Mafuriko yaikumba Mtwara, nyumba 200 zazingirwa na maji, RC atoa saa 24 yaondolewe
Wakazi wa Mtaa wa Kiangu Manispaa ya Mtwara Mikindani wakipita kwenye maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo. Picha na Haika Kimaro
Mtwara. Zaidi ya nyumba 200 zimezingirwa na maji katika
Manispaa ya Mtwara Mikindani kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na
kusababisha hasara kubwa ambayo thamani yake bado haijajulikana.
Kufuatia
hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu ametoa saa 24 kwa
wataalam kuhakikisha wanayaondoa maji ndani ya makazi ya watu.
Mkuu
wa Wilaya ya Mtwara, Wilaman Ndile amemwambia mkuu huyo wa mkoa
alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo kuwa zaidi ya
nyumba 200 zimezingirwa na maji katika mitaa mbalimbali ya manispaa
hiyo.
Alisema kuwa hakuna mtu aliyeripotiwa kupoteza
maisha kutokana na mafuriko hayo lakini kumetokea uharibifu mkubwa wa
mali na vyakula.
“Mvua kubwa zilizonyesha jana usiku
zimeshababisha mafuriko haya…tatizo kubwa mji wetu hauna mifereji ya
kupeleka maji baharini…athari ni kubwa sana,” alisema Ndile.
Aliongeza kuwa “Mitaa ya Magomeni, Chuno, Kiangu, Skoya,Kisutu Nabwada ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na tatizo hili”
Alia
Mussa ni mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo kutoka Mtaa wa Kisutu
eneo la Nabwada alisema kuwa amepoteza fedha kiasi cha Sh300,000, nguo,
chakula na vyombo vya ndani.
“Tunaomba msaada kwa
viongozi kunusuru hali hii, tunaona serikali yetu kama imetutupa, hatuna
chakula, wala fedha za kununua chakula, kila kitu kimeloa,” alisema
Mussa.
Dendegu amewaagiza wataalam wa mipango miji,
zimamoto na manispaa kuhakikisha ndani ya saa 24 wanayaondoa maji hayo
katika ya makazi ya watu.