BSS haijafa, sasa kuja kivingine- Madam Rita Poulsen
Akizungumzia
changamoto zilizolikabili shindano hilo, Rita alisema: “Lakini
ninashukuru kwa sasa zimeanza kupungua na tunafanya kazi vizuri,
nisingependa kukumbusha changamoto zilizomalizika ila ifahamike ipo siku
BSS itateka soko la Bongo Fleva, wasanii wote wakubwa utaona wana nembo
ya BSS.”
Dar es Salaam. Jaji kiongozi wa mashindano
ya kusaka vipaji vya muziki, maarufu BSS, Rita Poulsen amewataka
mashabiki na wapenda muziki kuondoa hofu akieleza kuwa mashindano hayo
hayajafa.
Mwaka jana mashindano hayo hayakufanyika tofauti na ilivyozoeleka.
Hali hiyo ilizua hofu miongoni mwa mashabiki kwamba huenda mashindano hayo yamekufa.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana Rita alisema kuwa licha ya shindano hilo
kuchelewa kuanza katika msimu huu, litafanyika na kwamba mipango
inakamilishwa.
“Najua Watanzania wana hamu ya
kushuhudia msimu mwingine wa ukianza. BSS ni mapinduzi hasa kwa vijana
nayo hayaishi kwa siku moja, lakini kwa sasa kuna mambo tunayaweka sawa,
hadi mwishoni mwa Februari mipango itakuwa imekamilika,”alisema Rita.
Alibainisha
kuwa amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa wadau na wapenzi wa
mashindano hayo wakihoji kuhusu kuchelewa kuanza kwa msimu mpya wa BSS.
Jaji huyo maarufu kwa jina la Madam Rita alisema kuwa kuanza kwa msimu kutakwenda sanjari na udhamini mpya.
Rita
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark, alidokeza kwamba
udhamini wa awali wa Kampuni ya Zantel kwa BSS umekwisha muda wake na
msimu mpya utakuwa na wadhamini wapya.
Alifafanua pia
tayari kampuni mbalimbali zimeomba kudhamini shindano hilo ambalo
hujumisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini na baadhi ya nchi za
Afrika Mashariki.
BSS ilianza mwaka 2006 kwa kusaka vipaji vya vijana wa
Kitanzania na kufanikiwa kuibua vipaji mbalimbali vya wasanii huku
baadhi wakiendelea kufanya vizuri.
Baadhi ya wasanii
walioibuliwa na BSS na wanaendelea kufanya vizuri ni pamoja na; Kala
Jeremiah, Peter Msechu, Baby Madaha, Meninah, David Rogers, Pascal
Casian na Walter Chilambo na Emmanuel Msuya.
Kuhusu majaji wa shindano hilo, Rita alisema yeye ataendelea kuwa jaji kiongozi akiwa na Master J na Salama Jabir.
“Timu
ya ushindi itakuwa ni ile ile, mimi nitakuwapo, Master J na Salama.
Niwaondoe hofu mashabiki na wanaotaka kuibua vipaji vyao katika muziki.”
Mshindi
wa msimu uliopita wa BSS alikuwa ni Emmanuel Msuya, huku wa msimu wa
kwanza katika mashindano hayo mwaka 2007 akiwa Jumanne Iddi.
Mshindi
wa msimu uliopita katika shindano hilo lililojulikana kwa jina la Epic
Bongo Star Search alizawadiwa kitita cha Sh50 milioni, huku msindi wa
msimu wa kwanza akizawadiwa gari.
Akizungumzia
changamoto zilizolikabili shindano hilo, Rita alisema: “Lakini
ninashukuru kwa sasa zimeanza kupungua na tunafanya kazi vizuri,
nisingependa kukumbusha changamoto zilizomalizika ila ifahamike ipo siku
BSS itateka soko la Bongo Fleva, wasanii wote wakubwa utaona wana nembo
ya BSS.”
Aliongeza: “Haya ni mapinduzi subiri kidogo
utakuja kuniambia,sitakata tamaa kwani mapinduzi hayafanyiki siku moja,
sifanyi kwa manufaa ya kupata jina wala fedha ila ni kubadilisha maisha
ya vijana kupitia vipaji vyao.”
Ritha alisema mbali na
kutafuta vipaji mikoani wamekuwa wakitoa elimu ya vijana kujitambua na
athari za magonjwa mbalimbali ikiwamo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.-