Vita vya Profesa Muhongo
Profesa Sospeter Muhongo
Sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
linaweza kuwa limefanya jina la Profesa Sospeter Muhongo kuzungumzwa
sana na kuonekana amekuwa kwenye wakati mgumu tangu lilipoibuka, lakini
ukweli ni kwamba lilikuwa hitimisho tu la matukio mengi tangu msomi huyo
aanze kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
Muhongo,
ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge Mei 3, 2012 kabla
ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri, amekuwa kwenye kiti
moto wakati wote tangu ashike uwaziri kutokana na kashfa ambazo hazikomi
kwenye sekta ya madini na nishati, na tabia yake ya kushambulia
wanaotoa hoja kwa maneno ya dhihaka na kujisifu, ambayo mara nyingi
yalikera watoa hoja.
Mikataba 26
Waziri
Muhongo alianza kazi kwa kuliagiza Shirika la Mafuta (TPDC) kupitia
upya mikataba 26 ya utafutaji gesi, hatua ambayo iliungwa mkono na wengi
huku wakitaka ripoti ya kazi hiyo iwe bayana ili Watanzania wajue uozo
uliopo, hata hivyo, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi huo, Profesa
Muhongo hakuweka bayana matokeo ya ripoti hiyo, badala yake akasema
ripoti hiyo itatumika wakati wa kuingia mikataba mipya tofauti na
alivyoeleza mwanzo kuwa angefuta mikataba mibovu.
Akajikuta
anaingia kwenye mzozo na wadau, hasa wabunge, na miaka miwili baadaye,
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ikaiagiza menejimenti ya TPDC
kupeleka mikataba hiyo kwenye kamati, lakini menejimenti ikagoma,
kitendo kilichosababisha viongozi wa shirika hilo wakamatwe.
Kampuni ya Puma Energy
Hatua
iliyozua tafrani zaidi ni ile ya wizara yake kuipa kampuni ya Puma
Energy zabuni ya ugavi wa mafuta mazito kwa kampuni ya kufua umeme ya
IPTL. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa, hasa bungeni ambako watunga
sheria walidai kuwa zabuni hiyo ilitolewa bila ya kufuata Sheria ya
Manunuzi. Wabunge walidai kuwa Puma Energy haikuwemo kati ya kampuni
zilizoomba, na kutuhumu kuwa kulikuwa na rushwa.
Wabunge
walitaka Profesa Muhongo na katibu wake, Eliackim Maswi wawajibishwe,
hoja iliyosababisha mgawanyiko mkubwa bungeni kiasi cha CCM kuitisha
kikao cha wabunge wake kupanga mikakati ya kumuokoa waziri huyo.
Katika
sakata hilo, Profesa Muhongo aliingia kwenye mgogoro na mbunge wa
Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye alichangia hoja. Katika
majibu yake, Profesa Muhongo alisema kuwa alikuwa akidhani mbunge huyo
kuwa ni msomi, na akalazimika kufuatilia elimu yake. Alipotaka kueleza
matokeo ya kidato cha nne ya Ole Sendeka, Spika Anne Makinda alimzuia na
kumtaka aendelee na hoja iliyokuwa mbele yake.
Wafanyabiashara wazawa
Tabia
ya Profesa Muhongo kujibu hoja kwa kushambulia walioitoa iliamsha
mjadala mkubwa baada ya wafanyabiashara wakubwa kulalamika kuwa wizara
hiyo haitoi kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa leseni za utafutaji
gesi na mafuta. Katika kujibu hoja hiyo, mtaalamu huyo wa jiolojia,
aliwaita wafanyabiashara hao kuwa ni madalali na hawana uwezo wa kufanya
kazi hiyo.
Alieleza kuwa kazi hiyo inahitaji mtaji
mkubwa. Alisema maombi tu ya kazi hiyo yanagharimu Dola 700,000, wakati
takwimu za kazi hiyo zinagharimu Dola 3 milioni, utafutaji Dola 15,000
hadi 20,000 kwa mita moja ya mraba, kuchoronga kwenye kina kirefu kuna
gharimu Dola 1 milioni kwa siku, wakati kumaliza tundu moja ni Dola 1 na
yanahitajika matundu 12.
Pia alisema kuchimba kwa
ajili ya kupitisha mabomba kwenda nchi kavu kunagharimu dola 200.
Profesa alisema hayo bungeni huku akitamba kwamba yeye ni msomi na
wabunge wanaojaribu kujenga hoja hizo ni mawakala ambao “wana-retire
imprest” kwa kuzungumza bungeni, akimaanisha kuwa wanaonyesha kwa
waliowalipa fedha kuwa wametekeleza kazi waliyotumwa.
Kufuta leseni za vitalu
Pia
alizua kizaazaa kingine aliposema kuwa atapitia leseni zote za vitalu
vya madini na kufuta vile ambazo hazifanyi kazi kama sheria inavyotaka.
Alisema kuna leseni 597, lakini wanaolipa kodi ni wanaomiliki vitalu 10
tu na baadaye akatangaza kuwa alishafuta leseni za vitalu zaidi ya 150
na alikuwa anakusudia kufuta nyingine 78.
Mkakati wake
uliwagusa wafanyabiashara wengi wazawa na mara kadhaa walipokutana
walitoa kauli ya kulaani misimamo ya mbunge huyo wa kuteuliwa.
Wakati
kashfa ya escrow ilipoanza, Profesa Muhongo alitumia tena mbinu yake ya
kushambulia watoa hoja kwa kueleza kuwa maneno hayo yote yanatokana na
uamuzi wake wa kufuta mkataba wa Tanesco na kampuni ya uwakili ya Mkono,
akisema ililipwa Sh62 bilioni na hivyo kuwa moja ya taasisi
zinazotafuna fedha za shirika hilo la umma.
Katika
kashfa ya escrow, Profesa Muhongo anatuhumiwa kwa kushindwa
kushughulikia vizuri sakata hilo la uchotwaji fedha kwenye akaunti hiyo
iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco na IPTL baada ya pande hizo mbili
kuingia kwenye mgogoro na kufungua kesi mahakamani.
Akitoa
utetezi wa Serikali bungeni, Profesa Muhongo alitumia staili yake ya
kuwananga waliokuwa wakituhumu huku akijisifu kuwa ni msomi. Alieleza
kuwa fedha hizo, Sh306 bilioni, hazikuwa mali ya umma bali za IPTL,
lakini hoja zake zikapingwa vikali na wabunge ambao walionyesha nyaraka
mbalimbali kuthibitisha kuwa msomi huyo hakusema ukweli.