FASIHI YA KISWAHILI
FASIHI YA KISWAHILI
SWALI: Je, kuna umviringo wowote katika fasihi ya mwafrika? Kama upo ni katika maeneo yapi? Rejea ujumi katika fasihi mifano yako ijikite Katika mila na desturi za wasafwa na Wanyakyusa.
DONDOO
UTANGULIZI
Ø
Historia fupi ya Wanyakyusa na Wasafwa.
Ø
Dhana
ya umviringo katika Fasihi simulizi.
KIINI
Ø
Maeneo yanayothibitisha uwepo wa umviringo
katika fasihi simulizi ya Wasafwa na Wanyakyusa.
HITIMISHO
MAREJEO
Wanyakyusa ni
kabila linalopatikana nyanda za juu kusini magharibi mwa Tanzania tangu
karne ya 10. Walitokea nchini Malawi
kusini mwa ziwa Nyasa wakijulikana kama
Wangonde. Kutokana na wenyeji waliowakuta (Wasafwa na Wanyamwanga) kuwaita
Wanyasa jina la kabila lao lilibadilka. Waliamua kuboresha jina la kabila lao
(Wanyasa) kwa kuchopeka herufi za kiongozi wao wa kidini (Kyungu) na kuwa
Wanyakyusa (waumini kutoka Nyasa). Kuja kwao katika maeneo ya kabila la Wasafwa
naWanyamwanga kulisababisha kutoelewana nao kwa sababu ya majigambo yao. Hata hivyo, tofauti
zao zilimalizika kwa sababu ya kuungana dhidi ya biashara ya utumwa na Wangoni
ambao waliwavamia wakazi wa mkoa wa Mbeya. Mpaka sasa Wanyakyusa wamechangamana
sana na Wasafwa, Wanyamwanga na makabila
mbalimbali ya Tanzania
kutokana na shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutawala. (www.habarileo.co.tz/index.php.makala/14765-wanyakyusa)
Aidha, Wasafwa
ni wenyeji hasa wa mkoa wa Mbeya mjini na makabila mengine ni wahamiaji tu
kutoka sehemu mbalimbali. Aidha, kutokana na Wahehe kupigwa sana na Wasangu wakisaidiwa na Wajerumani
ambao walipigwa kibabe na katika maeneo ya Lugalo Iringa, ilisababisha Wasafwa
wengi kukimbilia maeneo ya milimani. Jambo hili lilisababisha Wasafwa kuwa
washamba na wachafu pia. Wasafwa wamegawanyika katika makundi mbalimbali
kutegemea na sehemu wanazoishi na ndiyo maana kuna wasafwa wa Ilomba, Mbalizi
na maeneo mengine. Kuongea kwao hutofautiana, wengine huongea kwa kuvuta lakini
wengine kuharakisha lakini wanaelewana wote ni wamoja.
Mviringo ni
dhana inayoturudisha palepale, dhana hii tunaiona katika saa, siku, miezi, miaka
na karne (Kezilahabi, 2002:165). Hivyo, umvirngo katika fasihi simulizi ya Mwafrika
ni hali ya kujirudiarudia kwa tendo au namna ya nyanja za maisha, kiutamaduni, kisiasa
na kijamii. Umviringo huu huenda sanjari na ujumi katika kazi za fasihi
simulizi.
Katika eneo la
utawala au uongozi umviringo unajidhihirisha katika upatikanaji wa viongozi kwa
njia ya kurithishwa. Kurithishwa huku hutokea ndani ya ukoo wa mtawala. Kwa mfano
utawala katika jamii ya Wasafwa ulikuwa kwa muundo wa kichifu. Familia za
kichifu ziliogopwwa sana kiuchawi, na Wasafwa
zamani walikuwa na imani ya uchawi sana.
Pia, kulikuwa na waganga wa miti shamba wa uhakika. Zamani hizo ambapo chifu
Mwanshinga mhamiaji kutoka Ukinga alipofika maeneo ya Wasafwa yeye ndiye
aliyewasha moto kwa mara ya kwanza Usafwani. Pia alikuja na mbegu katika nywele
zake ambazo hakuwahi kuzikata tangu azaliwe. Kutokana na maajabu hayo akatoroshwa
na baba yake na kuhamia Usafwani na ndicho chanzo cha ukoo wa Mwanshinga.
