NADHARIA ZA MAANA
NADHARIA ZA MAANA
Habwe na Karanja (2007:204), Crystal (1987), Matinde (2012), Ogden
na Richards (1923), wanakubaliana kuwa neno maana lina fahiwa nyingi, linaweza kudokeza
sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelekezo, ufafanuzi, kufaa na ukweli.
Kutokana na ugumu uliopo katika kufafanua maana ya maana, wanaisimu wamefafanua
aina kuu mbili za maana ambazo ni maana ya msingi na maana ya ziada. Utetezi wa
nadharia hii umesababisha kuibuka kwa nadharia mbalimbali ambazo zinajaribu
kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali, ambazo chimbuko lake ni
wanaisimu, wanafalsafa, wanamantiki na wanasaikolojia.
Nadharia ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya
au kutekeleza jambo fulani (Mdee na wenzake, 2011). Kwa msingi huo nadharia
hubeba mawazo, dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au kwa lengo la kueleza hali
fulani, chanzo, muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.
Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu,
mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa
sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira na mwongozo wa kulikabili
jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
Nadharia za maana ni miongozo ambayo hutambulisha mbinu mbalimbali
za kujifunza namna ya kufasiri maana katika lugha (Matinde, 2012:247). Katika
kufafanua maana nadharia zinazohusika ni nadharia ya urejeleo, dhana au
taswira, matumizi, uelekezi, masharti‒ukweli, kichocheo‒mwitikio, na vijenzi
Semantiki.
Ufuatao ni ugumu unaojitokeza katika kufasili maana ya maana kwa
kuzingatia nadharia za maana kama zinavyo
pambanuliwa.
Nadharia ya urejeleo iliasisiwa na Ogden na Richards, wanafalsafa
hawa wanadai kuwa maana hujitokeza pale palipo na kirejelewa chake (Lyons, 1981). Waasisi wa
nadharia hii wanadai kuwa lazima kuwe na kirejelewa. Mfano mtu kipo kitu
kinachorejelewa, waasisi hawa waliibuka na dhana ya pembe tatu ili kueleza
nadharia yao kama
inavyoonekana hapa chini.
Dhana (fikra)
Umbo la isimu kirejelewa (kitaje)
Kuna umbo la isimu kama kitaja neno,
misemo, kauli au sentensi na vitu hivi hufanya tujenge dhana akilini. Dhana hii
ndiyo inatufanya tupate kirejelewa, kuna uhusiano imara kati ya umbo la isimu
na dhana. Dhana na kirejelewa akilini hakuna uhusiano imara kati ya umbo la
isimu na kirejelewa, kiunganisho kati ya neno na kirejelewa katika dunia halisi
bali ni fikra tu (Matinde, 2012).
Ugumu unaojitokeza katika kueleza maana ya maana katika nadharia ya
urejeleo ni kwamba si kila kinyambo au leksimu yenye maana ina kirejelewa chake
(Austin, 1970).
Ni dhahiri kuwa pamoja na kuwepo kwa maneno mengi yenye virejelewa vyake kuna
baadhi ya maneno yasiyokuwa na virejelewa. Nomino dhahania hubeba maana fulani
katika jamii ya watu. Kwa mfano Mungu, malaika, jini, shetani, njaa, upole,
upepo, hasira na furaha ni vinyambo vyenye maana ijapokuwa havina kirejelewa kama nadharia inavyodai. Kukosekana kwa kirejelewa
kunasababisha utata au ugumu katika kufasili maana kwa kuzingatia nadharia ya
urejeleo.
Kielelezo 2
Umbo la isimu↔
dhana ↔kitajwa
↓ ↓ ↓
Mungu X – mwenye kuumba ulimwengu na vyote
vilivyomo ndani yake.
Upepo X − hewa isiyotulia na aghalabu huenda kwa kasi.
