MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI) USULI WA LUGHA YA KISWAHILI
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI)
USULI WA LUGHA YA KISWAHILI
Kabla ya kuingia kwa undani kuangalia lugha hii ya Kiswahili baada ya uhuru. Tunaweza kutalii dhana ya lugha na usuli wa lugha ya Kiswahili.
Dhana ya lugha
Wanaisimu wamekuwa wakitazama dhana ya lugha kwa mitazamo mbalimbali.
Mitazamo hiyo huweza kutoa taswira ya maana ya lugha inavyo weza kuwa.
Lado (1964) Lugha ni chombo cha mawasilianoa baina ya binadamu katika jumuia Fulani.
Potter (1960) Lugha ni utaratibu wa alama za sauti
zilizopangiliwa kutokana na mazoea au matamshi ya watu kwa njia ya sauti
ambazo wanadamu wanapelekeana habari na wanasikilizana
TUKI (2004) Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno
unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili
ya kuwasiliana.
Kutokana na mitazamo hiyo lugha ya weza kufasiliwa kuwa
ni sauti za nasibu za binadamu zinazobeba maana na zilizokubaliwa na
jamii ya watu ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku.
LUGHA YA KISWAHILI
Kama zilivyo lugha nyingine za kitaifa na kimataifa,
Lugha ya kiswahili ina tabia ya kusemwa, kuzungumzwa na kuandikwa kwa
nia ya kukamilisha mawasiliano miongoni mwa wanajamii wa kiswahili.
Lugha ya kiswahili ni lugha rasmi na Lugha ya Taifa kwa upande wa
Tanzania ingawa kwa Watanzania ni lugha ya Pili. Lugha ya kiswahili ina
watumiaji wanaokadiliwa kuwa ni zaidi ya milioni 37 kwa Tanzania.
Kiswahili kinafundishwa katika shule za msingi, sekondari na vyuoni.
Hivi sasa kiswahili kimeteuliwa na kupewa baraka zote kuwa lugha ya
Umoja wa Afrika na Kiswahilli kina hadhi ya nafasi ya sita kimataifa
kikitanguliwa na na Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiarabu, na
Kireno. Pia inakadiriwa kuwa Kiswahili kina wazungumzaji zaidi ya
Milioni 160 Duniani. Kuna vituo mbalimbali vya redio na luninga
vinayotangaza kwa kiswahili Ndani na nje ya bara la Afrika kama vile
Sauti ya Amerika, BBC London, Sauti ya uajemi, KBC, na vingine vingi.Pia
kuna vyuo vingi duniani vinavyofundisha lugha ya kiswahili mfano katika
bara la Afrika, Asia, Ulaya, na Marekani. Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo
Kikuu cha Minesota, Vyuo vikuu mbalimbali duniani mfano Ujerumani,
Uingereza kwa kutaja baadhi.
HISTORIA YA LUGHA YA KISWAHILI
Kuna nadharia mbalimbali zinazoeleza historia ya lugha
ya kiswahili, mfano wa nadharia hizo ni nadharia ya kihistoria, na
nadharia ya kiisimu
Katika nadharia ya kihistoria inaeleza historia ya
kiswahili kwa ujumla. Mfano historia ya Kilwa, ushahidi wa marco Polo na
Ushairi wa Fumoliyongo unaosemekana ni ushairi wa Kiswahili ulioandikwa
karne ya kumi na tatu BK. Nadharia ya kiisimu inaeleza taratibu na
kanuni za lugha. Mfano upatanisho wa kisarufi, maumbo ya maneno (umoja
na wingi), muundo wa tungo (kiima na kiarifu) mnyumbuliko wa maneno
(kitenzi) na tabia ya vitenzi vya lugha ya kiswahili.. Hivyo lugha ya
kiswahili inaweza kutazamwa kwa mtazamo ya kiisimu na kihistoria katika
kupata historia ya lugha ya kiswahili kwa usahihi wake. Pamoja na kuwa
wananadharia hawa hutofautiana, huweza kukubaliana kwa kutojua au kwa
kujua kuwa kiswahili kimetokana na Kibantu.
Kutokana na shahidi mbalimbali Mfano
Shihabuddin Chiraghdin na Mathias Mnyapala (1988) wanaeleza kuwa asili
ya lugha ya kiswahili ni kibantu ambacho kinazungumzwa zaidi katika upwa
wa Afrika Mashariki mfano Pate, Unguja, Lamu, Comoro, Pemba, Mombasa,
Kilwa, Tanga kwa kutaja baadhi. Wageni walikuja hususani Waarabu
walikuta lugha hii ya kiswahili ikiwa inazungumzwa na wenyeji wao wa
mwambao wa upwa wa Afrika mashariki kwa Lahaja tofauti tofauti kulingana
na maeneo mfano kimakunduchi, kimtang`ata (Pangani na Tanga), Kingozi,
(Pate na Kisumayu) Kitumbatu, Kimrima(Dar es salaamu na Tanga) Kimvita
(Mombasa) Chimiini (Mogadishu/ Somalia) kwa kutaja baadhi. Lugha hizi
zinafanana. kutokana na kufanana huko walipokuja Waarabu wakaziita lugha
zote zilizokuwa zikizungumzwa upwa wa mashariki mwa Afrika ni Sahil.
Kutoka na sababu kadha wa kadha na athari za matamshi ikatokea swahili
na baadaye ikapatikana lugha ya kiswahili
Katika ujio wa waingereza ndipo shughuli za usanifishaji
zilipoanza. Katika shughuli za usanifishaji shughuli mbalimbali
zilifuatwa ikiwa ni pamoja na uteuzi wa lahaja moja miongoni mwa lahaja
nyingi zilizokuwepo. Lahaja ya kiunguja ikateuliwa na kufanyiwa mchakato
wa usanifishaji. Ndipo tukapata kiswahili sanifu. mfano wa maneno
yaliyosanifiwa ni kama :-
Kiunguja Kiswahili sanifu
Cai Chai
Cumba Chumba
Ceza Cheza. Kwa kutaja baadhi
KISWAHILI BAADA YA UHURU
Baada ya uhuru kuna harakati mbalimbali zilizochukuliwa
na serikali ya Tanzania katika kukiendeleza na kukikuza kiswahili.
Harakati hizo ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi 1962.
1964 kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na
kuwa kitatumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa mfano
katika elimu hususani elimu ya msingi.
Kundwa kwa Chombo cha usanifishaji ambacho kilikuwa na
kazi ya kuhimiza maendeleo ya kiswahili, kutayaricha kamusi na vitabu
mbalimbali vya sarufi na fasihi ya lugha ya kiswahili na kuandaa
wataalamu watakaoshughulikia usanifishaji wa kiswahili
Pia baada ya uhuru kulianzishwa Taasisi mbalimbali
zitakazoshughulikia lugha ya kiswahili. Mfano:- BAKITA, TUKI, TUMI,
UKUTA, UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha Dar es salaamu.
Baada ya uhuru nchini Tanzania kiswahili kilienea kwa
kasi kubwa sana. Kuna sababu mbalimbali ambazo zilichangia kukua na
kuenea kwa kiswahili hapa nchini. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na
kuteuliwa kwa kiswahili kuwa lugha ya Taifa, Kiswahili kitumike katika
Elimu, mfano kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi. kuundwa
kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na kuneza kiswahili, Kiswahili kuwa
Lugha rasmi na lugha ya Taifa, shughuli mbalimbali za kidini, shughuli
za kisiasa na kiutawala na shughuli za kiutamaduni na uchapishaji wa
vitabu na majarida mbalimbali.
