mwanzo Habari Kitaifa Kitaifa Kamati za Bunge zawagwaya kina Chenge, Ngeleja

Dar es Salaam. Wajumbe wa kamati tatu za Kudumu za Bunge ambazo wenyeviti wake wanatakiwa kuvuliwa nyadhifa zao kutokana na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ‘wanasuasua’ kuwaondoa na kuchagua viongozi wengine.
Kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati hizo ambazo ni Bajeti, Nishati na Madini na Katiba, Sheria na Utawala wamekuwa wakishangazwa na hatua za wahusika hao kuendelea kujitambulisha kuwa ni wenyeviti, sambamba na kuongoza vikao vya kamati hizo, wakati wakijua wazi kuwa hawatakiwi kufanya hivyo.
Wenyeviti wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba) na Andrew Chenge (Bajeti).
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah aliliambia gazeti hili jana kwamba jukumu la kuwaondoa wenyeviti hao lipo mikononi mwa wajumbe wa kamati hizo, kwamba kama wakishindwa Spika wa Bunge atachukua jukumu hilo.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge liliazimia kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wakiwepo viongozi wa Kamati hizo tatu, wachukuliwe hatua za haraka na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 27 mwaka huu.
Akinukuu azimio hilo Kashilillah alisema, “Wajumbe husika ndiyo wanaotakiwa kuwaondoa wenyeviti hao, hilo ni lazima mlitambue jamani. Waulizeni ni lini watafanya hivyo.”
Alisema ndiyo maana kamati ikiwa haina mwenyekiti, wajumbe wenyewe huchagua mmoja kati yao kwa ajili ya kuongoza kikao cha kamati.
“Spika hawezi kumwondoa mwenyekiti wa kamati husika, anachoweza kufanya Spika ni kumhamisha mwenyekiti kutoka kamati moja kwenda nyingine. Akifanya hivyo maana yake ni kwamba mwenyekiti husika anapoteza sifa za kuwa mwenyekiti,” alisema.
Alisema jambo hilo Spika Makinda anaweza kulifanya kama wajumbe wa kamati hizo tatu zitashindwa kuchagua wenyeviti wengine. Kuhusu Chenge ambaye aliteuliwa na Spika Makinda kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bajeti alisema, “Chenge aliteuliwa katika kipindi cha mpito ambacho kikiisha atachaguliwa mwenyekiti mwingine. Hivyo naye anaweza kuondolewa tu na wajumbe wa kamati.”
Mvutano katika kamati
Taarifa kutoka ndani ya kamati ya Bajeti zilieleza gazeti hili kwamba, juzi kamati hiyo ilikutana na Wizara ya Maji na Uchukuzi na Chenge alijitambulisha kama mwenyekiti, jambo ambalo liliwashangaza wajumbe wa kamati hiyo.
“Tumeshangazwa jinsi alivyojitambulisha kwa sababu awali kamati tulikubaliana kuwa akae pembeni na kumwachia Makamu mwenyekiti, Dk Limbu (Festus) kuongoza vikao vya kamati. Inavyoonekana ni kama anang’ang’ania nafasi hii,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

0
Share


Powered by Blogger.