Vuta nikuvute bungeni, Spika Makinda ahairisha Bunge
Spika Anna Makinda akitoa ufafanuzi Bungeni
Spika wa Bunge Anna Makinda leo amelazimika kuahirisha kikao
cha Bunge kilichoanza jana, baada ya vuta nikuvute iliyotokea baada ya
kutolewa kwa hoja binafsi kutoka kwa Mbunge na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuhusu jeshi la polisi kumshambulia Profesa Ibrahimu Lipumba jana akiwa kwenye maandamano .
Akizungumza
katika Bunge hilo Mbatia amesema kuwa kitendo cha polisi cha kuwapiga
raia wasiokuwa na hatia, kuwazalilisha waandishi wa habari na kupiga
mabomu ya machozi kiasi cha kuwafanya watoto wadogo kuhangaika
hakikubaliki.
Amesema polisi wakiendelea kuachwa
kufanya vitu vya uvunjifu wa Amani Serikali haitatawalika hivyo ili
kurejesha amani na imani ya wananchi kwa Serikali yao ni vema shughuli
zote za Bunge zikaahirishwa kupisha mjadala wa hoja hiyo binafsi kwa
lengo la kuinusuru nchi.
“Mheshimiwa Spika naliomba
bunge lako liahirishe shughuli zake ili leo tuweze kujadili suala hili
la uvunjifu wa amani uliofanywa na jeshi letu la polisi jijini Dar es
Salam jana, wao wanasema kuwa wamepewa amri kutoka ngazi za juu tunataka
serikali ituambie ni nani anayetoa amri hizi za kupiga watu wasiokuwa
na hatia yeyote, amesema Mbatia.
Baada ya kuwasilisha
hoja hiyo asilimia kubwa ya wabunge walisimama juu isha ya kuunga mkono
hoja hiyo lakini Spika Makinda akawaomba wakae ili aweze kutoa ufafanuzi
kwa mujibu wa kanuni.
Spika makinda aliwaeleza wabunge
hao kuwa suala hilo ni nyeti kwa sababu ni la kiusalama, ili kupata
ufafanuzi zaidi anaiagiza Serikali kufikisha bungeni hapo majibu ya hoja
hiyo kesho ili wabunge waweze kujadili.
Baada ya
maamuzi hayo ya Spika Makinda kelele zikasikika bungeni huku wabunge
wakitaka kufanyika kwa mjadala huo leo leo, ndipo Spika alipoamua
kuahirisha bunge hadi saa kumi jioni.