1. KISWAHILI KUWA LUGHA YA TAIFA
Baada ya uhuru mwaka 1962 kamati iliundwa ili kuangalia
uwezekano wa kutumia kiswahili katika shughulizote rasmi, mfano bungeni
na shughuli zote za kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha ya
taifa 1964 ambapo katika shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa
kutumia lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili kilihimizwa kutumika katika
mawasiliano yote hususani katika mawasiliano yote hasa katika shughuli
za umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili kiliendelea kupanda
hadhi zaidi wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani azimio hilo
lilitungwa na kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
2. KUUNDWA KWA VYOMBO VYA UKUZAJI NA UENEZAJI WA KISWAHILI
Tanzania baada ya uhuru ilifanya jitihada za kuunda
vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza kiswahili katika nyanja
mbalimbali mfano wa vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA TUMI TUKI Taasisi ya
Elimu,TAKILUKI na Chama cha Kiswahili Chuo Kikuu Dar es salaam.
3. KUTUMIKA KATIKA ELIMU
Kiswahili licha ya kutumika katika shughuli mbalimbali
za kiserikali, kilipendekezwa kutumika katika shule za Msingi na
kufundishwa katika elimu ya sekondari kama somo na katika vyuo vikuu
wanatoa shahada mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia katika Elimu ya
watu wazima ambao hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza
masomo mbalimbali kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua
kusoma, kuandika na kuzungumza lugha ya kiswahili fasaha. Kampeni hii
ilikuwa kwa nchi nzima ambapo walijifunza elimu ya Afya, Siasa,
Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu
wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
4. VYOMBO VYA HABARI
Tangu uhuru ulipopatikana kuna vyombo mbalimbali vya
habari vilivyoanzishwa. Vyombo hivi hutumika kueneza kiswahili kwa kiasi
kikubwa na hufikiwa na watu wengi licha ya kuwepo kwa changamoto za
kiuchumi. Vyombo hivyo ni magazeti na majarida mbalimbali ambayo
huandikwa kwa lugha ya kiswahili lakini kuna redio na runinga ambazo
matangazo yake hutangazwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kukifanya
kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.
5. BIASHARA
Shughuli za kibiashara nchini husaidia kuenea na kukua
kwa kiswahili kutokana na kuwepo kwa makabila tofauti tofauti ambapo
wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo
kiswahili hudumishwa na kutumika katika biashara hizo.
6. SHUGHULI ZA SIASA NA UTAWALA
Tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kiswahili
kimetumika kama nyenzo muhimu kuwaunganisha wananchi. Shughuli nzima za
kisiasa zimetumia lugha hii katika kujiimarisha; mfano wakati wa chama
kimoja, Azimio la Arusha na Mfumo wa vyama vingi Kiswahili kimetumika
kama njia kuu ya mawasiliano. Pia katika utawala chama kinachotawala
kimekuwa na harakati za kukiendeleza kiswahilli katika nyanja zote.
Ambapo kiswahili kimekuwa kikitumika katika shughuli zote za kiutawala.
Hivyo shughuli za kisiasa na kiutawala zimechangia kwa kiasi kikubwa
katika kukuza, kukieneza na kukiendeleza kiswahili.
7. UANDISHI NA UCHAPISHAJI WA VITABU
Kuibuka kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili
vya sarufi na fasihi ambavyo vilichambua kwa kina mambo mabalimbali
yahusuyo lugha ya kiswahili na utamaduni wake, mfano :- F Nkwera,
Shabani Robart, Mathias Mnyapala na Shaffi Adam Shaffi. Waandishi
wengine chipukizi walijitokeza na wanaendelea kujitokeza katika tasnia
hii ya uandishi wa vitabu.
8. SHUGHULI ZA KIUTAMADUNI
Shughuli za kiutamaduni zimechangia kueneza
kukuza na kuendeleza lugha ya kiswahili. Shughuli hizo ni pamoja na
harusi, misiba, matanga na sherehe mbalimbali za kijamii ambazo
zimesaidia kukiendeleza kiswahili kwa kuwa huwakutanisha watu
tofautitofauti katika shughuli hizo, ambapo huwalazimu kutumia lugha ya
kiswahili katika mawasiliano na kufanya kiswahili kuendelea. Pia katika
Sherehe mbalimbali vikundi vya sanaa na muziki vinavyotumia lugha ya
kiswahili kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa nyimbo zao kwa ajili ya
kukieneza kiswahili Mfano;-( ) Pia katika sherehe mbalimbali za
kiserikali na kisiasa hususani vyama mbalimbali vya kisiasa mfano bendi
ya TOT inayoongozwa na kepteni Komba .
MAFANIKIO YA KISWAHILI WAKATI WA UHURU MPAKA SASA
Kiswahili kimeweza kujizolea na kinendelea
kujizolea sifa kemkem ndani ya Miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu hatuna
budi kukitolea mifano ili tuone kwa namna moja au nyingine jinsi
kilivyofanikisha kuwaunganisha Watanzania katika mapambano dhidi ya
utawala wa kikoloni na kusababisha matokeo hasi kwao ambapo kubwa zaidi
ni kujipatia uhuru. Kwa maana nyingine, Kiswahili kiadhimishwe kama
lugha ya ukombozi wa nchi yetu wa mwaka 1961.Mpaka sasa kiswahili kimefanikiwa kuwaunganisha watanzania wote na kwa maneno yake yaliyojaa faraja na matumaini, kimeweza kudumisha amani ya Tanzania (nchi yetu) kwa miaka hamsini sasa. Bado kinaendelea kuwaweka pamoja watanzania na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Pia kimetoa mchango mkubwa katika kuipa sifa kubwa nchi yetu ya Tanzania na kuwa mfano wa kuigwa duniani kote. Tanzania imepewa sifa ya kisiwa cha amani kutokana na amani ya muda mrefu iliyopo nchini ambayo inasimamiwa vilivyo na lugha yetu ya kiswahili.
Katika nyanja ya fasihi, Kiswahili kimeweza kuelezea
utamaduni wa nchi nyingine kama vile Kongo Afrika kusini, Uganda n.k .
Kwa kutumia muziki kwani sasa kuna wanamziki wengi wanaotoka katika nchi
hizo wanaotambulisha utamaduni wao kwa lugha ya kiswahili. Baadhi yao
ni Mbili Abel Kutoka kongo, Ivon Chakachaka kutoka Afrika Kusini,
Marehemu Miriam Maakeba Kutoka Afrika Kusini pamoja na Jose Kamilion
kutoka nchini Uganda. Pia kuna baadhi ya wanamziki kutoka Korea waliweza
kuonesha hisia zao kwa kutumia lugha ya kiswahili katika uimbaji wao.
Lugha ya kiswahili ina utajiri wa maneno (msamiati)
ambao katika lugha nyingi za kimataifa hazina msamiati huo kama
Kiingereza hakina msamiati wa aina hiyo, Mfano wa misamiati hiyo ni
pamoja na Shangazi, Baba mdogo, Baba mkubwa, Ugali nk. Kutokana na
tafiti zilizofanywa kiswahil kinaonekana kuwa ndiyo lugha pekee kwa sasa
ambayo inakubarika kwa kasi zaidi duniani kote kuliko lugha nyingine
zinazokua. Hii ni kutokana na ongezeko la watu wanaohitaji kujifunza na
kuzungumza kiswahili duniani kote.
Pia kiswahili kimeweza kufikia kiwango cha juu sana cha
kusikika kwani sasa kinasikika dunia nzima. Hii ni kutokana na mashirika
makubwa ya habari yanayorusha matangazo kwa kutumia lugha ya kiswahili.
