Mwijage: Sikushtuka, sikubabaika
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Charles Mwijage amesema hakushtuka wala kubabaika Rais Jakaya
Kikwete alipomwambia kuwa anataka ampe kazi katika wizara hiyo, badala
yake alifurahi kupewa kazi anayoielewa.
“Haikunishtua
kwa sababu naijua hiyo sekta, nimeingia nishati tangu mwaka 1984 na
ninafahamu mambo mengi. Ninachoweza kuwaahidi wananchi ni kuwa,
nitafanya kazi,” alisema Mwijage.
Waziri huyo mpya
alisema jana kuwa, miongoni mwa mambo atakayoyafanyia kazi kwa nguvu ni
kubuni njia za kuzalisha umeme nchi nzima.
Pia, alisema atahakikisha mafuta yanapatikana kwa bei nzuri na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Nimepewa kazi, nitamsaidia kazi waziri, kwa kifupi nimewekwa kitengo ninachokiweza,” alisema
Mbunge
huyo wa Muleba Kaskazini alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, gesi
itakuwa imefika Dar es Salaam na kuzalisha umeme kwenye gridi ya Taifa,
hivyo nchi itakuwa na umeme wa kutosha.
“Si kwamba tumeanza leo, suala la gesi ni la mchakato kwa sababu tulishaanza kulifanyia kazi muda mrefu,” alisema.
Akizungumzia
changamoto za wizara hiyo likiwamo suala la mikataba mibovu, alisema
kuzungumzia changamoto za nyuma ni sawa na kufukua makaburi, hivyo
anachokifanya ni kuendelea na kazi iliyo mbele yake. Naibu Waziri mpya
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anna Kilango Malecela alipopigiwa simu
ili azungumze, alisema anaingia darasani na kutaka apigiwe simu baadaye,
lakini alipopigiwa simu iliita bila kupokewa.Naibu Waziri wa Sheria na
Katiba, Ummy Mwalimu ambaye alihamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), alimshukuru Rais kwa kuwa na imani naye kumweka katika
wizara hiyo yenye masuala nyeti ya kikatiba na kisheria.
“Nitasaidiana
na Migiro katika Wizara ya Sheria na Katiba, kazi ambayo ina changamoto
nyingi hasa katika wakati huu ambao Taifa linakwenda katika mchakato wa
Katiba mpya,” alisema.
Alisema atatumia uwezo,
uadilifu, juhudi na taaluma yake kuhakikisha kila kitu kinakwenda
kisheria huku akitolea mfano masuala atakayoyafanyia kazi kuwa ni sheria
kandamizi na sheria ya ndoa inayoruhusu wasichana wenye umri mdogo
kuolewa.
“Tulianza kuifanyia kazi sheria hii wakati
nipo Wizara ya Jinsia, Wanawake na Watoto na kwa sasa nitaifanyia kazi
vizuri zaidi katika upande huu wa Wizara ya Katiba na Sheria,” alisema.