“Umwene
umwinza wuwula wakupapwa ishimwene”
“Chifu mzuri ni yule anayezaliwa kichifu”
Kwa hiyo, katika
kuendeleza uongozi kwa Wasafwa ilibidi mrithi wa chifu atoke ndani ya familia
ya kichifu na awe amezaliwa kichifu, mfano azaliwe akiwa ameota meno.
Vilevile simulizi
za Wanyakyusa zinasisitiza utawala wa mfumo dume. Mwanaume ndiye kichwa cha
familia na ndiye mwenye maamuzi katika familia.
“Wanyakyusa wameshawahi kuwa na kiongozi mwanamke anayefaahamika
kwa jina la Nyanseba.
Inasemekana kuwa kiongozi huyo alijaribu kuweka
utawala wa mfumo jike, lakini hakufanikiwa kwa kuwa alipinduliwa na
wasaidizi wake ambao waliweka dola la mfumo wa utawala wa kifalme” (habarileo.co.tz)
Kwa maana hiyo
umviringo katika uongozi kwa pande za makabila yote mawili unajidhihirisha kwa
kitendo cha kurithishana majukumu kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Dhana ya wakati katika
fasihi simulizi inaonesha umviringo na ujumi katika fasihi. Tunaiona katika
saa, siku na karne. Mfano katika kabila la Wanyakyusa suala la wakati
linatumika katika uvunaji wa mazao (mfunjo) kwa kila mwaka. Kwa mfano mwezi wa
pili, tatu na nne ni kipindi cha mavuno ya mahindi ambacho kila mwaka
kinajirudia. Kuanzia mwezi wa saba na wa nane ni kipindi cha mavuno ya maharage
ambapo kipindi hiki hujirudia kwa kila mwaka. Hivyo dhana ya wakati ilikuwa
inatumika kwa mtindo huo na inajidhihirisha kuwa ni mviringo kwa kuwa kila
mwaka vipindi hivi hujirudiarudia.
Aidha, kumteua
mchumba ni eneo mojawapo linaloonekana kuwepo kwa umviringo. Tamaduni za Kiafrika
zinasisitiza kuoa au kuolewa na mtu wa kabila au dini moja. Kwa hiyo basi
utamaduni huu upo hata kwa makabila ya Wanykyusa na Wasafwa kwani vijana
husisitizwa kuoa au kuolewa miongoni mwa makabila yao wenyewe. Pia, hata wachumba huweza
kuchaguliwa na wazazi wao lakini huteuliwa miongoni mwa makabila yao yaani Wanyakyusa au
Wasafwa. Malengo ya kufanya hivi ni kulinda utamaduni na kuzuia magonjwa ya
kurithishwa.
“Tamaduni tofauti zimeangalia namana ya
kutafuta wachumba au kuoa au
kuolewa. Baadhi ya jamii uchaguzi wa
wachumba hufanywa na wazazi hii
inaweza kufanyika hata kabla ya kuzaliwa kwa mtoto”
(Mbiti, 1971:135).
Pia, majina katika
kabila la Wanyakyusa na Wasafwa huwa na desturi ya kurithishwa kutoka mtu mmoja
hadi mwingine. Imani yao ni kwamba mtu wa makamo
jina lake hupewa mtoto mchanga azaliwaye kwa
madhumuni ya kwamba tabia alizonazo mtu huyo wa makamo ambazo kwa mategemeo ya
wengi ni zile nzuri hurithiwa na mtoto mchanga aliyezaliwa. Kwa mfano kama jina
la ukoo ni Mwakalindile mtumiaji wa jina hilo
hurithishwa kwa wajukuu wa kiume ambapo atabakia kuitwa Mwakalindile wakati
mtoto wa kike atachukua au atarithi jina la bibi yake.
Kifo na mazishi
ni matukio ambayo yalikuwepo tangu zamani. Kiutamaduni wasafwa walimwogesha
marehemu na kumkalisha kwenye kiti kabla ya kucheza ngoma ya msibani. Iwapo
mtoto wa kwanza katika familia amefariki maiti huzikwa kwa babu mzaa mama,
mtotowa pili akifariki huzikwa kwa babu mzaa baba, mtoto watatu na kuendelea
ndio mali
ya wazazi husika hivyo ilikuwa ni lazima kuzaa watoto zaidi ya watatu ilifamilia
changa ipate mtoto wao.