Mfano BBC, Sauti ya Ujerumani. (Deutsche Welle ) Sauti ya Amerika,
Pamoja na shirika la utangazaji la Tanzania TBC kupitia kituo cha
runinga kinachorusha matangazo yake kupitia kituo cha DSTV kilichopo
nchini Uingereza, kinachorusha matangazo kwa njia ya setilaiti.
Mafanikio mengine ya kiswahili ni kufanikiwa katika
sayansi mbalimbali katika jamii ambapo kiswahili kimetumika kuandika
vitabu mbalimbali kwa kutungwa au kufasiriwa na wataalamu mbalimbali.
mfano kitabu kinachohusu afya ya binadamu kilichotafsiriwa ambacho hata
sasa hutumika katika kufundishia wataalamu wa afya katika vyuo vikuu.
kitabu hiki kimefasiliwa na Daktari(....)
Pia Watanzania wanaoishi katika nchi za dunia ya kwanza wameonyesha nia ya dhati ya kuwasaidia vijana wakitanzania kutambua thamani kubwa ya lugha yao ya Kiswahili. Kwa mfano, Freddy Macha, Mtanzania aishiye Uingereza kwa kushirikiana na watanzania wengine waliopo barani Ulaya. Wamedhamiria kwa dhati kulifanikisha hilo kwa vitendo, ambapo hivi karibuni wanatarajia kufanya semina na vijana wa Tanzania hapahapa nyumbani. Kwa kushirikiana na Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania (MMVT) na vijana wengine na kujadili mada mbalimbali ikiwamo mada ya Kiswahili inayohusu umuhimu wa kujua lugha mbalimbali kikiwamo Kiswahili na namna ya kukitumia kama nyenzo ya maendeleo na biashara.
Pia Watanzania wanaoishi katika nchi za dunia ya kwanza wameonyesha nia ya dhati ya kuwasaidia vijana wakitanzania kutambua thamani kubwa ya lugha yao ya Kiswahili. Kwa mfano, Freddy Macha, Mtanzania aishiye Uingereza kwa kushirikiana na watanzania wengine waliopo barani Ulaya. Wamedhamiria kwa dhati kulifanikisha hilo kwa vitendo, ambapo hivi karibuni wanatarajia kufanya semina na vijana wa Tanzania hapahapa nyumbani. Kwa kushirikiana na Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania (MMVT) na vijana wengine na kujadili mada mbalimbali ikiwamo mada ya Kiswahili inayohusu umuhimu wa kujua lugha mbalimbali kikiwamo Kiswahili na namna ya kukitumia kama nyenzo ya maendeleo na biashara.
Nao Watanzania waliopo Denmark wamepongeza juhudi
zinazofanywa na wadau wa Kiswahili nyumbani (Tanzania) kwa namna moja
au nyingine katika kukikuza na kukieneza Kiswahili na wanakubaliana na
misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere na
Abeid Amani Karume katika kuitumia lugha ya Kiswahili kama kitambulisho
cha taifa, ambapo Kiswahili kinatumika kama lugha ya taifa.
Pia wanawapongeza viongozi waliofuata kwa kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nyanja ya muhimu za elimu, uchumi na utamaduni wa taifa letu la Tanzania
Pia wanawapongeza viongozi waliofuata kwa kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nyanja ya muhimu za elimu, uchumi na utamaduni wa taifa letu la Tanzania
Pia, watanzania na wadau wote wa lugha ya
Kiswahili wanampongeza Rais mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan
Mwinyi na Rais wa awamu ya tatu Mh.Benjamini Willium Mkapa wamekuwa
Viongozi hodari wa kukisimamia na kukieneza Kiswahili. Hawakuwa nyuma
kumpongeza Raisi Kikwete kwa kuhakikisha Watanzania wanafahamu
umuhimu wa lugha ya kiswahili nchini na duniani kote yeye alitia
msisitizo kwa kuhutubia mkutano wa Umoja wa Afrika kwa Kiswahili .
Kituo cha runinga cha TBC 1 nacho kwa nafasi na mchango
wake katika lugha, kimekuwa kikirusha kipindi cha Lulu za Kiswahili
pamoja na kipindi cha Ulimwengu wa Kiswahili na kujadili masuala ya
lugha ya Kiswahili nchini na nje ya nchi. Pia vituo vingine vya runinga ni kama star TV na ITV Ambayo havipo nyuma katika kukieneza na kutangaza Kiswahili.
Vilevile, kuingizwa Kiswahili katika mtandao ni hatua kubwa inayoonyesha kwamba, Kiswahili kinaendana na hali ya utandawazi ambapo watu wamekuwa wakipata taarifa ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Na kufanya watu wengi hususani wanaojua Kiswahili kusoma makala mbalimbali katika matandao na kupata habari kwa kina.
Kuwapo kwa kamusi za lugha katika tovuti ambazo huwezesha watu kujifunza lugha kupitia njia ya mtandao.
Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Skuli ya Sanaa na Lugha
pamoja na kuongezeka kwa vyuo vinavyofundisha shahada ya lugha ya
Kiswahili nchini kama vile vyuo vikuu vya SAUT, Chuo Kikuu cha Kiislamu
Morogoro, Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar (Suza), Tumaini na pia Chuo
Kikuu Dar es Salaam (UDSM) hatua hiyo imesababisha kuwa na wasomi wengi
wenye taaluma ya Kiswahili, licha ya changamoto ya wanafunzi hao wa
Kiswahili kuwa na upungufu wa maeneo ya kufanya mafunzo ya vitendo, ni
changamoto inayopaswa kuangaliwa na kufanyiwa kazi.
Kuongezeka kwa istilahi za lugha ya Kiswahili ni jambo linaloashiria
kupanuka kwa matumizi ya Kiswahili na ndiyo maana kumekuwapo na
machapisho ya kamusi mpya mara kwa mara ili kukidhi mahitaji na matumizi
ya lugha ya kila siku katika mawasiliano . Istilahi hizo zinaongezeka
kutokana na sababu mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi
lakini pia maendeleo ya sayansi na teknolojia Mfano wa istilahi hizo ni
kama zifuatazo;-
Chakachua, ngangali, ng`atuka, ngamizi.
Vilevile, kuingia katika mfumo wa mawasiliano kwa njia ya setelaiti (digitali) kumehamasisha zaidi matumizi ya Kiswahili hasa katika tasnia ya utangazaji hususani redio na runinga, mfano TBC na ATN. Hivyo hufanya mawasiliano kuwa rahisi miongoni mwa wasikilizaji wao.
Vilevile, kuingia katika mfumo wa mawasiliano kwa njia ya setelaiti (digitali) kumehamasisha zaidi matumizi ya Kiswahili hasa katika tasnia ya utangazaji hususani redio na runinga, mfano TBC na ATN. Hivyo hufanya mawasiliano kuwa rahisi miongoni mwa wasikilizaji wao.
Mafanikio menginie ni kuongezeka kwa watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ulaya, Amerika, Asia na kwingineko kuja Tanzania kujifunza Kiswahili. Pia kufanya tafiti kuhusiana na lugha ya Kiswahili
Kuongezeka kwa nchi nyingi dunia zinazotumia lugha Kiswahili katika
mawasiliano na kuhitaji wataalamu wa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya
watu wao kujifunza Kiswahili mfano Botswana, Libya, Malawi na Afrika Kusini.
Kiswahili kimekuwa kama sehemu ya ajira katika taasisi na mashirika mbalimbali ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali. Mfano
katika tafsiri na ukalimani, pia katika kutoa Elimu Kiswahili
kinatumika. Hii inawafanya watumiaji wa lugha hii kuongezeka kwa kasi
kubwa.
Kuwepo kwa machapisho mengi ya Kiswahili na kuwepo kwa
waandishi wengi wanaoandika kazi mbalimbali za Kiswahili mfano katika
fasihi na sarufi ya Kiswahili.
