Mwenyekiti CCM Marekani afungwa miezi 18
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Texas, Houston nchini Marekani, Simon Makangula (katikati). Picha ya Mtandano
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Texas, Houston nchini Marekani,
Simon Makangula amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela na
kulipa faini ya zaidi ya Sh92.4 milioni kwa kosa la kughushi nyaraka za
ulipaji wa kodi.
Makangula ambaye ni mmiliki wa kampuni
ya kutoa huduma za malipo ya kodi iitwayo Mshale Investment & Tax
Service, alihukumiwa Ijumaa katika Mahakama ya Wilaya na Jaji Gray
Miller kwa udanganyifu huo wa kuwasaidia wateja wake kughushi nyaraka za
kodi ya mapato, kwa mujibu wa tovuti ya click2houston.com.
Wakili
wa serikali nchini humo, Kenneth Magidson pamoja na Lucy Cruz, wakala
maalumu wa kitengo cha uchunguzi wa makosa ya kihalifu katika masuala ya
mapato ya Marekani, kwa nyakati tofauti waliiambia mahakama kuwa
Makangula alimsaidia mmoja wa wateja wake ambaye ni raia wa Marekani
kutayarisha malipo ya kodi yasiyo halali.
Sambamba na kifungo cha mwaka mmoja na nusu, pia Makangula anatakiwa kulipa faini ya Dola 51,645 sawa na Sh92.4 milioni.
Oktoba
15, mwaka jana, Makangula alikiri kosa hilo mbele ya hakimu Miller na
kuwa malipo ya kodi hiyo yalikuwa na udanganyifu katika vipengele
kadhaa, yakiwamo katika makadirio na idadi ya wategemezi wa mlipakodi,
mambo yaliyosababisha hasara ya Dola 9,731 za Marekani (Sh17.3 milioni).
Pia,
katika kesi hiyo, Makangula alikiri kuwa alimsaidia mteja wake kughushi
kuwa yeye ndiye mmiliki pekee wa biashara hiyo, hatua iliyosaidia watu
wengine, washirika wa mteja wake, wakwepe kulipa kodi.
Kampuni
ya Makangula inajishughulisha na huduma za ulipaji wa kodi, uhasibu,
mfumo wa ulipaji wa kodi za mapato, biashara za ardhi, kodi za majengo
na ushauri wa masuala ya kodi ya mapato.
Makangula,
ambaye ni mwenyekiti wa tawi la CCM la Texas, anawaongoza wajumbe tisa
wa halmashauri ya tawi wanaoishi Marekani na mara kadhaa ameonekana
kwenye picha akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM
wanaotembelea Marekani.