Mfano wa kaburi la Wasafwa likiwa
katika umbo la duara ndani ya kaburi la pembe nne.
Sambamba na
mzishi haya kufuata mila na desturi za maumbo ya makaburi, kabila la Wasafya
hutumia kakavu (tarumbeta) kutoa taarifa kwa wanajamii ili waweze kujua kuwa
kuna msiba kijijini.
Mfano wa picha
ya kakavu (tarumbeta) itumikayo kutoa taarifa ya msiba ikiwa
begani kwa mtu wa pili kutoka kulia.
Tukio hili lilijulisha jamii nzima kuhudhuria
msiba nyumbani kwa marehemu ambapo marehemu alizikwa nyuma ya nyumba.
Mfano wa
picha ya mazishi yanayofanyika nyuma ya nyumba
Pia, Wanyakyusa
wanadesturi ya kumwogesha marehemu kabla ya kumzika. Uwepo wa vipengele
vinavyofanana hadi leo kunadokeza umviringo katika Fasihi simulisi zao.
Kwa upande wa
kuzika Wanyakyusa walifanya ibada za kimila zikiambatana na matumizi ya unyuso nguo za kufunika maiti. Jambo hili
linafanyika hadi leo na nguo hizo ni maarufu kwa jina la sanda.
“Marehemu walifungwa nguo
iliyotengenezwa kwa magome ya miti
Inayojulikana kwa jina la unyuso.
Nguo hiyo ilitumika
kumfunika
marehemu mithili ya sanda kisha
aliwekwa kwenye shimo la duara
Maumbo ya mashimo ya kuzikia kwa Wanyakyusa
yanadokeza umviringo katika fasihi simulizi japo siku hizi taratibu hizi
zinadorora siku hadi siku.
Kipengele cha imani na dini nacho kinagusia
umviringo katika Fasihi simulizi ya Wanyakyusa na Wasafwa. Kwa asili watu hawa
walikuwa na dini na imani zao za asili walisali katika miti mikubwa, mito na
makaburini kama njia ya kutatua matatizo yaliyowasonga. Kuingia kwa wamisionari
wa kwanza mnamo mwaka 1892 wakiongozwa na Merensky na Nauhans wakiwa na madhehebu
ya misheni ya Berlin kulianza kuwabadilisha imani zao hata kabla ya kuja
wamisionari wa Morovian (www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa).
Hata hivyo, wabantu hawa wanapokubwa na matatizo
makubwa kama magonjwa, vifo na magonjwa mengine ambayo hushindikana kutatuliwa
kanisani huamua kwenda kwa waganga wa jadi (Tembels, 1959:13). Pia Wasafwa na
Wanyakyusa wa sasa bado wanaamini waganga wa jadi licha ya kuokoka. Hili
linajidhihilisha wazi kwa jinsi kipindi cha Dr.Mlingolingo kinavyopata wapenzi
wengi katika radio Generation FM. Mlingolingo hupokea simu za watu wengi hasa
waishio mkoa wa Mbeya licha ya kuwepo kwa makanisa mengi. Dodoso za mganga huyu
kwa njia ya simu hudokeza jinsi watu hawa walivyoshindikana katika maombi
kanisani huamua kutaka msaada kutoka kwake. Aidha maeneo waliko na majina yao
yanadokeza kuwa wapenzi wa kipindi hiki ni Wanyakyusa na Wasafwa hata
waliobatizwa na kuokoka.
Vilevile kipengele cha ngoma za Wanyakyusa na
Wasafwa kinaonesha ujumi wa duara. Jambo hili linadhihirishwa na jinsi ngoma
zao zilivyo na zinavyochezwa. Wanyakyusa wanacheza ngoma za asili ambazo
hujulikana Kama Ipenenga na Miparano. Mara nyingi Ipenenga huchezwa na wazee au
machifu wa ukoo na huvalia vizuri na kucheza kwa umakini. Miparano huchezwa
katika kufurahia mavuno yao. Jambo la msingi hapa ni mkao wao na vifaa wanavyotumia
wakati wa mchezo ambavyo hutengenezewa dhana ya mduara. Wachezaji hushika
mkongojo na kucheza kwaduara (www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa).