Mfano wa waandishi maarufu walio kama chachu ya
maendeleo ya Kiswahili ni F. Kezilahabi, F. Nkwera, J.
Madumulla, I. Huseni, T.Sengo, Kingo, Chachage, Penina Mlama, S. Shaffi
na Asha Kunemah. Ambao wametoa changamoto kubwa katika kukikuza na
kukiensza Kiswahili. Pia wameonesha mafanikio makubwa katika kazi zao.
Kiswahili kimekuwa maarufu sana na kukubarika katika
nchi za Afrika Mashariki. Mfano nchini Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya,
mathalani nchini Kenya Kiswahili kimekuwa lugha ya Taifa. Kuandikwa kwa
katiba ya Kenya kwa lugha ya Kiswahili na kuwa lugha ya Taifa katika
nchi za Afrika Mashariki. Hivyo kukifanya kiswahili kuwa na hadhi kubwa
ndani na nje ya bara la Afrika
KISWAHILI NA UTANDAWAZI
Utandawazi ni dhana pana ambayo imeenea na kugusa nyanja
mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Kiswahili ikiwa ni sehemu ya utamaduni kimeguswa na kuathiriwa na
utandawazi.
Dhana ya utandawazi inaweza kuangaliwa kwa mitazamo
mbalimbali. Miongoni mwa dhana hizo ni aina ya tabaka jipya la kibepari
lililojitutumua kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi, kisiasa, na
kiutamaduni. Kujiinua huku hudhihirika katika taaluma na vyombo vya
habari mfano matangazo na kufanya kuwa dhana inayoenea kwa kasi na
kugusa nyanja mbalimbali duniani. Hivyo utandawazi unaweza kuifanya
dunia kuwa kama kijiji . Utandawazi una muonekano wa mradi wa kiitikadi
na ajenda ya kujenga mahusiano ya kibinadamu na ambayo ni ngumu
kueleweka kwa wanazuoni mbalimbali na kuonekana kuwa ni dhana mpya.
UTANDAWAZI KATIKA UTAMADUNI
Utandawazi huendana na mambo mbalimbali kama vile Lugha,
Sanaa, Mavazi, na namna ya kula na hivyo jamii kuathirika kwa sehemu
kubwa. Jamii huweza kuathirika kwa kupoteza amali za jamii kwa kupokea
mambo ya jamii nyingine hususani mambo ya kimagharibi. Hivyo kiswahili
kama sehemu ya utamaduni wa Taifa letu imeathirwa kwa sehemu kubwa.
KISWAHILI NA UTANDAWAZI.
Utandawazi ulianza kuingia katika lugha ya kiswahili
wakati wa utawala wa kikoloni. Ambao ulisababisha mabadiliko mbalimbali
katika lugha ya kiswahili. mfano Dini, biashara, utawala na elimu
vilisaidia kukuza na kueneza lugha ya kiswahili. Utawala wa kikoloni
uliambatana na kuanzishwa kwa vyombo vya habari kama vile magazeti,
redio. Runinga, tovuti na simu ambapo kuliimarisha utandawazi na
kiswahili kupata matumizi makubwa.
Kutokana na utandawazi kumekuwa na ushindani mkubwa
katika mambo mengi ikiwemo Lugha. Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa
lugha zilizo kwenye ushindani huo. Lugha hii inakubalika na watu wengi
wanaoitumia katika mawasiliano, na kukifanya kiswahili kuingia katika
utandawazi kwa lengo la kuiunganisha jamii.
Katika utandawazi ajira inaongezeka, Mathalani mtu
anayetumia lugha nyingine nje ya kiswahili anakuja nchini kwa lengo la
uwekezaji hulazimika kujifunza kiswahili ili kudumisha mahusiano na
wenyeji wake. Hivyo huongeza walimu wa lugha kwa ajili ya kufundisha
lugha ya kiswahili pia huweza kueneza lugha kwa njia ya ukalimani.
Watanzania wengi huchukuliwa na nchi mbalimbali kwa lengo la kufundisha lugha ya kiswahili katika nchi zao.
Utandawazi huweza kusaidia kuongeza msamiati wa lugha.
Kiswahili ni miongoni mwa lugha inayopokea maneno kutokana na matumizi
yake yanayotokana na utandawazi hususani katika maendeleo ya sayansi na
teknolojia, siasa, utamaduni na uchumi. Mfano katika maendeleo ya
sayansi na teknolojia, kuna istilahi nyingi za kimtandao.
Utandawazi umeweza kuongeza idadi ya watumiaji wa lugha
ya kiswahili. Ambapo ikadiliwa kuwa katika nchi za maziwa makuu idadi ya
watumiaji wa lugha kiswahili ni zaidi ya milioni 60.
MADHARA YA UTANDAWAZI
Kila kitu kina pande mbili, kadharika utandawazi nao una
pande mbili faida na hasara. Baada ya kuangalia upande mmoja wa
shilingi uzuri wa utandawazi katika kiswahili. Sasa tuangalie madhara ya
utandawazi katika lugha ya kiswahili
Mosi kutokana na utandawazi kumekuwa na kudharau lugha
ya kiswahili. ambapo lugha hii ya kiswahili inaonekana kuwa ni lugha ya
watu wa tabaka la wasionacho. Pia Watu huiona lugha ya kiswahili kuwa ni
lugha ya watu wasiojua kitu chochote duniani. Kiswahili kinaonekana
kuwa si lugha ya sayansi na teknolojia na kwamba haiwezi kutumika katika
shughuli zote za kisayansi hususani katika taaluma ya ufundi.
CHANGAMOTO KATIKA LUGHA YA KISWAHILI
Pamoja na hadhi na umaarufu wa kiswahili, bado lugha hii
inakumbana na matatizo makubwa ya dhana na matumizi ya lugha ya
kiswahili.
Katika dhana ya kiswahili bado kuna baadhi ya watu
wanaonasibisha kiswahili na dini ya kiislam hili limekuwa ni tatizo
kubwa miongoni mwa watumiaji wa lugha hii.
Pia upinzani mkubwa kutoka katika lugha ambazo
zimekwisha jitanua katika dunia Mfano:- Kiingereza, Kifaransa, Kireno na
Kiarabu. Watumiaji au watu wenye asili na lugha hizo wanakipiga vita
kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitazimeza lugha zao.
Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo
kwa lugha za kigeni kwamba ndio pekee zinazofaa kutumika katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi. Hivyo kiswahili kuonekana kuwa hakifai kutumiwa
katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kasumba mbaya na mtazamo hasi wa Watanzania katika lugha
ya Kiswahili ambao unawafanya watanzania kukitukuza zaidi kiingereza na
kutojua kuwa kiingereza ni sawa na lugha nyingine tu.
Kucheleweshwa kwa maamuzi ya sera ya kukipa hadhi
kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika nyanja zote za elimu, na
kiingereza kuwa somo tu. Hivyo inarudisha nyuma maendeleo ya kiswahili.
Watanzania kuwa nyuma katika kufanya tafiti mbalimbali
juu ya lugha ya kiswahili ili kuona ni jinsi gani tunaweza kufunguka
kiakili na kufahamu umuhimu wa kuwa na lugha ya kiswahili
Uchumi mdogo wa nchi yetu unakwamisha kwa sehemu kubwa
maendeleo ya haraka ya lugha ya kiswahili duniani. Kwa kuwa nchi
inashindwa kuzalisha wataalamu wengi wa lugha hii, pia inashindwa
kufasiri maandiko kutoka lugha nyingine kuwa katika lugha ya kiswahili
kwa sababu ni ghari mno.
