Muswada wa Kadhi balaa, Jukwaa la Wakristo laupinga
Dar/Dodoma. Wakati mjadala mkali
ukitarajiwa kuibuka katika Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza leo kuhusu
uanzishaji Mahakama ya Kadhi, Jukwaa la Wakristo Tanzania limeitaka
Serikali kuachana na muswada huo ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa
inayopinga ubaguzi na kutofungamana na dini yoyote.
Suala
la kuanzisha Mahakama ya Kadhi limo katika Muswada wa Marekebisho ya
Sheria Mbalimbali unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo na
unalenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya Tamko ya Sheria za Kiislamu
Sura ya 375 ili suala hilo litambuliwe kisheria.
Endapo
muswada huo ambao tayari umechambuliwa na wadau utapitishwa, katika
sheria hiyo kutafanyika marekebisho kwenye kifungu cha tatu baada ya
maneno ‘all courts’ (Mahakama zote) wataongeza maneno ‘including Kadhi
Courts’ (Ikijumuishwa na Mahakama ya Kadhi).
Hata
hivyo, Jukwaa la Wakristo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Makanisa
ya Kipentekoste nchini (CPCT) limesema mapendekezo hayo “yanaibua mambo
mazito ya kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na sheria hiyo itawaathiri hata wenye
imani tofauti.”
Tamko la Jukwaa hilo lililokutana
Januari 20 kujadili uanzishwaji wa mahakama hiyo ni mtihani kwa Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ambaye Septemba 29, mwaka jana katika mkutano wa
Bunge la Katiba aliahidi kuliwasilisha suala hilo katika mkutano wa
Bunge unaoanza leo ili kuanza mchakato wa uanzishwaji wa chombo hicho.
Pinda
alitoa ahadi hiyo kuwapoza wajumbe wa Bunge hilo kutokana na baadhi yao
kuhamasishana kuipigia kura ya kukataa Rasimu ya Katiba, iwapo chombo
hicho kisingeingizwa katika Katiba.
Pinda aliahidi
ifikapo Januari 2015, Sheria ya Mahakimu, sura ya 11 na Sheria ya
Kiislamu sura ya 375 zitafanyiwa marekebisho ili kutambua Mahakama ya
Kadhi kwa lengo la kuhakikisha umoja na mshikamano vinadumu kwa
Watanzania.
Wapingwa katika Kamati
Uanzishwaji
wa mahakama hiyo pia uliibua mvutano mkali katika vikao vya Kamati ya
Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wiki iliyopita na wajumbe walisema
uwezekano wa kuanzishwa kwake ni mgumu.
Katika vikao
hivyo, ilielezwa kuwa kati ya wadau 15 kutoka taasisi za dini,
wanaharakati, wanasiasa, wanasheria na wasomi waliofika mbele ya kamati
hiyo, ni mdau mmoja tu aliyekubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Miongoni
mwa wadau hao ni; Islamic Propagation Centre (IPC), Baraza la Sanaa la
Taifa (Basata), Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, CCT, TEC,
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.
Wengine ni
Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (BMKT), Mwakilishi wa Kanisa
la Wasabato (SDA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), Profesa Abdallah Safari na Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata).
Tamko la Jukwaa
Katika
tamko lake, Jukwaa wa Wakristo limetoa hoja nane likieleza kuwa ni
mapendekezo makubwa yatakayokuwa na athari kubwa na nzito kwa kuwa
yanahoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini.
Sababu nane
Kwanza, licha
ya sababu na madhumuni ya muswada huo kuwa ni kutambua Mahakama ya
Kadhi, kwa utaratibu wa sasa wa kisheria, Mahakama za Kadhi hazipo.
“Kwa
maana hiyo, hoja ya kutambua uwepo wa mahakama hizo si sahihi. Kama
inavyofahamika, Mahakama za Kadhi, pamoja na Mahakama za Wenyeji (Native
Courts), zilizokuwapo wakati wa ukoloni, zilifutwa na Sheria ya
Mahakama za Mahakimu ya mwaka 1963. Tangu wakati huo, mahakama hizi
hazipo na hazitambuliwi na sheria yoyote na mapendekezo ya muswada huu
yakipitishwa ndiyo yatazianzisha.”
Pili,
kwa mapendekezo hayo, ni wazi kuwa Serikali inachukua jukumu la
kuanzisha yenyewe taasisi za kidini kinyume na utaratibu wa kikatiba na
Serikali imekuwa haijishughulishi na uanzishwaji na uendeshaji wa
taasisi za kidini.
“Sheria ya tamko la Sheria za
Kiislamu (Inayorekebishwa) haikuanzisha mahakama au taasisi nyingine
yoyote ya kusimamia sheria hiyo bali iliweka utaratibu wa mahakama za
kawaida kuitambua na kuisimamia sheria hiyo.”
Tatu, mapendekezo hayo yanampa Waziri Mkuu mamlaka ya kutunga kanuni za utekelezaji wa uamuzi, hukumu na amri za Mahakama za Kadhi.
“Kwa
maana hiyo dola ya Tanzania, siyo tu inakusudia kuanzisha mahakama ya
kidini, bali pia kuweka utaratibu wa kutekeleza uamuzi, hukumu na amri
za mahakama hizo.”
Nne, mapendekezo
hayo yanafuta utaratibu ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka hamsini,
ambao unatambua matumizi ya sheria za dini zisizokuwa za Kikristo katika
masuala ya hadhi ya mtu, mirathi, ndoa na talaka kwa mujibu wa Sheria
ya Ndoa, Mirathi na Talaka.
Tano, kwa
mapendekezo ya muswada huo, hakuna uhakika kama mamlaka za mahakama za
sasa za kusikiliza na kuamua masuala ya hadhi ya mtu, mirathi na ndoa
kwa mujibu wa Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu itaendelea kuwapo.
“Aidha
mapendekezo ya muswada huu yako kimya juu ya uhusiano wa Mahakama za
Kadhi na mahakama za kawaida. Kwa mfano, haieleweki kama kutakuwa na
utaratibu wa rufaa, marejeo na mapitio ya uamuzi wa mahakama hizo…”
Sita, mapendekezo
hayo yako kimya juu ya kesi zinazohusu Waislamu na watu wa imani
nyingine, kwamba hata kwa wadaiwa ambao ni Waislamu, ikiwa upande mmoja
(mdai) unakwenda kwa hiari ila upande mwingine (mdaiwa) unataka shauri
lisikilizwe na mahakama ya kawaida, muswada hautoi jibu nini kifanyike.
Saba,
baadhi ya madhehebu na taasisi za Kiislamu hazikubaliani na mamlaka ya
Mufti kwenye masuala yao, hivyo kumpa Mufti mamlaka ya kutunga kanuni
zitakazotumika katika Mahakama za Kadhi na kuwateua makadhi, kunaweza
kusababisha migongano na migogoro ndani ya jamii za Waislamu.
Nane, haturidhiki na hoja kwamba mahakama hizo hazitatumia fedha za umma.
“Mfano,
Waziri atakapokuwa anatunga kanuni atatumia fedha na rasilimali
mbalimbali za umma. Vilevile, utekelezaji wa amri na hukumu za mahakama
hizi utahitaji polisi na madalali wa mahakama ambao wanalipwa kwa fedha
za umma.”
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Boniface Meena na Sharon Sauwa