DHANA YA MOFU NA AINA ZAKE

 DHANA YA MOFU NA AINA ZAKE
TUKI(1990), katika Dafina ya Lugha wanasema kuwa, “Mofu ni kipashio cha isimu maumbo kiwakilishacho mofimu”.
Massamba (2004), katika Dafina ya Lugha anasema , Mofu ni kipashio cha kimaumbo ambacho huwakilisha mofimu.
Kwa mujibu wa Nida (1949), wanasema, Mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo huthihirika kifonolojia na kiothografia.
Mofu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana katika lugha.Mofu hawezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi bila kuharibu maana yake. Mofu huwakilisha maana za kileksika na zile za kisarufi. (Platt,1985).
Kwa ujumla, Mofu ni kipashio cha kimofolojia ambacho husitiri maana za mofimu katika lugha na huweza kudhihilika kifonolojia zinapotamkwa na kiothografia zinapoandikwa katika lugha.
Mofu huainishwa kwa kuzingatia vigezo viwili; Kigezo cha maana zinazowakilishwa na mofu na Kigezo cha mofolojia ya mofu.
Tunapotumia kigezo cha maana zinazowakilishwa na mofu, tunapata aina tatu za mofu, yaani; mofu huru/sahili, mofu funge na mofu tata, kwa upande mwingine tunapotumia kigezo cha mofolojia au maumbo ya mofu zenyewe tunapata aina mbili za mofu, yaani; mofu changamano na mofu kapa. Hivyo, kwa kuanza na kigezo cha maana zifuatazo ni aina za mofu;
 Mofu huru/sahili; Mofu huru ni zile mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yenye maana inayoweza kueleweka bila kusaidiwa na mofu nyingine. Aghalabu, mifano mingi ya mofu huru hupatikana kutoka kwenye vipashio vya lugha, kama ifuatavyo:
-Nomino:  {baba}, {kuku}, {sungura}, {ndege}, {dada}, {paka}.
-Vivumishi: {safi}, {baya}, {dhaifu}, {zuri}, {imara}, {hodari}.
-Viwakilishi:{mimi}, {sisi}, {wewe}, {ninyi}, {yeye), {wao}.
-Vielezi:  {upesi}, {haraka}, {sana}, {leo}, {jana}, {juzi}.
-Vitenzi: {tafiti}, {samehe}, {arifu}, {sali}, {jibu}, {badili}.
-Viunganishi:{na},{halafu}, {bado}, {ila}, {aidha},{pia}.
Kwa hiyo, Kiswahili kinazo mofu huru/sahili nyingi ambazo zimo katika aina karibu zote za maneno(vipashio) za lugha. Hivyo, mofu huru ni mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yanayoeleweka bila kusaidiwa na viambishi.
 Mofu funge/tegemezi; Mofu funge au Mofu tegemezi ni mofu ambayo haiwezi kutumiwa peke yake kama neno lililo na maana yake kamili; aghalabu mofu funge hutumiwa kama kiambishi tu kinachoambatanishwa na mzizi au viambishi vingine ili kulikamilisha neno husika. Mofu funge ina sifa zake ambazo ni pamoja na;
-Mofu funge haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili.
-Mofu funge ni lazima iambatanishwe na angalau mafu nyingine moja ndipo tupate neno
kamili. 
Mifano ya Mofu funge/tegemezi ni kama ifuatayo;
Idadi ya Umoja       Idadi ya Uwingi
m-toto (m)                 wa-toto (wa)
ki-su (ki)                    vi-su (vi)
m-ti (m)                      mi-ti (mi)
Ukumbwa wa Nomino        Udogo wa Nomino
ji-tu (ji)                                  ki-ji-tu (ki)
ji-su (ji)                                  ki-ji-su (ki)
Maana za mofu funge hutegemea sana muktadha wa mofu husika. Mofu funge ikiondolewa kwenye muktadha wake hukosa maana na ni vigumu kujua maana yake bila kuiweka katika muktadha wa neno. Mofu funge inaponing’inizwa peke yake haituwezeshi hata kidogo kujua maana yake. Umbo moja linaweza kuwa na maana nyingi kwa mujibu wa miktadha ambamo imeambatanishwa katika mzizi wa neno.
Aghalabu, mofu funge ni sawa na viambishi vya mizizi mbalimbali katika neno. Hii ina maana kwamba viambishi vilivyo vingi katika lugha huwa ni mofu funge. Tunasema viambishi vingi kwa sababu si viambishi vyote ambavyo huundwa kwa mofu funge.Yapo maneno mengine ambayo ni mofu huru. Baadhi ya mizizi ya maneno pia huwa ni ya mofu funge kwa sababu mizizi hiyo huwa haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili. Mifano mizuri ya mizizi ya maneno ya Kiswahili ambayo huundwa kwa mofu funge ni ile ya vitenzi vya silabi moja moja,kama ifuatavyo:
Mfano (i): Mizizi ya maneno yenye silabi moja.
Mofu funge               Neno                   
{-l-}             kula 
{-f-} kufa
{-nyw-}       kunywa   
(ii): Mizizi ya maneno yenye silabi nyingi.
Mofu funge Neno
{-chez-} cheza
{-lim-} lima
{-sem-} sema
 Mofu Tata ,Mofu tata ni mofu ambazo huwa na maana zaidi ya moja au kuanzia mbili na kuendelea. Mfano, Ntomoka alimpigia Malamla mpira.
Sentensi hii ni tata kwa sababu ina maana zaidi ya moja.  Utata wa sentensi hii haupo kwenye muundo wake wa kisarufi, bali upo katika kitenzi alimpigia.  Kitenzi hiki kina mofu sita, yaani:
{a-} + {-li-}  + {-m-} + {-pig-} +  {-i-}   + {-a}
   1           2             3            4             5           6
Kati ya mofu hizi zote sita, mofu ya tano {-i-} ndiyo yenye utata. Mofu {i} ni mofu ya kutendea kwa sababu tukisema: ‘Ntomoka alimpigia Malamla mpira’, maana zinazoweza kueleweka na wasikilizaji ni nne:
 (a)   Ntomoka aliupiga mpira kwa niaba ya Malamla; yaani Malamla ndiye aliyetakiwa aupige mpira ule, lakini kwa sababu ambazo hazikuelezwa, badala ya Malamla kuupiga mpira ule, Ntomoka akaupiga.
(b)    Ntomoka aliupiga mpira kuelekea kwa Malamla; yaani Ntomoka na Malamla walikuwa wakicheza mpira. Ikapatikana fursa, Ntomoka akaupiga mpira ule kuelekea kwa Malamla. Kwa hiyo, hapa tunazungumzia mwelekeo wa mpira.
(c)    Ntomoka alimpiga Malamla kwa kuutumia mpira; yaani, Ntomoka anautumia mpira kama ala (silaha) ya kumpigia Malamla.
  (d)  Ntomoka alimpiga Malamla kwa sababu ya mpira; yaani hapa, mpira ndio sababu kubwa ya Ntomoka kumpiga Malamla. Tuseme labda Ntomoka alikuwa na mpira wake, halafu Malamka akauchukuwa kuuchezea na kwa bahati mbaya akaupoteza. Ntomoka anapogundua kwamba Malamla ameupoteza mpira wake, basi ndipo akampiga.
Kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba sentensi yetu ina utata kwa kuwa inatupatia maana tofauti tofauti zipatazo nne ambazo zimesababishwa na mofu {-i-} ya kutendea.
Kwa kutumia kigezo cha mofolojia au maumbo ya mofu zenyewe, zifuatazo ni aina za mofu;
Mofu Changamani; Mofu changamani ni mofu ambazo huundwa kwa kuweka pamoja angalau mofu huru mbili au mofu funge na mofu huru na kuunda neno lenye kuleta maana kamili, kwa mfano:
Mofu huru + Mofu huru
- {fundi}  +  {chuma} = fundichuma.                     
- {gari} +  {moshi} =  garimoshi.
Mofu funge + Mofu huru
-{mw} + {ana} + nchi = mwananchi. 
  • {ki} + {ona} + mbali = kionambali.
Mofu Kapa; Mofu kapa ni mofu za pekee ambazo hazina umbo. Mofu kapa hazitamkwi wala kuandikwa. Mofu kapa hazionekani katika neno, lakini athari zinazotokana na hiyo mofu kapa husika hueleweka. Ingawa mofu hizi huwa hatuzioni wala kuzitamka au kuziandika, lakini maana zake tunazipata. Nomino za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali kulingana na maumbo yake ya umoja na wingi kama ifuatavyo;
=Nomino zilizo na kiambishi awali cha umoja tu, cha wingi ni kapa  (ø)
Mfano:          
            Umoja                        Wingi
- kuta                       ø - kuta
            - funguo                  ø - funguo
            – kucha                    ø- kucha.
        