Pia nadharia hii inapata ugumu wa kufasili maana ya maana kwa maneno
yenye uhusiano wa kihomonimia ambapo kuna baadhi ya maneno yanayorejelea zaidi
ya hali au kitu kimoja (Matinde, 2012:252). Kwa mfano paa [+ondoa mamba ya samaki kwa kuparuza
kwa kitu kama kisu]
[+enda juu]
[+chukua baadhi ya
makaa ya moto weka mekoni]
[+mnyama wa porini
anayefanana na mbuzi aliye mwembamba sana]
Kaa [+kipande cheusi cha kuni kilichochomwa na kuzimwa kabla ya kuwa
majivu]
[+mnyama mdogo wa
majini mwenye miguu sita au zaidi]
[+kuweka matako au
makalio juu ya kiti]
Panda [+mgawanyiko katika kitu]
[+pembe kubwa na ndefu iliyotobolewa tundu
katika ncha yake inayopigwa katika ngoma au kutoa
taarifa]
[+paji la uso]
[+enda kuelekea juu
ya kitu]
[+weka mbegu au
mche katika ya ardhi ili ikue]
Kutokana na mifano hiyo hapo juu ni dhahiri kuwa kwa kutumia
nadharia hii ya urejeleo ni vigumu kufasili maana ya maana kwa kuwa neno paa, panda na kaa hurejelea fahiwa nyingi.
Nadharia ya urejeleo haifanyi kazi kwenye maneno yenye uhusiano wa
kipolisemia (Holm na Karlgren, 1995:3). Polisemia ni maneno ambayo yana
uhusiano kimaana, na mara nyingi maana ya maneno huwa imepanuka kadri ya mpito
wa wakati. Mfano wa maneno kama vile;
Kichwa [+ cha binadamu]
[+ kama kiongozi]
Jicho [+ la sindano]
[+la binadamu]
mguu [+wa binadamu]
[+wa gari]
Kutokana na mifano ya maneno hayo hapo juu, nadharia ya urejeleo
haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kipolisemia. Kwa sababu
waasisi wa nadharia ya urejeleo wanadai kuwa katika urejeleo lazima kuwe na
kirejelewa kimoja na jina moja tu, lakini maneno yenye uhusiano wa kipolisemia
huwa na kirejelewa zaidi ya kimoja ambavyo huweza kurejelea maana
tofautitofauti.
Maneno kama vielezi, na vihusishi yanakosa maana katika nadharia hii
(Filp, 2008:20). Kwa mujibu wa wanaurejeleo maana ya neno ni kitu
kinachorejelewa na neno husika, kwa msingi huu maneno ni majina ambayo hutaja
vitu. Aidha dhana hii inaonesha kuwa maneno yasiyokuwa nomino kama
vile vielezi na vihusishi hayana maana, jambo ambalo halina ukweli. Hii ni kwa
sababu lugha yoyote inajumuisha aina mbalimbali za maneno na si majina tu.
Nadharia hii haiwezi pia kufafanua maana katika kiwango cha
sentensi, ambapo sentensi ni tungo inayojitosheleza kimaana, kimsingi huhusisha
na mtendaji, neno sentensi haliwezi kufafanuliwa na kupata urejeo sentensi.kwa
mfano (a) Mwalimu anafundisha darasani
(b) Juma anapika ugali
Katika sentensi hizi urejeleo wa maana ya sentensi nzima hauwezi
kupatikana.
Aidha nadharia ya uelekezi ni dira ambayo waasisi wake wanadai kuwa,
njia nzuri ya kufafanua maana ya kitu au dhana ni kusonta kwa kidole kile
kinachorejelewa (uelekezi kwa kutumia kidole) (Matinde, 2012:252). Ni muhimu
kuelewa kuwa kalamu ni nini, na mbuzi nini
na kuelewa kuwa umelenga kalamu nzima na mbuzi mzima na wala si sehemu tu ya
kitu. Hivyo basi nadharia hii ya uelekezi inapata ugumu wa kufasili maana ya
maana kama ifuatavyo;
Baadhi ya maneno katika lugha hayawezi kufafanuliwa kwa kusonta
kidole ( uelekezi kwa kutumia kidole), mfano usingizi, urafi, njaa, hekima na
busara. Kwani unaposonta kidole tumboni tunaweza kupata fahiwa mbalimbali kama vile njaa, shibe, ujauzito, minyoo na utumbo.
