Waziri amsuta Kamanda Kova kuhusu Panya Road
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe amesema Watanzania wamepoteza imani na Jeshi la Polisi
na ameliagiza kujitathmini na kutoa majibu kuhusu kukamatwa kwa vijana
1,200 wa kikundi cha uhalifu maarufu Panya Road.
Waziri
Chikawe aliyekuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka kwa maofisa
waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, amelitaka jeshi hilo kujiuliza na
kutoa majibu kutokana na madai kwamba baadhi ya vijana hao wamekamatwa
kwa matakwa tu ya polisi.
Alisema kuwa anazo taarifa
kuwa polisi wamejikita zaidi katika makusanyo, badala ya kuangalia
usalama wa watu na ndiyo maana wamekuwa si watu wa kuzuia tena uhalifu
kama inavyotakiwa lakini wanasubiri matukio yafanyike.
Alitaka
polisi pia watoe sababu za kwa nini wananchi wanasema kuwa kumeibuka
kitengo cha dhuluma, ambacho wamekibatiza kuwa ‘kuingia bure na kutoka
kwa hela’, jambo linalotia doa chombo hicho.
Kwa upande
wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest
Mangu, alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo uhaba
wa vifaa na mafunzo katika kipindi hiki ambacho wizi wa mitandao
unaonekana kupamba moto.
IGP Mangu alikiri kuwepo baadhi ya polisi ambao wanatumia vibaya viapo vyao na kusababisha shutuma kwa jeshi zima.
Hivi
karibuni, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alitangaza kuwakamata zaidi ya vijana 1,500 kuwa madai ni Panya Road.