Sudan Kusini wasaini makubaliano 43 ya kutatua mgogoro wao


Rais Jakaya Kikwete akishuhudia Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir (kushoto) akipeana mikono na aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Riek Machar  baada ya kuweka saini makubaliano ya kurejesha amani nchini mwao na ndani  chama Sudan People's Liberation Movement(SPLM) katika hafla iliyofanyika juzi mkoani Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
Arusha. Viongozi wa Chama tawala cha nchini Sudan Kusini, Sudan People Liberation Movement (SPLM) wametakiwa kuheshimu makubaliano 43 waliyosaini juzi usiku ili kusitishwa vita na kurejesha amani na kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.
Wito huo ulitolewa juzi na marais watatu wa Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Chama cha SPLM kimegawanyika katika makundi matatu na kusababisha vita vya wenyewe tangu mwaka 2013.
Makubaliano hayo yalisainiwa saa tatu usiku baada ya majadiliano ya marais hao na viongozi wa makundi yanayopingana ndani ya chama hicho katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Arusha na kumalizika saa sita usiku.
“Ili makubaliano haya yadumu, mnapaswa kwanza wote muwe na utashi wa kisiasa, mzungumze kila mnapoona kuna jambo linawakwaza katika kutekeleza maazimio haya,” alisema Kikwete.
Alisema CCM na Chama cha African National Congress (ANC), wamekubaliana kushirikiana kutoa msaada wowote utakaohitajika katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
Aliwataka viongozi hao kusitisha vita vinavyoendelea katika nchi yao ili iwe rahisi kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa.
Rais Museveni alisema baada ya makubaliano yaliyosainiwa na makundi matatu ndani ya SPLM, lazima sasa yarejeshe umoja na mshikamano Sudan Kusini.
Alisema chanzo cha kugawanyika viongozi wakuu wa SPLM, akiwamo Rais wa Sudan Kusini ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Dk Riek Machar ni kutofautiana kimtazamo.
“Mgawanyiko wenu unatokana na kuwa na mitazamo tofauti katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini sasa baada ya majadiliano mmeweza kufikia mwafaka, hivyo hatutarajii kurejea kwenye mapigano,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta aliwataka viongozi wa SPLM kurejea katika mazungumzo ya kuboresha chama kwa manufaa ya Sudan Kusini.
“Leo ni faraja kwa wananchi wa Sudan Kusini na Waafrika wote, kwani mmefikia makubaliano yatakayorejesha amani ndani ya Sudan Kusini,” alisema.
Akizungumzia makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa aliwapongeza viongozi wa CCM kwa kufanikisha makubaliano hayo na anaamini sasa amani imepatikana.
Alisema mazungumzo hayo yalikuwa yanafuatiliwa na Afrika yote, hivyo hategemei maazimio yake yatashindwa kutekelezwa kwa wakati.
“Nawapongeza CCM kwa kuendeleza kazi ya kusaka amani Afrika iliyokuwa inafanywa na hayati Julius Nyerere na leo mnaendelea kuthibitisha kuwa Tanzania ni kitovu cha kusaka amani ya Afrika,” alisema.
Kwa upande wao, Rais Kiir, Dr Machar na kiongozi wa kundi la viongozi waliokuwa wamefungwa, Dk Peter Njaba walieleza kuridhia makubaliano yote na kuyatekeleza. Akisoma baadhi ya makubaliano waliyosaini viongozi hao, Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana alisema ni pamoja na kuifanyia marekebisho Katiba ya SPLM, kutoa fursa kwa mwanachama yeyote wa SPLM kugombea uongozi, kufuata misingi ya demokrasia na utawala bora ndani ya SPLM.
Powered by Blogger.