Pia nadharia hii ni ya kidhahania kwani huakisi tu kuwa anaye
elekezwa anaufahamu au maarifa awali kuhusu kile kinachorejelewa. Mfano inatuwia
vigumu kumfafanua ng’ombe kwa kusonta kidole kwa mtu asiyekuwa na maarifa ya
awali ya ng’ombe kuwa anasifa zipi.
Aidha sababu za kiutamaduni huweza kuleta ugumu katika matumizi ya
nadharia hii katika ufasiri na ufafanuzi wa kile kinachorejelewa. Mfano sehemu
nyingi nchini Kenya neno
mchele hurejelea uliopikwa na ambao haujapikwa, tofauti na Tanzania ambapo neno mchele
hurejelea usiopikwa tu, na mchele uliopikwa huitwa wali. Hivyo ni vigumu
kufafanua maana ya maana kwa kutumia nadharia hii ya uelekezi.
Nadharia vijenzi semantiki ni nadharia inayopambanua leksimu au
vinyambo vilivyo katika kikoa kimoja cha maana kwa kutumia seti isiyo na ukomo (Baron,
1972). Kwa kigezo hiki sifa za leksimu hupambanuliwa kwa kutumia alama ya
kujumlisha (+) inayodokeza uwepo wa
sifa hiyo na alama ya kutoa (-)
inayodokeza kutokuwepo kwa sifa tajwa. Aidha sifa bainifu za leksimu moja
huitofautisha na leksimu nyingine.
Kutokana na matumizi ya mbinu ya uwili kinzani kutofaa katika
leksimu ambavyo vijenzi vyake havibainishiki kwa urahisi, maana ya maana bado
ni tata. Alama kinzani (+ na -) haviwezi kuwa na uzito katika aina zote za
maneno kama vile vihusishi na vinganishi
vinapotumiwa kufasili maana ya maneno husika. Kwa mfano ni rahisi kufasili neno
mvulana kwa kutumia kijenzi MTU, MTU MZIMA na ME kwa kutumia alama + au – lakini ni vigumu kubaini vijenzi semantiki katika kufasili
kiunganishi kwa.
Pia kutokuwepo kwa vigezo vya uteuzi wa vijenzi, kunatatiza fasili
ya maana kwa kuzingatia nadharia ya vijenzi semantiki. Nadharia hii haiweki
wazi sana
kilichozingatiwa katika kuteua vijenzi husika wakati wa kufasili leksimu
mbalimbali. Kwa mfano kijenzi ME kinatumiwa katika ufafanuzi wa leksimu
zinazohusu binadamu na udugu. Jambo hili linatatiza na kuibua hisia zisizo na
jibu la haraka kama kusahaulika kwa kijenzi
KE, ni mfumo dume au la. Aidha matumizi ya vijenzi mlalo na mfuatano katika
fasili za udugu hauzingatii umbali au ukaribu. Kwa mfano ndugu wa tumbo moja
(kaka au dada) si lazima wafuatane kwa karibu.
Vile vile hakuna ukomo wa vijenzi katika fasili ya leksimu, pamoja
na nadharia hii kufanikiwa kubainisha vikoa maana katika lugha, hakuna uthibiti
wa idadi ya vijenzi vinavyotumika. Leksimu moja katika lugha inaweza kuwa na
idadi tofauti ya vijenzi semantiki ukilinganisha na neno jingine katika lugha
ile ile. Kwa mfano neno mvulana linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi [MTU], [MTU
MZIMA] na [ME], wakati neno kaka linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi semantiki
[ME], [MZAZI], [MLALO] na [MFUATANO]. Tofauti hii ya vijenzi semantiki kutoka
neno moja na jingine inazua uvulivuli wa kufasili maana ya maana kwa kutumia
nadharia ya vijenzi semantiki.
Aidha uwepo wa orodha ya vijenzi semantiki vya jumla vinavyotumiwa
katika kufasili vinyambo vya lugha mahususi unakosa uthibitisho. Hii inatokana
na ukweli kwamba kila lugha ina kanuni zake mahususi. Hivyo, ujumla
unaosisitizwa na wanadharia ya vijenzi semantiki ni wa kutiliwa shaka kwani
lugha inaweza kutofautiana na lugha nyingine katika vijenzi-semantiki kutokana
na utamaduni wa jamii husika.
