa kisasili hiki. Mwandishi anaeleza kuwa Samsoni alizaliwa na mwanamke tasa ambaye alitokewa na malaika wa bwana na pia sio tu kuzaliwa bali anaeleza kuwa hakuwahi kunyolewa mpaka Delila alipoamua kumpeleleza na kujua siri hiyo na kumnyoa jambo lililosababisha kuishiwa nguvu. Kuwepo kwa nguvu za Ajabu za Samsoni iliwezesha simulizi nzima kunoga na kuzua taharuki nyingi katika sura mbalimbali. Aidha kisasili hiki matukio yake yote kwa kiasi kikubwa yamefanikishwa kwa fantansia mbalimbali hasa ya nguvu za ajabu za Samsoni.Kujenga Taharuki kwa wasomaji au wasikilizaji.Madumulla (2009) anamueleza msanii mzuri kuwa ni yule anayepanga kazi yake kiasi kwamba tukio moja linasababisha lingine na kusababisha kujenga hamu msomaji ya kutaka kujua kulikoni, nini kitatokea hii ndiyo huitwa taharuki. Matumizi ya fantasia katika tendi inasaidia sana kujenga taharuki na hii humfanya msomaji atake kujua zaidi kujua nini kinaendelea katika simulizi baada ya tukio fulani. Mfano katika kisasili cha Samsoni Delila anampeleleza Samsoni kuhusu asili ya nguvu zake basi Samsoni anamueleza mara ya kwanza kitu kinachomfanya msomaji anakuwa na hamu ya kujua ni nini kitatokea baada ya kutoa siri na hivyo hivyo kwa mara ya pili na tatu na hata mara ya mwisho alipotoa siri yake lazima mtu ajiulize hivi itakuwaje je atakufa? Hivyo fantansia husaidia msomaji kupata hamu ya kuendelea kujua kitakachotokea na kufanya kazi ivutie zaidi.Kuibua dhamira mbalimbali kwani kila fantasia ina maudhui fulani.Dhamira huweza kuibuliwa kwa kupitia fantansia mbalimbali zinazojitokeza katika tendi. Masuala kadhaa huibuliwa kupitia mambo ya kiajabuajabu yanayojitokeza. Katika kisasili hiki cha Samsoni dhamira nyingi zimeibuliwa katika matumizi ya fantansia, mfano siri ya Samsoni kuwa na nguvu nyingi inaweza kuwa na dhamira mbalimbali kama vile, kujua kutunza siri, kwani Samsoni alimwambia Delila siri yake na hivyo kusababisha kuanguka kwake, pia dhamira ya kuwa msaada kwa taifa lako, kupambana na adui na pia kuacha uonevu kwa wengine kama ambavyo Wafilisti walivyokuwa wanawapiga na kuwatawala waisraeli.Lakini pia agizo alilotoa malaika kwa wazazi wa Samsoni la kutokumnyoa nywele nalo pia huibua dhamira ya kuwa tunapaswa kuwa watiifu tunapopewa maagizo na wakubwa zetu kwani wazazi wa Samsoni hawakumnyoa na walitii maagizo yote.Mgogoro husaidia sana kumvutia msomaji kutaka kujua ni nini hatima ya mgogoro fulani kitu ambacho huipa uzito kazi ya fasihi, na matumizi ya fantansia kwa ujumla yanasaidia sana katika ujenzi wa migogoro ya kiusimulizi.Kutimiza matamanio ya BinadamuKupitia matumizi ya fantansia, mambo yote hata yale yasiyowezekana kwa binadamu huwezekana, hii ni kutokana na kuwa binadamu ana uwezo wa kufanya mambo mengi sana katika ulimwengu wa kihalisia, kwa upande mwingine, yapo mambo mengine ambayo binadamu hutamani kufanya lakini hana uwezo nayo. Mambo yale yanayobanwa na mikatale ya kijamii huwezekana kuyasema kupitia kazi za kifasihi kupitia fantansia.Sigmund Frend katika nadharia yake ya Saiko-changanuzi anaifananisha kazi ya fasihi na ndoto, anasema kazi za fasihi ni kazi za ubunifu, kazi hizi ni sawa na ndoto tu ya mtunzi. Hata wahusika wanaopatikana ni wanadamu wanaoishi katika ndoto na njozi za mwandishi (Wafula na Njogu, 2007).Hivyo matumizi ya fantansia huonesha matamanio ya mtunzi mfano katika kisa cha Samsoni. Suala la Wafilisti kuwatawala Waisraeli mwandishi alikuwa anatamani kulipinga kupitia mambo mbalimbali ya kiajabuajabu, pia kufanya mambo makubwa na yanayohitaji nguvu kwa urahisi mfano. Kumuua simba kirahisi jambo ambalo kwa kawaida ni gumu lakini pia kuangusha nyumba kubwa kwa urahisi nyumba iliyokuwa imara na yenye nguzo mbili. Hivyo kwa kutumia fantansia mtunzi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza matamanio yake.Kwa kuhitimisha tunaweza kusema makala hii inasisitiza kuwa fantasia ni mbinu muhimu katika kazi za kitendi kwani huwa na mchango/dhima nyingi katika kazi hizi ambayo kwa kiasi kikubwa husaidia kukidhi sifa za kazi fulani kuwa tendi na fasihi kwa ujumla. Kutokana na uwepo wa fantasia nyingi katika kazi mbalimbali za fasihi bado waandishi na wahakiki wanapaswa kufanya utafiti zaidi juu ya umuhimu wa fantasia katika kazi za fasihi.MarejeoMadummulla, J. S (2009). Riwaya ya Kiswahili; Nadharia, Historia, na Misingi ya Uchambuzi.Dar es Salaam: Mture Educational Publishers Limited.Mohamed, S. A (1995), Kunga za Nathari ya Kiswahili; Riwaya, Tamthilia na Hadithi Fupi,Nairobi; English Press Limited.Mulokozi, M. M (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili,Dar es Salaam; Chuo kikuu Huria.Njogu, K na R. M. Wafula (2007), Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo KenyataFoundation.Senkoro, F.E.M.K (2006) Fasihi. Dar es salaam: KauttuThe Bible Societies of Kenya and Tanzania (1997) Biblia; Maandiko Matakatifu. Kenya naTanzania.Wamitila. K.W (2003), Kamusi ya fasihi; Istilahi na Nadharia. Nairobi. Focus publication Ltd.Wamitila K. W. (2011) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi English press.