Kwa upande wa Wasafwa kuna ngoma zao zinazoitwa
Mbeta, Ndingala, Mwadede na Bidubidu. Ngoma hizi mara nyingi zilichezwa wakati
wa mavuno na mara chache wakati wa msiba (mwengulo) wa watu maarufu. Hata hivyo,
zimepungua kasi kutokana na mwingiliano wa tamaduni na dhana kuwa kuchezwa
kwake katika mwengulo kunazidisha haja ya kulogana ili watu wapate kula na
kunywa. Jinsi wanavyocheza na vifaa wanavyotumia hudhihirisha mduara katika
ngoma. Mwashinga (2012) anasema:
“mguuni kunavaliwa njuga za chuma za
duara (INSAHALA) ambazo
zinagonganishwa kwa kufuata mlio wa pembe
zinazokuwa zinapigwa
na wanaume na kuleta mziki mzuri. Pembe hizo ndiyo jina lenyewe
la ngoma yaani MBETA.”
Mila ya utani imeenea sana kwa Waafrika. Watu
wanavyokutana hutanina kwa maneno na vitendo huku wakizingatia masharti
yanayotawala uhusiano wa utani huo. Waafrika hutaniana baina ya mtu mmoja na
mwingine au kabila moja na kabila jingine. Kwa mfano Wanyakyusa wanataniana
baina ya babu na mjukuu wake, bibi na mjukuu wake, pia mashemeji. Aidha, Wanyakyusa
huweza kutaniana na Wahehe huku masharti ya uhusiano wa utani yakizingatiwa.
Utani huu hujirudiarudia kwa kurithishwa katika jamii zao. Hivyo kufanya ujumi
wa mviringo katika fasihi simulizi ya Kiafrika.
Desturi ya kula chakula kwa waafrika inatetea ujumi
katika mviringo. Waafrika huwa na mila na desturi za kula chakula kwa kuzunguka
mahali palipo na chombo cha chakula. Mfano kabila la Wanyakyusa ambao hula
chakula chao maarufu msibani (kande) kwa kuweka katika sinia na watu
wanalizunguka wakila kwa kutumia majani ya mgomba ambayo huitwa ndundu. Pia, hunawa maji katika chombo
kimoja, baba huanza na watoto wa kiume hufuata. Baadaye mama hufuatiwa na
watoto wa kike. Watu hula chakula kwa kutumia chombo kiitwacho lwangabya
(sinia). Tendo lile la kunawa hujirudia tena kuanzia baba, mtoto wa kiume, mama
na baadaye watoto wa kike. Hivyo basi kujirudia kwa tendo hilo la kunawa kabla
ya kula chakula na namna ya ukaaji wakati wa kula kunadhihirisha umviringo wa fasihi
simulizi ya Mwaafrika.
Aidha, Wasafwa katika desturi ya kula hutumia
baadhi ya vyombo kama vile chungu kikubwa (usuyi).
Chungu hiki hutumika kutekea na kutunzia maji na kuwekea pombe pia. Ungo (uveto) uliotengenezwa kwa majani na kamba
za porini zinazoufanya uwe imara zaidi. Vifaa hivi hutumika kulia chakula na
umbo lake huwa la mviringo na kusadifu ujumi wa mviringo katika fasihi ya
Kiafrika.
Maumbo ya vitu katika fasihi ya kiafrika
yanadhihirisha uwepo wa umviringo. Kutokana na umbo hilo la mviringo jamii za
kiafrika ziliamini kuwa umbo hilo ni zuri. Kwa kuangalia jamii za Kinyakyusa na
Kisafwa kuna vitu vyao vingi ambavyo vina umbo la mviringo. Kwa upande wa jamii
ya Wanyakyusa kuna vifaa vyao vingi vya umbo la duara kama:
Kiswahili Kinyakyusa Matumizi
Ungo uluseko
kupepetea
Chungu
Syala/videko kutunzia
nafaka na kupikia
Kigoda ikikota kukalia
Kibuyu ulupale
kutunzia maziwa
Jiwe
la kusagia ukwala
kusagia nafaka nafaka
Kata ingata kujitwishia
mzigo na kukalishia
vyungu vya nafaka
Mfano wa picha ya
kigoda katika kabila la Wanyakyusa (ikikota)
Mfano wa
picha ya chungu (ndeko) kwa kabila la Wanyakyusa
Aidha vitu
vyenye umbo la mviringo hupatikana pia katika jamii ya Wasafwa ambapo baadhi ya
vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:
Kiswahili Kisafwa matumizi
Chungu usayi kutunzia na kutekea maji na kuwekea pombe
Ungo
uveto kupepetea
Kikapu ishitundu kuwekea
vitu mbalimbali
Kikombe upandi kunywa
maji au pombe
Hata nyumba za
kale za Wanyakyusa zilikuwa za mduara ambapo chifu alijengewa (isyenge) na nyumba za wake zilijegwa
pembeni kuzunguka nyumba ya chifu. Pia kwa upande wa Wasafwa nao walikuwa na
nyumba zao ambazo ziliitwa isonze
ambazo pia zilijegwa kwa umbo la duara.