- Nomino zilizo na kiambishi cha wingi tu, cha umoja ni kapa  (ø)
Mfano:
            Umoja                        Wingi
           ø -kasha                 ma – kasha.
           ø -debe                    ma – debe.
ø-jembe                 ma – jembe
-Nomino zisizo na kiambishi cha umbo la umoja wala wingi.(ø)
Mfano;
Umoja Wingi
ø -mama ø-mama
ø-mbuzi ø-mbuzi
ø-manukato ø-manukato
 Sherehe kuhusu mofu kapa.Kinachotokea hapa ni kwamba ukisema ukucha watu wanaelewa kuwa ni ukucha mmoja tu. Lakini ukisema kucha,  watu wataelewa kuwa ni kucha nyingi.Na hali hii ndivyo ilivyo kwa maneno ufunguo – funguo, ukuta - kuta, inajulikana kuwa ni ufunguo mmoja tu na akisema funguo, ni kwa maana ya wingi lakini umbo  lenyewe linaloileta hiyo maana ya wingi halionekani bayana katika neno.
Ili kuyaeleza haya maumbo ambayo hayapo lakini maana zinazowakilishwa na maumbo hayo zipo, Wanaisimu wamekubaliana kuyaita maumbo  haya kapa, yaani mofu ambazo hazipo. Mofu hizi ni   dhahania tu katika akili zetu kwa kufahamu tu kwamba maana fulani haiwezi kuja tu yenyewe lazima iletwe na mofu fulani. Kwa hivyo, hata kama mofu hiyo haionekani, lakini ipo ni mofu-kapa.
Kwa kuhitimisha, mofu ni umbo muhimu sana katika lugha kwani kupitia maumbo haya ndipo tunaweza kuelewa maana mbalimbali za vitamkwa katika neno kidhahania yaani mofimu, hata mzizi pia ni mofu. Kila lugha ina mofu zake mfano lugha ya kiingereza, Kiswahili na hata lugha za kibantu.


MAREJELEO
Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha
5na6.  Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo.
Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
Matinde, S.R.(2012), Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia.Mwanza: Serengeti
Educational Publishers.
TUKI. (2014).Kamusi ya Kiswahili Sanifu ,Nairobi:Oxford university press.

Powered by Blogger.