Watanzania wanakosa moyo wa kuthamini na kujali tamaduni
zao ambapo kiswahili ni lugha inayotangaza utamaduni wao lakini wao
wanathamini sana utamaduni wa kimagharibi. Kwa hakika hii ni changamoto
kubwa ambayo inakikumba kiswahili katika harakati zake za kujitanua
duniani kote.
Pia kuna dhana kuwa Kiswahil ni lugha ya watu duni
kitaaluma mathalani watu walioishia darasa la saba. Hivyo hufanya watu
kutaka kujifunza Kiingereza. Hii ni dhana ya watu potofu kabisa ambayo
inajitokeza kwa watu ambao ni wasomi kabisa.
Kwa upande wa matumizi ya lugha ya Kiswahili, kumekuwa
na matatizo makubwa ya kutumiwa isivyosahihi na matumizi yasiyofasaha
katika nyanja zake za kimatamshi, kimaandishi na kimaana. Matatizo hayo
ndiyo yanayopelekea kutokuwa na kiswahili sahihi na fasaha. Jambo la
kusikitisha na kushtua zaidi ni kuwa kwa muda mrefu, kumebaini na kuwa
na kiswahili sanifu nchini lakini kiswahili hiki kinazungumzwa na
kuandikwa kimakosa mno. Makosa haya hutendwa na taasisi mbalimbali
zikiongozwa na vyombo vya mawasiliano. Mfano katika magazeti waandishi
wanatumia lugha inayokiuka misingi na kanuni za kiswahili sanifu
tunachokielewa au wanachofundishwa wanafunzi.
MAKOSA YANAYOFANYWA NA UMMA WA WATANZANIA
Makala hii inadokeza na kubainisha makosa ya matumizi ya
kiswahili yanayofanywa na umma wa Watanzania, Vyombo vya mawasiliano na
Walimu katika shule na vyuo. Pia inaeleza sababu za msingi na athari na
matumizi yasiyosahihi kwa jamii ya watumiaji wa Kiswahili hususani
Watanzania wote. Baadaye kutakuwa na mapendekezo ya nini kifanyike ili
kupunguza au kuondoa kabisa matatizo hayo ya makosa ya matumizi
yasiyosahihi ya lugha hii kwa vyombo vyote vya umma na watu binafsi
watumiaji wa kiswahili.
Kabla ya kuangalia makosa ya matumizi yasiyosahihi ya
Kiswahili sanifu ni afadhali kwanza kudokeza maana ya umma wa
Watanzania, maana ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya Kiswahili na maana ya
mawasiliano sahihi na fasaha.
MAANA YA UMMA WA WATANZANIA
Umma wa Watanzania kwa muktadha wa makala hii ni watu
wengi wenye kutumia stadi ya kusema na kuandika kwa lugha ya kiswahili.
Kwa upande wa kusema au kuzungumza makosa hayo hutokea katika shughuli
zisizo rasmi na zile zisizorasmi katika mazingira tofautitofauti ya
mawasiliano ya kila siku, kama vile mitaani, nyumbani, ofisini, shuleni
na kazini. Kwa upande wa uandishi makosa hayo hutokea katika vitabu,
magazeti, majarida na vipeperushi vya matangazo mbalimbali.
MAANA YA MAKOSA YAMATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU
Maana ya makosa ya matumizi ya kiswahili sanifu kwa
upana wake ni yale matumizi ya kiswahili ama ya kuzungumzwa au kuandikwa
ambayo yanakiuka taratibu na makubaliano ya kimawasiliano ya kisarufi
ambayo ni sahihi na fasaha na kusababisha karaha au upotofu wa
mawasiliano rasmi kwa wazawa na wajuzi wa kiswahili fasaha.
MAAN A YA MAWASILIANO SAHIHI NA FASAHA
Mawasiliano sahihi na fasaha ni yale mawasiliano ya kuitumia lugha ya
yenye kufuata taratibu za maneno, miundo ya kisarufi pamoja na maana na
kuweza kukubalika na wazawa na wajuzi wa lugha hiyo. Ikiwa inasemwa au
kimaandishi, bila kuwa na uvulivuli, ukakasi au chukivu kwa wasikilizaji
au wasomaji. Kigezo kikubwa cha lugha sahihi na fasaha ni ile lugha ya
mazungumzo au maandishi ambayo ikisemwa au ikiandikwa haitagunwa na
wazawa au wajuzi mahiri wa lugha ile. Mfano wa lugha ya Kiswahili
isiyosahihi na isiyofasaha ni kama mtu akisema au kuandika hivi
“Tuende wote pale tulikuwa juzi”
Sentensi hii ina makosa ya taratibu za kisarufi, katika upatanisho wa
vipashio na muundo unaokubalika kwa wajuzi wa lugha hii na kuleta
ukakasi na uvurivuri na kusababisha kukosa ufasaha. Sentensi hii
ilitakiwa kusemwa au kuandikwa hivi “Twende sote pale tulipokuwapo jana”
Hivyo ni uandishi na usemaji wa lugha ya kiswhili ni dhahiri kuwa huwa
na taratibu wa kisarufi, muundo na upatanishi wa vipashio unafuatwa na
unapelekea sentensi hiyo kuwa na mawasiliano sahihi na fasaha mbele ya
wajuziz wa lugha
MAKOSA YA KISWAHILI YANAYOFANYWA NA UMMA WA WATANZANIA
Makosa hayo ya kimatumizi yanabainika kutawala katika maeneo ya
matamshi, maumbo, miundo na maana; ama kimazungumzo au kimaandishi.
Makosa makuu ya mawasiliano ya umma yanabainika katika nyanja
zifuatazoa;-
1 Matamshi
na maandishi mfano thamani badala ya zamani, arubaini badala ya
arobaini, samanini badala ya themanini. sambi badala ya Dhambi na sahabu
badala ya dhahabu. Wngine pia hushindwa kutofautisha kati ya kula na
kura hii inatokana na watu hawa kuwa wamawameathiliwa na lugha mama.
Hivyo hata wakati wa kujifunza au kufunza lugha hufunza kwa makosa hayo.
2 Maumbo ya maneno ambayo kwa sehemu kubwa huendana na maana za maneno.
mfano:- Zoezi (kazi), zoezi (jaribio)
3 Miundo
ya sentensi, miundo mingi ya sentensi zinazotolewa huwa si sahihi na
huleta ukengeushi mkubwa kwa wajuzi wa lugha mfano:- hadi hapo
nawaageni, nachukua nafasi hii, kwa niaba yangu. Pia katoka muundo wa
sentensi za Kiswahili huanza na nomino na kufuatwa na aina nyingine za
maneno Mfano:- Mtoto mzuri anacheza jikon
N V T E
Tena katika muundo kuna makosa ya upatanishi wa
kisarufi ambapo watu wanapotosha au kuchanganya sarufi ya lugha ya
Kiswahili.
Mfano:- sisi wote tunapenda nyama badala ya kusema Sisi sote tunapenda nyama.
4 Machapisho
na majarida mbalimbali ambayo kwa sehemu kubwa hutumia lugha
inayopotosha jamii, mfano:- pia vyombo mbalimbali vya habari kama
Televisheni, Redio, Runinga. ambayo hutumia lugha hii visivyo na pengine
hupotosha kabisa umma au jamii. mfano wa matumizi ya neno Chakachua
ambapo mtu akakifanya vibaya wanasema amechakachua.
5 Pia
katika elimu kumekuwa na mkanganyiko mkubwa ambao unatoka na sera
zisizo na msingi. Pia matatizo ya kimtaala ambayo huleta changamoto
kubwa inayotokana na muhutasari wa elimu na mitihani inayotolewa. Katika
muhutasari huonesha wanafunzi kujifunza kwa mlengo wa kimawasiliano
unaopigia chapuo wanafunzi kupewa stadi za kuwasiliana zaidi huku
ikilenga katika masuala mengine hususani upade wa sarufi.