Nadharia ya dhana au taswira iliasisiwa na
wataalumu wa isimu ambao ni Sapir na Desassure (Ogden na Richards, 1923). Ambapo
msingi wake mkuu unaeleza kuwa maneno ya kiambo ni dhana au taswira
inayoibuliwa na kiambo hicho akilini mwa mwanalugha wakati kiambo hicho
kinapotumika. Kwa mujibu wa nadharia hii maana ya neno, kisemo na sentensi
hujengeka akilini mwa msikilizaji au mzungumzaji. Kwa mfano tunaweza kuwa na NENO ↔ DHANA. Nadharia ya dhana huhusisha moja kwa moja maana na
wazo, taswira au hisi badala ya kuhusisha maana na kitu moja kwa moja. Pia
husaidia kutoa majibu ya vinyambo visivyoweza kurejerewa kama
vile: Mungu, shetani, upepo, njaa, usingizi, upendo na furaha, kwa kuwa
nadharia ni wazo kuu linalomwongoza mtu ama jamii kutenda jambo fulani, ni dhahiri
kuwa nadharia ya dhana humwongoza mwanalugha kuhusisha maana na wazo, taswira
au hisi. Kutokana na upungufu wa nadharia hii upo utata au ugumu wa kufasili
maana ya maana kwa sababu;
Dhana ya picha au taswira si bainifu na haiwezi
kuchunguzika na kutabiri chochote. Huwezi kutabiri maana ya neno wala kufanya
utafiti wa aina moja. Kwa sababu maana ya kiashiria hutokana na picha au
taswira zinazojengeka akilini mwa mwanalugha. Hivyo maana ya maana inabaki kuwa
telezi kwa kuwa kila kiashiria kinajengewa maana kulingana na picha
iliyojengeka akilini mwa mwanalugha. Kwa mfano, kiashiria kiti kinaweza
kujengewa picha tofauti akilini mwa mwanalugha kulingana na mazingira au uzoefu
wa mwanalugha huyo. Kielelezo kifuatacho kinaonesha ni kwa namna gani picha ya
kiti inaweza kuwa na maana mbalimbali kulingana na picha ya mwanalugha
aliyoijenga akilini mwake.
Kiashiria Taswira au picha
KITI
- kiti
cha ofisini
- kiti cha
kinyozi
- kiti cha umeme
Picha kama hizi zinajengwa na mwanalugha huku
akiwa anafahamu kuwa kiti ni kifaa kilichotengenezwa kwa kutumia mbao, kwa
ajili ya mtu mmoja kuketi, kina miguu minne, kina sehemu ya egemeo la nyuma.
Ugumu wa kufasili maana ya maana unakuja pale mwanalugha anapokuwa na picha au
taswira ya kiti chenye mguu mmoja na kile chenye miguu mitatu. Pia kiashiria
nyumba kinaweza kuwa mfano wa kiashiria chenye kujengewa picha tofauti tofauti
akilini mwa mwanalugha. Ikiwa nyumba ni jengo ambalo limekusudiwa kukaliwa na
watu. Utata unakuja pale mtu anayejua kuwa banda ni nyumba ambayo hutumika
kuwekea vitu au wanyama.
Aidha, picha za akilini ni dhahania ya kutosha
kuweza kuwakilisha maana za nomino au vitenzi vya kawaida. Dhana anayoijenga
mtu akilini mwake haiwezi kufumbata maana ya kitu halisi. Kwa mfano, mtu anaposikia
neno mbuzi, dhana itakayojengwa inaweza kuwa dhana ya kiumbe mnyama, kiumbe hai,
kifaa cha kukunia nazi, kiumbe mwenye miguu minne. Maana inayojengwa hutegemea
zaidi ukomo wa fikra zake. Aidha utofauti katika uwezo wa kujenga dhana akilini
juu ya leksimu fulani unapunguza maana ya kitu kinachojengewa dhana.
Hakuna picha ya jumla ya mguso katika nadharia ya
dhana au taswira, kwani kila mwanalugha hujenga picha akilini mwake kulingana
na imani yake, uzoefu wake, na mazingira yake (Holm na Karlgren, 1995:6).
