Siri ya wizi mafuta ya transfoma yabainika
Dar es Salaam. Ile dhana ya kuwa mafuta ya kupoza transfoma
yanaibwa na wauza chipsi, imebainika siyo ya kweli baada ya uchunguzi
kuonyesha kuwa yanatumiwa viwandani kuendesha mitambo, kuchanganywa
katika vipodozi na mengine yakisafirishwa nchi za nje.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa wanaoiba mafuta hayo ya
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pia huchukua nyaya za shaba katika
transfoma hizo kwa ajili ya kutengeneza mapambo mbalimbali kama herini,
mkufu na bangili.
Kutokana na wizi huo, mwaka jana
pekee transfoma 34 zenye ukubwa mbalimbali ziliibiwa mafuta na shaba,
hivyo kuisababishia Tanesco hasara ya Sh306 milioni.
Meneja
Mwandamizi, Masoko na Mauzo wa Tanesco, Injinia Nicholaus Kamuleka
alisema utafiti uliofanywa na wahandisi wa shirika hilo unaonyesha kuwa
mafuta ya transfoma yanaibwa kwa ajili shughuli mbalimbali.
“Kazi
ya mafuta ya transfoma ni kupoza nguvu ya umeme mkubwa,” alisema
Injinia Kamuleka na kuongeza kuwa mafuta hayo pia huchanganywa na ya
gari.
Transfoma kubwa moja inaweza kuwa na lita 200 za mafuta wakati dogo kabisa lina ujazo wa lita 40.
Kamuleka alisema pia hutumiwa na mafundi wa kienyeji kuchomelea vyuma ambao huyanunua kwa Sh5,000 kwa lita.
Mmiliki wa kiwanda cha chuma kilichopo Mikocheni ambaye
hakutaka jina lake litajwe alisema: “Sisi hatuwezi kuharibu transfoma na
kuchukua mafuta, sisi tunaletewa hapa hapa.”
Dhana ya chipsi
Injinia
Kamuleka alikanusha kuwa mafuta ya transfoma hutumiwa na
wafanyabiashara kukaanga chipsi na kusema kuwa harufu kali ya mafuta
hayo isingefaa kwa matumizi ya kula.
Baadhi ya wafanyabiashara wa chipsi walisema ni vigumu kutumia mafuta hayo kwa kuwa yanauzwa bei ghali.
“Huwezi
kununua mafuta lita Sh10,000 kwa ajili ya biashara ya chipsi, siyo
kweli kabisa,” alisema mfanyabiashara wa Tabata, Elisha Mungai.