6 Pia kuna makosa ya kimsamiati ambapo watu huchanganya sana
hususani wakati wa kuzungumza hutumia msaniati usiolingana na maana
iliyokusudiwa, pengine hutokana na kushindwa kutofautisha maneno hayo.
Mfano: nenepa na nona, wasilisha na wakilisha, ajali na ajili, na
mazingira na mazingara. Mfano:- Siku hizi Rachel amenona, badala ya Siku
hizi Rachel amenenepa.
Haya ni baadhi ya makosa ya matumizi yasiyokuwa sahihi yanayofanywa na
umma wa watanzania. Uzoefu unaonesha kuwa kati ya umma wa watanzania
watu wa vyombo vya mawasiliano na habari vya umma huchukua nafasi kubwa
ya kufanya makosa ya Kiswahili sanifu watu hao ni waandishi wa habari,
wahariri wa magazeti na watangazaji wa redio runinga. kwa kubainisha
vyombo hivi vichache ni kama
vifuatavyo: Magazeti Mtannzania, Mwananchi , uwazi, Nipashe, Uhuru
Mzalendo Mwanahalisi na habari leo. Kwa upande wa Redia ni TBC Taifa,
Radio one, Sauti ya Zanzibar,
Redio uhuru nk Pia runinga ni TBC, ITV, Star TV, TVZ, ATA, EATV na DTV.
Kinacho jitokeza hapa ni kuwa makosa yanayofanywa na watu hawa husambaa
sana na kuchukua asilimia kubwa takribani pande zote za Tanzania
na duniani kote tena kwa haraka zaidi. Matarajio ya wengi ni kuwa umma
wa watanzania kuwa na uchungu wa lugha hii adhimu ya Kiswahili na kuwa
mstari wa mbele katika kusimamia na kuthibiti uenezi wa Kiswahili sahihi
na fasaha. lakini hali haiku hivyo, bali iko kinyume na matarajio
TAATHIRA ZA UMMA WA WATANZANIA KUTANYA MAKOSA KATIKA KISWAHILI SANIFU
Kuna taathira nyingi ambazo zinasababisha mawasiliano ya umma wa watanzania kuwa na matumizi yasiyosahihi kama yalivyoonekana hapo awali. Taathira za msingi hasa ni kama zifuatazo
TAATHIRAYA KUTOELEWA LUGHA YA KISWAHILI NA UTAMADUNI WAKE
Kiswahili ikiwa ni lugha kamili yaa mawasiliano ina kanuni zake za
kisarufi na kiutamaduni. Kwa mfano kanuni za kisarufi katika kitenzi
ambacho husimama kuwa sentensi basi lazima kiwe na kiambishi cha
utendaji, kiambishi cha wakati na shina la kitendo chenyewe. Yaani kama
kitenzi atakuja. Kwa upande wa utamaduni mbele ya wenyewe waswahili mtu
hawezi kusema au kuandika kwa mfano:- Kama nilivyosema hapo mbeleni. kwani nene mbeleni ni matusi kwa mswahili mzawa.
Kinachoonekana kwa watanzania ni kutokuwa waledi na mahiri wa sarufi na
utamaduni wa lugha ya Kiswahili. Kwa watu waliowageni wa lugha hii ya
Kiswahili hususani katika sarufi ya Kiswahili wanafanya makosa makubwa
na kuleta matatizo makubwa. Kwakuwa katika mawasiliano, kwao kufanya
makosa sio tatizo ikiwa mazungumzo au maandishi yao yanaeleweka. Mhina anasema Kiswahili ni lugha ya watu wa unguja kwa hiyo tunapata Kiswahili safi kutoka kwa watu wa jamii ya waunguja.
TAATHIRA YA KUKIDHARAU KISWAHILI KUWA HAKINA MWENYEWE
Taathira nyingine inayopelekea Kiswahili kuzungumzwana kuandikwa
kimakosa na vyombo vya habari ambayo inasikitisha zaidi ni kuwa kila
mmoja ana uhuru wa kuzungumza kukizungumza na kukiandika anavyoona au
atakavyo. Hali hii ndiyo inayofanya wengine kusema kuwa Kiswahili hakina
mwenyewe. hii ni dharau kubwa na kejeli ya hali ya juu kwa wazawa na
wajuzi wa lugha hususani kwa wanazuoni.
Hii inadhihilisha ule usemi usemao anayekutukana hakuchagulii tusi,
umechukua mkondo wake. Kwani haijapata kusikika wa haitarajiwi kusikika
kuwa Kingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kihaya, Kisukuma, Kibena na Kihehe
kuwa lugha hizi hazina mwenyewe. Kwa hakika lugha kama
haina mwenyewe basi haipo. Ikiwa lugha ya mazungumzo au maandishi
lazima lugha hiyo iwe na wenyewe ambao ni binadamu tu. Wala si lugha ya
wanyama, wala si lugha ya miti wala si lugha ya majabali na wala si
lugha ya anga ombwe. Hivyo ni muhimu kuunga mkono mawazo ya Mnyapala na
Shiragddin wanaposema “… kiswahi kama zilivyo lugha nyingine hakina
budi kukua na …” mawazo haya ni ya kweli kwa yameandikwa na na wageni
wa lugha nautamaduni wa Kiswahili ndio walioanza na matumizi ya yasiyo
sahihi na yasiyofasaha. kinachobainika katika maandishi hayo ni kuwa wao
ni wataalamu zaidi kuliko wale waswahili wenyewe katika kuandika vitabu
vyao. ukweli usiopingika kuwa mawazo ya mazungumzo au maandishi yenye
makosa yaliyotendeka na yanayoendelea kutendeka hayakubalikia na
hayatakubalika kamwe na baadhi ya waswahili , kwani Kiswahili kina
wenyewe. Amabao hawaoni kuwa lugha kama
kifaransa au kiingereza ni bora au ni tajiri kuliko Kiswahili. Pia hawa
hawaha wala hawatakuwa na dhana kuwa sarufi au lughawiya ya Kiswahili
lazima ifuate lughawiya ya lughaya kiingereza au lugha nyingine. Msimamo
huu pia unaoneshwa tena na Mnyapala na Shiraghdin “kulazimisha lugha
ya Kiswahili katika sarufi ya kiingereza ni kama
kupika mchanyato wa ndizi mbivu… matokeo yake utakuwa si mchanyato bali
ni bokoboko la ndizi. Kwa sababu sarufi ya kizungu ni kitu mbali na
sarufi ambayo isingefaa katika Kiswahili kwa namana nyingine.”
TAATHIRA YA WIGO NA KUTOJIAMINI KWA BAADHI YA WANAHABARI
Baadhi ya wanahabari hususani watangazaji wa redio runinga waandishi na
wahariri wana mtindo wa kuiga kwa kutojiamini. hali hii hujitokeza pale
wanahabari wanapowaiga ama wanahabari wenzao ambao nao wanafanya makosa
katika kazi zao. Wanahabari hao huwaiga wanasiasa au viongozi wa nchi
japokuwa kile kilichosemwa au kuandikwa ni makosa kabisa hapo ndipo
utakapowasikia wakisema:- Chakachua kusimikwa kwa watu kumi na watano,
katoto kale kanaingia sasa. nk. Wanahabari hutumia maneno hayo kwa kuiga
bila kujiani. ikitokea nafasi ya kuuliza mbona unatumia maneno hayo?
utasikia jawabu atakalo kupa kuwa “mbona watu wengi wanalitumia neon hilo na limekwishaenea. Hoja ya msingi hapa si suala la neon kutumiwa na watu wengi au kuenea, bali ni kuwa neno hilo matumizi yasiyokuwa sahihi na halikubaki katika jamii ya wanazuoni wa Kiswahili.