Katika majina au nomino dhahania mwanalugha hawezi kuvigusa viashiria ila huvijengea
picha viashiria hivyo akilini mwake kama vile
kiashiria shetani hakina mguso. Hakiwezi kuonekana wala kushikika bali
mwanalugha hujenga picha akilini mwake kuwa kiashiria shetani kina maana ya
kiumbe mwenye pembe ndefu, mbaya wa sura, kiumbe wa kutisha, tena mtoa roho za
watu ambaye kwa hakika ni laghai lakini pia shetani kama
kiumbe anaweza kujengewa picha na mwanalugha kuwa ni mtu yeyote mwenye matendo
mabaya. Kutokana na ujengaji wa picha au dhana akilini mwa mwanalugha inakuwa
vigumu kueleza maana ya maana kutokana na ujenzi tofauti wa picha katika akili
ya mwanalugha.
Pia ugumu wa kueleza maana ya maana unakuja pale
tu ambapo nadharia ya dhana inadai kwamba kila kinyambo kina husiana na taswira
wakati si kila kinyambo kinahusiana na taswira (Holm na Karlgren, 1995:3). Kwa
mfano, kinyambo kama vile ingawa, lakini na
japokuwa havina taswira ambayo mwanalugha anaweza kuijenga akilini mwake. Hivyo
basi kutokana na ugumu huu wa baadhi ya vinyambo kukosa taswira kunakuwa na
utata wa kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia ya dhana au taswira na
kuifanya maana ya maana kubaki kuwa dhana telezi tu.
Haiwezi kuelezea vinyambo viwili kuwa vyaweza kuwa
visawe. Taswira au dhana inayojengwa akilini kuhusishwa na kinyambo kimoja tu
haiwezi kukubalika kwani inaweza kuvitenga visawe kwani si kila dhana
inawakilishwa na neno moja tu (Matinde 2012:256). Kwa mfano badala ya kusema
nyati mwanalugha mwingine anaweza kusema mbogo, chumvi kuwa munyu, dagaa kuwa
kauzu, tembo kuwa ndovu. Uwepo wa visawe
unadhihirisha udhaifu wa nadharia hii katika kufasili maana ya maana kwani
taswira au picha ya akilini si kigezo toshelevu cha uchanganuzi na ufasiri wa
maana. Hii ni kwa sababu kila mzawa wa lugha huwa na picha tofauti kuhusu
maneno, vitu, dhana au hali mbalimbali.
Pia, nadharia hii haiwezi kuelezea maana ya
sentensi au nahau, kwa kuwa maana ya kinyambo haipatikana katika leksimu tu na
wala si utungo mrefu kama vile nahau na
sentensi. Nahau ifuatayo inaweza kutumika kama
mfano kuntu wa hoja hii. “amekula chumvi nyingi” katika hali ya kawaida ni
vigumu mtu kujenga maana ya dhana hiyo kama
hana uelewa wa wazo. Kwa maana hiyo dhana atakayoijenga itahusiana na chumvi
moja kwa moja, wakati maana ya nahau hii ni kuishi miaka mingi.
Nadhria
ya kichocheo-mwitikio iliasisiwa na wanasaikolojia Skinner na Watson, wao
wanadai kuwa maana ya neno au dhana husika hufafanuliwa katika hatua tatu
ambazo ni kichocheo, tamko na mwitiko (Holm na Karlgren, 1995:4). Hivyo
nadharia hii inaeleza kuwa maana ya umbo la kiisimu linalotamkwa na msemaji
hutokana na mwitiko wa msikilizaji. Kwa hiyo nadharia hii huchukulia kuwa maana
ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Pia maana ya tamko huwa
katika muundo wa kitendo –uneni kama
inavyooneshwa hapa chini.
Kichocheo …→ (mwitiko…kichocheo) …→ mwitiko
Tamko
……………… Jibu la msikilizaji.
Kwa mfano; Musa ameamua kuvuta sigara chumbani, kuna harufu nzito
inayotokana na moshi wa sigara. Hali hii inamlazimu Juma kutoa tamko; fungua
madirisha yote. John na Kulwa wakaitikia kwa kufungua madirisha na yule mvuta
sigara akazima sigara yake. Hivyo basi katika hali hii kichocheo cha tamko la
Juma ni harufu ya moshi wa sigara, kiitikio ni John na Kulwa kufungua madirisha
na mvuta sigara kuzima sigara. Kwa hiyo maana ya usemi inabainishwa na mwitiko
wa John, Kulwa na mvuta sigara.
