Mbunge abwagiwa mtoto kikaoni Dar
Hawa Kundani (mwenye vazi jeusi), anayedai kuzaa na kutelekelezwa na mbunge wa Dimani, Abdallah Sharia Ameir, akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuvamia kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kilichokuwa kikifanyika Dar es Salaam jana. Picha na Beatrice Moses .
Dar es Salaam. Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Hawa
Kundani amezua taharuki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala, baada ya kuvamia ghafla na kupiga kelele akidai
kutelekezwa na mumewe ambaye ni Mbunge wa Dimani (CCM) visiwani
Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir.
Tukio hilo la aina
yake lilitokea jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere, na mwanamke huyo akiwa ameongozana na mtangazaji wa kituo
kimoja cha redio, Joyce Kiria aliingia na kusababisha mshtuko kwa
wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa dini ya Kikristo waliokuwa
wamealikwa hapo. Wakati huo walikuwa wakijadiliana suala la Mahakama ya
Kadhi.
Hawa akizungumza na gazeti hili alidai kwamba
Ameir ni mume wake walifunga ndoa mkoani Arusha mwaka 1999 na kuzaa naye
watoto wanne, lakini mmoja alifariki dunia.
“
Nashangaa amebadilika ghafla amekuwa mtu wa kuoa wanawake na kuacha mara
kwa mara, hadi sasa ameshaoa wanawake wanne na kuwaacha mimi nipo tu,
alinioa bado mdogo,” alidai Hawa.
Alidai kuwa watoto
wengine wawili, mkubwa ana miaka tisa na mwingine miaka sita
walichukuliwa na mumewe huyo akawapeleka kulelewa na mwanamke aliyemuoa
jambo ambalo alidai linamuuma.
“ Naumia wanangu sijui
wanaishi vipi, huyu niliyembeba ni mlemavu, hamtaki amekuwa akininanga
kwa maneno mengi sana, mimi nimetoka naye mbali nilibadili dini kwa
ajili yake, leo hii ananitesa, hanitaki anipe haki yangu ili niishi
mwenyewe,” alisema Hawa.
Kwa upande wa mbunge hiyo Ameir alidai kwamba kesi yao
ipo kwenye Mahakama ya Kadhi, akidai kwamba mwanamke huyo amekuwa
akimdhalilisha kwa kupitia mtoto huyo mlemavu ambaye alikiri ni mwanaye.
“
Huyu ni mwanangu sishindwi kumhudumia, lakini sitaki fedha ziende kwa
huyu mwanamke atazitumia kwa mambo yake mengine, mimi nilimpeleka kwa
mama yake mzazi akakae naye huko lakini yeye hataki,” alisema Mbunge
Ameir.
Akizungumzia tukio hilo Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema ni tukio ambalo limewafedhehesha
kwa kuwa hawakulitarajia.
“Tulivamiwa na wanawake kama
wanne na wanaume wawili nafikiri mmoja alikuwa ni mpiga picha, mwanamke
mmoja akawa anapiga kelele, tulitaharuki kwa sababu maaskofu walikuwa
wameanza kutoa maoni yao,” alisema.
Alisema kwamba
waliomba msaada kwa maofisa usalama wa ukumbi na walifika na kuwachukua
wahusika hao, kisha kuwapeleka polisi kwa hatua zaidi.