FANTASIA KATIKA KITABU CHA ADILI NA NDUGUZE



TOFAUTI KATI YA FASIHI YA WATOTO NA FANTASIA

Leo tutaenda kuangalia dhana mbili tofauti ambazo watu wengi huzichanganya na wengine huzani kama ni dhana moja. Dhana hizo ni fasihi ya watoto na dhana ya fantasia katika lugha ya kiswahili. Pia tutachambua fantasia ilivyojitokeza katika kitabu cha Adili na Nduguze cha Shaaban Robert. Basi tuanze kwa kuangalia fasihi ya watoto kisha tuje kuangalia fantasia.

FASIHI YA WATOTO

Wamitila (2003) anafafanua fasihi ya watoto kuwa ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto. Hii ni fasihi ambayo ni tofauti na ngano au hurafa.

Hivyo tunaweza kusema kuwa fasihi ya watoto ni aina ya fasihi ambayo madhumuni yake makuu ni kwa ajili ya watoto katika jamii husika

SIFA ZA FASIHI YA WATOTO

fasihi ya watoto hutumia maandishi makubwa
Kazi za watoto hasa vitabu huchapishwa kwa maandishi yenye ukubwa tofauti. Kazi inayowalenga watoto wadogo sana hasa wale ambao kwanza ndio wameingia katika ulimwengu wa usomaji huwa zimesheheni maandishi makubwa yanayoweza kuonekana. Iwapo mtoto ni wa kiwango cha kati yaani darasa la nne na tano maandishi yao bado yatakuwa makubwa lakini si kama yale ya darasa la pili.
Pia maandishi ya kazi za fasihi za watoto wa darasa la sita na saba yatakuwa madogo kuliko yale ya watoto wadogo zaidi. 
Maandishi hayo pia hutiwa rangi ili yavutie macho ya watoto. Rangi zenyewe huwa za kupendeza na huteuliwa kiufundi. Hali hii huchangia kuvuta makini ya watoto na kuwachochea kuisoma kazi teule.
Msuko mwepesi (hutumia muundo wa moja kwa moja)
Misuko ya kazi za watoto huwa miepesi ili kumwezesha msomaji kuweza kufuata matukio yenyewe. Msuko huo mwepesi hutilia maanani sana matukio na aghalabu hukitwa kwenye muundo wa A-B-C-D.  Muundo huu wa A-B-C-D ni muundo sahili, yaani wa moja kwa moja. Pengine muundo huu huzingatia kuwa mtoto akichanganyiwa matukio, anaweza kuchoka na kuacha kufuatilia kazi husika au labda hata asiielewe kabisa.

Matumizi makubwa ya fantasia
Fantasia ni hali ya kuwepo kwa mambo ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi yasiyotarajiwa kutokea katika maisha ya kawaida. Ni dhana inayotumiwa kueleza kazi ya fasihi ambayo ina sifa ambazo zinakiuka uhalisia, Wamitila (2003). Fantasia huleta mvuto wa kipekee katika kazi za watoto na hivyo kufanya watoto wengi kufurahia sana kazi ambazo zina fantasia.

Lugha nyepesi na inayoeleweka kwa watoto
Kazi ya watoto huwa na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto. Lugha 'changa’ hutumiwa. Uchanga wake unakuwa katika hadhi ya tungo kama sentensi fupi.  Miundo migumu na sentensi changamano hazipendekezwi kutumiwa katika fasihi ya watoto isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo. Wepesi wa lugha hutokana na umri na uwezo wa wasomaji. Urazini wa watoto kwa kawaida ni mdogo. Hivyo basi, sharti sentensi zinazotumiwa ziwe fupi, sahili na zenye kueleweka bila mkanganyo.  Hata hivyo, usahili wa lugha haupaswi kuchukuliwa au kueleweka kuwa uchapwa au hali duni ya matumizi ya lugha.