Udhaifu wa nadharia hii ya kichocheo-mwitiko ni kwamba, kichocheo
kimoja kinaweza kusababisha utokeaji wa viitikio viwili au zaidi. Kwa mfano
mvua imeanza kunyesha, mama anawaamrisha watoto waingie ndani. Watoto
wanaitikia kwa kukimbia kwenda ndani ya nyumba.
Kichocheo……………………mvua
Tamko………………….ingia
ndani
Kiitikio
……………….watoto kuingia ndani ya nyumba upesi.
Katika mfano wetu huu viitikio vinaweza kuwa; watoto kuchukua ndoo
na sufuria na kuanza kuteka maji, kuingia ndani na kuchukua miavuli, kuingia
ndani na kukoka moto (Matinde, 2012:259).
Maneno mengi katika lugha hayataji vitu vinavyoonekana, kwa hiyo
basi maneno hayo hayawezi kusababisha mwitikio wa msikilizaji. Mfano wa maneno
hayo ni kama vile njaa, busara, upendo, uchoyo
na huruma (Alston, 1967). Hii ni kwa sababu maneno dhahania hayawezi kuelezwa
kwa kutumia nadharia hii.
Pia wakati mwingine wanalugha hawaitiki maneno kwa vitu vinavyowakilisha
maneno hayo (Holm na Karlgren, 1995:4). Hii ina maana kuwa kujenga maana ya
kinyambo kwa kutumia nadharia ya kichocheo mwitiko inalazimisha upekee wa
vinyambo au maneno husika. Ukweli ni kwamba wanajamii huitikia vitu
vinavyowakilisha maneno hayo.
Aidha semi nyingi sana
katika lugha hazidhibitiwi na kichocheo katika muktadha peke yake. Kwa mantiki
hii nadharia ya kichocheo mwitiko inakosa mashiko kwani wakati mwingine mtu
anaweza kuulizwa swali na asijibu au akajibu kinyume kabisa na swali. Kwa mfano
ni kawaida kwa Mtanzania kusema nakuja wakati anaonekana anakwenda.
Nadharia ya masharti – ukweli husisitiza dhana ya ukweli katika
ujasiri wa maana, hivi kwamba maana sharti iwe ya kweli na ukweli huo
ubainishwe bayana. Nadharia hii iliasisiwa na wanamantiki na wanafalsafa, kisha
ikafafanuliwa na wanaisimu.
Mfano (a) Ukweli wa kihistria
i/ Muungano wa Tanzania na Zanzibar 1964
ii/ Rais wa kwanza
wa Tanzania
ni J. K.Nyerere
(b) Ukweli wa
maarifa ya kiulimwengu
Ukweli huu
hutokana na uhalisia wa kiulimwengu ambao kila mwanajamii anakuwa nao. Mfano shairi
huundwa na beti, mistari, vina na mizani au mwanamke hujifungua.
(a)ukweli wa kiisimu
Ukweli huu hubainishwa kupitia mfuatano wa
maneno katika sentensi na usahihi wa mfuatano huo.
i ) Hadija aliolewa na Kanyansa (sahihi)
ii) Kanyansa aliolewa na Hadija ( si sahihi)
Nadharia hii hushughulikia sentensi arifu tu, kwa kuwa ndizo hutoa
kauli ambazo zinaweza kuwa kweli au si kweli. Hivyo ni vigumu kubashiri maana
ya sentensi swalifu na amrishi kwa maswali na amri haviwezi kubainisha ukweli
au si kweli. Vilevile ni vigumu nadharia hii kutumiwa kubainisha ukweli au wigo
wa sentensi tendezi, kwani sentensi tendezi hazielezi matukio. Kwa mfano; Ninakubali
kuwa yeye si jambazi. Katika sentensi hiyo ni vigumu kuamini au kutoamini
ukweli wa kauli hiyo. Sentensi moja au zaidi huweza kuibua seti nyingi za
masharti ukweli hali ambayo huifanya nadharia hii kuwa na mzunguko usiokikomo
katika ufasiri na ufafanuzi wa maana.