Mfano wa picha ya msonge (insyenge) kwa Wanyakyusa, (insonze)
kwa Wasafwa
Vitu vyote hapo
juu kwa makabila yote vina umbo la umviringo na viliandaliwa kwa umbo hilo kwa kuwa ndilo umbo
lililoaminiwa na waafrika kuwa ni zuri.
Aidha umviringo
katika kazi za fasihi za Kiafrika inaonekana pia katika nyimbo mbalimbali
ambazo zinaweza kuimbwa msibani au kwenye sherehe mfano harusi na ngoma. Katika
kutekeleza utanzu huu wa fasihi umviringo hujidhihilisha kwa kuwa nyimbo hizo
hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mfano katika kabila la
Wanyakyusa mara nyingi sehemu za sherehe huimbwa wimbo ufuatao:
“lelelele amba
Ujo
tubhapele umwana
Amba lelelele…amba
Mungu nkomagha
Amba lelelele…amba
Mungu mfyundagha
Amba lelele…amba
Tafsiri yake.
Mtoto
huyo tumewapa
Ambaa…lelele
Msimpige
Ambaa…lelele
Msimfinye
Ambaa.lelele
Umviringo pia
hujidhihirisha kwa upande wa nyimbo za Wasafwa. Mavazi yao huonekana hadi wakati huu kutokana na
baadhi ya Wasafwa kuendeleza tamaduni hizo kwa mfano; kuvaa kitambaa
kilichorembwa shanga (Igoyi), mguuni
kuvaliwa njuga za chuma za duara (Insahala), kupuliza pembe (Mbeta).
Kuna vifaa
mbalimbali vinavyotumika katika kufanya matambiko kwa kabila la Wanyakyusa
ambapo hufanyika kama kuna tatizo limetokea kama
vile njaa, ukame na magonjwa. Mfano wa vifaa hivyo ni pamoja na vibuyu (kata), moto, ndizi na pombe. Jamii ya
Wanyakyusa ilitumia moto kama kifaa cha tambiko
katika kuomba Mungu wao. Moto huu ulikokwa na chifu wakati wa kutambika na mara
baada ya majibu mazuri ya maombi yao,
walichukua moto huo na kurudi nao kijijini. Huko uliandaliwa moto mwingine
nyumbani kwa chifu ambao ulitumiwa na wanakijiji wote kuwasha moto huo kama ishara ya kufurahia kutii maombi waliyojibiwa na
miungu wao. Umviringo unaozungumziwa hapa ni moto unapozungushwa toka nyumba
moja hadi nyingine.
Sambamba na hilo matumizi ya vibuyu
(kata) vilivyotumika kunywea pombe wakati wa tambiko vilikuwa na umbo la duara
na hata wakati wa kunywa pombe hizo walikaa mkao wa duara. Kwa upande wa
Wasafwa ibada za matambiko zilifanyika kuendana na tukio lililoikumba jamii
hiyo. Mfano wa matukio hayo ni njaa, ukame na magonjwa katika jamii. Kuhusu
suala la ukame chifu (mwene) wa
Wasafwa aliwaita wafuasi wake kujadili namna ya kulitatua tatizo hilo, wakati mwingine
kulikuwako na watu waliosadika kwamba walitumiwa na mizimu kuleta taarifa juu
ya jamii fulani.
“mzimu (izimu) ni watu ambao walikufa ambao inasadikika
kwamba
nafsi zao zinarudi kwa kupitia mwili au
ufahamu wa mtu mwingine
na kutoa ujumbe kwa ndugu zao ambao wako hai
bado” (Mwasinga, 2011:20)
Katika suala
hili umviringo unajidhihirisha pale ambapo nafsi ya mtu aliyekufa kurudi kwa
aliye hai.
