Kagasheki: CCM kazi ipo mwaka huu
Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki akizungumza na waandishi wa gazeti hili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Na Mpiga Picha Wetu.
Dar es Salaam. Hofu kuhusu nafasi ya CCM kwenye Uchaguzi
Mkuu ujao inazidi kuongezeka baada ya mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi
Khamis Kagasheki kukitabiria chama hicho tawala “kazi kubwa”, akisema
hali ya sasa “siyo ile iliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita”.
Kagasheki
pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa nguvu ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo utamchagua
mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Balozi
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kabla ya
kujiuzulu kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, alisema hayo
mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi.
Kauli
yake inaungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo
wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri
Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama
hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.
Akijibu
swali la maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao na nafasi ya CCM,
Kagasheki alisema: “Ipo kazi, nafasi ya CCM sasa... Jamii imeanza kuwa
na maswali mengi kuhusu chama chetu, viongozi wachukue hili kwa umakini,
wakifuatilia watajua.”
Mbunge huyo alisema kuwa
matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni yametokana na
wananchi kuona CCM imeshindwa kuisimamia vizuri Serikali.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika Desemba mwaka jana CCM ilishinda kwa asilimia
79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa mingi
ikiwa maeneo ya mijini kimeshuka kikipata asilimia 66.66, ikilinganishwa
na ushindi wa asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji
na asilimia 91.6 katika vijiji katika uchaguzi huo mwaka 1999.
Kwa
mujibu wa matokeo hayo, kulikuwa na ongezeko kubwa la ushindi wa
wapinzani kwenye baadhi ya maeneo, hasa kutokana na kusimamisha mgombea
mmoja chini ya Ukawa inayounganisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi
na NLD.
“Mengine yametokana na CCM kutoisimamia vizuri
Serikali au kutotimiza wajibu. Wapo wananchi wanaosema CCM inakumbatia
waovu. Kama inataka kuendelea kuaminika na kutumainiwa, CCM isibweteke,
isione aibu kuikosoa Serikali.
“Hapa natambua juhudi za
Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kuwa karibu na watu. Ipo haja kwa CCM
kujitazama upya, itazame mikakati yake, inaweza kujipanga kurudisha
imani.” Kauli hiyo ya Balozi Kagasheki imekuja siku chache baada ya
Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumbuli kuwataka wanachama wa chama hicho
kikongwe kujiandaa kisaikolojia kwa matokeo yoyote yanayoweza kutokea
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
“Wana-CCM wanatakiwa
kujiandaa kisaikolojia kwani walizoea ushindi wa asilimia 90 au 80, huu
ulikuwa ushindi wa nyuma. Tusishangae tukipata ushindi wa asilimia 50,
60, 57 au 70 ni kitu cha kawaida kutokana na kukua kwa demokrasia,
hususan ushindani wa vyama vingi vya siasa kuanza kuimarika,” Makamba
alisema katika kipindi cha Power Breakfast cha Radio ya Clouds.
Nguvu ya Ukawa
Kuhusu nguvu ya Ukawa, Balozi Kagasheki alisema kwamba itakuwa ni makosa kwa watu na CCM kuudharau umoja huo.
“Watu
wasidharau Ukawa. Hiyo ni kitu tofauti. Wakiweka mtu anayeeleweka, CCM
iwe makini. Iweke mtu atakayeonekana anaweza; isikurupuke, lazima awe
mtu mwenye kujiamini.”
Ukawa iliibuka wakati wa Bunge
la Katiba baada ya wajumbe kutoka vyama hivyo kupinga mwenendo wa vikao
vya chombo hicho maalumu wakidai kuwa kilikuwa hakijadili maoni ya
wananchi yaliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
badala yake kuweka maoni ya CCM. Uamuzi wao wa kupinga mwenendo huo
uliishia kwa vyama hivyo kujitoa kwenye mchakato wa Katiba na baadaye
kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye chaguzi zote.
Atishwa na wanaosaka urais
Akizungumzia
nafasi ya urais na waliojitokeza au kutajwa kutaka kuwania nafasi hiyo
hasa ndani ya CCM, Balozi Kagasheki alisema anatishwa na wimbi la watu
wanaosaka nafasi hiyo kwa nguvu na kutumia pesa.
“Na hiyo mimi ndiyo inanitisha, kila mtu anaamini kwamba anaweza akakabidhiwa nchi. Jamani urais ni kitu kizito.”
Mbunge
huyo alinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema:
“Mimi hupenda kumnukuu hayati Mwalimu Nyerere, yeye alisema ‘Ikulu ni
mzigo’. Watu wasichukulie kauli hiyo kama mzaha.”
“Kwanza
wajipime, kuna mtu akitangaza kuwania urais watu watasema tulitegemea,
lakini mwingine akitangaza nia, watu watasema kazi ipo, hata huyu?”
Alisema
kuwa Tanzania inataka kiongozi imara, shupavu mwenye maadili
atakayeivusha nchi kutoka ilipo sasa kuipeleka wanapotaka wananchi na
kwamba wapo watu wenye rekodi nzuri za utendaji wanaofaa kwa nafasi ya
urais.
Balozi Kagasheki pia alisema kuwa utaratibu
uliopo sasa nchini hauandai viongozi wa baadaye kwa nafasi za kitaifa,
akibainisha kuwa siyo haramu kuandaa watu na kujua mapema watu wanaofaa
kuwa viongozi.
“Nashangaa kila mtu kutaka kuwa rais,
binafsi naona ni zito. Ingekuwa (jambo) jepesi, ningeshatangaza
kuuwania,” alisema Balozi Kagasheki na kusisitiza:
“Nadhani
wapo watu wanaweza kuwa rais, watu wasiwachukulie tofauti kwa hili au
lile. Lakini walio wengi wanajaribu jaribu tu bahati zao. lakini pahali
penyewe pabaya, Ikulu ni sehemu nyeti.”
Alipotakiwa
kutaja watu watano anaodhani wanafaa kwa nafasi hiyo ya urais ndani ya
chama hicho, Kagasheki alisema hawezi kutaja kwa kuwa kazi hiyo
itafanywa na CCM kupitia vikao vyake.
Hata hivyo,
alitaja sifa za mtu anayefaa kuwa rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania akisema ni lazima aweze kuisimamia na kuitetea Katiba ya nchi
bila woga.
“Zipo sifa za msingi, huwezi kuwa na makundi
ukawa rais; huwezi kuwa rais wakati Katiba inavunjwa; asiwe chanzo cha
kuvunja Muungano. Wanaotaka urais wajiulize wanaweza kusimamia hayo,”
alisema Balozi Kagasheki.