Maandamano:CUF yaapa kuendelea na maandamano kila mwaka
Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na ofisa wa Polisi jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF)
kimesema, hakitarudi nyuma na kitaendelea kufanya maandamano na mikutano
ya hadhara kila Januari 26 na 27 kila mwaka kuazimisha mauaji ya
wanachama wake yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.
Katika
maadhimisho yaliyofanyika mwaka huu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba na wanachama 32 wa chama hicho walipigwa kisha kushikiriwa na
Jeshi la Polisi kwa madai ya kuendesha maandamano yasiyokuwa na kibali.
Kutokana
na kosa hilo, jana Profesa Lipumba alipandishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa na kusomewa shtaka la kuhamasisha
wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa leo, Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa,
Juma Duni Haji alisema hakuna ubaya wowote kuwaenzi na kuwakumbuka
wapendwa wao kwa kufanya mikutano na maandamano.
“Jeshi
la Polisi linatakiwa kutambua ya kwamba kila Januari 26 na 27
tutaendelea kufanya mikutano na maandamano, kama hawataki kuelewa hilo
wakae mkao wa mapambano na wananchi kila mwaka.”
“Nadhani
maadhimisho ya Januari 26 na 27 mwaka 2016 yatakuwa makubwa zaidi
kulingana na Jeshi la Polisi litakavyokabiliana nayo,” alisema Haji
Aliongeza:
“Jeshi la Polisi limekosa maadili halifai, linahitaji marekebisho
makubwa na tunamtaka Rais (Jakaya Kikwete) kuwawajibisha wahusika wote
wa tukio hili-viongozi wa Jeshi la Polisi.”
Haji
alisema, “Tunalaani kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa Chama chetu na
Jeshi la Polisi na tunalitaka kutekeleza majukumu yake kwa kutumia
weledi na kuacha ushabiki na kutumiwa kisiasa kwa visingizio vya
kiitelinjensia.”
Kuhusu afya ya Profesa Lipumba,
Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alisema, “Profesa Lipumba
Manaendelea vizuri na kwa ushauri wa daktari amemwambia apumzike kwa
siku tatu bila kufanya kazi ya aina yoyote.”
Aliongeza:
“Mwenyekiti (Lipumba) hana maradhi ya shinikizo la damu lakini kutokana
na kadhia hiyo ndiyo iliyosababisha yeye kupata shinikizo hilo kwani
alipokamatwa alitumia saa 6 kuhojiwa na polisi waliokuwa wakibadilishana
mahojiano yaliyofikia hatamu saa 6 usiku.”-