Kazi nyingi huwa ni fupi
Aghalabu fasihi ya watoto huhusisha tungo fupi. Mtoto anapopewa kitabu asome, kwanza huangalia picha na baada ya hapo huangalia ukubwa wa kitabu. Ikiwa kitabu kina kurasa chache, hapo huhamasika kukisoma kwa sababu anajua atamaliza kukisoma kwa haraka. Kama ni kitabu kikubwa, mtoto hushikwa na uvivu hata kabla hajaanza kukisoma.
Kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo huweza kupoteza mvuto kabisa kwa watoto. Hadithi za watoto hazina kina au undani wa kimasimulizi ambao hudhihirika katika fasihi ya watu wazima. Usimulizi hujikita katika maelezo ya mambo ambayo huwa ni muhimu tu katika kuijenga hadithi na kuubainisha muktadha wake.

matumizi ya vielelezo; picha au michoro yenye rangi
Fasihi ya watoto huwa na vielelezo na picha tena zenye rangi. Hali hii huwafanya watoto kutosahau kwa urahisi kile walichosoma lakini pia huwasaidia kuhusisha matukio katika hadithi na ulimwengu halisi.

Wahusika na uhusika
Fasihi ya watoto huwa na wahusika na uhusika wa aina mbalimbali. Kuna kazi ambazo huwa na watoto kama wahusika wakuu. Vinginevyo, fasihi ya watoto hutumia kwa kiasi kikubwa wahusika wanyama. Wanyama hawa hufuata tabia za watu; wanazungumza na kutenda matendo ambayo kwa jumla yanahusishwa na watu.
Isitoshe, katika fasihi ya watoto, wahusika wanaweza kuwa mazimwi na majitu. Zimwi ni kiumbe ambaye anapewa sifa zinazokiuka sifa za binadamu na huwa na sifa hasi kama ulafi, ukatili, ubaya, uovu na kadhalika.


FANTASIA KATIKA KITABU CHA ADILI NA NDUGUZE: SHAABAN ROBERT

kabla hatujaangalia fantasia ilivyojitokeza katika kitabu hili basi tuangalie maana ya fantasia yenyewe.

Fantasia ni hali ya kuwepo kwa mambo ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi yasiyotarajiwa kutokea katika maisha ya kawaida. Ni dhana inayotumiwa kueleza kazi ya fasihi ambayo ina sifa ambazo zinakiuka uhalisia, Wamitila (2003).
hivyo basi, fantasia ni hali ya kudhihika kwa matukio ya ajabuajabu yasiyokuwa na uhalisia wa moja kwa moja kwa jamii ndani ya kazi ya fasihi. Kawaida fantasia hupambwa na sifa mbalimbali ambozo ndio muongozo wa kuchambua kitabu chetu cha Adili na Nduguze. Baadhi ya sifa hizo ni matumizi ya taharuki, kuelezea mambo ya ajabuajabu, kutumia wahusika wa ajabuajabu, matumizi ya taswira kwa wingi na matumizi ya tashihisi.


SIFA ZA FANTASIA ZILIVYOJITOKEZA KATIKA RIWAYA YA ADILI NA NDUGUZE.

UTANGULIZI

Adili na Nduguze ni riwaya iliyoandikwa na mwandishi mashuhuri sana Shaaban Robert. Kitabu kinachoelezea maisha ya jamii zetu katika muktadha mbalimbali. Riwaya hii inaonyesha jinsi gani watu tulivyogawanyika duniani kutokana na matendo yetu. Mwandishi anamtumia Adili kama kielelezo chema kuwa alikuwa ni mtu mwema sana na mwenye upendo wa dhati kwa ndugu zake na jamii kwa ujumla licha ya ndugu zake kumchukia mpaka walifikia hatua ya kumtupia baharini ili apoteze maisha lakini siku zote mtenda mazuri hulipwa jamala naye kuokolewa na watu wengine. Adili na Nduguze ni kitabu ambacho kimeelezea matukio mengi sana ya ajabu na wahusika wake wengi ni waajabu sana, mwandishi ameweza kufikisha ujumbe kwa jamii kwa mtindo wa aina yake. Basi hebu tuangalie fantasia ilivyojitokeza katika kitabu hili cha mwandishi mkongwe Shaaban Robert.