Nadharia hii hutegemea zaidi maarifa ya kiulimwengu imani, mielekeo
na tajiriba pana kuhusu kila tungo. Sentensi inayodokeza maarifa ya kiulimwengu
ni ya kijumla kuhusu taaluma mbalimbali kama
vile; maji hayana rangi- itakuwa kweli endapo tu maji hayatakuwa na rangi.
Hivyo basi ukweli huu ni wa kiulimwengu kwa sababu kila mwanajamii anakuwa nao.
Nadharia ya masharti-ukweli hujikita zaidi katika maswala ya taaluma
ya mantiki na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana. Hii ni kwa sababu tu
nadharia hii inajikita zaidi katika kujua maana ya neno. Kwa mfano nini maana
ya kifo na ukweli ni nini. Hivyo basi kutokana na mifano hiyo hapo juu nadharia
hii huenda mbele zaidi na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana.
Nadharia ya utendaji au matumizi ilianzishwa ili kutatua upungufu
uliojitokeza katika nadharia zilizotangulia. Nadharia hii inasema kwamba si
sahihi kuangalia maana ya neno au kisemo kuwa si kitu ambacho kinajitosheleza.
Msisitizo upo wa maana ya neno hupatikana katika utumizi uliotumika, kwani neno
halina maana moja. Mwasisi wa nadharia hii ni Ludwing Wittgenstein, yeye aliona
nadharia hii itatoa upungufu ulijitokeza katika nadharia zilizopita (Matinde,
2012:260). Katika kitabu cha Philosophical
Investigation (1963) anasema ni kosa kubwa kuangalia kama
kitu au kiumbile kamili. Hivyo alipendekeza kuwa maana ya neno iangaliwe kwa
kuzingatia muktadha wa neno au kisemo jinsi kilivyotumika. Kwa maana hiyo maana
au kisemo ni matokeo au athari inayopatikana.
Neno moja huweza kuwa na maana nyingi kutokana na muktadha au
kutokana na matumizi yake. Kwa kuangalia muktadha wa jamii kuna baadhi ya
maneno ambayo huwa na maana katika jamii fulani. Kwa mfano matumizi ya tumsifu
Yesu kristo huendana na muktadha wa ibada au waumini wawili hasa wa kikatoriki.
Usemi huu utakapotumiwa msikitini utazua utata wa imani za kidini.
Pamoja na
ugumu uliopo katika kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia
mbalimbali zilizojadiliwa na wataalamu wengi, kila nadharia ina ubora na
mapungufu yake katika kufasili maana ya maana katika kiwango cha neno na sentensi.
Kwa hiyo maaana ya maana inabaki kuwa dhana telezi kutokana na utata wa kufasili
dhana hii. Ni vema tafiti mbalimbali ziendelee kufanyika ili kuziba pengo
la ugumu wa kufasili maana ya maana.
MAREJEO
Alston, W. P. (1967) Meaning
The Encyclopedia of philosophy, vol 5 Macmillan and
Free press,
PaulEdwards, Editor in Chief,
(pp.233-241), imesomwa tarehe 11/04/2014 saa 22:00
Baron, J. (1972) Semantic Components and Conceptual
development, Elsevier imesomwa tarehe 11/04/2014
saa 22:15
kutoka www.sciencedirect.com/science/article.
Bloomfield, W. L. P. (1983) Language, London
–New york.
Filp, H (2008) What is Semantics, What is Meaning,
imesomwa tarehe 11/04/2014, saa 20:00 kutoka
Habwe, J. na
Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya
Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.
Holm, P. and
Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning
and Different perspective on information System,
Stockholm
University, Marburg.
Lyons, J. (1981) Language; Meaning and Context, Fontana Paperbacks.
Matinde, R. S.
(2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia,
kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,
Serengeti Education publishers (T) LTD,
Mwanza.
Mdee, S. J. na
wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21:
Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne
Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi.
Sengo, T. S. Y.M
(2009) Fasihi za Kinchi, The
Regestered Trustees of Al Amin Education and Research
Academy, Dar es Salaam.
Wamitila, K. W,
(2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia,
Kenya Focus Publications LTD, Nairobi.