Usimuliaji wa
hadidhi upo katika hali ya umviringo hasa katika maeneo mbalimbali. Hadidhi
hurithiwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine, hasa kutoka kwa watu
wakubwa kwenda kwa watoto. Pia eneo la hadithi na mtindo wa ukaaji ni wa
mviringo kwani hadithi husimuliwa wakati wa jioni wakiwa wameuzunguka moto kwa
umbo la duara jambo hili hufanyika ili kumsaidia kila mtoto kushiriki katika
usimulizi wa hadithi hizo. Mfano hadithi ya Kinyakyusa huadithiwa kama ifuatavyo:
“Kapango kapango:
Ijolo alipo bhabha jumo alinumwana unyambala
bho akulile kafikile akabhlilo ka
kwegha, bhabha ghwake alimbulile ukuti atikulondighwa ukwegha kutali,(ikikolokyapanja)ghwegheghe
unyakyusa,lelo umwene akanile ukwegha unyakyusa abhukile ikikolo kyapanja,
bhoafikile munjila alimwaghile undindwana jumo bhalina mama ghwake pasi pa
mpiki pakaja pa myabho.Alinganile nukulonda ukumwegha,bho alalusisye ifyuma,
mama jula atile ungasosya ufyuma nafimo loli kumpimba mpaka kumyenu. Loli
bhobhafikile munjila undindwana jula akanile ukusuluka alyandile ukwimba”
“ Ghwali nyeghile kumyitu x2
ikisu kya kutukuju kumyetu kula kula x2”
Pitasi
unyambala jula alambalele nu ndindwana jula pa nyuma ngimba akalimundu lyali
setano. Lyali ngoghile nukwega ubhula bhwake, undumyana jula alinkwenda nu
kufwa.
Tafsiri yake kwa
lugha ya Kiswahili;
Hadith hadithi:
Hapo zamani za kale palikuwepo na baba mmoja
aliyekuwa na mtoto wa kiume. Alipofikia umri wa kuoa baba yake alimwonya kuwa
sheria ya Kinyakyusa hairuhusu kuoa nje ya kabila lao lakini yeye alikataa
akaondoka kwenda nje ya kabila lake. Alipofika njiani alimkuta binti mmoja na
mama yake wakiwa chini ya mti nyumbani kwao. Akampenda yule binti na kuridhia
kumuoa. Alipouliza kuhusu mahali yule mama akasema asitoe kitu chochote ila
kumbeba hadi nyumbani kwake. Lakini walipofika nyumbani yule binti alikataa
kushuka na kuanza kuimba.
“ulinitoa
kwetu x2
Kaniweke
kwangu mji wa Tukuyu, kule kwetu kule x2
Kijana yule baadaye aliamua kulala huku
binti akiwa mgongoni. Kumbe hakuwa binti bali ni jini likamuua kwa kumtoa
utumbo na ikawa mwisho wa maisha ya yule kijana.
Pia michezo ya
watoto hudhihirisha ujumi katika umviringo wa fasihi simulizi ya Mwafrika. Watoto
hucheza michezo mbalimbali kifamilia au kwa kukutana na makundi ya familia
nyingine. Mfano mzuri ni mchezo ujulikanao kama
Azyungule katika kabila la Wasafa, wachezaji
hucheza kwa duara. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kwa mahojiano
tuliyoyafanya na mzee wa Kisafwa Ndele Mengo anayepatikana katika kijiji cha
Nzenga kitongoji cha Mbogo, mara nyingi michezo hii hufanyika usiku. Watoto
hukusanyika kabla ya chakula cha usiku na kuimba nyimbo mbalimbali huku
wakizungukazunguka. Mambo haya yamekuwa yakifanyika tangu zamani hadi sasa. Kwa
hiyo umviringo katika fasihi simulizi ya kisafwa inajidhihirisha katika mduara unaotokeza
katika michezo yao.
Kwa upande wa
wanyakyusa kuna michezo mbalimbali ya watoto. Watoto hucheza michezo hiyo hasa
wanapokuwa hawanashughuli za kufanya.baadhi ya michezo hiyo ni “salo” (mdako) na “kubhasabhasa” au “kudumbadumba”.