kwa kutumia sifa zifuatazo za fantasia basi tutaweza kuhusianisha na riwaya ya Adili na Nduguze jinsi zilivyoweza kujitokeza :-
Fantasia hueleza matukio ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi,
haya ni matukio ambayo huwezi kuyakwepa katika kazi yeyote ile ya kifantasia katika riwaya ya Adili na Nduguze kuna matukio mengi ya ajabuajabu yaweza kudhihilika mfano katika uk 22 tunaona Tandu anajigeuza kuwa binadamu na kuwa msichana mzuri, tukio lingine ni katika uk 25, pale watu katika mji wa mawe wamebadilishwa na kuwa mawe matupu ndipo ukapatikana mji wa mawe,pia ajabu jingine ni pale ndugu zake adili wanapobadilishwa na kuwa manyani kama adhabu kwao.n.k

Fantasia hutumia sana michoro pamoja na picha katika matukio mbalimbali.
Katika kitabu hiki cha Adili na Nduguze mwandishi ametumia michoro mbalimbali mingi tena yenye kushangaza mfano katika uk 12 manyani yamepanda farasi, uk 26 adili amewasili katika mji wa mawe na kukuta watu wote wamegeuzwa mawe, pia uk 35 mhusika Mrefu alivyokuwa akimshauri mfalme tukufu, pia uk wa 41 adili alipokuwa anatupwa baharini na Ndugu zake na uk 49 ambapo yule msichana jina lake mwelekevu alipojitosa habarini.

Fantasia kutawaliwa na mandhari ya kubuni kwa kiasi kikubwa.
Pia hii ni moja ya sifa ya fantasia kutumia mandhari ya kubuni mfano ughaibuni, mji wa mawe,janibu, majini miji ambayo haipo haipo sehemu yeyote ile duniani.

Fantasia hutumia wahusika wa ajabuajabu katika kazi ya fasihi,
mfano mrefu, manyani, mwelekevu, nyoka, tandu. Katika riwaya hii utaona jinsi wahusika hawa walivyokuwa na sifa za ajabuajabu mfano mhusika “mrefu” alikuwa na sifa zifuatazo uk 35,
alikuwa na miguu mikubwa na mapaja manene,
kiuno cha utambo na kifua kipana,
shingo yake ndefu ilichukua kichwa kikubwa,
kwa kimo cha kurithi alitembea baharini bila ya kuguswa na maji magotini,
aliweza kukamata ndovu chini au nyangumi baharini akamwoka kwa jua mbinguni,
sauti yake ilikuwa kama radi. n.k zote uk 35.

fantasia huwa na taharuki ya hali ya hali ya juu.
Taharuki ni hali ya msomaji wa kazi ya fasihi kutaka kujua nini kinaendelea au nini kitatokea baada ya tukio fulani kulisoma (mshawasha wa kujua cha mbele zaidi katika kazi ya fasihi). Katika riwaya yetu ya adili na nduguze mwandishi ametumia taharuku nyingi sana baadhi ya taharuki hizo ni :-
  • Adili alipotupiwa baharini na ndugu zake msomaji anajiuliza adili atakufa au atanusulika basi inabidi aendelee ili aweze kujua zaidi uk 41.
  • taharuki nyingine ni pale mfalme Rai alipomuandikia barua binti mfalme wa majini (Huria) kuomba msaada wa manyani kusamehewa ili waweze kurudi katika umbo la ubinadamu uk 57, msomaji anajiuliza je? Kweli binti mfalme atakubali basi hamu inakuja ya kutaka kuendelea kujua zaidi.

Matumizi makubwa ya taswira
mfano wa taswira zilizojitokeza katika kitabu hiki cha Adili na Nduguze ni :-
manyani – watu wakosefu
mji wa mawe – mji wa dhambi
ughaibuni – mchi au jamii bora ambayo haikuwai kupatikana. n.k

matumizi ya tashihisi
tashihisi ni kipengele cha matumizi ya lugha ambacho vitu visivyoweza kutenda kama binadamu hupewa uwezo wa kibinadamu. Hivyo basi katika kazi ya kifantasia matumizi ya tashihisi hushamili sana mfano ;:-
wakati umefka wa mawe kusema ,miti kujibu na wanyama kuwa watu uk uk 13.
Tandu alijigeuza mwanadamu uk 22.
fantasia hutumia lugha ngumu.( si ya kawaida kila mtu kuelewa)
Hii imejidhihirisha katika kitabu hiki cha Adili na Nduguze kwa mtu wa kawaida anaitaji muda mwingi sana kuweza kugundua nini ambacho mwandishi amekikusudia ndani ya jamii yake.

Powered by Blogger.