Shahidi atumia saa mbili kutoa ushahidi kesi ya Ponda
Morogoro. Kesi inayomkabili Kiongozi wa
Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, imeanza
kusikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro na shahidi wa kwanza
katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro, Sadick
Tindwa, ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga
kutoa ushahidi wake kwa zaidi ya saa mbili.
Tindwa
alitoa ushahidi mbele ya ulinzi mkali nje viwanja vya mahakama hiyo
iliyojaa watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kiongozi huyo.
Akitoa
ushahidi wake mahakamani hapo na kuongozwa na Wakili wa Serikali,
Benard Kongola, Tindwa alidai kuwa Julai 31, mwaka 2013, akiwa mkuu wa
polisi Wilaya ya Morogoro, alipokea barua kutoka kwa Umoja wa Wahadhiri
wa Dini ya Kiislamu wakiomba kufanya Kongamano la Sikukuu ya Eid Pili
kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya
Morogoro, Agosti 9 mwaka 2013.
Shahidi huyo alieleza
mahakamani hapo kuwa, kwa mamlaka aliyokuwa nayo alitoa kibali cha
kuruhusu kongamano kwa sharti la kutotoa maneno ya kashfa dhidi ya dini
nyingine na viongozi wa Serikali au maneno ya uchochezi.
Tindwa alidai kumsisitizia mwenyekiti wa kongamano hilo, Iddi Musa kufuata masharti.
Alieleza
kuwa, siku ya kongamano yeye kama mkuu wa polisi wilaya na maofisa
wengine, walikwenda kwenye kongamano hilo kwa lengo la kuimarisha
ulinzi.
Alidai baadhi ya wahadhiri walifuata masharti
waliyopewa, lakini msemaji wa mwisho, mshtakiwa Ponda Issa Ponda alitoa
maneno yenye mtazamo wa uchochezi, kashfa na kuumiza imani za dini
nyingine, jambo ambalo ni kinyume na kibali kilichotolewa, pia ni kosa
kisheria.
Tindwa alinukuu maneno ya Ponda: “Waislamu
wenzangu, tuiangalie Serikali yetu, wananchi wa Mtwara walikuwa wanadai
haki yao ya gesi, lakini wamepata matatizo makubwa ya kupelekewa jeshi
kwa sababu tu asilimia kubwa ya wananchi wa Mtwara ni Waislamu.
“Angalieni
wananchi wa Loliondo, walikuwa wanadai haki yao ya ardhi, lakini
hawakupelekewa majeshi kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wa Loliondo
ni Wakristo.
“Pia kamati za ulinzi na usalama za dini
zimeundwa na Bakwata pamoja na Serikali kwa manufaa yao binafsi, hivyo
kamati hizo zikija katika misikiti yenu kujitambulisha wafungieni
milango kisha wapigeni.” Kutokana na maneno hayo, alitoa taarifa kwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro wakati huo, Faustine Shilogile
aliyeamuru Ponda kukamatwa, lakini ilishindikana.
Upande
wa utetezi ulimuuliza maswali shahidi huyo kuhusu nafasi ya Ponda
katika kongamano hilo na uhusiano uliokuwapo kati ya mashtaka
aliyofunguliwa na maneno aliyotoa.