TAATHIRA YA LUGHA ZA VIJANA KUKIINGILIA KISWAHILI SANIFU
Kiswahili mara nyingine hupata Taathira ya lugha za vijana na baadhi ya
watu kuanza kuhusudu na kuyatumia maneno ambayo hayana asili ya
Kiswahili na utamaduni wake. mfano Kama neno mambo? kwa maana ya uhali gain? na jawabu lake ni poa yaani sijambo au haliyangu ni njema. Pia kuna neno jingine linalouliza Vipi? na jawabu lake ni Fresho au hamna noma. lakini kuna maneno mengine kama
vile Matingo, kughairisha, magharibi na kujiongeza. Kwa hakika lugha
hizi si sahihi wala si fasaha kwa kutumiwa na watu wote katika shughuli
zilizo rasmi. Lakini la kushangaza ni kuwa utawasikia baadhi ya viongozi
wanahabari, wazee na walimu ambao tunawategemea wawemstari wa mbele
kukilinda na kukienzi Kiswahili wanatumia lugha hizi zinazotumiwa na
vijana. Lakini ilivyo lugha hizi kwa vijana zina sehemu zake maalumu kwa
vijana wenyewe tu si kwa watu wenye kustahiwa kama hao waliotajwa hapo juu.
TAATHIRA YA KUCHANGANYA KISWAHILI NA KIINGEREZA (ATHARI ZA UMAGHARIBI, WINGI LUGHA)
Kuchanganya mazungumzo ya lugha ya Kiswahili na lugha ya kiingereza ni
suala lililotawala mno katika mawasiliano ya umma na katika vyombo vya
habari. Mara nyingi utawasikia watu wakichanganya Kiswahili na
kiingereza. Hii ni kutaka kuhakikisha kuwa wanakifahamu kiingereza na
kujitukuza mbele yaw engine. Mfano:-
Ok ndugu wasikilizaji sasa tunaendelea na mchezo wa drama.
well nimekusikia ndugu mtazamaji kwa mchango wako lakini kwa upande mwingine perhaps watu wana mtazamo mwingine juu ya issue hiyo.
Uchanganyaji wa Kiswahili na kiingereza kama
huo umewatawala watu wengi wakati wanapozungumza Kiswahili na
kukichanganya na lugha hii ya kigeni. wakiti mwingine baadhi ya watu
hufikia hatua ya kusema sijui nitumie neno gain hapa la Kiswahili ili
ajihalalishie kuchanganya Kiswahili na kiingereza.
TAATHIRA YA KUTOLINGANA KWA TAALUMA YA FONOLOJIA NA OTHOGRAFIA
Mara nyingi wasomi wa lughawia za kiingereza wanatengua baadhi ya
matamshi na maandishi ya Kiswahili kwa kuathiliwa na lugha ya iingereza
ambacho nacho kimeathiliwa na taaluma ya kifaransa. hali hii husababisha
matamshi ya sikuwa sahihi na yasiyokuwa fasaha katika Kiswahili ambacho
kina utaratibu wa lugha za kiafrika kuandikwa kama kinavyotamkwa. mfano
maneno kama;- themanini, tofauti,
arobaini na dhoruba. Maneno kama haya hutamkwa vingine na kuandikwa
vingine. ukihoji utajibiwa kuwa ndivyo yalivyokubalika kuandikwa
kisanifu na pia baadhi ya maneno huandikwa kinyume na yanavyotamkwa
yaani hapa ni kuiga kiingereza lakini hakuna hoja kwani tukiyaandika
kama yanavyotamkwa kama maneno mengine
kuna ukakasi gain? Na wenyewe waswahili ndivyo wanavyotamka? Kwa hoja
hizi ni wazi kuwa kuna matumizi yasiyosahihi ya matamshi ya maneno haya.
La kusikitisha zaidi katika makosa hayo yamoo katika maandishi yote
yaliyomo vitabuni, magazetini na katika majarida. Kwa ujumla sababu hizo
kama zilivyofafanuliwa hapo katika matumizi yasiyo sahihi ya Kiswahili sanifu. Sababu hizi ni kama
sababu zilizofafanuliwa na Pamela Ligami na wenzake wakisema “ kuna
sababu mbalimbali zinazochangia matatizo katika lugha ya Kiswahili.
Miongoni mwao na athari za lugha ya kwanza: makosa ya kimatamshi,
mazingira, sarufi, matatizo ya kijamii na namna ya ufundishaji”
TAATHIRA YA KUDHARAULIWA KWA LUGHA YA KISWAHILI
Taathira nyingine ya msingi ni iayopelekea lughaya Kiswahili
kudharauliwa na ama wageni au hata wale wenyeji hasa vijana ambao hawana
uchungu wa asili wa lugha yao
na utamaduni wao na vilivyo vyao. Hali hii huwasononesha wataalamu
wengi hususani wenye uchungu na lugha hii na wakereketwa wa Kiswahili na
ambao wanaithamini lugha yao
na kujivunia katika Afrika mashariki. Wakereketwa au watu wenye uchungu
na lugha yao wanapoona au kusikia matumizi yasiyokuwa sahihi ya lugha
yao tukufu huwa na majonzi na masikitiko na ndipo baadhi yao huchukua
hatua ya kukemea ama kwa kusema au kwa kuandika kama inavyokemea
kimaandishi makala hii
MAKOSA MBALIMBALI YANAYOJITOKEZA KATIKA LUGHA
Kutokana na taadhira hizi kuna aina mbalibali za makosa yanayojitokeza
kwa watumiaji wa lugha. Makosa hayo yamegawanyika katika sehemu kuu
mbili ambazo ni makosa ya Kisarufi na makosa ya kimantiki. Katika kipengele hiki tutaangalia makosa hayo na namna ya kurekebisha.
MAKOSA YA KISARUFI
Kila lugha ina kanuni na taratibu ambazo hutawala katika
matumizi ya lugha ili watu waweze kuelewana kanuni hizo zipo vunjwa au
kukiukwa huweza kusababisha makosa kujitokeza na upotovu katika lugha.
Makosa ya kisarufi yanaweza kugawanyika katika sehemu zifuatazo:- makosa
ya kimsamiati, makosa ya kimuundo, makosa ya matamshi, kuongeza
vitamkwa au viambishi, kuacha maneno, makosa ya tafsiri sisi.
MAKOSA YA KIMSAMIATI
Watumiaji wa lugha huchanganya masamiati wakati wa
kuzungumza au kuandika. Watu hutumia msamiati usiolingana na msamiati
usiolinga na maana iliyokusudia
Mfano:- Nona na nenepa
Wengi husema siku hizi umenona sana.
Badala ya kusema, Siku hizi umenenepa sana.
mazingira na mazingara
Watu husema Mazingara yameharibiwa sana siku hizi.
badala ya kusema Mazingira yameharibiwa sana siku hizi.
Ajali na ajili
Watu husema Amefariki wa ajili ya gari.
badala ya kusema Amefariki kwa ajali ya gari.
Wakilisha na wasilisha
Watu husema, Waziri wa fedha atawakilisha bajeti ya mwaka kesho.
Badala ya kusema Waziri wa fedha atawasilisha bajeti ya mwaka kesho.
MAKOSA YA KIMUUNDO
Kwa kawaida sentensi za kiswahili huanza na nomino ya mtenda au mtendwa.
Mfano:- mtoto mpole anacheza
Mzungumzaji asiye fuata kanuni husema Mpole mtoto anacheza.
Kalamu yangu imeibwa.
badala ya kusema kalamu yangu imeibiwa.
