Madiwani Chadema wasusia kikao Moshi

Moshi. Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro limesusia kushiriki kikao cha bajeti na kuamua kutoka nje ya ukumbi, wakimtuhumu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Shaban Ntarambe kushiriki katika mgogoro wa kiwanja.
Madiwani hao walisema, kiwanja kinachodaiwa kuhusishwa na mkurugenzi huyo ni namba L.O NA 9850 chenye hati namba 10660.
Kiwanja hicho ndipo kuna Ofisi za Kata ya Mawenzi mjini hapa.
Madiwani waliotoka nje wanazidi theluthi mbili ya madiwani wote wa manispaa hiyo.
Kabla ya Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffary Michael kufungua kikao hicho, Diwani wa Kata ya Rau, Peter Kimaro aliomba mwongozo na kudai kuwa kutokana na mkurugenzi wa manispaa hiyo kushiriki ‘kupora’ kiwanja chenye Ofisi ya Kata ya Mawenzi, hawako tayari kuendelea na kikao.
Hatua hiyo ilifuatiwa na madiwani hao wa Chadema kutoka nje ya ukumbi na kuwaacha wajumbe wachache.
Kwa upande wake, Ntarambe alisema kikao hicho kisingeweza kuvunjwa pamoja na madiwani hao wa Chadema kutoka nje ya ukumbi.
“Walikubali kushiriki kikao hiki na ajenda ziko mezani, hatuwezi kuvunja kikao,” alisema. (Rehema Matowo).
Powered by Blogger.