Namna na vifaa wanavyochezea hudokeza umviringo kwani mashimo ya kuchezea huwa
ya duara. Pia, michezo hii bado infanyika hadi leo. Mahojiano yaliyofanyika
wakati wa kukusanya data yalidokeza kuwa watoto hucheza mdako kwa kushindana
ili kujua ni nani anayeweza kupangua kete huku akidaka nyingine.
Aidha, michezo
hii inakuza fikra za watoto na uwezo wa kutenda mambo mengi kwa wakati
mmoja.Michezo hii bado ipo hadi sasa hasa kijijini japo kuna michezo mingine
inapungua umaarufu kutokana na maingiliano ya tamaduni na utandawazi.
Kwa upande wa
Wasafwa elimu ya jando na unyago ilitolewa kwa watoto wa kiume na wa kike.
Binti wa Kisafwa baada ya kuvunja ungo aliwekewa ndani peke yake. Ilikuwa ishara
inayoonesha kuwa binti akiwa katika siku zake haruhusiwi kupika wala kushiriki
na mwenzake katika kazi yoyote ile. Mafunzo yaliyotolewa unyagoni ni pamoja na
kufanya kazi kwa bidii, mfano kuchota maji, kutafuta kuni porini na kulima. Ila
tohara kwa Wasafwa haikuwepo. Hivyo suala hili la jando na unyago linaendelea
katika baadhi yakoo na familia chache ambazo ndizo zinazoendelea na suala hili.
Pia kwa upande wa kijana wa Kisafwa mara tu baada ya kubalehe naye huanza kupewa
mafunzo ya jando. Akiwa mafunzoni alifundishwa namna ya kujitengemea kama vile kujijengea kinyumba chache (invanza), kuanza kwenda kwenye magita na
huko ndiko anaweza akapata mchumba. Suala la tohara kwa kijana wa Kisafwa halikuwepo,
lakini baada ya kuanza kujichanganya na makabila mbalimbali limeenea sana kwa watu wote. Hivyo
basi kuwepo kwa jando na unyago kunadhihirisha kabisa uwepo wa umviringo wa fasihi
simulizi ya Mwafrika.
Suala la
matumizi ya lugha katika fasihi za kiafrika ndani yake kuna umviringo ingawa
kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia jamii hulazimika kubuni
misamiati mipya ili kukidhi mahitaji yao
na kuendeleza mawasiliano. Hata hivyo kuna baadhi ya vipengele vya lugha bado
vinaendelea kuwa hai hadi sasa, mfano wa vipengele hivyo kwa upande wa
wanyakyusa ni;
Vitendawili,
mfano i . Inguku jangu jitelile mmifwa (ikinanasi)
Tafsili yake : kuku wangu
katagia mibani (nanasi)
Mfano ii. Kunokununu
pakati pakali na kuno kununu (isuba)
Tafsili yake : huku
kutamu katikati pachungu na mwisho patamu (jua)
Nahau ni kauli
zilizojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini zinatoa maana isiyo ya
kawaida. Mfano i. kinyakyusa: ali
mumbabhu
Kiswahili: yuko kwenye
kuni
Maana yake yuko kwenye siku zake/ yuko mwezini
Mfano ii. Kinyakyusa: Ali na masusu
pammilo
Kiwsahili: Ana mavi ya kuku kooni
Maana yake ni
binti mdogo asiyeelewa kitu.
Methali nazo
huonesha wazi umviringo kwa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine, mfano
wa methali ni;
i. Kinyakyusa: Imbwele ndukama
Kiswahili : Inzi kwenye maziwa
Maana yake: Mtu kuingilia jambo
lisilomuhusu
ii.kinyakyusa : Ingongobe jangu
nduluka jikukolela bho bhukali
Kiswahili : Jogoo wangu anawika kabla ya wakati
Maana yake ni kusherehekea
kabla ya mafanikio.