MAKOSA YA KIMATAMSHI
Watu wengi hushindwa kutamka baadhi ya sauti za
kiswahili wakati mwingine huchanganya na kubadili sauti hizo Mfano
Wakurya hutumia ’r’ badala ya ’l’
Nenda karare
badala ya kusema nenda kalale
Wandali hutumia ’s’ badala ya ’z’ na ’dh’ na ’th’
mfano selasini
badala ya thelathini
Sahabu
badala ya dhahabu
Samani
Badala ya zamani
Makosa haya mara nyingi yanatokana na athari ya lugha
mama. Kwa kuwa lugha ya kiswahili ni lugha ya pili kwa wazungumzaji
wengi. Hivyo lugha ya kwanza huwa na athari kubwa kwa mzungumzaji wa wa
lugha ya pili.
KOSA LA KUONGEZA VITAMKWA
Baadhi ya wazungumzaji huongeza vitamkwa mahari pasipo hitajika na hivyo kuharibu lugha.
Mfano. Nendaga
badala ya nenda
Mashule
badala ya shule
Huwaga anapenda fujo
badala ya huwa anapenda fujo
KOSA LA KUACHA MANENO
Watumia lugha huweza kuacha maneno katika sentensi na bado wakafikiri wanatoa ujumbe uleule uliokusudiwa.
mfano, Watu husema Juma ameondoka kazini akiwa na maana kuwa Juma ameondoka kwenda kazini lakini sahihi ni kuwa Ametoka kazini.
Alfredi amerudi kazini akiwa na maana kuwa Afredi ametoka kazini.
Kwa mzungumzaji anatoa maana ambayo ni kinyume kabisa na
ile maana aliyo kusudia kusema. Ambapo anakusudia kuuliza kama Alfredi
amekwenda tena kazini.
MAKOSA YA TAFSIRI SISISI
Tafsiri sisisi ni tafsiri ya neno kwa neno. Tafsiri hii inapofanywa huleta matatizo ya kisarufi katika lugha
mfano. Kimbizwa hospitali She runed to hospital
badala ya kusema amepelekwa hospitali
At the end of the day
Mwisho wa siku.
Badala ya kusema hatimaye.
MAKOSA YA KIMANTIKI
Mantiki ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Makosa ya
kimantiki ni yale yanayoonesha kukosekana kwa utaratibu wa fikra.
Nimakosa yanatokana na upotovu wa mawazo ya mzungumzaji
Mfano watu wengi husikika wakiema hivi: Usimwage kuku kwenye mchele mwingi
Badala ya usimwage mchele kwenye kuku wengi
Nyumba imeingia nyoka Badala ya kusema Nyoka ameingia ndani ya nyumba
Chai imeingia nzi Badala ya kusema Nzi ameingia kwenye chai.
MSWAHILI
Kutokana na mtazamo hiyo na dhana na maendeleo ya lugha ya kiswahili, inaonekana wazi kuwa ni vigumu kumpata mswahili ambaye ni mmiliki wa lugha hii ya kiswahili. Inaonesha dhahili kuwa mswahili anaweza kutazamwa kwa namna tofauti kama zifuatazo;-
i). Mswahili anaweza kuwa ni mtu mahuruti yaani ni mtu chotara ambaye ni lazima awe ametokana mwingiliano wa pande mbili ambao ni wabantu na watu wanaonasibishwa na Waarabu
ii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu wa mjini aliyeacha dini, utamaduni, mila na desturi zake za asili na kukimbilia dini, utamaduni, mila na desturi kutoka mataifa mengine kutoka uarabuni na nchi za kimagharibi
iii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya kiswahili
iv). Mswahili anaweza kuwa ni mkazi wa ya Afrika Mashariki hususani paeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
v). Mswahili anaweza kuwa ni mtu anayeishi katika maeneo ya kawaida ya mjini (uswahilini)
vi). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye ni mwafrika asili, anayepatikana katika nchi za Kenya na Tanzania
v). Mswahili ni mtu mwenye maumbile na ya kiafrika, ikimaanisha kuwa ni mtu wa miraba minne.
Kutokana na mtazamo hiyo na dhana na maendeleo ya lugha ya kiswahili, inaonekana wazi kuwa ni vigumu kumpata mswahili ambaye ni mmiliki wa lugha hii ya kiswahili. Inaonesha dhahili kuwa mswahili anaweza kutazamwa kwa namna tofauti kama zifuatazo;-
i). Mswahili anaweza kuwa ni mtu mahuruti yaani ni mtu chotara ambaye ni lazima awe ametokana mwingiliano wa pande mbili ambao ni wabantu na watu wanaonasibishwa na Waarabu
ii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu wa mjini aliyeacha dini, utamaduni, mila na desturi zake za asili na kukimbilia dini, utamaduni, mila na desturi kutoka mataifa mengine kutoka uarabuni na nchi za kimagharibi
iii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya kiswahili
iv). Mswahili anaweza kuwa ni mkazi wa ya Afrika Mashariki hususani paeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
v). Mswahili anaweza kuwa ni mtu anayeishi katika maeneo ya kawaida ya mjini (uswahilini)
vi). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye ni mwafrika asili, anayepatikana katika nchi za Kenya na Tanzania
v). Mswahili ni mtu mwenye maumbile na ya kiafrika, ikimaanisha kuwa ni mtu wa miraba minne.
HITIMISHO
Kabla ya uhuru kulikuwa na juhudi za makusudi za waasisi
wa Taifa letu kukuza na kukiendeleza kiswahili. Miaka hamsini baada ya
uhuru kiswahili kimekuaa na kuenea kwa sehemu kubwa dunia. Pamoja na
hayo kiswahili kimekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zimeweza
kupotosha lugha hii. Upotoshwaji huo hufanywa na wazawa au watumiaji wa
kiswahili na kukifanya kiswahili kionekane kuwa hakina maana wala
thamani kwa watu wengine. Watanzania ambao ni watumiaji wakuu wa lugha
yakiswahili wanatakiwa kuchukua juhudi za makusudi katika kukifanya
kiswahili kiwe katika hadhi yake. Kimatamshi, kimuundo, na kimsamiati.
Pia Serikali ichukue juhudi za makusudi za kukikuza na kukiendeleza
kiswahili kwa kuwaelimisha na kuwatunza wataalamu wa lugha hii adhimu ya
Tanzania. Wataalamu wawe na msimamo mmoja katika taaluma hii maana
wakati mwingine huwachanganya watu wanaojifunza lugha hii. Lugha hii ya
kiswahili ibaki katika misingi ya sarufi yake ya lugha za kibantu ambazo
kwazo zimeunda kiswahili.
VITABU VYA REJEA
Chiraghdin S. na Mnyapala M. (1977) Historia ya Kiswahili, Oxford University Press Nairobi
Nkwera, F.M.V, (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo, THP, Dar es salaam.
Massamba na wenzake (1999) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA), TUKI, Dar es salaam
Khamis, A.A, 2003 Uchambuzi Halisi wa Matumizi ya Kiswahili Asilia, Zanzibar. SUZA Press
Msokile M (1992) Historia na Matumizi ya Kiswahili EPD Kibaha
TUMI ( ) Kiswahili Sekondari,
Broomfield (1930) Sarufi ya Kiswahili, London, The sheldon press
Habwe J. na Karanja P. (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Nairobi phonex Publishers LTD
Mwansoko HJM na Tumbo. (1996) Matumizi ya kiswahili Bungeni, TUKI, Dar es salaam
BAKITA, (2004), Makala ya siku ya Kiswahili Kiswahili na Utandawazi, Dar es salaamu
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la pili, Oxford university press, Nairobi