Aidha kwa upande
wa Wasafwa kumekuwa na umviringo katika matumizi ya lugha kwa kuendelea kutumia
baadhi ya vipengele japokuwa kuna mabadiliko na maboresho kwa baadhi ya
vipengele vya lugha. Mfano wa vipengele vya lugha ambavyo vina umviringo ni;
vitendawili, nahau, misemo na methali. Mfano wa misemo Kisafwa: hwasha hwalenga
(kumekucha)
Nkulembela
zitonela enyau (ukizubaa wajanja watachukua nafasi)
Kwa kuchunguza
vipengele vyote vya lugha vilivyofafanuliwa hapo juu ni wazi kuwa umviringo
unapatikana kwani kizazi kipya hupata tanzu hizo kwa kurithishwa kizazi kimoja
hadi kizazi kingine.
Umviringo katika
fasihi za kiafrika hujionesha pia katika maleba/mavazi yanayotumika katika
utambaji wa baadhi ya tanzu za fasihi simulizi. Ukweli wa jambo hili unajibainisha
kwa kutumia kabila la Wanyakyusa na Wasafwa. Kwa upande wa Wanyakyusa kwa
kawaida katika uchezaji wa ngoma kuna vifaa kama
vile; njuga, mkia wa fisi, mkwiju, filimbi, kaptura na shati jeupe, ngoma za
asili.
Aidha kwa upande
wa kabila la kisafwa kuna matumizi ya maleba pia ambayo nao huyatumia katika
uchezaji wa ngoma. Mfano wa malena
hayo ni: njuga, malimba, filimbi na ngoma. Hivyo katika eneo hili umviringo
unajitokeza kwa kuwa vifaa hivyo bado vinatumika hadi sasa ingawa kumekuwa na
maboresho kidogo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa mfano
badala ya kutumia ngoma za asili kwa sasa huweza kutengeneza muziki kwa kutumia
kinakilishi na nyimbo nazo hurekodiwa kwenye vinasa sauti na kanda.
Kupambana na
mfumo dume nako hudokeza umviringo katika fasihi simulizi za Wasafwa na
Wanyakyusa. Kihistoria, Wanyakyusa wamekuwa wakipambana na mfumo dume tangu
zamani hasa kupitia kipengele cha majina. Watoto wa kiume hurithi majina ya
upande wa ma mfumo mama ilihali watoto wa kike hurithi majina ya upande wa baba
zao. Simulizi zinamtaja mwanamke ( Nyaseba) aliyewahi kujaribu kuweka mfumo
jike, suala hili bado linajitokeza hadi leo japo limekuwa changamani. Siku hizi
wanawake wa Kinyakyusa na Kisafwa wanapambana na mfumo dume kupitia asasi
mbalimbali zinazotetea wanawake nchini na ulimwenguni kwa ujumla. Uchunguzi
uliofanywa na gazeti la Habarileo gwiji la habari linataja juhudi hizi:
……… wanawake wa kinyakyusa wanaungana na
wanawake
ulimwenguni kote kukabiliana na
changamoto ykubwa ya mfumo
dume na
kujenga mfumo unaozingatia haki na usawa hasa katika
upatikanaji wa elimu, haki ya kumiliki
ardhi, mali na kushika
Kwa kuhitimisha,
suala la umviringo katika fasihi simulizi ya kiafrika huweza kujitokeza katika makabila
mbalimbali ya Tanzania
na Afrika kwa ujumla. Hivyo basi si makabila ya Wasafwa na Wanyakyusa tu ambapo
umviringo huweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali. Haa hivyo, kutokana na
kuingia kwa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia suala hili la
umviringo limeanza kupungua siku hadi siku.
MAREJEO
Kezilahabi ,
E.(2002), Makala ya Nadharia ya Fasihi Simulizi na Maendeleo katika Sayansi na
Teknolojia, TUKI, Dar es salaam.
Mbiti, J. S.
(1971), African Religions and philosophy,
Heinemann Educational Book Ltd, Nairobi.
Msokile, M.
(1992), Misingi ya Hadithi Fupi, Dar
es Salaam University Press, Dar es Salaam.
Mwanshinga, S. P.
(2012), Wajue Wasafwa Kutoka Mbeya.
Ngure, A.
(2006), Fasihi Simulizi Kwa Shule Za
Sekondari, Phoenex publishers Ltd, Nairobi.
Tembles, P. (1954),
BantuPhilosophy, Presence Afrcaine Kutoka
www.aequtoria.be/temples/BiblioDetemplesEnglish.html.
16.10.2013 saa 15:00
www.sw.wikipedia.org/wiki/fasihisimulizi, 16.10.2013 saa 15:00